Tuesday, July 30, 2013

SINDI.....NA LAURA PETTIE (32)

32

Alikirudisha kile kifaa cha kupimia ujauzito katika kile kibahasha kidogo cheupe na kukiweka pembeni yake. Kichwa kilikuwa na matundu ghafla. Ufahamu ulimtoka na kukimbilia kusikojulikana. Akashusha pumzi ndefu, akihisi pia tumbo likimcheza. Akanyanyuka na na asijue kilichomnyanyua. Akalikodolea macho kochi lililokuwa mbele yake pasipo kuelewa kwanini alilitumbulia macho.


Pumzi nyingine ndefu ikamshuka, alihisi kuchoka maradufu, alihisi vichomi vikimvamia ghafla  na kutoweka. Mwili ukamsisimka!

Katika safari yake ya mapenzi hakuwahi kukumbana na kadhia kama hii. Mbija fupi ikamtoka na akili yake ikimtuma amtafute Sindi popote alipo aje kumtoa katika suluba ile ya wasiwasi. akaufuata mlango lakini akili nyingine ikamzuia kuugusa ule mlango na akajikuta akigeuka na kukitazama kitanda, pale ilipokuwepo ile bahasha yenye kifaa.

Sekunde mbili alizosimama hapo, zikampa uamuzi aliouona wa busara zaidi. akarejea na kukichukua kile kifaa kisha akakitia kwenye wa shati alilokuwa amelitundika mlangoni. Akarejea kitandani na kujilaza chali akimngoja mhusika!

Kule kwa Jamilla Sindi alikuwa alikuwa amejilaza kitandani naye mawazo yakionekana kumjia na kutoweka pamoja na stori za kuchekesha alizokuwa akipewa na Jamilla. akili yake ilikosa utulivu kwa kiasi Fulani na chanzo kikiwa siri yake.

Wakati wakiongea hili na lile mlango ukafunguliwa na mpangaji mmoja akatumbukiza kichwa tu
‘Mkubwa wa jiko kidogo?’ akasema akipenyeza mkono ili amiminiwe chumvi mkononi
Jamilla akaachana na upishi na kuifuata chumvi kwenye kikabati kidogo humo chumbani
‘we umelala hapo mumeo uko ndani anajua uko hapa?’ yule mpangaji akauliza na kufanya Sindi na Jamilla wageuze shingo zao na kumtazama kwa mshangao

‘Mume wa nani?’ Jamilla akauliza
‘Nani?’ Sindi naye ukaunga na swali
‘Jerry!...mbona kaja saa nyiiingi katupita hapo nje kitambo tu’ yule mpangaji sasa akaingiza kiwiliwili chote ndani.

‘Khe makubwa!’ Sindi akanyanyuka na kuteremsha miguu chini akizitafuta ndala zake kwa miguu yake huku akiikusanya khanga yake  na kuikaza vema kiunoni. Sindi akatoka na kuwaacha yule mpangaji na Jamilla
‘Utamkatia safari ya talaka mwenzio….unamvundika humu kwako kule kwake mumewe anapiga mihayo tu’ yule mpangaji akasema akitania huku akikinga mkono na Jamilla kummiminia chumvi kiganjani. Jamilla akabinua midomo yake  na kuguna.
‘Sasa hivi utasikia ngumi zao…’ akajibu Jamilla na kufanya yule mpangaji acheke kishambenga.

Sindi aliingia chumbani kwake na kumkuta Jerry ameketi kitandani. uso uliojaa wasiwasi ulimfanya Jerry amtazame kiudadisi zaidi.
‘Umekuja muda mrefu?’ akauliza Sindi akionyesha kukosa amani na macho yake yakiangalia kitandani pale alipoiacha ile bahasha. Hakuiona!

‘Ulikuwa wapi?’ Jerry akauliza kwa upole tu akijiinusha na kuketi kitako
‘Kwa jamilla hapo….nilijua huji’ akajitetea na macho yake yakiangaza chini kama mtu anayetafuta kitu na Jerry akajua alichokuwa akikitafuta.
‘Una njaa?’ Sindi akamuuliza akisimama na kusugua sugua mikono yake kwenye mapaja yake.
‘Sijala mama’ Jerry akajibu huku akiitazama miko ya Sindi iliyokuwa inahangaika kwenye yale mapaja. Aliuona wasiwasi wake dhahiri pamoja na kujitahidi kuwa sawa mbele ya Jerry.

‘Ngoja nikuombee mboga kwa Jamilla…maana sikununua kitu leo’ Sindi akasema akigeuka
‘Kuna samaki nimeleta wako hapo kwenye mfuko’ Jerry akamuonyesha mfuko alioutua kwenye kochi mara tu alipofika.

Sindi alipoutanua ule mfuko akaona sendozi na khanga. Tabasamu pana likaupamba uso wake. Akageuka na kumtazama Jerry kwa furaha. Lile tabasamu, ule uso wa furaha ndio hasa Jerry alitaka kuuona kila siku kila mahali. Akafarijika kumuona Sindi akiviweka vile viatu chini na kujaribisha. Vikamtosha.

‘Asante’ Sindi akajibu akavivua na kuvikamata mkononi na kisha kupiga goti la heshima kwa Jerry. Avirudisha viatu kwenye mfuko na kutoa khanga iliyokuwa kwenye nailoni lake. Akaikunjua kwa upana akiitazama kwa furaha
‘Imeandikwaje?’ Jerry akamuuliza na Sindi akaiinua juu zaidi ile khanga na kuisoma kwa sauti kidogo.

‘Nikikosa nirekebishe’ Sindi akasoma haya maneno na kumgeukia Jerry na lile tabasamu la kukata na shoka. Akamfuata Jerry kitandani na kumtazama tu huku tabasamu likishindwa kukatika.
‘nimekusamehe’ Sindi akatamka kwa sauti ndogo na Jerry akamkumbatia.

Kuna amani ilipita kati yao kwa wakati ule, amani ambayo ambayo Jerry alitamanni idumu maisha yao yote. Sindi akatoka mule chumbani na kwenda chumbani kwa Jamila. Akamkuta anapakua
‘Sijadondosha bahasha yoyote nyeupe wakati natoka?’ Sindi akauliza wasiwasi ukimfanya akunje uso kidogo. Jamilla akatikisa kichwa kukataa na akiangaza pia huku na kule kuona kama angeiona.

Sindi akarudi kwake, akamuwekea Jerry maji ya kuoga. Alipotoka kwenda bafuni Sindi akaanza upya kuisaka ile bahasha kwa kasi ya ajabu. alikung’uta  mpaka shuka na kulitandika upya. akasimama akihema kwa nguvu akijaribu kufikiria pengine alikuwa ameiweka mahali alipopasahau.

Akainama na kuchungulia uvunguni, wakati huo Jerry naye akaingia chumbani na Sindi akanyanyuka haraka na kujibaraguza kumalizia kutandika kitanda
‘Unatafuta nini?’ Jerry akamuuliza na Sindi akakataa kuwa hakuna anachotafuta. Almanusura Jerry acheke kwa sauti namna Sindi alivyozuga kuwa hakukuwa na kitu anachotafuta.

 Wakati wa kula Sindi akaonekana kuzama mbali kimawazo na mara kadhaa Jerry alimshtua na kumuuliza kama kulikuwa na tatizo. Sindi akakataa katakata. Wakati wa kulala Jerr akatangulia kulala akimuacha Sindi anaenda kuoga nay eye akalala akijifanya yu usingizini wakati Sindi akirudi toka bafuni.

Sindi akamchunguza kama ameshalala aliporidhika akaanza upya kuangaza na kupekua kwa tahadhari huku na kule. Alichokitafuta hakukipata. Akasimama kinyonge katika kati ya chumba hiki akiwaza na kuwazua Jerry alimtazama na kutabasamu kwa vile alijua ni nini kilikuwa kinamsumbua na kumhangaisha vile.
888888888888888888888

Asubuhi ya jumapili, jua lilishakuwa na makali ya kutosha kukausha hata nguo. Nyumbani kwa Mzee Agapela kulikuwa na pilika pilika nyingi za hapa na pale. Kulikuwa na sherehe ndogo ya kuzaliwa ka Mzee Agapela na pia alitaka sherehe hiyo iwe ya kumshukuru Mungu kwa kumrejesha kijana wake nyumbani.

Mzee Agapela mwenyewe alikuwa ofisini kwake ndani ya nyumba yake akizungumza na Mwanasheria wake Dennis Mazimbwe. Walikuwa wakiongea mengi kuhusu kampuni ya Mzee Agapela na masuala mengine ya kisheria. Mazungumzo yalipoanza kumhusisha Jerry, Mzee Agapela akataka kuyakata mazungumzo.

‘sitakaa nikuelewe Kristus!... kwanini will ina jina la Fiona….yaani asilimia 80 ya mali zina jina la Fiona…kwanini?...huoni unachofanya ni kucheza pata potea…na mbali na hayo siogopi kumtuhumu kuhusika na kupotea kwa Jerry na…’ Dennis akakatizwa

‘Enough Dennis!’ Mzee Agapela akakemea kwa jazba kidogo akifumba macho na kusikilizia hali ya mapigo yake ya moyo kwenda kasi. Akajitahidi kujituliza!
‘….unachofanya ni hatari Krist…’ Dennis akashindwa kuvumilia
‘She is my wife…’ Mzee Agapela akapangua hoja
‘and what about Jenifa….Jerry?’ Dennis hakuelewa
‘najua uliandika will hii ukiwa na hasira baada ya lile tukio la Jerry na Fiona….but…eeh…huwezi…I mean…’ Dennis alishindwa hata kuweka sawa sentensi zake

‘Nakulipa ufanye ninavyotaka…. nitakapohitaji ushauri nitakueleza kwa sasa the meeting is over’ Mzee Agapela akahitimisha mazungumzo na Dennis akajikuta akilazimika kukubaliana na mteja wake. Wakaagana na Dennis akatoka mule ofisini na kuelekea sebuleni.

Wakati akiikaribia sebule akasikia akiitwa nyuma na alipogeuka alimuona Fiona akija kwa mwendo wa maringo huku akitabasamu.
‘Habari za asubuhi?’ Dennis akamsabahi na Fiona akamrembulia macho tu huku akiimung’unya midomo yake

‘Utakuja kwenye party usiku?’ Fiona akauliza akiitupilia mbali ile salamu na wakati huo akikitumia kidole cha shahada kuchora chora kwenye kifua cha Dennis ambaye aliukamata mkono wa Fiona na kuuondoa kwenye mwili wake
‘Sijajua bado…’ akajibu Dennis akitaka kugeuka na kuondoka

‘Wait’ Fiona akamzuia kwa kuushika mkono wa kushoto wa Dennis kwa kutumia mkono wake wa kushoto. aliukamata barabara kama mtu alitaka apewe usikivu kwa lazima. Dennis akauangalia ule mkono wa Fiona kuanzia pale alipomshika mpaka usoni pake. Akamtlizia macho!

‘I need to talk to you’ Fiona akasogeza uso wake mpaka na uso wa Dennis na kuyatamka maneno haya kwa sauti ya kutafuna maneno lakini iliyofika vema masikioni mwa Dennis.
‘Excuse me ma’am’ Dennis akaukwatua tena mkono wa Fiona na kugeuka. Akachapua hatua za haraka akimuacha Fiona anamtazama kwa ghadhabu iliyofichwa na tabasamu la kulazimisha.

Dennis alipoishia Fiona alielekea kule ofisini kwa mumewe Mzee Agapela. Alipoingia tu mumewe aliyekuwa ameshika kitu mkononi alivuta droo na kukiweka haraka. ingawa alifanya haraka sana lakini tayari Fiona alishaliona tukio lile.
‘Happy birthday my babe’ akamfuata mumewe na kumkumbatia kwa nyuma pale kwenye kiti aichokuwa amekaa.
‘thanks honey’ Mzee Agapela alijibu akitabasamu huku akigeuza kiti upande na kumvuatia Fiona mbele yake.

‘A shopping will do you good…’ akamwambia mkewe na kumfanya amkumbatie tena kwa furaha na kumbusu kwa fujo. Kule kukumbatiana kulileta picha tofauti. Fiona alibinua macho yake kuonyesha kile alichoambiwa wala hakikumgusa. Mzee Agapela naye alionyesha  kile alichosema wala hakikutoka moyoni. Lakini walipoachiana kila mmoja alikuwa na tabasamu lake usoni. Unafiki ulishafikia ngazi ya digrii!

Baada ya kuchangamshana kwa hiki na kile walitoka mule ofisini lakini dakika mbili baadaye Fiona alifungua mlango wa ofisi kwa tahadhari ya kutotaka upige kelele kisha akajitoma ndani na kuufunga tena kwa tahadhari. Akatembea kwa kunyata akipiga hatua kubwa kubwa mpaka ilipo ile meza ya kazi ya Mzee Agapela. Akaifungua droo aliyohisi mumewe alitumbukiza kile alichokuwa amekishika wakati ule alipoingia.

Alipoivuta droo kwa urefu wa kukaribia kuing’oa yote, akaiona fremu ya picha iliyokuwa imelazwa kwa kuficha picha iliyokuwepo. Akatabasamu na kuitoa taratibu pengine akijua ni yake. Alikosea!

Moyo ulimdunda mara mbili ya kawaida, mikono ikamtetemeka alipoigeuza na kuiona sura ya Sophia Agapela. Marehemu rafiki yake aliyemuua kwa mikono yake, marehemu mke wa Agapela. Alihisi koo likimkauka ghafla kiasi cha mate kupita kwa taabu. Akaikodolea macho ile picha na asiamini kama ndio iliyokuwa mikononi mwa mumewe. Alimuua Sophia na kumtoa machoni pa Kristus lakini kumbe hakuwa amemtoa moyoni mwa mwanaume huyu. Alihamanika!
8888888888888888888888

Sherehe ya Mzee Agapela ilileta mihangaiko mpaka kwa familia zilizoalikwa kwenye sherehe hiyo. Pamella na mama yake walikuwa katika moja ya maduka ya nguo mjini wakichagua hiki na kile. Walikuwa wakitembea taratibu Pamella akiwa na nguo walizochagua, akiwa amezining’iniza kwenye kiwiko cha mkono huku wakitembea na mama yake sehemu iliyokuwa na nguo nyingi zilizotundikwa.
‘Nataka kumjua anayetoka na binti yangu….kwanini unanificha?... I’m your mother…’
‘Najua mama wakati ukifika nitasema…’ Pamella akagoma kumtajia mama yake jina la mwanaume aliyenaye katika mahusiano. Mama yake akamtazama kwa jicho la kumrai awe wazi na Pamella akaona aweke wazi.

‘Patrick Mazimbwe’ akatamka kwa aibu kidogo
‘Mazimbwe?... ana undugu na yule lawyer Dennis Mazimbwe?’ Mama yake Pamella aliuliza kwa shauku akiacha kutembea na kusimama mbele ya Pamella.

‘Yees mom… Patrick Mazimbwe ni mdogo wa mwisho wa Dennis Mazimbwe’ Pamella alijibu swali la mama yake huku akigeukia nguo aliyokuwa anataka kuichukua. Akaitoa na kuiweka kwenye kiwiko na kumgeukia mama yake ambaye bado alikuwa akimtazama kwa mshangao wa wazi kabisa.
‘Mama nini?’ akamzindua mama yake ambaye alitikisa kichwa katika namna ya kujitoa katika ule mshangao lakini furaha yote ikiwa imetoweka usoni mwake

‘Mama!... hutaki niwe na mtu au ni nini?’ Pamella akamuuliza mama yake ambaye uso wake ulishahamanika zaidi
‘No!...no darling…tunahitaji muda tuongelee hili suala…’so you have been dating Mazimbwe and…’ akakosa maneno na kumfanya Pamella amshangae zaidi

‘Kuna nini mama?’ Pamella akaona aulize kwa marefu na mapana na mama yake akashusha pumzi na kutikisa kichwa. Jasho likionekana kumvaa lakini akajitutumua kujiweka sawa kidogo na wakaendelea kutembea.

Mwisho wa lile eneo lililotundikwa nguo kulikuwa na kioo kikubwa kilionyesha nje vizuri kabisa. Pamella alifika pale mwisho na kusimama akitazama nje huku akigeuka na kumtazama mama yake alikuwa akipekua mkoba wake kama mtu anayetafuta kitu.
Pamella akiwa amesimama pale kwenye kioo akawaona watu wawili wakiwa wamesimama nje ya duka wakitazama upande uliokuwa na nguo za kiume. Kwanza aliwatazama na kuwapuuza tu huku akigeuka na kumtazama mama yake ambaye bado alikuwa akitafuta hicho alichokuwa anatafuta.

Ghafla akili yake ikagonga ubongo wake na kuushughulisha, akayarudisha macho yake haraka kwenye kioo, upande ule waliosimama wale watu wawili wakiongea na kunyooshea midoli iliyovishwa nguo za kiume iliyokuwa kwa ndani.

Akakunja uso na kukaza macho yake, kati ya wale wanaume wawili aliokuwa anawatazama mmoja alikuwa ameshapata kumuona mahali. Ule urefu, kile kicheko na ile sura havikuwa ngeni kwake.
‘Oh my God…Nyanza!’ akapiga ukelele na kumshtua mama yake na baadhi ya wateja waliokuwa mle ndani. Akageuka na kumfuata mama yake kwa kasi akambwagia zile nguo alizokuwa amezishika na kutoka nje kwa kasi.

Alipamiana na watu kadhaa, na kukimbia kuelekea nje ya duka lile. Akaangaza na asione mtu tena zaidi ya wapiti njia wengine. Akakimbia mpaka kwenye kona ya mwisho wa duka lakini watu walikuwa wanapitapita kiasi cha kutoona dalili za uwepo wao. alichokiona Pamella hakikuwa kivuli.

Alikuwa amemuona Nyanza mwenyewe akiwa na Sakala na wakati Pamella akikimbia kuelekea ule upande aliohisi wameelekea Nyanza na
Sakala walikuwa wamesimama kwenye kibanda cha magazeti pembeni wakisoma magazeti huku wateja wengine wakiwa wamewaziba. Pamella akabaki amesimama pale nje uso ukiwa umetahayari!

Kule ndani mama Pamella alikuwa na simu sikioni, kwenye kona ya duka
‘Dennis huu sio wakati wa kufanya utani unanielewa…..?’ Mama Pamella aliongea kwa jazba
‘Patrick hatoki na Pamella…nina uhakika asilimia zote…. msichana aliyetambulishwa kwangu sio Pamella… nashangaa hiki unachoongea…. niko katikati ya majukumu muda huu…’ Dennis Mazimbwe aliongea kwa sauti ya ukali kidogo

‘I don’t have to remind you Pamella is your blood daughter and Patrick is your brother….’ aliyatamka maneno haya akiuma meno na kufumba macho kuonyesha ni kiasi gani aliumia kuyatamka na kukata simu. Jasho lilikuwa linamtoka!


…… TWENDE TU UTAYAJUA YOTE…..

1 comment:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger