Friday, July 5, 2013

SINDI.....NA LAURA PETTIE (24)

24
‘Kuna nani uko?’ Pamella akauliza akihamisha uso toka kule alikokuwa akitazama na kumuangalia Meddy ambaye naye aliurudisha uso wake haraka usoni  pa Pamella.
‘Mmh nadhani ni Dodo amengusha kitu uko jikoni’ Meddy akajibu akijibaraguza kwa kumsingizia  paka wake.


 Pamella akashusha pumzi kwa nguvu kiasi cha mabega yake kuinuka juu na kuteremka chini sambamba na pumzi ile. Akajivuta kinyonge na kuketi sofani na Meddy naye akiketi kando yake huku mara kadhaa akigeuka na kutazama kule uliko mlango wa kuingilia jikoni. Ni kama hakumini Jerry angetulia uko aliko bila kuzua kashi kashi nyingine.

‘Tatizo ni nini Pam?’ Meddy akauliza akijaribu kujituliza mwenyewe na kurudisha mazungumzo katika mstari. Pamella akamtazama Meddy kwa huruma mno, uso wake ulionyesha hali ya kukata tama

‘Jerry…’ akatamka taratibu akilaza shingo yake uoande mithili ya mtoto anayejitetea mbele ya mzazi wake huku akibetua mabega yake na kutikisa kichwa kulia na kushoto.
‘Amekufanyaje?’ Meddy akadakia huku pia akigeuza tena shingo yake na kutazama kule jikoni. Wasiwasi ulimjaa kwa kiasi Fulani akijua wazi Jerry alikuwa anasikia kila walilokuwa wakizungumza

‘Hivi Jerry ni mtu wa kumpa mwanamke simu apokee nikimpigia?’ Pamella alilalamika
‘Ehh!... nini?’ Meddy akashangaa, uso ukijenga matuta kadhaa na kisha kutoweka ghafla
‘Nimempigia simu Jerry asubuhi ya leo na simu imepokelewa na mwanamke’ Pamella akajieleza na Meddy akajikuta akiguna na kurudisha kichwa chake nyuma kidogo katika namna ya kushangaa zaidi.

 Asubuhi hiyo alikuwa na Jerry, ni mwanamke gani alikuwa amepokea simu ya Pamella? alijiuliza hili swali kichwani na asipate jibu la haraka

‘Mbona mimi nimeongea naye asubuhi….ulimpigia saa ngapi?’ Meddy akazungumza akishangaa kwani alizungumza na Jerry asubuhi sana akihisi Pamella alikuwa akitafuta cha kumlaumia Jerry.
‘Muda mfupi tu uliopita’ Pamella akajibu na kule jikoni Jerry aliipapasa mifuko ya suruali yake na kuachama mdomo kwa mshangao.

Simu yake ilikuwa imebaki kwa Sindi! Akakumbuka alipoipokea simu ya Meddy hakuirudisha simu mfukoni, aliitupia kwenye kochi ili achomekee shati. Akauma meno kwa tukio lile la kukumbuka kuwa aliisahau simu yake kule kwa Sindi!

Meddy akawa kama mtu asiyeelewa kitu!
‘Hivi hizi dharau za ghafla ghafla zinatoka wapi?’ Pamella akahoji kwa uchungu
‘..labda alikuwa mbali na Simu na Sindi akapokea simu yake’ Meddy akamtetea Jerry
‘Tangu lini amekuwa opareta wa Jerry?’ Pamella alihoji kimamlaka zaidi na Meddy akamkata maini

‘Tangu wawe wapenzi….huwezi jua wamekubaliana nini’
Pamella akacheka kwa dharau akisahau huzuni yake
‘Jerry is mine!....He is mine?... angekuwa Clarita sawa sio ile takataka isiyojua tofauti ya mkoba na pochi…excuse me!...’ Pamella akatamba na asijue Jerry mwenyewe alikuwa akimsikia

‘Twende mbele turudi nyuma Pam…wewe si una Petrick… Jerry ana nafasi gani kwako hapo?....au ulitaka awe anakulilia kila siku…na umburuze unavyotaka?’ Meddy akampasulia ukweli ambao Pamella aliumeza kwa kiburi

‘Patrick ni Patrick na Jerry ni Jerry…. mimi ndio najua nani nampenda na kwanini….Jerry loves me….na mpaka sasa sidhani kama anaweza kujishusha heshima na ku’date na kitu kama Sindi….kina nini kile kitoto?... uzuri hana, elimu hana, pesa hana, exposure hana… kwa Jerry ninayemjua mimi kumkataa mwanamke kama Clarita sababu yangu na kisha kumchkua Sindi ni sawa na kunitukana matusi yote makubwa duniani….that will never happen!’ akajiaminisha mwenyewe!

Meddy akacheka na kutikisha kichwa. Tambo za Pamella Okello zilimuacha hoi mno, alitamani sana amwambie ukweli wa hali halisi ulivyo lakini akaona ilimpasa kukaa kando na kuwa mtazamaji asiyefungamana na upande wowote.

Pamella Okello, akalikata tabasamu la Meddy kwa kubadili maongezi ghafla.
‘Fiona amekuja kuniona leo asubuhi’ akatamka kwa utulivu kama mtu aliyetaka aeleweke na hakueleweka.
‘Nini?...Fiona?!’ Meddy alitoa macho na Pamella akaitikia kwa kutikisa kichwa juu chini

‘Anataka nini?’ Meddy sasa alibadili mkao na kumtazama Pamella kwa wasiwasi kana kwamba jibu la Pamella lingemlipulia mbali. Hali ile ya hamaniko haikumtokea peke yake. Jerry kule jikoni alikaribia kujigonga kwenye mtungi wa gesi wakati akiisogea zaidi baada ya kulisikia jina la Fiona.

‘Sio anataka nini…just uliza amegundua nini?...  yule mwanamke ni pacha wa shetani Meddy…hisia zangu zilikuwa sahihi… ndiye aliyesuka mipango yote ya kumuua Jerry’ Pamella aliongea kwa kujiamini

‘Pamella!’ Meddy aliita kwa mshangao, ni kweli walikuwa wakifanya utafiti wa chini chini lakini Meddy hakuwahi kukubaliana na Pamella kuwa Fiona anahusika. Hakuiona sababu ya Fiona kufanya vile. Meddy alikuwa upande wa Jerry wakiamini Mzee Agapela ndiye hasa aliyetaka kumuua Jerry sababu ikiwa ni ugomvi wao ukiwa juu ya Jerry kumtongoza Fiona.

‘Trust me Meddy!...’ Pamella akasisitiza na Meddy akajikuta akigeuza shingo na kuchungulia kule jikoni huku akijua wazi Jerry alikuwa na hali gani uko aliko.
‘Amekwambia nini?’ Meddy akataka kujua kwa undani
‘Amemuona Jerry akiwa na gari langu…na nahisi ni ile wiki tuliyotibuana maana ndio gai alilokuwa anatumia….’ akajieleza naye uso ukionekana kujaa wasiwasi

‘Mungu wangu!....’  Meddy akakosa la kuongeza
‘Nilisema siku ile….Jerry anatakiwa atulie na afanye uchunguzi akiwa mafichoni… you guys mkaona naingilia uhuru wake…. na ile takataka isiyojua kinachoendelea ndio inayomfanya azurure ovyo hali akijua it is too dangerous out there…stupid!’ Pamella akaongea kwa mtindo wa kufoka akiwa amemuacha Meddy anamtazama na wala sielewe anachoongea. Hofu yake ilikuwa kubwa mno, aliiona vema hatari iliyokuwa mbele yake!
888888888888888888888

Wiki moja baadaye….
Magari matatu makubwa ya kisasa yaliyofanana yaliongozana barabarani yakitokea eneo la uwanja wa ndege. Kila aliyekuwa kando ya barabara aligeka kuyatazama hali wale waliokuwa katika magari yao walitoa vichwa nje kushangaa magari haya yaliyokuwa yameongozana. Msafara ule usio rasmi ulikuwa unaelekea  Oysterbay muda huo wa saa kumi jioni.

Dakika arobaini na tano baadaye msafara huo ulisimama katika nyumba moja ya kisasa na geti kufunguliwa. Mwanaume wa makamo, mwenye kimo cha kutosha, mweusi ti mwenye sura nzito kidogo iliyojaa umakini usioeleweka aliteremka baada ya kufunguliwa mlango na msaidizi wake.

Alisimama na kuitazama nyumba ile iliyokuwa mbele yake huku akitabasamu na kutikisa kichwa juu chini mara kadhaa kuashiria kuridhishwa na hali aliyoiona. Mzee yule akifuatiwa na wasaidizi waliokuwa na mizigo pamoja na mkewe aliyekuwa kando yake waliingia ndani na kupokelewa na mwanamke mtu mzima aliyekuwa amevalia sare za wasaidizi katika nyumba ile.

Mzee akaingia na kuikagua sebule yake huku akitabasamu kisha akakifuata kiti na kuketi, wakati huo wasaidizi wakikimbizana huku na kule. wengine wakiingiza mizigo na wengine wakihakikisha hali ya usafi pale alipoketo bosi wao ili mradi kulikuwa na pilika pilika. Mzee huyu alikuwa Mzee Okello!

‘Pamella yuko wapi?’ Mzee akauliza na mkewe akichungulia kordoni kana kwamba angemuona huyo Pamella. Yule mama mtu mzima akainamisha kichwa chini kama mtu aliyekosa jibu kwa wakati ule.
‘Sijui nimesikika?’ Mzee Pamella akakazia swali lake
‘aahm…Pam… amehama hapa’ Yule mama mtu mzima akamung’unya maneno lakini alisikika vizuri tu.

Mama yake Pamella akamtazama mumewe, na mumewe akamtazama mfanyakazi wake katika namna ya kutomuelewa
‘Amehama?!... binti yangu anaondoka nyumbani anatangatanga nje na nyie mpo tu humu ndani…. hamniambii?...kwa hiyo mnaishi wenyewe tu humu ndani’ Mzee Okello akauliza jibu na yule mtumishi akaitikia kwa kichwa akionyesha woga utadhani yeye ndiye aliyemuahamisha huyo Pamella.

‘Gadna!....Gadna!’ Mzee Okello akapaza sauti na kumuita mfanyakazi wake ambaye pia ni dereva wake. Gadna akafungua mlango na kuingia ndani
‘Naam Mzee’ akaitikia wito, akiwa kasimama kwa heshima mbele ya bosi wake
‘Two hours from now…nataka kumuona Pamella humu ndani…. and you…’ akamuonyeshea kidole yule mtumishi mtu mzima na kumatzama kwa sekunde kadhaa

‘…you are fired!’ akatamka kwa sauti kali na kusimama. Mama wa watu akaduwaa na hapo hapo akaweweseka na kutetemeka akimtazama Mzee Okello alivyokuwa akiiacha Sebule na kupandisha ngazi kuelekea chumbani.

Mama Pamella akasimama pia na kumatazama yule mama mtu mzima kwa huruma. Ni kama vile hakuwa na mamlaka wala maamuzi ya kubadili hali ile. Akasikitika na kumfuata yule mtumishi akamkumbatia. Kazi ndio ilishapotea!
8888888888888888888888

Sindi Nalela alikuwa chumbani kwake akimalizia kukunja nguo alizotoka kuanua na kuzitia katika sanduku. Akachukua shuka moja na kutandika kitandani huku akitikisa kichwa chake na kuonekana kuufurahia muziki uliokuwa ukisikika redioni. alitabasamu mwenyewe na kuufuatisha hali akizunguka kile kitanda na kuchomekea shuka.

Wakati akivalisha kava za mito ya kulalia, mlango ukafunguliwa na Jerry akaingia na kimfuko chake cha Rambo kikiwa na fungu la mchicha na samaki waliofungwa kwenye  kipande cha gazeti.
‘Umewahiiii…’ Sindi akamtania akiachana na mto wa kulalia na kwenda kumpokea Jerry.
‘Hebu washa feni aisee…joto kweli’ Jerry akalalamika na Sindi akamuwashia Feni iliyokuwa imesimamishwa kando ya kitanda.
Wakati akiketi kitandani akagundua pazia jipya lilikuwa linaning’inia mlangoni
‘Umenunua pazia jipya?’ akamhoji Sindi aliyekuwa anachota maji kwenye wenye ndoo na kumimina kwenye sifuria
‘Lile lingine lilikuwa baya…’ akajitetea akitabasamu
‘hili bdio baya sasa dah…’ Jerry akambeza na sindi akachota vijimaji kwenye mkono na kumrushia Jerry pale kitandani. Jerry akayakwepa akicheka.

‘unataka maji ya moto sana?’ Sindi akamuuliza akiajiandaa kwenda nje kuyachemsha kwa ajili ya Jerry.
‘kwanza hata usichemshe kama naoga saa hizi …kuna joto mno’ Jerry akatoa wazo na Sindi akarudi kuyamimina maji kwenye ndoo
‘Basi ngoja nikuchotee kisimani hapo’ Sindi akataka kutoka tena
‘Njoo kwanza bwana…’ Jerry akamshika mkono na kumvutia pale kitandani

Sindi akamkalia Jerry kwenye paja huku mkono wake wa kulia ukizunguka mgongoni na kutulia bega la kulia la Jerry na mkono wa kushoto ukivitumbua tumbua vijiupele pajini mwa Jerry. Mahaba juu ya mahaba!
‘Nimekuletea zawadi’ Jerry akainua uso na kumwambia Sindi ambaye tabasamu lake lilitosha kumfanya Jerry ajisikie bukheri wa afya
‘Zawadi gani..’ Sindi akauliza akiiuma uma midomo yake.

Jerry akaufungua ule mfuko na kutoa kibahasha cheupe. akampatia Sindi ambaye aliutoa ule mkono wake wa kulia mgongoni mwa Jerry na kuifungua bahasha. Akatoa nguo ya ndani nyeupe. Sindi akacheka na kujiinamia akizidi kucheka
‘Yaani unafanya kazi uko huku unawaza kuninunulia chupi khaaa…’ Sindi akatania
‘Yaani hata nikiwa wapi akili yangu inakuwaza tu… nakuwaza tu…’ Jerry akajibu naye akianza kumpapasa Sindi kimahaba.

Sindi Nalela alishaingia mtegoni, hakutamani kukutana na Nyanza tena. Si kwamba hakumpenda, bali hakujua angemtazamaje na angemwambia nini kuhusu ahadi ya kuwa wake peke yake. Ngome aliyomuahidi ilishabomolewa. Alitembea na hatia moyoni mwake lakini pia moyo huo huo ulifunguka kwa kasi ya ajabu na kumpkea Jerry Agapela! akimpenda maradufu ya alivyompenda Nyanza!
8888888888888888888

Kijijini aliko Nyanza Mugilagila, maisha yalikuwa yanaendelea pamoja na yote yaliyotokea. Nyanza alikuwa akimalizia kibarua chake cha kulima na taratibu alisimamisha jembe na kutuliza macho ule upande ambao jua lilikuwa linazama. Alitulia vile akilitazama lile jua kana kwamba alitaka kulipa salamu zimfikie Sindi popote alipo.

Moyo wake ulikuwa na maumivu, moyo wake ulikuwa na hekaheka kila siku iliyoenda kwa Mungu. Akainama na kupinda mgongo kumalizia kazi yake. Wakati akifanya yote haya Alma rafiki kipenzi wa Sindi alikuwa amesimama nyuma ya mti mkubwa akimtazama Nyanza kwa huruma. Roho yake ilikuwa inataka kufanya jambo ambalo alihisi lingemletea ahueni. Alitaka kumwambia Nyanza ukweli wa alipoenda Sindi Nalela!

Akajishauri pale nyuma ya mti kwa dakika kadhaa kisha ataratibu akajitokeza mbele ya Nyanza ambaye wala hakuwa na habari naye. Aliendelea kulima huku akimsifu Mungu kwa nyimbo za mapambio. Alma akapiga hatua za kutetemeka na kumfuata Nyanza. Alitaka kusema yote jioni bila kujua zahma ambalo angelizua!

Wakati Alma akitaka kukiri, Huku mjini Wazee wawili walikuwa simuni wakizungumza na bila kujua wake zao walikuwa wamebanisha mahali kila mmoja mahali pake wakiwasikiliza.

Mke wa Okello alikuwa akimsikiliza mumewe kwa kuibia hali kadhLIKA Fiona Agapela alikuwa amebanisha mlangoni akimsikiliza Mzee Agapela.
‘Jerry hawezi kuwa mfu…. come on…. harusi ya kifahari niliyonayo kichwani haiwezi kufutika kwa kitu cha kufikirika’ Mzee Okello alizungumza kwa kujiamini
‘….na hatuwezi kumpa Pamella matumaini kwa kuongea naye kuhusu ndoa wakati hatujui alipo Jerry…. it is not that easy kukubali my son is still safe and sound…. it os hard Okello!’ Mzee Agapella aliongea kwa uchungu akishusha pumzi.

Fiona aliyekuwa akisikiliza alitoa macho na kuduwaa pale mlangoni. Haya yalikuwa mapya mno masikioni mwake.

….. MAMBO NDIO YAMEANZA KUCHANGANYIA.... 

3 comments:

  1. dada una kipaji keep it up! frm salehe masoud wa ilala n tha'ts ma really name

    ReplyDelete
  2. Asante sana Salehe....nimefurahi mno kujua nimerunga hadithi kwa jina la mtu anayeexist kabisa kiukweli hahahahaaa...pengine siku itakapotakiwa kuwa movie...itabidi uchukue nafasi ya huyu Salehe...i hope unajua kuigiza!!

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger