3
SEHEMU YA TATU....
Nyanza alikimbilia bondeni kidogo kulikokuwa na vijana
wakivua samaki, akawapigia mbija na kuwapa ishara ya kumfuata. Sindi
alikimbilia kijijini na kukusanya watu waliokuwa karibu na baada ya dakika kumi
na tano Jerry alishazungukwa na wanakijiji, wengine wakimtazama kwa mbali,
wengine wakijaribu kumuinua na wengine wakishauriana cha kufanya.
Wakiwa bado katika hekaheka ya kumhoji yeye ni nani na
imekuwaje, Jerry akapoteza tena fahamu palepale na taharuki ikazuka kwa hofu
kuwa pengine amekufa.
‘hivi Mzee Sagati yupo saa hizi?’ mtu mmoja aliyekuwa
amemshikilia Jerry akamuuliza mwenyekiti wa kijiji.
‘Atakuwepo tu….leo wanagawa mbolea tangu asubuhi’ mwingine
akajibu na mtoto mdogo wa kiume akiagizwa akimbie kwenda kumuita mwenyekiti.
Mwingine akaagizwa alete baiskeli ya kumbebea toka eneo lile
na hapo hapo wengine wakishauri akimbizwe zahanati huku wengine wakifikiria
kuita polisi. Mabishano yakawa hayaishi, kituo cha polisi kilikuwa mbali sana
na kijiji kile, jengo la kituo cha polisi kilichokuwepo hapo kijijini
kilishageuka pagale baada ya kukosa polisi.
Mabishano yao
yakatulia alipowasili Mwenyekiti na wazee wachache ambao waliamua kumpeleka
nyumbani kwa mwenyekiti wakati wakitafuta namna ya kumfikisha zahanati.
Baiskeli ikaletwa na Jerry akapakizwa na kushikiliwa mpaka
kijijini. Alilazwa kwenye mkeka nje ya nyumba na mtu akatumwa kumuita mama Alma
ambaye ni muuguzi aje kumtazama.
Kufika kwa mama Alma
kukaongeza umati wa watu pale nje ya
nyumba ya Mzee Sagati, watu wakiwa wamesimama makundi makundi, wengine na
majembe, wengine na magunia na makapu huku wengine wakiwa mikono mitupu. Baada
ya kumtazama na kukitazama kidonda chake. Mama Alma alishauri mgonjwa apelekwe
Zahanati haraka baada ya ile huduma ya kwanza aliyopewa.
Jerry akabebwa tena na safari ya Zahanati ikaanza. Msafara wa
kumpeleka hospitali ulikuwa na watu sita. Mwenyekiti, Mama Alma, Nyanza na
vijana wenzake watatu. Pale Zahanati alipokelewa na huduma zikaanza akiwa chini
ya uangalizi wa Mama Alma muuguzi wa siku nyingi wa Zahanati ile. Mpaka saa
mbili usiku, hali ya Jerry ilikuwa na nafuu kubwa huku mwili wake ukiwa
umekunywa drip za maji na dawa za kutosha.
Asubuhi ya siku iliyofuata Mama Alma alimtaka binti yake
aandae uji na kuupeleka hospitali kwa mgonjwa yule aliyeokotwa hapo kijijini. Alma
alifanya kama alivyoagizwa na mama yake huku akimtafuta
Sindi amsindikize uko zahanati. Saa moja baadaye Alma
alimpitia Sindi na wakatoka pamoja kuelekea Zahanati.
Walipoingia ndani ya wodi aliyolazwa Jerry walimkuta Mzee
Sagati akizungumza na Jerry ambaye sasa aliweza kuketi kwa taabu baada ya
kurudiwa na fahamu muda mfupi tu uliopita.
Mzee Sagati alipomaliza kumuhoji alitoka kwa kupishana na
akina Alma aliyemfuata Jerry kwa
wasiwasi kidogo akionekana kumtazama kwa kuibia ibia. Alma
alitua mfuko uliokuwa na chupa ya uji juu ya stuli ya wastani iliyokuwa kando
ya kitanda cha mgonjwa.
‘pole…’ Alma
alitamka kiuoga kwa sauti ya chini ambayo hakuwa na hakika kama
ilisikika vyema au lah, akijaribu kujizuia kutabasamu na hapo hapo akitaka
kutabasamu pia. Jerry akaitikia kwa kichwa, akiuma meno na kufumba macho kwa
uchungu wakati akijitahidi kuketi vyema.
‘Nikumiminie sasa hivi?’ Alma
akauliza akimuonyesha Jerry chupa ya uji na Jerry akaitikia kwa kichwa tena uso
ukiwa bado na makunyanzi ya maumivu.
kadiri alivyokuwa akizidi kumtazama Sindi ndivyo alivyojikuta
akiyasahau maumivu aliyokuwa nayo ubavuni. Akashindwa kuvumilia alipomuona
Sindi akicheka na kuzungumza na yule mtoto ngonjwa.
‘Yule binti ni nani?’ akauliza huku macho yake yakiwa kwa
Sindi na Alma
aliyekuwa akihangaika kuupooza uji akageuka na kutazama kule alikokuwa
akiangalia Jerry. Kwa tabasamu pana akageuza kichwa na kumuuliza Jerry ambaye
alishindwa kuyaondoa macho yake kwa Sindi hata
kwa sekunde kadhaa
‘Nani Sindi?...’ Alma
akauliza katika namna ya kupata uhakika
‘ Anaitwa Sindi?...huyo anayezungumza na mtoto’ Jerry
akamnyooshea kidole Sindi na Alma
akageuka tena kutazama kule alikoelekeza kidole. Akajibu kwa kutikisa kichwa
‘jina zuri’ Jerry akaunda tabasamu ambalo kwa wakati ule
lilikuwa tabasamu la kwanza tangu akumbwe na masaibu ya dunia yaliyomkuta. Alma
naye akatabasamu huku akimkabidhi Jerry
bakuli la uji. Akalipokea na kulipeleka mdomoni kwa taabu kidogo.
Sindi alimaliza mazungumzo na yule mama na taratibu akajongea
mpaka kitandani kwa Jerry. Tabasamu pekee lilitosha kumfanya Jerry ajimwagie
uji na hivyo kupiga ukunga wa uchungu na Alma
akahangaika kumsaidia kuufuta ule uji uliommwagikia usifikie bandeji aliyokuwa
amefungwa ubavuni.
‘oooh pole..’ Sindi
alilipokea bakuli la uji wakati Alma
akimfuta ule uji uliommwagikia. Kikafuata kicheko cha chini chini kati yao .
Hali ilipotulia Jerry akamtazama Sindi usoni wakati akilipokea bakuli la uji na
Sindi akakwepesha kwepesha macho kama mtu aliyepoteza
kujiamini.
‘Sisi tunaondoka…atakuja nesi mama mtu mzima na ndiye ataondoka na hivi vyombo’ Alma
akatoa udhuru haraka sana akitaka
yeye na Sindi watoke eneo lile.
‘Unaitwa nani?’ Jerry akamuuliza Alma
ambaye alijikuta akicheka na asijue kilichomchekesha
‘Alma …’ akajibu
huku aibu za kike zikimzengea na Jerry akaitikia kwa kichwa, pengine akitamani
kuuliza maswali zaidi lakini ugeni ulimzuia. Hawa mabinti wakatoka nje ya wodi
na kuanza kuondoka eneo la zahanati.
Kule ndani ya wodi Jerry aliuma meno tena wakati akijikunja
na kulitua bakuli la uji juu ya ile stuli. Akashusha pumzi na kufumba macho
‘Sindi…’ akatamka kwa sauti ya chini lakini iliyojaa mwangi
kichwani pake. Hakujua kwanini alikuwa amelitaja jina lile, alichojua lilimpa
faraja kwa kiasi Fulani.
8888888888888888888888
Jijini Dar, familia ya Mzee Agapela ilikuwa katika hekaheka
kubwa sana . Matumaini ya kupatikana
kwa Jerry yalikuwa yanazidi kufifia siku hadi siku. Familia ilikuwa imeingiwa
na kiwewe cha kutosha hasa baada ya kiatu chake alichovaa mara ya mwisho
kuonekana pasipo yeye wala daliliza uwepo wake eneo lile kilipokutwa kiatu.
Mzee Agapela aliikumbuka vema asubuhi ya siku aliyoonana na
mwanawe kwa mara ya mwisho. Alipita pale nyumbani kuwaaga kuwa alikuwa na
safari ya kuelekea morogoro kikazi. Hakupitiwa hata na hisia kuwa safari ile
ndio ingewaletea sakata kama lile. Alikuwa peke yake
garini, pengine angelikuwa ameongozana na mtu labda ingelileta hali ya
matumaini kwa kujua kwanza mwenzake yuko wapi.
Masaa sita baadaye gari lake
liliokotwa pembezoni mwa barabara
likiwa limeegeshwa na milango ikiwa haijafungwa, hakukuwa na dalili ya mtu
ndani. Nyaraka za kazi na mizigo ya Jerry ikiwa kama
ilivyokutwa na askari wa doria. Uchunguzi ulionyesha kulikuwa na kashikashi
wakati wa kumuondoa eneo lile.
Hapakuwa na kijiji jirani wala dalili za watu kuweka makazi
hata ya muda mfupi. Mazingira ya tukio lile yaliacha maswali mengi zaidi
yaliyokosa majibu. Polisi walikuwa wakiendesha uchunguzi wako kwa kadri
walivyoweza.
Ilishatimia wiki moja na siku kadhaa tangu Jerry Agapela
aripotiwe kupotea jijini na yeye ndio alikuwa anatimiza siku ya nne tangu
aokotwe pale kijijini. Tayari alishatoka zahanati na alikuwa akiishi nyumbani
kwa Mwenyekiti. Usiku ule aliotoka hospitali Jerry alimweleza Mwenyekiti ukweli
wa yaliyomtokea na kama binadamu Mwenyekiti alimpa
nafasi Jerry ajipange kukabiliana na lile lililokuwa mbele yake. Alimuonea huruma kijana huyu!
Jioni hii Mzee Agapela alikuwa ameketi sofani akiwa mwenye
mawazo tele kichwani. Mkewe alisimama
mbali kidogo akimtazama na akitamani pia kujua kilichokuwa akilini mwa mumewe.
Akatembea taratibu na kumfuata, akaketi kando yake na kumtazama mumewe kwa
upendo
‘Unawaza mno mume wangu….polisi wamesema tusubiri kama
ni watekaji si watasema wanalotaka’ mkewe aliongea polepole na Agapela
akamtazama tu asichangie ile hoja wala kukubaliana naye
‘leo hujala tangu asubuhi…. kazi hazifanyiki….kila mtu ana
hofu na uchungu ila ndio tumeweka imani yetu kwa Mungu…’ Mkewe alizidi kujaribu
kumtia moyo na akatikisa kichwa kulia na kushoto bila tafsiri rasmi kuwa
alikuwa anapinganana maneno ya mkewe au alikuwa akisikitika. Ukweli wa ishara
ile ukabaki moyoni mwake. Akanyanyuka na kuondoka pale sofani akimuacha mkewe
anamtazama mpaka alipotokomea.
Fiona, mke wa Agapela alisimama kwa kunyata na kuchungulia kwenye
ngazi zilizobebana kuelekea ghorofani. Alisikilizia kwa muda na aliporidhika
akashusha pumzi na kutoa simu yake iliyokuwa kwenye bukta aliyovaa ndani ya
sketi yake. Kwa tahadhari akasogea kwenye kona huku akiwa na wasiwasi na
kubinyeza namba kadhaa kwa haraka. Akaiweka simu sikioni, macho yakimcheza
cheza na akizitazama zile ngazi mara kwa mara. Namba aliyopiga ilipokelewa
Mkono wa kushoto ulikuwa umeshikilia simu iliyokuwa sikio la
kushoto hali mkono wa kulia ulikuwa ukiziba mdomo katika namna ya kuzuia sauti
isisikike mbali na pale alipokuwa amesimama
‘Mmeshampata?...’ aliuliza kwa sauti cha chini akiwa na
wasiwasi
‘….nini?....hebu kwanza nini…’ aliuliza kwa mshtuko, uso
ukijaa ndita na macho kumtoka, wakati huo huo sauti ya kufunguliwa kwa mlango
ikisikika ghorofani. Akaikata simu kwa kiwewe na huku akihema na kuirudisha
alikoitoa. Akatembea kwa haraka kuzifuata ngazi, akivifuta viganja vya mikono yake katika
sketi ya kitenge aliyokuwa amevaa. Alitambaliwa na hofu, hofu ya kubumburuka
kwa mpango wake. Hofu hiyo ndio iliyomfanya
asitazame alikokuwa anakanyaga na kujikwaa kwenye ngazi zile na
kuserereka, akatua chini kwa kishindo. Huku akitumia jicho moja kuchungulia
kule alikokuwa mumewe na hapo hapo akikunja uso kwa maumivu. Ikamdibi tu
ajifanye ameishiwa nguvu ghafla kwa kutulia palepale chini alipoanguka.
Mumewe aliyekuwa akianza kuteremsha ngazi kueleka chini
alimuona Fiona akianguka na hivyo akakimbizana kushuka na kumuwahi huku
akimuita Jenifa binti yake aje kutoa msaada.
‘nini mama?....’ Agapela alihoji alipomfikia mkewe hali
kadhalika Jenifa akitoka chumbani kwake mbio na kuja kusaidiana na baba yake.
‘Mama unawaza mno jamani….’ Jenifa alimlalamikia Fiona ambaye
alijitahidi kulegea kadiri alivyoweza.
888888888888888888888888
‘a…e…i…o..u…haya anza tena…’ sauti ya Sindi ilisikika ndani
kijumba kidogo cha udongo ikifundisha watoto kusoma na wao wakimfuatisha nyuma
kwa sauti za kuvuta. watoto walikuwa wamekalia vitofali vidogo vidogo wakiwa na
madaftari yao .
‘hamnisikilizi nitawachapa….mnaangalia nini uko nje’ Sindi
aliwakemea wanafunzi walijikuta wakitazama sehemu moja kwa pamoja.
Akaguna na kugeuka kutazama uko walikokuwa wakitazama.
Akakumbana uso kwa uso na Jerry aliyekuwa anatabasamu.
‘Oh! karibu…’ akamkaribisha na Jerry akacheka na kushukuru.
‘Hamjambo?’ akawasabahi wale watoto
‘Hatujambo… shikamoooo mwalimu’ wakaitikia kwa pamoja na
kufanya Sindi na Jerry wacheke kwa pamoja
‘Marhaba watoto wazuri…’ Jerry alijibu akisogea zaidi na
kuegemeza mikono yake iloe sehemu ya dirisha. Akaanza kuzungumza nao
akiwachekesha hapa na pale na mwisho Sindi akaamua kufunga darasa na kuwaruhusu
wanafunzi wake waondoke.
Alikusanya vitu vyake na kutoka nje ya kile chumba cha
udongo, Jerry naye akiwa ameshazunguka toka kule dirishani hadi mlangoni
‘Wanakulipa?’ akamuuliza Sindi wakati akisindika mlango wa
bati sehemu iliyotumika kama mlango
‘kiasi kidogo tu….’ akajibu akigeuka na taratibu wakianza
kuondoka eneo lile kuelekea nyumba za wanakijiji zilipo. Walizungumza wakicheka
na kutaniana hapa na pale. Jerry akionekana kumfurahisha Sindi kwa kila
aliloongea.
Wakati wakikatiza sehemu yenye miti na pori
dogo, Nyanza aliyekuwa akikata kuni aliwaona. Akajibanza kidogo na
kuwachungulia namna walivyokuwa wakizungumza na kucheka. Jerry akimtolea
iuchafu vya miti vilivyomdondokea kichwani wakati wakipita sehemu ile. Nyanza
alitulia na panga lake mkononi ,
akihisi damu yake ikiongeza kazi mwilini, akihisi jazba zikianza kumtawala
lakini akajipa nafasi ya kuwatazama wakipita eneo lile bila kuwabughudhi.
Wivu uliomtomasa moyoni ulimfanya amtazame Jerry kwa chuki
pasipo hata kujua ni nini walikuwa wakiongea. Kitendo cha Sindi kuonekana
mwenye furaha, akicheka na kushiriki mazungumzo yao
kwa furaha kilimfanya Nyanza ahisi Jerry hakuwa mtu mzuri kwake. Alichomeka
panga kwenye mzigo wake wa kuni na kuanza kuwafuatilia kwa kunyatia nyuma
…..FIONA ANA SIRI GANI?....HOFU YA NYANZA INAHISTAHILI?.....
NI NINI KIMEMPATA JERRY?
No comments:
Post a Comment