Sunday, July 28, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (31)

31
Sindi Nalela aliiona wazi hali ya kubabaika aliyokuwa nayo Jerry pale juu yake. Akatumia mkono wake wa kushoto kumsukumia kando Jerry na kuanza kuikusanya khanga yake iliyokuwa imeshatolewamaungoni. Muziki wa simu wa simu ukakatika na Jerry aliyekuwa ameangukia chali kando ya Sindi hakutamani hata kunyanyuka pale kwenda kumjua mpigaji. alimshamhisi!


Sindi akaketi kikato, akimtazama Jerry vile alivyokuwa amelala chali akiitazama dari.
‘Umenunua simu mpya?’ akamtwanga swali mwenzake uso ukiwa umeshajenga shari
‘ Sindi…. sitaki kugombana na wewe muda huu’ Jerry akakwepa swali na asijue alimkera Sindi kiasi gani.  Akiwa bado anaitazama dari vilevile akamshuhudia Sindi akitoka pale kitandani na kuufuata mlango. Hisia zake zikamwambia alikuwa akiifuata simu. Akajikuta naye akinyanyuka na kumfuata Sindi kwa kasi.

Taa ikawashwa na Sindi akainyakua suruali aliyohisi ilikuwa na simu. Jerry alishamfikia na kutaka kumzuia.
‘Niachie…Jerry niachie..’ Sindi alimpandishia kwa sauti ya ukali asijali usiku ulishakuwa mnene kiasi. Aliukwatua mkono wa Jerry uliotaka kumgusa huku akiiweka ile suruali mgongoni ili Jerry asimpokonye

Ikazuka purukushani ya kunyang’anyana ile suruali na wakati huo simu ikaanza tena kuita na Jerry akajua sasa ilimpasa kutumia nguvu kidogo ili kuipata ile simu. Akambana Sindi kwa nguvu na kumnyang’anya ile suruali, wakati akiivuta ili kuitoa mikononi mwa Sindi Simu ikadondoka sakafuni katikati yao na jina la mpigaji likaonekana wazi.
‘Pam!’ Sindi akaita kwa mshangao na hasira zikiongezeka

Jerry akajua Sindi angeiokota ile simu na kuibamiza kama ilivyo kawaida yake lakini haikuwa hivyo. Sindi aliiruka ile simu na kwenda kuketi kitandani. Akijiinamia na kutulia kama mtu anayesikilizia maumivu. Jerry akajua ameshaharibu. akashindwa kuipokea ile simu na akashindwa na akashindwa kumfuata Sindi pale kitandani.
Simu ilipoacha kuita, Jerry naye akairuka na kumfuata Sindi. Akaketi pembeni yake na kutaka kusema maneno ambayo yalimpotea pia. Kukaa kando yake kukamfanya ajue Sindi alikuwa analia. Akaumia sana!

‘Jerry…’ Sindi akainua uso uliolowa machozi na kumtazama Jerry
‘Nimekukosea sindi’ akajitetea
‘Hivi kweli unanifanyia hivi?.... kweli?’ Sindi akauliza machozi yakimporomoka
‘SIndi sikiliza mama…’ akatafuta cha kuongea
‘Nisikilize nini?.... hii mara ya ngapi tunagombana sababu ya huyu Pam?’ aliuliza kwa sauti ya kilio akiusukumia mbali mkono wa Jerry uliotaka kumbembeleza

‘Nimechoka!....Nimechoka!...Mungu wangu nimechoka’ Sindi aliongea kwa hasira na uchungu uliochanganyikana na wivu. Akanyanyuka ghafla na kulifuata sanduku lake. Jerry hakumuelewa!

Alipoanza kukusanya nguo zake na kuziweka kwenye sanduku ndipo Jerry aliposhtuka na kumfuata kwa kasi.
‘Sindi!...unafanya nini hiki?...unaenda wapi?’ Jerry akauliza kwa hamaki
‘kwani ulinitoa wapi?....uliniokota barabarani?...au ulininunua sokoni?’ Sindi aliuliza kwa kiburi akifuta machozi na kuendelea kukusanya vitu vyake na kuvishindilia kwenye sanduku.

Jerry akaona mambo yalikuwa yanazidi kuwa mabaya. Akamzuia Sindi asiliguse lile sanduku na ndio hapo ugomvi ulipochachamaa
‘Naondoka…nenda kamchukue huyo Pam umlete hapa ukae naye kama ataweza kuvumilia umalaya wako na umaskini huu…’ Sindi alifoka akikaza khanga yake kifuani
‘huendi popote Sindi….unanisikia?’ Jerry alijibu kwa sauti ya kuonyesha mamlaka

‘Sijakusikia na sidhani kama nataka kukusikia tena….na kama yupo mwanaume anayeweza kuniamrisha nimsikilize ni Nyanza peke yake sio wewe’ Sindi akaropoka kwa jazba. Kwa sekunde mbili masikio ya Jerry yalivuma kwa kulisikia lile jina la Nyanza.
‘Umesemaje?’ uvumilivu wa Jerry ulishafika kikomo kwa kiasi kikubwa
‘Sikupendi na sijawahi kukupenda na sijui ni shetani gani alinivaa nikakuacha unibikiri… ilikuwa heshim ya Nyanza so wewe na kamwe usingeku…’ Kimya cha ghafla kikapita kati yao baada ya sauti ya mlio wa kofi kusikika.

Kule mlangoni wapangaji nao wakatazamana
‘Kampiga..mama yangu!...ngumi sasa’ wakapokezana kuitikia pale mlangoni wakitega vizuri masikio. ule ukimya ulifuatiwa na sauti ya Sindi akilia kwa kwikwi na kisha kelele za kukataa kuguswa

‘Usiniguse Jerry….unanipiga nimekosa nini?....niachiee’ Sindi aliongea kwa sauti ya la mgambo likilia kuna jambo. Wale wapangaji pale mlangoni waliposikia vitasa vya mlango vinafunguliwa kila mtu alishika njia ndani ya sekunde. Sindi akatoka kordoni na kuufuata mlango wa chumba cha Jamila. Hakugonga wala kungoja afunguliwe, alikinyonga kitasa na kuingia ndani akimkuta Jamil amesimama chumbani kwake naye akisikilizia ugomvi wao.

Jerry naye akamfuata Sindi hapo kwa Jamila lakini akazuiwa mlangoni na Jamila mwenyewe. ikawa Jerry  amesimama mlangoni akimwangalia Sindi aliyekuwa ameketi kitandani akilia kwa hasira huku jamila akiushikilia mlango nusu ili Jerry asiingie.

‘Nahitaji kuongea naye’ Jerry akajieleza, maskini hali zote za kuchanganyikiwa zikiwa zimemtembelea na kuweka makazi. hata yeye hakutarajia angeacia lile kofi kwa Sindi!
‘Hamtaweza kuelewana sasa hivi wewe umepandisha makata mwenzio kaandisha subiani… mtatoana nyongo bure….kalale kesho inshallah mtakaa meza moja…usiku huu mtachomana hata visu’ Jamila akaongea akimtazama Jerry usoni, Jerry mwenyewe akimtazama Sindi kule ndani.

‘Jerry!’ jamila akamzindua na kurudi nyuma kidogo kisha akaufunga mlango na kumuacha Jerry pale mlangoni. Alimama kama bwege akitazama chini na akiisikia vema sauti ya Jamila ikimtaka Sindi aache kulia. Alisimama pale kwa sekunde takribani tano akili yake ikishindwa kuamua cha kufanya. alipoinua uso na kuitazama ile kordo aliwaona baadhi ya wapangaji wakiwa wamesimama kwenye vizingiti vya milango yao wakimtazama. Akahisi soni!

taratibu akajiondoa pale mlangoni na kurudi chumbani kwake. Simu iliyoleta tafrani ikiwa pale pale chini. Akaiokota na kuitazama. Moyo ulimuuma mno. Sawa, alikuwa na akimpenda pamella lakini tangu awe naye hajamgusa Pamella kimahaba, amejizuia mno kwa ajili yake. aliumia zaidi kwa Sindi kumtaja Nyanza. midomo ikammwemweseka wakati akisigina magego yake na kufanya mishipa ya taya ichezecheze. Akafumba macho na kuusikilizia ule uchungu.
‘To hell with Nyanza…’ alipayuka kwa hasira akitetemeka
8888888888888888888888

Asubuhi iliyobarikiwa wingu lililopunguza makali ya jua, ilikuwa njema kwa Meddy. Alikuwa akifnya mazoezi ya kukimbia asubuhi hiyo ya jumamosi huku akiwa na chupa ya maji mkononi. Kikawoshi alichokuwa amevaa kililowa jasho sehemu ya kifuani kutokana na zoezi alilokuwa amepiga. alikimbia taratibu akiwa na headphones masikioni akisikiliza alichokuwa nasikiliza.

Wakati akiikaribia nyumba yake. Gari lililokuwa likija mbele yake lilimfanya apunguze mwendo na hatimaye kutembea kabisa kabla ya kusimama. Gari lile lilifunga breki kwenye geti la nyumba yake ambako yeye pia alishalifikia na kusimama.
‘I guess mmefight again…’ aliotea akitabasamu baada ya Jerry kushusha kioo
‘witch!...You are damn right’ jerry kajibu na kumfanya Meddy sasa acheke kwa sauti. mlinzi aliyekuwa anafungua geti aliikamilisha kazi yake na kumruhusu Jerry aingize gari ndani.

Jerry aliegesha sehemu ya maegesho na kuteremka, akaja kusimama nyuma ya gari na kuliegemea gari lake akimtazama Meddy aliyekuwa anaongea na mlinzi kabla ya kumfuata pale alipokuwa amesimama. huku akinywa maji yale aliyokuwa ameshika akimfuata Jerry na kusimama mbele yake. Wakati huo akitoa zile headphones na kumtazama Jerry kwa tabasamu
‘mpaka muoane tayari nitakuwa nimehitimu digrii ya masuala ya mahusiano na ugomvi’ akamtania tena rafiki yake ambaye hata kutabasamu hakuweza
‘I hit her’ Jerry akasema kwa sauti ya masikitiko na uso wake ukionyesha majuto
‘What!..mmh!..’ Meddy hakuelewa haraka, setensi ya Jerry ilikuwa na mana zaidi ya moja na Jerry aliliona hilo, akaweka sawa.

‘Sikutarajia ningemuwasha kofi Sindi…sijawahi kumsukuma mwanamke maishani mwangu let alone kumuwasha kofi…’ akaelezea tukio na kujitetea hapo hapo. Meddy akaweka ile chupa ya maji juu ya boneti ya gari aliyoegemea Jerry kisha naye akasimama kama Jerry na kuliegemea gari huku akigeuza shingo na kumtazama Rafiki yake kwa umakini mkubwa.

‘….najua nimekosea but it was …it was…you know…’ maneno hayakupatikana kujazia sentensi yake na Meddy akaijazia alivyojua mwenyewe kichwani.
‘Kwanini usimwambie ukweli Sindi?....muweke chini mwambie kila kitu kuhusu wewe….huwezi ishi maisha aina mbili ndani ya jiji moja na yasifikie tamati… hivi unadhani Sindi akigundua unamchezea akili atakupenda tena?’ Meddy alimuuliza akimkazia macho

‘na ameshakiri hanipendi…’ akaitikia
‘Na ndio ukamuwasha kibao?’ Meddy akakunja uso kidogo akisubiri jibu.
Jerry aliyekuw anaangalia mbele akageuza kichwa na kumtazama Meddy
‘She mentioned Nyanza…. sijui bikira yake ilikuwa ya Nyanza and  blah blah blah… I couldn’t take it anymore Meddy…. mimi ni mwanaume na kumbikiri hakujaongeza wala kupunguza kitu…. na hata ningemkuta bila hiyo kitu I swear ningempenda pengine kupitiliza….. but now yamekuwa masimango na…’ akakatizwa na Meddy

‘She is right!’ Meddy akaegemea upande wa Sindi
‘sikumbaka’ Jerry akajitetea akitoka pale alipoegemea na kusimama mbele ya Meddy
‘ulimtoa kijijini sawa?.... ulimuahidi kumleta Nyanza waje kuishi wote…. ni wewe huyo huyo ulimfuata kitandani na ukamuingiza majaribuni… imagine ungeiwekea mipaka tamaa yako…. binti wa watu angekuwa abado amemtunzia hiyo heshima huyo Nyanza… umevunja mahusiano yao Jerry…. worse enough bado kuna vitu unamficha…. na sasa umempiga… who is the Satan here?’ Meddy aliongea kwa hisia na jazba akiona wazi alichotendewa Sindi hakikuwa haki

‘,,,so uko upande wa Sindi sio?’ Jerry akauliza akionekana kuanza kupagawa
‘ndio…na hata ukiweka upanga shingoni mwangu nitakufa nikisema hiki nilichosema… binti wa watu hakukuomba msaada wa kuikimbia ndoa yam zee gani sijui uko kijijini….ni wewe ndio kisebengo kilikufanya umtoe kijijini and now unaplay victim… come on Jerry….. act responsibly….’ Meddy akaacha kuegemea gari na kugeuki maji yake. akayapiga funda kadhaa wakati Jerry akiwa ameinama chini akijifikiria

‘…Naenda kupumzika nyumbani kwangu….’ Jerry akazungumza akiinua kichwa na kuanza kuufuata mlango wa gari. Meddy akaachia mikono yake hewani akiashiria yote kheri
‘Kuna movie mpya cinemax leo usiku…got two tickets…vipi?’ Meddy akamuwahi kabla ya kuingia garini. Jerry akamtazama Meddy akitabasamu kwa huzuni.
‘unahitaji kuanza kudate Meddy… I’m not single anymore’ akajibu na kuingia garini akimuacha meddy anacheka peke yake. Wakapungiana mikono na Jerry akaondoka zake
888888888888888888

Nje ya jumba la kifahari. Mzee Okello anapata chai ya rangi huku akisoma gazeti. Upepo mwanana  uliokuwa ukivuma taratibu ulimletea mzee huyu burudani ya kutosha. alishusha gazeti alilokuwa anasoma baada ya binti yake Pamella aliyekuwa akitokea ndani na kumfuata pale alipokuwa ameketi. ni kama vile alikuwa ametoka kucheza mchezo wa tennis kwa yale mavazi aliyokuwa amevaa

‘Serena Wiliams!’ baba yake akamtania akimuita jina la mcheza tennis maarufu duaniani. Pamella akatabasamu na kuvuta kiti kilichokuwa kando ya baba yake. akavua kofia aliyokuwa amevaa na kuiweka mezani. Akivuta jagi la juisi na kujimiminia.

‘bado unacheza tennis?’ baba yake akamuuliza akilikunja kabisa lile gazeti na kuliweka juu ya meza mbele yake. Pamella akagugumia kwanza juisi yake na kisha akaitikia kwa kichwa na wakati huo baba yake akijilaza kwenye kiti chake na kumtazmaa binti yake kwa kina.

‘Jerry ameonekana…’ baba yake akampa taarifa zilizokaribia kumfanya Pamella apaliwe na juisi aliyoanza tena kuinywa. Akageuka na kumtazama baba yake kwa mshangao
‘Jerry?’ akauliza
‘Yes. Jerry Agapella’ baba yake akamjibu akitabasamu na Pamella anaye akajikuta akilazimisha tabasamu ambalo lilimgomea.
‘Lini?’ akauliza tena swali sasa akihisi mapigo ya moyo yakienda kasi
‘Sijui lini ila Mzee Agapella ameniambia jumapili usiku kutakuwa na sherehe ndogo nyumbani kwake’

Pamella akakunja ndita kadhaa usoni macho yake yakitembea taratibu toka usoni pa baba yake a kuelekea mbele. Akili yake ilifanya kazi kwa kasi kubwa na akajikuta amezubaa. Jerry Agapela, rafiki yake wa siku nyingi mno, hakuweza hata kumwambia ameshajitokeza kwa baba yake…. pamoja na msaada aliompatia wakati alipopotea leo anarudi kwao kimya kimya pasipo hata kumshirikisha achilia mbali kumwabia. Pamella akanyanyuka taratibu na kumuacha baba yake akimtazama kwa kumshangaa na wala asisikie vile alivyokuwa anamuita.

Kwake yeye Pamella hali ile aliihusisha na kuisha kwa mapenzi ya Jerry kwake. Akaumia mtoto wa kike, Akaumia mno na asijue maumivu aliyomletea mwanamke mwenzake upande wa pili wa dunia

Dakika kumi tu zilitosha kumtoa pamella pale kwao na kuelekea kwa Jerry akiwa na uhakika toka kwa Meddy kuwa Jerry alikuwa kwake. Wakati huo wa mchana, Jenifa alikuwa anapika nyumbani kwa kaka yake huku Jerry akiwa sebuleni na laptop yake. Kengele ilipolia Jerry kamuita Jenifa kwa sauti.

Jenifa akaingia pale sebuleni na kumtazama kaka yake.
‘Mi sio maid wako Jerry….’ akamwambia kaka yake kwa sauti ya kulalamika
‘but you are my only sister…please’ akamrai mdogo akiivuta ile please kama namna ya kubembeleza akafungue mlango. Jenifa akatabasamu na kuufuata mlango. alipoufungua tu  Pamella akampita na kuingia ndani.

‘it is not fair Jerry…’ alianza kwa kulalamika na Jenifa kule mlangoni akimtazama kwa jicho pembe bila mlango
‘Pamella!....kuna nini?’ Jerry hakumuelewa na akajikuta anaiweka ile laptop pembeni na kusimama. Pamella alikuwa analengwa na machozi

‘yote haya yanaletwa na Sindi?..... hivi ni Sindi ndio anafanya unanidharau hivi au ni nini?’ Pamella akazidi kulalamika na Jenifa kule mlangoni akatoa macho. Jina geni lilikuwa limetajwa masikioni mwake. Uso uliojaa umbeya ukamsimama, akasahau hata kuufunga mlango. Alichapua hatua kadhaa na kusimama nyuma ya Pamella kwa umbali wa hatua tatu za shamba.

Jerry alihisi hatari mpya. Jenifa ahakupaswa kuyasikia yale maongezi
‘Jeni tupe privacy kidogo’ akamtazama dada yake na Pamella anaye ndio akageuka na kumtazama Jenifa kuanzia chini kwenda juu. Alimpandisha bila kumshusha!

Jenifa akatanua uso wake kuashiria kukubali kutoka pale. Jerry akachungulia kama Jenifa alishapotelea ndani akamfuata Pamella kwa ukaribu
‘Grow up Pam!.... huwezi kutumia akili nini uongee na wapi?’ akamfokea kwa sauti ya kutotaka kusikika.

‘Nigrow up?...and this is about Sindi too isn’t it!....hivi  unamlinda unamficha for what?’ Pamella akaongea kwa sauti iliyomfikia Jenifa kule alikobanisha na kutega sikio. Jerry akaona angeharibu kila kitu. Akamshika mkono Pamella na kumburuza kwenda nje. kaufunga mlango na kusimama pale mlangoni. Jenifa anaye akitoka mafichoni na kuja kusimama mlangoni. akatega sikio!

‘Pamella….una tatizo gani?’ akamuuliza akiwa amekunja uso
‘Sijui hata nianzie wapi….baada ya kila nililokusaidia baada ya kutekwa bado unanilipa fadhila za dharau sababu ya mwanamke uliyemu…’ Jerry akaweka kidole cha shahada mdomoni mwa Pamella ili kumnyamazisha. Aligeuza macho yake na kutazama mlango ni kama alihisi Jenifa alikuwa anawasikiliza.

Akaufungua mlango ghafla na mlango ule ukambamiza Jenifa kule ndani
‘Yalaah!’ Jenifa akapiga ukelele wa maumivu na Jerry akajikuta akitikisa kichwa kulia na kushoto mara kadhaa na kumtazama Pamella ambaye aliangua kicheko kilichokosa tafsiri rasmi
8888888888888888888888888

Usiku saa moja jioni, Chumbani kwa  Jamila, Mkeka uliotandikwa pembeni ya kitanda ulikaliwa na watu wawili Sindi na  Jamila. Sindi alikaa kwa kujiegemeza kwenye kitanda na Jamila alikuwa anachambua dagaa wa mwanza kwenye sinia akiwa kajiegemeza ukutani.
‘….sasa hata ukirudi kijijini huyo Nyanza utamwambia nini kuhusu ahadi yenu?’ Jamila akamuuliza Sindi ambaye sasa alikuwa anajitazama kwenye kioo kidogo mkononi na kujitumbua kijiupele kilichokuwa kidevuni.

‘sijui ila kosa limeshatendeka Jami…’
‘…. halafu unamuonea sana huyu kaka maana jana full kumuwakia na dharau juu..sijui bikira sijui nini jamani….’ Jamilla akafanya kumsuta Sindi ambaye alicheka tu
‘…kama alikubaka vile nyooo!... yaani nilitamani nikufuate nikuchape makofi…kila mkizua sinema…hueshi kumsimanga….angekuwa na pesa ungemsimanga hivi aiii’ Jamilla alizidusha mashambulizi

‘alinikera sana…. yaani sana…’ Sindi akajitetea
‘Na ndio maana alikunasa kibao…. mwanamke uliunyanyua mdomo kama greda la konoike… poh! kashfa zingine mtakuja kung’olewa meno wallah’
Sindi akacheka tena na akilijua kosa lake. Hakulalamikia kupigwa kule kwa jana yake kwa vile yeye binafsi alijua kilichoongea kilimuumiza mno Jerry.

‘pamoja na yote mwenzangu….  wanaume wanafanana tu… utakimbia huku uende kule mwisho wa siku ugundue wote ngano tu tofauti maumbile yule maandazi huyu chapatti… msake huyo mwanamke umpe vipande vyakeeee….mkato, umpe madongooo koma, kisha umalizie naa onyo kituo!’ Jamila akanesa nesa akiyasema haya na Sindi akacheka tena

‘Nigombee mwanaume?.... kha!’ Sindi alibweua akitua kioo chini
‘sio kila mwanaume uingie ulingoni….ila kwa mwanaume kama Jerry hebu weka akili yako sawa….hivii…’ Jamila akakatisha maongezi na kucheka. kucheka kule kukamfanya Sindi amkunjie sura

‘Nini?’ Sindi akauliza
‘alipokuja ile jana ulimtazama vizuri?’ Jamilla akauliza akitabasamu
‘Mmmh…. sikumbuki…kwani nini?’ Sindi akauliza tena
‘Omba Mungu arudi mapema leo umuone sawasaw…. haki ya nani na hamu ya kurudi huku mashambani itakuisha….’ Jamilla akasema kishambenga na Sindi akaguna

‘Kanyoa nywele na ile mindevu ka’ uoto wa asili…. kaka kawa kaka… yaani huyu mumeo akipata hela hivi akawa na maisha Fulani ya juu kidogo aisee dada unavyopenda kulia…. utalia karne kwa milenia’ Jamilla alijiiinusha toka pale chini wakati Sindi akicheka kwa sauti na kutikisa kichwa.

‘ huko kwangu sijafunga hata mlango kwa ufunguo…’ Sindi akasema anaye akijiandaa kunyanyuka
‘Nani wa kuingia uko saa hizi… kaa unipe kampani bwana… saa mbili hivi ukishakula ukalale tu….mumeo leo haji wallah…’ Jamilla akajibu na Sindi akatulia

Wakati wao wakiwa kule ndani. Jerry alifika kwake na kuingia chumbani. Taa ilikuwa inawaka na iliashiria Sindi hakuwa mbali. mkononi alikuwa na mfuko uliokuwa na khanga mpya, viatu na samaki wa kukaanga waliofunga kwenye mfuko mwingine.

aliutua ule mfuko kwenye kochi na kuangaza angaza mle chumbani kabla ya kuketi kitandani na kuanza kufungua vishikizo vya shati. Akahisi amekalia kitu. taratibu akajinyanyua kidogo na kupapasa pale alipohisi kipo hicho alichokalia. akatoa bahasha nyeupe ndogo nyeupe iliyokuwa hapo kitandani.

Uso ukasinyaa kidogo wakati akiitanua ile bahasha na kuchungulia ndani. Akakivuta kipakti kilichokuwa ndani humo na kukiweka usawa wa macho yake.
‘Pregnacy test’ akayasoma maandishi ya blue yaliyokuwa juu ya kile kipakti. Ukubwa wa macho ukaongezeka kidogo na hali ya kuduwaa iliyochanganyikana na hofu, wasiwasi na kutoamini ikamtembelea. Kwa Sekunde alizokitazam kile kifaa alitamani Sindi angekuwepo na kumpatia majibu ya kwanini kifaa kile kilikuwa pale/

…….. WIKENDI NJEMA WASOMAJI WANGU…..

1 comment:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger