Tuesday, May 21, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE(16)

16

Taarifa za kutoweka kwa Sindi zilisambaa kama upepo wa kimbunga. Nyumbani kwa Mzee Nalela kulikuwa na hekaheka kubwa. Watu walikuwa wakijazana kila dakika iliyokatika. Kulikuwa na hekaheka ya kutosha muda huo wa saa nne usiku.

Wakati haya yote yakitokea Nyanza alikuwa chumbani kwake akiwa amepitiwa na usingizi baada ya kikao kirefu na mama yake na wakishindwa kufikia muafaka na kuelewana.


Saa sita  na vichapo kadhaa, Nyanza alikurupushwa usingizini na kishindo cha hali ya juu. Aliinuka na kuketi kitandani akitega masikio kwa bidii na kujaribu kuiweka akili yake sawa.

Maruweruwe ya usingizi bado yalikuwa yamemganda kichwani wakati alipoona mwanga mkali wa tochi mbili au zaidi vikipishana katika namna ya kusaka kumulika kitu wakati huo huo sauti ya mama yake ikisikika. Akachanganyikiwa!

‘Yuko wapi?...’ kikasikika kibao Pah! ‘...sema upesi’ sauti ya kuamrisha iliyoenda sambamba na mlio wa kibao kingine ukasikika tena. Nyanza akajiinusha haraka na kukwanyua T shirt iliyokuwa imetundikwa kwenye msumari ukutani. Akatoka huku akiwa anaivaa na wakati huo huo akigongana na watu wawili walioonekana kutoka chumba kilichotumika kama ghala yao na kuja kule alikokuwa.
Akataka kuwauliza walichokuwa wanakifanya mule ndani lakini hakuipata nafasi hiyo. Wale watu wawili ambao baadaye alikuja kuwatambua kama polisi walimvamia na kumtandika virungu mwilini wakimkwida kama mwizi na kumtoa nje.

Kwa namna alivyokuwa akishambuliwa kwa kipigo Nyanza hakupata hata nafasi ya kuinua uso kumtazama mama yake aliyekuwa analia na kuomba mwanawe aachiwe kwa kuwa hana hatia. Pale nje walimtandika vya kutosha kisha wakampigisha magoti, mikono yake ikikutana nyuma ya shingo kama mateka. alikuwa hoi, akivuja damu kama mhalifu.

Kulikuwa na giza lakini mwanga wa mbalamwezi ulikuwa mkubwa wakutosha kumuona Mzee Dunia akipishwa na polisi wakati akimkaribia pale alipokuwa amepiga magoti. Mzee Dunia akamuinua uso kwa kukinyanyua kidevu chake kwa fimbo ya kutembelea aliyopenda kutembea nayo mkononi.

‘kijana…. sidhani kama nahitaji kutumia nguvu zaidi ya hii niliyotumia….ukinipa ushirikiano sekunde moja tangu sasa utakuwa huru…’ Mzee Dunia aliongea kwa kituo, kwa hatua akimpa nafasi Nyanza amuelewe kama alivyotaka kueleweka lakini Nyanza ahakumuelewa!

‘Nimekosa nini?’ Nyanza akauliza akihema, meno yake yakiwa na rangi nyekundu kutokana na damu iliyokuwa inamtoka mdomoni sababu ya kipigo.
‘Sindi yuko wapi?’ Mzee Dunia akauliza kwa upole kama mzazi anayemuuliza mwanawe ni wapi alipoiweka kalamu yake.

‘Sindi?..yuko wapi?....unamaanisha nini?’ Nyanza alitoa amcho kwa taharuki ya ghafla akiwa hajamuelewa Mzee Dunia ambaye alifumba macho na kutabasamu kwa sekunde kadhaa na alipofumbua, alimtandika Nyanza kofi kali la shavuni lililompepesusha Nyanza na kumdondosha chini, yowe kubwa likimtoka na kumfanya mama yake alie kule ndani na kuwasihi wampige yeye sio kijana wake.

Wale askari wakamnyanyua Nyanza na kumpigisha tena magoti kama mwanzo.
‘Narudia tena Sindi yuko wapi?.....usidhani nimeacha shughuli zangu kuja kukubembeleza kijana…..wala sikuharibu mafuta yangu mpaka mjini kuchukua polisi kuja kukubembeleza mtoto….najua alikuwa msichana wako na nilishakuona naye…. usinichezee akili…Sindi yuko wapi?’ Mzee Dunia akalirudia lile swali ambalo sit u lilimchanganya Nyanza bali pia lilimuongezea maswali ambayo kwa wakati ule yalikosa majibu kabisa sembuse jiu la kumpa Mzee Dunia.

Kushindwa kule kujibu na kubaki kimya akiwa amehamanika vibaya mno, kulimfanya Mzee Dunia awape ishara wale polisi ya kumpakiza Nyanza kwenye gari walilokuja nalo. Wakati wakimnyanyua mama Nyanza alishasota kwa magoti mpaka mlangoni akijaribu kuvuka kizingiti cha mlango huku akilia na kupiga mayowe kijana wake aachiwe.

Nyanza alilia kama mtoto sio kwa maumivu ya kipigo aliyokuwa nayo bali kwa ile hali ya mama yake aliyoisababisha na kabla hajarekebisha alikuwa katika sakata ambalo hakujua hata lilipoanzia.

Nyanza akachoropoka mikononi mwa polisi na kumkimbilia mama yake. Watu waliokuwa wamesimama mbali na eneo lile walisikitika, wanawake walilia na wengine walitazama pembeni kwa huzuni wakichelea kuona namna Nyanza alivyokuwa akipigwa kama Nyoka wakati askari wale walipokuwa wakimtenganisha na mama yake.

Mama na mwanawe walikumbatiana kwa nguvu zaidi wakati polisi wakiwaachanisha kwa kipigo.
‘Wataniua mama…wataniua’ Nyanza alilia kama mtoto mdogo aliyehitaji ulinzi wa mama yake, alilia kwa hofu. Wakati wakizidi kukumbatiana kwa nguvu askari mmoja alimpiga mama Nyanza kichwani kwa kirungu chake.

Kipigo kile kilimteteresha mama Nyanza na taratibu akaachiana na mwanawe a kulegea kurudi ardhini. Nyanza akaburuzwa  kama gunia  huku akilia na kumuita mama yake ambaye aliangua chini na kutulia pasipo kutikisika.

Akapandishwa kwenye gari la polisi huku akiendelea kupigwa naye akipiga makelele kumuita mama yake. Gari la polisi likaondoka likifuatiwa na gari la Mzee Dunia.  Watu waliokuwa wamesimama mbali wakakimbizana kumuwahi mama Nyanza pale chini.

Watu walikuwa wamesimama makundi makundi kila mmoja akiongea lake. Wapo waliojifanya kuujua ukweli na wapo ambao walihangaika kuujua ukweli ila walioujua ukweli halisi walikuwa wamesimama pamoja. Jitimai ikiwa imewatembelea! Mchezo walioucheza ulikuwa umeleta matokeo tofauti na waliyotegemea. Mpunga waliolima ulichipusha mchicha!

Jerry Agapela, Alma na Maria walikuwa wamesimama kama wafu, wakilitazama gari la polisi lilivyokuwa likiishia huku polisi wakiwa wamekanyaga Nyanza pale kwenye gari alipokuwa amelala kwa kujikunyata.
Jerry aliumia sana, alikuwa anajua kila kitu, alikuwa anajua alipo Sindi Nalela, ilikuwa kama vile yeye ndiye aliyeleta sakata lote lile.
888888888888888888888

Asubuhi ya saa mbili na nusu, Sindi alikuwa stendi ya mabasi akingoja basi la Allys katika eneo la kukatia tiketi za basi hilo. Mkatisha tiketi alishafahamishwa kuhusu Sindi na alishamfahamisha atakaye mpokea uko Dar kuwa Sindi angekuja na basi lipi la Allys.

Masaa machache baadaye Basi la Allys lilikuwa likiiacha Shinyanga na kuanza kuitafuta Tabora. Sindi alikuwa ameketi dirishani, akiwa amekilaza kichwa chake kwenye kioo cha dirisha. Mikononi mwake akiwa amekumbatia mfuko uliokuwa na nguo zake. Alionekana kuzama mbali sana kimawazo. Roho ilimuuma sana kwa Nyanza kutoukubali wito wake.

Alikuwa akiweweseka kimoyomoyo na kushindwa kuelewa ni kipi hakikueleweka kwa Nyanza hadi asifike kugana naye. Kuna wakati alihisi kumasirikia na kumlaani kwa ujeuri wake. Hakujua tu, dhoruba iliyokuwa imemkumba Nyanza sababu yake!

Sindi alisafiri salama na kuingia Dar saa mbili usiku. Pamoja na giza lile Sindi alishangaa wingi wa magari na watu mara tu walipoikaribia ubungo. Alikuwa akiangaza angaza huku na kule akionekana kuifurahia mandhari ya Dar aliyokuwa akiisikia miaka mingi tu.

Basi lilipoingia kituoni na kusimama, abiaria walianza kushuka, madereva taksi nao wakijazana mlangoni mwa basi kuwahi wateja huku ndugu na jamaa nao wakitaka kuwalaki ndugu zao. Sindi aliteremka kwenye basi kwa tahadhari, akafanya kazi ya ziada kubenjua bega lake la kulia kukataa kule kuguswa guswa na madereva taksi ambao wengine walimpa nafasi na wengine walizidi kumuandama sasa.

‘Sitaki!’ Sindi alijibu kwa ukali, mtu mmoja alipotaka kumpokea kile kifurushi cha nguo zake. Akajitoa mbali na basi lile na kusimama akiangaza angaza lakini ghafla akamuona mtu akimjia pale alipokuwa amesimama huku akitabasamu na kuchezesha funguo mkononi. Sindi hakutabasamu, alimkazia macho yule mtu mpaka alipomkaribia.

‘Hujambo Sindi?’ Meddy Hakim, rafiki wa Jerry alimsabahi Sindi ambaye aliposikia jina lake likitajwa akajua huyu ndiye aliyekuwa mwenyeji wake
‘Shikamoo’ akasalimia na kupiga goti la kugusa sakafu. Madereva taksi na makuli kadhaa waliokuwa eneo lile waliwatupia macho huku wengine wakimtania Meddy

‘Kaka mali ya wapi hiyo?...kaka umeona ulete toka kijijini kabisaa…. wacha weee’ makelele yalisikika na Meddy alijikuta akicheka na kutikisa kichwa. Akataka kumpokea kile kimfuko chake cha nguo
‘hapana asante’ akajibu akipiga tena goti

Meddy akamuonyesha mahali alipokuwa amepaki gari ambalo lilikuwa taksi iliyoandika Ilala ubavuni. Wakati wakitembea Sindi akashangaa kumuona mwanamke mnene aliyekuwa akipita kando yake na kikaptura kifupi kilichoacha sehemu kubwa ya mapaja yake nje. Sindi akaachama mdomo na kushangaa waziwazi. kule kushangaa kulimfanya asione mwisho tofali lililokuwa mbele yake. Akajikwaa almanusura aanguke.

Meddy alitaka kucheka lakini akajizuia na kumpa pole Sindi ambaye aliona aibu hata kuipokea. Wakaondoka pale na kuelekea Sinza kwa Remmy.

Akakaribishwa kwenye chumba kilichokuwa kama sebule na hapo hapo kukiwa na kitanda. Meddy Hakim akampa ufunguo wa chumba na pesa kadhaa. akmataka amngoje kidogo. Meddy akatoka.

Sindi aliangaza angaza huku na kule na akishangaa vitu vya mule ndani ikiwemo zulia zuri la kuvutia. Akajiweka sawa aliposikia mlango ukifunguliwa na Meddy akitangulia akiwa amefuatana na msichana mwingine wa rika lake.

‘mgeni mwenyewe huyu hapa anaiwa Sindi Nalela’ Meddy akamtambulisha
‘Anhaa…karibu anti’ yule dada akaitikia akimpa mkono Sindi ambaye aliupokea na kubonyea chini kwa adabu kiasi cha kumfanya yule dada atabasamu zaidi
‘Sindi…huyu ndio atakuwa mwenyeji wako kwa kipindi hiki…anaitwa Jamila’ MEddy akamtambulisha Jamila kwa Sindi
Asante…nashukuru kukufahamu’ Sindi akajibu kwa aibu kidogo

yakafuatia maongezi madogo madogo kati ya Jamila na Meddy kisha MEddy akaaga na kuondoka zake akimuacha Jamila pale ndani.
‘Ngoja nikuletee chakula…kama unataka kuoga kuna bafu nje….maji tunachota kwenye kisima nyuma  nitakuonyesha kesho….ila jiandae ukaoge ngoja nikuwekee maji’ jamila akamsemesha kisha akatoka na Sindi akabaki mwenyewe akikitazama hiki chumba mara mbilimbili. Kwake kilikuwa chumba kizuri mno kulinganisha na alikotoka.

Akaoga, akala, akalala, siku yake ikawa imeshia hapo huku kule kijijini hali ikiwa tete siku nzima.  Alma na Maria wakiogopa hata kujadiliana kuhusu Sindi. Waliogopa mno kuunganishwa na Nyanza katika kesi ile. Mzee Dunia alikuwa amegoma kuupokea pesa zake za mahari, yeye alimtaka Sindi tu!

Mzee Nalela aliziona pesa alizoachiwa na Sindi na maelezo kuwa zilikuwa fidia ya mahari. Hakujua alikozitoa mwanaye lakini alipozitoa kwa Mzee Dunia zilikataliwa. Mzee Dunia akidai pesa ile isingefidia aibu aliyompatia mpaka dakika ile.

Mama Sindi na wanawe walishafukuzwa pale kwao na walikuwa wanajisitiri kwa rafiki wa Mzee Nalela. Waliambiwa wasikanyage pale mpaka Sindi apatikane.  Sindi alikuwa ameacha zahma ya kutosha kwa kila mtu!
8888888888888888888

Kuna kitu kilikuwa kimetokea pale kijijini, kitu kikubwa sana ambacho kilikuwa kinamsubiri Nyanza aachiwe hata kwa dhamana. Wiki mbili baada ya kukamatwa, Nyanza aliachiwa kwa masharti. Huku akichechemea alirudishwa kijijini na kuachwa mbele ya nyumba yao.

Nyanza aliuhisi ukimya uliokuwa umeitembelea nyumba yao. Alitembea kwa taabu na kuingia uani huku akiangaza huku na kule. Muda huo wa saa mbili asubuhi wanakijiji wengi walikuwa mashambani wakilima. Wakati akiukaribia mlango wa kuingilia ndani mdogo wake Nyanza alitoka na kukimbilia kaka yake, akamkumbatia na kulia kwanza.

‘Mama yuko wapi?’ Nyanza akauliza lakini mdogo wake hakujibu kitu. Alilia kwa kwikwi pasipo kusema chochote. Nyanza akaachana na mdogo wake na kuingia ndani haraka. Alimsaka mama yake huku na kule na asimuone. Akarudi nje pale alipomuacha mdogo wake.

‘Mama yuko wapi?’ akarudia swali lake, mwili ukimtetemeka. Mdogo wake alimtazama tu akitiririkwa na machozi huku akianza kutembea kuondoka pale uani na kutoka nje. Nyanza akawa anamfuata kama kivuli, wakaiacha nyumba yao na kushika njia iliyokuwa inaelekea makaburini. Nyanza akahisi kichwa kikiwa na uzito wa dunia.

‘Pale…’ akamuonyesha tuta kubwa lililokuwa na msalaba wa mti. Nyanza akatulia tu akilitazama lile tuta. Hakulia wala kuongea alisimama pale pale akilitazama lile tuta ambalo ndilo lilikuwa kaburi la mama yake.

Akatembea taratibu mpaka kwenye lile kaburi, akapga magoti mbele yake na kutulia akilitazama kama mtu asiyeamini kile alichokuwa anakitazama. Mikono ilikuwa inamtetemeka kadiri alivyokuwa analitazama lile kaburi huku mboni za macho yake zikielekea katika maji. Akafumba macho na kuruhusu mtiririko wa machozi.

Sindi alikuwa ameondoka maishani mwake na asijue alipo, alikuwa amepigwa vya kutosha na kuzuiwa kumuona mtu yoyote ndani ya wiki mbili, anaporudi nyumbani anakuta mama yake amelala usingizi wa mauti, pasipo kumtimizia ahadi ya nyumba mpya, pasipo hata kumzika. Nyanza alilia, alilia, alilia mno lakini machozi yale hayaubadili ukweli uliokuwa mbele yake…..

Wakati akilia na kuomboleza, mdogo wake alimpatia ile bahasha aliyoikuta kwenye mtonwa kulalia wa mama yake. Nyanza akaifungua na kuisoma huku akiilowanisha na machozi. Uchungu ulimshika maradufu. akanyanyuka na kushika njia kuelekea kule kilima moto ambako alipaswa kuonana na Sindi. Kama mwehu akazunguka eneo lile akiliita jina Sindi kwa kupayuka. Nyanza alikuwa amechanganyikiwa!

JE NINI KITAFUATA?....JERRY YUPO AU NAYE AMETIMKIA MJINI?....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger