Tuesday, May 14, 2013

SINDI.....NA LAURA PETTIE(14)

14


Mara baada ya kumaliza kufundisha darasa lake, Sindi alibaki darasani, kwenye kile kiti chake kama mwalimu, akiwa ameegesha viwiko vyake juu ya meza iliyokuwa mbele yake na mikono yake ikiwa imeshikana na kumfanyia egemeo la paji lake la uso. Alikuwa akilia kimya kimya.

Alipotulia na kunyanyua kichwa chake, akafuta machozi kwa viganja vyake na kujaribu kujiweka sawa lakini huzuni ilimtembelea tena akajikuta akijiiinamia na kuanza upya kulia.



Alilia mpaka pale alipohisi vishindo vya miguu vikisikika kuelekea pale alipokuwa. Akanyanyua kichwa na kugeuka kutazama mlangoni, akianzia miguuni mpaka usoni pa yule mtu aliyekuwa amesimama pale mlangoni. Wakatazamana!

Ni kama vile ujio wa yule mtu ulimuongezea uchungu, akageuka na kumpa mgongo, sasa akilia kwa sauti na hisia huku kwikwi za kilio zikipamba moto na kufanya mabega yake kupanda na kushuka kufuata mirindimo ya kwikwi zake.

Nyanza aliyekuwa mlangoni hakumsogelea, wala hakupiga hata hatua moja kumkaribia achilia mbali kumgusa. Aliendelea kusimama pale akimtazama Sindi alivyokuwa analia na asitamke chochote.

Akageuka taratibu na kuanza kuondoka eneo lile, Sindi akanyamaza ghafla na kugeuka kutazama mlangoni mara tu aliposikia hatua zikipigwa kuelekea mbali na lile darasa. Akanyanyuka kwa pupa kidogo, akigonga meza ile iliyokuwa mbele yake na kuangusha baadhi ya vitu vilivyokuwa juu ya ile meza, hakuokota alivyoangusha, alitoka kwa kasi na  kukimbilia nje.

Alimuona Nyanza akitembea haraka akiliacha eneo lile na kukamata njia nyembamba iliyotengenezwa na miguu na matairi ta baiskeli. Sindi akakaza miguu Kumharakia  huku akiliita jina la Nyanza ambaye hakugeuka wala hakusimama.

Sindi alipomfikia alimkumbatia Nyanza kwa nyuma, mikono yake ikikutana mbele ya tumbo la Nyanza. Kitendo kile kilimfanya Nyanza asipige hatua nyingine zaidi ya kusimama kama nguzo, akimsikilizia Sindi aliyekuwa analia nyuma yake. Nyanza akauma meno na kusigina magego yake kwa nguvu. Machozi yalikuwa yanamlenga lakini alipigana kiume kuyazuia kutoteremka.

Alitulia vile kwa muda tu, kabla ya kutumia nguvu kidogo kuitanua mikono ya Sindi na kutaka kujitoa mikononi mwake, lakini Sindi aliikaza mikono yake kwa nguvu yake na kufanya Nyanza ahairishe zoezi lake.

‘Kwanini?....hujawahi kuniambia Sindi…kwanini? Nyanza aliongea kwa uchungu
Sindi hakujibu bado alikuwa analia. Nyanza akaushika mkono wa kulia wa Sindi na kuuvuta kiasi cha kumleta Sindi mbele yake. Macho yake yalikuwa yamejaa machozi na uso mzima uliloa machozi ambayo hayakukoma.

‘Sindi!...’ akamuita kwa upole huku wakitazamana
‘Ni kweli?’ akataka uhakika. ‘….nataka kusikia toka kwako…hivi ni kweli? akauliza tena kwa msisitizo lakini hakupata jibu toka kinywani mwa Sindi.
Lile hamaniko tu lilitosha kumfahamisha kuwa alichokuwa amekisikia kilikuwa na ukweli ndani yake. Sindi alikuwa anaolewa na Mzee Dunia, tajiri wa kijiji!

‘Ningeanzia wapi Nyanza….wapi?....ndoa yenyewe ya kulazimishwa…ningeanzia wapi kukuvunja moyo?’ Sindi aliongea akilia, viganja vyake vikibebana kifuani kana kwamba alikuwa akiuzuia moyo wake uliotaka kuchomoka na kukimbia.
‘Pamoja na ahadi zote zile Sindi…’ Sauti ya Nyanza  ilitoka kwa mtetemeko ulioashiria hasira zilizochanganyikana na hamaki.

Hakuna aliyeongea tena, walitazama tu Nyanza akitafuta neno la lawama la kufaa kuelezea alivyokuwa akijisikia muda ule na Sindi akitafuta neno la kujitetea kuelezea alivyopambana na hali ile ya kushindwa kumwambia ukweli tangu mwanzo. Nyanza akainamisha kichwa chini huku Sindi akihamanika zaidi na kumtazama usoni akiisubiri kauli ya Nyanza

‘Nitakufa kwa ajili yako Sindi…’ akainua uso na kumudu kutoa tamko lake lililomfanya Sindi aachame mdomo na kutanua macho yake na hapo hapo machozi yakijazana machoni pake na kutiririka. Nyanza alimtazama kwa jicho kali zaidi pengine akidhani yale machozi yalikuwa ya kinafiki tu.

Akapiga hatua pembeni ya Sindi na kuanza kuondoka akimuacha Sindi analia pasipo kugeuka. Safari hii alilia zaidi kiasi cha mwili wake kuonekana kutetemeka. Aliumia, aliumia sana na aliumia zaidi alipomfikiria Nyanza kuliko alivyojifikiria yeye mwenyewe.

Taarifa za ndoa yake na Mzee Dunia zilisambaa jioni ya siku iliyopita, baada ya Mzee Dunia kukamilisha mahari jioni ile nyumbani kwa Mzee Nalela. Tarehe ya ndoa ikatajwa siku jana hiyo na Sindi akaitwa na kuambiwa mpoaka dakika ile alishakuwa mke halali wa Mzee Dunia, alipaswa kuisubiri siku ya ndoa ya kimila tu kukamilisha uhalali huo.

Sindi Nalela hakuamini, hakuamini kama siku aliyokuwa akiisikia itawadia ilikuwa imewadia ghafla vile. Mzee Dunia aliposema Sindi angeishi kwenye nyumba ya peke yake aliyokuwa akiikarabati kijijini hapo familia ya Nalela ilifurahi mno na taarifa za Sindi kuolewa na Mzee Dunia na kujengewa nyumba zilisambaa kama moto wa nyikani lakini sasa aliposema Nyumba ya Mzee Nalela pia itakarabatiwa shangwe zilipiga hodi nyumbani kwa Nalela ikawa kama ndio Sindi anaagwa kwao.

Asubuhi ya siku hii, aliamkia kufundisha angalau kujitoa wahaka aliokuwa nao. haikusaidia! Alimuwaza Nyanza, aliiwaza hali atakayo kuwa nayo, aliwaza mno.
Kauli ya Nyanza kuwa atakufa kwa ajili yake hakuielewa lakini pia hakuipuuza kwa vile ilimuingia na ilimuumiza mno.
888888888888888888888

Jua la alasiri ilikuwa linaelekea ukingoni, kuzama kwake kulileta manadhari ya kuvutia kwa yeyote aliyapata kukaa juu ya kilima hiki akilitazama namna jua linavyozama. Sindi Nalela alikuwa ameketi juu ya kilima hicho akiwa ameikunja miguu yake na kufanya magoti kugusana na kidevu. Mikono yake iliikumbatia miguu yake hali kidevu chake kikiwa juu ya magoti.

Macho yake yalitazama mbele yakifumba na kufumbuka taratibu huku muda mwingi yakiwa yamelikodolea  jua lililokuwa likizama wakati ule. Ndege walisikika kwa mbali wakipiga kelele za kuvutia, utulivu ukionekana kuchukua nafasi sehemu kubwa ya eneo lile. katika hali ya kawaida mandhari ya eneo lile ilikuwa ya kuvuta akili ya mtu na kuituliza lakini kwa Sindi haikuwa hivyo.

Kuna mengi yalikuwa yakizunguka kichwani mwake. Aliongea na kujijibu mwenyewe mawazoni, alibishana na akili yake na mara kadhaa alikunja ndita chache usoni pake. Mawazo yalikuwa yamemchota mno kiasi kwamba hakumsikia Jerry Agapela aliyekuwa amefika eneo lile kitambo na kusimama akimtazama Sindi.

Jerry akaamua kwenda pembeni ya Sindi na kuketi kule ndiko kulikomtoa Sindi mawazoni. Akageuza uso wake taratibu na kumtazama Jerry, tabasamu la huzuni likichanua usoni na kutoweka haraka, akarejesha kichwa kule alikokuwa akitazama, pumzi zikimshuka taratibu.
‘Pole..’ Jerry akamsemesha lakini Sindi hakujibu kitu wala hakugeuka
‘Samahani kama nitakuudhi Sindi….ila …’ akasita kidogo kwanza
‘… umekubali kuolewa?’ Jerry akauliza sauti ikipungua kama vile ilimlazimu kuuliza vile. Sindi hakujibu kitu, aliendelea kutazama kule mbele kana kwamba bado alikuwa mwenyewe.
‘Najaribu kukusaidia Sindi’ Jerry akaomba kueleweka
‘Kwa misingi ipi?’ Sindi akisogeza kichwa na kutazama kando zaidi kiasi cha kukaribia kumpa kisogo Jerry’

Kama rafiki!...’ Jerry akajibu na Sindi akajikuta akigeuza kichwa chake haraka na kumtazama Jerry usoni.
‘Rafiki?!’ swali lenye mshangao ndani yake lilimtoka, akamkazia macho Jerry mara mbili.

Jerry akatikisa kichwa kulithibitisha lile swali lililo na jibu ndani yake.  Sindi akarudisha uso mbele. Akatulia hivyo kama mtu aliyeamriwa kufanya hivyo.
‘Nimeuvunja moyo wa Nyanza…. nimemuumiza…. natamani kungekuwa na njia ya kuikimbia ndoa hii…natamani sana…’ Sindi aliongea polepole na machozi yakifanya kiherehere cha kuanza kuelea kwenye mboni za macho ya Sindi.

‘Jerry…. sikuomba kuzaliwa maskini… kwanini Mungu aniletee mitihani kama hii wakati umaskini nilionao ni mtihani tosha kwangu….eeh Mungu wangu’ Sindi aliongea akilia sasa akiwa ameikumbatia miguu yake vile vile huku akiyumba kwa kwenda mbele na kurudi nyuma.

Jerry akajisikia vibaya sana, akahamanika na kutafuta cha kumuondoa Sindi katika hali ile. Akajilaumu kwa kuyaanzisha mazungumzo yale. Alikuwa ameambiwa kila kitu na Maria, rafiki wa Sindi.
‘Nikikusaidia karo ya kaka yako…si nitakuwa nimekuokoa na hii ndoa?’ Jerry akauliza kwa huruma, akitamani kumvutia Sindi ubavuni pake na kumbembeleza.

Macho mekundu, yaliyojaa machozi yakamtazama Jerry, ni kama vile Sindi hakuisikia ile kauli
‘nasikia unaolewa sababu inahigtajika karo ya kaka yako….what if nikikusaidia hiyo karo?’ Jerry alitaka Sindi aamini kuwa alikuwa ana nia ya kumsaidia. kwa kulirudia swali lake lile kukamfanya Sindi acheke kicehko cha kivivu katikati ya huzuni ile

‘Sio muda wa utani huu Jerry….napitia wakati mgumu sana….nikishaolewa hapo sina maisha ya kuwaza wala kuendeleza zaidi ya kuzaa na kulea….na hayo sio maisha niliyomuomba Mungu’ Sindi alilalamika na Jerry akamuwahi
‘Just tell me….nikikupa karo si nitakuwa nimekuokoa?’

Sindi akauvaa uso wa umakini kidogo akiona Jerry hakuwa anatania.
‘Utaitoa wapi karo wakati wewe mwenyewe unasaidiwa na baba Chidi’ Sindi akamuuliza akimtaja mwenyekiti kwa kijiji kwa jina la mwanaye.

‘Nitamuomba yule rafiki yangu aliyekuja hapa’ Jerry akajibu akimaanisha Pamela Okello. Sindi akaguna kwanza
‘Rafiki yako au mpenzi wako?’ Sindi akauliza na ile huzuni ikisambaa na kutoweka kadiri mazungumzo yao yalipopamba moto.

‘Nampenda ila hanipendi so anabaki kuwa rafiki’ Jerry akawa mkweli
‘Pole!’ Sindi akajibu  akitabasamu, hakuiamini kauli ya Jerry na wala hakutaka kybishana nanye hata kidogo.
Asante!’ Jerry naye akajibu akitabasamu
‘….ulisema hivi ulisema ulipata ajali na wenzako mkiwa mnaenda mjini kutafuta maisha?’ Sindi alibadili uelekeo wa mazungumzo, na uelekeo ule ulikuwa wa ghafla kiasi kwamba Jerry alilazimika kukunja uso na kuifanyisha akili yake kazi ya ziada ya kukusanya uongo wote aliomueleza Sindi kuhusu maisha yake.

‘Yeah…’ akaitikia Jerry macho yakiwa kodo!
‘sasa msichana kama Pamela umejulia wapi?....kwanini asikupe kazi?’ Sindi alizidi kuhoji, sasa akijigeuza mwili mzima na kuketi bila kujikunyata akimtazama Jerry aliyejikuta akijikuna nyuma  ya shingo pasipo kuwashwa.

‘mimi naishi dar huku nilikuja tu kutafuta maisha na wenzangu….ndio bahati mbaya nikapata ajali…. Pamela namjua siku nyingi tu namjua…ila  siwezi kumuomba msaada zaidi ameshanisaidia vya kutosha’ Jerry alijieleza, akikwamba hapa na pale na nyakati zingine akirudia rudia maneno.

‘kwanini hukuondoka naye alipokuja?’ Sindi akazidi kuhoji
‘Aaah…mmmh… sikuwa najisikia vema….ila karibu nitaondoka’ Jerry akajibu na Sindi akakunja uso kama mtu anayefikiria kitu
‘wenzio mliopata nao ajali wako wapi?..... au uko kwenu hawakutafuti?’ maswai ya Sindi yalianza kumchosha Jerry.

‘Wanajua kila kitu…. ndio maana sina wasiwasi…. sina wazazi nina ndugu tu….unadhani nani anajali niko wapi na anafanya nini?’ naye akamrudishia swali. Sindi akatikisa kichwa kulia na kushoto akionekana kumuelewa angalau na akisahau habari kuhusu wale ambao Jerry aliopata nao ajali.

Wakaongea mengine mengi, robo tatu Jerry akiongea uongo na robo iliyobaki akisema ukweli. Alikuwa akificha utambulisho wake halisi. Walipogeukia suala la karo ya Sega kaka yake Sindi, Sindi alikubali baada ya ushawishi mwingi kuwa karo ingepatikana. Sindi akashukuru na kunyanyuka akijiandaa kuonndoka eneo lile kwani giza lilishaanza kuingia.

Alipohakikisha Sindi alikuwa ametoweka pale. Jerry alitoa simu yake toka katika suruali aliyokuwa amevaa na kumpigia Pamela.
‘Msaada kidogo’ akatamka haraka simu ilipopokelewa
‘what is the matter honey?’ Pamela akauliza kwa sauti ya kujali lakini lile neno Honey ndilo liliondoa tafsiri ya kujali kwa Jerry, kwake ilikuwa kama dhihaka!
‘Nahitaji milioni mbili na nusu cash!....’ Jerry akasema kwa sauti ya chini

‘Jay!.... two millions!?....kuna shamba unataka kununua?’ Pamela akahoji uso wake ukiwa na mikunjo ya kutosha na ilen wine iliyokuwa kwenye glasi mkono wake wa kushoto, ikigeuka kuwa na uzito wa tani moja. Akaiweka kwenye meza ya vinywaji iliyokuwa mbele yake na kuketi kwenye kiti hapo hapo karibu na meza

‘nina shida nazo haraka…fanya juu chini nizipate ndani ya siku mbili hizi please….it is urgent Pam’ Jerry akasisitiza na kumfanya Pamela ashindwe kumuelewa zaidi
‘Umeanza lini kunificha mambo yako Jerry?....what is going on there?’ kama mama anayemjali mwanawe, Pamela alihoji kimashaka akitembeza macho yake huku na kule

‘Pamela please!’ Jerry akasisistiza
‘Okay!...will do so… take care’ akaaga sati yake ikionyesha kutoridhika na kule kuamrishwa kutuma pesa bila kujua matumizi yake.
‘I’ll refund you once nikifa uko na kupata kadi….usijli hilo’ Jerry akamhakikishia kurudishiwa hela zake

‘It is not about kurefund….ni what are you up to?.....two millions!!...come on Jerry!’ Pamela alibebesha mguu mmoja juu ya mwingine huku ule mkono wa kushoto ukiparaza kichwani kuanzia pajini na kuzichachafya nywele zake kisogoni kwa kucha zake ndefu zilizonakshiwa kiustadi.

‘it is a long story’ Jerry akataka kukatisha maongezi
‘Okay… hope you are not in trouble’ Pamela akataka uhakika kwanza
‘No!...’ Jerry akakata simu na kushusha pumzi ndefu, akicheka pia peke yake kwani wasiwasi wa Pamela juu ya afya yake, usalama wake au chochote kumhusu yeye ulimfanya ahisi Pamela alikuwa anampenda lakini Pamela mwenyewe alilikana hilo kwa vitendo vya kumuumiza!
888888888888888888888888

‘Usiniletee wazimu wako Nyanza…sikukwambia mimi?’ Mama Nyanza alikuwa akiongea kwa jazba akiwa anafuatana na Nyanza toka ndani mpaka uani.
‘Nataka kumuoa mama…. nitamkosa Sindi bila pesa’ Nyanza alichachatika akaongea uso ukiwa na huzuni ambayo ndani yake ilijaa hali ya kukata tamaa

‘sasa ndio utake kuuza kibanda changu sababu ya mwanamke?....Nyanza!’mama Nyanza aliongea kwa hasira akizungumzia nyumba ya vyumba viwili aliyokuwa amemaliza kuijenga eneo la mbali kabisa na pale walipokuwa wanaishi. alishachoka maisha ya kupanga na kuhangaika na kodi hivyo aliamua kudunduliza pesa  na kujenga numba hiyo ya matofali ya kuchoma iliyoezekwa mabati yaliyotumika.

‘Nifanyeje sasa….nitoe wapi hata laki moja nikamgomboe Sindi?..... unataka kuniambia mama nikae chini niangalie tu Sindi akichukuliwa bila kufanya lolote?’ Nyanza alionekana kuchanganyikiwa
‘Sasa hilo lolote ndio ukauze nguvu zangu ili uone…huyo mke utamuweka wapi?’ mama yake hakumuelewa

‘Mama nitakujengea…. nitakufanyia mambo makubwa mama….nisaidie angalau nizuie ndoa ya Sindi….nitampoteza’ Nyanza alimfuata mama yake na kumbembeleza akishuka miguuni

‘Hebu ondoa huo upumbavu kichwani….baba yako nilimpenda kidogo nilete maafa nyumbani kwetu…leo hii yuko wapi?.... yuko wapi?.....yuko wapi huyo baba yako’ Mama Nyanza aliongea kwa hisia, akitumia sauti ya kukaripia
‘Amekufa’ Nyanza akajibu kinyonge akiwa pale miguuni pa mama yake
‘Nimekufa naye?....amenisubiri tufe wote?.....amejali hata kungoja niagane naye?....’ Alimporomoshea mwanaye maswali

‘Mama….Sindi yu hai…. nisaidie mama’ Nyanza alikuwa naomba ruhusa ya mama yake ili akauze ile nyumba  na kupata mahari amabyo alihisi ingelipia deni la Mzee Dunia wakati akiwa hajui hata hilo deni ni kiasi gani. Kichwani mwake alitaka kuiuza nyumba ya mama yake kwa shilingi laki saba akiamini laki 5 zingekuwa mahari na laki mbili zingekuwa za kufanyia harusi.

Wakazozana na mama yake sana, kiasi kwamba mama yake akaamua kuondoka pale uani na kuelekea kazini kwake. Nyanza kama mtu aliyechanganyikiwa alitoka pale kwao na kuelekea kule bondeni iliko nyumba ya mama yake.
Akili yake ilishaamua kuwa angeiuza ile nyumba potelea mbali, kwake yeye alihitaji laki tano za kugomboa Sindi bila kujua mwenzake Mzee Dunia alishagharamia kwa milioni na uchafu na Jerry Agapela alikuwa anakuja na kitita zaidi ya wote wawili….

……..NYANZA ATAMGOMBOA SINDI WAKE…..??

2 comments:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger