Monday, May 6, 2013

SINDI....na LAURA PETTIE (12)

12
SEHEMU YA 12
Jerry Agapela alimtazama mdogo wake  kwa huzuni, katika umri kama ule alipaswa kuwa mwenye furaha na ari ya kutimiza ndoto zake, lakini haikuwa hivyo Jenifa alikuwa na jukumu kubwa la kumuangalia mama yake kwa takribani saa 24 za siku yake.

Alilala kwa taabu akiingoja kesho bila matumaini yoyote. Kutoka maisha ya hali ya juu mpaka maisha duni ya kutojua kama angepata hata mlo wa siku moja au la ulikuwa ni mtihani mkubwa mno kwa Jenifa Agapela.



Jerry alijitahidi kutulia, akiacha kulia kwa kugundua alizidi kumchanganya Jenifa ambaye alikuwa akimtazama kama mhimili wake kwa wakati ule. Akashusha pumzi na kutazamana na Jenifa ambaye sasa alicha kulia kwa kwikwi na kuendelea kufuta machozi yaliyomjaa machoni mwake kila sekunde.

‘Umepata kodi?’ Jenifa akauliza akivuta kamamsi nyepesi ziloiozletwa na kule kulia. Kerry akaitikia kwa kichwa, maskini alijaribu kutabasamu katikati ya ile huzuni.
‘Umepata wapi?’ Jenifa akauliza kwa sauti ya upole lakini macho yake yakimtazama Jerry moja kwa moja kwenye mboni ya macho yake, ni kama vile hakutaka kudanganywa.  Jerry hakujibu swali lile, alishusha kichwa chini nah ii ikampatia jibu Jenifa.

‘Pamela!’ akajijibu lakini pia alilitamka lile jina kujiridhisha kuwa alichokuwa amejibu kilikuwa sahihi. Jerry akaitikia kwa kichwa, moyo wake ukipata dhoruba kali kwa kuhisi kushuka kwa uanaume wake mbele ya mdogo wake. Hakutaka kumdanganya!

‘Here we go again…’ Jenifa akatamka akiwayawaya
‘unadhani ningefanyaje Jeni….huoni karibia tutatupiwa vitu nje’ Jerry akajitetea kwa bidii akiwa ameshusha sauti isiisikiwe na baadhi ya wtau waliokuwa butanini pale. Jenifa akanyanyua mikono kama mateka, uso wake ukiwa umetahayari na yale machozi yakikatika ghafla.

‘hata kama Jerry….tatizo sio msaada…’ akadakia Jenifa
‘kumbe?’ Jerry naye akamdaka haraka wote wakionekana kuanza kutembelewa na jazba
‘tatizo mtoa msaada…. hukuweza kufanya kitu kingine tukapata kodi zaidi ya kusbiri pesa za Pamela kila siku?’ Jenifa alihoji kwa hasira bila kujua ni kiasi gani alikuwa anazidi kumuumiza Jerry

‘Jenifa!’ Jerry aliita kwa sauti iliyojaa ghadhabu, akiwa amemtolea macho mdogo wake na ile sauti yake ikipaa na kuwageuza shingo watu waliokuwa eneo lile. Kule kuangaliwa na watu kumfanya ajishushe na kupepesa macho kuangalia ni wangapi walikuwa wameshtushwa na kelele zake. Akashusha pumzi na kujaribu kuidhibiti hasira aliyokuwa nayo wakati Jenifa aliyekuwa anamtazama kaka yake kwa hasira akigeuka na kutazama pembeni.

‘Najaribu kufanya kila ninachoweza Jeni…..I’m trying….mle, mama apate chochote cha kutia tumboni…najaribu Jeni….angalau tusiadhirike zaidi….it seems huoni jitihada zangu…’ Jerry aliongea akipepesa macho na kutetemeka midomo
‘Sijasema sioni jitihada zako’ Jenifa alijibu pasipo kumtazama kaka yake
‘then tatizo liko wapi?’ Jerry akauliza akimtazama mdogo wake na asimuelewe

‘Pamela!’ akajibu Jenifa na kumfanya Jerry afinye uso wake kidogo na kupunguza ukubwa wa macho yake, ilhali paji la uso wake likijenga ndita kadhaa
‘Amefanya nini?’ Jerry akauliza akizidi kuukunja uso wake
Jenifa akajibu. Jibu jepesi tu, jibu lililomfanya Jerry ajikute akitabasamu kwa huzuni na kutikisa kichwa kulia na kushoto mara kadhaa huku akitazama chini.
‘unasemaje?’ akamtaka Jenifa alirudie jibu lake
‘Simpendi!’ Jenifa akalirudia kwa msisitizo

Jerry akashusha pumzi kwa mkupuo wa nguvu, alihisi hasira. Kama si kuwa katika mazingira yale waliyokuwepo si ajabu angemtandika mdogo wake kofi moja la kumrejeshea ufahamu katika neva zake. Jerry hakuwa na kazi ya maana licha ya elimu aliokuwa nayo, aliishi kwa vibarua vya hapa na pale ambavyo wakati mwingine alijisikia hata aibu kuvifanya, lakini ilimpasa kugangamala ili maisha yaende.

Pamela Okello, msichana aliyekuwa rafiki yake na mtu wake wa karibu ndiye hasa aliyekuwa akiokoa jahazi mara kwa mara kila alipikwama uko kwenye vibarua vyake.
Hakupenda kumtegemea Pamela, wala hakuwa najisikia fahari kupokea pesa za mwanamke kwa matatizo yake, lakini angefanyaje?....angelipaje kodi hali pesa yote aliyopata ilitumika kuwatunza wao watatu.

Jerry alihisi mdogo wake alikuwa akiyatazama maisha kirahisi zaidi kwa vile tu alikuwa akiletewa chochote kilichopatikana pasipo kujua shuruba na madhila aliyokuwa akikutana nayo kaka yake katika hizo harakati za kutafuta pesa na kisha kuambulia pesa ndogo sana iliyotosha kuishia kwenye chakula na nauli.

‘Tutaonana baadaye’ akaamua kuaga ili kuepusha shari zaidi
Kama anakupenda sana aje akusaidie kumuuguza mama hapa hospitali’ Jenifa akaipalilia shari wakati Jerry akinyanyuka

‘Jeni Please!...’ Jerry akamjia juu mdogo wake akimsonta kwa kidole cha shahada cha mkono wa kushoto, Jeni akageuza uso na kuunyanyua kidogo kumtazama usoni kaka yake aliyekuwa amesimama kando yake.
‘na bado huoni dharau anayoifanya?....mtu anakuja kumuona mama yako hata kumgusa mkono anaona kinyaa?.... halafu bado unamtetemkea kwa vijipesa vyake…’ jenifa aliongea kwa hisia na hasira ndani yake. Jerry akazidi kumkunjia uso!

Jenifa naye akasimama, na kuivutia juu suruali ya jeans aliyokuwa amevaa, kisha akamtazama kaka yake aliyekuwa bado amemkunjia uso, akimtazama katika namna ya kutomuelewa
‘na sijaona kinachokufanya umkatae Clarita sababu ya mwanamke kama huyu…  kwa Pamela you are after money Jerry ..shame on you!’ Jenifa alitoa dukuduku lake. Akimtaja Clarita rafiki yake kipenzi ambaye amekuwa akimlilia Jerry miaka kwa miaka kiasi cha kuamua kuondoka nchini na kwenda nje kimasomo angalau kujiweka mbali na mwanaume anayempenda.

Jenifa akaondoka na kuelekea wodini, akimuacha kaka yake anamtazama mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yake. Jerry akarudi chini taratibu na kuketi pale alipokuwa ameketi mwanzo. Kauli za Jenifa zilimuumiza sana, alimpenda Pamela toka moyoni ingawa ni kweli Pamela hakuwahi kumkaribia mama yake kila alipofika hospitali kumsindikiza kumuona.

Ni kweli mara kadhaa Pamela alikuwa akibaki garini na kutoenda wodini kumuona mama yake, akidai kelele za mama yake na vile alivyokuwa amekonda kulimuogopesha. Yeye binafsi hakuona ubaya wowote lakini matendo yale kwa Jenifa yale yalikuwa matusi ya nguoni!
88888888888888888888888

Hali ya Sophia Agapela ilizidi kuwa mbaya siku hadi siku na mumewe hakukanyaga kumuona mkewe hata siku moja, wala hakujali watoto wake walikuwa wapi, na  wakifanya nini. Alisha muhamishia Fiona ndani ya jumba lake uko masaki na maisha kwake hayakusimama, yaliendelea!

Mchana wa siku hiyo ya jumamosi. Fiona alitoka kwa rafiki yake Azda wakiwa wanasindikizana kuelekea getini, Fiona alicheka kicheko kirefu cha ushindi, akiongea kwa tambo za kike. Yake mavazi ya gharama aliyokuwa amevaa yalimfanya azda amkodolee macho mara mbilimbili.

‘hajaenda hata kutoa pole ya uongo na kweli?’ Azda akauliza kwa mshangao, wakisimama kwanza na kuongea vizuri
‘Nini kumuona? hata simu ya kumjulia hali hakuna….unamjua Fiona au unamsikia?....niliaga kwetu, nikaagwa nikaagika!’ Fiona alitamba. Mkono wake wa kushoto ulijikunja na kuining’iniza pochi kubwa ya gharama, kitenge cha wax toka Holland kilimkaa vyema na fundi akautendea haki ule mshono wa ile nguo ya Fiona.

Kichwani alikuwa na nywele za bandia, zilizoshonewa kiumaridadi, achilia mbali kabisa kiatu kirefu alichokuwa amevaa, kilicholandana na rangi ya kitenge alichokuwa amevaa.mapambo ya dhahabu za uzani wa kutosha yalihitimishwa na ufunguo wa gari aliokuwa ameushika mkono wa kushoto sambamba na simu za bei mbaya mbili. Kwa jicho la kwanza tu ungekiri mwanamke huyu alikuwa na maisha ya hali ya juu mno!

‘Heheheheeee haloo ya kihindi….’ Azda akashabikia akicheka pia
‘Veeevee’ wakaitikia pamoja kishabiki na kucheka zaidi
‘Yule mganga kiboko ya reli wallah…. waganga na waganguzi uko Saint Imakulata wanamshindilia midawa tu hahahahaaa….wangejuaaaa!...’ Fiona alitamba
‘Yaani balaa…. ‘ Azda akaitikia wakianza tena kutembea kisha wakasimama tena

‘Wiki hii ..’ Fiona akasema akifanya ishara ya kufunika kitu
‘Eeeh! usinambie!’ Azda akakodoa macho yake kwa bidii
‘Ndi hivyo…nataka hizi karaha za simu kila siku sijui anakulilia sijui kazidiwa sijui bili ziniondoke kabisaaa’ Fiona akaongea kwa kujiamini na sasa wakianza tena kuelekea getini.
‘Mmh! una roho mwaya…’ Azda alitembelewa na hofu kidogo
‘Ya chuma cha pua….shoga ngoja niwahi uko kwa babu ikamalizie kazi, utasikia tu….’ Fiona akaaga, na azda akamsindikiza mpaka getini alikomuacha atoke mwenyewe kisha yeye Azda akafunga geti na kusimama pale getini akiwa na uso uliojaa hali ya kutoamini.

‘Vipi ameenda?’ mdogo wake Azda aliyekuwa anaanika nguo mbali kidogo na lilipo lile geti akamshtua dada yake
‘Kaenda mwenzangu….yaani Fiona ana roho jamani…. Sophia huyu huyu ndiye aliyemsitiri alipofukuzwa kazi….. Sophia huyuhuyu ndiye aliyemtafutia hii kazi anayofanya na ndiye alimsaidia hata akaonekana mtu hapa mjini…’ Azda akaongea kwa mshangao uliochanganyikana na huzuni, mkono wa kushoto ukilala kifuani kama mtu anayesikia maumivu ya moyo.

‘Hivyo!?’ mdogo wake Azda aliachana na nguo zile na kumsogelea dada yake
‘Yaani alikuwa rafiki yake wa kupika na kupakua…. leo hii kamfanyia mandingo dada wa watu jamani…maana aliona kumtoa kwa mumewe haitoshi…kamlaza na kitandani….na hivi ndio anataka kumzika kabisa!’ Azda akamfanya yule mdogo wake amtolee macho kana kwamba Azda alikuwa akigeuka kuwa zimwi mbele ya macho yake.

Wakasikitika kwa pamoja, huku kila mmoja akiwaza lake
8888888888888888888

Sophia hakumaliza wiki tangu ile siku ambayo Fiona aliongea na Azda. Sophia alikufa!
Saa chache kabla ya kufa Fiona alimtembelea hospitalini na akamkuta akiwa na hali yake ya siku zote ya kulia na kuomba aitiwe mumewe. Alipomuona Fiona alinyamza ghafla, alitulia tu akimtazama Fiona huku machozi mengi yakimtoka. Alimeza mate kwa uchungu, yakipita kooni kwa taabu.

‘hata wewe?...hata wewe Fie?’ Sophia alimuuliza akilikatiza jina la Fiona kama alivyopenda kumuita enzi za urafiki wao.
‘Mume wangu yuko wapi?’ Sophia akauliza akizidi kutiririkwa na machozi
‘Mumeo?...Sophie!...bado unahesabia tu kuwa una mume?’ Fiona akamuuliza kwa kejeli lakini uso wake ukionyesha huruma, kama mtu angelikuwa mbali akiwatazama si ajabu angelihisi Fiona alikuwa akitoa maneno mazuri ya faraja kwa mgonjwa.

Sophia hakujibu kitu, aliendelea kumtazama Fiona kwa huzuni na pengine majuto ya kumkaribisha nyoka maishani mwake. Fiona akangaza angaza huku na kule kabla ya kufunua mkoba wake na kutoa kitu kama unyoya, akaupitisha haraka usoni pa Sophia na kuurudisha mkobani kwa kasi ya ajabu. Sophia akapoteza uwezo wa kuongea hapo hapo!

Huku akitabasamu Fiona akamuinamia Sophia na kumtazama namna alivyokuwa akihangaika kutoka kuongea pasipo kuweza. aliyaona mateso yote aliyokuwa akiyapata Siphia pale kitandani wakati mishipa ya shingo ikimkakamaa kwa nguvu alipotaka kuzungumza.
‘Tulia ufe taratibu dear…uhitaji kukurukakara zote hizi’ akamwambia kwa upole akitabasamu, taratibu akajiinua na kusimama wima, kwanza akatoa gloves na kuzivaa, kisha akitoa kile alichokikusudia!

Fiona akaangaza tena kitahadhari na kisha kwa haraka akaikamata chupa ya drip iliyokuwa pembeni yake ikining’inia na kuipachika ile sindano aliyoitoa mkobani. Sophia akafurukuta, akitamani kupiga kelele, akitamani kumzuia Fiona asimtendee unyama ule lakini hakuweza kusogeza hata kidole.

Sumu iliyokuwa ndani ya Sindano iliishia kwenye drip na Fiona akairudishia sindano mkobani.
‘Kalale pema peponi’ akasema akitabasamu, tabasamu la ushindi kisha akatoka kwa madaha na kutokomea. Sophia alilia kwa uchungu, akionekana kuumizwa na ila hali pasipo kuweza hata kusogea.

Jenifa aliyekuwa anasuuuza vyombo nje, alirejea  wodini alikokuwa mama yake na akipishana na Fiona pasipo kumtambua lakini aligeuka na kumtazama pengine akivutiwa na vile alivyovalia.
Akaingia na kuweka vyombo juu ya kabati,  kisha akaketi kwenye kiti kilichokuwa kando akisoma gazeti lake. Hakumtazama mama yake, aliketi na kuendelea kusoma gazeti la udaku alilolikuta juu ya kabati huku mama yake akimtazama katika namna ya kutaka kumuomba msaada. Jenifa alizidi kutopea gazetini, akicheka ile alichokuwa anakisoma pasipo kujua mama yake alikuwa katika maumivu makali mno!

……TUKUTANE HAPAHAPA….. UNA MAONI GANI MSOMAJI?

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger