9
SEHEMU YA TISA
Kule ndani ya gari yule binti alikuwa kitetemeka kiasi kwamba
alishindwa kuiokota simu iliyokuwa imengukia miguuni pake huku ikiita. Wakati
akiitazama taswira ya uso wa mtu uliokuwa ukimchungulia kwenye kioo cha dirisha,
ghafla tu akayahamisha macho yake na kutazama kioo cha mbele cha gari, akamuona
mwanaume wa rika la kati akiteremsha kimpando kidogo kilichokuwa kikishuka
kuelekea pale alipokuwa, alimtazama mwanaume huyu aliyekuwa na jembe begani na
moyo wake ukaingia amani toka kusikojulikana. Alihisi ahueni ikimjia!
Yule mwanaume aliwafikia na kuwaelekea wale wanaume wengine
waliokuwa upande wa kulia wa gari lake. Akamuona akizungumza nao huku akicheka,
taratibu akanyoosha shingo yake mbele akitaka kumtazama vizuri kijana huyo aliyekuwa
amesimama mkabala na tairi la mbele la kulia, akiwa amelitua jembe lake
chini na kuliegesha kwenye gari
lake.
Hakujua kwanini, lakini ujio wa kijana yule pale, ulimletea
amani na tumaini la kutoka pale salama.
Baada ya mazungumzoa mawili matatu huku akicheka na wale wanakijiji wenzie.
Nyanza alizunguka upande ule aliokuwa ameketi yule binti, akipita mbele ya gari
na kumfanya yule msichana amfuatize kwa macho mpaka aliposimama kwenye kioo cha
dirisha la gari na kumgongea kidogo.
Kwa mikono yenye kutetemeka, alibonyeza kitufe kilichoruhusu
dirisha lizame chini taratibu na kukutana uso kwa uso na Nyanzambe. Akamuinulia
macho na kumtazama mwanaume huyu ambaye kwa tabasamu la kiuungwana alimsabahi
kwanza.
‘habari yako?’ Nyanza alimsalimu
‘Kama unavyoona…..’ alijibu binti yule
kinyonge huku uso wake ukiwa bado haujaondokana na wasiwasi uliomletea jasho
usoni.
Nyanza alijirudisha nyuma kidogo na kuangalia tairi la nyuma
lililokuwa limetitia katika udongo kiasi cha kutoonekana. Akatikisa kichwa
kuashiria hali ilikuwa mbaya mno huku akitoa mlio uliofanana na ule wa kumuitia
paka chakula!
‘limetitia sana
dada…’ Nyanza alimwambia yule binti akionyesha kina cha kutitia kwa kwenda
chini.
Msichana hakujibu kitu, alimtazama Nyanza kama
mwokozi wake na hili Nyanza alilielewa.
‘Shuka tujaribu kuliondoa hapa’ Nyanza akampa maelekezo
ambayo binti yule aliyatii kwa haraka, akionyesha imani yake kwa Nyanza.
Aliteremka na kusimama kando akiwa amekumbatia mkoba wake mkubwa kifuani na
sasa ndio akawaona vizuri wale vijana waliokuwa vifua wazi.
Wakamsabahi kwa kumpungia, pamoja na kujaribu kumuonyesha
walikuwa pale kwa nia ya kumsaidia, bado binti huyu aliwatazama kwa mashaka
kidogo, akiyatupia macho yake mapanga waliyokuwa wameshika sambamba na zile
sura zao ngumu zilizoonyesha kukomaa kwa shida za kijijini hali weusi wa dhiki
ukiwa umewakomalia miilini.
Nyanza akasemezana nao kilugha na wale vijana wakacheka sana ,
wakianza kuzunguka kule alikokuwa amesimama Nyanza akilitazama lile tairi.
Baada ya majadiliano ya hapa na pale ambayo binti yule hakuyaelewa sawasawa
sababu ya kuchanganywa kwa Kiswahili na lugha yao .
Vijana wawili waliweka mapanga yao
chini na kukimbia kurudi kule walikotokea huku waliobaki wakijaribu kuinua ule
upande wa gari uliozama udongoni.
Tairi lilikuwa limechimba mno, Wakashauriana kutumia jembe
kuchimba sehemu ya udongo ili kulipa tairi nafasi ya kuchomoka pale. vijana
wengine wawili nao wakaondoka kufuata majembe huku mmoja akimletea Nyanza lile
jembe lake.
Akabaki Nyanza peke yake na yule binti alikuwa bado amesimama
umbali mfupi akimtazama Nyanza kwa udadisi. Taratibu akaivuta tshirt yake na
kuivua, misuli ya kiume iliyojengeka vyema kifuani pake na mikononi ilimfanya
binti yule amkodolee macho Nyanza katika namna ya kuvutiwa naye.
Akachuchumaa na kuvuta panga mojawapo lililokuwa pake chini
na kuanza kuchimba, akiweka nafasi kwa ajili ya jembe. Aliifanya kazi ile kwa
dakika kadhaa na ndipo wale vijana wawili walioondoka mara ya kwanza wakarejea
na chumba kipana kilichoonekana kuwa na uzito wa kutosha kuwaelemea wale vijana
kwani walionekana kukibeba kwa taabu kidogo.
kisha wale waliofuata majembe nao wakarejea, kazi ikaanza.
Haikuwa kazi rahisi lakini ilitimia na Nyanza akamwambia binti yule aingie
garini na kuliondoa gari huku tairi likipita juu ya kile chuma kipana. Gari
likanasuka na binti yule akaliendesha mpaka sehemu aliyohisi ni salama na
kuliegesha. Akashuka akitabasamu na kuwafuata wale vijana waliomsaidia.
Akashukuru, akashukuru tena na tena nay ale mashaka
aliyoyajenga kwa kuwatazama sura tu, yakatoweka! Akafungua mkoba wake na
kuupekua pekua, akatoa noti kadhaa za elfu kumi kumi na kuwapatia wale vijana
ambao walizipokea kwa furaha nao wakishukuru. Nyanza akakataa kuzipokea zile
pesa!
‘Kwanini?’ binti yule akauliza akishangaa pia
‘Ni msaada tu dada yangu….’ Nyanza akajitetea akiokota jembe
lake
‘Kwani hawa waliopokea si nao wametoa msaada’ utetezi wake
ulipanguliwa. nyanza kacheka kidogo na kuamua kuupokea ile shukrani.
‘Samahani kwa mwenyekekiti wa kijiji ni wapi?’ binti aliuliza
akifunga zipu ya pochi yake.
‘Nyanza anaishi’gi uko….ukienda naye atakufikisha’ga mpaka
nyumbani’ kijana mmoja akamjibu na Nyanza akatabasamu wakati binti yule
alipomtazama kuashiria kuhitaji msaada wake kwa hali na mali .
Wakaongozana kueleka kwenye gari, Nyanza akivua yeboyebo zake
na kuzipakata mapajani mara tu alipoingia garini. Binti yule akacheka kwanza
‘Kwanini umevua sasa….’ akauliza akimtazama Nyanza uso ukiwa
bado na tabasamu
‘matope dada’ Nyanza akajibu
‘Hapana vaa tu bwana….mbona mimi nimekanyaga matope na
sijavua jamani…. ooh jembe tuliweke kule kwenye buti’ akasema yule binti
akitaka kufungua mlango wa gari lake kwa
ajili ya kuliweka hilo jembe kwenye
buti lakini Nyanza akamuwahi..
‘Nitalipakata dada….usipate taabu’ Nyanza akaliingiza jembe lake
kwa taabu kidogo na akipata shida
pia kuliweka sawa pale alipolipakata, akinusurika pia kumgonga nalo yule binti
ambaye alitamani kucheka kwa sauti lakini alijizuia na baada ya kukaa sawa.
Msichana aliwasha gari na wakaondoka kuelekea kijijini.
‘Huku mbali sana
na mjini…. kuna mabasi yanatoka mjini
kuja huku?’ binti yule akavunja ukimya ulioanza kushika usukani kati yao
‘yapo magari ya Ngosha Trans…ila yana masaa ya kuja na
kuondoka….ukiyakosa hayo tunatumia baiskeli au pikipiki za kukodi’
‘Ooh…. hakuna watu wenye magari binafsi’ binti yule akadadisi
na Nyanza akaonekana kumshangaa kidogo
‘Kijijini hapa?’ akataka kwanza uhakika
‘Yeah…yaani kama watu wenye magari yao
kwa shughuli binafsi tu’ akatoa ufafanuzi na kumfanya Nyanza acheke kidogo
‘Anhaa…kuna tajiri Mzee Dunia na maduka kule juu ndio ana gari yake’ Nyanza akajibu
akimtazama kwa umakini yule binti
‘Mtu mmoja tu ndio ana gari?’ binti yule alishangaa na Nyanza
naye akamshangaa kwa kule kushangaa
‘Ehee….alikuwaga nayo mawili…akauza moja….ni tajiri ndio
maana ana gari’ Nyanza akajibu na kumfanya yule binti apate picha uko aendako.
Umasikini ulikuwa wa kutosha kiasi cha mtu kuhisi kumiliki gari ni utajiri.
Akatabasamu tu na kushusha pumzi.
‘Unaitwa nani?’ akatabasamu zaidi alipouliza hili swali
‘Nyanzambe Festo Mugilagila’ akajibu akilitamka jina lake
lote
‘Wow! what a name!...naitwa Pamela’ akajitambulisha yule
msichana
‘Nashukuru kukufahamu….pindia huko hivi’ Nyanza akamuonyesha
kona ya kupiga
‘…nyumba ile pale ndio
kwa mwenyekiti’ akajibu Nyanza na hapo hapo akitazama ile njia inayoelekea kwao
‘Mi’ naishi huku …nishushie tu hapa’ Nyanza akaomba msaada
tutani na Pamela akaliegesha gari kando ya barabara, akamgeukia Nyanza
‘ooh…okay!....una namba za simu’ Pamela akauliza na Nyanza akatikisa
kichwa kuashiria hapana.
‘Sina simu dada…. Asante
sana kwa lifti’ Nyanza akashukuru
akifungua mlango wa gari ili ashuke
‘ Okay…basi ….’ akamkatiza Nyanza asishuke na Nyanza
aliyekuwa ameshashusha mguu mmoja
‘Chukua hii business card yangu…kama
utapata mawasiliano…usisite kunitafuta…asante
sana Nyanga kwa msaada’ Pamela
akashukuru tena
‘Ni Nyanza…Nyanzambe’ Nyanza akamrekebisha na Pamela akacheka
‘Pole!...Nyanza …Nyanza …Nyanza…nimekariti sasa’ Pamela
alifanya mzaha uliomfanya Nyanza acheke kwa sauti kidogo na kuteremka.
Akampungia mkono na Pamela akapunga pia na kuliondoa gari kuelekea pale
alipoelekezwa.
Alifika na kumuulizia mwenye nyumba, kisha akamuulizia Jerry.
Dakika tano baada ya kuongea na mwenye nyumba Jerry na chidi waliingia. Pamela
akainuka haraka na kumkumbatia Jerry kwa nguvu mno. Wenyeji wakiwashangaa sit u
kwa kule kukumbatiana bali pia kwa mavazi ya Pamela, kwa kuvaa kile kikaptura
na blauzi iliyoishia juu kidogo ya kitovu kwao alikuwa nusu uchi!
Baada ya kutambulishana na mazungumzo madogo madogo. Jerry na
Pamela wakatafuta faragha kwa kuamua kuongelea garini.
‘I still cant believe you are alive Jerry…’ Pamela aliongea
kwa hisia akilipapasa shavu la Jerry
‘Yes I am… na tuombe Mungu azidi kuniweka hai…it is so scary
Pam…very dangerous…’ Jerry aliongea taratibu akionyesha ni namna gani alikuwa
amejaa hofu juu ya usalama wake.
‘I know…’ Pamela alijibu kwa huzuni
‘….una uhakika hakuna anayejua umekuja huku?...’ Jerry
alihoji akiwa ametoa macho na Pamela akaitikia kwa kichwa.
‘So una mipango gani kichwani?’ Pamela akauliza akibetua
mabega yake yote mawili. Jerry hakujibu haraka, alishusha pumzi na kufumba
macho kichwa chake kikilala kwenye kiti. Akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa
kabla ya kufumbua macho yake na kukigeuza kichwa chake kumtazama Pamela.
‘….Sijui’ kwa sauti ya kukata tamaa Jerry alijibu huku
akiuondoa uso wake machoni pa Pamela na kutazama mbele.
‘kuna chochote naweza kukusaidia?’ Pamela akauliza akianza
kufukuza fukuza mbu waliokuwa wameanza kujazana katika gari. Giza
lilikuwa linaingia kwa kasi sasa.
Wakaongea mengine mengi, Pamela akimpa picha ya hali ilivyo
uko mjini, kuhusu baba yake na matamko yake magazetini. Jerry alikaa kimya tena
akiwaza kitu. kisha kama aliyekurupushwa akamgeukia
Pamela.
‘….utarudi Dar kesho?’ akamuuliza
‘yeah! I have to… kuna kitu unahitaji?’
‘…simu! na pesa ila sina kadi ya benki hata moja….nimepoteza
wallet na kila kitu’ Jerry akasikitika
‘Jerry…huu sio wakati wa kuwaza hayo…niko hapa, nimekuletea
simu na pesa…I guessed ungehitaji vyote hivyo…..all I need ni usalama wako tu…kama
unadhani hapa uko salama kwa sasa basi….tulia kwanza tujue nini ni nini’ Pamela
aliileta nuru usoni pa Jerry akaitikia kwa kichwa.
‘You are the best friend Pam…sijui nikushukuru vipi?....’
Jerry aliugusa mkono wa pamela na kuusugua sugua wakati Pamela akitabasamu
‘You don’t have to thank me….hili ni jukumu langu’ Pamela
akajibu akiona soni kwa mbali
‘Baada ya hili nataka kukuoa Pamela…sichoki kukueleza hili
hata wakati kama huu’ Jerry sasa aliuhamisha mkono wake
toka kwenye kiganja cha Pamela mpaka kiunoni na Pamela akajinyonga kidogo
alipouhisi mkono wa Jerry kiunoni pake.
‘na lini utakubali ukweli kuwa we are friends and that is all
Jerry….’ Pamela alikazia msimamo wake
‘Come on Pam…. ‘ Jerry alibembeleza
‘No!....’ Pamela alikataa na kuutoa mkono wa Jerry maungoni
mwake
‘two years now….miaka miwili Pamela…hunitaki at the same time
wanaume wanakuja maishani mwako na kuondoka….cant you see I’m here to stay!’
Jerry alimsogelea Pamela zaidi
‘Jerry!....sikuja kujadili mapenzi.. sawa!.... we can’t be
together Jerry that is all’ Pamela alitoa tamko lililomfanya Jerry amtazame tu
pasipo kuongeza neno.
Pamela Okello alikuwa aina ya mwanamke ambaye mwanaume yoyote
angevutiwa naye. alikuwa mrefu, mwenye weusi wa mng’ao uliochagizwa na sura
yake iliyokaa kitutsi. alikuwa na umbile tamu, umbile jembamba la wastani
lakini lililogawanyika kike. Alikuwa rafiki yake wa karibu na wa muda mrefu.
Alimuamini mno na alimshirikisha katika mambo yake mengi.
Baada ya kuachana na msichana wake wa kwanza maishani mwake,
Jerry aliumia sana na alikaa muda
mrefu bila mahusiano yoyote mpaka pale moyo wake ulipomchagua Pamela, lakini akakumbana na
kizingiti kikubwa cha kukataliwa huku akishuhudia Pamela akitoka na wanaume
wengine ambao waliishia kutengana naye.
Miaka miwili ilikatika na Pamela aliendelea kushikilia
msimamo wake. Ndani yah ii miaka miwili Jerry aliweza kuufikia mwili wa Pamela
mara mbili na kukutana naye kimwili. halikuwa jambo la hiyari ya moyo, Jerry
alibembeleza mno tena kwa machozi ndipo Pamela alipoamua kumvulia nguo. Mara
hizo mbili alizolala na Pamela ilikuwa kama alimlia
yamini, Jerry alimpenda Pamela maradufu na ombi lake la kuwa naye likakuwa mara
mbili zaidi.
Pamela Okello alimgomea na alikatalia katakata, akimweleza
wazi kuwa hakuwa tayari kumpoteza kama rafiki kwa sababu
ya kujaribu kamari ya mapenzi. Alihisi kama uhusiano wao usingedumu basi
angempoteza pia Jerry ambaye kwake alihisi alikuwa kama
mhimili wa maisha yake.
Pamela Okello aliiona hali ya mfadhaiko aliyokuwa nayo Jerry,
akabadili mada haraka sana
‘Kuna mbu sasa…. twende ndani nikukabidhi kila kitu…but
unaiaminihii familia?’ Pamela akauliza akijipiga piga vikofi kukimbiza mbu na
Jerry akaitikia tu kwa kichwa kisha akafungua mlango wa gari na kutoka. Pamela
akamtazam Jerry alivyopita mbele ya gari na kuielekea ile nyumba ya mwenyekiti.
Akashusha pumzi kwa nguvu na kupandisha vioo vya madirisha. Akashuka na
kumfuata Jerry ndani.
88888888888888888888888888
Fiona Agapela alikuwa restaurant pamoja na rafiki yake Azda
walipata chakula cha usiku. Fiona alitafuta funda lake la mwisho la chakula kwa
haraka na kukishushia na kinywaji chake, alipoitua glasi yake, akatumia ulimi
wake kusafisha safu ya meno yake ya juu kabla kuchukua kijiti cha kuchokonolea
meno.
Rafiki yake aliyekuwa ndio kwanza yu katikati yam lo
alinyanyua kichwa chake na kumtazama Fiona usoni.
‘hivi akija kujua hizi hekaheka utatokea mlango gani?’ Azda
alimuuliza
‘Hawezi….mpaka leo hii hajajua aliyempumzishia Sophia wake
ndio aje kujua hili la usia?..... aah wapi’ alijiamini
‘….lakini hili sekeseke lingekuwa na amani kama
J angepatikana tukalia tukazika….haya mambo ya kupotelea wapi sijui…siku ya
siku mtu anakuibukia vuuup!’ alionya Azda
‘niliowatuma kazi ni watu wanaoijua kazi yao ….wamenihakikishia
alikokimbilia siko kabisa…maana walimchukua mpaka porini uko…..wakampakiza
kwenye helkopta…wakampeleka vijiji gani uko sijui ila ni Shinyanga….sasa
walipompakiza kwenye gari ndio akaanzisha ngumi….piga nikupige ikatembea….ndio
mwehu yule akatoroka ila tayari alishakula kisu cha ubavu na walimsaka kweli
ikaonekana kakimbilia porini zaidi…’ Fiona aliongea kana kwamba alikuwepo
‘Enhee!’ Azda akaitikia kishabiki huku akitafuna kuku
aliyekuwa bado kamshikilia mkononi
‘hawezi kuwa hai….tatizo linabaki ‘Will’ ya bwege huyu sijui
itabadilishwa lini’ akalalamika kidogo
‘ukute na hekaheka hiyo wewe ndio umendikwa humo’ Azda
akatania
‘Subutu! ….Kristus huyu huyu ….niliwahi kumdadisi Dennis yule
mwanasheria wake…akaniambia ameandikwa Jerry…just imagine mali
zote zile arithi Jerry wakati mimi miaka nenda miaka rudi napoteza nywele
kisogoni…kha!’ Fiona alimchekesha Azda ambaye alicheka kidogo apaliwe.
‘Wanawake tuna dhambi jamani….yaani mzee wa watu anajua
anapendwa kwelikweli kumbe wapi….watu tunatimiza wajibu tu…’ azda alishabikia
‘kumbe je….na will ikikaa sawa tu nay eye anawafuata
wenzake….’ Fiona akasema kwa sauti ya kunong’ona kidogo akimsogelea Azda.
Wakacheka na kugongeshana viganja vyao
8888888888888888888
Asubuhi ya siku iliyofuata Sindi Nalela alimkia shambani
kwanza kisha karejea nyumbani ambako aliweka jembe lake
jikoni na kuchapa mwendo kuelekea
nyumbani kwa mwenyekiti. Alifika pale nje ya kubisha hodi huku akiendelea
kushangaa gari lililokuwa limeegeshwa nyumbani kwa mwenyekiti.
Akatoka mama mwenye nyumba na kusabahiana na Sindi. Sindi
akaomba mzigo aliotumwa na mama yake. Mke wa mwenyekiti akaingia ndani na
kumuacha Sindi amesimama pale mbele ya nyumba, akilitazama lile gari.
Wakati akilisanifu kwa macho, mbele yake akamuona Jerry akiwa
na binti aliyevalia mavazi ya kisasa, wakitembea taratibu kuelekea pale
alipokuwa amesimama. Ni dhahiri walikuwa wanatoka matembezini. Sindi akarudi
nyuma kidogo kutoa nafasi mlango ingali wakiwa mbali kidogo.
Walipomfikia, Jerry alimchangamkia Sindi ambaye alishindwa
kutoa ule uchangamfu wa siku zote akichelela kumkwaza Pamela ambaye hakumjua ni
nani kwa Jerry.
‘utaenda kufundisha leo?’ Jerry akamuuliza na Sindi akaitikia
kwa kichwa, wakati wote huo Pamela akimtazama Sindi kama
kinyago asichokielewa.
Aliazia utosini kwenye nywele nyingi, ndefu na za asili,
akaja katika gauni lililopauka na kushikizwa ovyo ovyo, akahamia kwenye khanga
kuukuu aliyokuwa amevaa, kisha akaitazama miguu yake iliyokuwa peku ikiwa na
tope la shamba. Alimuonea kinyaa!
Sindi akatabasamu tu kipumbavu kila Jerry alopomzungumzisha
mpaka pale mwenye nyumba aliporejea na mfuko mdogo ambao Sindi aliupokea kwa
kupiga goti mpaka chini kama ilivyokawaida yake na heshima ile ilimfanya Pamela
azidi kumtazama kama kituko ila ndani ya moyo wake wa kike alikiri Sindi
alikuwa msichana mzuri sana kwani pamoja na uduni wake wote, uzuri asilia wa
Sindi ulionekana dhahiri!
Pasipo sababu ya msingi alihisi tu kutompenda Sindi!
....UNA LA KUSEMA?..... LISEME TU!
No comments:
Post a Comment