7
SEHEMU YA SABA
Siku mbili baada ya ugomvi wa ngumi kati ya Jerry na
Nyanzambe. Jerry alikuwa akizungumza na Mama Alma ,
nesi aliyekuwa akimhudumia na kumtazamia kidonda chake.
‘Hali yako haijawa njema bwana mdogo….sitarajii ujitoneshe
kiasi hiki na uone ni jambo dogo’ Mama Alma alimgombeza Jerry wakati akifunga
vifaa vyake baada ya kumsafisha kidonda
‘Ilikuwa bahati mbaya mama…’ Jerry alisema akijitutumua
kutabasamu katikati ya maumivu aliyokuwa anayasikia
‘Na isijirudie tena…umenielewa?’ Mama Alma alimuuliza uso
ukiwa na ile huruma ya kimama. Jerry akaitikia kwa kichwa na akuagana na mama Alma
ambaye alitoka na kuishia akimuacha Jerry pale alipokuwa akiuma meno na
kujilaza chali.
Akili yake ilikuw ana mengi kwa wakati ule. Alitabasamu
alipofikiria sababu za yeye kutoneshwa vile. Mwanamke!
Hakuwa mtu wa kupigana sababu ya mwanamke na mpaka dakika ile
hakukuwa na mwanamke mbaye angesimama na kudai Jerry alikuwa mali
yake. Wakati akiwaza hili jina la mtu likapita katika akili yake Pamela Okello!
Mwanamke mrembo, msomi mwenye maisha yake, rafiki yake wa muda mrefu sana
na mwanamke ambaye alikuwa akimpigia misele siku nyingi, akimbembeleza awe
wake, akimshawishi na kujitahidi kumvutia kwake bila mafanikio.
Pamela Okello alikuwa amegoma kuwa mpenzi wake, alikuwa
amegoma kuvunja urafiki wao sababu ya mapenzi, alimkatalia Jerry katakata
akiutetea urafiki wao. Alikuwa akimngoja Pamela maishani mwake lakini ghafla
hisia zake zilianza kutekwa na Sindi Nalela ambaye ni kama
alimvamia na kuuchukua moyo wake jumla jumla. Jerry alicheka kivivu akikumbuka
tukio la yeye kutandikwa ngumi.
Tabasamu lile likafifia taratibu alipoirudisha akili yake
katika kile alichokuwa akikiwaza usiku na mchana. Moyo wake uliumia na
akajikuta akifumba macho na kuyasikilizia maumivu yale sambamba na hasira
zilizomtembelea kila alipofikiria kitu hiki
‘baada ya kumuua mama ameona na mimi animalize….i hate you….i
hate you’ alitamka kwa ghadhabu kali alimfikiria baba yake. Alizisikia vema
kauli za wale waliomteka na kumburuza kama gunia.
Aliwasikia vema wakati wakipokea maelezo ya namna ya kumuua na aliisikia vema
mmoja wa wale watu waliomteka akimuarisha mwenzake ampigie simu Agapela.
Moyo ulitikisika kwa ghadhabu…. Aliuma meno na kudumba tena
macho safari hii akiyasikilizia maumivu ya moyo na maumivu ya kidonda chake.
8888888888888888888888888
Jerry Agapela alishusha pumzi na kuikodolea macho dari kana
kwamba ingempatia majibu ama japo tulizo la moyo kwa wakati ule. Alikuwa na
mipango mingi kichwani aliyotaka kuitekeleza mara baada ya kupona kidonda chake
ubavuni. Kwa wakati huu alitaka kujificha kujijini pale huku akijipanga ni wapi
aianzie mipango yake. Maisha yake yalishakuwa hatarini na kibaya zaidi akihisi
baba yake ndiye aliyekuwa anamuwinda.
Alitulia vile akiipa akili yake nafasi ya kutulia, akiomba
Mungu aliyoyaongea na mwenyekiti yawe kama alivyoahidi.
Kumficha!
Akashusha tena pumzi kwa mkupuo na kugeuza kichwa chake
taratibu akitazama dirishani. Moyo wake ulijaa utusitusi na ghafla tu
alimkumbuka marehemu mama yake. Aliumia, aliumia sana
lakini akajikaza kiume na kutabasamu kizembe akijifariji, faraja ya uongo,
faraja ambayo haikudumu moyoni walau kwa sekunde tano. Uso wake ulijaa
makunyanzi ya huzuni akafumba tena macho kuupisha uchungu uliomchoma mithili ya
mshale wa moto.
Wakati akiwa katika hali ile, Chidi aliingia mule chumbani
akiwa na kikombe cha uji. Akamtazama Jerry namna alivyokuwa amezama mawazoni na
kutikisa kichwa. Haikuwa mara ya kwanza kumkuta katika hali kama
ile. Alitamani kujua yanayomsibu lakini Jerry alikuwa msiri kwake. Akamfuata
mpaka pale kitandani na kumshtua
‘Hey…’ alipaza sauti kidogo na kumfanya Jerry ageukie kule
alikosimama, tabasamu dogo likiijiunda usoni pake.
‘Usiniambie bado unamuwaza Sindi?’ akamtania Jerry akingoja
anyanyuke kidogo na kumkabidhi kile kikombe cha uji
‘hahahahaaa…. kama tu nataka kupokea
kichapo kingine….’ Jerry alijibu akipokea kile kikombe na moja kwa moja
kukikimbizia mdomoni. uji wa moto ulimchoma midomo yake na akajikuta akiupuliza
kupunguza makali.
‘Nyanza yule bwege sana
aisee…. ameshapigana sana sababu ya Sindi….kuna siku alichapana ngumi
sokoni kidogo alale polisi’ Chidi alikuza stori akivuta kiti cha chuma kilichokuwa
pembeni na kukalia kwa mtindo wa kukigeuza sehemu ya mgongo wa kiti kuelekea
mbele.
Jerry akaacha kupuliza uji na kuangua kicheko kidogo
‘Jamaa akajiunge na masumbwi tu….yaani alinishtukiza na ngumi
za ghafla acha kabisa….kwanza nilidhani ananitandika na kipande cha ubao….ila
niliposhuhudia anatoka mikono mitupu nikasema dah!.... jamaa noma’ Jerry
alisimulia akicheka na kumfanya chidi naye acheke kwa sauti zaidi.
‘Yule na mimi hazipandi kabisa….tulishazinguana kipindi
f’lani sababu ya huyu huyu Sindi…. ikawa kila tukikutana mahali ugomvi tu….
mpaka tukawekewa kikao na wazee…. jamaa hajiamini na demu wake kabisa’ Chidi alisimulia sakata lake
na Nyanza
‘Na ndio atampoteza sasa…. but honestly….yule binti
hamstahili mtu kama Nyanza…. she is smart upstairs na
ikitokea akaoga akatakata…akavalishwa kimjini mjini unaweza kuporwa mtoto yule
na rais’ Jerry alitania
‘mambo ya shigongo rais anampenda mke wangu….’ Chidi alirejea
moja ya vitabu vya mwandishi mahiri wa simulizi na kuleta kicheko kati yao
‘Toka moyoni I love that girl….’ Jerry alizungumza akitikisa
kichwa kulia na kushoto
‘we lala hapo umuote tu…. kuna jamaa wa mitaa ya kule karibu
na soko….baba yake ndio anamiliki shule inayoonekana kule kilimani…. alipiga
misele pale miezi na jeuri ya pesa zake mpaka akawekeana na dau na mchizi mmoja
anamiliki mabasi ya kutoka town uko…..
hela zilienda na mtoto alimkosa’ Chidi alimvunja moyo Jerry ambaye alimsikiliza
kwa makini, usoni akionyesha mshangao na dalili za kutoamini.
‘ watoto wa kike wanavyopenda hela…huyu wa wapi sasa’ Jerry
aliuliza kwa mshangao
‘Ndio ujue mshamba mshamba Nyanza kakamatia kifaa….wewe na
pesa zako utaishia kula kwa macho tu’ Chidi alitania akinyanyuka toka pale
alipoketi
‘Kakamatia wapi na mnasema hajafungua kizibo’ Jerry alibisha
akipiga funda kadhaa za uji na kujilamba midomo
‘na ndio ukisogolea unakula ngumi zako mbili tatu hurudi
tena’ Chidi sasa alifanya Jerry acheke kwa muda na kwa sauti zaidi.
Chidi akajinyoosha na kupiga mwayo mrefu
‘napeleka mahindi hapo mashine….tutaonana mida’ Chidi akaaga
akipiga tena mwayo na Jerry akaitikia kwa kichwa akimpa ishara ya dole gumba.
Akabaki mwenyewe.
‘Sindi Nalela…’akalitamka jina hili kwa sauti ya chini ya
kuvutia yenye mbwembwe, akirejesha tabasamu lake
usoni . Kwa wakati ule hakuwa na
hakika kama alitaka kufanya alichokuwa anataka kufanya ingawa
moyo wake ulishamwashia taa ya kijani.
88888888888888888888888
Wakati Jerry Agapela na Chidi wakimzungumzia Sindi Nalela.
Binti huyu alikuwa ameketi kitandani akichezea chezea kucha zake akiwa
amejiinamia. Alitulia hivyo mpaka pale mlango wa chumba chake ulipofunguliwa na
Alma kuingia kwa kasi na kuufunga
mlango. Hali ya kiwewe ikamshika Sindi ambaye alimtolea macho Alma
akimtazama toka alivyoingia mpaka alipoketi kando yake.
Wakatazamana! Alma
akimshika Sindi viganja vyake na kumtazama kwa huruma wakati Sindi alikuwa
akimtazama Alma kwa usongo wa kujua
atakachotamka Alma .
‘Niambie tu…’ Sindi alimudu kutamka akipepesa macho yake
meupe yaliyoanza kujaa chembechembe za machozi. Alma
akameza mate na kumtulizia macho Sindi,
akimtazama machoni kana kwamba hakutaka kutamka lakini ilimpasa kutamka
alichotaka kutamka
‘Amekataa…’ akajitutumua na kumpa jibu Sindi na akishuhudia
mtetereko wa Sindi uliyoyaruhusu mafungu ya machozi machoni yake yadondoke kwa
awamu, akiangua kilio cha chini chini huku akiwa ameziba mdomo wake kwa mkono
wake wa kuume uliokuwa ukitetemeka.
‘nitafanyaje?’ akauliza kwa sauti ya kukata tama
‘muache kwanza apoe….bado ana hasira….’ Alma
alimpa ushauri ambao Sindi aliukataa kwa kutikisa kichwa
‘Vipi ikiwa ndio ameamua kuniacha?..... Mwambie Maria
akaongee naye jamani’ Sindi akazungumza akiomboleza
‘haitasaidia Sindi…mwache atulize akili yake atakufuata tu’
‘Sidhani Alma….alimuona akinigusa, alisikia yote aliyoongea’
Sindi akatoa wasiwasi wake akiuvuta upande wa ncha ya khanga kukausha kamasi
nyepesi puani.
‘kwani kosa lako nini…. si hukumgusa wala kufanya kitu cha
ajabu?’ Alma alitaka uhakika
na Sindi akabetua bega lake la kushoto
juu chini akikataa kutofanya chochote
‘sasa hekaheka ya nini?....unavyo mpaparikia ndio unamjaza
kiburi….hebu tulia kwanza tuone mwisho wake’ alma
alitoa pendekezo ambalo kwa Sindi ilikuwa kama vile
kumtaka ajisahaulishe kuhusu Nyanzambe wake! Hakujibu, alijiinamia kinyonge
machozi yakimuandama tena.
888888888888888888888
Jioni ya kesho yake Mama Sindi akiwa anatwanga mahindi nje,
anaona pikipiki ikija upande wa nyumba yake. Anaachana na kazi ya kutwanga na
kusimama akiitazama ile pikipiki mpaka ilipofunga breki uwanjani pake. Wifi
yake Mama Solomon akiwa na sanduku lake
dogo alishuka katika pikipiki naye
akaweka mchi kando na kumlaki. Wakisalimiana kilugha wakati Mama Solomon
alipokuwa akitafuta hela ya kumlipa dereva wa pikipiki.
Dakika mbili mbele walikuwa mkekani nje ya nyumba, vicheko
vikitawala na stori za kilugha zikichukua nafasi. Nusu saa baadaye Denzi
alikuwa alileta uji wa ulezi katika vikombe na kuwakabidhi. Mkeo wao wape nje
ulizaa kikao ghafla mara baada ya baba yake Sindi kufika.
‘…..Sijaona mantiki ya kumuoza Sindi kwa mtu mzima
aliyejiishia vile’ Mama Solomon alipinga hoja ya kaka yake kumuoza Sindi kwa
Mzee Dunia
‘Imebidi mama Solo…..Sega anahitaji kwenda chuo…hela
inayotakiwa ni nyingi sana …. shamba
langu ndio walichukua na fidia sikupata…. hatumuozi kwa kupenda hata yeye
anajua anaolewa ili tumsomeshe kaka yake’ Mzee Nalela alijieleza kwa dada yake.
‘Sega mwenyewe yuko wapi?’ Mama Solo akauliza
‘yuko mjini uko kwa rafiki yake’ Mama Sindi alijibu, yeye na
mumewe wakimkodolea macho Mama Solomon, dada mkubwa wa Mzee Nalela ambaye ni
mwalimu katika shule moja ya kata kijiji kingine.
‘Kwanza mmemnyima Sindi haki yake ya
kupata elimu…. na pale alipo Sindi sio mtoto jamani….lazima kuna mahali moyo
wake umeshawekeza hisia zake na matarajio ya maisha ya pamoja na kijana
mwenzake….’ Mama Solo aliongea kwa hisia na Sindi pale alipojibanza akatikisa
kichwa kukubaliana naye.
‘…..mnazikatili hisia zake na kumuoza kwa mzee kama
yule….mnamtoa kafara kwa manufaa ya elimu ya kaka yake ambaye sidhani kama
akija kufanikiwa atakumbuka kuna mtu amemfikisha hapo alipo kwa gharama ya
kuuza furaha yake…. yeye Sega kama anajua zinahitajika pesa za chuo kwanini
asiingie shamba akafanya vibarua akakusanya hela?.....wenzake wanalima huku
wanavua samaki na bado wanaingia mtaani kubeba matofali ili wapate hela ya kununulia
mashamba wayamiliki…yeye kaweka miguu mjini anasubiri dada aozwe huku yeye
akasome….kitu gani hiki?’ Mama Solomon aliongea kwa sauti yenye jazba kidogo
‘Sasa mtu msomo kama Sega utamshikisha
jembe wapi wifi jamani….mwenyewe anasema kilimo kazi ya kishamba….’ Mama Sindi
akalalamika
‘na atawatukana sana
tu…kilimo kazi ya kishamba wakati ndio kazi iliyomfikisha hapo alipo…..’
Alizidi kugomba wifi mtu.
‘…Mahari tumeshapokea dada….cha msingi tunamngoja arudi toka
uko mjini dasalama alikokwenda …akirudi amalizie mahari achukue mkewe…. mwisho
atazalia hapa nyumbani adodee hapahapa…..’ baba Sindi alitoa neno lake
ambalo lilionekana wazi kupingwa na
Mama Solomon. Mabishano yakazidi kuchanganyia huku jikoni Sindi akisikiliza
kila neno.
‘Pwachaaaa!’ mlio wa sufuria kudondoka ndio uliokatiza
mjadala mzima. Sindi akageuka haraka kutazama kule ulikotokea mlio. Peter
alikuwa amesimama, mikono kichwani huku sufuria lililokuwa na mahindi ya
kuchemsha likiwa sakafuni na mahindi kadhaa yakiwa yametawanyika huku na kule.
Denzi aliyekuwa anasonga ugali aliachama mdomo wake kwa mshangao wakati Danze
pacha wa Denzi aliyekuwa anakatakata majani ya maboga alikunja tama akiwa na
kisu mkononi, wote wakimtazama Peter.
‘Sindiii….kuna nini uko’ mama yake aliuliza na pasipo kumjibu
Sindi alimfuata Peter na kumtandika vibao mfululizo. Peter akapiga mayowe na
wale wanawake pale sebuleni wakanyanyuka na kukimbilia jikoni.
‘Basi imetosha jamani…’ Shangazi akamdhibiti Sindi ambaye
alikuwa akimtandika mdogo wake vibao huku machozi yakimlenga.
Sindi akajikwatua toka mikononi mwa shangazi yake na kutoka
mule jikoni, akipita kwa kasi pale sebuleni na kuishia chumbani baba yake
akimtazama kwa mshangao pia. Alijitupa kitandani na kulia kwa kwikwi. Hasira!
Mama Sindi na wifi yake wakatazamana.
‘kuna la zaidi hapa wifi….kuna la zaidi ya haya mahindi….’
Mama Solomon akaweka wazi hisia zake na mama Sindi akashusha pumzi kinyonge
akigeuka kumtazama Peter aliyekuwa amejikunyata chini akilia.
Wakati wakitoka mule jikoni Sindi aliwapita na kutoka nje.
Akajitosa katika giza lililopaushwa
na mwanga wa mbalamwezi na kutembea mwendo wa haraka akizipita nyumba kadhaa na
kukata kona moja iliyomuingiza kwenye kichochoro kidogo na kuibukia nyumbani
kwa mama Nyanza. Alimkuta mama Nyanza akichoche moto wa kuni ili uji wa ugali
uliokuwa jikoni uchemke. Akamsalimia mama Nyanza kilugha huku akipiga goti na
mama Nyanza akaitikia akimkazia macho binti huyu.
Kigugumizi kikamshika ghafla, lilikuwa jambo la aibu
kumuulizia mwanaume kwa mama yake. Mwanaume ambaye hakuwa ndugu yake wala mume
wake. Alibaki akimtazama Mama Nyanza kwa huruma akitamani sana
kutamka lolote la kuelezea shida yake lakini maadili yalimbana. Alifuata nini
pale! akajikuta akijiuliza, wakati alipoiburuza miguu yake mpaka pale
alitegemea nini?....angezumza nini?...akajiona mjinga mwenye shahada ya
upumbavu!
‘ Yupo ndani…’ Mama Nyanza alimuelewa akamrahisishia njia lakini bado hakunyanyua miguu yake
kupiga hata hatua moja kuukaribia mlango wa nyumba ya mjane yule. Angevunja
miiko, haikuwa desturi kuingia nyumbani kwa mwanaume ambaye hajakuoa ila mwenye
kujulikana kuwa angelikuoa siku moja. Akazubaa tena palepale akiomba huruma ya
mama Nyanza ambaye sasa alimtazama Sindi katika namna isiyoeleweka.
‘Sidhani kama atataka kukuona’ Mama Nyanza akamkata Sindi
maini
‘Kwanini?’ akazungumza neno la kwanza tangu afike pale na
mama Nyanza akamtazama tu kwa jicho kali kidogo na kuinama, akichochea tena
kuni zake
‘Sijamtendea kitu mama….sijamuumiza Nyanza na sitarajii
kumuumiza’ Sindi alijitetea
‘Naomba uendoke Sindi…. imetosha sasa… Nyanza anahitaji
mwanamke mwenye maadili na anayejua thamani yake….’ Mama nyanza alisimama tena
na kuongea kwa msisitizo.
Sindi akawayawaya, akalengwa na machozi, akatamani kuangua
kilio kilichokwamia kooni. Alikuwa anajua fika mama Nyanza hakuwa anampenda,
alikuwa analijua hili tangu alipoanza uhusiano na Nyanza. alijitahidi mno
kumshawishi mama huyu japo amchukulie chanya na mkamwana bora lakini haikuwa
hivyo. Mama Nyanza hakuonyesha kumkubali
hata kidogo. Daima alimwambia mtoto wake kuwa Sindi Nalela alikuwa si mwanamke
wa kukaa naye kwani angempa jakamoyo na maisha ya wasiwasi kutokana na uzuri
wake na kule kufuatwa fuatwa na wanaume, lakini Nyanza aliponusurika mara
kadhaa kulala polisi au kuumizwa katika ugomvi uliosababishwa na Sindi. Mama
Nyanza alihitimisha kuwa Sindi hakumfaa mwanawe!
Machozi yakamporomoka Sindi hali akimtazama mama Nyanza namna
alivyokuwa akijishughulisha pasipo kujali uwepo wake pale.
‘Naomba nimuone tu mama…’ alirai kwa sauti ya kubembeleza
huruma ya mama Nyanza ambaye aliacha kujishughulisha na kumtazama tena Sindi.
‘Nyanza….’ akaita kwa sauti hafifu midomo ikimtetemeka na
Nyanza aliyekuwa amesimama mlangoni akataka kumfuata lakini mama yake akampa
ishara ya kubaki pale pale.
‘Binti nenda nyumbani…’ mama Nyanza akatoa amri ambayo
haikutekelezeka kwani Nyanza alikatilia mbali na kumfuata Sindi pale alipopiga
magoti. Akamnyanyua na kumkumbatia mbele ya mama Nyanza ambaye alinyesha wazi
kutofurahia hali ile.
Ni kama vile Nyanza alikuwa anangoja Sindi amfuate na
waumalize mgogoro. Wakavutana pembeni na kushikana vizuri kimahaba,
wakikumbatiana kwa nguvu zaidi.
‘Sitaki kuumia tena Sindi…. sitaki kupigana tena…niahadi wewe
ni wangu’ Nyanza alitaka kuhakikishiwa kwa mara nyingine na asikumbuke ni mara
ngapomaliomba kuhakikishiwa juu ya hili na akahakikishiwa.
‘….Nyanza kwanini huaniamini jamani….twende tukale kiapo
chini ya ule mti pale kanisani labda utaniamini….’ Sindi alitoa wazo na
sifikirie mara mbili
‘Kesho jioni twende….pengine nitakuwa na amani….nakupenda
mpaka najihisi kuwa mwehu…’ Nyanza alimshikilia vema Sindi pale chini ya mti
waliposimama
Wakaongea mengi ya wapendanao wakisuluhisha kilichotokea na
Sidni akijaribu kumhakikishia Nyanza kuwa hakukuw ana wa kumtoa kwake.
wakati wakisindikizana, gari dogo aina ya Toyota
corolla muundo wa zamani iliwapita taratibu na wao bila hofu walisimama kando
na kuipisha. Gari lile liliendelea na safari na wao pasipo kujua aliyekuwa
ndani ya lile gari ni Mzee Dunia, mwanaume aliyekwisha toa sehemu ya mahari ya
sindi.
Walishikana mikono wakiendelea na safari yao
hali kadhalika Mzee Dunia akiwatazama kupitia kioo na kukunja uso. Mwanamke
mrembo aliyekuwa ameshikwa mkono alikuwa Sindi, mkewe mtarajiwa. Ghadhabu
zilimmendea taratibu…
…….TUKUTANE TENA HAPAHAPA TUJAZANE NINI KILIFUATA?.....
USIKOSE KUIFUATILIA TAMTHILIYA HII….LETA MAONI YAKO MSOMAJI
No comments:
Post a Comment