11
Pazia jepesi lililojaa matundu yaliyotosha kuigeuza pazia ile
kuwa kama nyavu ya kuvulia samaki, ilipepea dirishani na kuruhusu hewa safi
iliyosukumwa na upepo ipenye kwa mapana na kumfikia Sindi Nalela pale kitandani
alipokuwa amejilaza chali, akili yake ikiwa imekimbilia kusikojulikana na
kukiacha kichwa chake wazi mithili ya mtungi uliotoboka.
Macho yake yaliitazama
dari huku yakifumba na kufumbuka taratibu mithili ya mtu aliyekuwa
akinyemelewa na usingizi. Alikuwa ametopea mawazoni kiasi cha kutojielewa
sawasawa kwa wakati ule.
Roho ilimsuta na kumchonyota kisawasawa, alikuwa amefanya
kitu ambacho hakuwahi kukifanya maishani mwake. Kuguswa na mwanaume mwingine
zaidi ya Nyanza! Wakati roho yake ikimsuta lile tukio kati yake na Jerry
lilipita akilini mwake kama marudio ya sinema na
kumsisimua vibaya mno.
‘hapana…’ akajikuta akitamka kwa sauti, akili ikimrejea na
kumuamrisha kutoka pale kitandani na kusimama katikati ya chumba chake cha
kulala huku mikono ikiwa kiunoni. Alitembea tembea pale chumbani akijaribu
kujiweka sawa lakini haikuwa vile alivyotaka. Shoti ndogo ya msisimko ilimpitia
tena na akajikuta akirejea kukaa kitandani na kuketi kitako, akikipakata
kichwa chake mikononi mwake na kufumba
macho kwa juhudi kubwa.
Ghafla akanyanyuka tena akiwa amejaa hamaniko lililomfanya
aheme bila mpangilio. Kama mtu aliyekumbuka kitu, Sindi
alipiga magoti mbele ya kitanda chake, viwiko vya mikono yake vikiegemea katika
kitanda na viganja vyake kukutana pamoja mbele ya uso wake, akashusha pumzi ndefu
na kufumba macho!
‘…Mungu baba najua nimekosa….najua nimekukosea na nimemkosea
mchumba wangu Nyanza. Mungu… eeh Mungu….’ akasitasita akikosa cha kusema zaidi,
midomo yake ilimwemweseka tu pasipo kutoa neno lingine na shetani akampitia na
kumfumbua macho, akishindwa kuhitimisha sala yake na akajikuta akinyanyuka na
kuketi tena kitako, akiwewesesha macho yake, asijielewe asijitambue!
Wakati Sindi akihamanika peke yake, Jerry naye alikuwa
ameketi kitandani. Kitabu kilichokuwa mikononi mwake kikiwa kama
pambo. Uso wake ulikuwa na hali ya kukosa utulivu hali macho yake yakipepesa na
kuchezacheza mithili ya mtu aliyekuwa akizungumza na mwenyewe mawazoni mwake.
‘Sindi…’ akaita taratibu na kuteremsha pumzi. Simu aliyopewa
na Pamela ilikuwa juu ya meza ndogo kando ya kitanda alichokuwa ameketi. Mlio
wa simu ile ndio uliomtoa mawazoni. Akaharakia kuichukua na kubonyeza kitufe
cha kupokelea baada kukitazama kioo cha simu na kumtambua mpigaji.
‘Hallow…’ akaipokea ile simu
‘Sema Jerry….umefikia wapi?’ sauti tamu ya Pamela ilimfanya
atabasamu kidogo na kuinua ule mkono uliokuwa na kitabu, akakiweka mezani na
kujitelezesha taratibu akijilaza chali.
‘Nimemtafuta Meddy aisee….kasema ndani ya wiki mbili nitakuwa
na sehemu salama ya kuishi na kufuatilia zaidi’ Jerry alijibu na kuusikilizia
upande wa pili.
‘Ooookay!....cant wait to see you here…and… wait…’ Pamela
alikatisha maongezi na akasikika akiongea na mtu pembeni yake, na Pamela
akalalamika kimahaba akimtaka huyo aliyefanya akatishe maongezi asimtekenye.
Jerry akafumba macho kwa na kuyafinya kwa nguvu kidogo, wivu
ukimtekenya moyo na kumuamshia hisia za uchungu.
‘Jerry..’ Pamela akarudi hewani
‘Pam…’ Jerry akaita kwa sauti iliyojaa wahaka
‘Yes dear…kuna tatizo?’ Pamela akauliza kawaida asijue ni kwa
kiasi gani alimuumiza Jerry
‘Uko na Patrick si ndio?’ Jerry akauliza sauti yake
ikionyesha kukosa uvumilivu
‘Come on Jerry…. Pat and me have been dating for almost a
year now…and you know it’ Pamela akajitetea
‘Why are you doing this to me Pam?’ Jerry akauliza
kiunyenyekevu huku akisikilizia maumivu ya wivu
‘I’m your bestfriend na nimeshakwambia hili mara elfu moja
zaidi…. ‘ Pam akajibu kwa sauti iliyoshiria hakutaka kusikiwa na yule aliyekuwa
naye.
‘na hujali hisia zangu…unanipigia simu ukiwa na mwanaume
mwingine na bado unasikilizisha mnayoyafanya sio’ Jerry akalalamika zaidi
‘…umechukulia vibaya Jerry….hukutakiwa kusikia
ulichosikia…I’m sorry!.... and how are things there?’ Pamela akamtaka radhi na
kubadili mada haraka sana . Jerry
hakujibu, akakata simu na kuirushia pembeni ya kitanda. Sekunde mbili
zilipokatika simu ile ilianza kuita tena na mpigaji alikuwa Pamela.
Jerry akainyakuwa simu na kuitazama tua pasipo kuipokea. Simu
ikaita kwa muda na kukatwa. Jerry akaiweka kifuani na kutulia kwanza. Moyo wake
ulikuwa na hekaheka ya ajabu mno. Kiherehere cha moyo kilimfika na amani
aliyokuwa nayo ikachukuliwa mateka. Mlio wa meseji ukasikika, Jerry akainyanyua
simu na kuufungua ule ujumbe.
‘….Unanikasirikia bure Jerry I know you love me lakini bado
mimi ni rafiki tu kwako, anyway ukija tutaongea zaidi. Love you’ aliusoma ule
ujumbe kimya kimya na kutikisa kichwa.
Haikuwa mara ya kwanza kukutana na vitimbi kama
hivi lakini alivivumilia akijipa matumaini ipo siku Pamella angemuelewa na
angekubali kuwa wake wa maisha. Alitabasamu kwa huzuni na kujisikitikia tena na
tena. Mwisho akanyanyuka toka pale kitandani na kutoka mule chumbani,
akijumuika na familia ya Mwenyekiti wa kijiji kwa mlo wa usiku.
88888888888888888888
MIAKA MITATU ILIYOPITA
Ndani ya hospitali ya misheni ya Imakulata, mwanamke mwenye
afya dhohofu alikuwa kitandani akionekana kuwa na maumivu makali mno. Jasho
lilikuwa likimtoka kwa fujo na kuweweseka. Sophia Agapela alikuwa kitandani
pale akiugulia ugonjwa ambao hakuna aliyeujua mpaka dakika ile licha ya vipimo
vyote kufanyika.
Machozi yalimchuruzika pembezoi mwa kona za macho yake wakati
akilalamikia maumivu aliyokuwa anayasikia mwili mzima.
‘Jeni….Jeni…niitie baba yako’ alizungumza kwa taabu akiwa amemshikilia
binti yake kwa nguvu nyingi. Jenifa binti yake wa mwisho akamtazama mama yake
kwa uchungu naye akifuta machozi.
‘Niitie Kristus wangu…Kristus…’ alizungumza akihema kwa taabu
zaidi na akiuma meno kwa maumivu na macho yake yakionekana kukosa nguvu ya
kumudu kumtazama Jenifa ambaye alimtazama mama yake pasipo kumjibu, alikuwa
akiisikia kauli hii kila siku, kila muda na kila wakati aliokaa na mama yake
pale hospitali.
Siku hii ya leo ombi la mama yake lilizidi, aligoma kunywa
hata maji akitaka aitiwe mumewe Mzee Kristus Agapela. Jenifa aliumia zaidi kwa
vile alikuwa anajua ombi lile lisingetimia pamoja na kule kugoma kula na kupiga
kelele za kuitiwa mumewe.
Manesi waliokuwa wakimhudumia walimuita Jenifa pembeni na
kumsihi akamtafute baba yake na kumleta.
‘Hawezi kuja jamani…..nimeshamfuata sana ,
ananifukuza kama mwizi….najua hawezi kuja… hawezi’
jenifa aliongea huku akilia kwa kwikwi
‘basi mpigie simu umwambie hali ya leo ilivyo….mwambie
amegoma kula, hataki dawa wala hatulii ni fujo mtindo mmoja’ nesi mmoja mtu
mzima akamshauri Jenifa ambaye alikuwa akifuta machozi kila dakika.
Pale pale Jenifa akatoa simu yake na kumpigia baba yake, Simu
ile iliita kwa muda pasipo kupokelewa na ilipopigwa mara ya pili simu ikakatwa
haraka sana . Ukimya ukapita kati yao
kwanza kila mtu akiwa ameduwaa. Yule nesi mtu mzima akaichukua simu ya Jenifa
na kupiga namba za Mzee Agapela kwa kutumia simu yake, ikaita mara mbili tu na
kupokelewa
‘Hallow…’ sauti nzito ya Mzee Agapela ikasikika
‘hali ya mke wako si nzuri…kuwa na utu angalau ufike…’ yule
nesi akakatizwa
‘Who the hell are you?’ akauliza Mzee Agapela kwa ukali
‘Mimi ni nesi namhudumia mkeo hapa hospitali…Mzee hali ya
mkeo si nzuri kabisa’
‘Sasa mimi nikija ndio atapona au?...’ akauliza kwa kejeli
‘anakuhitaji... na kiubinadamu huyu ni mkeo…na…’ akakatizwa
tena
‘mkimaliza kazi yenu bili inalipwa kama
kawaida….akifa mnamjua pa kumpeleka…haya mengine naomba sana msijaribu
kuyaingilia hayawahusu’ Mzee Agapela akajibu na kukata simu, akiwaacha wale
manesi na Jenifa wakitumbua macho kana kwamba waliamriwa kufanya vile kwa
pamoja.
Wale manesi wakamtazama Jenifa kwa huzuni iliyochanganyikana
na mshangao.
‘Mzee Agapela ni baba yako mzazi kabisa?’ nesi mmoja akauliza
akionekana wazi kutoamini alichokisikia. Jenifa akaitikia kwa kichwa wakati
yule nesi mtu mzima akimdaka pia kwa
swali
‘na huyu mama yako ni mkewe wa ndoa?’ Jenifa akaitikia tena
kwa kichwa, akiwaacha hoi wale manesi
‘Wanaume!....’ nesi mwingine akashangaa zaidi huku
akijinyanyua toka pale alipokuw ameketi na kusimama akijiandaa kuondoka
‘Mume si ndugu yako mwenzangu….hebu ona huyu mama
anavyoadhirika jamani…. ndugu wengine wako wapi?’ Nesi yule aliyesimama
akamhoji Jenifa
‘Mama hana ndugu…. kuna marafiki zake walikuwa wanakuja siku
hizi siwaoni’ Jenifa akajibu akinyoosha shingo yake na kutazama mlangoni mwa
kile chumba walichokuwemo. Manesi nao wakageuka kutazama kule alikotazama
Jenifa.
Jerry Agapela alikuwa amesimama kwenye kizingiti cha mlango.
Jenifa akamkimbilia na kumkumbatia kwa nguvu, akipata nguvu ya kulia tena akiwa
kifuani kwa kaka yake. Jerry akajikaza na kumbembeleza mdogo wake a hapo hapo
yule nesi mtu mzima akianza kuzungumza na Jerry.
Wakatoka na kurudi wodini alikolazwa mama yao .
Jerry alipomkaribia mama yake alihisi nguvu zikimuishia. Alikuwa anazidi
kudhoofika kupitiliza. Sophia alifumbua macho kwa taabu na alipomuona Jerry,
akatabasamu kivivu huku macho yake yakijaa machozi kwa kasi ya ajabu.
‘Naumia…Jerry…’ akalalamika na kuita mwanawe
‘Naam mama..’ Jerry akamuinamia mama yake
‘Naumia….naumia…’ akalirdia neno hili mara kadhaa machozi
yakizidi kumchuruzika.
‘Pole mama…’ Jerry akamjibu mama yake akijikaza kiume kiasi
cha mishipa ya kichwa kumsimama.
‘Yuko wapi?....’ Sophia akauliza kwa sauti hafifu akijaribu
kutabasamu katikati ya yale maumivu. Jerry akainamisha kichwa chini. hakuwa na
jibu, hakuwa na la kumwambia mama yake, hakuwa na kusema kwa wakati ule. Sophia
akapaza sauti na kuangua kulio ambacho kilileta kelele kidogo ndani ya chumba
kile na ikabidi yule nesi na wenzake wamshike Sophia na kumlazimisha kutulia
huku wakimchoma sindano ya usingizi ili atulie.
Jenifa na Jerry waliliona tukio lile na mioyo yao
haikuvumilia kuendelea kuona hali ile. pamoja na uanaume wake, Jerry alilengwa
na machozi, mishipa ya shingo ikimtutumka wakati alipojaribu kujizuia kulia.
‘hatuwezi kuendelea kumlewesha madawa ya usingizi kila
siku….’ Nesi mtu mzima aliwaambia akina Jerry waliposimama nje ya chumba cha
mgonjwa
‘na nini kitafuata sasa?’ Jerry akauliza kwa suati ya kukata
tama
‘Anamuhitaji mumewe…baba yenu….hatujui nini kitafuata akishamuona
lakini ni vema aje…amsikilize….vipimo vyote vilivyochukuliwa hakuna hata kimoja
kinachoonyesha hata minyoo basi….hakuna!.....’ yule nesi aliongea kwa huzuni
‘Baba hawezi kuja…. hawezi….’ Jerry alijibu kwa simanzi
akionyesha wazi kukata tama kwa hali ya mama yake
‘Hivi yuko Dar es salaam
hii hii kweli?’ yule nesi aliuliza kwa mashaka na watoto wa Sophia wakajibu kwa
kuitikia kichwa. Nesi akashusha pumzi na kuwatazama hawa ndugu wawili katika
namna ya kutamani kuwasaidia na asijue awasaidie vipi.
Akaagana nao na kuwaacha wenyewe kwanza. Wakatoka nje na
kwenda kuketi sehemu iliyokuwa na bustani ya kupumzikia. Jenifa alilia kwa
uchungu na kwa hasira pia, akimtazama kaka yake kama
tumaini pekee lililobaki maishani mwake
‘Jeni…it is gonna be okay…. mama atapona and… and…’ alikwamia
hapo, akishindwa kuhimili donge lililomkaba kooni na kumfanya atiririkwe na
machozi. Wakakumbatiana na kulia kwanza, wakishindwa hata kufarijiana.
Familia yao
ilikuwa imeparaganyika. Baba yao
alikuwa amewafukuza nyumbani kwao na hivyo Sophia na wanawe walikuwa wakiishi
chumba kimoja mitaa ya kinondoni. Jerry alikuwa amemaliza chuo na harakati za
kutafuta kazi zilikuwa zimepamba moto. Jenifa alikuwa ameishia kidato cha tano
baada ya baba yake kutomlipia karo.
Mwaka mmoja tangu ndoa yake iingiliwe na Fiona na kisha
Sophia kufukuzwa, Sophia alianza kwa kuchanganyikiwa kisha kuanza kuumwa
ugonjwa usioeleweka. Miezi sita tu ilitosha kumkongorosha na kubaki mifupa
mitupu. Mumewe alifika mara moja tu ndani ya hiyo miezi sita akimlipia bili ya
matibabu pekee baada ya kikao cha wanandugu kumlazimisha kufanya hivyo.
Sophia hakuwa na ndugu, mtu pekee aliyekuwa kama
ndugu yake alikuwa ni mumewe aliyemchukua toka katika kituo cha watoto yatima
na kumuajiri kama mfanyakazi wa ndani na baadaye akajikuta
akimpenda na kumuoa.
Jerry na Jenifa waliishi maisha magumu mno, wakitegemea
vibarua vya Jerry hapa na pale na misaada kidogo ya ndugu. Kuna wakati walilala
njaa, kuna wakati mgonjwa wao alitegemea makombo ya wagonjwa wenzake ili
asilale njaa.
Ni bili tu ndio
iliyolipwa na Mzee Agapela, mengine yote yaliyobaki hayakumhusu. Sophia
aliteseka sana na aliumia zaidi
alipowatazama watoto wake waliopeana zamu kumhudumia yeye huku mumewe akila
maisha na mwanamke mwingine. Mwanamke ambaye yeye Sophia alimuita rafiki!
.......NIPE MAONI YAKO MPENZI MSOMAJI.....
.......NIPE MAONI YAKO MPENZI MSOMAJI.....
No comments:
Post a Comment