5
SEHEMU YA TANO
Jua la asubuhi lilichomoza taratibu kwa miale hafifu
huku miale hiyo ikisindikizwa na mvua za
rasharasha zilizoanza alfajiri ya siku hiyo. Upepo mdogo uliokuwa ukivuma kwa
mbwembwe uliiyumbisha miti iliyotapakaa kijijini hapo.
Watu wachache
walionekana wakikimbia huku na kule wakikatisha katika ile mvua ya rasharasha
na wanakijiji wengi walijifungia ndani
kwanza kuipisha ile mvua huku wachache wengine waliojihimu mashambani
wakiendelea na kilimo kama kawaida.
Sindi Nalela alikuwa akiandaa chai jikoni, jiko la kuni
alilokuwa akilitumia lilitoa moshi mwingi uliomfanya afikiche macho na kukohoa kila alipoinama na kupuliza
zile kuni zilizobebana katikati ya mafiga.
‘Kuni mbichi Sindi….kwanini usingewasha zile zilizoko nyuma
ya mlango?’ Mama yake aliyekuwa anaingia pale jikoni alimsemesha Sindi baada ya
kukutana na moshi umetapakaa na kuleta hali ya kukera
‘za nyuma ya mlango ndio hizi mama…’ akajibu akimtazama mama
yake kwa taabu kidogo sababu ya moshi
‘Mmh…ndio zimeloa hivi?’ mama akauliza kwa mshangao
‘Sehemu ya bati hapo nyuma ya mlango inavuja’ Sindi akajibu
akitoka pale jikoni na kupishana na mama yake mlangoni. Akafungua mlango wa nje
na kusimama kizingiti cha mlango akitazama nje kama mtu
anayemtafuta mtu. Mvua ile ya rasha rasha ilimzuia kusogeza kichwa mbele zaidi
hivyo kutoona umbali aliotaka kuona.
Akiwa hapo mama yake naye akamfuata hapo kizingitini,
akichungulia kule alikokuwa anachungulia Sindi.
‘kuna nini uko?’ Mama akauliza
‘Nilimtuma Peter mihogo kule chini naona muda unaenda tu’
akalalamika Sindi
‘Na mvua yote hii unamtuma Peter uko chini…’akaulizwa
‘Mama jamani…mbona huwa namtuma kila mara’ akajitetea
‘Nazungumzia mvua Sindi…. unamjua Peter ni mgonjwa wa kifua
alitakiwa awe ndani muda huu….hebu acha
upumbavu mfuate mtoto uko ulikomtuma’ mama Sindi aliongea kwa hasira na Sindi
alitoka na kujitosa kwenye ile mvua.
Akiwa amenyanyua mabega yake juu akipambana na baridi.
Ni kama vile Manyunyu yale yalikuwa yanamngoja Sindi
alijitose kimiani. Kasi ya manyunyu iliongezeka na kufanya mvua kamili ya
kusimamisha shughuli zote. Sindi alitembea katikati ya mvua ile akipaza sauti
yake na kuliita jina la Peter. Alivuka nyumba kadhaa akimuulizia mdogo wake.
Nyumba ya sita toka pale kwao ndio sehemu aliyomtuma Peter.
‘Aliondoka saa nyingi sana
yaani kabla hata ya hii mvua kuanza….atakuwa kwa rafiki yake Mbwana maana ndio
alikuwa ameongozana naye’ Mama muuza mihogo alimpa Sindi mwanzo wa safari nyingine.
Sindi akashukuru na hapo hapo akisonya na kujenga ndita za kuonyesha kukereka
zaidi na kule kutembea katika mvua akimsaka Peter.
Aliumaliza mtaa wao na
kuingia mtaa wa pili sasa kwa kuvuka barabara, nyumba ya tatu toka barabarani
ilikuwa nyumba ya mwenyekiti na nyumba ya jirani ndio ilikuwa nyumbani kwa huyo
Mbwana rafikiye Peter.
Alipoivuka nyumba ya Mwenyekiti na kuikaribia ile nyumba
aliyokuwa anaelekea alisikia jina lake
likiitwa . Hakugeuka alichapa mwendo
akikimbia mpaka kwenye ile nyumba. Akasimama mlangoni akikausha uso kwa mikono
na kukamua khanga yale iliyokuwa imelowa.
‘Sindi….umemfuata Peter?’ sauti toka ndani ilimuuliza wakati
akikamua ile khanga yake ambayo hata hivyo bado ilikuwa mwilini mwake.
‘eeh… yupo?’ akauliza akikung’uta mikono yake
‘Peteeer… Mbwana hebu muite Peter uko uani….mwambie Sindi
amemfuata’ sauti ile iliagiza na Sindi hakuona sababu ya kuingia ndani mule
ndani akasimama pale pale nje akimngoja
mdogo wake.
‘Mama hajambo lakini?’ sauti toka ndani ikamhoji
‘Hajambo…’ Sindi akajibu akiugeuzia uso mlangoni kule ili
muulizaji alipate jibu kwa urahisi. Akiwa amesimama pale kwa takribani dakika
moja nzima Sindi alionyesha hali zote za kukereka lakini alishindwa kujitosa
mule ndani na kwenda kumvuta Peter ili amtoe nje.
Sura yake iliyokuwa imejaa makunyanzi ya hasira huku misonyo
midogo midogo ya hasira ikimtoka, ilikunjuka ghafla na kuvaa tabasamu. Jerry
Agapela alikuwa akija sehemu ile aliyokuwa amesimama. Alipomkaribia Sindi
alijikuta akitabasamu zaidi kiasi cha kuonyesha meno yake yaliyokuwa katika
safu nzuri ya kuvutia, mwanya mdogo uliochongeka kiustadi ukizidisha thamani ya
lile tabasamu pana la kuvutia.
‘umelowa sana …’
Jerry alimsemesha wakati alipomfikia na kusimama mbele yake akiwa na mwamvuli
mkubwa alioushikilia mkononi.
‘Si Peter huyo….nxa!’ akalalamika na kumfanya Jerry acheke
‘Mtoto ni mtoto tu….’ akamtetea
‘Peter naye mtoto aargh!...’ akabetua midomo yake na Jerry
akacheka chini chini.
Wakatazamana na ukimya ukapita kati yao ,
ukimya wa ghafla tu kila mtu akikosa cha kuongea. Sindi akaamua kujibaraguza
kwa kumuita Peter kwa sauti kubwa na bahati ikawa yake. Peter aliitika akidai
anakuja.
‘Sindi…’ Jerry aliita kwa sauti ya chini. Sauti ambayo
kwa mwanamke yoyote yule lazima mwili
ungemsisimka kidogo. Sindi akajibaraguza zaidi kwa kuamua kuushika mlango
uliokuwa mbele yake na kuufungua, akichungulia ndani na kumhimiza Peter afanye
haraka.
Sindi aliutanua mlango zaidi na Peter akatoka, akipokelewa na
konzi matata toka kwa dada yake.
‘Usimpige jamani…’Jerry alimtetea Peter ambaye alisharuka na
kusimama kule alikokuwa amesimama Jerry. Ukatokea mvutano kati ya Peter na
Sindi huku Jerry akiwa katikati. Mvutano huo ukaisha kwa Jerry kumuombea Peter
msamaha.
Kwa vile mvua ilikuwa inaendelea kunyesha, Jerry alijitolea
kuwasindikiza kwa kutumia mwamvuli aliokuwa nao. Wakabanana katika mwamvuli ule
wakikatiza kona kadhaa hadi kufika nyumbani kwa akina Sindi. Wakashukuru na Peter akawa wa kwanza
kukimbilia ndani na mfuko wake wa mihogo wakati Sindi akiagana na Jerry.
‘utaenda kufundisha kule chini…’ Jerry akauliza taratibu
wakati akiagana na Sindi ambaye aliitikia kwa kichwa na kutoka katika ule
mwamvuli. Akampungia Jerry mkono na kuingia ndani. Jerry akageuza njia na
kurudi alikotoka. Uso ukiwa na tabasamu la matumaini aliyoanza kujenga moyoni
mwake.
‘teeena?’ mama yake akamdaka kule ndani
‘Tena nini?’ Sindi akauliza kwa mshangao
‘huyo kijana mnavyozungushana hapa kijijini….. hivi mwanangu
huoni picha mbaya unayojengewa?’ Mama yake akalalamika
‘Jamani….hao wajenga picha sasa wajenge tu hata ghorofa la
tuhuma … katusindikiza hapa sababu ya mvua…watu mnawaza mengine kabisa….
nimechoka na maneno ya watu sasa…waseme tu’ Sindi akajibu na kupilizia chumbani
kwake
Wakati alipoufunga mlango wa chumba chake, Peter aliyekuwa
amesimama pembeni ya mama yake aliutazama ule mlango wa chumba cha Sindi kwa
tahadhari kisha akamvutia chini mama yake ili usawa wa kichwa cha mama yake
ulingane na wake.
‘Kamtomasa tomasa…’ akasema haraka haraka kwa sauti ya chini
‘Nini?...nani katomasa’ mama yake akauliza kwa sauti
iliyomfanya ajishtukie na kupunguza sauti, akimtazama mtoto wake kwa mshangao
si tu kwa lile neno alilotamka Peter bali ni ile picha iliyomjia ghafla
kichwani.
‘Jerry kamtomasa Sindi huku….’ Peter akaonyesha ubavu wake
‘Kamtomasaje?’ safari hii mama aliuliza kwa sauti ya chini
zaidi, macho yakiwa yamemtoka vibaya mno.
‘wakati tunatembea wametomasana’ Peter akajibu, uso
ukimaanisha kile alichokuwa anakisema. Mama Sindi akanyanyuka na kusimama wima,
mshangao, taharuki na hali ya kutoamini vikimtembelea kwa wakati mmoja na muda
huo huo mumewe akifungua mlango wa kuingilia ndani huku akiwa ametanguliza
majembe. Mama Sindi akajitoa katika ule mshangao na kwenda kumpokea mumewe.
Akili yake haikuwa pale tena, alihisi hatari ambayo hakutaka hata kuiwazia
namna ambavyo ingeleta majanga pale kwake ila kwa wakati ule, damu ilimchemka!
88888888888888888888
Gari dogo aina Suzuki Vitara ilitembea kwa mwendo wa taratibu
upande wa pili wa dunia, mjini huku, jua lililokimbia kijijini kule lilihamia
huku mjini. Gari lile liliacha njia ya lami na kuchukua njia ya vumbi
iliyoishia katika nyumba moja iliyoonekana kutomaliziwa kujengwa kitambo.
Mwanamke aliyevalia maridadi aliteremka kwa kasi na akiwa amejifunika ushungi
na kuzama katika ile nyumba akionekana mwenye wasiwasi kupitiliza. alitembea
kwa shida kidogo kutokana na sakafu ya ile nyumba kuwa yenye mawe na mchanga.
Viatu vyake virefu vilivyombeba kiustadi havikuhimili mabonde mabonde
yaliyokuwa katika ile sakafu. Mara kadhaa alilazimika kujishikilia ukutani
wakati akikatiza chumba hadi chumba mpaka alipotekezea katika sehemu ya nyuma
ya nyumba iliyokuwa wazi.
Alitulia pale akiangaza angaza huku na kule, uso wake uliojaa
mashaka ukiongeza ndita kadhaa. Aliporidhika na hali ya usalama alioutaka.
Mwanamke yule alipiga mbija moja kali na kutulia, akingoja jibu la ile ishara
iliyotoa. Wakati huo akitazama pori
dogo lilikokuwa mbele yake. Alitulia kimashaka mashaka mpaka pale vijana wanne
wenye miili iliyoshiba walipojitokeza na kumfuata pale alipokuwa amesimama.
‘imekuwaje?.....nilisema yasifanyike makosa ya aina
yoyote….na hiki ni nini….waliokota kiatu kiatu na sasa wallet yake imeokotwa…hamuoni
itawapa njia ya kumpata?’ alifoka kwa ghadhabu akiwatazama wale wanaume
‘nimetoka milioni 5 za kumteka Jerry na kumuua kimya kimya…..sio
kumteka na kumuachia….hebu ona mipango yote imeharibika…..ujinga gani huu?’
aliendelea kufoka
‘Lakini dada tuna
hakika Jerry hatakuwa mzima mpaka dakika hii..’ kiongozi wao alijitetea
‘Una uhakika gani?....hii sio sandakalawe Jimmy….sio mchezo
wa pata potea….trace ndogo tu inaweza kugharimu maisha yangu….’ yule mwanamke
alihamanika akiwa tazama wale vijana kwa wahaka
‘Alikokimbilia ni porini na jeraha lile la kisu si la
kumuweka duniani mpaka sasa….wataokota maiti sio mtu aliye hai… tuamini
sisi…ndio tuliopambana naye…inshu ni kungoja iokotwe maiti vinginevyo jua maiti
inaozea porini uko….ila la Jerry kuwa mzima sahau kabisa’ Yule kiongozi
alijitetea na wenzake wakiitikia kwa kichwa.
‘Vipi kuhusu usiri wa hiki kitu?’ yule mwanamke alitaka
uhakika
‘Hii sio kazi yetu ya kwanza Mama….weka imani na sisi na
ukisikia popote tuhuma zozote nifuate’ alihakikishiwa na akabaki kuwatazama
wale vijana kana kwamba moyo wake ulisita kuwaamini.
Fiona Agapela, mke wa Mzee Agapela alifungua pochi yake
aliyokuwa ameibana kwapani na kutoa burungutu la fedha ambazo hakuzihesabu.
Aliwakabidhi wale vijana na wao pasipo
kuhesabu walizitia kibindoni. Waliaminiana!
Fiona alitoka eneo lile na kurudi garini, aliingia ndani ya
gari na kutulia kwa sekunde kadhaa pasipo kuendesha wala kuugusa usukukani.
Alitulia tu akiutazama usukani pasipo kuutambua akilini. Alikuwa na jakamoyo
lililomtokota kwa wakati ule. Moyo wake
uligoma kuamini kuwa hatua ya mwanzo ya mpango wake ulikuwa umefanikiwa.
Aliitaka maiti ya Jerry, alitaka kumzika na kulishuhudia
kaburi lake ndipo
moyo wake ungetulia kwa amani. Akashusha pumzi taratibu, mkono wa kushoto
ukishika usukani na ule wa kulia ukitekenya ufunguo, akaliwasha gari, akigeuka
nyuma kuangalia akianza kulirudisha nyuma taratibu.
Alitabasamu alipoliingiza gari lake
kwenye barabara ya lami.
888888888888888888888888
Nyanza alijitazama mara mbilimbili wakati alipokuwa
akijiandaa kutoka nyumbani kwao. Jioni hii alipanga kukutana na Sindi kwenye
makutano yao . Pesa kidogo aliyokuwa
nayo alimnunulia Sindi doti ya khanga aliyokuwa ameihifadhi kwenye mfuko mdogo
mweusi wa nailoni.
Ijapokuwa shati lake
lilikuwa limejikunja kiasi cha
kuchekesha, lilimkaa vyema mwilini, na kulandana na suruali ya kitambaa
iliyokuwa imepauka kiasi kuishia juu kidogo ya viatu chakavu aina ya mokasi
alivyokuwa amevaa.
Nyanza alitoka pale kwao mpaka eneo alilotarajia kumkuta
Sindi. Akatulia hapo akiifurahia mandhari tulivu iliyokuwa mbele yake huku
akimngoja Sindi wake.
Pasipo kukumbuka miadi yake na Nyanza, Sindi alimalizia
darasa lake na
kusimama nje ya lile jengo alilolitumia kama darasa
akizungumza na Jerry Agapela.
‘Kwani ukimpenda mtu lazima uwe naye….’ Sindi alibisha akiwa
amekumbatia vitabu vyake kifuani
‘Sio lazima lakini….lazima utapigania kumpata tu’ Jerry
alijitetea
‘Nimeshakwambia nina mtu’ Sindi alikaza uzi
‘Najua… na mimi sio mbuzi ni mtu….’ Jerry alipagua hoja ya
Sindi akimsogelea zaidi
‘Sitaki…siwezi kuwa na watu wawili kwa wakati mmoja….’ Sindi
alirudi nyuma kidogo na kuanza kupiga hatua za kuondoka eneo lile na Jerry
akamkimbilia na kuanza kutembea naye sambamba
‘Sindi…’ akamuita, akimuwahi na kumzibia njia
‘Nakupenda…’ akatamka kwa sauti ya chini lakini iliyomfikia
Sindi mpaka mtimani. alikuwa na namna ya kulitamka jina la Sindi kimahaba
zaidi.
‘Sitaki Jerry’ Sindi akampita Jerry tena akikaza mwendo na
Jerry alijua Sindi alitaka kumuacha njia panda. Ile ishara ya kumtekenya
ubavuni wakati alipokuwa amewafunika na mwamvuli ilipokelewa na Sindi kwa hali
tofauti. Hakuutoa mkono wake pale alipompapasa lakini pia hakumuonyesha dalili
za kuikubali hali ilea ma tu kumkubali kama alivyokubali
kupapaswa.
Walibishana njiani, wakijibizana na Jerry akipangua hoja za
Sindi kila alipomkatalia alilotaka
‘Sitaki sawa?.... nnajiheshimu Jerry…achana na mimi’ Sindi
alikuwa mkali sasa, akimjibu kwa sauti kali na yenye mamlaka
‘Najua u bikira’ Jerry akatamka kwa kujiamini na kumfanya
Sindi asimame ghafla na kumgeukia Jerry
‘Nini?...umesemaje?’ Sindi akauliza kwa ukali
‘Najua wewe ni bikira’ Jerry akarudia tena na kabla
hajatuliza kichwa chake akashtukia akipokea kibao kikali shavuni, kilimfanya
aone nyota kadhaa za rangi tofauti
‘Usirudie kuniambia upuuzi kama huu….’
Sindi alionya na kuondoka kwa kasi zaidi. kofi la mpenzi haliumi!
Jerry alimfuata Sindi kwa kasi zaidi na kumzuia kwa mbele,
akijitoa mhanga na kuitanua mikono yakekumgusa Sondi ambaye aliipangua kwa
kasi.
‘Usinishike Jerry’ alimuonya
‘Nakutaka Sindi…’ Jerry alibembeleza na hapo hapo akitumia
nguvu kidogo kumsogelea Sindi ambaye naye alikuwa akirudi nyuma taratibu. Macho
yake hayakuweza kumtazama Jerry kwa ukali ule ule. Ni kama vile maneno ya Jerry
yalimpunguzia nguvu.
‘Nakupenda sindi…. nakutaka…’ alirai kimahaba akiwa
ameshamfikia Sindi na kutaka kumgusa tena. Sindi aliyekuwa amegota kwenye mti
uliokuwa nyuma yake alihema bila mpango midomo ikimwemweseka pasipo kukemea.
kufumba na kufumbua, Jerry alihisi akitupwa kando kwa nguvu.
Wakati akili yake ikikaa sawasawa na kutaka kutambua kilichomsukumia mbali
vile, alishtukia ngumi ya shavu ikimpata sawia na hapo hapo akitandikwa ngumi
ya mbavu iliyomfanya apepesuke na kudondoka tena kama
gunia la mpunga.
Sindi alipiga yowe la uchungu, akimtaka Nyanza kuaca
kupigana. Haikusaidia Nyanza alimtandika Jerry ngumi za kutosha kabla ya
kumuachia na kumgeukia SIndi ambaye alirudi nyuma kwa kasi na asitazame aendako.
Nyanza akampita taratibu, akiokota ule mzigo wake wa Khanga
na kutokomea, akimuacha Sindi amesimama katikati asijue akamsaidie Jerry au
amkimbilie Nyanza.
……. TUKUTANE TENA HAPA HAPA…….
No comments:
Post a Comment