Tuesday, May 24, 2011

SIRI YANGU 9....Na Laura Pettie

...Aliongea kwa uchungu mno huku mikono ikiwa imelishikilia tumbo lake mithili ya mama mjamzito aliyeshikwa na uchungu wa uzazi. Nilimtazama mama bila kuelewa nimwambie nini cha kumtuliza.

Nilijua alikuwa ananiwazia sivyo! Kelvin hakuwa katika fikra zangu kabisa na wala hakuwa chanzo cha huzuni yangu. Ilikuwa ni siri yangu kuwa kilichotokea kati yangu na Jonas ndicho hasa kilichokuwa kinanimaliza. Sikujua nianzie wapi kuuelezea ulimwengu masahibu haya yaliyonikumba pasi ulimwengu huo kunihukumu vikali!

“…wenzio wanatelekezwa na watoto wewe Kelvin hajakuachia chochote cha kumkumbuka sasa mawazo ya nini, bado u msichana mrembo na najua mungu atakupatia mume bora wa kukufuta machozi yako, cha msingi tulia, jiheshimu na tafakari upya maisha yako” alimeza funda la mate na sasa akaketi pale kochini nilipokuwa nimeketi na kunikumbatia.

“ hupaswi kulia hivi mwanangu!” alinikumbatia zaidi
“ lakini mama…”
“ shh.shhh! najua umeumia moyo mno lakini anza kubadili maisha yako sasa, anza upya Karen, pigania maisha ya furaha karen!” aliniachia na kunitazama usoni hali akionesha wazi kutopendezwa na hali yangu, akaelekea jikoni. Wakati nikiwa nimeketi pale sofani nikitafakari, mlango uligongwa na haraka niliinuka na kwenda kuufungua.

Alikuwa Kelvin! Hakungoja kukaribishwa alinipita mlangoni na kujitoma ndani kwa haraka. Nikaufunga mlango na kugeuka kumtazama. Akili ilikuwa imekimbilia kusikojulikana na kuyaacha macho yangu yakimtumbulia Kelvin bila hata salamu.
“…Karen! Sasa imetosha na unahitaji msaada wangu kwa vyovyote iwe ni kama daktari ama kama Kelvin!” aliketi na kuendela kuongea kwa msisitizo

“hali yako inanitisha Karen mpaka leo ukashindwa kuendelea na misa kanisani Karen, umeshindwa kupiga kinada na kuimba imekuwaje!?” alinionyesha wazi mshangao wake. Machozi yalijaa ndani ya mboni za macho yangu na kilio cha kwikwi kilinikaba kisawasawa.

Kwa haraka alinyanyuka na kuja kunikumbatia pale nilipokuwa nimesimama kama mlingoti wa bendera. Sikumpa pingamizi lolote na hakika alinipa faraja kuwa mikononi mwake kwa dakika kadhaa, harufu ya jasho lake ilinifikia barabara na kuichanganya zaidi akili yangu.


Alinisogeza mbali kidogo na kifua chake kisha nyuso zetu zikapata nafasi ya kutazamana kwa ukaribu zaidi. Macho yake yenye mvuto yalimetameta hali midomo yake ikimwemweseka na kunikumbusha wakati ule alipokuwa sehemu ya maisha yangu.

Mikono yake iliyojaa upole ilipita usoni pangu na kufuta michirizi ya machozi iliyokuwa ikizidi kuweka vijito katika paji la uso wangu!. Nilitamani aendelea kuyafuta machozi hayo milele na milele.

“hustahili huzuni Karen!” alininong’oneza na kunirudisha tena kifuani pake.ilikuwa ni kama mtoto aliyempoteza mama yake kwa miaka kadhaa na sasa mama huyo alikuwa mbele yake na tena mikononi mwake. Tulikumbatiana hivyo kwa muda huku kila mmoja akisikilizia mapigo ya moyo ya mwenzake. Kuwa mikononi mwa Kelvin lilikuwa jambo la faraja mno kwangu.

Hisia zangu kwa Kelvin zilikuwa palepale japo mara kadhaa nilijaribu kuzikana hisia hizi ambazo nalazimika kukiri sijui kma zitatoweka.
Mama aliporejea pale ukumbini alitunduwaa kwa sekunde kadhaa kabla ya kujikohoza ili kutujulisha kuwa alikuwa pale. Kelvin alinitoa maungoni mwake na kugeuka kumtazama mama. Alijiweka sawa na kumsalimia mama ambaye alikuwa akimtazama katika namna isiyoeleweka.

“ umeamua kuja kummaliza kabisa!” mama alimtupia swali
“ hapana mama! Nadhani Karen anahitaji msaada wangu ili arejee katika hali yake”
“ sikiliza Kelvin…” mama aliketi sofani na kumtazama Kelvin kwa macho makali zaidi mithili ya mwanamke aliyetelekezwa kwa miaka mingi na mumewe na sasa mwanaume huyo alikuwa mbele yake akimtaka warudiane.

kisha akaendelea kusema “ kwa vyovyote vile unapaswa kukaa mbali na huyu binti tangu sasa! Na hilo si ombi bali ni amri mwanangu, tangu lini ungo ukaomba msaada wa sinia kupepeta mchele?”
“ mama yaliyopita si ndwele…” Kelvin alitaka kujitetea
“ na ndio tunaganga yajayo hivyo!” mama alidakia kwa dharau
“ nilikosa lakini sitaki Karen ajutie kuwa na mimi maishani mama” alijaribu kumuelewesha
“ ajutie! Karen ajutie mara ngapi? Kelvin nakuheshimu kijana! Na sitaki kukuvunjia heshima yako. Mlango ule pale!” alimuonyesha kwa kidole chake cha shahada! Huku naye akinyanyuka na kwenda kuufungua kabisa.
“ mama… najua nina makosa…mama nipe tu nafasi mama…” Kelvin alishindwa hata kuzipangilia sentensi zake katika mpangilio unaoeleweka lakini ni dhahiri akili yake iliduwazwa na maneno yale ya mama.

Nilitaka kumtetea Kelvin lakini mama aliniwahi na kunitazama kwa jicho kali mno! Kelvin aligeuka na kunitazama. Alishusha pumzi ndefu mara kadhaa na machozi yalionekana kwa mbali yakizinyemelea mboni za macho yake. Hakuamini!

“ Kelvin! Hii iwe safari yako ya mwisho hapa! Iwe kwa kheri au shari Kaa mbali na Karen tafadhali kwa namna yoyote ile” mama alizidi kuupigilia msumari moyo wa Kelvin. Hakumudu hata kupiga hatua moja. Kelvin alifumba macho yake taratibu na kuyaruhusu machozi yatiririke mbele ya mama.

Hata alipoyafumbua alibakia kuyapepesa na kuyafanya yabubujike mithili ya kijito kitokacho mlimani. Midomo yake iliwayawaya isijue hata itamke nini cha kuibadili hali ile. Alishidwa kupigana na hisia zake kabisa.
Nilihisi uchungu mkubwa moyoni mwangu. Sikutaka kumshuhudia Kelvin akizidi kulia mbele zangu. Nilikimbilia chumbani huku nami nikiomboleza. Kelvin aliondoka zake na mama alinifuata chumbani. Aliponikuta nalia aliguna kwa sauti na kuniambia
“ anza upya maisha Karen! Mapenzi ni sehemu tu ya maisha na wala si maisha! Hivyo Kelvin si maisha yako binti!”
“ lakini si Kelvin mama! …”

“ what! Si Kelvin anayekupa wazimu huu?” mama aliniuliza kwa mshangao. Nikazinduka na kutambua kosa! Nilikuwa nimeropoka bila kufikiria. Nilijituliza na kumtazama mama ambaye sasa alinifuata kwa kasi pale kitandani na kuketi!
“ Karen! Ni nini kinakusumbua mpenzi?” aliniuliza kwa upole kana kwamba ndio kwanza alikuwa ananiona katika hali ile ya masononeko.

“ni hisia tu za kumkosa Kelvin lakini si kosa la Kelvin!” niliirekebisha kauli yangu na mama akanisogelea na kunikumbatia. sikumuona tena Kelvin mpaka siku niliyofikishwa hospitali baada ya kuzirai.

Hali yangu haikuwa ya kuridhisha. Ujauzito ulinisumbua sana na hasa kwa vile ulikuwa wa kuficha. Sikujua ningeficha mpaka lini lakini pia sikuwa tayari kuitoa kwa kuhofia kufa na kutenda dhambi ya uuaji wa kiumbe kisicho na hatia. Iloma alisimama nami bega kwa bega huku mara kadhaa akija nyumbani kunipa kampani. Hata yeye hakujua kuwa nilikuwa na ujamzito wa nani.

“ lakini Karen mimba hii ni ya nani?”
“ utamjua tu, kwa sasa yuko nje kibiashara!” nilimjibu kimkato na alikubaliana nami japo kwa shingo upande kwa vile tangu niachane na Kelvin hakuwahi kuniona karibu na mwanaume yeyote.

Siku hiyo nilikuwa ofisini nikimalizia kufunga hesabu za kampuni. Wakati nikiendelea na kazi zangu mlango wa ofisini ulifunguliwa na Jonas akaingia na kuurudishia kisha akasimama mlangoni pale. Kwa vile nilikuwa na kazi nyingi sikuyaondosha macho yangu kwenye kompyuta iliyokuwa mbele yangu zaidi ya kumpa karibu ya mbali mgeni huyo. Baada ya kukamilisha hesabu zangu niliinua uso wangu na kumtazama jonas

“ jonas! Karibu” nilijitutumua kumkaribisha kiti nikichelea kuvuruga taratibu za kazi kwa kuingiza mambo binafsi. Hakujisumbua hata kukitazama kiti zaidi ya kuendelea kunitazama kwa pozi akiwa bado amejisimika pale mlangoni.
“ Karen!” aliniita kwa upole nami sikuitika si kwa kupenda bali kwa kisirani kilichokuwa moyoni mwangu.
“ tunahitaji kumlea mtoto huyo ndani ya ndoa! Tunahitaji kuwa pamoja katika kipindi hiki kigumu”
“ sihitaji msaada wako Jonas!”
“ I’m serious Karen! Nataka kukuoa”
“ what!” nilipayuka kwa sauti bila kutarajia mkono wangu wa kuume ukikimbilia kinywani na kuziba pumzi za mshangao huo wa ghafla..

“ nataka kumpa iloma talaka, sitajali ulimwengu utanihukumu vipi lakini nimetambua nakupenda sana na wewe ndio chaguo langu halisi. Najutia kuchelewa kulitambua hilo lakini sina budi kuwa mkweli mbele za mungu na hata mbele za ulimwengu. Karen, you mean the world to me”

“ sikiliza Jonas! Sijapata kuona mwanaume mpumbavu kama wewe!”
“ Asante mama!” alijibu hali akitabasamu
“ hata kama nitakufa leo hii nakuhakikishia hutanioa! Na tangu sasa…” nilimpa msimamo
“ karen! Kwanini unapigana na hisia zako…unanipenda sawa! Unanipenda Karen lakini hutaki kuwa wazi, just look into my eyes Karen! You love me…you love me Karen!” alinifuata pale mezani. Nikanyuka na kuzunguka upande wa pili nikiwa na nia ya kuuelekea mlango na kumtaka atoke nje lakini hata hivyo aliniwahi na kunivutia kwake kwa nguvu za ajabu.

Mikono yake ilitutumka na kujaa mishipa ya damu, alinibana vema kifuani pake na kuziacha nyuzo zetu zikitazamana. Nilikuwa nahema mithili ya mpiga mbizi ndani ya tope.

Aliiunganisha midomo yetu na kunipa busu moja lililounyong’onyeza mwili wangu! Aliponiachia Jonas aliachia tabasamu, tabasamu lile lile lililokuwa na uwezo na kuiteka akili yangu kwa sekunde tu!

“ fungua kitabu cha moyo wako na usome nini mungu amekuandikia karen! Unajikana mwenyewe kwa kuzikana hisia zako…Karen tunapendana ila tunaogopana kuwa wazi Karen, haitakuwa na maana tukiendelea kuteseka na hisia hizi moyoni!” alizungumza kwa upole nami nikajikuta nazishusha pumzi taratibu na kumtazama Jonas usoni nilikiri kimoyomoyo lakini hali uso ukionyesha utulivu!

“ Karen! Unanipenda?” aliniuliza kwa sauti ndogo ya kubembelezea jibu
“ labda jonas!” nilijikuta nimetamka hilo bila kutarajia. Kwa mara ya kwanza tangu nimfahamu jonas nilimbusu kimahaba kwa hiari yangu, Nilimkumbatia kwa mapenzi yote bila kushurutishwa na kumruhusu anitawale alivyotaka yeye na nilihisi raha ya ajabu kuwa na jonas karibu.

Raha ambayo ilizidi hata kuwa na Kelvin usiku na mchana. Tulipoachiana alinitazama kwa muda kisha akatabasamu na kuniambia “ nimebarikiwa kuwa nawe na nitakuoa tu!” akanikumbatia tena na kunibusu. Aliponiachia nilihisi upweke wa ghafla. Nilitamani aendelee kuwa pale mara zote.

Aliuelekea mlango akaufungua na kusimama kizingitini hali akinitazama katika namna isiyotabirika kabisa. Alirudi ghafla ndani kuja kunikumbatia tena safari hii akilia machozi.
“ Jonas unalia nini?”

“ siamini Karen! Siamini kama umekubali kuwa mke wangu…Karen nakupenda sana mama sana tu” nilitamani kumwambia hata mimi nilikuwa nampenda lakini nilihofu kutamka hilo haraka. Nilitaka kujifikiria mara mbili na sikutaka kuonekana rahisi mno mbele ya Jonas. Aliniachia na sasa akatoka na kuniacha ofisini peke yangu.

Nilijisikia amani na furaha nikisahau kuwa jonas alikuwa mume wa mtu tena mume wa rafiki yangu mpenzi iloma. Nusu saa baadae Jonas alinipigia simu akiwa ofisini kwake.
“ nitakuwa mwanaume mtiifu kwako naahidi…karen unanipenda?” alirudia tena swali lake lakini sikujibu kitu zaidi ya kutabasamu na kuangua cheko simuni
“ nitakujibu leo usiku” nilimwambia kwa upole
“ saa ngapi maana sidhani kama nitalala vema bila kuisikia kauli yako juu yangu”
“ unipigie saa moja usiku na nitakwambia kila kitu”
“ Karen! Wewe ndio ubavu wangu halisi na si Iloma”
“haya kazi njema mpenzi”

“ my god! Unaniitaje! Hebu rudia Karen can’t believe it baby!” aliongea kwa furaha
“ kazi njema mpenzi” nilirudia kusema na wote tulicheka simuni. Baada ya hapo ilikuwa ni ubishani wa nani aanze kukata simu. Ilinibidi nisalimu amri na kukata simu ili niendelee na kazi. Nilipouweka mkonga wa simu chini Iloma alifungua mlango na kuingia ofisini kwangu.

Alishuhudia nikiangua kicheko kirefu cha bashasha.
“ mbona uso umeng’aa na tabasamu vipi kuna mtu kaikuna roho yako nini?”

“ sana tu!” nilimjibu iloma kisha taratibu nikanyanyuka na mafaili yangu na kuelekea ofisini kwa bosi wetu Mr.Tummy nikimuacha iloma ananitazama kwa mshangao wa waziwazi.laiti angejua….

ITAENDELEA....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger