10
SEHEMU YA 10
Asubuhi ya Siku iliyofuata Pamela Okello aliondoka na gari lake
alilokuwa amekodi mahali uko
Shinyanga mjini, akiwa amemuachia Jerry Agapela pesa za kutosha pamoja na simu
ya mawasiliano. Wakati anaondoka pale kijijini alimkumbuka Nyanzambe
Mugilagila, kijana aliyeonana naye jana yake na kumnasua toka katika zahma la
kukwama matopeni.
Moyo wake ulitaka kumuona tena kijana huyu, alitaka tena
kuisikia ile lafudhi nzito ya kiume iliyomchangamsha jana yake, alitaka tena kukiona
kiumbe hiki na nafsi yake haikumpa hata nafasi ya kuipuuzia hamu yake ya kumtia
machoni. Akaegesha gari palepale alipoegesha jana yake na kuteremka.
Hatua mbili tatu zilimfikisha katika kibanda kidogo
kilichokuwa kikitumika kama sehemu ya kutengenezea
baiskeli. Waliokuwepo eneo hilo
hawakuingia hata nusu ya hadhi ya mtu aliyetaka kumuuliza. Akatulia kidogo akiwatazama
na wale aliowakuta wakimshangaa.
‘Namtafuta Nyanzambe’ akatoa shida yake asijali uungwana wa
kujuliana hali kwanza na hakuna aliyemjibu. Lafudhi yake laini iliyorembwa kwa
sauti maridadi iliwafanya watazamane kwanza na kusemezana kilugha. Naye Pamela
akawatazama kwa awamu akikunja uso
kidogo kuonyesha kutowaelewa.
Wakasemezana na kucheka kisha wakamgeukia Pamela, wakizidi
kumshangaa sio tu kwa yale mavazi yake bali pia kwa ule umaridadi wake ambao
haukulingana hata theluthi na huyo aliyemuhitaji.
Pamela akazungusha macho katika namna ya kuonyesha kuchoshwa
na zile mbwembwe zao na mishangao yao
wale mafundi baiskeli. Akasonya na kugeuka akitaka kuanza kuondoka lakini uko
alikogeukia ndiko huyo aliyekuwa anamtafuta alikuwa anatokea, akiwa na baiskeli
yake akiikokota taratibu huku ikiwa na magunia makubwa mawili ya mkaa.
Pamela akatabasamu na kusimama akingoja Nyanza amfikie pale
alipokuwa
‘Pole!’ likamtoka hili neno pengine bila kutarajia, macho
yakikisawiri kifua kipana cha Nyanza kwa matamanio. Nyanza akatabasamu akishika
baiskeli ile kwa mkono mmoja na mwingine akinyanyua baiskeli kwa nyuma na
kuiweke breki yake ya kusimamia.
‘Unaondoka?’ akamuuliza Pamela akitanua mikono yake hewani
‘Yeah….nilitaka kukuaga na kukushukuru tena na tena’ Pamela
akaeleza nia yake na Nyanza akatabasamu tu kwani moyoni hakuona umuhimu wa
msichana kama yule kuhangaika kumtafuta ili kumshukuru
tu.
‘Unaishi wapi?’ Pamela akauliza tena lakini Nyanza
akainamisha kichwa chini akitoa tabasamu lililomfikishia ujumbe Pamela kuwa
hakutaka kumfikisha anapoishi.
‘Okay…usijali’ Pamela akaligundua hilo
‘Safari njema…’ Nyanza akamuaga pasipo kuondoka wala
kuonyesha dalili za kuondoka. Ni kama alitaka kuhitimisha mazungumzo na
mwanadada yule kwa wakati ule.
Pamela Okello akaganda kama sanamu
akimtazama Nyanza ambaye alijikuta akitaka kucheka pia kutokana na wale mafundi
baiskeli kusimama wima wakiwasikiliza kana kwamba waliambiwa wakariri kila watakalosikia.
Tendo lile la kutaka kucheka hali akitazama walionyuma ya
Pamela, lilimfanya Pamela ageuke na kutanza hicho alichotazama Nyanza. Wale
mafundi wakajibaraguza kushika hiki na kile na hilo
likamfanya Nyanza acheke kwa sauti kidogo na angalau kumletea Pamela tabasamu
la kulazimisha.
‘ Karibu tena dada…’ Nyanza akaaga tena akiikwatua breki ya
baiskeli na kuiweka tayari kwa kuondoka.
Pamela Okello akaitikia kwa kichwa, huku moyo wake
ukimshinikiza amwambie Nyanza wakaketi katika gari na kuzungumza, hakuweza
kuyasema hayo, hakuweza hata kidogo, ugeni ulimsumbua na mazingira hayakumruhusu.
Akashusha pumzi na kuondoka eneo lile kurejea kati ka gari lake. Akalondoa gari
kwa kasi.
Nyanza akakipita kile kibanda akitaniwa na wale mafundi
baiskeli, akapiga kona na kufika kwao. Kibanda kile kilikuwa mbele ya nyumba yao .
Akaingia katika uwanja wa nyumba na kumkuta mama yake akivaa raba zake kwa
ajili ya kwenda kazini.
‘leo umechelewa sana
mama’ Nyanza akamsemesha mama yake huku akishusha yale magunia toka kwenye
baiskeli
‘Nimekuona na mwanamke hapo nje’ mama yake akiwa na uso wa
shari akamvaa mwanaye. Nyanza akashindwa kulitua lile gunia alilokuwa amebeba
na akashindwa kulirejesha alikolitoa, akabaki ameduwaa nalo mikononi hali likimuelemea
‘Mama unanifuatilia!?’ Nyanza akamuuliza mama yake uso
ukijikunja kutokana na ule uzito wa gunia la mkaa changanya na hali ya
kumshangaa mama yake ambaye sasa alisimama wima mbele yake.
‘hebu tua hilo
gunia kwanza khe!...’ mama yake akajibu na kumfanya Nyanza auweke chini ule
mzigo na kusimama wima akimtazama mama yake kiudadisi
‘nina mwanamke mmoja tu maishani mwangu’ Nyanza akajitetea
‘Kwani nimesema unao kumi….na huyo mwanamke wa kumtambia hivi
yuko wapi?....Sindi? Sindi huyuhuyu mtoto wa Nalela ekhee…..na kama
ndiye mwanamke uliyeokota uko unamleta tumlipie mahari…. basi mwaka huu wangu!’
Mama aligeuka na kweda kuufunga mlango wa nyumba kisha akageuka na kuanza
kuondoka, kijana wake akiwa bado anamtazama tu na asimmalize.
‘Hivi ni kitu gani Sindi amekukosea mama….kwanini unamchukia
hivi?’ Nyanza alimfuata mama yake haraka kabla hajavuka kizingiti cha geti la
bati.
‘Mama siku zote humtakia mema mwanawe…..Sindi sio wa daraja
lako mwanangu’ Mama yake akamuasa
‘Kivipi mama?....wote tumeshindwa kufika mbali kielimu sababu
ya umasikini, wote tumetoka familia masikini na isitoshe tuko imani moja…na
sasa kipi cha kunitofautisha na Sindi’ Nyanza aliongea kwa jazba kidogo,
alishaanza kuchoshwa na risala za kumtaka aachane na Sindi.
Mama yake akamtazama usoni kwa muda, asipepese hata macho.
‘Mungu anipe uhai…siku moja utarudi hapa hapa na utaniangukia
miguuni na utakiri kuwa huyu binti sio daraja lako’ Mama yake amamweleza
taratibu lakini kwa sauti ya ukali
‘Kwanini?’ aliuliza akisisitiza na sauti ikipaa hewani zaidi
‘Sindi Nalela!...Sindi!....umeshapigana mara ngapi sababu ya
Sindi?....unaishi maisha ya mashaka, wasiwasi na dhoruba zote sababu ya
Sindi!....bado tu huoni kama ni mtu wa kukimbiliwa na mamia ya
watu?....hujagundua tu atakupa ugonjwa wa moyo?....’ Mama yake aliongea kwa
uchungu sasa, akitaka kijana wake aone ugumu wa kummiliki Sindi Nalela.
‘Mama….sijashindwa kummiliki Sindi….na hakuna mwanamke chini
ya jua nitakayempa moyo wangu zaidi ya Sindi….’ akajiapiza mwenyewe na
asikumbuke Mapenzi ni kama kamari, ukipata wewe anakosa
yule.
Mama akasikitika sana ,
akatoka na kuishia zake akimuacha kijana wake amesimama pale kama
mjinga fulani. Sauti ya mama yake ikirindima kwa mara ya pili kichwani na
mwangwi wake uligota kwenye akili yake na kumkumbusha Jerry Agapela na wanaume
wengine aliowahi kukunjana nao mashati sababu ya Sindi. Akachoka!
8888888888888888888888888
Sindi Nalela alikuwa jikoni akikoroga uji uliokuwa unakaribia
kuanza kuchemka. Alikuwa akizungusha mwiko kwenye sufuria pasipo hata kuangalia
ni nini alichokuwa anakikoroga. Macho yake yalikuwa yakipepesuka huku meno yake
ya juu yakibarizi mdomo wake wa chini. Ni dhahiri akili yake haikuwa pale kwa
wakati ule.
‘Ooh….yallah!’ akapiga yowe akiruka na kukuna sehemu ya mguu
iliyorukiwa na uji ulioanza kuchemka kwa fujo. Akababaika akitafuta cha
kuipulia, mwisho akatumia khanga yake kuipua lile sufuria la uji na kulitua
kando.
Akaufunika ule uji na kuchochea kuni kidogo, kisha akabandika
sufuria lililokuwa na viazi vitamu. Sindi akarejea kuketi katika kilekile
kigoda alichokuwa amekalia. Akilala kwa nyuma kidogo na kujiegemeza katika
ukuta mchakavu.
Akashusha pumzi kwa nguvu na kutikisa kichwa kulia na
kushoto, akisikitika, na muda huo kelele zikisikika sebuleni kwao.
Akasogeza shingo karibu na mlango na kutega sikio, akiwa
ameifumbata mikono yake kifuani
‘….nilishasema, nikasema na sasa nasema….kama kuna baba
mwingine humu ndani mwenye mamlaka zaidi yangu mfanye mnavyotaka lakini kama
mimi ndio baba humu ndani…Sindi anaolewa na Mzee Dunia….sitaki mjadala’ sauti
ya baba yake ikiongea ilimfanya atanue macho yake zaidi na kusikiliza kwa
makini uso ukiwa na ndita kadhaa.
‘Baba Sega….Sindi ni mtoto wetu…hebu angalia hiki
tunachomfanyia jamani…hebu…’ mama yake alimtetea
‘Nyamaza!...pumbavu!’ Baba yake alikemea
‘Sio suala la kunyamaza angalau tumsikilize mtoto
jamani…mwanamke ana haki sawa na…’ Mama Sindi hakumalizia sentensi yake, sauti
ya kuchapwa kibao cha uso ilimfikia vema Sindi ambaye alijikuta akifumba macho
na kusikilizia kile kibao kana kwamba alichapwa yeye.
ukimya ukatawala kwa sekunde
‘Afunue tena mtu mdomo kuhusu hili suala na ndio tutajua nani
ana mamlaka humu ndani…. hayo mambo yenu ya vikao na harakati za jinsia na
takataka gani sijui….ziishie kwenye madawati ya mikutano huko huko…msiniletee
upumbavu wenu ndani mwangu…nimeeleweka?....nauliza nimeeleweka?’ Mzee Nalela
aliuliza kwa jazba
‘Ndio…’ sauti ya mama yake ikajibu ikiwa na kwikwi za kilio.
Sindi akajiinamia kwa uchungu, akingoja sauti ya kufungwa kwa mlango ndipo
amfuate mama uake. Baada ya kusikia mlango ukibamizwa Sindi alichomoka na
kumfuata mama yake sebuleni. akamkuta amekaa sofani akilia kichinichini.
‘Mama…’akamuita akimkumbatia huku naye akilengwa na machozi.
Wakalia kwanza
‘Sindi mwanangu….kubali yaishe tu….hata mimi niliozwa hivi
hivi…ona mpaka leo niko ndoani na sijathubutu kuachika’ Mama Sindi alisema
akifuta machozi
‘Angalau uliolewa na kijana mama….Mzee Dunia?...Dunia?
aaargh…mama…. na kujitunza kote huku…leo nikampe heshima yangu yule mzee kama
mke wa ngapi sijui… mama kweli?’ Sindi alilalamika akijua wazi mama yake hakuwa
na la kumtetea.
‘na anajua u bikra na ndio maana ametoa mahari kubwa
kwako….tafadhali usifanye ujinga wowote ukatuletea aibu ambayo itageuka adhabu
kwangu….ndio kuzaliwa mwanamke mwanangu….ndio kuwa mwanamke….kifua hiki
hakikupewa milima hii ili unyonyeshe tu….ni ili uhifadhi pia machungu na magumu
kama haya…’ Mama Sindi aliongea kwa huzuni akimtazama
mwanawe usoni na machozi yakimtiririka.
Sindi akatazama pembeni, hakutaka kuyashuhudia machozi ya
mama yake. Akanyanyuka na kuelekea chumbani akimuacha mama yake anamtazama kwa
huruma.
8888888888888888888888
Suala la kuolewa na Mzee Dunia lilimuumiza sana
Sindi Nalela. Angemueleza nini Nyanzambe, angeanzia wapi. aliutumia muda mwingi
akiwaza mno. Sku hii mara baada ya kumaliza darasa lake
alibaki pale darasani akiwaza na
kuwazua.
Aliukumbuka usiku uliopita, aliukumbuka vema. Nyanza alilia
mbele yake akimuomba amruhusu kuwa mwanaume wake wa kwanza usiku huo. Akiwa na
nguo za ndani pekee juu ya kitanda kichakaavu cha Nyanza, mwanaume huyu
alimbembeleza sana amruhusu
amuingilie lakini Sindi alimkatalia katakata. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa
Sindi kubaki mtupu vile mbele ya Nyanza.
Aliumia sana
kuona Nyanza akihangaika na kumbembeleza
namna ile, laiti tu ingekuwa si ile
mahari ya Mzee Dunia si ajabu Sindi angekubali kuukata utepe wake usiku huu
katika kitanda hiki.
‘Niahidi nitakuwa mimi…’ Nyanza alikata tamaa
‘Nimekuahidi mara ngapi Nyanza…huniamini?’ Sindi aliuliza
huku akiumia zaidi kujua alikuwa akiahidi uongo kwa mara nyingine tena. Nyanza
asingeweza kuwa mwanaume wa kwanza maishani mwake. Nyanza akapiga magoti mbele
ya Sindi akimtazama namna alivyokuwa akiivaa blauzi yake hali matiti yenye
ujazo wa wastani, yaliyosimama imara na
kuiva kama embe bolibo yakitikisika katika namna ya
kuvutia pale Sindi alipoinua mikono juu kuipitisha blauzi yake.
Nyanza alihema kwa mhemko mkali, akifumba macho na kuivumilia
ile hali kwa juhudi kubwa. Akayatazama mapaja manono yaliyojaa na kuvutia mbele
yake. Akili yake ikavurugika kabisa alipopitisha mikono yake mapajani hapo
akianzia magotini na kuteleza kueleka kiunoni. Nguo ya ndani nyekundu aliyokuwa
ameivaa Sindi ilimsisimua zaidi na almanusura apotewe na fahamu.
‘Sindi….niahidi nitakuwa wako milele’ alirai tena na Sindi
akatulia sasa na kumtazama Nyanza, akitamani sana
kumueleza ukweli wa hali halisi na akashindwa.
‘nitakuwa wako milele Nyanza….angalau nipunguzie hizi ahadi
unazonishinikiza kuahidi kila siku’ Sindi akalalamika na Nyanza akamtazama
Sindi kwa kiulizo
‘Nakushinikiza?.....ni kweli nakushinikiza?’
‘Ni kama huamini mimi ni wako’ Sindi alimuelewesha na Nyanza
hakujibu kitu tena. Alinyanyuka na kukaa kitandani akihema.
‘Kwanini usiniruhusu tu’ akazungumza akigeuka kumtazama Sindi
‘Hapana….. nilisema nitakaa hivi mpaka siku ya ndoa’ Sindi
alijitetea
‘Ndoa yako na nani?’ Nyanza akauliza, lilionekana swali la
kipumbavu kwa wakati ule
‘Nyanza!...’ sindi akaita kwa sauti, na kuita kule kukamfanya
Nyanza aukimbize mkono wake wa kushoto
mdomoni mwa Sindi na kumfumba mdomo
‘Shhhh!...mama amesharudi’ akamkumbusha na Sindi akajikuta
akicheka kichinichini. Akanyanyuka na kuvaa gagulo lake
kabla ya sketi, kisha akatupia
khanga yake kwa juu. Nyanza alikuwa akimtazama muda wote alipokuwa akivaa.
Alishavumilia sana na akiingoja kwa
hamu siku ambayo Sindi angemruhusu kumgusa, mara zote aliishia kumbusu na
kumpapasa hapa na pale pasipo hata kumruhusu kumvua nguo lakini leo walifika
mbali zaidi, Sindi alitoa nguo zake na Nyanza akayaona ambayo aliyagusa tu juu
ya nguo. Yote haya yalizidi kumchanganya kupitiliza!
Nyanza akatoka na kuchungulia nje akihakikisha usalama kisha
akamtoa Sindi, huku wakiwa wameinama wakakimbia kitahadhari na kutoka pale kwa
akina Nyanza. Waliikamata njia yenye vichaka kidogo na kutokezea kwa akina
Sindi. Wakapitia dirishani pale pale alipotorekea siku ile aliyokwenda kumngoja
Nyanza kule porini.
888888888888888888888888
Wiki moja baadaye Sindi Nalela alikuwa kwa rafiki yake Maria
ambaye alikuwa anaishi peke yake sasa baada ya familia yake kuhamia mashambani
ambako walikuwa wakilima mpunga. Jioni hii mara baada ya kufundisha, alipita
kwa Maria kwa minajili ya kumjulia hali na kuongea naye hili na lile. Akiwa
amejitupa kwenye sofa dogo lililokuwa sebuleni hapo Sindi alimuona Jerry
Agapela akija usawa wa mlango. Kwanza aliachama kwa
mshangao kwani hakutarajia kumuona Jerry
pale tena wakati kama ule. Akajiweka sawa na kuendela
kushangaa zaidi pale Jerry alipoingia na kusimama mlangoni akimtazama Sindi kwa
tabasamu pana.
Jerry aliuona mshangao wa Sindi waziwazi akamfuta na kuketi
kando yake. Akili ya Sindi akigutuka na kuuona uenyeji wa Jerry ndani ya nyumba
ile.
‘Unafanya nini hapa’ akamuuliza Jerry
‘Kwani ni dhambi mimi kuwa hapa?’ Jerry akajibu kwa mtindo wa
swali na wakati huo huo Maria aliyekuwa nje akiingia ndani na kumkuta Jerry
‘Loh! Jerry….haya vipi?’ Maria akamuuliza Jerry huku
akitabasamu pia na kutua beseni la vyombo alivyokuwa naosha kule nje. Kule
kuchangamkiana kwao kulimfanya Sindi awatazame kwa awamu na kwa viulizo vingi.
Maria na Jerry wakaongea wakitaniana na mazungumzo yao
yakimpa picha kuwa walikuwa wameshaonana mara kadhaa na kufahamiana. Sindi
akatulia tu akiwasoma na asiwaelewe kwa alfabeti wala namba.
‘Naenda kununua kiberiti Sindi….nisubiri’ Maria akaaga ghafla
na Sindi akasimama naye akitaka kuaga na kuondoka
‘Ningoje bwana nakuja!’ Maria kamsisitizia bila kungoja jibu
la Sindi, akatoka na kuwaacha wenyewe
Sindi akarejea kuketi kwenye kochi
akitazama pembeni na Jerry aliyekuwa kando yake akimtazama yeye.
‘Sindi..’ akaita kwa sauti ya chini akiipeleka mikono yake
maungoni mwa Sindi ambaye aligeuka na kuikwatua mikono ya Jerry
‘Sitaki’ akajibu kwa ukali ambao haukuakisi ukali aliotaka
uonekane, neno sitaki lilitoka katika namna ya kubembeleza
Jerry akasimama na kuuelekea mlango, kaurudishia na kurudi
pale sofani wakati Sindi akimtazama kwa
wasiwasi
‘Nakupenda!’ akasema kwa kujiamini
‘Nilishakwambia nina mtu Jerry…..na isitoshe nilimuona
msichana wako siku ile….’ Sindi alijibu akimkumbuka Pamela
Jerry hakujibu kitu, alimkazia macho Sindi kana kwamba
alikuwa akimpigia mahesabu na Sindi hakuhimili yale macho, akayakwepesha na
kuangalia mbele
‘Jerry akamsogelea kwa ukaribu zaidi, Sindi alipojaribu
kuinuka, Jerry alimuwahi na kumrejesha kitini na kufumba na kufumbua Sindi
alijikuta mikononi mwa Jerry hali midomo yao
ikiwa imeungana. Alihea kwa taabu kidogo akijaribu kujinasua mikononi mwa Jerry
wakati huo huo akiifurahia ile hali na akitamani iendelee. Mikono ya Jerry
ailimiliki na kumpapasa kiustadi zaidi, alihisi nguvu zikimuishia, mwili
ukimsisimka na pumzi zikikimbizana puani mwake bila mpangilio.
Jerry akamuachia, kisha akatulia akiwa ameinamisha kichwa
chini kwa sekunde kadhaa
‘I’m Sorry!’ akatamka akiinua uso na kumtazama Sindi ambaye
alikuwa akihema na kuusikilizia ule msisimko ambao bado ulipita mwili kama
shoti ya umeme. Alitamani kushikwa tena na kupapaswa tena wakati rohoni
alitamani kumtandika Jerry kibao cha kumkumbusha kuwa ahakupaswa kumgusa! Mwili
nafsi vilipingana!
Jerry akanyanyuka na kuishia zake wakati Sindi akimtazama
anavyoishia. Dakika moja baadaye Maria akarejea na kumkuta Sindi amejiinamia
‘Nimepishana na huyu mtu hapo nje akili iko maili sita…nimemuita
hajasikia…vipi? ’ Maria akauliza akionyesha sehemu aliyokuwa amekaa Jerry
Sindi hakujibu, naye alinyanyuka na kuondoka. Maria akaguna
na kugeuza kichwa haraka kutazama kule mlangoni alikotokea Sindi. Hakuwaelewa!
.....KUNA NINI KINAENDELEA HAPA?....TWENDE TU UTAJUA YOTE!
No comments:
Post a Comment