8
SEHEMU YA NANE
Sauti ya kilio ilisikika ndani ya nyumba hii sambamba na
sauti ya mkanda uliokuwa unatua juu ya mwili wa huyo aliyekuwa akipiga mayowe.
Mama Sindi alikuwa amesimama nje akihaha huku mikono ikiwa kichwani.
Wanawe
mapacha nao walikuwa wakizunguka zunguka huku na kule na mara chache wakiukaribia mlango na
kuchungulia kwa tahadhari kisha kutoka hapo na kukung’uta kung’uta viganja vyao
mithili ya mtu aliyeungua na moto. kichapo kiliendelea ndani!
Punde mlango ukatanuliwa na Mzee Nalela akatoka akiwa
amefura, mkanda wake ukiwa begani. Akawapita aliowakuta nje kana kwamba hakuwaona.
Mama Sindi na wanawe wakakimbizana kuingia ndani na kumkuta Sindi akiwa ameketi
chini akilia na kusugua sugua zile sehemu zilizosulubiwa na mkanda.
‘Ona sasa unakoelekea mwanangu….’ Mama Sindi aliongea kwa
huzuni, akimtazama binti yake mbaye kipigo kilimtembelea jioni hii, siku mbili
mbele tangu Mzee Dunia alipomuona na Nyanza kule njiani.
Mzee Dunia alimtafuta Mzee Nalela na kudai mahari yake,
akichochea utambi wa kuelezea aliyoyaona, hili lilimkasirisha Mzee Nalela mno.
Sindi alipaswa kuenenda kama msichana aliyechumbiwa
tayari na si kuonekana akiwa na mwanaume mwingine wakizurura kama
wapendanao.
Sindi alilia kwa uchungu akizitazama alama za mkanda uliopita
mwilini mwake kwa nguvu zote. Mama Sindi akamuagiza Danze akalete maji ya moto
na kitambaa kwa ajili ya kumkanda Sindi wakati yeye na Denzi wakimnyanyua na
kumpeleka chumbani.
‘ninavyokukanya uwe unanisikiliza Sindi…’ Mama Sindi
alimsemesha mwanawe kwa kilugha wakati akikamua kitambaa na kukibandika kwenye kiwiko cha mkono wa
kushoto wa Sindi.
‘Yalaaah…Mamamamamamaa….uuuuuwi’ Sindi aligugumia maumivu
akijinyooosha na kuyasikilizia maumivu ya maji ya moto na ya mkono pia. Wadogo
zake waliokuwa wameketi karibu naye nao waliuma meno wakiyaakisi maumivu ya
dada yao .
‘Mzee Dunia amechukia sana ….anaweza
kutudai hata mahari aliyotoa kwanza’ mama akamlalamikia binti yake
‘ aje tu aidai…. hivi hamkumuelewa shangazi?....Sega atafute
pesa ya karo kwa nguvu zake… mama hukulazimishwa kuolewa na baba kwanini mimi
mnanifanyia hivi’ Sindi aliongea haraka haraka hapo hapo akipiga piga mguu
chini sababu ya maumivu ya kukandwa.
‘….ukikaa kumsikiliza shangazi yako yule hata mume hutapata….tayari
ana ndoa mbili zilizovunjika….atakufunza nini cha maana?….mwanamke aliumbwa kuvumilia
hali zote…kumvumilia mwanaume mwanangu…..usianze mashindano na malumbano…’ mama
aliacha kumkanda na kujaribub kumuweka sawa Sindi lakini akakatizwa
‘ hata kama nanyanyasika mama?....ona
nilivyopigwa… kwa vile tu sitaki kununuliwa..’ Sindi alilengwa na machozi upya
‘kutolewa mahari si kununuliwa Sindi….’ mama akadakia
‘Sio kununuliwa ikiwa inatolewa na mtu unayempenda na
uliyemruhusu ailete hiyo mahari sio hivi mama…sio hivi jamani’ Machozi
yaliteremka kwa kasi naye hakujishughulisha kuyafuta, alikuwa anakitazama
kiwiko cha mkono wake kilichokuwa imevimba kuliko sehemu nyingine alizopigwa.
Mama Sindi akanyamaza, akatulia tu akimtazama binti yake,
akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa kisha taratibu akanyanyuka na kutoka mule
chumbani. Sindi akautazama kwa hasira mlango uliorudishiwa na mama yake wakati akitoka, aolewe na dunia kwa ajili ya Sega..... kwanini yeye awe kafara?.... aliutamani muujiza ambao ungemtoa katika mtihani ule, akamfikiria Nyanza, akaumia maradufu alipokumbuka itampasa kumwambia ukweli wa hali halisi, ataupokeaje?
'Sijui...Sijui jamani' akaropoka kwa sauti akitikisa kichwa. Wadogo zake wakimtazama kwa mshangao!
88888888888888888888888888
Ofisi wa Mzee Agapela ilikuwa na watu wawili ndani yake. Mzee
Agapela mwenyewe na mwanasheria wake aliyekuwa ameketi huku akiwa amepakata
faili kubwa ililokuwa limeegemea mguu wake uliokuwa umebebeshwa juu ya mguu
mwingine.
Mwanasheria yule mtu mzima, alikuwa akimtazama Mzee Agapela
kwa umakini mkubwa, wakati Mzee huyu alipokuwa akizungumza hali akiwa amesimama
dirishani akitazama nje, kikombe cha kahawa mkononi, na mkono mwingine ukiwa
mfukoni mwa suruali.
‘sibadili kitu….’ Mzee Agapela alitamka akigeuza shingo na
kumtazama mwanasheria wake kwa macho yaliyokosa tafsiri ya moja kwa moja
‘Lakini robo tatu ya mali
zakokumuachia Fiona?.....Kristus!....sitaki kuingilia maamuzi yako lakini
kwanini awe Fiona?’ Yule mwanasheria aliliondoa lile faili mguuni pake na
kulibwaga mezani, wakati huo huo akimtazama mzee Agapela alivyokuwa akitoka
pale dirishani na kurejea kwenye kiti chake.
‘Nilimuandika yeye tangu ‘will’ yangu ya kwanza….na atabaki
kuwa yeye mpaka nitakapoona umuhimu wa kubadili’ Mzee Agapela alikisukumizia
mbali kikombe cha kahawa alichokitua bele yake wakati alipokuwa anaketi.
‘What about your son?....your blood?’….’ Mwanasheria alimbana
zaidi, akiweka maadili ya kazi yake pembeni na kumvaa mteja wake kama
rafiki yake wa siku nyingi.
Kristus Agapela hakujibu, alimtumbulia macho yule mwanasheria
kana kwamba jibu la swali lake lingepatikana
usoni mwake.
‘Hujamsamehe?’ swali jepesi lilimtoka yule Mwanasheria na
swali lile ndilo lililomfanya Mzee Agapela ayakimbizie macho yake mbali na
kushusha pumzi. Ni kama vile Swali lile ndilo lilobeba jibu la swali la
mwanasheria wake.
‘….the past is over Dennis….’ alijitetea
‘lakini makovu bado yapo na umeyawekea alama…..come on
Kristus unajisikiaje kumfanyia hivi mtoto wako…. and now hujui alipo how do you
feel?…. Fiona ni…’ Yule mwanasheria aliikaza sauti yake kuonyesha msisistizo
lakini Mzee Agapela alitikisa kichwa akikataa kuyaelekeza mazungumzo upande ule
na akamkatisha.
‘No changes kwenye hiyo will…na mikataba mingine yote make
sure iko legally right…’ Mzee Aliweka msimamo wake na hapo hapo akibadili mada,
akanyanyuka a kupandisha suruali yake vema, akikusanya baadhi ya mafaili na
kuyashika mkononi.
Dennis, mwanasheria wake alisikitika lakini alikuwa nje ya
uwezo wa kutatua kile kilichokuwa kikiendelea. Akaichukua briefcase yake
iliyokuwa kando ya kiti chake na kuanza kupakia mafaili yake katika ile
briefcase.
Akaagana na Agapela, wakipeana mikono na kutakiana siku
njema. Dennis Mazimbwe akaondoka akimuacha mzee Agapela amesimama pale pale,
vile vile akiitazama picha ya Jerry Kristus Agapela, iliyokuwa juu ya meza. Akameza
mate kwa taabu kidogo. Alikuwa amemsamehe kijana wake lakini moyoni mwake bado
ukungu wa hasira ulikuwa umemtawala.
888888888888888888888888
Nyanza alikuwa shambani akilima, jua la utosi lilishasogea na
kuweka kivuli sehemu kubwa ya eneo lile. Pamoja na hali ile Nyanza alikaza
mkono na kulima kwa bidii zote akimalizia kipande cha shamba kilichobaki.
Wakati akiendelea kutupa jembe ardhini na kutifua ardhi kwa bidii zote, mdomoni
alikuwa akiimba nyimbo za lugha yao
ili kujiongezea morali ya kulima.
Ghafla tu akasimamisha lile zoezi na kutazama ng’ambo ya pili
ya eneo lile. Kulikuwa na njia nyembamba iliyotengenezwa kwa baiskeli
zilizokuwa zikikatiza hapo mara kwa mara. Kilichomfanya asimamishe shughuli
yake ni gari dogo lililokuwa likitumia njia ile kufika likotaka kufika.
Wakulima kadhaa waliokuwa shambani walisimama wima mithili ya
watu waliokuwa wakitoa heshima zao, wakilishangaa lile gari. Nyanza akakaza
macho yapate kuona vema aliyekuwemo ndani ya gari lile lakini hakuona mtu. Vioo
vilikuwa vyeusi ti!
Njia ile haikuwa ya magari, ni dhahiri aliyekuwa andani ya
lile gari alikuwa mgeni wa maeneo yale an ndio kilichoichota akili za wakulima
wale akiwemo Nyanza. Gari lile likakazimisha njia mpaka sehemu ambayo miti
iliyofungamana ilimzuia dereva kupenya zaidi.
Akalirudisha nyuma kidogo ambako nako lilikwambia katika tuta
lililochimbwa na tairi kwa kadiri alivyotaka kujiondoa katika mkwamo ule. Wale
waliokuwa wakilishangaa lile gari sasa wakakaza macho zaidi waangalia hekaheka
ya dereva na gari lake. Likamshinda!
Mlango wa dereva ukafunguliwa na mguu wa kike, wenye rangi
tulivu, ulionakshiwa na kiatu cha kisasa chenye soli fupi ulitangulia kuonekana
kabla ya mwanamke mrefu, aliyekuwa ndani ya Tshirt nyeupe na kikaptura cha
jeans, kutokezea.
Nywele zake ndefu, zilizolainishwa na kemikali zikipepea
sababu ya upepo uliokuwa ukivuma kuelekea kule alikokuwa. Akashuka na kuiondoa
miwani ya jua aliyokuwa amevaa, akazunguka upande ule uliokuwa na tairi
lililochimba tuta na kulitazama. Akaonekana kuchoshwa na ile hali. Akaachana na
lile tairi na kuangaza huku na kule., moyo wake ukijaa hofu kidogo kuona robo
tatu ya wakulima kule mashambani wakiwa wima wakimtazama yeye.
Kwa hali ya woga, akatoa simu yake na kupiga namba kadhaa
kisha akaiweka sikioni na kusikilizia upande wa pili. Wakati simu ile ikiita,
yule binti akaliona kundi la wanaume wakiwa na mashoka na majembe wakija
uelekeo ule aliokuwa amesimama. Akaikata simu haraka na kuugeukia mlango
aliokuwa ameuegemea. Akaufungua haraka na kujitoma ndani kwa kasi. Aliogopa!
Nyanza aliyekuwa analiona tukio hili vema, alitabasamu na
hatimaye kuangua cheko ndogo akiburudika na woga wa yule binti. Alijua wazi
watu wale walingelimdhuru hata chembe. Yule binti akawasha gari na kutaka
kuliondoa pale lakini tairi likachimba zaidi udongo na kulifanya gari lititie
zaidi.
Akahamanika zaidi alipowaona wale wanaume wakiwa wamesimama
karibu na gari lake wakimtazama
pasipo kumsemesha wala kumpa ishara yoyote. Nao walikuwa wakilitazama gari
namna lilivyokuwa likizidi kudidimia
Wakati akihangaika kuvurumsha gari ili litoke eneo lile,
kijana mmoja akalisogelea dirisha la gari na kuchungulia ndani. Tukio lile
lilimuwewesesha binti yule na akajikuta akiuachia usukani na kupiga yowe mikono
ikitetemeka. Simu iliyokuwa mapajani mwake ikiita haikumzindua.
Alikuwa katika hamaki kubwa, akili yake iliyawazia mabaya
mengi ambayo yangemkuta muda ule pasipo kujipa hata nafasi ya kuwazuri zuri
moja ambalo lingefanya akili yake itulizane na kuomba msaada!
Nyanza aliweka jembe lake
begani na kuanza kushuka taratibu
akilifuata lile kundi la wanaume lililokuwa limesimama katika lile gari,
wakisemezana kwa kilugha….
….BINTI HUYU NI NANI?..... JERRY NA BABA YAKE WANA SAKATA GANI?.....TWENDE
TARRRRTIIIIIBU …UTAYAJUA YOTE!
No comments:
Post a Comment