Friday, May 6, 2011

SIRI YANGU 4....Laura Pettie

Niliduwaa tu na barua ile mkononi. Nikairudisha bahashani na kuanza kutafakari ujumbe ule. Jonas alikuwa akinitafutia nini mimi au naye alikuwa akimuhisi vibaya iloma na ndio alikuwa anataka anitumie mimi kama mpelelezi. Kwa hakika sikuwaelewa wanandoa hawa hata chembe. Sikuendelea na kazi tena.

Nilitoka na kumpitia Iloma kwa ajili ya kwenda kupata chakula cha mchana. Tuliingia mgahawani city garden na kuchagua mahali pazuri na kuketi. Tuliagiza chakula na ndipo Iloma alipoanza kunisimulia mambo mbalimbali ya Jonas. Alinieleza kuwa Jonas hakuwa akila chakula cha nyumbani pale kwa muda mrefu sasa.
`
Mara nyingi alisingizia kuwa alishakula hotelini na kama haitoshi hata chai Jonas hakunywa nyumbani kwake. Iloma alizidi kunilalamikia kuwa mumewe huyo alionesha wazi kuwa alikuwa amemchoka kwa namna Fulani na yeye hakumvutia tena kwani hata katika hafla mbalimbali Jonas hakutaka kuongozana na mkewe, Alinilalamikia vitu vingi ambavyo vilinifanya nianze kumuona jonas katika muonekano mpya wa mwanaume wa ajabu na mnafiki.

“ nimebadilika nini Karen hata Jonas anione sifai tena jamani” Iloma aliniuliza swali ambalo nililikwepa kwa vile ukweli ni kuwa Iloma alikuwa amebadilika mno kimaumbile na pia kitabia tangu amzae mtoto wake wa kwanza kim. Alikuwa ameongezeka mno na kupata umbile jipya lisilo la kuvutia. Urembo wake uliisha kwani sasa hata nywele zake zilichanwa katika mtindo wa kifagio kila siku na hakujiremba kabisa. Na kama haitoshi hakuvalia kinadhifu kama ilivyokuwa zamani na hivyo kupoteza kabisa mvuto aliokuwa nao.

Niliogopa kumwambia kuwa hakuwa akivutia lakini pia nilijua kuwa Jonas hakustahili kumtendea mkewe mambo ya ajabu eti kwa vile tu hakuvutia tena. Nilipanga akilini kumwambia jonas ajirekebishe katika makutano yetu ya jioni hiyo.

Iloma alikoseshwa raha na tabia za jonas, aliendelea kunilalamikia juu ya Jonas.
“ Karen hata chai!... Chai tu ushindwe kunywa nyumbani kwako hebu niambie anamaanisha nini sasa”
“ kwa kweli sijui nini kimemsibu shemeji, hata hivyo inawapasa kuketi chini na kurekebishana Iloma”
“ wapi! Nimrekebishe Jonas wapi Karen! Nianze kumlazimisha kunywa chai nyumbani kwa fimbo?”
niliangua kicheko kifupi kwa majibu ya Iloma ambaye aliendelea kukiweka akiba kicheko chake, alinitazama bila hata tabasamu na kushuhudia nafsi yake ikipigana na uchungu aliokuwa nao. Machozi yalimlengalenga na haraka aliyafuta na kitambaa chake cha mkononi na kuniambia kwa sauti ya kulalamika

“ Bado mapema mno kufikiria talaka, mtoto wetu ndio kwanza ana mwaka sasa na yeye ameshaanza vituko nitamvumilia mpaka lini na kama haitoshi karen Jonas sasa anarejea nyumbani usiku wa manane kila siku hata kama ni biashara Karen biashara ya saa nane za usiku, biashara gani hizo jamani!”
nilishusha pumzi ya nguvu. Nilipata faraja ya kusikia haya kwa namna moja nilianza kumshukuru mungu kwa kumuweka mbali Kelvin kwa vile pengine tungeoana naye angeniumiza hivi kila uchao.
Nilimfariji na kumpa maneno ya matumaini ya kumbadili Jonas. Angalau aliachia tabasamu na kuipa nafasi roho yake iliyokuwa imesongwa na mawazo mengi mno. Tuliondoka pale mgahawani mara baada ya kumaliza chakula na kurudi ofisini. Niliendelea na kazi zangu huku nikiwa na mawazo mengi lakini pia nilikuwa na hamu ya kuongea na Jonas ili nimsikie naye alikuwa na yapi juu ya Iloma. Sikutaka kuhukumu upande mmoja tu!
Jioni ya saa kumi na moja na nusu nilimaliza kazi zangu na kufunga ofisi. Nilipita ofisini kwa Iloma na kumkuta akimalizia kutunza nyaraka mbalimbali za mle ofisini. Kichwani nilikuwa ninatafuta njia ya kumkimbia Iloma na kwenda kukutana na mumewe. Nilihofu kuwa angeweza kuhisi vibaya endapo ningemweleza ukweli wa kule niendako lakini pia Jonas alikuwa ameniasa kumkwepa Iloma. Binafsi yangu nilihisi msuto ukipita nafsini mwangu kwa kuona kuwa kukutana na Jonas bila idhini ya Iloma lilikuwa ni kosa kubwa.
“ Iloma acha mimi nitangulie kaka yangu Brian alisema atanipitia pale kituoni ili twende wote mahali”
“ oh! Itakuwa vema mkinipa lifti pia si unajua pale posta usafiri ulivyo wa shida na leo sijaja na gari” alinijibu pasipo kunitazama na laiti angelifanya hivyo si ajabu angeliushuhudia wasiwasi uliokuwa juu ya paji la uso wangu.
“ aah! Hatuendi nyumbani na… isitoshe alisema atanipitia kwa taksi ya Dulla” nilibabaika kidogo
“ amepata nyumba ndogo nini maana teksi ya Dulla ndio usafiri wa kwenda kona!” aliniambia kiutani nami nikashusha pumzi na kumshukuru mungu
“ pengine huwezi kujua ati! Na labda anataka kwenda kunitambulisha wifi mdogo” nilizidi kumdanganya rafiki yangu huku nikijifaragua faragua kwa vicheko vya uongo na kweli. Moyoni nilihisi mzigo mzito kumtendea rafiki yangu unafiki kama huu. Tulitoka ofisini mpaka kituoni na baada ya dakika kama kumi teksi ya dulla ilisimama umbali mfupi toka pale tulipokuwa tumesimama na Iloma. Ni yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuiona na akanishtua
“ haya mama Dulla huyoo … na angalia msifumaniwe huko ukarudi na ngeu” alinitania huku akinionyesha mahali ilipokuwa imepaki teksi ile.
“ tupo makini michapo yote kesho Iloma”
“haya msalimie Brian!”
“salamu zimefika, tutaonana kesho!”
nilimpungia mkono na kuanza kuchapua hatua za haraka kuielekea teksi ile. Vioo vyeusi vya teksi ya Dulla vilimfanya Iloma asimuone mumewe ndani ya gari. Nilifungua mlango wa nyuma na kujitoma ndani ya gari. Jonas alikuwa ameketi kiti cha nyuma.

Tulisabahiana na Dulla akaliondoa gari. Kama mtu alikuwa amepewa maelezo kabla Dulla alitupeleka Lightness Hotel. Tuliingia mle hotelini na kwenda moja kwa moja mapokezi. Cha kushangaza Jonas aliomba funguo za chumba na kupatiwa. N

ilihisi alikiandaa chumba hicho mapema na sikumuelewa kwanini alichukua chumba wakati tulihitaji kuongea mara moja na kuachana. Sikuwa mjinga kiasi cha kuburuzwa na Jonas. Nilisimama nyuma yake na alipogeuka tulikutanisha nyuso zetu sambamba.
“ hii ina maana gani Jonas!?” nilimuuliza kwa hamaki
“ hatuwezi kuongelea pale mgahawani Karen, mimi ni mume wa mtu na mfanyabiashara ninaye julikana sana hapa jijini, wewe ni rafiki wa mke wangu. Kuketi mgahawani pale tukiongea hakutaleta picha nzuri kwa jamii na isitoshe Iloma hajui kama wewe uko na mimi muda huu” alijitetea kwa kadri alivyoweza lakini pia sikuwa mjinga kiasi ambacho alifikiria. Nikampachika swali
“ sasa Jonas kuonekana mgahawani tukiongea na kuonekana tukielekea vyumbani kipi kina unafuu?”
“ okey! Kwahiyo tukakae mgahawani sio?” aliniuliza kwa sauti kali kidogo
“ nadhani ni bora zaidi Jonas” sikungoja maelezo zaidi nilianza kuchapua hatua kuelekea mgahawani. Nikachagua meza moja iliyokuwa kwenye kona na kuketi. Alinifuatia nyuma na kuketi kiti kilichokuwa mbele ya meza iliyokuwa kati yetu. Aliagiza vinywaji na chakula na kwa pamoja tukaanza kula huku maongezi yakichipukia
“ ni bora uniambie kiini cha mwito huu shemeji” nilimrudisha katika mada kuu
“ mbona una haraka Karen kula kwanza mama” alinijibu hali akiachia tabasamu lake zuri la kuvutia
“ halafu ninayo mengi ya kukuuliza Jonas”
“ juu ya nini?” alionesha mshtuko akaacha kula na kunitumbulia macho
“ mbona una haraka kula kwanza shemeji” nilimtania na wote kwa pamoja tukaangua kicheko. Tulipomaliza kula mhudumu aliondoa baadhi ya vyombo na tukabaki tunaburudika na vinywaji.

Ni hapo ndipo Jonas aliponitobolea kiini cha mwito ule, sikupata hata nafsi ya kumsuta Jonas kutokana na yale niliyoyasikia toka kwa mkewe.

Kwa takribani dakika moja na nusu nilibaki nikiwa nimemtumbulia macho jonas pasipo kujitambua akilini. Nilijaribu kushusha pumzi ndefu na kuangaza huku na kule ili japo nitoke ndotoni lakini bado ilibaki dhahiri kuwa sikuwa ndotoni.

Sikuwa naota wala sikuwa nawaza ilikuwa ni kweli kuwa masikio yangu yalikuwa yamesikia kile kilichotoka mdomoni mwa Jonas.

ITAENDELEA....

4 comments:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger