Monday, May 23, 2011

SIRI YANGU 7......Na Laura Pettie

Muda wote huo nilikuwa nimeshastahimili ile harufu mbaya niliyokuwa ninaisikia na sasa nilishanza kuhisi kichefuchefu! Nikaona nisipoaga mapema nitaweza kutapika mbele ya wenyeji wangu!

Binafsi nilihisi kuna kinyesi cha mtoto kimesahaulika pale ukumbini au choo cha mle ndani hakikuwa safi! Nikashindwa kuelewa kama iloma hakuwa akikerwa na ile harufu au ndio pua zimeshajizoelea kuvuta uvundo wa aina ile!

Niliondoka kwa iloma na kurejea nyumbani. Niliingia nyumbani huku tayari giza likiwalimeshatanda. Ilikuwa saa mbili na robo. Nilimkuta dada yangu Debby akiwa ananingoja wimawima ukumbini hali mama akiwa amelala sofani akitazama televisheni. Niliwasabahi akaitikia mama peke yake. Nikajiweka sawa!
“ Karen! Hivi ni nini kinaivuruga akili yako we mtoto?”
“hata salamu Debby?” nilimkatiza
“Najua u mzima wa afya, lakini huku unakoelekea nadhani utakuwa na matatizo katika akili yako”
Nilishusha pumzi fupi ya kero, nikamtaza Debby kwa hasira .
“ Debby! kaka brian alichanifokea sana asubuhi hivyo inatosha, hakuna mtu anayehoji kilichonikuta, hakuna mtu anayehoji sababu za msingi nilizonazo wote mnaniona hayawani tu! Kama ni kustarehe basi ningeanza siku nyingi na si leo hii nikiwa na kazi na maisha yangu” nilikuja juu na tayari machozi yalisha tengeneza mfereji mashavuni mwangu. Niliwaza juu ya kubakwa kwangu na kulinganisha na lawama ninazopewa nikaona uonevu mkubwa juu yangu!
“ Okey! Nini kilichokufanya ulale nje jana?...brian amenipigia simu akanieleza kuwa umerejea asubuhi ya leo na tena ulilala nje bila hata taarifa kwa mama” Debby sasa alihoji taratibu na kuketi kochini
“ haitabadili akili ya mtu kati yenu! Endeleeni kuniona punguani!” nilimjibu kwa mkato na kutokomea chumbani. Nikajifungia na kuanza kulia. Nililia muda mrefu na hatimaye nikapitiwa na usingizi. Hata mama aliponigongea sikutaka kumfungulia kabisa. Nikalala na njaa mpaka asubuhi.

Asubuhi na mapema niliamkia kujiandaa. Wakati nikijishughulisha kwa hili na lile simu yangu ya mkononi iliita na haraka nikaipokea pasipo hata kuangalia jina la mpigaji. Moyo ukapiga paa! Ilikuwa ni sauti ya Jonas

“ Nimeshindwa kulala kwa amani Karen!...nakupenda sana, sijui niseme nini unielewe Mpenzi…” sikumpa nafasi ya kuendelea kuongea upuuzi wake. Nilikata simu na kuirushia kitandani.

Nilihisi kubanwa na binadamu huyu aliyekuja ghafla katika maisha yangu. Nikatamani kumweleza Iloma ukweli wa kile alichonifanyia mumewe lakini pia sikuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani!

Wiki hiyo nzima sikuwa na amani moyoni. Ijapokuwa mama alijitahidi sana kuniweka sawa lakini akili yangu ilikuwa bado inazungukwa na mambo mengi.

Siku hiyo kama kawaida ya jumamosi zingine niliamka mapema na kufanya usafi wa nyumba pamoja na kufua. Mida ya saa nne Iloma alinipigia simu na kuniambia kuwa alikuwa njiani kuja kwangu. Nilimalizia kazi zangu haraka na kujiweka tayari kumngoja iloma.

Sikuwa na shaka kwa vile ilikuwa kawaida yake kunitembelea nyumbani. Saa nne juu ya alama iloma aliingia nyumbani, alionekana mchangamfu na mwenye furaha. Mara baada ya kusabahiana na utani wa hapa pale kupita tuliketi barazani na yeye akawa ananisaidia kumenya baadhi ya viungo vya kupikia.

“…angalau sasa Jonas ametulia Karen” aliniambia kwa bashasha
“ matatizo ni sehemu ya uhusiano” nilimjibu kimkato huku nikishusha pumzi. Masikini Iloma hakujua kuwa katika kipindi hicho Jonas alikuwa akinipigia simu kila usiku kunibembeleza niwe mpenzi wake kwa siri. Nilikuwa nikijitahidi kwa kadri nilivyoweza kumkwepa Jonas!
“ umenisaidia sana Karen nadhani napaswa kukuombea upate mume bora kabisa!”
“ dua imefika…vipi Kim anaendeleaje?” nilibadili mada ili kukwepa kuongelea zaidi masuala ya ndoa.
“alikuwa na anaharisha sana wiki iliyopita lakini sasa hali yake nzuri kiasi” Iloma alitamka taratibu hali akiendelea kumenya vutunguu swaumu vilivyokuwa ndani ya ungo. Nilipepesuka kidogo na haraka nikajishikiza kwenye sinki lililokuwa kando yetu.
“Karen nini?” iloma aliuliza kwa hamaki akiweka ungo chini na kuja kunishikilia
“najisikia vibaya Ilomaa…mama nakufa!” nilipiga ukelele hafifu kabla ya kuanza kuona kizunguzungu, nikajikuta nakosa nguvu. Nilifumba macho na kuyafumbua taratibu lakini uwezo wa kuona ukatoweka ghafla sikuelewa kilichoendelea.

Nilipokuja kuzinduka nilijikuta juu ya kitanda cha hospitali. Niliangaza huku na kule pasipo kumuona yeyote. Nikajituliza tuli hali akili ikianza kutafakari kilichonikuta.

Wakati nikiwaza hili na lile mlango wa wodi ulifunguliwa na kijana mmoja aliyevalia mavazi ya kitabibu aliingia akiwa na faili mkononi. Taratibu nikaiweka shingoyangu sawia na kumkodolea macho yule kijana. Nikatunduwaa alikuwa Kelvin Nashon! Mchumba wangu aliyeniacha nikiuguza madonda ya roho!

“ unaendeleaje Karen!” alinihoji taratibu kwa sauti yake ile ile ya upole iliyojaa kila aina ya ukarimu. Sikumudu kufungua mdomo na kujibu kitu. Nadhani akili ilichanja mbuga na kukiacha kichwa kikiwa kitupu mithili ya mtungi uliotoboka! Macho yalitanuka zaidi na nikawa ninamtazama mwanaume huyu aliyekuwa mbele yangu kama kiumbe cha ajabu toka sayari nyingine.

Nilihisi mkuki moyoni, machozi ya hasira ya kuachwa solemba, machozi ya hasira ya kusalitiwa yalitanda katika mboni za macho yangu na kufanya macho yametemete mithili ya mbalamwezi!

“ ondoka…go away kelvin!” nilimudu kutamka maneno hayo kwa sauti ya kitetemeshi kabla ya kukabiliana na kwikwi nilizoshindwa kuzivumilia, nikaangua kilio cha kugugumia. Sikujali kuwa alikuwa pale kunisaidia kama daktari na wala si kama Kevin Nashon.

“ weka hasira kando Karen… unahitaji kusaidiwa kama mgonjwa” Kelvin alinisemesha taratibu hali akijivuta na kusogea karibu zaidi na pale nilipokuwa nimelala. Nilihisi kuumia kana kwamba nilikuwa nimeachwa jana tu!

“ sitaki Kelvin! Kama ni kufa acha nife Kelvin ungekuwa nia ya kunisaidia usingenitendea vile… ni msaada gani ulio nao wewe… msaada gani Kelvin, wewe! Wewe una msaada gani kwangu?” nilimpayukia kwa hasira tayari nikiwa nimeshaketi kitandani na kumtazama vema Kelvin. Alikiinamisha kichwa chake chini kwa sekunde kadhaa kisha kama ilivyoada yake aliachia tabasamu lake tulivu.

“ Karen! Hayo ni masuala binafsi na hapa niko kazini” alijaribu kunituliza lakini kinyume chake aliwasha moto nyikani. Niliteremka toka pale kitandani huku nikipepesuka na kuangaza huku kule kuangalia kama kuna kitu changu. Nilipotaka kupiga hatua nilihisi uzito kichwani nikayumba na kutaka kudondoka. Kelvin akaniwahi na kunidaka haraka.

“ niache, usiniguse Kelvin…” nikamkemea na kujitoa mikononi mwake huku nikiwa nimejiegemeza kitandani nilimtazama kwa chuki kiasi ambacho hata yeye Kelvin alishindwa kuamua la kufanya juu yangu.

Alionekana wazi kutafuta maneno yatakayotosheleza kuelezea huruma yake kwangu. Akakosa!
“ Karen!...karen” aliniita kwa upole
“ sitaki kusikia na…” sikumalizia kauli yangu kwa vile mlango ulifunguliwa na mama pamoja na Iloma wakaingia. Mama alikuja mbio kunikumbatia.
“ooh! Karen unajisikiaje?” mama alinihoji nami sikushughulika kusikiliza
“ Iloma sitaki kulala hapa ni bora mkinihamishia hospitali nyingine”nilipayuka kwa hasira
“ kwanini?” mama alihoji haraka akiwa amekumbwa na mshangao
“ Iloma umenielewa?” nilisisitiza bila kujali swali la mama
“ lakini Karen …”alitaka kupingama nami
“ hakuna cha lakini kama hakuna kati yenu mwenye uwezo wa kunitoa hapa mpigieni baba yangu simu aje ama kaka yangu Brian” nilizidi kuja juu mno. Mama akamtazama Iloma na kumwambia
“ nenda kalipie kule mapokezi na tumpeleke Marie stopes sasa hivi” alichomoa pochi yake na kutoa pesa alizomkabidhi Iloma. Kabla hata Iloma hajapangua hatua moja Kelvin alimuwahi na kumzuia mlangoni.
“ nitalipia mimi acha tu!”
“ Sina haja na msaada wako Kelvin si umetoka kuniambia sasa hivi kuwa uko kazini na sasa unataka kuyalipia matibabu yangu kama nani?” nilimtupia swali la kebehi lililomfanya Kelvin anitazame kwa mshangao wa waziwazi.
“ sikudhani kuwa ungebeba kisirani kama hiki Karen!” aliniambia kwa sauti ya upole nami nikaangusha cheko fupi la dharau na kumwambia “ sikudhani kuwa ungekuwa mkarimu kiasi hiki Kelvin!” .

Akabaki kunitazama tu asijue aongee nini mbele yangu. Nadhani pia aligundua ni kiasi gani nilikuwa na majibu ya ovyo. Mama alinitoa nje huku akiwa amenishikilia na tukaelekea mapokezi nilikomkuta dada yangu Debby. Moja kwa moja walinipeleka hospitali ya maries topes mwenge.

Daktari aliniambia nilikuwa na malaria pamoja na upungufu kiasi wa damu. Nililala hospitalini pale kwa siku moja na kutoka jioni. Mwezi mmoja baadae hali yangu ilitengamaa lakini nilianza kupata dalili Fulani ambazo zilinipa mashaka. Mwezi wa pili dalili hizo zilionekana wazi nami nikaanza kuhisi kitu kisicho cha kawaida katika mwili wangu.

Ijumaa moja tulivu niliamua kwenda hospitali kupata uhakika wa hisia zangu. Nilichohisi kilikuwa kweli kabisa. Nilikuwa na mimba changa! Pamoja na daktari kunithibitishia kwa vipimo lakini bado sikuamini.

Mimba! Kwa asilimia mia moja na pengine na moja ya ziada mimba hii ilikuwa ya Jonas! Shemeji yangu, mume wa rafiki yangu mpenzi Iloma.
“Dokta una hakika na majibu yako?” nilimuuliza Daktari kwa wasiwasi
“ Huniamini?” naye alinirudishia swali huku akinipatia karatasi iliyokuwa na majibu toka maabara. Niliikodolea macho mara mbilimbili nikitamani majibu yasomeke visivyo. Nikairudisha mezani na kusimama.
“inaonekana hukuitarajia kabisa eeh!...” dokta alinisemesha lakini hakuwa katika mawazo yangu. Nikazidi kuchanganyikiwa nisijue hata nianzie wapi kutatua tatizo hili. Nadhani nilitoka katika chumba cha daktari pasipo hata kumuaga. Nilikatiza kordo mbili tatu na kutokezea mapokezi. Niliketi katika benchi moja lililokuwa kando huku akili ikinizunguka isivyo kawaida “ nitafanyaje sasa?” nilijiuliza kwa sauti bila kujali kama kulikuwa na mtu wa kunipatia jibu la swali hilo.

Nilifikiria kuitoa kwa siri lakini nikaona bora kumshirikisha Jonas ili nijue yeye ana mawazo gani juu ya tatizo hili. Nilikosa raha kabisa, nilikosa amani moyoni kiasi kwamba hata wale walionizoea hawa kuacha kunighasi kwa maswali ya kutaka kujua kilichonisibu.

Haya yalikuwa maji ya shingo na kwa hakika nilimlaani Jonas kwa lugha zote! Baada ya kufikiria sana nilimpigia jonas simu na kutaka kukutana naye nyumbani kwetu kwa vile kwa wakati huo mama alikuwa amemfuata baba Nairobi. Jioni ya siku hiyo Jonas aliwasili nyumbani na baada kupata viburudisha koo, niliamua kumpasulia jonas ukweli.

Alitunduwaa kwa sekunde kadhaa huku macho yakiwa yamemtoka mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango. Jasho lisilo rasmi lilimbubujika mwanaume wa watu hali kiyoyozi kilikuwa kikitimiza wajibu wake ipasavyo. Midomo yake ilimwemweseka pasipo kutoa neno lolote. Nilimtazama kwa sekunde kadhaa kisha taratibu nilijitoa kochini na kusimama mbele yake.

“ najua lawama hazijengi jonas lakini huu mzigo si wangu peke yangu!” nikauvunja ukimya uliotutembelea ghafla.

“ hakuna njia Karen inabidi uitoe…mimi ni shemasi Karen, mimi ni kiongozi ndani ya kamati ya vijana kanisani…mimi ni mume wa mtu…unadhani nitasimamaje endapo suala hili litajulikana?” alijitutumua kujibu katika namna ya kupayuka na kuhamanika. Eti kwa wakati huo ndio alikumbuka nyadhifa zake kanisani na kuwa yeye ni mume wa mtu.
“ ungeyafahamu hayo mapema usingenitendea unyama ule jonas na tena nataka ufahamu kuwa mimba hii siitoi ng’o! kuzini uzini na kabla hujajua hata adhabu ya uzinzi unataka ujiongezee dhambi ya kuua, utamjibu nini muumba?”

“ itakuwa juu yako Karen siwezi kuhatarisha ndoa yangu sababu yako!” alinijia juu akizidi kuhamanika vibaya mbele yangu, akinitazama kwa chuki ilichonganyikana na hali ya kutoamini...sikutarajia hali ile na sikutegemea jonas angebadilika vile, nilichoka mara mbili ya mwanzo!


ITAENDELEA.....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger