Thursday, May 26, 2011

SIRI YANGU 10....Na Laura Pettie

...Saa kumi jioni niliondoka kazini na kurejea nyumbani. Nilimkuta mama anaandaa chakula cha jioni lakini pia akiwa na uso uliosawajika. Nilibadili nguo kisha nikajiunga naye jikoni.

Mama alionekana kuwa mwingi wa mawazo na kila mara alinitazama kwa kituo. Mwisho alitoa dukuduku lake.

“ Karen utanificha mpaka lini mwanangu!” aliacha kukata kata nyanya na kuniuliza

“ juu ya nini” moyo ulipiga mkambi lakini ilinipasa kuuliza kujua kisa. Mama alivuta pumzi na kuziteremsha kwa kasi. Alitikisa kichwa kabla ya kurudia kunitazama kwa kituo na kuniambia

“ wewe mjamzito Karen, mimi ni mama yako nakujua kama ninavyokijua kiganja cha mkono wangu wa kuume, umejitahidi kuficha lakini mwanangu unasahau kuwa mimba haina siri!”
“ mama!” nilishtuka
“ unakataa nini Karen!?” alianza kunijia juu hali akionekana wazi kukerwa na mshangao wangu.

“ kwanini umeniwazia hivyo mama” nilihoji badala ya kujibu huku nikijigeuzia dirishani na kuyatumbua macho yangu kwa woga.

“ sikulazimishi ukiri lakini kumbuka mficha maradhi kilio umuumbua!”

sikujibu kitu kuchelea kubanwa zaidi lakini tayari nilishakaa mguu sawa nikijua ipo siku bomu litalipuka tu lakini pia nilijipa tumaini kuwa Jonas angenioa bila kujali kama ningevunja ndoa ya rafiki yangu Iloma.

Masaa yalikuwa hayaendi hata kidogo. Mara kadhaa niliitazama saa yangu ya mkononi na kuutumbulia macho mshale wa dakika uliokuwa ukienda kwa maringo bila kujua moyo wangu uliokosa subira ulikuwa ukipiga mara mbili ya kawaida.

Saa moja usiku nikiwa chumbani simu yangu ya mkononi iliita. Zilikuwa ni namba ngeni kabisa machoni pangu. Nilihisi jonas alikuwa ameamua kunishangaza.

Nikaipokea kwa mbwembwe lakini baada ya kusikia sauti nyingine tena ya kike nilijiweka sawa na kusikiliza na sasa nikaitambua sauti hiyo kuwa ni sauti ya iloma. Nikajiinusha toka kitandani na kusimama wima sakafuni simu ikiwa sikioni.

Nikatega sikio kwa makini.
“ Karen!... Mungu wangu!...Karen… mdogo wangu… Jonas ameniacha” huku akilia aliyatamka maneno hayo kwa uchungu hasa. Nikahisi bomu la talaka limelipuka. Nami kiherehere cha moyo kikanikumba

“ kakuacha! Sikuelewi Iloma” niliongea kwa sauti ya mshangao huku nikiwa katika hali ya kawaida kabisa kwa vile nilishahisi Jonas amemweleza mkewe juu ya talaka lakini wakati nikiwaza hayo Iloma alitamka maneno ambayo mpaka leo hii ninapoyakumbuka natokwa na machozi ya uchungu.

“ Karen! Jonas amefariki usiku huu kwa ajali ya gari kinondoni” nilihishiwa nguvu, simu ikaniponyoka mkononi na pasipo kujitambua nilianguka chini na kuzirai.

ITAENDELEA....

2 comments:

  1. Eeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeenglish!!!!! pleeeeeeeeeeease??? we want to participate... I tried to translate, but the flow was not good..

    ReplyDelete
  2. hahahahahaa pole sana! you are missing a lot of fun, keep on learning swahili kwame...u will get along with all these swahili words..thanks for visiting the blog i hope i will learn yoruba so soon

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger