Saturday, May 7, 2011

SIRI YANGU 5..... na Laura Pettie

“ sikuelewi jonas… hivi…ina maana …my god!” niliwaya waya tu pasipo kujua la kusema

“ Karen huelewi nini hapo nina maanisha kile nilichokisema”

“ hauko makini na akili zako Jonas! nilikuheshimu sana na sikutarajia kusikia upuuzi kama huu toka kwako na kumbe ndio maana Iloma hana amani moyoni mwake…. sikutarajia ungelikuwa mpumbavu kiasi hiki Jonas. Umenivunjia heshima na umemvunjia Iloma heshima yake”

nilinyanyuka na kujiandaa kuondoka lakini sikumudu hata kupiga hatua moja Jonas aliudaka mkono wangu na kuungandamiza mezani. Nilimtazama tu pasipo hata kumkemea. Mboni za macho yake zilimeremeta na kuyaonyesha dhahiri malengelenge ya machozi yaliyotuama machoni pake.

“ kwanini unanifanyia hivi Karen, kwa vile umegundua kuwa nakupemda sana”
“ sihitaji kusikia upuuzi wako Jonas” nilimfokea
“ narudia kile nilichokisema Karen nakupenda sana na hilo nililitambua siku nyingi Karen, nimekuwa nikihangaika na kuteseka sana juu yako lakini hutaki kuzielewa hisia zangu! Hutaki kunipa nafasi ya kukuonyesha namna ninavyokupenda Karen” machozi yaliteremka taratibu mashavuni pake.

Nikahisi kumuonea huruma Jonas. Kwa namna alivyokuwa akilia nilihisi imani lakini alikuwa mume wa mtu tena mume wa rafiki yangu mpenzi.

“ na Iloma je?... anayonafasi katika maisha yako Jonas” nilirejea kuketi pale kitini na kuuondoa mkono wangu katika kiganja cha mkono wake wa kuume.

“ hilo nalitambua lakini nafasi iliyo ya kipekee ni ile ninayotaka kukupa wewe Karen. Unaisumbua nafsi yangu mno na kama si Iloma kubeba mimba yangu kabla ya ndoa Karen ningekuoa wewe”

Nilishusha pumzi ndefu na kumtazama mwanaume huyu kwa mshangao mkubwa.

“ siwezi kumsaliti Iloma siwezi Jonas nataka ufahamu hilo na…” simu yangu ya mkononi iliita na mpigaji alikuwa mama.

Nilinyanyuka haraka na kwenda kuipokelea kando. Mama alikuwa anataka kujua mahali nilipo kwani muda wa mimi kuwa nyumbani kama kawaida ulikuwa umeshawadia na ikizingatia alikuwa mgonjwa.

Nilimwambia mama avute subira kwani ningekuwa nyumbani muda mfupi baadae. Niliporudi mezani niliimalizia juisi yangu na kumwambia Jonas kuwa nahitajika nyumbani haraka.

Nilikurupuka asubuhi ya saa moja nikiwa mahali ambapo ilinichukua dakika kadhaa kupatambua. Yalikuwa ni mazingira mapya kabisa tofauti na yale niliyoyazoea.
Niliangaza huku na kule pasipo kupatambua mahali pale na hali mwili mzima na hasa kichwa kikiwa na uzito wa ajabu.

Nikiwa ndani ya tafakari hizo mlango wa chumba nilichokuwamo ulifunguliwa na Jonas akaingia akiwa na sinia lililokuwa na staftaha. Niliduwaa!

“Jonas!...umenifanyia nini hiki…mungu wangu…Jonas…nitasema nini …hapa ni wapi sasa?” nilishindwa hata kuzipangilia sentesi zangu katika mpangilio unaoeleweka.

Akili ilianza kufanya kazi na mara moja nilitambua kuwa nilikuwa katika moja ya vyumba vya hoteli ya Lightness.

ITAENDELEA....

2 comments:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger