25
Fiona Agapela alishusha pumzi kwa nguvu zote na kusimama
kichovu pale alipokuwa amejibanza akimsikiliza mumewe kwa siri. Akazikusanya
nguvu na kutoka kwa mwendo wa kunyata huku kichwa kikitazama ule mlango wa
kuingilia chumba cha ofisi ya Mzee Agapela ndani ya nyumba yake.
Kule kutazama nyuma kukamfanya apamiane na Jenifa
aliyetokezea kwenye kona
‘Whaaat!’ Jenifa akamshangaa
‘Hebu njoo..’ akafanya kuamrisha, akimshika mkono Jenifa na
kuelekea naye kule alikotokea Jenifa. Ilikuwa kama alikuwa anamburuza kwa ile
haraka aliyokuwa nayo. Wakapelekana chumbani kwa Jenifa na kufunga mlango.
‘Kuna nini?’ Jenifa akauliza kwa mchecheto na Fiona akampa
ishara ya kutulia kwanza, akimshika mkono na kumketisha kitandani, Mashaka yakiwatawala
kila mmoja kwa sababu yake.
‘Baba yako alikuwa anaongea na Mzee Okello’ Fiona akaongea
kwa sauti ya tahadhari
‘Mmh…kuhusu nini?’ ile sauti ya tahadhari ikahamia kwa
Jenifa, macho sasa yakimtoka na masikio yake yakifunguka kwa mapana na marefu
‘Ndoa!’ Fiona akajibu haraka haraka kana kwamba jibu lile
lingempatia ahueni ya wasiwasi na jakamoyo lililomkumba ghafla.
‘Ndoa?’ Jenifa ahamaki kwa sauti kiasi cha kumfanya Fiona
amzibe mdomo haraka sana
‘Shi shi shii..’ akatamka Fiona akiupiga piga mdomo wa Jenifa
kwa kiganja chake akizifuatisha zile Shi alizozitamka. Jenifa akajishtukia na
kushusha sauti yake
‘Ndoa ya nani na nani?...’ akauliza kwa sauti ya kunong’ona
‘Pamella na Jerry…’ aliyeulizwa akajibu akigeuka pia kutazama
mlangoni kuangalia usalama.
‘Khaa! ndoa ya Pamella na mzimu au?... wana uhakika gani
Jerry yupo?... mi mwenyewe sina uhakika na kama niliyemuona ni Jerry kwa kweli
na kama ulvyosema Pamella amekataa hajui alipo basi itakuwa miujiza kupanga
ndoa na mume hajulikani aliko’ Jenifa akaongea kwa mshangao na asielewe
‘Hata mimi ndio nashangaa au kuna kitu kinaendelea hapa na
sie hatuna habari?’ Fiona akauliza kidadisi
‘Sijui…’ Jenifa akakataa kwa kutikisa kichwa bao alikuwa
hajaielewa mantiki nzima ya wazee wale kuongelea ndoa hali Jerry mwenyewe
alikuwa hajulikani alipo.
‘nenda kazungumze na Pamella…’ Fiona akamsukumizia Jenifa
mzigo mzito alioutua hapo hapo
‘Pamella!?...aaah! yule mtu?...hapana bora nikae posta masaa
kumi naongea na sanamu la bismack kuliko kutumia hata dakika zangu tano kuongea
na yule mwanamke…I hate her mnoooo’ Jenifa akakiri yake akiukwepa mzigo wa
Fiona.
‘Sasa tutajuaje kinachoendelea?’ Fiona akahoji akionekana
wazi kusumbuliwa na hali ile kupita maelezo
‘Tukae tu kimya tuone mwisho wa mchezo utakuwaje…. watajua
wenyewe wanaotaka kuandaa harusi na mume hewa…’ Jenifa akajitoa na asijue
mwenake Fiona alikuwa na maslahi gani katika sakata lile. Fiona akashusha pumzi
na hapo hapo wakajikuta wakitazamana na kutoleana macho bada ya kumsikia Mzee
Agapela akimuita Jenifa kwa sauti.
Jenifa akanyanyuka na kutoka akimuacha Fiona peke yake. Lile
hamaki aliyokuwa nayo sasa ikajitokeza kama kama sindano itoboayo nguo. Jerry
alikuwa hai! huu ukweli alioanza kuuamini ulimnyima usingizi, ulimtesa tangu
Jenifa alipomwambia alimuona Jerry akiwa na gari kama la Pamella. Aliweweseka!
Hakutaka jambo lile liwe kweli hata chembe.
Alihema kwa nguvu kiasi cha kutoa sauti mdomoni, mabega yake
yakinyanyuka na kushuka kila sekunde iliyokatika. Uso wake uliojaa jitimai
iliyochanganyikana na mashaka ulipoteza nusu ya urembo wake. Alihisi maji
aliyoyafumbata kiganjani yalianza kuchuruzika!
8888888888888888888
Pamella Okello alitoka supermarket akiwa na mizigo
iliyoonekana kumuelemea kidogo sambamba na kule kuongea na simu wakati
akilielekea gari lake. alipata tabu kidogo kuibana simu kwa bega lake la
kushoto hali pia akijaribu kufungua mlango wa gari pasipo kudondosha kifurushi
hata kimoja. Akafanikiwa!
Akiwa ameibana simu yake vile vile akarudi nyuma na kufungua
mlango wa siti ya nyuma na kutua vitu vyake vyote, kisha akarejea siti ya mbele
na kuingia garini. Hakuwasha gari, aliiondoa simu upande wa kushoto na
kuihamishia mkono wa kulia sasa ikiwa imeshikiliwa kwa mkono.
‘Baba?... amekuja lini?’ akauliza akiwa amekunja uso katika
namna ya kutomuelewa mpigaji
‘OMG!.... kweli?....Khaa!...sasa?.....Yesuuu… amekuja na
mama?.... okay…sawa…poa basi…. poa…. haya bwana’ akawa anaujibu upande wa pili
na kisha akakata simu na kuilaza mikono yake juu ya usukukani, mdomo ukiwa
wazi, macho yakikikodolea kioo cha mbele pasipo kukitambua akilini. Alikuwa
ameduwaa!
Akawasha gari na kuondoka eneo lile akielkea nyumbani kwao,
alikokuwa baba yake. Njia nzima alikuwa akipanga na kupangua kipi cha kuongea
na kipi cha kuficha. Kipi cha kujitetea na kipi cha kukiri. Nusu saa baadaye alishafika nyumbani na
kushuka kwa kasi akilifuata lango la kuingilia ndani. Pale sebuleni hakumuona
mtu zaidi ya watumishi waliomtazama tu na wasitamani hata kuongea naye.
Akazikwea ngazi haraka haraka na kuelekea sehemu ya mapumziko iliyokuwa
ghorofani.
Akamkuta mama yake ameketi akinywa juisi na kusoma majarida
ya urembo
‘Mamaaa’ Pamella akaita kwa furaha na kukimbilia mama yake
mbaye naye alipogeuka na kumuona Pamella alisimama kwa furaha na kumlaki binti
yake. Wakakumbatiana kwa nguvu zote.
‘Pam…where have you been?’ mama yake akamuuliza akimtazama
kuanzia juu mpaka chini. pamella akamtazama tu mama yake na kutabasamu
‘hebu kaa chini kwanza…’ mama akamvutia kiti binti na kuketi
pamoja naye
‘amekuja saa ngapi’ Pamella akauliza
‘muda mrefu kidogo…. baba yako ana hasira sana wewe…you lied
to us Pam why?’ mama yake akamhoji
‘….baba yako alijua unaishi humu ndani....amekuja
hajakukuta…and dada wa kazi amefukuzwa sababu yako’ Mama yake hakumpa hata
nafasi ya kujitetea
‘It is a long story mama…. na…’ hakumalizia akageuka nyuma na
kumuona baba yake akiingia pale walipokuwa
‘Oooh Dad…’ Pamella akajikuta akinyanyuka na kumkimbilia baba
yake, akamkumbatia kwa furaha mno. Mzee Okello akaonekana kufurahi sana kumuona
Pamella binti pekee kati ya wanawe wanne wa kiume.
Mazungumzo yakaanza. Lawama, maonyo, maswali na kila aina ya
mawaidha ya mzazi kwa mwanawe yakaongelewa. Pamella akieleza sababu za kuhama
akificha ukweli kuhusu kuwa na mahusiano na Patrick Mazimbwe. Akaficha tena
kuhusu kujua alipo Jerry na akaeleweka na kupewa masharti ya kukaa uko aliko
kwa miezi miwili tu na angepaswa kurejea nyumbani pale.Kwa shingo upande
akakubaliana na wazazi wake.
Wakati akinyanyuka na kuagana na wazazi wake huku
akiwahakikishia alikuwa salama Pamella alisikia mama yake akimwambia baba yake
kwa sauti ya ukali huku akimbinya mkono kwa staili ya kumzuia asiseme alilotaka
kusema
‘Not now Daniel please!...’ aliisikia vema kauli hii lakini
hakuielewa. Akaaga na kuondoka akiwa na mtumishi mmoja ambaye aliambiwa aondoke
naye. kichwani alikuwa na maswali mengi mnoo kuhusiana na kauli ile.
8888888888888888888
Pamoja na furaha yote ya kuwa na Sindi Nalela mule ndani,
bado Jerry alionekana mara kadhaa akipoteza furaha yake na kuzubaa. Sindi
aliyekuwa ameketi kwenye kigoda akichambbua mchele alimtazama Jerry kila mara
na asimuelewe.
Mvuke uliotoka kwenye
sufuria lililokuwa kando yake juu ya jiko ndio uliomshtua Sindi na akajikuta
akiutua ungo na kuufunua mfuniko. maji yalikuwa yamechemka.
Akanyanyuka kivivu akiuweka ungo wa mchele kitandani na
kusimama, huku akiikaza khanga yake kiunoni. Akamatazama tena Jerry.
‘unawaza nini Jerry?’ akamzindua na Jerry akatabasamu tu
asijibu lolote.
‘si uniambie’ Sindi akakazania akiwa amesimama pale pale na
Jerry akatikisa kichwa kulia na kushoto kukataa
‘Niko poa tu….halafu hilo jiko lako linaongeza joto humu
ndani bwana’ akabadili maongezi na Sindi akaligundua hilo. Hakutaka kumsinikiza
amwambie hilo lililokuwa linamtatiza. Akachukua jiko lake na vitu vyake vingine
vya kupikia na kutoka kordoni.
Jerry alikuwa na msususiko moyoni. Alikuwa na hasira
zilizochanganyikana na kutoelewa hatima ya maisha yake ya kujifichaficha. tangu
amsikie Pamella akimuongelea Fiona, moyo wake ulishaanza kufikiria mengine
mengi tofauti na alivyokuwa akiwaza mwanzo. Angeishi vile mpaka lini?
Alishachoka kungoka kuambiwa mara hivi mara vile na watu aliwaajiri kufuatilia
suala lake.
Akakumbuka aliyoongea na Meddy nay eye Jerry kujiapiza
angejitokeza mbele ya familia yake ili lwalo na liwe kuliko huku kuishi kama
digidigi akiwakwepa watu asiowajua. Wakati akiwaza na kukata shauri kujitokeza
alikumbuka mchezo mchafu anaomchezea Sindi.
Moyo ukamuuma mno, alitamani sana kumwambia Sindi ukweli kuwa
yeye hakuwa masikini wala yatima kama alivyomuaminisha. Alikuwa akiipima imani
ya Sindi kama angempenda pamoja na hali ile ya umasikini. Ndio kwanza mapenzi
yao yalichanua na moyo wake ulishakubali kuwa na Sindi. Alijiuliza uongo ule angeliuendeleza
mpaka lini?
Akatulia tena na kuwaza zaidi, mikanganyiko ilikuwa mingi
kichwani mwake. Akasonya kwa sauti na kutoka kitandani pale alipokuwa
ameketi. Akasimama katikati ya chumba
chake akishusha pumzi kwa ghadhabu na kuipiga teke ndoo tupu iliyokuwa
imesahaulika pale karibu na kitanda. Ndoo ile ilipaa kidogo na kubamiza kiti
kilichokuwa na ndoo nyingine yenye maji ya kunywa. Mlio ukasikika mpaka kordoni
na Sindi akaingia pale ndani haraka.
‘Hey…kuna nini?’ akamuuliza Jerry akimshangaa
‘Leave me alone’ akamjibu akitoka mule ndani na kuishia zake.
Sindi akaduwaa kwanza. hakuwahi kumsikia Jerry akiongea kiingereza hata cha I
love you I miss you. Akakunja uso zaidi akitafuta kilichomtibua Jerry na
hakukiona. Muda mfupi tu walikuwa wamepakatana wakicheka. Sindi akashusha pumzi
ndefu kidogo akishindwa kumuelewa mwenzake. Laiti tu angelijuayaliyokuwa
kichwani mwa mwenzake ngelimuonea huruma.
8888888888888888888888
Nyanza Mugilagila kule kijijini shinyanga alikuwa na hekaheka
kubwa mno. Mpaka muda ule aikuwa hajaamini alichoambiwa na Alma kuwa Sindi
alikuwa Dar es Salaam. Alma hakumueleza ukweli zaidi kuwa Sindi alikuwa na
Jerry uko aliko. Aliogopa kumchanganya na asijue kuwa taarifa ile tu
aliyompatia ilishamchanganya mno Nyanza.
kichwa chake kiliwaza kuliko kawaida. Alitoka pale kitandani
na kulifuata boksi lililokuwa limehifadhiwa darini na kulitoa. akarudi nalo
kitandani akiikalia biblia iliyokuwa pale kitandani. Akasonya na kujiinua
kidogo, akiondoa ile biblia na kuitupilia kando. Mungu alisahaulika kwa muda!
Akalifungua lile boksi na kulimimina kitandani, akilikung’uta
kuhakikisha pesa zote zilzokuwa mule ndani ya boksi zilizondokea kitandani.
Akaanza kuzihesabu kwa pupa mpaka alipoziweka zote kiganjani na kupata idadi.
Macho yalimcheza cheza kama mtu aliyekuwambuka kitu.
Akaziacha zile pesa kitandani na kutoka mbio mpaka kwenye
kona moja ya chumba. Akalifuata panga na kuchimba chimba kwa tahadhari kisha
akatoa kibubu kilichokuwa kimezikwa hapo. Akakikung’uta na kurejea nacho
kitandani kwa kasi.
Akakifungua kwa kutumia lile panga na kutoa noti zilizokunjwa
kunjwa na kuziweka kitandani, akianza
tena kuzihesabu kwa kuziokota na kuzikunjua kisha kuzilaza kiganjani.
Alipohitimisha akaunganisha na zile alizokuwa nazo. Akatabasamu kwa huzuni. Alishapata
nauli ya kumleta Dar!
Akili yake ilishamuamrsha kuja jijini kumtafuta Sindi na
asijiulize wapi angempata, angeanzia wapi na kwa nani? hayo hakujiuliza wala
hakusumbuka kujipa muda wa kuuchambua uamuzi wake. Alishaamua kuja Dar na hata
kama mama yake angefufuka na kumzuia si ajabu asingemsikia!
Alfajiri ya siku iliyofuata Nyanza Festo Mugilagila akaondoka
kijijini kwao Mzimbuni. Akiwa amemuaga Alma na mdogo wake ambaye alikuwa shule
karibu na kijiji chao. Akaondoka akiwa na uso wenye furaha na matumaini,
matumaini makubwa ya kumuona Sindi Nalela, mwanamke aliyeuteka moyo wake na
kukimbia nao.
8888888888888888888888
Mitaa ya mbezi beach ilishatulia muda huu wa saa tano kasoro
usiku. Baa chache zilizokuwa bado ziko wazi eneo hilo zilijaa utulivu wa kutosha.
Jerry alikuwa akiendesha gari la Meddy
alilokuwa akitumia na kuliegesha hoteli ya New Afrika kila alipoelekea
kwa Sindi.
Aliliendesha akiifuata barabara ya vumbi kidogo yenye
changarawe iliyokuwa na utulivu wa aina yake. Akakata kona kadhaa na kulielekeza
gari moja kwa moja mbele ya geti kubwa lililokuwa limekumbatiwa na ukuta mrefu
wenye nyaya za ulinzi juu.
Mlinzi aliyekuwa zamu akatoka na kama mtu aliyemfahamu Jerry
akamruhusu kuingiza gari ndani kwa kumfungulia geti. Jerry akaingia na kuzima
gari. kisha kwa sekunde kadhaa akainamisha kichwa kwenye usukani kama mtu
aliyekuwa anawaza.
Akakata shauri na kuteremka, taratibu kwa mwendo wa
kujikokota akaufuata mlango mkubwa wa kuingilia ndani ya nyumba hiyo na akasita
kubisha hodi. Sekunde chache zikakatika mlangoni pale akiwa ametumbukiza mikono
mfukoni na kuinua kichwa chake juu kama mtu aliyeitazama dari, pumzi zikiyajaza
mashavu yake kama puto na kutoka taratibu.
Akageuka kama mtu aliyetaka kutoka lakini moyo wake ukasita
na akajikuta akiugeukia tena mlango na kuufungua. Kitasa kikatii na mlango
ukafunguka. Sebule ilikuwa kimya. Akaingia na kuurudishia mlango nyuma yake.
Huku akiangaza huku na kule. Kama mwenyeji ndani ya ile nyumba akaifuata kordo
iliyokuwa inampeleka kwenye mlango uliokuwa wazi nusu na taa yenye mwanga
ikiwaka.
Alitembea kwa tahadhari mpaka alipoufikia mpango na
kuchungulia ndani. Pamela alikuwa na simu sikioni kama kawaida akiwa ameibana
kwa bega lake akizunguka huku na kule. alikuwa akichagua nguo kabatini na
kuiweka kifuani kisha kujitazama kwenye kioo kama ilimpendeza. Nguo kadhaa
zilikuwa kitandani.
Yote hayo Jerry hakuyaona, aliuona mwili mzuri wa Pamella
aukiwa ndani ya gauni laini la kulalia lililomkaa vema na kuvutia. Aliduwaa
pale akili yake ikisambaa na kutawanyika.
Pamella akakata simu na kuirusha kitandani, akageuka taratibu
kama mtu aliyetaka kutoka mule chumbani na akagongana uso kwa uso na Jerry
Agapela. Hakumtarajia wala hakutarajia kumuona pale. Ujio ule ulimfanya
amtazame Jerry kwa mshangao wakati akizipiga hatua kumfuata. Wakakumbatiana
kimya kimya pasipo kusemeshana lolote. Wakatulia vle wakiwa wamefumba macho
kimya kimya…..
....... NYANZA HUYOOO ANAKUJA MJINI.....
sis kip it up
ReplyDelete