Wednesday, January 15, 2014

SINDI.....na LAURA PETTIE (53)

53

Mwanga wa jua ulizidi kupungua kadiri sekunde zilivyotengeneza dakika. Hatimaye giza likabisha hodi na kuleta utusitusi eneo kubwa la msitu ule waliokuwa wakiukatisha kwa msaada wa mwanga wa tochi moja na mbalamwezi iliyosafiri pamoja nao.


Ulikuwa ni usiku wenye hali ya ukimya uliokuja na kutoweka, uliovamiwa na kelele ndogondogo za ndege wa usiku na kutoweka huku ukitawaliwa zaidi na mlio wa nyasi kavu na hatua walizokuwa wakipiga binadamu hawa watatu waliokuwa katika safari iliyojaa mashaka.

Wanaume wale wawili walikuwa mbele, hatua mbili tatu mbele ya Sindi ambaye alishahisi kuchoka sasa, mimba yake ya miezi minne ilishaanza kumletea mahangaiko na masumbufu ya kutosha aliyolazimika kuyavumilia kwa hali na mali sembuse kule kutembea kulikoonekana kutokuwa na mwisho.

Akajikwaa, na kujikwaa kule kukamdondosha chini kama mzigo. Wale wanaume wakasimama na kumgeukia, wote wawili wakimtazama kwa macho ya kumtaka aharakishe kusimama na safari iendelee. Hakuna aliyejitolea hata msaada wa kwenda kumsaidia kunyanyuka, wote walimtumbulia macho vile alivyokuwa akiuma meno na kujitahidi kuyavumilia maumivu ya kuanguka kule. Safari ikaendelea huku akichechemea!

Pamoja na hali ya upepo iliyokuwepo bado Sindi alilowa jasho usoni, hofu aliyokuwa nayo ilipanda dakika hata dakika. Mkono wake uliokumbatia vitu vyake kifuani, uliishikilia pia ile rozari aliyopewa na Nadina wakati ule walipoagana.

Alitaka kusali, alitaka kuongea na Mungu lakini akili yake ilijaa hofu iliyomfanya akahamanike na asiweze hata kuiweka akili yake katika mpangilio wa kufanya alichotaka kufanya. Alibaki kuamini tu kuwa Mungu alikuwa anajua ni kwa kiasi gani alihitaji msaada wake.

Ghafla tu wale wanaume wawili wakasimama na kumgeukia. kule kusimama ghafla kukafanya moyo wa Sindi ukaribie kuacha kudunda! Alitoa macho pima! akayatoa zaidi huku akirudi nyuma hatua moja na uso wake kukunja ndita kadhaa…pua ilishindwa kufanya kazi ipasavyo na mdomo ukachukua kazi ya upumaji.

Yule mwanaume mwenye mwili mkubwa kupita mwenzake, aliyeongea na Tima kule mwanzoni mwa safari alipeleka mkono kiunoni na kuchomoa kisu toka katika ala yake. Macho ya Sindi yalifuatiza kila alichofanya kisha ghafla akapeleka macho yake kwa yule mwanaume mwingine aliyekuwa kijeba, akamtazama anavyochomoa kisu kidogo cha kukunja kilichokuwa mfuko wa nyuma na wote wakaanza kumfuata kwa mwendo wa kumnyatia.

Alitaka kupiga yowe la kuomba msaada lakini sauti ilimsaliti, akatamani kugeuka na kutimua mbio lakini miguu haikuwa hata na nguvu ya kugeuka nyuma sembuse kukimbia na kuokoa maisha yake.

Sindi akarudi kinyumenyume,mwili ukimtetemeka na vile vitu alivyokuwa ameshika mkononi vikimponyoka na kuanguka pasipo yeye kujua. Akagota kwenye mti na hapo hapo akapepesa macho huku na kule kana kwamba alitarajia kuona upenyo ambao ungelimsalimisha. hakuona kitu! Giza lilikuwa zito mno, vichaka na miti iliyoshikamana ilimtisha maradufu ya hawa watu waliokuwa mbele yake.

Wakamfikia!
Yule kijeba akampeleka mkono nyuma ya shingo ya Sindi na kumvuta kwa mbele nia yake ilikuwa kumtoa katika ule mti
‘Piga magoti’ akamuamrisha akimkandamiza chini na Sindi akatii ile bila kupinga. Machozi yaliyokuwa yanamporomoka kwa mtu mwenye roho ya utu asingestahimili kumtazama Sindi mara mbili.

‘Msiniue…naombeni msiniue’ Sindi akajikuta akirejewa na sauti na ombi lake la kwanza likawa kuusalimisha uhai wake. Meno yake yaligongana mithili ya mtu aliyekuwa anasikia baridi. mikono yake iliyokuwa juu kama mateka ilitetemeka katika namna ya kusikitisha sana

Wakati Sindi akilia na kuomboleza, akiombea uhai wake. Tima alikuwa chumbani kwake, akitembea toka kona moja mpaka nyingine ndani ya lile vali lake la kulalia. Mikono yake ilikuwa imefumbatana pamoja kama mtu anayesali. Alienda na kurudi huku akipiga ishara ya msalaba mara kadhaa, mwisho akaketi kitandani kwake na kujiinamia kam mtu anayesali.

Alimuombea Sindi, hakuwa na imani sana na wale watu waliotumwa na Adella nay eye kuongezea pesa ili wamtoroshe. Hakuwa na imani kama wangeyasamehe maisha ya Sindi. hakukuwa na njia nyingine ya kumsaidia Sindi na mtoto wake zaidi ya kujifanya alitaka auawe kabisa ili kuondoa matatizo. Kuuawa kule ndiko kungemtoa Sindi pale ndani lakini sasa moyo wake ulikosa amani kwa vile hakujua kama aliowatumia kumtorosha Sindi wangemsikiliza yeye au Adella.

Kule porini, Yule mwenye mwili mkubwa akakiweka kile kisu chake kirefu mdomoni pa sindi kama njia ya kumtaka anyamaze. Sindi akaitikia kwa kichwa akikimbiza mikono yake inayotetemeka mdomoni na kujizuia kutoa sauti na kule kutetemeka kukazidi zaidi.

Akainua macho juu na kuwatazama hawa watu wawili waliokuwa wakiongea lugha ambayo hakuielewa ni ya kabila gani. Ilikuwa kama vile walikuwa wakibishania kitu Fulani.
‘Muue tu… wewe unamsikiliza nani?.. Tima?’ yule mfupi alimhoji yule mrefu kwa Kiswahili sasa na kumfumbua akili Sindi. ile kauli ya kuuawa kwake ndio ilimfanya amshike yule mrefu miguu

‘Nihurumieni jamani… msiniue… sina kosa jamani…msiniue’ Sindi akaomboleza na yule mfupi akamvuta nywele na kumrudisha alipokuwa amepiga magoti, akampa ishara wa kukaa kimya na Sindi akaitikia kwa kichwa akirudia tena kujitahidikuufumba mdomo wake.
‘Lakini ametoa pesa za juu ili tumtunze ule pangoni’ yule mrefu aliongea akisita kutimiza agizo walilopewa na Adella
‘unamjua Adella vizuri?... hivi tukimfuata Tima kisha akaja kugundua huyu Malaya wake yuko hai unajua ataanza na mkeo kisha akumalize na wewe… ni bora tufanye kazi yetu tusibaki na deni na mtu… pesa za Tima mrudishie au mpotezee tu… ana nini yule… si Malaya tu kama huyu’ yule mfupi aliongea kwa jazba akionekana kuwa na haraka ya kutimiza aliloagizwa.

Kwa unyonge yule mrefu akamtazama Sindi ambaye sasa alishauachia mdomo na kuweka mikono hewani akiwasihi wasimuue kwa machozi na vitendo tu.
‘ile asidi za kuozesha maiti iko wapi?’ yule mrefu akamuuliza mfupi naye akaelekea kule walikokuwa wanaelekea mwanzo na kuchimba chini ya mti. akatoa kontena la lita tano likiwa na kitu kama maji ndani yake.

Akaja nalo haraka sana na kuliweka kando ya ule mti aliokuwa ameugotea Sindi.
‘Sali mama… sisis tumetumwa tu na tumelipwa tayari’ yule mfupi akamhimiza Sindi
‘Kaka zangu… naombeni jamani… nina kiumbe hai tumboni mwangu… sijamkosea kitu Adella… sija…’ akakatishwa na kipigo cha ubapa wa kisu mgongoni. Sindi akajikunja mgongo na kulia kwa maumivu
‘umeambiwa usali dada sio utueleze una nini na nini…’yule mrefu aliyemchapa kwa ubapa wa kisu kirefu alimtolea macho na kumuwekea ncha ya kile kisu shingoni chini ya sikio.

masikini hakuweza hata kusali, hakuweza hata kutamka neno lolote la kumsihi Mungu amuokoe. Aliishika ile rozari yake na kufumba macho huku machozi yakimtoka, mkono mwingine ulilishika tumbo lake. Akauma midomo yake na kufumba macho kwa nguvu zote.

‘kwanini tusimshughulikie kwanza?... kitu kizuri kama hiki?’ yule mfupi alitamka kwa sauti na kumfanya Sindi afungue macho ghafla na kumtazama akiwa amemtolea macho ya hofu zaidi. Yule mrefu akacheka kama namna ya kukubaliana naye

Mfupi akaweka kisu chini na kuanza kuhangaika na mkanda wa suruali yake wakati Sindi akilia kwa sauti na kuomba auawe tu bila kufanyiwa ukatili ule. Alipofungua zipu na kumshika Sindi, akapiga yowe baada ya Sindi kumng’ata mkono ule uliotangulia kumshika. Jambo lile likamuamshia hasira yule mfupi na akajikuta akimtandika ngumi Sindi kwa hasira mpaka pale yule mrefu alipomnasua mwenzake.

‘…unaleta umaaluni hapa… ngoja sasa tukuonyeshe kazi’ yule mfupi alioongea kwa jazba akiwa mikononi mwa mwenzake.
‘hakika …nakuwekea kwanza alama za kisu ndio naridhisha nafsi yangu…’ akajikung’uta toka mikononi mwa mwenzake na kumnyang’anya mwenzake kile kisu kirefu. Alikuwa amelala chini akitweta kwa maumivu lakini pia jicho lake kali lililotiririsha machozi lilimtazama yule mwanaume akimlaani kwa lugha zote. Mikono iliendelea kushikilia tumbo na rozari kwa nguvu zote

Akanyanyua kile kisu kirefu na kukielekeza juu tayari kwa kukitua katika mkono alioudhamiria. Sindi akafumba macho na kuuma tena midomo yake
‘Yesu!’ ndilo neno pekee alilomudu kutamka kabla ya kuuma midomo yake

Aaaarrrgh! sauti iliyoashiria maumivu makali ilipaa hewani na kumfanya Sindi afumbue macho haraka. Yule mwanaume aliyekuwa na kisu alikuwa amesimama kama mtu aliyegandishwa akiwa na mshale kifuani pake. Damu zilikuwa zimeruka kama maji yaliyotulia na kisha kutupiwa kipande cha jiwe. kile kisu kirefu kilimponyoka taratibu wakati akiwa bado ametoa macho na mikono yake kukimbilia kuushika ule mshale uliompiga kifuani.

Sindi akaweweseka sasa… akajivuta kando na kumtolea macho huyu mtu ambaye sasa alikuwa akisaidiwa na mwenzake ambaye woga aliokuwa nao pengine ulizidi ule uliokuwa ndani ya Sindi. Kifo huwa sherehe kinapokuwa kwa mwenzio!

Mwanaume mfupi akaenda chini kama mzigo na damu zikibubujika kiasi cha kutisha. Yule mrefu akaruka kwa hofu akiangaza huku na kule. akaokota kile kisu kirefu na kukitanguliza mbele asijue adui alikuwa upande gani. Akamfuata Sindi ambaye naye alirudi nyuma kwa kusota na matako. Alipomkaribia na kutaka kumshika  tu

Yowe la maumivuu likamtoka wakati akitanua kifua na kukitanguliza mbele kama mtu aliyepigwa ngumi kali ya mgongo. Sindi akamshuhudia na huyu akipiga magoti kwanza kisha kuanguka kufudifudi. mshale ulikuwa katikati ya mgongo wake. Sindi akaachama mdomo safari hii akihisi yu ndotoni.

Nguvu za kusimama hakuwa nazo, hata mkojo uliokuwa umemlowanisha hakuusikia. Alihisi baridi mpaka kwenye mifupa. Akakodoa macho kule alikosikia kama nyasi zikikanyagwa. mikono yote miwili ikashika rozari kwa bidii licha ya kutetemeka vibaya mno.

Mbwa mweusi mwenye macho makali akatangulia kutokezea akiwa na kamba shingoni. Sindi akaifuatiza ile kamba kwa macho akianzia pale shingoni mwa mbwa mpaka ule mkono uliokuwa umeikamata ile kamba.
Kwa hofu akakiinua kichwa na kumtazama yule aliyeishika kamba ya mbwa. Aliyatembeza macho yake mpaka usoni pa yule mtu ambaye giza lilimfanya asiione sura yake.

Jamaa akapiga hatua, na zile buti alizokuwa amevaa zikapiga ukelele uliomsisimua Sindi. Macho yake yalikuwa na ukubwa wa kutosha lakini bado aliona kama vile alihitaji kuyatoa zaidi ili aone zaidi ya pale. alipozidi kumkaribia, Sindi akasota kwa matako kurudi nyuma
‘usiniue… naomba usiniue… usiniue…’ ndiyo maneno pekee aliyomudu Sindi kwa muda ule. Akalia akiyarudia rudia na hatimaye akaweka mikono kichwani na kujikunyata akificha uso wake kana kwamba hakutaka kuona yule mtu angemuua na nini.

Ikawa Sivyo alivyowaza, Yule jamaa alimshika mkono na kumvuta kwa juu. Sindi akajiachia na kujaribu kusimama lakini miguu haikuwa na nguvu. Yule jamaa akatua kibobo chake kilichokuwa na mishale na upinde na kukiweka chini. Akamshika Sindi ili kunyanyua kwa mikono miwili na kisha kumuweka begani. Wakati Sindi akiwa amesimama upande yule jamaa akainama ili kuokota kibobo chake. wakati anainama akatazama kule alikolala yule aliyemtandika mshale wa mgongo. Hakumuona!

Akageuka kwa haraka na kuangaza mkono mwingine ukienda nyuma na kumkinga Sindi kwa hatari yoyote ambayo ingetokea. Kule alikotazama kwa haraka hakuona mtu  na yowe la Sindi na kubweka kwa mbwa wake kukamfanya ageukie kushoto kwake haraka sana. Akakutana uso kwa uso na yule jamaa akiwa anaonekana kulegea  na kuyumba.

Haraka akapeleka mkono kiunoni sehemu ya nyuma na kuchomoa bastola. kwa wepesi wa ajabu akaachia risasi moja iliyotua pajini mwa yule mwanaume mrefu. Akaenda chini kama kiroba.

Alipomtazama Sindi ndio akagundua yowe lile halikuwa yowe la hofu, kulikuwa na kisu kidogo kilichokuwa kimejikita begani mwa Sindi na damu zilikuwa zinambubujika.
jamaa akamuinamia haraka na kukichomoa kisu, akiharakisha kuvua koti alilokuwa amevaa na kuchana shati lake vipande. Alionekana kuijua huduma ya kwanza vizuri. Akamfunga Sindi na kuzuia damu kutoka zaidi kisha akamfunika na lile koti na kumbeba akiwa ameshapoteza fahamu ingawa hakuwa na uhakika kama angefika naye alikokuwa anaelekea akiwa hai.
888888888888888888888888888888

Nadina alikuwa amezubaa wakati mteja wake akimpapasa huku na kule. Akili yake haikuonekana kuwa pale kabisa wala hakuwa na ile bashasha ya kuhudumia wateja. Alizama mbali kimawazo na uso wake ulijaa huzuni.

Yule mteja akaachia kofi kali la shavuni na kumzindua Nadina
‘we’ vip?’ akamuuliza akimvuta kidhalilishaji
‘samahani… nina matatizo’ Nadina akajitetea akisugua shavu lake na machozi kumlenga
‘khaa! sikulipia dollar mia kuja kusikiliza matatizo yako… hata mimi nilikotoka nina matatizo yangu … hebu sogea hapa’ yule mwanaume alimkaripia akimvuta kwa nguvu na kumkandamiza kitandani. Nadina akafumba macho na kuruhusu machozi wakati mwanaume yule akihangaika naye bila ridhaa yake. Aliumia sana. Kazi yake haikujalisha alikuwa na hisia zipi. Donge kubwa lilimkaba kooni na akalimeza kwa bidii zote kiasi cha kuruhusu machozi yamtoke.

Hakuwa na furaha, hakuwa na amani wala hisia za kukutana kimwili na mtu, lakini ilimlazimu kufanya hivyo kwa manufaa ya Adella. Hasira yake ikachanganyikana na hasira ya kuondolewa kwa Sindi eneo lile. Alimchukia Adella, alimchukia kupitiliza na kwa hakika alikiri Adella alikuwa binadamua wa pili kumchukia namna ile baada ya  Fiona mwanamke anayedhani ni mama yake mzazi.

Akauma meno kwa uchungu wakati mteja yule akitumia nguvu nyingi kumuingilia bila kujali hali ya binti yule. Nadina akagundua wepesi wa maisha ya pale ulikuwa unaletwa na uwepo wa Sindi, angalau walifarijiana kwa madhila waliyokutana nayo na sasa Sindi alikuwa hayupo, alikuwa hajui aliko, alitaka kukuche upesi na amuulize Tima kuhusu Sindi.
888888888888888888888

Jerry Agapella anajipindua kitandani na kulala chali akiitazama dari. Aliiweka mikono yake yote miwili kisogoni pake wakati akionekana kuwaza na kuwazua. Alikunja shingo yake taratibu na kutazama kushoto kwake kulikokuwa na meza ndogo iliyokuwa na saa ya mezani. kwa msaada wa taa ndogo iliyokuwa kando ya saa, akasoma muda.

Saa nane na dakika ishirini na tatu!
katikati ya usiku wa manane. Hakuwa na usingizi hata wa kuzugia. Pamoja na pombe alizokuwa amekunywa akili yake ilikuwa imegoma kulewa. Akashusha pumzi ndefu kiasi cha kufanya kifua chake kipana kinyanyuke juu na kushuka chini.

Akatupa pembeni shuka alilokuwa ameliegesha mpaka kiunoni na kuketi kitako, miguu ikining’inia kueleka sakafuni. Ilikuwa imebaki wiki sasa na siku mbili tatu tu aifikie siku ya ndoa.
Akatulia kwanza kwa sekunde kadhaa kisha taratibu akanyanyuka na kupiga magoti huku vidole vya mikono vikikutana pamoja na viwiko vya mikono kugota juu ya godoro. Alitaka kusali!

Ilikuwa imepita muda tangu apige magoti vile na kuzungumza na Mungu. Yaliyokuwa mbele yake yalikuw amaji ya shingo sasa. Akayumba yumba kidogo kabla ya kutulia na kujishauri kipi cha kumwambia Mungu

‘… Mungu…nampenda Sindi Nalela…’ akatamka taratibu mwenyewe akihisi mpaka vinyweleo vinamsimama.
‘sijui alipo… sijui ana hali gani… sijui yu mzima ama yu mfu… lakini Mungu nataka kukuomba jambo moja tu… mlinde Sindi na mtoto wangu… mpe amani… mpe furaha… mpe kile ambacho mimi nimeshindwa kuwa… mpe mwanaume bora!...’ akanyamaza kwanza na kutulia. Nafsi ilimsuta, alikuwa namdanganya hata Mungu sasa. Si kweli kwamba alitaka Sindi awe na mwanaume mwingine zaidi yake

‘… hapana Mungu namtaka Sindi awe wangu… awe mke wangu…’ akaongea kwa uchungu na kisha kufumbua macho alishindwa kuendelea kusali. Shetani alikuwa amesimama nyuma yake akimzidi nguvu. akanyanyuka na kutembea kuelekea mbele kisha akarudi na kupiga magoti tena. safari hii hakufumba macho

‘… nataka kuwa mume bora… nimemkosea Sindi na nimekukosea wewe Mungu… nipe amani moyoni mwangu… haya maisha ya ndoa ninayotaka kuanza yawe ya amani na utulivu… niondolee huzuni na hali ya kukumbuka ya nyuma… nataka kuanza upya sasa pamoja na Pamela… Mungu unajua sikumtelekeza Sindi… sikumfukuza…’ akaacha kusali na kuweka mikono kichwani.

Akatulia tu akitazama mbele na asijielewe. Kuna kitu alikuwa anakihisi moyoni mwake, kuna hali alikuwa anaihisi moyoni mwake. Katika kitu hicho na hali hiyo kulikuwa na mtu aliyehisi alikuwa nyuma yake. Mtu huyo alikuwa Sindi Nalela. alihisi alikuwa karibu kumuona na kwamba alikuwa anaharakisha kuoa wakati Sindi alikuwa yu karibu kuja tena kwake!

Alipotulia vile aligundua hali ile ilikuwa ni majuto kwa yale aliyomfanyia Sindi. Alitaka kunyanyuka toka pale chini akiwa na uamuzi mmoja tu wa kuendelea na maisha mengine pasipo maumivu.
‘Sindi!’ akaliita jina hili kwa unyonge mkubwa, akaliita kwa mara ya mwisho na kujiapiza kuwa jua litakapochomoza siku inafuata angelianza maisha mapya bila majuto wala kumbukumbu ya Sindi Nalela! Alikata shauri.

Aliyemuokota Sindi ni nani?... Je Sindi yu hai?

ITAENDELEA….

2 comments:

  1. maskini sindi!!!! eeeh mungu sikiliza maombi yake umuokoe na kifo

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger