Wednesday, January 22, 2014

SINDI.... na LAURA PETTIE (54)

54

Miale ya jua la asubuhi ile ilipenya kwa kasi kupitia dirishani na kugonga barabara usoni pa Sindi Nalela. Alikunja uso kidogo na kuhangaika kufumbua macho  yake, na hata alipoyafumbua yalibaki katika udogo uliomzuia kuona vizuri kilichokuwa mbele yake. Aliyafumba tena na kutulia huku lile jua likimfanya akunje uso maradufu ya mwanzo, akaunyanyua mkono wake wa kushoto ili kujikinga na ule mwanga wa jua. Lahaula!


Akahisi maumivu makali yaliyomfanya aume meno kwa nguvu zote na kufinya uso zaidi. Maumivu yale yalimfanya ageuze shingo kwa taabu na kutazama eneo lililomletea yale maumivu. Alitweta!... sehemu ya bega lake ilikuwa imefungwa kwa kitambaa cheupe pakiwa na dalili zote za kuwekewa dawa aliyoanza kuhisi ilikuwa ikimletea hali ya maumivu kila sekunde iliyokatika tangu atoke usingizini.

Akajikakamua na kujiinua ili aketi kitako, akaweza. taratibu akaangaza mandhari ya lile eneo alilokuwemo. Akagundua kwa haraka kuwa alikuwa kwenye nyumba iliyojengwa kwa mbao, kuta za nyumba ile zilikuwa na michoro ya wanyama pamoja na maandishi ambayo kwa wakati ule hakuyaelewa hata chembe. Akayateremsha macho yake na kushuhudia magome ya miti, majani na mkusanyiko wa makopo ya yaliyoonekana kujaa vitu alivyohisi ni dawa. Akabeua macho yake katika namna ya kutoelewa yale yote yaliyokuwa mbele yake.

Alipotazama kando ya godoro alilokuwa amelalia aliona majani yaliyosagwa pamoja na unga unga uliomwagika hapo, na jibu likawa aliyemfunga lile eneo lenye jeraha aliitumia sehemu ile kutengenezea dawa aliyomuwekea. Sindi akashusha pumzi na kutulia, akili yake ikisafiri maili nyingi kuzisaka kumbukumbu za wapi alipokuwa kabla ya kufika hapa.

Akafumba macho na kufinya uso tena na kitu pekee kilichomgonga akilini ni picha ya mtu akimlenga na kisu na hapohapo kuhisi maumivu makali kisha kuona mtu aliyeshindwa kuitambua sura yake sababu ya giza akimuinamia na kumuhangaikia.

Akafumbua macho ghafla na kuangaza huku na kule. Alitaka kumuona mtu huyo! Alijua ni yeye ndiye aliyemuokoa toka mikononi mwa wale watu waliotaka kumuua kule msituni. hakuona mtu zaidi ya macho yake kugota kwenye mlango ulioonyesha uwepo wa chumba kingine ndani ya nyumba hiyo.

Akanyanyuka kwa tabu akiwa amelishikilia tumbo lake kwa mkono mmoja, ule mkono uliokuwa hauna jeraha na kusimama. Akavaa viatu vyake vilivyokuwa vimewekwa pembeni ya godoro. Akatembea taratibu na kuufuata mlango aliohisi ungemfikisha chumba kingine. Akajaribu kuusukuma na ukamshinda. Akaachana nao ana kuufuata mlango wa kutokea. Akajikwaa kwenye moja wa yakopo yaliyokuwa yamezaa chumbani humo na kumwaga mbegu zilizokuwemo humo ndani.

Ikabidi achuchumae hapo na kuanza kuzizoa  na kurudishia ndani ya kopo. Wakati akiendelea na zoezi lile akasikia mngurumo wa gari, ulimfanya aachane na lile kopo na kuufuata mlango wa kutokea nje.

Hakuona gari lolote lakini mngurumo uliendelea kusikika na kumpa hali ya udadisi. Akatoka nje kabisa na kuangaza huku na kule. Pori lilikuwa zito na hakukuwa na dalili ya kuwepo kwa nyumba nyingine eneo lile. Alihisi hofu na akajikuta akijikumbatia si tu kwa ubaridi aliokuwa nauhisi bali pia kwa woga wa kuwepo pale peke yake. Akatazama nyuma yake na kuhisi mngurumo ule ulitokea kule nyuma ya nyuma. Akatembea taratibu na kuzunguka nyuma ya nyumba lakini pia hakuona gari lolote. Akasimama hapo na kuangaza huku na kule akitega sikio pia na kujikumbatia zaidi. Jua lilipiga katikati ya miti lakini upepo uliokuwa ukivuma ulileta baridi ya kusisimua. Akiwa amesimama hapo akaona njia nyembamba iliyokuwa inaelekea katikati ya pori.

Sindi akaitazama tu, akijishauri cha kufanya. Alitaka kuifuata akiamini ingemfikisha kule alikokuwa akiusikia mngurumo lakini pia aliogopa kwa vile hakujua ilielekea uko alikodhani au lah!

Sekunde mbili tatu za kujishauri zikakatika na Sindi akapiga moyo konde na kuifuata ile njia. Kwanza ilimuingiza kwenye miti mingi mirefu iliyokuwa na nyuzinyuzi na kwa hakika hakuelewa miti ile ilikuwa miti gani. Akatembea kwa tahadhari mpaka alipoona bonde dogo lililoelekea sehemu tambarare iliyomilikiwa na bahari. Akaachama mdomo kwa mshangao.

Maji yalirudi nyuma na kusogea mbele katika namna ya kuvutia, mchanga uliozunguka lile eneo la tambarare ulikuwa mweupe, msafi wenye kuvutia machoni.  Akapiga hatua kadhaa na kulifikia lle bonde. Taratibu akaanza kushuka kwa tahadhari mpaka alipofika chini na kuikanyaga ardhi ya mchanga wa bahari.

Mita kadhaa upande wake wa kulia kulikuwa na landrover ya kizamani sana iliyokuwa imefunuliwa eneo la mbele kwa matengenezo, bodi la juu la landrover ile lilikuwa limeondolewa ma kuliacha katika staili mpya. Mwanaume mrefu aliyevalia kofia ya maarufu ya cowboy, alikuwa kifua wazi huku chini akiwa na suruali aina jeans nyeusi. Sindi alimtazama namna alivyokuwa ameliinamia gari lake akiendelea na matengenezo ya gari lake. Kwa haraka alishindwa kuelewa alikuwa mtu wa maji ya kunde au chotara.

Mbwa wa yule jamaa aliyekuwa amelala pembeni ya tairi akabweka na kusimama akitikisa mkia na yule jamaa akajikuta akiinua kichwa na kutazama nyuma, kule alikobwekea yule mbwa. akakutana uso kwa uso na Sindi Nalela ambaye hofu ilimvaa mara mbili baada ya yule mbwa kusimama.

Pengine alitarajia yule jamaa angelimfuata na kuzungumza naye, au kumjulia hali ama tu kujitambulisha lakini haikuwa hivyo. Jamaa alimpa ishara ya kutulia yuke mbwa wake na kisha kuendelea na alichokuwa anafanya. Sindi akaduwaa. Akilini aliwaza pengine hakuwa yule jamaa aliyemuokota usiku. Akawaza mengi kwa wakati mmoja akiwa amejikunyata vile vile kwa mtindo wa kujikumbatia. Yule jamaa akaingia ndani ya gari na kujaribu kitu alichokuwa anatengeneza. Akatoka tena na kurudi kuchokonoa gari lake kule alikofungua safari hii akiwa amelizima gari.

Upepo zaidi ukavuma na Sindi akahisi kidonda kikiuma zaidi. Yule jamaa kwa kujua hali ile ya hewa ilikuwa inamuumiza Sindi, akaingia garini tena na kutoka na jaketi ambalo alilifinyanga na kumrushia Sindi. Likatua mikononi mwa Sindi katika namna ya kushtukiza. taratibu akalivaa akiwa bado hamuelewi huyu jamaa.

Mawimbi ya bahari alipiga kwa nguvu na kulikuwa na dalili ya jua kuanza kupoteza ukali wake na kuruhusu mawimbi meusi yaanze kutawala anga.
Jamaa akafunga lile eneo alilofungua na kulibamiza kwa nguvu.
‘dans la voiture! (…ndani ya gari)’ akamuamrisha mbwa wake kwa lugha ya kifaransa akimuonyesha  ndani ya gari. Mbwa yule akaingia garini na Jamaa akaingia upande wake a kuwasha gari. Aliliendesha mpaka usawa wa Sindi na kusimamisha. Akageuka na kupeleka mkono siti ya nyuma, Akavuta kifurushi kidogo na kumrushia Sindi ambaye alikidaka kwa taabu pia.
‘je serai bientôt de retour (nitarudi sasa hivi)’ akamuaga Sindi na akimuonyesha ishara ya kuelekea kule kwenye kibanda. Sindi aliielewa ile ishara lakini maneno yalipita masikioni mwake kama lugha ya ajabu kwake. Akaendelea kuduwaa akilitazama lile landrover likitoa mngurumo na moshi wa kutosha kuelekea mbele. akatikisa kichwa asielewe angeelewanaje na binadamu huyu ambaye kwa mara ya kwanza alikuwa amemuona kwa ukaribu zaidi na kugundua alikuwa mtu mzima mwenye sharafa zenye mvi, macho makali na mzungu mwenye macho ya bluu bahari aliyepigwa jua kiasi cha weupe wake kupoteza nuru kabisa. Aliligundua hilo baada ya kuona nywele zenye rangi la blonde zilizofichwa na ile kofia ya cowboy. Alikuwa na mwili mkubwa uliojengeka haswa na kwa kiasi Fulani ulimtisha Sindi.

Sindi akairudisha akili yake katika kile kifurushi, akakifungua na harufu iliyotoka mule ndani ilimchefua mno. Akahisi kichefuchefu, kulikuwa na nyama iliyobanikwa ambayo alihisi ilikuwa inaelekea kuharibika. Harufu ile ikamkwaza Sindi vibaya mno na akajikuta akiinama na kutapika kwanza.
88888888888888888888888

Tima alishazunguka eneo lililokuwa na Pango akiingia na kutoka pasipo dalili zozote za kumuona Sindi. Akatembea kwa mwendo wa haraka na kukatiza pori akirudi kwa kasi lile eneo ambalo usiku uliopita kulikuwa na mapambano. Alilishuhudia dumu la asidi likiwa katikati ya eneo lile huku likiwa robo na mfuniko wake ukiwa kando. Tumbo lilimvurugika.

Akawaya waya eneo lile akitafuta chochote ambacho kingempa japo ahueni lakini hakuona cha maana zaidi ya muinuko mdogo uliokaa kama kaburi kabla ya kufikiria hata kulifukua akaiona rozari ya Sindi kando ya ule mwinuko. Tima akahisi nguvu zikimuishia akajikaza kwanza baada ya kusikia mngurumo wa gari. Akasimama wima na kushuhudia landrover ikikatiza porini kwa kudunda dunda na kufika eneo lile. Landrover ikataka kumpita tu lakini Tima akaipungia mkono na yule jmaa akasimamisha
‘Shikamoo’ Tima akasabahi uso wake ukiwa hauna  nuru hata chembe. Jamaa aliyesalimiwa

Jamaa hakujibu kitu, alimtazama Tima usoni pasipo kuongea lolote na Tima alipogundua aliyekuwa mbele yake ni mzungu akananaika zaidi na asijue aongee nini.
‘you see any girl around here?’ Tima akaunga unga unga sentensi yake akitarajia mzungu yule angemuelewa
‘qui êtes-vous(wewe ni nani?) yule jamaa akamuuliza Tima ambaye lugha iliyotamkwa ilimfanya ababaike kwanza. Alidhani hakumsikia vizuri yule mzungu. ukimya wa sekunde tatu ukapita kati yao.

Jamaa akamuonyesha kule kuliko na muinuko ambao tima aliuona na kujua kulikuwa na kitu kimezikwa pale. Tima akatoa macho sasa akiwa haamini alichoonyeshwa

‘The girl?!’ akauliza Tima akitaka uhakika wa alipo msichana aliyemuulizia, safari hii swali lake likienda sambamba na vitendo vya hapa na pale kuonyesha aliyekuwa anamuulizia ni msichana mwenye mimba na nywele zilizofungwa nyuma, jamaa akamuonyesha kilekile kikaburi kule nyuma yake. Tima akaduwaa na mzungu wa watu akapangua gia na kumtazama Tima kwa kituo!

Mzungu yule alikuwa amemuelewa Tima, lakini hakumuamini, alidhani tu kuwa pengine alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakimsaka yule binti aliyemuokoa jana usiku. Akaamua kumuonyesha kaburi alililolichimba yeye mwenyewe. Ni yeye ndiye aliyeikusanya miili ya watu aliowaua jana yake na kuichimbia eneo lile kabla ya kuimwagia asidi na kuizika pale.

Tima akatembea kama mlevi na kulifuata lile kaburi. Akaangukia hapo na kuanza kulia, akalia kwa uchungu na hali ya kutoamini. Akalia akiitazama ile rozari ya Sindi ambayo alikuwa amepewa na Nadina. Mpango wake ulikuwa umekwenda kombo, tofauti na alivyouombea, tofauti na alivyodhania. Tima akalia kwa uchungu pale kwenye lile kaburi, kichwani akiwaza namna ya kumwambia Nadina kuwa wazo alilotoa ili kumtorosha Sindi lilikuwa limemletea mauti …Sindi alikuwa ameuawa. Tima alihisi maumivu ambayo kwa wakati ule hakuweza kuyafananisha na kitu chochote!!

Wakati akihamanika na kuweweseka yule jamaa kwenye landrover alikuwa akimtazama kwenye kioo cha pembeni huku akiendesha gari lake taratibu na kutoweka kabisa eneo lile. Huyu mzungu ni nani?
8888888888888888888888
Pamella Okello akiwa na mama yake mkubwa Annie walikuwa kitandani wakitazama album ya picha za mapambo ya ukumbi ya aina mbalimbali. Walibishana hiki na kile wakicheka na kufurahi. Wakati wakendelea na ile kazi mama yake Pamell akafungua mlango na kuchungulia
‘Pam hebu njoo mara moja!’ akamuita
‘Mama bado hatujamaliza hii kazi’ Pamella akalalamika
‘Weka hiyo album chini nina uhakika hutajuta kuitikia huu wito… haya njoo’ mama yake akamhamsisha na kwa kujivuta Pamella akajiinua na kuanza kumfuata mama yake. Wakaikatiza kordo na kuzishuka ngazi zilizokuwa zinaelekea sebuleni

‘Oh my God!... Oh my God…Santinaaa.. Santina!’ Pamella aliharakia kushuka ngazi baada ya kumuona rafiki yake akiwa amesimama na mabegi yake mlangoni huku akitabasamu.
Marafiki hawa wakakumbatina kwa furaha kubwa, Santina akiukamata mkono wa kushoto wa Pamella na kuitazama ile pete
‘Mungu wangu Almasi!!!’ Santina akapiga yowe la mshangao lililoambatana na kelele za furaha, wakakumbatiana tena kwa nguvu zote.

Mama yake Pamella akamuita mtumishi wa kuondoa yale mabegi nay eye akabaki anawatazama mabinti hawa kabla ya kuachana nao na kuendelea na mambo yake.
‘unajua siamini!... it is just like siku ya harusi nitamuona Patrick na sio jerry’ Santina aliongea akicheka mara baada ya kuketi chini

‘It is Jerry dear… believe me!...Oh Mungu wangu nimefurahi jamani uwiiii… nilidhani ndio basi uliponiambia una mitihani chuoni’ Pamella aliongea akiweweseka kwa furaha
‘ningekosaje harusi ya rafiki yangu kipenzi wa miaka na miaka?... how?...no way out darling!’ Santina akamkumbatia tena Pamella kabla ya kutazamana na kucheka kwa furaha.

‘Meddy yuko wapi?’ Santina akauliza kwa shauku
‘Usiniambie baada ya safari ndefu hivi unayetaka kumuona ni Meddy’ Pamella akamtania mwenzake
‘Come on Pam!... yuko wapi?’ Santina alikuwa na shauku kubwa
‘Kwake!...’ Pamella akajibu akifinya midomo yake kujizuia kucheka na Santina akamtazmaa kwa udadisi kana kwamba alihisi Pamella alikuwa anamficha kitu

‘What?’ Santina akamuuliza na Pamella akaendelea kubana kicheko chake huku taratibu akitabasamu, akamzidishia mwenzake shauku ya kujua ni nini alitaka kusem muda ule
‘Stop it Pam… hebu niambie bwana’  Santina alimpiga pamella kijikofi kidogo kwenye paja na Pamella akaropoka

‘….Sijaona siku zangu mpaka leo’ Pamella akasema akitabasamu
‘ Paaaaaam!! Oh my God’ Santina akapiga yowe na hapo hapo akiruka kwa furaha na wote wakachekelea
‘two in one! ndoa na mtoto… Pam am happy for you darling! so so happy…’ Santina akamkumbatia pamella

‘Sijamwambia mtu...’ pamella akajihami
‘It is okay dear… you can tell him after ndoa… after all mtakuwa ndoani… ina muda gani?’ Santina akauliza akilitazmaa tumbo la Pamella
‘nadhani wiki nne… nimezidisha siku sita tu na nikaamua kucheck…’ Pamella akaongea kwa furaha zaidi.

‘okay..okay..okay we need to get outta here… tuna mengi ya kuongea … nataka uniambie kila kitu about Patrick alivyopokea hii breaking news…plus kila kitu kuhusu Meddy na kuhusua Clarita Gabson!’ Santina akafanya Pamella acheke zaidi

‘…that bitch!.... alinikuta kamili gado…wait let me grab my pochi… kuna kiota kizuri kimefunguliwa…. we are gonna die talking honey’ Pamella akanyanyuka na kutoka kuelekea chumbani kwake kuchukua mkoba.

Santina akabaki mwenyewe pale sebuleni akiangaza angaza na ghafla mlango ukafunguliwa na Mzee Okello akaingia. Pengine ilitarajiwa wawili hawa wangelitazama kwa furaha na kukumbatiana kwa upendo lakini ikawa tofauti. Mzee Okello alimtazama Santina kwa mshangao wa waziwazi na Santina akamtazama kwa jicho la upole tu na kubaki kimya.

Okello akatembea mpaka alipo Santina na kubabaika kidogo, akitaka kuongea na maneno kupotea.
‘Tulikubaliana nini Santina?’ Mzee Okello akauliza kwa sauti ya chini yenye msisitizo na wahaka wa kutosha.
‘Sidhani kama ni wakati muafaka wa kuongelea hili’ Santina akajibu akitazama mbele pasipo kumtazama Mzee okello
‘why are you doing this to me?’ Mzee akazidi kubabaika
‘Your secret is safe…’ Santina akajibu akitabasamu na hapo hapo akimgeukia mzee Okello na kupaza sauti ya juu, Alikuwa amewasikia Pamella na mama yake wakiongea kwenye kordo

‘Nimeshakaribia..asante sana’ akaushika mkono wa Mzee Okello kama mtu anaye salimiana naye na akumzindua Okello aliyekuwa amezubaa akimtazmaa Santina ambaye tayari alishazuga kusalimiana na Mzee okello na kuuachia mkono. Pamella akamshika Santina mkono na kumharakishia kutoka

‘Muwe waangalifu uko…’ Mama yake pamella akawaaga akiwapungia mkono huku Mzee Okello bado akiwa amewapa mgongo na akili ikionekana kutokuwa pale.
Rebecca, mama yake Pamella akamtazmaa mumewe
‘Nini?’ akamuuliza kwa udadisi na Mzee Okello akamtazmaa mkewe

‘sijawahi kuufurahia urafiki huu kati ya Santina na Pamella’ Mzee Okello akalalamika
‘Anakaribia kuolewa na kuwa na kwake bado tu una mchagulia marafiki?... hebu muache mtoto afurahie wiki ya harusi yake…usianze kelele zako tafadhali…Santina ni msichana anayejisheshimu mno…’ Rebecca akamjibu mumewe na kumuacha hapo sebuleni akiwa bado na ile hali ya kushangaa. Je ni siri gani hiyo inayotunzwa na Santina?
88888888888888888888888

Mwanga wa mbalamwezi uliongeza nuru na kufifisha utusitusi ulioletwa na giza lililokuwepo eneo lile la kibanda alichokuwemo Sindi. Alikuwa amelala kwenye kigodoro kile akiwa ameuma kipande cha nguo mdomoni, mishipa ya shingo ilikuwa imemtoka kwa kukakamaza shingo. Yule jamaa wa kizungu alikuwa anamnyunyuzia dawa katika kile kidonda cha kisu. Jasho lilikuwa linamtoka wakati akijikaza na kuvumilia ukali wa ile dawa. Alipomaliza kumuwekea akamuondolea kile kitambaa mdomoni na Sindi akapumua kwa nguvu akiwa mdomo wazi. Jamaa akachukua vitambaa safi na kumfunga upya. alipomaliza akalifunua tumbo la Sindi na kuchukua kitu kama tarumbeta ndogo. Akaiweka tumboni mwa Sindi na kusikilizia mapigo ya moyo.

Akamuonyesha Sindi alama ya dole gumba na Sindi akatabasamu kufurahia kujua kiumbe chake kilikuwa sawa. Jamaa akaondoa vifaa vyake na kuingia chumba kile alichotaka kuingia Sindi asubuhi. Akarudi na sahani yenye chakula na kumpatia Sindi.

Kwa kukitazama tu Sindi akahisi kuchefukwa. Kilikuwa kitu kama supu iliyokosa viungo na viaz viwili na nyama. Sindi akafumba macho na kujizuia kutapika. kisha taratibu akabana koo na kuchota kijiko kimoja. alipokipeleka mdomoni akajitutumua kumeza lakini chakula kile hakikufika tumboni kikarudi kwa nguvu na akakitapika.

Yule mzungu mzee akamtazma Sindi kwa mshangao kwa vile yeye alikuwa anakishambulia chakula chake kwa furaha kubwa. Sindi akataka kunyanyuka ili afute yale matapishi lakini jamaa akamzuia akimpa ishara kuwa atasafisha mwenyewe.

Wakati Sindi akiwa porini huku, Nadina alikuwa kwenye Casino pamoja na Meddy. Alikuwa amemaliza kumhudumia Meddy na alikuwa akivaa ili aondoke
‘hauna furaha kabisa Nadina’ Meddy akamsemesha
‘rafiki yangu ameondoka… nashindwa kuvumilia’ Nadina akaongea kiunyonge akimgeuzia mgongo Meddy ili amfunge zipu.

‘Yule uliyetaka nimuone siku ile?’ Meddy akauliza akipandisha zipu
‘Yeah!’ Nadina akajibu akivuta chini gauni lake fupi lililomkaa vyema
‘Ameenda wapi?’ Meddy akamuuliza huku akimtazama anavyoketi kitandani ili avae viatu
‘ni habari ndefu… nadhani  unahitaji kuisikia utakaporudi tena pengine utakuwa na msaada’ Nadina akaongea kwa huzuni


‘Jisikie huru Nadina…jisikie huru kabisa… nipo tayari kusaidia wakati wowote’ Meddy akampa moyo Nadina, akimhurumia sana. Nadina akasimama na kumtazma Meddy
‘Samahani naomba nikuache sasa hivi nahitaji kuonana na Tima… kuna kitu anataka kuniambia kuhusu huyo rafiki yangu’ Nadina akaongea akitabasamu kwa huzuni
‘amekuita?’ Meddy ahakutaka Nadina amuache haraka vile
‘Yeah!’ akajibu kiufupi
‘naomba uje kesho nikwambie kila kitu kuhusu mimi na Sindi’ akasema akilengwa na machozi na hapo hapo akigeuka na kutoka haraka sana.

Meddy akajitupa kitandani na kuitazama dari. Ghafla akatoa macho na sentensi ya Nadina ikajirudia kichwani mwake haraka sana
‘naomba uje kesho nikwambie kila kitu kuhusu mimi na Sindi’ sentensi hii ikajirudia kama ilivyo na Meddy akakurupuka na kutoka kitandani akiwa na boxer tu. Akafungua mlango na kuchungulia kordoni. Hakukuwa na mtu. Nadina alishatokomea.

Akarudi mule chumbani na kusimama katikati ya kile chumba kama bwege fulani
‘sindi…Sindi..Sindi’ akaliita hili jina, lilikuwa ni jina la kipekee mno kuikuta kwa watu wawili tofauti. Akatulia na taratibu akaanza kuvaa huku akijiapiza kuwa angewahi hiyo kesho ili aongee vizuri na Nadina kuhusu huyo Sindi.

Nadina alikatiza kordo iliyokuwa kimya mno na kukifuata  chumba cha Tima. Akagonga mara mbili na kuambulia ukimya kisha taratibu akakishika kitasa na kukinyonga huku akikisukumia mbele. Mlaango ukafunguka na Nadina akaingia na kuufunga.

Tima alikuwa amelala kitandani akamfuata huku akitabasamu na kuketi pemebni yake.
‘Da’Tima!...Da’ Tima… Timaa’ akaita kwa sauti ya chini akimtikisa. Tima hakuamka wala kujitikisa. Nadina akapeleka mkono kukishika kidevu cha Tima ili augeuzie uso wa Tima upande wake. Mdomo ulikuwa na mapovu mengi mno na macho yalikuwa wazi. Nadina akapiga yowe akianguka toka kitandani  na kutua chini, akasota kwa matako kurudi nyuma huku akihamanika.

Pumzi zilizoingia hazikulingana na zilizotoka, aliweweseka, akalia kwa wakaha na kumeza mate kwa juhudi. Dakika nzima ilimkatikia pale chini akiwa ajiwezi kwa mshtuko kisha taratibu akasimama akitetemeka na kuitazama meza iliyokuwa kando ya kitanda. Kulikuwa na bahasha yenye maandishi makubwa juu yaliyosomeka  NADINA. bahasha ile ilikuwa pembeni ya glasi yenye maji, kalamu, chupa iliyokuwa na vidonge ambavyo vingine vilikuwa vimetapakaa juu ya meza, kulikuwa na rozari ambayo Nadina aliitambua kuwa ni yake kwa kuiangalia tu. pembeni ya rozari kulikuwa na redio iliyokuwa inaporomosha wimbo wa Mbilia Bel uitwao Nadina.

Mikono ikatetemeka mno wakati akiishika ile rozari na kuitazama, moyo ulimuenda kasi mno, ilikuwa rozari aliyompatia Sindi siku ile waliyoagana. Akaharaki kuishika ile bahasha na kuifungua kulikuwa na barua ndani yake… huku machozi yakimlengalenga kiasi cha kutoona maandishi vema Nadina aliisoma….

Nadina,
Natangulia alipo Sindi
Haikuwa nia yangu kumletea mauti,
na kama nitaendelea kuishi huku nikiwa nimemuua Sindi sitakuwa na amani.
Angalia kabatini kuna pesa pamoja na  funguo za lile geti tulilotokea na Sindi.
ONDOKA USIKU HUU, ondoka Nadina na unyooshe na njia hiyo mpaka utakapopata msaada. kimbia kwa nguvu zote ulizonazo. Najua utakuwa umeumia sana lakini kaza moyo Nadina na uondoke eneo hili. Nisamehe kwa kumletea Sindi mauti, Nisamehe Nadina.
Usiketi hapa ukinililia, Usinililie, haitacukua muda mrefu watu kujua nimeshakufa. ondoka ukayaanze maisha yako upya.
Buriani.
Dada yako Tima.

Wakati anamaliza kuusoma ule ujumbe Nadina akaketi chini kama mzigo akitiririkwa na machozi, hata nguvu ya kusogeza mguu hakuwa nayo sembuse kukimbia kama alivyoamrishwa. Alikuwa amebaki mwenyewe, Alikuwa ameachwa mpweke kupita maelezo. Aliitazama maiti ya Tima pale kitandani na machozi yakazidi kumchuruzika. Akimbie? akiembeje? akimbilie wapi? wapi sasa? kwanini Tima? kwanini hakungoja kuzungumza naye? maswali yalipita kichwani mwa Nadina akiwa amelegea pale chini na ile barua.

Ule wimbo wa Mbilia Bel kwenye redio ulisikika vizuri sasa masikioni mwake

Nadina yoo Nadina yooo …..Nadina yoo Nadina yooo…. tuombe Mungu ….baba yoo atuhurumie dhambi zetu mama…. hata uso mwenye dhambi rudisha roho nyuma… hata we ni wa shetani jua yu aliyekuumba… tumsifu Mungu baba ee ee hata mara moja ujuma…

Nadina hakusimama, aliusikiliza ule wimbo, akalitazmaa lile kabati lililokuwa wazi. Aliziona zile funguo, aliziona zile pesa lakini nguvu ya kumuinua pale hakuwa nayo. Aliendelea kulia tu.


ITAENDELA….

1 comment:

  1. da!Petty natamani nikuhonge mdg wangu unisimulie story yote iishe fasta!

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger