Monday, January 6, 2014

SINDI....NA LAURA PETTIE (51)

51

Maneno yaliyokimbizana toka kichwani mwake yaliishia kusikojulikana, kinywa kilibaki wazi wakati macho yakiongezeka ukubwa kwa kadiri alivyoyatumbua, ile mikono aliyoifumbata kifuani ilitetemeka kiasi cha kuonekana dhahiri ikitingishika, Kwa wakati ule kichwa chake hakikufanya kazi sawa sawa, hakuna alililofikiri kwa muda ule, fuvu lilibaki tupu tu kama mtungi uliotoboka. Wahaka juu ya wahaka!


Patrick akasimama, naye akitanua macho na kuvuta pumzi kwa nguvu kidogo, kujipa nafasi ya kuzuia yale machozi yaliyomtoka kwa uchungu… akayafuta kwa mkono ule ule uliokuwa na bastola, akitumia ile sehemu ya mkono wa sweta alilokuwa amevaa.

Zile hatua chache alizopiga zilimrejeshea Pamella akili yake na akagundua maisha yake yalikuwa hatarini. Hakujipa nafasi nyingine ya kufikiri, aliugeukia mlango na kuhangaika na kitasa, akijaribu kulilenga tundu la ufunguo pasipo hata kukitazama kile kitasa alichokuwa anahangaika nacho.

Hakufikia hata theluthi ya lengo lake, Patrick alishamfikia na kumuondoa pale mlangoni kwa mtindo wa kumvuta na kumsukumia mbali

‘Mama yangu…Mungu wangu!’ yowe la hofu likamtoka, wakati akipepesuka na kuangukia kando ya meza iliyokuwa katikati ya sebule yake. Hofu ya kifo aliyokuwa nayo ikamrejea maradufu ya mwanzo wakati akimtazama Patrick aliyekuwa amesimama pale mlangoni akimtazama pamoja na ile bastola mkononi. Kwa sekunde zile hakuwa Patrick mchumba wake wa zamani… si tu kwa ile sura ya kikatili aliyokuwa nayo muda ule bali kwa kule kumshikia bastola, kwa Pamela kulimaanisha kifo!

‘Patrick Please…Patrick nisikilize’ aliita sasa machozi yakizivamia mboni za macho yake na taratibu akisota kurudi nyuma, aliyekuwa anamlilia akamuacha asote mpaka afike aendako na akagotea kwenye sofa na kutulia hapo akijikunyata na kutetemeka zaidi. Zilikuwa zimekatika dakika kadhaa na Patrick alikuwa hajaongea chochote. Hili lilimuwewesesha kupitiliza!

‘… haikuwa nadhiri  yangu Patrick’ akarai, akijaribu kukisia sababu ya ujio wa mtu huyu
‘Patrick nakuomba’ akarai tena na sijue ombi lake lilimaanisha nini. Aliyekuwa anamrai alikuwa ameinamisha kichwa chini tu pasipo kumsemesha wala kumfuata pale alipokuwa akitetemeka.

Ukimya ukapita kati yao hadi pale Patrick alipoamua kwa hiyari yake kuuvunja ule ukimya kwa swali lililotua kichwani mwa Pamella kama kipande cha tofali.
‘Unaolewa na Jerry.. si ndio?’ Patrick akauliza akinyoosha shingo yake na kuikakamaza kana kwamba swali lile aliliuliza akitarajia jibu tofauti. Pamella hakujibu alimtazama Patrick kwa huruma, uso ulishalowana machozi yaliyochanganyikana na jasho… kwa dakika zile tu alishachakaa. Hofu kitu kingine!

‘Nimekuuliza swali!’ Patrick akasisitiza kujibiwa na Pamella hakujua ajibu nini kunusuru maisha yake. Alitaka kukataa lakini akili yake ilimuonya kuwa Patrick alikuwa anaujua ukweli wote sasa… alitaka pia kukubali lakini akili yake ikamuonya pia kuwa angesambaratishwa palepale. Akabaki njia panda na asijue ni kiasi gani alizidi kuipandisha hasira ya Patrick Mazimbwe.

‘…Pamoja na yote niliyokufanyia Pamella… Pamoja na yote Pam… hivi hiki ndio umeamua kunilipa?... kuniacha kwa staili hii… namna hii… come on Pam… niambie ulihitaji nini ambacho sikuweza kukupatia?... I worked hard kama mtumwa nikidhi mahitaji yako…starehe zako… na kila kitu… ni hiki ndicho ninachostahili in return?’ Patrick aliongea kwa hasira akitembea toka pale mlangoni na kumkaribia Pamella na kisha kurudi mlangoni.

‘Patrick sivyo unavyowaza… sivyo Pat… sivyo dear’ akajitetea Pamella akiinua mikono juu katika namna ya kuomba huruma ya Patrick.
‘usiniite dear Pam…usicheze na akili yangu…’ akakemea Patrick
‘Namaanisha ninachoongea…’ Pamella akapata nguvu ya kujibu sasa baada ya Patrick kuweka nyuma ile bastola aliyokuwa nayo mkononi

‘kipi?...kuwa unampenda Jerry kuliko mimi…si ndio?’ Patrick akauliza kwa sauti ya juu ya kupayuka
‘No… ni chaguo la wazazi wangu Pat… why would I break up namna ile bila sababu…why?... sikuwa na jinsi’ akajitetea Pam machozi yakimtiririka na taratibu akijiinusha na kupiga magoti mbele ya Patrick… mikono yake ilinesa nesa hewani wakati akitafuta cha kujazia sentensi za utetezi wake na asikipate
‘So unaolewa na Jerry?’ swali likarudi palepale
‘Patrick I love you…I swear…I love you’ Pamella akaropoka akidhani pengine angeliweza kuibadili hali ile na ghafla tu akasikia risasi ikipiga hewani na kumfanya aangushe yowe lingine kali a kujikunyata. Alitetemeka kuliko mwanzo, akalia kuliko mwanzo

‘Uongo mwingine ukiongezeka… watakuta maiti mbili hapa… tukukose wote’ Patrick akaonya na sasa akimvunja nguvu zote Pamella aliyekuwa analia bila mpangilio. Akikiona kifo mbele yake. Patrick akaokota chupa ya pombe na kupiga funda kadhaa.

Ule mlio wa risasi ulisikika mpaka kwa mlinzi pale nje, alitoka mbio mpaka dirishani na kujaribu kuchungulia ndani. Lakini vioo vya madirisha havikumruhusu kuona ndani ispokuwa aliisikia sauti ya Patrick na vilio vya Pamella.

‘Hofu aliyokuwa nayo ilimfanya atoke kuomba msaada kwa walinzi wenzake. Dakika kumi tu zilitosha kukusanya watu kadhaa nje ya nyumba ya Pamella.
‘Usiniue Pat… nakuahidi it is me and you mpaka mwisho hata kama nitaolewa na Jerry kwa shinikizo la wazazi… moyo wangu uko kwako Pat’ Pamella alilia na akamlilia Patrick mno.

Majibiszano yao yakakatizwa na sauti za watu kule nje… Patrick akatanua pazia dirishani na kuona kijiumati kidogo cha watu. Akaiweka bastola yake kwenye midomo yake akimpa Pamella ishara ya kunyamaza kimya. Akatulia na kusikilizia zile kelele nje
‘Utafungua mlango na kutoa kichwa tu na uwaambie hakuna tatizo… kinyume na hapo nitaachia risasi ya kisogo’ Patrick akaongea kwa sauti ya amri akimuamrisha Pamela asimame pia.

Kwa woga akasimama na kujifuta machozi, akampita kwa hofu Patrick na kufungua mlango. Akasita kwanza na kuusikilizia mdomo wa bastola uliokuwa kisogoni mwake. Dakika zile alijihisi kufungiwa kipande cha bomu kisogoni, alihisi baridi mpaka kwenye mifupa!

Akafungua mlango nusu, akimeza mate kwa juhudi kubwa mno, akajilazimisha kutabasamu na kuongea mawili matatu aliyoona yangeridhisha nyoyo wale watu pale nje. Mazungumzoa yakachukua sekunde za kutosha kumfanya Patrick aikandamize ile bastola kisogoni. Pamella akafumba macho na kuuma meno, alikaribia kuachia yowe kubwa lakini onyo alilopewa lilimkumbusha utamu wa uhai. Akagugumia  chini kwa chini.

Baada ya watu wale kujiridhisha wakaondoka ingawa mlinzi wake alibaki amesimama akishangaa pengine akili yake ikijiuliza mara mbilimbili kile alichokisikia. Mlango ukafungwa na Pamella akageuka na kusimama wima kama mlingoti, kisogo kikielekea mlangoni sasa.

Ile harufu ya pombe kali ikamfikia vema na wakati Patrick alipomkaribia zaidi na kuitumia bastola yake kuupapasa uso wake, Pamella alipeleka uso pembeni. Ikawa kama amempa ruhusa na kuibusu shingo yake hali mkono ule usio na bastola ukivifuata vifungo vya vya blauzi ya Pamella.

Akafurukuta akitaka kumzuia na mdomo wa bastola ukahamia chini ya kidevu. nguvu zikamuishia, akaweweseka na machozi yakashika kasi sasa wakati Patrick alipoitatua ile blauzi ya Pamella kwa nguvu zote na kuvisambaratishia mbali vifungo vya blauzi ile.
Alijua kitakachofuata, alijua kama angepambana kuna hatari kubwa ingempata, akajaribu kutulia kwanza wakati Patrick alipokuwa amesimama mbele yake akimtazama tu.

‘Nakupenda Pamella… usiniache’ Patrick akasema kinyonge akimtazama Pamella usoni. Akajitutumua kutabasamu macho yake yakiitazama kwa kuibia bastola ile aliyoshika Patrick.
‘Niahidi hutaniacha’ akaomba Patrick akimsogelea tena Pamella na safari hii akiirudisha nyuma ile bastola aliyokuwa nayo
‘…siwezi kukuua Pam… nitaanzia wapi… nitaanzia wapi Pamella’ akaongea kwa sauti ya kilevi akiuondoa mkono uliokuwa na bastola kule nyuma na kumshika Pamella aliyeshtuka kidogo na kumkodolea macho mwenzake akiwa badi na ile hofu.

Wakatazamana, wakatazamana tena na tena na taratibu Patrick akamfuata Pamella kwa ukaribu zaidi, akambusu, akampapasa wakati Pamella akishindwa kutoa ushirikiano wowote ule kwa sekunde chache za mwanzo kisha naye taratibu akajikuta akiinua mikono na kutoa ushirikino. hakujua tu kuwa hili alilokubali kulifanya sasa lingeiwinda furaha yake baadaye! kwa wahati huu hakuwaza, hakujua wala kufikiria!
88888888888888888888888888

Adella alitembea kwa kasi wakati alipoufungua mlango wa ofisi yake na kukifuata kiti chake cha kazi huku nyuma Tima naye akiingia na kuubamiza mlango,
‘Kwanini?... ili iweje?...’ Tima aliuliza kwa ghadhabu wakati Adella akishika afaili moja na kuliacha kisha kushika lingine na kulibamiza mezani kwa hasira

‘Kwasababu ni ofisi yangu na Sindi ni mjakazi wangu… tangu lini unanipangia cha kufanya Tima… tangu lini? Adella akauliza kwa hasira akiwa amesimama kando ya meza yake
‘Tangu sasa Adella… this is too much… mimba yake ni kubwa sasa…mtoto ameshajiumba… unataka kuitoa mimba ya miezi minne kwa roho gani uliyonayo… kwanini wako hukumtoa akiwa tumboni’ Tima naye akahoji kwa hasira akiweka mbali heshima ya mtu na bosi wake.

‘Wow! this is serious… isn’t it?’ Adella alikunja uso wakati akiuliza hili swali
‘na zaidi… kama unadhani binti yule nakuletea hasara niko radhi nishike nafasi yake mpaka atakapojifungua… niko tayari kutumika tena kama ninavyokutumia ili niokoe maisha huyu kiumbe… kama ni pesa ndio inayokupa roho hii ya kinyama acha nika hudumie wateja wako kwa ajili ya Sindi’ Tima akongea kwa kujiamini

‘…huyu binti anakuhusu nini Tima?’
‘Hanihusu kitu na kumsaidia mtu si mpaka akuhusu… nimepitia magumu mengi lakini haijaniondolea utu wangu… never… never’ Tima alizidi kuwa mkali

‘Unapambana na mimi sio?’ Adella alikuwa bado hajaamini kama Tima alikuwa ameamua kulishupalia suala lile kwa nguvu zote
‘Sina cha kupoteza… kufa?.. nani ambaye hatakufa?... uniue?... tangu nilipopoteza mtoto wangu nilipotea naye…nilikufa naye… sina cha kupoteza Adella.. sina’ Tima alikuwa amesimama imara mno na Adella akamtazama na asiamini. Alikuwa amemtumikia kwa miaka mingi mno na pamoja na yote mabaya aliyomfanyia. Tima ndiyo alikuwa kama nguzo yake kwa nyakati kadhaa ingawa bado alikuwa mtumishi wake

‘unahitaji kupumzika Tima… niache peke yangu kwanza’ Adella akajibu na Tima akaondoka taratibu na kumuacha mwenyewe. Machozi yakalenga Adella, kwikwi moja kali ikamkaba kooni na akajikuta akiuma midomo yake na kubana pumzi kwa ndani kisha akshusha pumzi moja ya nguvu. Akakaza roho akaufuata mlango na kutoka!

Kule chumbani kwa Nadina na Sindi kulikuwa na maongezi kati yao. Sindi alikuwa analia wakati akisimulia alikoyapata yale madawa. Alikuwa amemuibia yule muhindi anayemchezea nachi. Alitaka kufa taratibu, alitaka kufa bila maumivu, hakukuwa na dawa yoyote ya kumfanya ajiue kama alivyotaka, njia pekee na rahisi aliiona ni ile.

Sindi aliongea mengi na kwa mara ya kwanza Nadina alibaki mdomo wazi wakati akimsikiliza Sindi huku naye akitiririkwa na machozi. Sindi alikuwa kimya siku zote lakini hakuacha kukumbuka kwao, kumkumbuka mama yake na familia yake hususani mdogo wake Peter.

 Sindi hakuacha kuumia kwa yale maisha aliyokuwa anaishi, hakuacha kuumia alipomkumbuka Jerry na ulaghai aliomfanyia, akaumia zaidi kuwa alikuwa na mimba ambayo aliamini alipewa na mtu ambaye hakuwahi kumpenda bali alikuwa akimtumia. Aliamini Jerry hakuwa na mapenzi na yeye na pengine alishasahau kama aliwahi kuwa na msichana kama yeye.

‘lakini bado unampenda Jerry’ Nadina akamuuliza kwa upole na Sindi akajilazimisha kutabasamu na kuitikia kwa kichwa
‘Sana…sana tu!’ akajibu akilishika tumbo lake. kuna mtu mmoja tu hakugonga kichwani mwake. Nyanzambe Mugilagila!

Wakati wakiongea na kufarijiana, mlango ukafunguliwa na Adella akaingia na kusimama karibu na mlango
‘Uwe tayari kesho jioni… kuna mtu atashughulikia suala lako… kama unataka kulia na kuomboleza… it is okay… baada ya wiki utarejea kazini… abortion njema’ akatamka kwa tabasamu kana kwamba alichokuwa anaongea kilikuwa kitu cha maana na faraja. Akatoka na kuwaacha mabinti hawa wamepigwa na butwaa kisha ghafla wakaangua kilio na kukumbatiana.

Kule kuponea chupuchupu kukiona kifo kulimfanya Sindi aione thamani ya mtoto wake na dhambi yake ya kutaka kumuondoa lakini hili la mtu mwingine kumuondolea mwanaye tumboni kwa nguvu na shurti lilikuwa zaidi ya maumivu. Aliutamani muujiza! kwa mara ya kwanza alishuka sakafuni na kupiga magoti akiinua mikono juu… Akamuita Mungu kwa sauti, akilia na akageuka kulia na kushoto akiitazama dari na kusihi Mungu amsikie japo katika hili tu.
8888888888888888888

Kulikucha! siku nyingine ya juma, siku mpya. Sebuleni kwa Okello, sehemu ya kunywea chai wanawake wawili walikuwa mezani wakistaftahika. Wakiongea na kucheka kuonyesha namna asubuhi ile ilivyokuwa njema kwao
‘… lakini hivi Dennis Mazimbwe alishatalikiana na mkewe?’ Annie, dada yake Rebecca akauliza wakati akitua kikombe cha chai kwenye kisosi chake
‘Waaapi!... Daniella amerudi mwaya… tena kwa kashda na tashtiti’ Rebecca akajibu akivuta midomo yake
‘usiniambie!...’ Annie alisukuma kikombe cha chai mbele kidogo
‘karudi… kajaa tele… na wiki aliyokuja… tuligongana supermarket… akaninyeshea mvua ya kejeli almanusura nimtie kofi’ Rebecca akaongea kwa hisia hasa

‘Hahahahaa umtie kofi mwenye mali… sijaona mzungu mvumilivu kama huyu… na yooote yale bado karejea tu?... na Dennis anasemaje?’ Annie akauliza akilaza shingo upande
‘Analo la kusema?... nimemuweka hapa’ vidole vinne toka kile cha mwisho vya mkono wa kulia vikagonga kiganja cha mkono wa kushoto. kumaanisha alipomuweka Dennis
‘Hafurukuti!’ akatamba Rebecca

‘Mmmmh… mwanasheria na mvi zake!’ Annie akashadadia na Rebecca akacheka
‘Yote kwa yote… huyu Mzee uliyemkubalia ndoa bila mapenzi toka moyoni  akijua hii misele yako tutachonga majeneza mangapi na  ya futi ngapi?’ Annie akaisema hofu yake

‘Atajulia wapi?... akili yake inawaza aninunulie gari gani… anipeleke wapi basi… ipo siku nitadai talaka yangu na nitaolewa na Dennis’ Rebecca akaonyesha dhamira yake
‘Na huyu Mzee akuache uende tu… na Dennis akupokee tu wakati Daniella yupo?’ Annie busara zilimuongoza kuliko mdogo wake

‘hawezi kunifanya kitu bwana… nasubiri kusikia wanatalikiana lini ili nijue naanzia wapi… siwezi ishi maisha ya kujifanyisha ninampenda mtu wakati nimependaye yupo hai tena karibu tu… it is time niishi maisha halisi’ Rebecca akaongea kwa kujiamini

‘Hayaa!... hakikisha kabla hujaomba talaka lile duka la jumla na lile duka la vifaa nya ujenzi unaandika jina la langu kabisa… hatutaki kugombea mirathi sie’ Annie akamfanya Rebecca acheke sana na wakati huo mlango ukafunguliwa na Pamella akaingia akiwa na mifuko ya shopping

‘Yaani umemrithi mama yako mpaka tabia za kipuuzi..’ Annie akamdaka Pamella aliyeanza kucheka kabla ya salamu
‘Shopping asubuhi asubuhi…’ Annie akajiinusha kumlaki Pamella. Akamsaidia baadhi ya mifuko na kuiweka mezani. Pamella akamuinamia mama yake na kumbusu shavuni kama salamu kisha  akaketi. Kulia kwake akiwa mama mkubwa na kushoto kwake akiwepo mama yake.

‘ gauni la kitchen party lipo tayari… naaa…’ akakatizwa na mama yake mkubwa
‘ya magauni na magagulo weka kando kwanza… mwanangu itabidi tuongee kidogo kuhusu uko unakotaka kwenda’ Annie akaanza
‘Aunt sidhani kama kuna jipya ambalo silijui… namjua Jerry ndani nje’ Pamella akataka kukwepa yale maongezi

‘Wapo waliowajua juu chini na ndoa zikawa chaaali!... mtoto mbishi wewe… hebu sikiza uko… usije ukatupa shida anayoileta mama’ako sasa hivi’ Annie akananga na Rebecca akaguna kuonyeshwa kutopendezwa na lile jiwe alilorushiwa

‘Unaguna nini?... una kipya kipi cha kumfunda mwanao ukajivunia kuwa mama… kakufuma na mwanaume mwingine kesho na keshokutwa mambo yakienda mrama tutasikia na yeye kafumwa na mwanaume mwingine… upuuuzi mtupu… weka masikio yako hapa… ujue ndoa sio kwenda kubadili mikao kitandani tu… sio kwenda kuamrisha watumishi ndani… sio kujivika mivyuma kidoleni mpaka mifupa inapata kutu… ni zaidi ya hayo na mumeo huyu… alivyo vile… ukileta ubishororo utageuka pazia la stoo ndani.. halifungiliwi wala halisogezwi… mwanaume anatunzwaa mwanangu’ Annie akaongea kwa kunesa nesa na Pamella akazungusha macho yake kuonyesha nusu aliyakubali na nusu aliyakataa

‘Siendi kuwa housegirl ma’ mkubwa!... na anajua nimetoka familia gani mimi’ Pamella akajitetea
‘Haya!... mwanaume wa kiafrika huyu… kijana kabisaa …umletee madoido ya kizungu… sawaaa… usijekuitisha tu kikao cha dharura kuomba silaha za maangamizi … nitakusuta na tarumbeta za bendi ya magereza’ Annie akawachekesha mtu na mama yake na maongezi mengine yakichukua nafasi. Pamella alidhani alikuwa amemjua Jerry vya kutosha bila kujua moyo wa mtu ni kiza kinene! Rebecca akasimama na kuwaambia alikuwa najiandaa kutoka!
88888888888888888888888

Dennis Mazimbwe alikuwa ofisini kwake pamoja na mzee Kristus Agapella. Walikuwa katikati ya maongezi yao ya kikazi na Mzee Agapella alikuwa anahitaji kubadili wosia wake tena. Alitaka kuliondoa jina la Fiona katika wosia ule na Dennis alikuwa anamshangaa.
‘ni maamuzi tu… huu utakuwa usia wa mwisho na sitaubadli tena’ Mzee Agapella akaweka msimamo wake ambao bado ulikuwa umemfanya Dennis amtumbulie macho Mteja wake na asiamini.
‘… wewe huyu huyu ndio unabadili usia?... unamuondoa Fiona?... hivi ni nini kimekuonyesha nilichokuwa nakiona?’ Dennis akauliza akitabasamu
‘wanawake watu wa ajabu sana Dennis…’ Agapella akatikisa kichwa
‘Fiona ni zaidi ya ajabu… yuko wapi kwanza?’ Dennis akauliza
‘Nilidhani unajua alipo… niliambiwa mko karibu sana’ akapiga kijembe akikumbuka maneno ya Mzee Okello aliyewahi kumwambia amchunge sana Dennis anaweza kuwa anatembea na mkewe

Dennis akacheka kwa sauti, akacheka sana kisha akamtazama Mzee Agapella
‘Fiona atakuwa mwanamke wa mwisho kuhatarisha maisha yangu sababu yake… huwa anakuja hapa kushawishi hiki na kile… ila ni muda sasa sijamuona… lakini sio kuwa na ukaribu… mimi na yeye hatuivi pamoja…’ Dennis akajitetea akianza kukusanya makabrasha yake kama mtu anayetaka kujiandaa kutoka

‘Sijui alipo… sijapokea simu yake hata moja… moyo wangu umekuwa na wingu zito juu yake.. nahisi nahitaji kukaa mbali naye kwa muda’ Agapella akaongea kwa masikitiko na wakati huo simu yake ikiita. Akaipokea na kuongea na mpigaji ambaye alikuwa Mzee Okello.

‘Okay, bwana sasa andaa kila kitu kuhusu wosia… nitakuja kesho jioni tuzungumze zaidi na kuhitimisha kila kitu… Mr. Okello yuko hapo kwenye maegesho… tunaelekea kwenye ule mkutano wa wawekezaji...’ akaongea Agapella akinyanyuka na kuweka sawa suruali yake kiunoni

‘Oh! kumbe ni leo… sawa basi… nadhani kabla ya wiki hii kuisha kila kitu kitakuwa kwenye mstari’ Dennis akaitikia na wakapeana mikono na Mzee Agapella akatoka. Dennis akabaki mwenyewe ofisini, dakika mbili tatu mlango ukafunguliwa na Daniella akaingia
‘That is my wife!’ Dennis akamlaki akisimama na kumbusu mkewe midomoni kabla ya kumuachia kiti chake na  yeye kujiegemeza kwenye meza

Wakatazamana tu huku Daniella akitabasamu kama mtu aliyetaka kusema kitu cha furaha
‘haya niambie…’ Dennis akamuhimiza
‘Nascom wamekubali kufanya kazi na mimi’ akaitoa hiyo taarifa iliyomfanya Dennis ataoe macho kwanza
‘Wow!...’ akabweua kwa furaha akimvuta mkewe na kumkumbatia kwa nguvu akamuachia kidogo na kumbusu mkewe kimahaba
‘…I’m proud of you babe’ Dennis akampamba Daniella na kumbusu tena pajini
‘But… umeahidi kuvunja uhusiano wako na Rebecca… na iwe hiyo Dennis… iwe hivyo darling… just you and me and our kids…’ Daniella akamdekea mumewe ambaye alitingisha kichwa kukubalinaa naye.

‘Nakupeleka lunch leo… kila kitu juu yangu’ Daniella akamwambia mumewe naye akainua mikono juu kama mateka. Akitoka pale kwenye meza na kulifuata koti lake.
‘Natumaini itakuwa mwanasheria wa Nascom  bi. Daniella Mazimbwe…’ Dennis akatania na kumfanya Daniella acheke kwa nguvu
‘… nadhani walitarajia kukutana na muafrika mwenzao...nilipotokezea mbele yao it was like… Huh?! are you bi. Mazimbwe?’ Daniella akaongea akicheka

Furaja ilikuwa imerejea maishani mwao, ndoa ilianza tena kuimarika .
Wakati wanandoa hawa wakiongea hili na lile Rebecca Okello alikuwa akiegesha gari lake  mbele ya jengo lile la ofisi ya Dennis. Alikuwa pale kumchukua Dennis kwa ajili ya chakula cha mchana kama alivyozoea kuja kumchukua kila alipojisikia.
888888888888888888888888

Fiona Agapela alikuwa akijipamba mbele ya dressing table. alihangaika na wanja, akauweka shika chini na kushika lipstick akauweka chini na kuokopa sponji ya kusawazishia poda… akaipitisha usoni mpaka aliporidhika na ule mwonekano.

Wakati alipojitazama tena akagundua kucha zake za mkononi zilikuwa zimebabuka rangi na hazikuvutia. akavuta droo ya dressing table na kutafuta pamba. Akapekua pekua mpaka alipoiona pamba lakini pia akavutika kuona kimkebe kizuri cha kuvutia kilichokuwa mule ndani ya droo.

Akataka kukipuuuzia lakini akajikuta tu akikichukua huku akitabasamu na kukifungua. Akakumbana na mkufu mzuri wenye kidani cha almasi. Kwanza aliduwaa nao mkononi kabla ya kukurupuka kuugeuza geuza kama mtu anayeuchunguza. Akatoka mbio mpaka kwenye sanduku lake. Akalifungua na kutoa mkebe mkubwa uliohifadhiwa chini ya sanduku na kuufungua. Akamwagia kitandani vitu vyote vilivyokuwa ndani humo.

akachakura kwa kupangua hiki na kile na hatimaye akaupata mkufu wake uliofanana vile vile na huu alioutoa kwenye dressing table ya rafiki yake iloma. akalinganisha, mikufu ilifanana kila kitu mpaka mkebe wa kutunzia. Akazubaa kwanza akili yake ikirudi nyuma miaka kadhaa… Mzee Agapella alipomletea zawadi ya mkufu huu siku ya kuzaliwa kwake.

Fiona akakunja uso, akili ilimletea maswali na majibu yasiyooana hata chembe. Rafiki yake alikuwa si mtu wa kuvaa vidani vya gharama kama hivi. hisia zilizomjia ghafla kichwani zilimfanya atunduwae, jazba nazo zikipanda sekunde hata sekunde
‘Iloma?!’ akajiuliza, akajiuliza kwa sauti kubwa akishangaa pia

ITAENDELA….
Mimba ya Sindi itakuwaje?... Dennis kule ofisini itakuwaje… Iloma na Fiona itakuwaje?
Usikose kurudi hapa hapa!...Tuko katikati ya starehe karibu tukielekea ukingoni


1 comment:

  1. tatizo unachelewa sana laura kurudi huku kwenye hadithi majani tunakaa week mbili hadi tatu jamani

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger