Tuesday, August 13, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (35)

35


Fiona Agapella alimeza mate kwa juhudi zote wakati akijaribu kujiweka sawa kumpokea Mzee Okello. Macho yake yalicheza kulia na kushoto katika namna ya kutafuta utulivu wa nafsi. Akameza tena mate kwa juhudi kiasi cha kufanya koo lake lididimie ndani kwa nguvu kidogo. Alihamanika!


Mzee Okello akamfikia Fiona na kuachia tabasamu lilienda sambamba na salamu ya mkono. Fiona akaupokea mkono wa Mzee Okello akijitahidi kutotetemeka kabisa lakini hofu na wahaka aliokuwa nao vilijionyesha usoni pake na kupotea.
‘Umekuja kumuona Mr. Dennis?…vipi yupo?’ Mzee Okello akamuuliza Fiona maswali mawili mazito ambayo kwa wakati ule jibu la haraka halikuibuka kichwani mwa Fiona.

‘Nilikuwa natokea uko juu… Nikaona nipite kumtaarifu hali ya Kristus’ Fiona akajibu akionyesha ngazi zilizokuwa zikielekea juu na Mzee Okello akakunja uso kama mtu aliyekosa kuelewa alichoambiwa. Uko juu alikoonyesha Fiona kulikuwa na ujenzi mdogo unaoendelea na hakuna mantiki ya Fiona kutokea uko juu na hapo hapo akili yake ikachukuliwa na suala la hali ya Kristus.

‘Kwani Mzee anaumwa?’ akauliza kwa sauti iliyowafikia vema Rebecca na Dennis ambao kwa wakati huo walikuwa wakihangaika kuvaa na kujiweka sawa.
‘Alipata matatizo ya kiafya asubuhi ya leo…mmmh…uko hospitali na mmm…he’ll be okay’ Fiona alibabaika waziwazi kiasi cha kumfanya Mzee Okello amtazame kwa mshangao wa chinichini.
‘Okay!...i see yuko hospitali gani?’ Mzee Okello akauliza na swali likawa gumu kwa Fiona kwa vile hakujua Jerry alimpeleka hospitali gani baba yake. Akababaika tena na Mzee Okello akaona anambana kwa maswali ambayo alikuwa anashindwa kuyajibu kwa uhuru.

‘So yupo…?’ Mzee Okello akauliza akiunyooshea mlango wa ofisi ya Dennis.
‘sidhani maana naona mlango umefungwa’ Fiona akajibu akijaribu kukishika kitasa na kukinyonga. Mlango ukafunguka!

Butwaa la ghafla likamvaa Fiona na akajiona mjinga zaidi mbele ya Mzee Okello ambaye sasa alishindwa kabisa kumuelewa Fiona. Akatabasamu na kumuonyesha ishara ya kutangulia kuingia. Fiona akaingia kizobazoba akiwa bado hajaelewa ni nini kilikuwa kinamtokea. Butwaa la pili likampiga alipomuona Dennis akiwa mbele ya laptop yake akiendelea na kazi na sasa aliinua uso wake na kuwatazama wageni wake kwa tabasamu.

‘Oh! karibuni…’ akainuka na kutangulia kushikana mikono na Mzee Okello huku Fiona akionekana kuangaza angaza na kuihoji akili yake kama ilikuwa sawa. alikuwa amemuona Dennis na Rebecca. aliwaona kwa macho yake, imekuwaje? alikuwa anaota?

‘Ms. Agapella!’ Dennis akamshtua Fiona aliyekuwa kama mtu aliyepotelea mawazoni ghafla. Fiona akazinduka na kumpa mkono Dennis hali akijaribu kutabasamu. Dennis akaongea mawili matatu na Mzee Okello kuhusu masuala ya kisheria huku Mzee okello akiomba muda na siku ya kuonana naye kwa shida zake.

‘Nimeona gari la mkeo wakati naingia getini…nadhani atakuwa around’ Fiona akaingilia maongezi akimtazama Dennis usoni na kutaka kuona mshtuko atakaoupata. Alitaka kujihakikishia kuwa alichokiona hakikuwa mazingaombwe. Dennis akashtuka sambamba na Mzee Okello mwenyewe. Fioba akahisi ushindi!

‘Mke wangu?’ Mzee Okello akamuuliza Fiona akiwa amekunja uso kiudadisi
‘Yeah…nilidhani labda amekuja kumuona Mr. Dennis… au may be alikuwa na shughuli zingine’ Fiona akaongea huku akimdadisi Dennis ambaye alimkunjia uso ghafla na kisha kumgeukia Mzee Okello

‘Hajafika hapa…’ akakanusha na ghafla akashtuka ‘ oh…au atakuwa duka la vipodozi uko nyuma’ akajitahidi kurudisha hali sawa lakini Fiona alimkaba
‘uko nyuma si wana parking yao…’ akamhoji Dennis

‘Kama kumejaa watu huwa wanaegesha magari yao huku mbele…’ Dennis akajibu na akiona wazi nia ya Fiona kukazania maelezo yale
‘Ooh!...i see hebu ngoja nimpigie nimuulize yuko wapi…ningependa kujumuika naye ….you know us women…tukifanya shopping pamoja …it is all about kipi bora kipi original…’ Fiona aliiinamia pochi yake na kuanza kutafuta simu wakati Mzee Okello akishindwa kuyaelewa mazungumzo ya hawa watu wawili.

‘Zunguka tu hapo nyuma…unaweza kumkuta’ Dennis akashauri akihofia simu kuita na kusikika wakati Rebecca akiwa anamalizia kupitia dirisha la chumba cha stoo ndogo iliyokuwa ofisini umo. Fiona akatabasamu na kupuuza ushauri wa Dennis. Akazitafuta namba za simu za Rebecca na kuzipiga. Simu iliita na ikapokelewa
‘Yes!’ Rebecca akapokea
‘Uko wapi?’ Fiona akauliza na Rebecca akajibu haraka tu
‘Niko duka la vipodozi huku nyuma… kuna nini?’ Rebecca akauliza wakati huo akitembea toka kule nyuma alikokuwa huku akijiweka sawa.

‘Okay!...fine…’ Fiona akakata simu na kuduwaa
‘Go join her… mkateketeze pesa zetu… women and shopping huwezi kuwatenganishaMzee okello akamsemesha Fiona na Dennis akiunga mkono na kuwatania wanawake. Fiona akaaga na kuondoka.
Wanaume wakabaki na maongezi yao kisha Mzee Okello akaaga pia.

Huku nyuma Dennis akashusha pumzi na kwenda stoo ambako mafaili yaliyokuwa yameliziba dirisha yalikuwa yametapakaa ovyo sakafuni. Akaanza upya kuyapanga huku akitikisa kichwa. Skafu ndogo iliyokuwa mikononi mwa Rebecca ilikuwa imebaki sakafuni. akaiokota na kuinusa huku akitabasamu na kushusha pumzi nyingine ndefu.
‘Rebecca!...i love you’ akatamka polepole akifumba macho na kuipeleka ile skafu puani. Alihisi mapenzi yake kwa mwanamke huyu yalikuwa yanaelekea kumuingiza hatarini.
88888888888888888888888

Muziki wa taarabu ulikuwa unasikika toka chumba kimoja wapo katika nyumba aliyopanga Sindi Nalela. Alikuwa Mzee Yusuph na kundi lake la Jahazi na huyo aliyekuwa akiusikiliza huo wimbo hakuuacha upite hivi hivi, aliimba sambamba naye kwa madoido yote wakati akiunga mboga yake jikoni. Alikuwa Jamila!

Mpangaji aliyekuwa anapita kordoni alipita kwanza kisha taratibu akarudi kinyume na kusimama mlangoni kwa Jamila ambaye alipomuona huyu mpangaji alilala ubavu na kuifikia redio iliyokuwa pembeni tu na kupunguza sauti.
‘Subalkheir Chemwali’ alimsabahi Jamila
‘Alkheir mgonjwa vipi?’ Jamilaa akauliza akifunika sufuria na kumgeukia mpangaji huyu ambaye alijikaribisha mpaka kitandani.

‘Mahututi garagara mauti….tunamsalia mtume tu!’ akajibu mpangaji akiutandua ushungi wake na kuubwagia mapajani
‘Kwani haongei kabisa?’ Jamilla akauliza akitoa macho
‘kakata na kauli nakwambia…ingekuwa vijijini kule tungesema keshakufa…wamemvisha mijimashine puani nasikia ndio anapumulia’ mpangaji yule mwanamke mwenye umri wa makamo akaelezea hali ya mgonjwa wake lakini ghafla kama mtu aliyekumbuka kitu akatoa macho pah!

‘Daada! kama duniani wawili wawili basi huyu niliyemuona ni pacha utozi kwa unyayo’ akajitanua kishambenga akianza stori yake
‘Nani huyo?’ Jamilla anaye shingo ikamsimama
‘Yaani nimemuona mtu kama Jerry…yaani Jerry mtupu…’
‘Umemuona wapi?’ Jamilla akasotesha matako kidogo akisogea mbele kana kwamba hakuwa anamsikia vizuri yule  mpangaji

‘Uko hospitali dada….yaani Jerry kabisaa ila sio kwa mavazi haya anayovaa wala si kwa huu umaskini ninaomuona nao….alikuwa na msichana kama wanafanana hivi…yaani jamani huyo kama akimuona Jerry atamkimbia wallah…ni mzimu wake kwa kule kufanana’ Mpangaji akajieleza mwenyewe na Jamilla akacheka kwanza.

‘Basi uliyoona wewe kuna siku nami niliyaona shosti… Kidogo nigongwe na gari kwa kushangaa mpaka nikahisi naingiwa na wehu….ila ndio hivyo mkewe anakataa kuwa si yeye…labda wanafanana…nikaguna tu nikanyamaza ila kama na wewe umeona basi shoga itakuwa ni mapacha hawajuani au ndio mtu mmoja anatucheza shere’ Jamilla akaongea akinesanesa na akitoka pale kigodani na kukaa chini kabisa

‘Kheee! makubwa dada!...mmmh ndio ukute ni mashushushu hawa watu….sie tunadhani ni wenzetu kumbe wapo kazini ohooo….kuna mama f’lani alikuwa anapenda kukaa posta pale karibu na ilipokuwa shule ya sekondari Forodhani…alikuwa kibonge flani kama mwehu hivi… tukijua mwehu tu siku alikuja kuzolewa pale na mapolisi wana mibunduki mirefu unaambiwa aligeuka mzima ghafla….’ Mpangaji stori ilipamba moto

‘Usinambie wewe…’ jamilla alishika tama
‘Ndio tukaja kujua kumbe alikuwa shushushu toka Malawi… mpaka leo yaani hawa vichaa nikiwaona huwa siamini wote wana matatizo ya akili….sasa ndio huyu mwenzetu ukute labda kaolewa na usalama wa taifa hajijui au anajua ila ndio yuko kazini’ Yule mpangaji akafanya Jamilla akanyanyuke ghafla

‘Hebu ngoja…’ akatoka na dakika moja tu akarudi na Sindi akiwa kamshika mkono. Wakamuweka chini. Wakimweleza yote waliyoyajua na Sindi akabaki mdomo wazi
‘Jerry???’ akauliza akiwa ahamini
‘humjui hata dada wa kufikia upo tu hivi leo akisema amemaliza kazi yake na akaondoka asikuage utaanzaje kumtafuta?’ Yule mpangaji akamuuliza swali la msingi sana

‘anatoka anarudi usiku anaenda wapi?....kazini kwake hupajui…eti anajenga nyumba…anajenga wapi?.... usala wa taifa huyu wenyewe tunaita mashushushu dada….uko kijijini ukute alikuja kupeleleza tu’ Jamilla akaongea kwa hisia hasa

‘Kijijini alikuja ameumia sana…ilikuwa tusingemuokota angekufa kwa kweli’ Sindi alijibu woga ukionekana kumtawala isivyo kawaida.

‘Wana mbinu hawa Sindi…. wapelelezi! wanaweza hata kuzaa na wewe akaishi na wewe akimaliza kazi anasepa zake… hapo ulipo una mimba tayari utazaa hapo na ataishia na mtoto siku moja unabaki kinywa wazi…’ Yule mpangaji alipigilia msumari wa hofu moyoni mwa Sindi ambaye sasa alikuwa ameshikilia kifua chake akisikiliza huku na huku.

‘Kama bado hata miezi miwili bado kaitoe shosti…. unamwambia imetoka bahati mbaya kisha unasepa zako…bora kuondoka bila kitu kuliko uachwe na mzigo wa kulea mtoto usiyejua asili yake… fanya ya kufanya urudi kijijini kwenu ukatulie na Nyanza wako… atakusamehe tu…. mwenyewe nimeogopa hapa mpaka basi’ Jamilla alitoa ushauri, akaongea kwa marefu na mapana akimuacha Sindi njia panda!
88888888888888888888888

Saa moja jioni, Mzee Agapella alikuwa wodini, hali ikiwa imetengamaa kiasi Fulani, Jerry alikuwa amesimama kando yake akimtazama baba yake kwa huzuni iliyochanganyikana na hali ya kukataa kile alichokuwa ameambiwa na baba yake.
‘I can’t marry Pamella…baba please!... na sidhani kama ni mahali sahihi kuongelea hili’ Jerry aliongea kwa kurai

‘Najua…lakini nahisi nahitaji kuona harusi yako…nahitaji kuona naondoka nikiwa nimekuacha kwenye familia…’ Mzee agapella akaongea kwa huruma
‘Baba huendi popote…. unaumwa na unatibiwa na utapona… stop this naondoka…naondoka…we still need you…I’ll marry for love na sio sababu nyingine’ Jerry alijitetea, akitaka baba yake amuelewe
‘What is wrong with Pamella?... amekuwa rafiki yako miaka… unamjua na tunaijua familia yake…baba yake amekubali kila kitu…’ Mzee akajaribu kushwishi zaidi
‘Baba!...how could you do that?....unafinalize makubaliano ya ndoa bila kunishirikisha?...’ Jerry alihisi kubanwa

‘It is for the best son!’ Mzee     Agapela akajiinusha kidogo kwa taabu akisaidiwa na kijana wake. Wakati Jerry akitaka kumpinga zaidi mlango wa chumba alicholazwa ukafunguliwa na Mzee Okello akaingia. Jerry akalazimika kukata malumbano na kutoka.

Wazee hawa wakasabahiana, wakazungumza hiki na kile na mwisho Mzee Okello akazungumza kitu kilichomuacha Mzee Agapella mdomo wazi.
‘…kuwa makini na Dennis’
‘Dennis Mazimbwe’ Mzee Agapela akauliza na Mzee Okello akaitikia kwa kichwa akionyesha wazi hakuwa anatania
‘Kwanini?...ni mwanasheria wangu’  Mzee Agapela alihisi ubaridi Fulani mwilini
‘Kuna kitu kinaendelea kati yake na mkeo Fiona…just chunguza tu….nahisi kuna kitu kati yao…maka si mahusiano basi ni dirty deals..si unazijua’ Mzee Okello alaiongea taratibu akitaka mzee mwenzake amuelewe na hakumuelewa!

‘Dennis!!....What I know hawa watu wawili hawaelewani kabisa!...what is going on?’ Mzee Agapella akaonyesha kushtuka sana kiasi cha kuhema kwa nguvu kila sekunde.
‘Relax!.... ufanye uchunguzi….wanawake si viumbe vya kuwaamini… Fiona anaweza kuwa anakusaliti…chunguza tu!’

Mzee Agapela akahisi kule kuhema kunamletea maumivu yale ya kichomi cha moyo. Akahema tena kwa nguvu na kumtia hofu Mzee Okello ambaye alimuuuliza kulikoni. Hali ikazidi kuwa mbaya na Mzee Okello akatoka kumuita daktari haraka.


……KARIBU TENA….TUBURUDIKE HAPAHAPA!

1 comment:

  1. mh! kizungumkuti! kweli babu jinga inama ufikiri.mali yako inaliwa

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger