Sunday, August 11, 2013

SINDI.....NA LAURA PETTIE (34)

34

Jua la saa nne asubuhi lilikuwa kali kiasi cha kufanya waliokuwa juani kukunja nyuso zao na  wengine kutafuta vivuli. Pilika pilika za hapa na pale zilishaanza na vurumai za jumatatu zilishika kasi kila kona. Sindi alikuwa uani akifua nguo zake na za Jerry.

Kulikuwa na ukimya mkubwa uani hapo kutokana na wapangaji wengi kutokuwepo asubuhi hiyo. Akiwa ameketi kwenye stuli yake aliendelea kufua taratibu  shati alilokuwa nalo mkononi huku akiimba wimbo alioutoa kwa sauti ya miguno tu na kutikisa kichwa.


Ukimya uliokuwepo ukatoweka mara baada ya Jamilla kuingia pale uani akitokea getini.
‘Kuko kimyaaa…. umebaki mwenyewe kama mwanga’ akamtania Sindi
‘ndio napenda pakiwa hivi… mtu unapata hata nafasi ya kuwaza kwa amani’ akaijibu Sindi akikamua lile shati na kulitia katika beseni lililokuwa na maji pembeni ya ndoo aliyokuwa anafulia. Wakati akijiandaa kuokota nguo nyingine, Jamilla akamsemesha

‘Nimekutana na yule kaka muuza mitumba hapo gengeni yuko na mwenzake…nadhani anakuja huku’ Jamilla akaongea akitabasamu na akijua wazi Sindi angefanya nini. Alichotarajia ndio kilichotokea. Sindi alisimama na kukunja uso wake
‘Akija mwambie sipo’ akazungumza huku akitoka pale alipokuwa amesimama na kuanza kuelekea ndani. Jamilla akacheka!

‘si umsikilize tu jamani….sasa utamkimbia mpaka lini na wewe?...’ Jamilla akataka kumzuia mlangoni
‘Aka!...nimsikilize wa kazi gani…bwana akija mwambie sipo’ Sindi akazama ndani mwake na alipoufunga mlango tu akaona vivuli vya watu kwenye pazia lililokuwa limeshushwa dirishani pake. Geti likasikika likifunguliwa na Sindi akatulia akisikiliza

‘Muite basi…’ Sakala alimbembeleza Jamilla ambaye alikuwa akicheka tu
‘Mwanaume huchoki kha!....hayupo leo ametoka kidogo’ jamilla akajibu na uso wake ukimfikishia ujumbe Sakala kuwa alichokiongea kilikuwa si kweli.
‘Mbona mnanifanyia hivi jamani eeh….muite basi hata nimsalimie tu… najua yupo ndani…mwambie hata aongee tu nisikie sauti yake’ Sakala alibembeleza na kumfanya Nyanza aliyekuwa kando yake acheke kichinichini.

Jamilla akaingia ndani na kumfuata Sindi chumbani kwake.
‘Toka japo uwasalimie…yuko na binamu yake leo’ Jamilla akabembeleza na Sindi akabetua mabega yake kukataa. Jamilla akatoka kurudisha ujumbe wake
‘Dah! mwambie hii zawadi yake kama hataipenda aitupe tu…’ Sakala akamkabidhi Jamilla kifurushi kilichokuwa kwenye mfuko mweusi wa plastiki. Jamilla akaupokea na wakaagana.

Sakala na Nyanza wakaondoka na kupita tena karibu na dirisha la Sindi ambaye alivitazama vivuli vyao na kutabasamu. Jamilla akafungua mlango na kuingia tena akimtupia Sindi kile kifurushi.
‘Sitaki..’ Akakikwepa kile kifurushi na kikaangukia kitandani. Jamilla akamfuata pale kitandani na kuketi kando yake. Akikichukua kile kifurushi na kukifungua,. Blauzi na sketi vikadondokea mapajani mwake. Akanyanyua moja baada ya nyingine na kuridhika nguo zilikuwa nzuri mno.

‘Unahongwa unakimbia…wakati wenzio hata tambara bovu la kudekia hatujawahi kupewa’ Jamilla akamnanga
‘Mi’ siko hivyo’ Sindi akajibu akinyanyuka
‘Kalaghabao!...we jitie unafanya kazi za hisani…mapenzi ya siku hizi haya…miaka kumi ijayo tutaanza kundikiana risiti za huduma kitandani…’ Jamilla akatania akinyanyuka na kujiandaa kujaribisha zile nguo.

Sindi akacheka huku akimsaidia Jamila kurekebisha blauzi aliyokuwa naijaribisha. Sindi hakujua tu kuwa kama angelitoka pale nje angekutana na mtu anayemtafuta, mtu anayemfanya na yeye asitamani kurudi kijijini kwa wakati ule. Mtu mwenyewe alikuwa Nyanza Festo Mugilagila! na Nyanza naye hakujua binamu yake alikuwa akimfukuzia mwanamke wa maisha yake na yeye ndiyebaliyemsindikiza! kweli Jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza!
8888888888888888888888888

Nyumbani kwa Patrick Mazimbwe, Clarita Gabson alikuwa na Patrick walikuwa mezani wakistaftahi. Clarita alikuwa bado ndani ya mavazi ya kulalia huku Patrick akiwa ndani ya mavazi yaliyoashiria alikuwa na safari baada ya kifungua kinywa. Clarita alichukua Jam ya matunda na kuifungua, akachukua kisu na kuanza kupaka Jam katika mkate uliokuwa kwenye sahani yake.

‘Ulikosa vitu vingi sana jana… hivi kwanini hupendi kujumuika kwenye sherehe za watu?’ Clarita alimuuliza Patrick aliyekuwa na kikombe mdomoni.
‘Sipendi sehemu zenye umati’ Patrick akajibu baada ya kutua kikombe na kuanza kukata yai lililokuwa kwenye sahani yake kwa kisu. Akakichoma kipande alichokata kwa uma na kukipeleka mdomoni.

‘I hope ungekuwepo ungemfunika Jerry… He was a show stopper jana… all eyes on him… ule wakati wa kukata keki yam zee wake he stood there…mic mkononi… akaanza kuimba wimbo wa happy birthday kwa mzee wake… it was like uwiiii…steve wonder wa bongo…yaani…’ Clarita akakatizwa na Patrick
‘Enough!’ Patrick alisema kwa jazba kidogo kiasi cha kumshangaza Clarita

Patrick akashusha pumzi na kumkazia macho Clarita ambaye naye alikuwa akimtazama katika namna ya kutomuelewa
‘It has been Jerry this….Jerry that tangu uliporudi jana usiku…. I’m interested kujua Jerry alifanya nini aliimba nini or whatever….’ Patrick aliongea taratibu lakini sauti yake iliashiria hasira ndani yake.

‘Kuna ubaya gani mimi kumzungumzia Jerry?...unamchukia?....humpendi? au nini?’ Clarita naye akauliza akiwa bado hajamuelewa Patrick.
Swali lake halikujibiwa, Patrick aliacha kula ghafla na kusukumia sahani mbele. Akachukua kitambaa cha kufutia midomo na kufuta pembe za midomo yake kabla ya kunyanyuka na kutoka eneo lile.

‘Patrick!’ Clarita akamuita kwa mshangao naye akiacha kula na kumkimbilia nyuma Patrick ambaye alishaokota briefcase yake iliyokuwa kwenye kochi na kuufuata mlango
‘What is wrong now?’ Clarita akamuwahi na kumuuliza
‘Nimesikia vya kutosha kuhusu Jerry… next time una lolote la kusema kuhusu Jerry jua sina interest ya kusikia habari zake’ akahitimisha msimamo wake na kutoka bila kugeuka nyuma.

Clarita Gabson akatikisa kichwa na kwa mbali akihisi alikosea kuonyeha hisia zake wazi kwa mpenzi wake. Hata ingekuwa ni yeye ndiye anayeambiwa kuhusu msichana mwingine kuwa bora zaidi yake lazima angeumia.

Clarita Gabson hakujua tu kuwa Patrick Mazimbwe na Jerry Agapella walikuwa na msuguano kuhusiana na Pamella Okello! Patrick alikuwa na kinyongo na Jerry, baada ya kumfumania na Pamella wakibusiana kwenye kochi usiku ule.

 Patrick aligundua Pamella alikuwa anampenda mno Jerry kuliko yeye. Hili lilimuuma sana na taratibu akajikuta akiugeuza moyo wake kwa Clarita Gabson msichana aliyemfahamu kwa kipindi kirefu wakiwa marafiki.

Akaanzisha uhusiano naye akiwa bado masomoni na mpaka amerejea Patrick alijikuta akimtambulisha Clarita kwa kaka yake Dennis Mazimbwe sio kwa vile alikuwa na mpango wa kumuoa Clarita ila Dennis aliwakuta pabaya katika mkao ulioashiria wao kuwa na mahusiano.

Ili kulinda heshima yake akajikuta akimtambulisha Clarita huku moyoni mwake akijua wazi penzi lake la dhati lilikuwa limenasa kwa Pamella Okello. Patrick Mazimbwe alikuwa njia panda sasa asijue ni namna gani ajikwamue toka mikononi mwa Clarita na ni namna gani aushinde moyo wa Pamella ambaye alijua wazi uko kwa Jerry. Hakujua tu kuwa wanawake wote hawa wawili mioyo yao ilikuwa kwa huyohuyo Jerry Agapella!
888888888888888888

Ngo ngo ngo ngo ngo!.... mlango uligongwa kwa mara ya pili na Jerry akakipindua kichwa chake upande mwingine huku akikunja uso kwa nguvu zote na kuuma meno kwa maumivu ya shingo na kichwa aliyokuwa anayasikia. Ule mlio wa hodi ndio uliomtoa usingizini muda huu wa saa sita mchana. Alikuwa amelala kupitiliza sababu ya pombe alizokuwa amekunywa usiku uliopita. Aliamka na kuketi kitako huku akijinyoosha na kupiga mwayo mrefu ulioenda sambamba na kujinyoosha tena.

Mgongaji akagonga tena na tena na kumfanya Jerry asonye kichinichini na kujivuta kuufuata ukingo wa kitanda. akateremsha miguu na kuvaa sendozi za kiume zilizokuwa hapo chini ya kitanda
‘Yes! nakuja’ akajibu akipiga tena mwayo na kusimama, akatembea kivivu mno kuufuata mlango. akiwa na bukta tu akaufungua mlango na kutoa kichwa tu nje. Jenifa alikuwa amesimama mlangoni.

‘Vaa utoke kuna matatizo huku’ Jenifa akamwambia akimuonyesha mlango wa chumba cha kulala cha wazazi wao. Jerry akakunja uso na kumtazama Jenifa kama mtu ambaye hakusikia alichoambiwa
‘we’ njoo bwana!’ Jenifa akasisitiza
‘Kwani kuna nini uko?’ Jerry akauliza akionyesha kutokuwa hata na haraka ya kuwahi uko alikotakiwa kuwahi
‘Sio utani Jerry….we vaa utoke uje’ Jenifa akaonyesha kukereka na Jerry akafunga mlango wake. dakika moja mbelle Jerry akatoka na akiwa anamalizia kuvaa tshirt yake. Wakaufuata mlango wa chumbani kwa wazazi wao na kutega sikio.

Ugomvi mkubwa ulikuwa unaendelea
‘siwezi kuionea wivu maiti mimi…. na usinilinganishe na maiti ya mkeo… unanielewa?’ Fiona alikuwa anaongea kwa jazba na kwa sauti ya juu mno huku mumewe Mzee Agapella sauti yake ikiwa ya chini isiyosikika vizuri. Jerry na Jenifa wakatazamana kwa mshangao!

Mabishano yakazidi na mara mlango ukafunguliwa na na Fiona akatoka kwa kasi kiasi kwamba hakujipa hata nafasi ya kuwatazama Jerry na Jenifa waiobaki wameduwaa pale mlangoni. Baba yao akatoka akiwa anachechemea kwa mkongojo wake. akimfuata Fiona kwa kasi.
‘Fiona sikiliza kwanza…. Fiona!...Fiona wait…Fiona!’ Mzee Agapella alimuita mkewe ambaye aliziteremsha ngazi kwa kasi akielekea sebuleni. Mzee wa watu naye akaanza kuteremsha ngazi kwa shida. Jerry akamuwahi baba yake na kumsaidia kushuka zile ngazi mpaka sebuleni. Fiona alikuwa amesimama katikati ya sebule akihema na machozi yakimtoka. Mikono yake ilikuwa na kazi na kupangua machozi yake na hayakukoma!

Mzee Agapela alipofika pale alipo Fiona alikuwa anahema kwa taabu kidogo. akatoka kuongea, akataka kutamka maneno mengi yaliyojipanga kichwani mwake lakini sauti yake ilimsaliti, nguvu ya kuongea ilimsaliti…midomo ikawayawaya kwanza na Fiona naye akimtazama kwa hasira.
‘Nisikilize Sophia…no I mean Fiona…’ akamudu kuongea na alichoongea kikazusha zogo upya

‘Unaniita Sophia?....mimi ni Sophia?.....Yaani sasa na mimi ni maiti si ndio?....kama bado unamtaka si ufe ili umfuate ukakae naye kwa amani’ Fiona akajibu kwa dhihaka lakini dhihaka yake ikakatwa na MzeeAgapella aliyejiinamia akiwa ameshikilia upande wa kushoto wa moyo wake.

Kama mtu anayesikia maumivu makali, Mzee Agapella akaishia nguvu na kuanza kutetereka akirudi chini taratibu. Jenifa akapinga ukunga, na Jerry akahisi kuchanganyikiwa wakati Fiona akiachama mdomo wake na kutoa macho kwa hofu.

‘Kristus…Krist…babe…babe…’ Fiona akamkimbilia mumewe na kuanza kumtikisa wakati Jerry akikimbilia nje kuomba msaada. Jerry aliporejea alimtoa Fiona kwa baba yake kwa kumvuta na kumtupia kando kiasi cha kumfanya Fiona adondokee kwenye sofa lililokuwa kando hapo.

Jerry na baadhi ya wafanyakazi wakamuondoa Mzee na kumkimbiza kwenye gari, Jenifa aakakipakata kichwa cha baba yake na Jerry akaondoa gari kuelekea hospitali. Fiona alibaki nje ya nyumba yake akiwa haamini kilichotokea. Moyo ulimsuta kwa kiasi Fulani kwa maneno makali aliyoongea na tukio lililotokea. Akajilumu kwa hilo na kurudi ndani kutafakari upya.

Badala ya kujenga alikuwa anazidi kuharibu mipango yake! Akawaza pale kochini alipokuwa amejiinamia kinyonge na ghafla jina la mkombozi wake likapita kichwani. Dennis Mazimbwe! akalitamka kwa hamasa ya kuanza mpango mpya na hamasa hiyo ikamuondoa pale sofani haraka sana, akaelekea chumbani kujiandaa kwa safari ya kwenda kumuona Dennis!
88888888888888888888888

‘Unahitaji kuongea na Patrick…. na unihakikishie umeongea naye Dennis!’ Rebecca aliongea kwa sauti ya juu akiwa mbele ya meza ya kazi ya Dennis, ofisini kwa mwanasheria huyu.

‘Patrick Patrick Patrick…..it is Patrick popote tunapokutana…hivi hakuna kingine cha mimi na wewe kuzungumza zaidi ya suala la Patrick?’ Dennis aliuliza kwa ghadhabu akimtazama Rebecca na asimuelewe

‘Na kama si suala la Patrick unadhani ningepoteza muda wangu kuja kujibishana na wewe hapa?....unadhani sina shughuli za maana za kufanya?.... talk to your brother Dennis…. amempigia binti yangu simu na nimewasikia wakiongea kama wapenzi… mdogo wako anatoka na binti yangu….mkanye na umuase aachane na Pamella for good’ Rebecca alikuja juu zaidi ya Dennis

Pumzi ndefu zikamtoka dennis alishachoka kusikia hili suala sasa. Sio tu kwamba lilimnyima raha bali pia hakuliamini kama Rebecca alivyotaka aliamini. akatoka pale kwenye kiti chake na kumfuata Rebecca pale alipokuwa amesimama. Akajiegemeza kwenye meza, miguu yake ikipishana na mikono yake ikizama mfukoni.

‘Patrick ni mtu mzima….he is a gentleman mwenye shughuli zake na utashi wake… sidhani kama anaweza kufanya ujinga wa kitoto wa kuwa na mabinti wawili kwa wakati mmoja…I know my brother yuko faithful kwa Clarita Gabson….sasa unapozungumza kana kwamba ni player f’lani….Becca sikuelewi’ Dennis aliongea taratibu na akivua mpaka miwani yake na kuiweka mezani.

Msisitizo wake ukiwa machoni pa Rebecca ambaye alikuwa akitikisa kichwa kukataa alichokuwa anasikia.

‘I’m not stupid….nikurupuke tu kukufuata kila mara kukueleza kuhusu hili suala… inaonekana ukweli kuwa Pamella ni damu yako bado haujakuingia akilini pamoja na vipimo vya DNA viliyokuthibitishia kila kitu…. kama hujali binti yako kulala na mdogo wako kwangu mimi ninajali…’ Rebecca aligeuka na kutaka kuondoka lakini Dennis akamshika mkono na kumzuia

Akamtazama tu Rebecca asiseme neno lolote lile kwanza. Wakatazamana! Pamoja na utu uzima uliowavamia wote wawili, sura zao za ujana hazikuwatoka machoni mwao. Dennis alimtazama Rebecca kwa upendo na hisia kali kiasi cha Rebecca kukimbiza macho yake pembeni.

‘I wish urudi ulikokuwa Rebecca….i wish!... it kills me kukuona hapa na pale tena… tumeishi tukikimbiana kwa muda mrefu sana na sasa tumerudi sehemu moja tena…. it is not good for us na unajua hilo…inatuweka hatarini zaidi… sasa naona mmoja wetu lazima aondoke na kukaa mbali….and this time itakuwa zamu yangu kuondoka….’ Dennis alisimama wima na kumsogelea Rebecca zaidi.

‘It is not about us…ni kuhusu binti yetu na mdogo wako…’ Rebecca aliukataa ukweli ambao ulijionyesha dhahiri machoni pake
‘una uhakika?...kweli Becca?...kwamba hili si kuhusu sisi?.... you are not in love with me anymore…kweli?’ Dennis aliuliza mfululizo akiwa anamtazama Rebecca machoni.

Mke wa Okello hakujibu kitu, alitazama pembeni akiwayawaya. Dennis akatembea mpaka ulipo mlango wa ofisi na kuufunga kwa kubana kitasa kimoja wapo. kisha akarudi mbele ya Rebecca na kusimama mbele yake wakitazamana…
‘Oh Dennis..’ Rebecca akaziachia hisia zake kwa kumvamia Dennis na kuanza kumbusu kwa fujo. Huku wakihema kila mmoja alionyesha wazi kuingojea nafasi hii kwa hamu kubwa. Dennis aliviachananisha vifungo wa blauzi ya Rebecca kwa kasi huku Rebecca akivifungua vifungo vya shati la Dennis kwa kasi hali midomo yako ikiwa imeungana.

Wakati purukushani hizi zikiendelea, Fiona Agapella alikuwa anaikatiza kordo kuufuata mlango wa ofisi ya Dennis Mazimbwe. Akaufikia na kujaribu kuufuangua lakini ulionekana kufungwa. Akafyonza na kuanza kuondoka lakini mlio wa kuanguka kwa kitu kule ndani ukamfanya arejee na kutega sikio.

Sikio pakee halikumkatia hamu ya kujua kulikoni. akatazaa pale kordoni na kupaona pako kimya, Taratibu akainama na kuchungulia kwenye tundu la ufunguo. Lahaula! akawaona, akawaona wote wawili. Rebecca akiwa ameketri mezani na Dennis akiwa amesimama mbele yake mikono yake ikiwa imezamandani ya nguo ya mke wa Okello.

Fiona akasimama akiwa ametoa macho mithili ya mjusi aliyebanwa na mlango, midomo yake ilibaki wazi kwa sekunde kadhaa huku akihisi macho yake yalikuwa yanamdanganya. Akainama tena kutaka kuchungulia lakini hakuwezakuna mtu a;ikuwa anatembea taratibu akija pale alipokuwepo. Kwa sekunde kadhaa macho yake yaliona kama ukungu tu, Mate yaliyohitajika kumezwa yaliganda ghafla na koo kumkauka.

alihisi baridi mpaka kwenye mifupa wakati alipoiruhusu akili yake itafsiri kile alichokiona. Ubongo ukapokea taarifa rasmi kuwa mwanaume aliyekuwa akitembea taratibu kuja pale alipokuwepo alikuwa Mzee Okello!


…… TUKUTANE HAPAHAPA…..

1 comment:

  1. uwiiii vipele vya baridi vimenito oooh god plz help mzee agapella asife

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger