Monday, September 30, 2013

SINDI...NA LAURA PETTIE (41)

41

‘yaani hatutalewana humu ndani leo… kamtoe umrudishe uko uko ulikomtoa’ sauti ya mwanamke mtu mzima ilimfikia vema Sindi Nalela pale sebuleni alikokuwa ameketi. Sauti ilitokea chumba cha pili alichohisi kilikuwa chumba cha kulala.


‘Mke wangu huyu binti ni sawa na tu na mwanetu Zamzam kwanini usikae naye ukamsikiliza basi… ana matatizo makubwa sana na hapo alipo hana makazi’ Mzee aliyemleta Sindi pale kwake aliongea kwa upole akijitahidi kuzishusha jazba za mkewe.
‘sasa kama hana makazi sisi ndio shirika la kupokea wakimbizi?... nenda kamtoe na kama huwezi niambie nikamng’oe mwenyewe’ sauti ya yule mama ilijaa shari zilizomfanya Sindi atamani kumuita yule Mzee kwa sauti ili amuage tu na kwenda kutafuta msaada mbele ya safari.

‘Una roho gani mke wangu?... binti huyu una mashaka yapi naye hali hujasikiliza tulichoongea mpaka mimi kumleta hapa’ Mzee akazidi kujieleza
‘Sijali mliongea ama mliimba… miaka hii si miaka ya nyuma kwamba utakaribisha usiyemjua na upokee mitume… miaka hii utakaribisha usowajua na upokee mashetani… binadamu tumewashinda wanyama kwa unyama… fanya fanya fanya baba kaniondolee mzigo wako huo sebuleni… wewe mwenye roho safi katafute pa kumuweka’ Yule mama alitamka kwa sauti na akitaka sasa Sindi amsikie vizuri

‘… mwanamke mwenzio sawa na mwanao kabisaa!’ Yule Mzee alishangaa
‘Mradi ni mtu mzima aliye sawa na mwanao anaweza pia kuwa mke mwenzio…. nenda kamuondoe’ akakazia mama mwenye nyumba na yule mzee akaachana na mkewe na kurudi pale sebuleni. Akampa ishara ya kumuomba Sindi amfuate kule nje na Sindi akanyanyuka na kumfuata. Wakatoka pale varandani na yule Mzee akasimama kama anayewaza kitu.

Alikuwa Mlinzi katika moja ya maduka yaliyokuwa karibu na kule nyumbani kwa Dennis. Sindi Nalela alipotoka nyumbani kwa Dennis alizurura na asijue pa kwenda. Pesa aliyokuwa nayo aliogopa hata kuipangia chumba kwa ajili ya kulala usiku mmoja kwani hakujua ya kesho yangeendaje na mbali ya yote, hakujua afanye nini na aende wapi.

Aliumia kuwa katika hali ile, alijuta na zaidi alihisi kuchanganyikiwa. Akajikuta tu akitafuta mahali na kuketi huku akilia. Sala iliyokuwa ikimtoka kimoyomoyo ilisikiwa na Mungu na akamleta Mzee Rajabu mlinzi wa eneo alilokuwa ameketi Sindi akilia.

Mzee yule alimhurumia, akamsikiliza na kumtia moyo huku akimpa hifadhi usiku huo. Asubuhi yake ndio hivi akamchukua na kumleta kwake kigogo Luhanga ila mkewe hakukubaliana na wazo la kumhifadhi Sindi siku mbili tatu.

Pale Varandani alipokuwa amesimama alikuwa akiwaza pa kumpeleka Sindi. Hakutaka tu kumwambia aende zake. Alimhurumia kama binti yake na kibinadamu tu aliguswa na madhila yake. Akapata wazo!
‘Twende mama’ akamsemesha Sindi aliyekuwa amesimama nyuma yake akiwa amepakata kimfuko kidogo kilichokuwa na nguo moja na pochi yenye pesa zake basi.

‘Unampeleka wapi sasa?’ mkewe akamuuliza wakati wakiiacha varanda na kuingia barabarani. Mumewe hakumjibu wala hakugeuka hata kumtizama mkewe. Akachapa mwendo na Sindi akimfuata nyuma. Wakavuka barabara na kupita kando kando ya maduka yaliyokuwa pembezoni mwa njia. Wakanyoosha tu huku Mzee Rajabu akisabahiana na watu kadha wa kadha waliomjulia hali au yeye kuwajulia hali. Alionekana kufahamika eneo lile.

Wakachepuka katika kichochoro kimoja na kukaza mwendo. wakatokezea barabara kubwa ya vumbi iliyokuwa na pilika pilika nyingi mithili ya soko lisilo rasmi. Sindi akalazimika sasa kufanya kazi ya ziada ya kupangua mikono ya wanaume iliyokuwa ikimgusa katika namna ya kumchokoza.

Wakanyoosha na njia ile mpaka kwenye kona iliyoungana na barabara kubwa ya lami. Kulikuwa na baa hapo, wakaingia na yule Mzee akamtaka Sindi aketi katika moja ya viti viliyokuwa hapo baa na amsubiri. Sindi akatulizana kwenye kiti huku akishangaa hiki na kile kwa kuzungusha macho hapa na pale.

Mzee Rajabu akatokomea upande ulionekana kuwa jikoni, akapotelea uko kwa dakika kadhaa kabla ya kurudi pale alipoketi Sindi akiwa na mwanamke nyuma yake. Sindi akasimama na kumsabahi yule mwanamke huku akimpigia lile goti la heshima.
Alikuwa kipande cha mwanamke, mrefu, mweupe kama karatasi, kidevu chake kikiwa na ndevu chache za mkorogo, kichwani akiwa na nywele zilizoparazwa na dawa ya relaxer na kuzifanya ziwe kama manyoya yaliyonyeshewa. Alikuwa na mwili tipwa uliosheheni nyama kila kona.

‘Marhaba mwanangu…za kwako?’ akaijibu salamu ya Sindi huku akimgeukia Mzee Rajabu
‘Ndio huyu binti mwenyewe?’ akamuuliza Mzee rajabu
‘Ndio huyu!...’ Mzee akaitikia akimuonyeshea kidole Sindi
‘Mmh sasa mkeo naye kile kichwa kimejaa vumbi la mkaa wallah… kwa akili gani ukamletee mke mwenza ndani kwa staili hii…’ yule mama akashangaa akisonya msonyo  mkali kidogo na kumgeukia Sindi

‘Una njaa?’ akamuuliza Sindi naye akatikisa kichwa kukataa ilhali tumbo lilikuwa likimsakama kupitiliza. Yule mama aliuona ule uongo waziwazi na akatabasamu
‘Kachirii…we kachiri…’ akapaza sauti akiwa amegeukia kule jikoni alikotokea na Mzee Rajabu

‘Sinasudi hebu niitie kachiri uko jikoni…’ akaagiza na kuwageukia wageni wake.
‘Kaeni sasa mpate kifungua kinywa kwanza ndio tujue yapi ya alifu yapi ya ujiti’ akatoa angalizo lake naye akikifuata kiti meza ya pembeni ili kuongezea kiti pale walipokuwa wamesimama.

Wakaketi na huyo Kachiri akaja mbio mbio kuchukua oda ya staftaha. Maongezi yakaendelea sasa. Yule mama akimhoji Sindi hiki na kile kujiridhisha na alichoambiwa na Mzee Rajabu.

‘sasa mama… mimi msaada wangu ni kukutafutia kazi za ndani au ndio nikufanyie mpango uuze baa hapa… kaa chini ufikirie leo, kesho unipe jibu… nijue tunaanzia wapi… umenielewa?’ yule mama akataka uhakika kama aliyoongea yalieleweka

Sindi akaitikia kwa kichwa akiona haya pia. Wakaletewa oda zao na kuanza kukishambulia chakula. Moyoni Sindi akiyaona haya yote kama ndoto tu. Alikuwa akitoka hapa na kuingia pale kama miujiza. Angalau alipata tumaini la wapi pa kuanzia kesho yake! lakini upande mwingine wa moyo wake ulijaa mzigo wa siri.

Alikuwa ameficha kuhusu mimba yake na alikuwa ameficha ukweli kuhusu Jerry Agapella. Stori yake ilikuwa ni kuletwa mjini kufanya kazi na aliyemleta amemfukuza. Akashusha pumzi akiyatupilia mbali mawazo yale na kukishambulia chakula chake. alishaamua liwalo na liwe.
888888888888888888888888

Mzee Agapella alikuwa amechangamka asubuhi hii, akionekana kuwa na nafuu kubwa pale kitandani alipokuwa ameketi. Daktari aliyekuwa anamhudumia alifunga faili lake na kuhitimisha matibabu yake huku akitabasamu
‘unaweza kutoka leo au kesho asubuhi… ila uko imara kabisa sasa…’ Dokta aliongea akimtazama Mzee Agapella

‘kuna dawa zozote ataendelea kutumia nyumbani?’ Jerry akamuuliza daktari
‘yeah.. yeah.. zipo na baada ya wiki mbili tatu atahitajika kufanya uchunguzi mdogo mdogo tu na kuhakiki afya yake’ dokta akajibu huku akiaga pia na kuwaacha mtu na baba yake wenyewe.
‘umeshaongea na Pamella?’ baba yake akamtupia swali mara tu baada ya dokta kufunga mlango
‘Baba!’ Jerry akashangaa mshangao uliotoka kwa sauti ya kukereka
‘nalizungumza hili suala kwa mara ya ngapi Jerry?...’
‘inshu sio kwa mara ya ngapi… siko tayari kuoa sasa hivi nina mengi baba na akili yangu ina vurugu nyingi sana…’ akajitetea
‘Mengi kama yapi Jerry?... ‘ baba yake akambana na Jerry akamtumbulia macho baba yake akitamani kumweleza kuhusu Sindi lakini stori ingekuwa ndefu na maswali toka kwa baba yake yangefanya siku yake iishe vibaya mno. Akameza mate akimezea na kinachomtatiza

‘Unaona!... sioni kipingamizi chochote na zaidi mimi ndio ninayekufanyia harusi Jerry… humpendi Pamella?’ akamuuliza swali lililougusa moyo wake na almanusura alijibu pale pale. Akajizuia tena na kuendelea kumtumbulia macho baba yake katika namna ya kupotea mbali kimawazo.

‘Hey!’ baba yake akamshtua
‘…Nahitaji muda zaidi baba’ Jerry akajaribu kukwepa majukumu
‘One week…’ baba yake akampa ‘deadline’ na Jerry akashusha pumzi zake ndefu angalau akishukuru kuhitimisha maongezi yale.
‘Tukutoe leo au kesho?’ akamuuliza baba yake akibadili mada haraka sana
‘Utakavyoona’ baba yake akamjibu akimkazia macho usoni na Jerry akatazama pembeni, alihisi baba yake alikuwa akijaribu kuisoma akili yake kwa wakati ule. Hakutaka kuendelea kukaa pale hata dakika moja zaidi alihisi angebanwa zaidi kuhusu suala la kumuoa Pamella. Akaaga na kuondoka!
88888888888888888888888

Mlango wa chumba cha kulala ulifunguliwa na  Pamella akaingia chumbani kwake huku mama yake akimfuata nyuma. Pamella akaenda mpaka ilipo meza ya kujirembea na kusimama hapo akiwa amegeuka na kumtazama mama yake kama mtu asiyeamini alichokisikia.

‘Mtapangaje vitu bila kunishirikisha?... mnajua mipango ya Jerry?... mnajua mipango yangu?’ Pamella aliuliza akija juu
‘It is for good darling!... na Jerry ni rafiki yako wa muda mrefu’ mama yake alijaribu kumuelewesha akimfuata mpaka pale aliposimama na kujaribu kumshika. Pamella akapangua mikono ya mama yake na kumpita akienda kusimama kule alikokuwa amesimama mama yake kabla ya kumfuata.

‘… I can’t believe mpaka leo hii kuna wazazi mnaamini katika kuunganisha watu bila idhini zao…’ Pamella alilalamika
‘unataka kuniambia humpendi Jerry?’ mama yake akamuuliz
‘I love him… I love him dearly mama but niko katika mahusiano na Patrick Mazimbwe’ Pamella akatamka kwa msisitizo na asijue nia kiasi gani aliupasua moyo wa mama yake.

‘What!... Pam!... wait…’ mama yake alikatakata maneno na asijue alichotaka kuongea kwa dakika zile. alifumba macho kama mtu anayesikilizia hali Fulani ya uchungu kisha akafumbua macho na kushusha pumzi. Akamkodolea binti yake macho ya mshangao, akiwa ameyatoa kwa upana wa kutosha.

‘darling! unaolewa na Jerry… hili sio ombi tena binti yangu… ni taarifa tu’ Rebecca aliongea kwa msisitizo akiaanza kuchapua hatua na kumpita binti yake ambaye naye bumbuwazi lililompata lilimfanya ageuke na kumfuata mama yake nyuma pasipo kuongea kitu. Wakatoka wakifuatana mpaka sebuleni ambako mama yake alichukua funguo za gari zilizokuwa juu ya meza na kuufuata mlango wa kutokea.

‘why are you doing this to me mama?’ akamuuliza mama yake kwa sauti ya kulalamika
‘kwasababu najua ninachoafanya!’ Rebecca akamjibu binti yake kwa sauti iliyoonyesha dhahiri kuwa hakuwa akitania.

‘nampenda Jerry ndio but niko na Patrick na nina hakika Jerry ana mtu anayempenda sasa…’ Pamella aliongea kwa uchungu wakati mama yake akigusa kitasa cha mlango.
Ukimya ukapita kati yao. Pamella akimtazama mama yake na mama yake akiitazama kitasa cha mlango kama mtu anayewaza kitu.

Taratibu akakizungusha na kuufungua mlango, akatoka pasipo kugeuka kumtazama binti yake. Rebecca aliingia kwenye moja ya magari yaliyokuwa yameegeshwa hapo nje ya nyumba yao na kuliingiza barabarani. Alikuwa anaelekea ofisini kwa Dennis Mazimbwe.

Alipoingia kwenye eneo la maegesho, Rebecca alitulia garini kwa dakika kadhaa akiwa ameulalia usukani. Alikusanya nguvu za kwenda kuongea na Dennis. Hata alipoteremka, alishuka kinyongea mno akitembea kwa hatua za taratibu mpaka mapokezi ambako alisabahiana na mtu wa mapokezi na kuifuata kordo iliyokuwa inaelekea ofisini kwa Dennis. akaufikia mlango na kusimama tena pale kwa sekunde kadhaa. Akishusha pumzi mara kadhaa kabla ya kugonga.

‘Karibu!’ sauti ya Dennis iliitikia kwa ndani mara tu alipogonga. Akashusha tena pumzi na kukishika kitasa cha mlango. akakinyonga na kukisukumia mbele na mlango ukatii amri na kufunguka. Akajitoma ndani!

Dennis Mazimbwe alikuwa busy na shughuli zake kwenye kompyuta iliyokuwa mbele yake, aliinua uso wake na kumtazama Rebecca mara moja tu kisha akazama tena kwenye kazi zake. Rebecca alitembea taratibu na kuifikia meza ya kazi ya Dennis ambaye bado aliendelea kujikita katika ile kazi aliyokuwa akiichapa kwenye kompyuta yake.

‘Habari yako!’ Rebecca akamsabahi na Dennis akanyoosha mkono wake wa kushoto akimuonyesha kiti cha kuketi pasipo hata kumtazama, akaendelea na kazi yake. Rebecca hakuketi! Dennis naye hakuacha ile kazi yake. ikakatika nusu dakika nzima kukiwa na ukimya kati yao.

Rebecca akatikisa kichwa kuonyesha kuumizwa na ile dharaua aliyofanyiwa na Dennis.
‘We need to talk Dennis’ akaongea taratibu akimtazama Dennis kwa upole
‘Nimekuonyesha kiti uketi’ akajibu Dennis pasipo kumtazama wala kuiacha kazi yake. Rebecca akashusha pumzi kwa sauti kidogo na kuketi.

Akangoja tena dakika mbili nzima na ndipo Dennis akaachana na kazi yake na kumgeukia Rebecca.
‘Nakusikiliza’ akamsemesha Rebecca akimtazama usoni
‘Ni kuhusu Patrick…’ akaanza Rebecca na Dennis akabweua kwa sauti ya kero akimtazama Rebecca kwa mshangao.
‘It is always about Patrick… you know what Mrs. Okello…’ Dennis aliongea kwa hasira kidogo akichukua simu yake na kuhangaika nayo, akavuta karatasi dogo na kuandika namba kwenye karatasi hiyo kisha akaisukumia mbele alipoketi Rebecca

‘Hizo hapo ni namba zake… talk to him!’ akaongea kwa jazba
‘Kwamba aachane na binti wa kaka yake… si ndio?’ Rebecca naye akaja juu
‘Whatever!’ akajibu Dennis akimkodolea Rebecca macho ya hasira
‘una uhakika?’ Rebecca naye akauliza akimtolea macho Dennis
‘ otherwise nisingetoa namba!...’ Dennis alijiamini
‘Na uko tayari Patrick amwambie Pamella ukweli kuhusu baba yake?’ Rebecca sasa aliongea kwa unyonge kidogo

Dennis hakujibu, alifumba macho na kuinamisha kichwa chini. Rebecca akaiokota ile karatasi na kuikunja vizuri, akaishika mkononi na kisha taratibu akajiinua toka kitini. Wakati alipotaka kukiacha kiti Dennis akainua kichwa na kumtazama Rebecca. alijizuia kuongea alichotaka kuongea lakini hakuweza kujizuia kutonyanyuka toka pale kitini na kumfuata Rebecca aliyekuwa anachapua hatua kuufuata mlango.

akamtia mikononi mwake na kumkumbatia kwa nyuma. Rebecca akafumba macho sambamba na Dennis. Hisia zao ziliongea kwenye miili yao iliyoshikamana. taratibu Rebecca akageuka na kumtazama Dennis usoni, wakipapasana na kuanza kutandikana mabusu kimya kimya. Rebecca akalishika shati la Dennis na kutenganisha vifungo na tundu lake hali mikono ya Dennis akihangaika na blauzi ya Rebecca

‘I love you Dennis…’ sauti uliyochoka na kukatika katika kwa mihemko ilitoka mdomoni mwa Rebecca wakati Dennis alipoitoa blauzi yake mwilini mwake. Mchezo waliousitisha miaka michache iliyopita walikuwa wameurudisha bila kujali hatari iliyokuwa mbele yao
888888888888888888888888888

Kwenye ile wodi aliyolazwa Mzee Agapella. Mtu aliyevalia kama daktari anatembea kwa wasiwasi akiangalia huku na kule. Anaikatiza kordo na kuufikia mlango wa chumba kile. Anasimama na kutoa simu yake ambayo anaipiga na kusikiliza
‘Hakuna mlinzi yoyote leo…poa’ akataka simu na kuingia ndani ya wodi kwa tahadhari. Moja kwa moja anakifuata kitanda cha mgonjwa na kutoa sindano ya sumu anaichoma kwenye chupa ya drip. Sindano ile inaachia sumu ichanganyikane na maji ya dawa yaliyokuwa katika chupa ile.

Anaitimiza kazi yake na kuharakia kutoka pasipo kuonwa na mtu yoyote. Anatoka na kuishia zake kwenye lifti. anavua mavazi ya bandia ya udokta na kubaki na nguo zake. anatoka na kuyafiata maegesho ambako analikuta gari linalomgonja.

Anaingia garini na dereva ni Fiona Agapella.
‘Done?’ anamuuliza kwa shauku
‘Done!’ anaitikia kwa furaha na Fiona akapiga ukunga wa furaha akicheka kwa sauti bila kikomo. Furaha aliyokuwa nayo muda ile sisngewezekana kuisimulia

Alichotaka kukitimiza kilikuwa kimetimia!

.... TUKUTANE HAPAHAPA....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger