Monday, September 23, 2013

SINDI.... NA LAURA PETTIE (40)

40

Pale alipokuwa amesimama, Sindi alinesa nesa mwili mzima, ilikuwa zaidi ya kutetemeka, zaidi ya hofu na kuchanganyikiwa kulikochanganyikana na hali ya kutoamini alichokiona. Mlango ulipogongwa mara ya pili, Sindi alifumba macho kwa nguvu zote na kujaribu kujikakamaza asianguke ila mwili uligoma kutulia, uligoma kutii amri ya kukakamaa na kinyume chake kila sehemu ya mwili ilimcheza mpaka utumbo!


Jerry hakuielewa ile hali ya ukimya mule ndani hali taa zilikuwa zinawaka. Akaachana na kugonga kwa mlango na kuamua kubonyeza kengele iliyokuwa sentimeta chache tu mbele yake. Kengele ile ilitoa mlio uliomfanya Sindi ababaike zaidi na kurudi kinyumenyume mpaka alipogota kwenye kochi.

Jasho lilikuwa linamtoka, alichoka kutetemeka na sasa machozi yalikuwa yakimnyemelea. Nguvu alizokuwa nazo hazikutosha hata kumpigisha hatua moja mbele sembuse kumuondoa pale na kumkimbiza ndani. Kengele ikalia tena na Sindi sasa akahamanika na kutoa ukelele mdogo wa hofu, akiziba masikio asiusikie ule mlio wa kengele. Haikusaidia!

Jerry akasimama pale mlangoni akikosa uamuzi wa haraka. Akageukia kule alikokuwa mlinzi na kutaka kumuuliza kama kulikuwa na mtu ndani lakini akasita. Akatembea taratibu na kulifuata gari lake. Akauegemea mlango wa dereva kwa kuulalia kwa mgongo huku mkono wake wa kushoto ukizama mfukoni na ule wa kulia ukipeleka simu sikioni.

Akazama kwenye maongezi! kutoweka kwake pale mlangoni kukaleta ukimya kule ndani. Ukimya uliompa nguvu Sindi. Akajikusanya hali akiweweseka na kunyata kulifuata dirisha lile lile alilotumia kuchungulia nje. Akajikwaa kwenye stuli iliyokuwa na ile sahani yenye chungwa alilokuwa anamenya kabla ya ujio wa Jerry. Stuli ikayumba na kuibwaga chini sahani iliyotua kwenye tiles kwa kelele huku chungwa likiserereka na kuingia chini ya meza.

Ukelele ule ukamfanya Jerry ainue uso na kutazama lile dirisha lililokuwa karibu na mlango wakati Sindi aliuma midomo yake kwa nguvu zote akiwa amefumba macho na kujichuchumisha chini kwa hofu. Kwa sekunde tano alisali sala zote zilizomjia akilini.

Jerry akaendelea na maongezi yake kwenye simu na Sindi akajinyanyua na kulifuata dirisha. Kwa tahadhari kubwa akalifunua tena pazia na sasa akamuona Jerry vizuri zaidi. alisimama kwenye mwanga wa taa uliommulika barabara. Alikuwa Jerry yule yule ila mwenye tofauti kubwa katika mavazi yake. Alionekana kuwa kijana mwenye maisha ya juu zaidi alivyowahi hata kufikiria. Lile wazo la Jerry kuwa mpelelezi lilipata nguvu zaidi. Moyo wake uligonga kwa kasi mno na mawazo ya ajabu ajabu yakipita kichwani mwake!

Jerry akasimama wima akimalizia kuongea kwenye simu na kuikata. Akampa ishara mlinzi afungue geti huku yeye akifungua mlango wa gari na kujitoma ndani, akawasha gari lake la kisasa na kuliondoa taratibu eneo lile. Jerry akaishia!

Sindi akashusha pumzi sasa na akili yake ikikimbizana na maswali ambayo kwa wakati ule yalikosa majibu na uhakika pekee aliojipa ni kuwa Jerry anamtafuta na pengine ameshajua yuko mule ndani. Akaogopa zaidi, akababaika kupitiliza. Kwa mwendo wa kusuasua akajipeleka kwenye kochi na kujiachia kama mzigo.
Akawaza alichoondoka nacho kwa Jerry kiasi cha kumsaka vile. Akalishika tumbo lake dogo, tumbo lililokuwa na mimba changa ya Jerry! Moyo wake uliokuwa ukigonga kwa nguvu nao ulipata kimuhemuhe pia, pamoja na hofu yote iliyomtembelea dakika chache zilizopita bado alitamani Jerry arejee pale tena, akatamani arejee na yeye ajitokeze na kumvaa kwa maswali na misuto, akatamani tu arejee tena na amchungulie tena na tena.
88888888888888888888888

Eneo la Mgahawa wa Samaki Samaki uliopo eneo la Mlimani City lilikuwa limechangamka mno. Muda huo wa saa mbili usiku. Watu wa mataifa mbalimbali walionekana wakifurahia maisha huku mabinti warembo walioingia na kutoka wakiongeza nakshi katika eneo hili. Dennis Mazimbwe alikuwa mmoja wa watu waliokuwa kwenye mgahawa huo akiongea na kucheka na baadhi ya marafiki zake aliokuwa nao.

Simu yake ilipoita, akajitoa kando na kuipokea huku akitembea taratibu na kuliacha mbali eneo la mgahawa. Alikuwa akiongea na Jerry Agapella wakati ule alipokuwa ameegemea gari. Waliongea kwa kirefu na wakamalizana kuhusu mambo yao, alipotaka kurejea akapata wazo la kuelekea ATM ya CRDB iliyokuwa ndani ya jengo la Mlimani City.

Akakumbana na foleni ndogo iliyomfanya ageuze na kusimama nje akiwaza cha kufanya, apange foleni au aende eneo lingine lenye ATM za benki hiyo. Wakati akiwaza hayo, akamuona mtu aliyetokea ndani akiwa na mifuko ya shoprite mingi. Hakutarajia kumuona mtu yule eneo lile na muda kama ule. Akakaza macho yake kujipa uhakika zaidi na akapata! Alikuwa Rebecca Okello.

Alimtazama alivyotembea upesi upesi kuelekea eneo la maegesho na akajikuta akimfuata nyuma. Sehemu aliyoegesha kulikuwa na kijigiza kidogo. Rebecca alilifikia gari lake na kufungua mlango wa abiria akatua vitu vyote alivyokuwa navyo na wakati akitaka kuufunga mlango. Simu yake iliyokuwa mkononi sambamba na ufunguo wa gari ikaita. Akakitazama kioo cha simu na alipolisoma jina la mpigaji akaikata na kuendelea kuweka sawa ile mifuko aliyoitua katika kiti cha abiria. Simu ikaanza upya kuita na alipoliona jina la mpigaji likiwa ni lile lile akatikisa kichwa chake kulia na kushoton akionesha kukereka na ile simu. Akaiacha iite kwa sekunde tatu kisha akaikata.

akaufunga mlango wa gari na kuzunguka kuelekea upande wa dereva. Akasimama ghafla, akichia sauti ya mshtuko huku mikono yake ikikimbilia kukishika kifua chake kana kwamba kilitaka kumponyoka ghafla. Akahema kwa nguvu huku akimtazama Dennis aliyekuwa amesimama karibu na ule mlango wa kuingilia kiti cha dereva.

‘Rebecca!... why?’ Dennis akaongea polepole asijali sana ule mshtuko aliomletea mwenzake kwa kusimama pale kama kizuka.
‘umenishtua mno… what are you doing here?’ Rebecca aliuliza akiwa bado na ile hali ya mshtuko
‘nataka kuongea na wewe… hupokei simu zangu…hujibu text… why?’ Dennis aliuliza taratibu akimakazia macho Rebecca ambaye aliangaza huku na kule kama vile hakutaka kuonekana na mtu yoyote akiongea na Dennis eneo lile

Wakatazamana! Rebecca akashisndwa kuhimili kutazamana kule na aukayashusha macho katika namna ya kubabaika kidogo huku akimfuata kwa kasi Dennis na kujaribu kumuondoa pale aliposimama ili aufungue mlango wa gari. alifanya kosa!

Dennis Mazimbwe alikwanyua ule ufunguo wa gari toka mikononi mwa Rebecca na kurudi nyuma hatua moja. Rebecca akajaribu kuuchukua ufunguo wake kimabavu na kuzua hali ya kugombea ufunguo kama watoto.

‘this is not funny Dennis… nipe ufunguo wangu niondoke eneo hili’ Rebecca akakemea na Dennis akacheka.
‘Huendi popote usipokubali kuwekana sawa na mimi…. hivi unajua ni kwa kiasi gani umeniathiri wiki hii nzima?... sijafanya lolote la maana…’ Dennis akaongea akimtazama Rebecca usoni

‘Sijali… una maisha yako nami nina yangu… usipofanya mambo yako ya maana … hainisumbui… wewe ni nani kwangu nijali unachofanya au usichofanya… hebu nipe ufunguo wangu niondoke’ Rebecca alijibu kwa sauti ya kufoka akiwa amekunjua uso. akamkaribia tena Dennis na likawa kosa lingine.

Dennis alimshika ghafla na kumuegemeza kwenye gari lake, akiuwahi mdomo wake na kuumiliki. akambana barabara kwa sekunde mbili tu na kumuachia huku tayari akiwa ameshatimiza azma yake. kumbusu!

Rebecca alifurukuta na hata alipoachiwa naye aliachia kofi kali lililotua barabara shavuni mwa Dennis.
‘Stupid!... usijaribu kunigusa tena Dennis…’ akakaribia akitaka kuuchukua ufunguo uliokuwa mkononi mwa Dennis ambaye aliukwatua mkono wake uliokuwa na funguo hali akisuguasugua shavu lililonaswa kibao.

‘Fine!... sitakugusa tena…’ Dennis akaongea polepole kisha taratibu akageuka na kuanza kuondoka eneo lile.  Rebecca akanyong’onyea. Alihitaji ufunguo wake. Akamtazama Dennis alivyokuwa akizidi kupiga hatua kuelekea eneo lingine la maogesho akahisi alitaka kuondoka.

akajikuta tu akimfuata kule alikokuwa anaelekea na mpaka anamfikia, Dennis alishalifikia gari lake na kusimama kando akimtazama Rebecca
‘Dennis Please!... nachelewa kwangu…’ Rebecca akabembeleza
‘Si mimi ninayekuchelewesha…. we need to talk Rebecca… hatuwezi kukimbiana hivi siku zote… it kills me Becca cause I love you and I can’t take it anymore… please naomba uni…’ akakatishwa na Rebecca aliyemnyooshea kiganja cha mkono mithili ya tafriki anayesimamisha gari. alimtaka anyamaze.

‘Unajua sisis sio sio watoto wala teenagers… niliona kwa macho yangu kilichotokea kati yako na Fiona… na uliutarajia niifurahie hali ile?...’ Rebecca alianza kuja juu
‘Na ndiyo nahitaji nafasi nijieleze Babe… ulichokiona sio hali halisi unayowaza’ Dennis alijitetea

‘Kwa hiyo yale yalikuwa mazingaombwe si ndio?’ Akauliza kwa sauti ya dhihaka akikusanya mikono yake na kuipishanisha chini ya matiti yake kwa mtindo wa nibebe nikubebe.

Dennis akamtazama Rebecca kwa kituo kwanza.
‘Unanichelewesha jamani… nipe ufunguo wangu haya mazingaombwe yako utanielelza siku nyingine… nahitaji kumuwahi mume wangu’ Rebecca akanyoosha mkono wake wa kushoto akisubiri kupewa huo ufunguo.

Dennis hakumjibu wala hakupepepesa hata macho, aliendelea kumtazama Rebecca na safari hii akiumizwa kidogo nay ale mashauzi ya Rebecca ya kumtaja mume wake. Haikuwahi kutokea!

‘So unamtaja mume wako ili uniumize zaidi au ni nini?’ Dennis aliongea kwa sauti ya kunung’unika
‘Kukuuumiza?... ni mume wangu wa ndoa… kipenzi changu…  kumtaja mbele yako ni haku yangu… iwe unapenda kusikia au hupendi kumsikia that is up to you… nipe ufunguo!’ Rebecca alizifisha nyodo sasa na aliyaona maumivu ya Dennis waziwazi

‘Rebecca unaniambia mimi hivi?’ Dennis alihisi kuumia zaidi
‘Khaa! kwani naongea na haya magari hapa…’ akamuonyesha magari yaliyokuwa eneo la maegesho ‘…naongea na wewe ndio!’ akahitimisha jibu lake akimsonta Dennis kwa kidole cha shahada cha mkono wa kushoto

Dennis akainamisha kichwa chini kwa muda kisha taratibu akainua kichwa na kumtazama Rebecca
‘Sijawahi kuwa na uhusiano na Fiona… I swear… ‘ akatikisa kichwa na kuvua miwani yake ya macho. Rebecca akazungusha macho yake kijeuri na kutazama pembeni akiimung’unya midomo yake

‘Nakupenda Rebecca… na unajua hilo na unajua mapenzi yangu kwako yalivyoigharimu ndoa yangu… you know it ni kiasi gani tumemuumiza Daniella… nikaubeba msalaba wote ili kuitunza ndoa yako… is it fair kuongea unachoongea hapa?’ Dennis aliongea kwa unyonge mno na kwa hisia kali

‘Unanipigia kelele Dennis… nini kilichokuumiza?.... kumtaja mume wangu?... yeaaah! Okello is my husband and I love him mno… na ndio ananimiliki kihalali…unipe ufunguo nimuwahi mume wangu…’ akairudia kauli yake kwa nyodo zaidi akijua ni kiasi gani alimuumiza mwenzake. alikuwa analipa kisasi cha maumivu aliyoyasikia yeye alipowakuta na Fiona Agapella.

‘Rebecca!... umekuwaje?....’ Dennis hakuamini
‘hebu nipe ufunguo’ akaamrisha
‘Wait… Do you love me?’ Dennis akauliza akiwa amehamanika
‘No!... nikupende kama nani?... wewe ni nani kwangu nikupende?...’
‘Kweli?... Rebecca aunaongea hivi?... sababu tu umemkuta Fiona ofisini akanibusu shavuni?....  like seriously?...’ Dennis aliweweseka

‘Busu?... you guys mlikuwa meshikana… na pengine nisingetokea mngefanya unayoyafanya ofisini mule na mimi…and it means sio mimi peke yangu ninayevuliwa mule ndani… I caught you red-handed’ Rebecca alikuja juu zaidi
‘Becca!... hivi unanichukuliaje?’ akahoji
‘Malaya!’ akajibiwa haraka tu
‘What!...ookay…fine…fine… fine’ akachachatika, akitikisa kichwa juu chini na tabasamu lisiloeleweka likimvamia. Akashusha pumzi na kuvaa miwani yake. Akaunyoosha mkono uliokuwa na funguo na kuuning’iniza mbele ya Rebecca, aliyeukwanyua haraka kana kwamba alihofia ungerudi ulikokuwa.

Dennis akafungua mlango wa gari lake na kujitoma ndani. akaufunga mlango na kuwasha gari. taratibu akampita Rebecca na kuishia zake akimuacha mwanamama huyu akiwa na hali ya maumivu kuliko hata aliyokuwa nayo kabla ya kuongea na Dennis. alijihisi hatia ghafla kwa vile alivyomjibu Dennis Mazimbwe.

Pamoja na yote yaliyotokea, hakustahili kumjibu Dennis vile! Maumivu aliyoyahisi baada ya Dennis kuondoka yalikuwa maradufu, badala ya kujisikia fahari kwa kulipa kisasi alihisi alikuwa amejiongezea jitimai kwa kuvuruga zaidi uhusiano wake na mwanaume aliyekuwa anampenda kupitiliza!
888888888888888888888888888

Asubuhi na mapema, jua la Karima lilishachomoza na kuleta mwanga juu ya anga la Karima. Fiona Agapella alikuwa sebuleni kwa rafiki yake Iloma akiongea na mtu kwenye simu. Jazba alizokuwa nazo zilitosha kabisa kumfanya Iloma amtazame kwa mshangao na kumfuatisha kwa macho zile nenda rudi nenda rudi alizokuwa akifanya pale mbele yake.

‘Kimeshindikana nini?... wapi?... kuna ulinzi gani mpaka mshindwe kutumia hata sindano ya sumu… siwaelewi… kwahiyo… kitu gani?... sio papara… sielewi nini kinachukua muda huu kutimiza kazi niliyowatuma… aaargh… hebu fanyeni kazi acheni upumbavu’ akakata simu na kumtumbulia macho  Iloma

‘…wameshindwa tena?’ Iloma akamuuliza
‘Wapumbavu hawa sijui wanaenda na mabango ya matangazo hapo hospitali… eti ulinzi mkali sijui takataka gani… the guys are not serious… yaani sijui nipate wapi vijana wa kazi wanaojua kazi zao… haya magumashi ndio yamesababisha Jerry bado anaisumbua akili yangu…’ Fiona alifoka akimfuata Iloma pale kwenye kochi na kuketi kando yake. akiirusha simu yake sofa la pili lililokuwa kando.

‘ukute ni kweli kuhusu ulinzi…’ Iloma alitetea
‘Aaah wapi… waoga tu wale… this time wakishindwa naenda mwenyewe’ akasema kwa kujiamini.
‘Fiona!... hebu tulia kwanza, ya Dennis umefikia wapi?’ iloma akataka kubadili uelekeo wa mada
‘Dennis ni smart… hawezi ingia mtegoni kijinga jinga tu… naweka sawa mitambo yangu ikimnasa kwenye kumi na nane zangu atafanya kila ninalotaka na zaidi…’ akaongeza kujiamini

‘ Usije tu ukamblackmail mwanasheria wa watu kwa inshu za mke wa Okello’ Iloma akaonya akigeuka na kuchuka gazeti aliloliweka kando kabla ya ujio wa Fiona pale. Fiona akamtazama shoga yake na kucheka
‘Kwanza nimeshawatibu nadhani… all in all Dennis is hot… na umri ule kwa muonekanano wake mwanamke yoyote lazima uvute pumzi kwanza… zaidi ya kumtumia namtaka pia…’ Fiona akatamka kwa majidai na kumfanya Iloma aliweke tena gazeti kando na kucheka kwa sauti

‘Nini?... you can’t be serious Fifi… unamataka Dennis?’ iloma akakaa kiumbeya zaidi akinaba bana kicheko chake
‘Siku nyingi tu… usiniambie hujawahi kumtazama Dennis ukamuwazia tofauti… changanya na kuolewa na zee hili yaani akibusu shavu akaandika cheque ya pesa amemaliza… a woman needs more than that’ Fiona alitetea tama yake

‘Hukuliona hilo kabla kumuondoa mwenzio?’ iloma akamshushua na kumfanya Fiona amtie singi na kunyanyuka. Alitaka kuelekea ndani na simu yake ikaita tena. Akaichukua na kuipokea.
‘Enhee… kweli?... sawa mwanangu… sawa mama… haya’ akakata simu na kumtazama Iloma
‘Nani?’ akauliza Iloma akikunja uso
‘Mwendawazimu wangu Jenifa… hakuna linalompita asiniambie… ananichosha tu na yeye mama mama… ingekuwa amri yangu nacho ningeshakifukuzia mbali kule… hivi ndio vinavyomaliza sehemu ya urithi tu… akafie uko aniachie nafasi’ akasonya zake na kuishia ndani akimuacha iloma anacheka pale kochini na hapo hapo akisikitika pia.
8888888888888888888888

Meddy alikuwa akisoma baadhi ya vitini vilivyokuwa juu ya meza ya kazi ya Jerry wakati akimsubiri Jerry.  akamalizana na vitini na kuchukua gazeti ambalo alilipitia juu juu kabla ya kugeuka na kuangalia mlangoni alikoingia Jerry na sekretari wake.

Jerry akakifuata kiti chake na kuketi, akavuta droo na kutoa faili moja kubwa aliloanza kulipekua huku akiongea na sekretari wake aliyekuwa anaandika mambo muhimu kwenye notebook iliyokuwa mkononi mwake
‘…umesema kikao na Mr. Otoyo kiwe juma ngapi?’ sekretari akauliza
‘Jumatano saa sita mchana’ akajibu Jerry akiwa amezamisha macho yake kwenye faili. Akaongeza na maelezo mengine huku akinyofoa karatasi kadhaa toka katika lile faili na kumpatia yule sekretari

‘Iwe tayari kabla ya saa kumi jioni… uitume kwa fax na risiti zote… hakikisha idara ya fedha ina nakala husika..right?’ akampa maelezo yule binti naye akaitikia na kuzipokea zile karatasi. Akaondoka.
‘Naomi is beautiful…’ Meddy akamsifia yule sekretari
‘Nimezungukwa na wanawake wazuri Meddy kiasi kwamba nimeanza kusahau uzuri ni nini… Enhee! umefanikisha inshu yako bandarini’  Jerry akabadili mada hali akionekana kuwa busy na kompyuta iliyokuwa kando yake.

‘Tuyaache yote a weka kila kitu kando… just talk to me Jerry…najua unajaribu kumeza hisia za maumivu but kupretend kila kitu kiko poa huku unaumia… ni hatari zaidi’ Meddy akaongea kwa sauti iliyojaa umakini na Jerry akaacha kila kitu na kumtazama Meddy kwa kituo

‘Nifanye nini?... nilie kila tunapokutana… you told me to be a man and that is what I’m doing right now…’ Jerry akajitetea
‘while drinking 24 hours…. hivi unadhani sijanotice uwepo wa chupa ya pombe kali hapo chini… au unadhani manukato uliyopata yanadrive away harufu ya pombe kinywani mwako…. Jerry!...’ Meddy alimuita rafiki yake kwa huruma na ule uso wa Jerry uliokuwa na hali ya kujiamini ukatoweka. huzuni ikautawala uso wake na hali halisi iliyopo moyoni mwake ikajitokeza usoni pake. akajiinamia kwanza!

‘… najua inauma lakini utaumia zaidi ukipretend uko sawa wakati moyoni hauko sawa’ Meddy akamsemesha
‘Nampenda Sindi… sijui nisemeje… but ni kama ameondoka na sehemu Fulani ya mwili wangu… I love her kwa moyo wangu wote na kukubali kuwa amenikimbia ni kitu ambacho sijui namna ya kupambana nacho… anakuja kichwani kila dakika kila… sekunde… I’m trying…najaribu…’ Jerry akaongea kwa kusitasita taya zake zikisigana na kuonyesha ni namna gani alipambana kiume asiangue kilio tu.

Meddy akashusha pumzi na kupunguza ukubwa wa macho yake kidogo, wakati huo huo akimtamza Jerry katika namna ya kumuhurumia. alishaipitia hali ya kuachwa solemba na mwanamke aliyempenda kupitiliza lakini kwa tukio la Jerry alihisi alichokipitia yeye kilikuwa theluthi tu ya anachopitia rafiki yake.

Jerry akajiinamia tena kisha akanyanyua uso na kujitahidi kutabasamu ili kuipoteza ile hali ya huzuni iliyopita kati yao
‘kaa karibu na Pamella, she will heal you baada ya muda ila uwepo wake utasaidia kucontrol huu unywaji unaoelekea kubaya’ Meddy akatoa wazo na Jerry akacheka kwa sauti na kujilaza kwenye kiti chake akijizungusha taratibu kulia na kushoto

‘Nahisi ipo siku atachapana makofi na Clarita’ akasema akicheka tena
‘na Clarita anakupenda aisee… baada ya kwenda na kurudi bado yupo available for you… wengine mliogeshwa na mitishamba gani mlipozaliwa … watu tunafukuzia watoto wakali kwa mitego wewe wanajileta wanajitega…’ Meddy akatania na Jerry akacheka zaidi

‘Kismati tu… ila funga kazi ni Sindi Nalela… pamoja na yote yeye ameweza kuniweka kando akaishia zake just like that… kwamba sikuwahi kuingia moyoni mwake… na mimba yangu sijui ameitoa sijui ataitunza…aaah Sindi… yaani akijitokeza leo akasema Jerry nenda kariakoo pale ukamhubirie kila mtu namna unavyonipenda aisee niko radhi kuhubiri mapenzi yangu kwake wiki nzima’ Jerry akalalamika na Meddy akamcheka kwelikweli

Wakachangamka sasa na kupiga stori zao mbalimbali
8888888888888888888888

Wakati Jerry na Meddy wakimzungumzia Sindi asubuhi hii. Nyumbani kwa Dennis nako Nanny na Dennis walikuwa wakimzungumzia Sindi Nalela pia.
‘Umegundua saa ngapi kuwa hayupo?’ Dennis aliuliza katika hali ya kuchanganyikiwa
‘Nilipofika tu!... nilienda kumuangalia chumbani ili nimsabahi ndio nikakuta hicho kikaratai kikisema ameondoka na tusimtafute…. cha kushangaza akaondoka bila nguo zake… nahisi aliogopa  kuulizwa na mlinzi’ Nanny akaelezea alichojua na Dennis akachoka zaidi

‘umeongea na mlinzi?’ akauliza Dennis
‘amesema alitoka usiku…sijui kuna mgeni alikuja alipoondoka yule mgeni naye akatoka akidai anaenda kununua soda na ndio hakumuona tena’ Nanny akazidi kumchanganya Dennis ambaye sass alikumbuka wakati alipoingia Mlinzi alitaka kuongea naye ila hakumsikiliza. Alikuwa na jakamoyo lake alilotoka nalo kule mlimani city alikozinguana na Rebecca. Pengine angemsikiliza  Mlinzi usiku ule labda saa hizi wangekuwa wanajua pa kuanzia.

Dennis akamtazama Nanny kama mtu aliyechoka akili kupitiliza. Akalegeza hata tai aliyokuwa ameikaza barabara.

Sindi Nalela alikuwa alikuwa ameondoka nyumbani kwa Dennis Mazimbwe, akimkimbia Jerry Agapella kwa hofu kuwa angerejea kumtafuta. Laiti tu angeliujua ukweli wa mambo ulivyo!


…. ITAENDELEA….

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger