2
SINDI......NA LAURA PETTIE (2)
Asubuhi ya siku hii ilikuwa siku ya ibada kwa wakristo
walioishi kijiji cha mzimbuni, Ndani ya kanisa lililoezekwa kwa mabati chakavu,
ibada ilikuwa inaendelea na waumini walikuwa wamesimama wakiimba wimbo kwa
kutumia vitabu cha nyimbo ambavyo vilionekana kumilikiwa na waumini wachache
huku waliobaki wakiwa wamekariri beti za wimbo huo.
Mbele ya moja ya mabenchi ya mbao yaliyosimikwa ardhini
alisimama mama yake Sindi, akifuatiwa na Peter kisha Sindi, Maria na Alma,
marafiki wa Sindi pamoja na bibi yake
Sindi. Wakati waumini wengine wakikazana kuimba Sindi na marafiki zake walikuwa
wakiimba huku nyuso zako zikionyesha wazi akili zao hazikuwa eneo lile.
Maria na Alma
walicheka kichini chini na kukanyagana huku wakiibia kuwatazama Sindi na Nyanzambe
aliyekuwa amesimama mstari wa katikati wa mabenchi akiwa na mama yake. Kwa vile
alikuwa mbele kidogo, aliweza kugeuka na kumtazama Sindi kwa kuibia kila mara
huku Sindi yake akimtazama na kukwepesha macho kila Nyanzambe alipoibia
kumtazama na wakati huo huo wakiendelea kuimba wimbo uliokuwa ukiimbwa.
Kuibia kule kukakoma baada ya Mama yake Nyanzambe kumvuta
mwanawe sikio katika namna ya kuchekesha na kumtaka aiweke akili yake katika
kile kilichokuwa kinaendelea ibadani. Tukio lile lilifanya Maria, Alma
na Sindi wacheke kichini chini kiasi cha kuwafanya Mama Sindi na bibi
wawatazame mabinti hawa kwa mshangao na macho ya kuwaonya kuacha upuuzi wa kucheka
wakati wa ibada.
Ibada ilipoisha, waumini walitoka nje, wakisambaa huku na
kule kwa minajili ya kusalimiana, kutambulishana na wengine kuelezana hili na
lile. Mama na Sindi pamoja na mama mkwe wake walikuwa na wakizungumza na akina
mama watu wazima huku Sindi akiwa nyuma ya mama yake na hapo hapo akitazama huku na kule, macho
yake yakimtafuta Nyanzambe.
Alipomuona, alifungua kitabu cha nyimbo na kutoa bahasha kwa
uangalifu, akainama kidogo na kumpatia Peter, akimuonyesha Peter mahali alipo
Nyanzambe ambaye naye alionekana kutotulia kabisa akizungusha shingo yake huku
na kule.
‘Haya twendeni!...’ Mama Nyanza alimsemesha kijana wake, huku
akimuhimiza mdogo wake Nyanza kuangulia wakati huo akiwa ametoka ksalimiana na
mchungaji aliyeendesha ibada hiyo. Nyanza akakunja uso na kugeuza shingo huku
na kule
‘Nyanza!...’ mama yake aliita akisisitiza na akiwa ameshapiga
hatua mbili tatu. Mdogo wake Nyanza alitabasamu akionekana wazi kujua kaka yake
alikuwa akitafuta nini. Kwa unyonge akaanza kumfuata mama yake ambaye naye
aligeuka na kuanza kuondoka. Alipogeuka tena nyuma akamuona Peter akimkimbilia
na uso wake ukachanua kwa furaha. Peter alimfikia na kumpatia ile bahasha
iliyokuwa imekunjwa kunjwa mno. Nyanza akaipokea haraka na kuitia mfukoni,
akikipapasa kichwa cha Peter kama namna ya kumshukuru.
Akakaza mwendo kumharakia mama yake.
Njiani wakati wa kurudi nyumbani, Mama Sindi alitoa duku duku
lake akionyesha
wazi kutofurahishwa na tabia ya Sindi.
‘naona umeanza kusahau maadili ya ibada…’ alisema Mama Sindi
akigeuza shingo nyuma na kumtazama Sindi aliyekuwa bega kwa bega na bibi yake
‘Unamfundisha nini Peter…mnapocheka cheka kanisani kama
mwehu…’ aliendelea kugomba na bibi yake Sindi akamtazama mjukuu wake na
kutikisa kichwa
‘Mi najua alichokuwa anacheka’ Peter akadakia akitabasamu na
kumtazama Sindi ambaye alimkazia macho kama onyo la
kutosema alichotaka kusema
‘Alikuwa anacheka nini’ mama akauliza akiwa amemshika mkono
Peter na safari ya kurudi nyumbani ikiendelea.
‘Niseme nisiseme?’ huku akifanya mbwembwe za kitoto
akamuuliza Sindi ambaye aliendelea kumkazia macho. Peter akacheka kitoto na
mama yake akimtaka aseme bila hofu
Mazungumzo yake yakakatizwa na mlio wa honi ya baiskeli toka
nyuma. Wote wakasogea pembeni kuipisha ile baiskeli, na muendesha baiskeli
akasimama kwanza kusalimiana na akina mama Sindi
‘wameleta mbegu za mahindi, unapeleka kitambulisho unapewa
mfuko wa mbegu na mbolea gunia tatu…’ yule muendesha baiskeli akazungumza kwa
lafudhi nzito yenye Kiswahili kibovu bovu mara tu baada ya salamu na Mama Sindi
kumuuliza alipotoa magunia ya mbolea aliyopakia nyuma ya baiskeli
‘Wanagawia pale pale pa siku zote au ?’ Mama Sindi akauliza
‘wanatolea kwa mwenyekiti….kule ofisi za kilimo nasikia
pamejaa maji…mamvua yaliyonyesha jana….maji mpaka kule sokoni…’ mwendesha
baiskeli akaeleza zaidi na kufanya wote washangae.
‘Ile mvua ya usiku ndogo vile ndio maji yamejaa’ bibi yake
Sindi alishangaa
‘yamejaa acha kabisa….tangu yule mzungu azibage mtaro wa maji
na lile liukuta lake… mvua ikinyesha maji yote yanakusanyikia sokoni kule hadi
ofisi ya kilimo….’ muendesha baiskeli sasa akapanda vizuri baiskeli yake
‘Haya bwana…ngoja na sisi tukaangalie….’ Mama Sindi aliagana
na yule muendesha baiskeli ambaye alianza kunyonga baiskeli yake na kuishia
‘Sindi nenda nyumbani na Peter…mama hebu twende tukaangalie kilichopo uko….tusije
tukakosa hata mbegu tu na mvua ndio hizi’ Mama Sindi alitoa maelezo ambayo
Sindi aliyapokea kwa kutikisa kichwa na taratibu wakatengana Sindi na Peter
wakiendelea na safari huku Mama Sindi na mkwe wake wakigeuza walikotokea.
8888888888888888888
Sindi Nalela ni mtoto wa pili katika familia ya Mzee Nalela
iliyobarikiwa watoto watano. Sega Nalela
akiwa mvulana na kifungua mimba, baada ya kuhitimu kidato cha sita alikuwa
nyumbani akingoja kujiunga na chuo kikuu. Alishapata chuo jijini Dar
es Salaam lakindi ndio kipato cha mzazi wake
hakikutosha kumuweka mjini hata wa wiki moja sembuse kulipia gharama za
usajili.
Alikuwa katika hati hati ya kukosa kujiunga chuo kwa kukosa
pesa ya usajili uliokaribia laki tano ukiachilia mbali sehemu ndogo ya ada
ambayo alitakiwa kulipia wakati akisubiri bodi ya mkopo imkamilishie ada
iliyobaki na kumpatia pesa za kujikimu.
Sindi Nalela alikuwa mtoto wa pili, binti mzuri mwenye urembo
uliofubaishwa na umaskini uliokuwa ndani ya familia yao .
Pamoja na kuishia darasa la saba Sindi alifahulu kujiunga na kidato cha kwanza
shule ya wasichana msalato lakini hakuwanikiwa kwenda shule kutokana na
umaskini.
Alikaa nyumbani akilima pamoja na wazazi wake mpaka pale Mzee
wake aliponyang’anywa shamba na uongozi wa kijiji baada ya sehemu kubwa ya
mashamba ya wanakijiji kununuliwa na Mwekezaji wa kizungu bila wao wananchi
kushirikishwa. Tangia hapo hata ile pesa aliyokuwa akiitegemea ingempeleka hata
shule binafsi ilipotea kabisa, na Mzee Nalela alijikaba alivyoweza ili angalau
amsomeshe hata Sega.
Pamoja kukomea darasa la saba, Sindi alitamani kusoma zaidi,
alikuwa na ndoto ya kuwa nesi. Aliipenda kazi hii sana
akivutiwa na mama yake Alma ambaye alikuwa
nesi wa zahanati ya kijiji. Alipenda mavazi yake na kile kitambaa cheupe alichovaa
kama taji kichwani. Alipenda alivyokuwa mkarimu na namna
watu walivyomkimbilia palipotokea tatizo. Ndoto yake ya kuwa nesi ilipotea
taratibu na baba yake aliponyang’anywa shamba bila fidia ndio kabisa ndoto ile
ilipotea na kutoweka, hatimaye akakubali kuwa majaaliwa yake yalikuwa yanaishia
pale.
Tatizo la Sega kukosa ada ya chuo ndio lililozaa shida kubwa
kwake. Baba yake aliamua kumuoza kama mke wa tatu kwa
Mzee mfanya biashara kijijini hapo, Mzee Dunia Hatia. pamoja na kuhitai ada
mzee Nalela alikuwa na madeni mengi kwa Mzee Dunia hivyo kuyakamilisha yote
walikubaliana kuwa amuoze binti yake kwa Mzee Dunia kwa mahari ya kusamehewa
deni na shilingi milioni moja na laki mbili taslimu.
Kwa Mzee Nalela ambaye sasa alikuwa na kijishamba kidogo tu
cha kulima mazao ya chakula, shilingi milioni moja ilikuwa pesa kubwa sana
kwake. Angetoa laki sita za Sega na laki nne zingekuwa zake. Tayari alishapokea
laki mbili na milioni moja ilikuwa ikimsubiri Mzee Dunia arejee toka safari na
kumchukua mkewe na kisha kumalizia mahari nzima.
Sindi alitaka sana
kaka yake arejee shule, alitaka sana
kaka yake atimize ndoto zake lakini ukweli kwamba alipaswa kuliweka rehani
penzi lake na
kijana mwenzake Nyanzambe ulimuumiza sana .
Alimpenda Nyanzambe mno. Uhusiano wao ulikuwa unatimiza mwaka sasa, wakipeana
ahadi za kuoana na Sindi akuutunza uanawali wake kwa ajili ya Nyanzambe.
Akimuahidi Nyanzam kuwa mwanaume wa kwanza na wa mwisho maishani mwake.
Ahadi hiyo ilishaanza kwenda mrama, furaha kati yao
ilianza kupungua taratibu, Sindi aliumia sana
kila alipotaka kumwambia Nyanza ukweli wa mambo ulivyo sasa si kama
ulivyokuwa mwanzo. Alishindwa hata kumwambia kuwa mzazi wake alikuwa
amemtafutia mchumba sembuse kumwambia kuwa sehemu ya mahari ilishalipwa.
Miezi michache iliyopita alikuwa ameanza kujitolea kufundisha
watoto wadogo kusoma na kuandika. Wazazi wa watoto hao walimpati chochote
walichokuwa nacho kama shukrani. Kiasi kidogo alichopata
alikitunza kwa bidii na sasa alikuwa amemnunulia Nyanza shati zuri la mikono
mirefu alilovaa kanisani na kiasi kilichobaki alikifunga katika bahasha na
kuamua kumpatia mpenzi wake. Alimpenda sana
Nyanza kama ambavyo Nyanza alimpenda Sindi. Walikuwa vijana wadogo tu
waliopendana na kuwekeana ahadi ya kuwa pamoja, wakiwa wametoka katika familia
za kimaskini na wote wakiwa wamekwama kuendelea na masomo sababu ya umaskini.
Baada ya Sindi kulikuwa na mabinti wawili Danze na Denzi
waliokuwa mapacha na kisha kitinda mimba Peter. Hawa ndio walikuwa watoto wa
Mzee Nalela. Mzee maskini aliyeweza kujenga nyumba ya matofali ya kuchoma
iliyoezekwa kwa mabati mabovu yaliyositiriwa na nyasi pia. Mzee aliyepambana na
maisha kwa kadiri alivyoweza mpaka hapo alipofikia. Akianza na kilimo, kuchoma
mkaa na hatimaye kurejea katika kilimo sasa akilima mashamba makubwa ya watu
kwa malipo ya mapatano.
8888888888888888888888888
Nyanzambe Festo Mugilagila alikuwa mtoto wa mjane, mtoto wa
kwanza kati ya wawili wa mwanamke mjane ambaye mumewe aliuawa kijijini hapo na
polisi akituhumiwa kuficha nyara za serikali. Pamoja kutumia akiba yake yote na
kuuza sehemu ya mali
zake kutafuta haki. Mama Nyanza aliishia kukubali kuwa haki ipo mbinguni tu si
duniani!
Ndugu wa mumewe walimalizia sehemu ya mali zilizobaki na
akajikuta akianza vibarua vya kulima huku akifanya biashara ya ndizi mpaka
alipopata ajali ya kugongwa na pikipiki ndipo alipoachana na shughuli hizo na
kupata kazi ya kufanya usafi nyumbani kwa mzungu mwekezaji aliyekuja kijijini
hapo na kununua sehemu kubwa ya ardhi ambayo sasa ilikuwa inakodishwa kwa
wanakijiji kwa malipo.
Hellena Mama yake Nyanza aliifanya kazi yake ya kuhudumia
nyumbani kwa Mzungu kwa juhudi zote na
ndio kwanza alikuwa natimiza mwezi wa pili tangu aajiriwe. Kipato kidogo
alichopata hakikutosha kumsaidia kijana wake hata mtaji mdogo hivyo Nyanza kama
vijana wengine walikuwa wakilima mashamba yaliyokodishwa kwa pesa ndogo au
nyakato zingine alivua samaki na nyavu za kukodi pia na kuwakaanga.
nyanza alitamani kupata pesa za kununulia nyavu au hata pesa
ndogo ya kununulia ardhi ili alime au naye akodishe lakini kipato kilimpiga
chenga. Alitamani sana kumtunza
Sindi Nalela msichana aliyyeotwa na robo tatu ya vijana pale kijijini, msichana
aliyesemekana kuwa mzuri zaidi kuliko wote kijijini, msichana aliyesemwa kuwa
na nidhamu na utulivu kuliko wenzake lakini zaidi msichana aliyeonekana
kuhangaika na maisha, mwenye kujiamini na mcheshi.
Wanaume wengi walimtamani Sindi, walimpenda, walimuota,
walimfuata kwa mitego mbalimbali lakini Sindi aliweka wazi kuwa alikuwa msichana wa mwanaume mmoja tu, na
mwanaume mwenyewe alikuwa Nyanza, kijana masikini kabisa.
Kashikashi ya wanaume kumkimbizia Sindi, Nyanza aliiona na
ilimuumiza kwa vile alihofu Sindi angemuacha na kukubali kuwa na mtu mwenye
hali bora. Alijitahidi sana kutunza
pesa aizopata ilia angalau amnunulie Sindi hata mafuta ya kujipaka lakini pesa
haikukaa.
Mdogo wake alikuwa sekondari ya kutwa, nyumba waliyoishi
lilikuwa kama banda na walikuwa wamepanga baada ya
kutimuliwa na ndugu wa baba yake. kodi ya banda ilimtazama, mambo mengine yote
yalimtazama. alimhurumia mama yake mno hasa kutokana na maumivu ya kifua
aliyokuwa akilalamikia kila mara kutokana na ajali. Pesa za kwenda kufanya
uchunguzi zaidi hakuwa nazo. Nyanza alipambana kiume na maisha lakini hakuwahi
kuyashinda!
Jioni hii Nyanza alikuwa ameketi kwenye jiwe kubwa lililokuwa
kwenye muinuko, akitazama mashamba na mapori madogo madogo yaliyokuwa
yakionekana mbele yake. Alizitazama zile pesa zilizokuwa kwenye bahasha na kutikisa kichwa. Alizihitaji sana
lakini si kutoka kwa Sindi. Yeye ndio alipaswa kumpatia Sindi pesa kama
ile na si kuipokea toka kwa mwanamke. Alihisi unyonge zaidi. Wakati Sindi
alipomtumia ujumbe kuwa alikuwa na zawadi yake ambayo angempatia kanisani,
hakuwazia hata kidogo kuwa zawadi ile ingekuwa pesa. Alitulia katika lile jiwe
kwenye mlima mdogo akiwa ameketi na
kukunja miguu yake, akifanya mikono yake iliyoshika bahasha ililale juu ya
magoti yake na kunyooka kwenda mbele.
Aliyatuiza macho yake akitazama mbele, mawazo yakimchota na
kumletea uso wa huzuni zaidi. Alikuwa akimsubiri Sindi eneo lile na mara kadhaa
aligeuka nyuma na kuchungulia kama Sindi angetokea.
jua lilishasogea na kujenga kivuli kilichoanza kulikaribisha giza ,
wakati akitabasamu kwa huzuni na kuanza kukiteremsga kile kilima akamuona Sindi
akija kwa mbali akiwa anakimbia. Akakunja uso kwa mashaka ana yeye akiteremka
kwa haraka na kuelekea kule alikokuwa akitokea Sindi. Sindi akamfikia, akihema
na kutokwa na jasho jepesi na hapo hapo akinyoosha kidole kuonyesha upande wa
kulia na kule kuhema kukimzuia kuzungumza.
‘Kuna nini Sindi…?’
Nyanza aliuliza kwa wasiwasi akimchunguza Sindi
Sindi akameza mate kwa nguvu na kushusha pumzi kwa mkupuo
‘Kuna mtu…kuna mtu sijui amekufa sijui amekutw ana nini…yuko
kule tunakokutania wakati mwingine…’ Sindi aliongea akihema na hapo hapo
akionyesha woga
‘Mtu!....unamjua?’ mamcho yalimtoka Nyanza
‘Simjui….sijawahi kumuona maeneo haya….nilidhani uko kule
ikaamua kuanzia kule ili nikikukosa nije huku…wakati natoka pale ndio nikaona
nyasi kama zimeingia ndani hivi…’ Sindi akaonyesha namna
alivyoona nyazi zimelala katikati ya eneo lenye nyasi ndefu
‘…hebu twende’ nyanza akasema haraka bila kungoja maelezo
mengine ya Sindi. Wakaondoka wakikimbia kuelekea eneo la tukio. Walipofika
Sindi akamuonyesha mahali mwili wa mwanaume wa rika lao tu ukiwa umelala
kiubavu ubavu katika nyasi. Nyanza akanyata na kumchunguza kwa mbali na nyuma
yake Sindi akichungulia.
Nyanza akaokota kipande cha mti na kukinyoosha kumgusa nacho
yule mwanaume. Akaligusa bega na kumsukuma kwa nguvu kidogo akitumia kile
kipande cha mti ili apate kuuona uso wa yule mtu. Yule mtu akateleza kidogo na
uso wake ukaonekana, Macho yake yakifumbuka taabu na kuwatazama akina Nyanza.
‘uwiiii….’ Sindi akaruka kwa woga kama
mtu aliyetambaliwa na nyoka huku Nyanza akitupa kile kipande cha mti na kumvuta
Sindi mbali na eneo lile. Wote walitembelewa na wahaka, wakapatwa na kiwewe kwa
dakika nzima walisimama wakitetemeka na kutazama sehemu aliyolala kijana yule
kwa wasiwasi na woga.
Aliyelala pale chini alikuwa Jerry Kristus Agapela. Mtoto wa
balozi mstaafu na Mkurugenz wa kampuni ya mafuta. Agape Oil!
NI NINI KILITOKEA MPAKA JERRY KUWA KATIKA HALI ILE?….
JE SINDI ATAMUACHA NYANZA ILI AOLEWE
NA HATIMAYE KAKA YAKE ASOME?
USIKOSE SEHEMU IJAYO!.....NIACHIE MAONI
No comments:
Post a Comment