1
Watoto walikimbizana na kupigizana kelele za kimichezo,
Wanaume wa kila rika wakiwa wamejikusanya mahali wakizungumza na wengine
wakipata pombe za kienyeji huku wanawake na mabinti wakiwa makini na shughuli
za upishi katika nyumba zao. Ndege wa usiku hawakuacha kupiga miluzi na kuleta
hali ya kuvutia, hali ya kijiji, hali ya maisha ya ujamaa.
Umbali mfupi nje
kidogo ya eneo lile la kijiji, kijana wa rika la kati anaonekana akiyumba na
kutembea kwa shida. Mikono yake miwili ikiwa imeshikilia ubavuni, ubavu
unaovuja damu na kumpatia kijana yule maumivu makali kupindukia. Anaonekana
kulowa jasho pamoja hali ya ubaridi iliyokuwepo eneo lile. Anayumba akikwepa
matawi ya miti iliyokuwa inaning’inia hali kadhalika akijaribu kulifikia eneo
lenye miale ya moto aliyokuwa anaiona kwa mbali
toka pale alipokuwa.
Akasimama kwanza akihema kwa sauti na kwa kutumia mdomo, hali
kadhalika akiinama na kusikilizia maumivu aliyokuwa nayo ubavuni. Alionekana
wazi kutoweza kushindana na ile hali zaidi. akagugumia uchungu akitoa mkono
mmoja toka pale ubavuni na kuutazama akiwa amepinda mgongo vile vile.
Aliutazama mkono wake uliokuwa umejaa damu tupu ukitetemeka mbele yake,
akafumba macho kwa uchungu na kuurudisha kushikilia ubavu ule uliokuwa na jeraha
Akajiinua kidogo ili aweze kusonga mbele lakini lakini
maumivu yalimzidia na akajikuta akiserereka kidogo na kuishia kushikilia tawi
la mti ili asidondoke. Kishindo cha kuserereka kiliwafikiwa mabinti watatu
waliokuwa karibu na eneo lile. Mmoja akivaa nguo zake baada ya kujisaidia haja
ndogo na mwingine ndio akiwa amechuchumaa. Kishindo cha kuanguka kwa kijana
yule kilimfanya yule aliyechuchumaa aruke sambamba na wale wenzake ambao
walikuwa akimsubiri yeye.
‘Ni nini?’ yule aliyekuwa akivaa nguo ya ndani aliuliza huku yule
aliyekuwa anajisaidia akikazana kupandisha nguo yake na kujibu ‘Sijui….’ wakati
huo mwenzao akikaza shingo kuangalia upande mwingine kabisa
‘Mi narudi bwana….kama unamngoja Nyanzambe wako we mngoje…’
yule binti wa kwanza alimsemesha binti aliyekuwa akiangaza upande mwingine
‘Jamani msiondoke….atafika sasa hivi?’ aliwasihi wenzake
‘hicho kishindo umekisikia lakini?.... tuje kuliwa na simba
vichochoroni kisa mchumba’ako kha!’ akaanza kugeuka na binti aliyekuwa
akimsubiri mpenzi wake akamuwahi na kumshikilia huku yule mwingine akicheka,
naye akiwa amemshikilia yule aliyetaka kuondoka.
‘Sasa akija akanikosa je?’ akauliza kwa wasiwasi shingo ikiwa
imegeukia kule alikotarajia Nyanzambe angetokea
‘bora kipi…akukose hapa akuone kesho au akukose hapa akute
umeliwa na simba’ aliuliza yule msichana aliyekuwa ameshikiliwa na wenzake na
yule binti akakosa jibu. Uso wake ulionyesha wazi alitaka kumsubiri huyo
aliyekuwa akimsubiri lakini pia hofu ya kubaki pale peke yake ilimsumbua.
Ukimya mfupi tu uliopita kati yao
ulifanya kishindo cha pili cha kuanguka kwa yule kijana kiwafikie barabara na
hapakuwa na mjadala tena. Walitoka mbio kila mtu akitafuta nafasi ya kuchanja
mbuga kuliko mwenzake. Wakakimbia na kukutana nyuma ya nyumba na kusimama hapo
wakihema na kucheka kimya kimya, mikono ikiwa kifuani.
‘Hivi ni nini?’ mmoja akauliza akiwa ameinama na kushika
magoti huku akihema
‘Sijui…’ akajibu mwingine akitikisa kichwa hali kadhalika
yule mwingine akitoa macho kwa woga na kutazama kule walikotokea
‘Sindi ingia basi tuondoke wenzio…’ yule aliyekuwa ameinama
akamharakisha yule aliyekuwa na hofu, Akimtaka afungue dirisha la mbao la ile
nyumba. Sindi akalifungua na wenzake wakamsaidia kumnyanyua na kumsukumizia
ndani. Puh! akaaanguka kama mzigo na wenzake huku nje
wakatazamana na kucheka huku wakifunika midomo kwa viganja vyao. Wakaondoka
eneo lile kwa kunyata.
Sindi aliokota vitu alivyogonga na kuangusha wakati
aliposukumiwa ndani na wenzake. Mwanga wa kibatari uliokuwa juu ya stuli ndogo
chakavu ulimtosha kuweka sawa eneo lile. Akajifunga khanga yake vizuri na
kurekebisha kilemba. Akatoka mule chumbani na kutokezea sebuleni kulikokuwa na
wadogo zake waliokuwa wakifanya kazi za shule wakiwa wameketi chini na
kuizunguka meza ndogo katikati yao .
Akapita kwa mwendo wa haraka na baba yake aliyekuwa anasoma kitabu akamtazama
juu ya miwani aliyokuwa akisomea kisha akaendelea kusoma kitabu chake.
Sindi akaingia jikoni na kumkuta mama yake akisonga ugali kwa
juhudi zote kwa kutumia mikono miwili. ugali ulikuwa mkubwa na jiko lilikuwa la
kuni. Ilimpasa kukanyaga sufuria la ugali kwa utumia miguu yake yenye ndala ili
aweze kusonga kwa ufanisi.
Sindi alipoingia jikoni mama yake akasonga kidogo na kuachia
mwiko, akivuta uoande wa khanga na kufuta jasho. akashusha pumzi kwa nguvu zote
na kumtazama binti yake aliyetembea kinyonge na kwenda kuketi kwenye kigoda
mbele ya yale mafiga aliyokuwa akitumia mama yake.
‘haya nini…’ Mama yake akamuuliza, akijua wazi kulikuwa na
linalomtatiza mtoto wake
‘sitaki kuolewa…’ akajibu na kutazama pembeni na mama yake
akatabasamu na kuirudia shughuli ya kusonga ungali uliokuwa umeanza kuungulia.
Akasonga kidogo na kuipua sufuria la ugali
‘nipe hilo
sufuria la samaki hapo chini’ mama yake akamsemesha akimuelekeza lilipo hilo
sufuria. Sindi akanyanyuka na kulifuata, akalileta na kulibandika. mfuniko
ulikuwa juu ya sufuria la samaki ukafunika ugali. Mama yake akamtulizia macho
‘husomi…umri wako unaruhusu…kwanini usifurahie ngekewa
iliyombele yako Sindi?’
‘Mama….’ Sindi akaita kwa msisitizo akinyanyua mabega yake na
kuyashusha chini
‘….basi angekuwa mtu ninayempenda’ Sindi akalalamika na mama
yake aliyekuwa akitazama samaki kwenye lile sufuria, akanyanyua uso ukiwa na
ndita kadhaa na kumtazama binti yake
‘Nyanzambe!?’ mama yake akatamka katika namna iliyomshinda
Sindi kung’amua kama lilikuwa swali au mashangao.
Akabaki kumtazama mama yake kwa uso uliojaa masikitiko. Mama akatikisa kichwa
kulia na kushoto akisonya kidogo na kutazama nyuma yake kulikokuwa na kishindo
cha kiguu. Akatokezea Peter mdogo wake Sindi. Akiwa anatafua kalamu yake
mdomoni
‘…Mama baba anauliza mbona chakula hakifiki mezani?’
‘Baba au wewe ndio una njaa….kamuamshe bibi…naleta chakula
sasa hivi’ Sindi akamjibu mdogo wake ambaye aliukusanya mdomo wake na
kuupindisha kando akidhamiria kumdhihaki Sindi
‘Peter!...nikikushika ntakuchapa’ Sindi alikarahishwa na ile
dhihaka, akavua ndala yake na kumtupia Peter aliyekuwa ameanza kukimbia kurudi
sebuleni. Mama yao aliwatazama na
kucheka. Shughuli ya kupakua chakula ikaanza na nusu saa baadaye walikuwa
wakipata chakula cha usiku. Baba akiwa na ameketi kwenye kiti cha mbao na meza
mbele yake ikiwa na sahani ya ugali na bakuli la samaki na samaki mzima ndani
yake.
Kulia kwake, Mkewe mama Sindi, mama mkwe wake mama Sindi,
Sindi na wadogo zake wa kike wawili na mmoja wa kike walikuwa wameketi kwenye
mkeka wakishea ugali kwenye sinia na vipande vya samaki kwenye bakuli. Kushoto
kwake kulikuwa na kijana wa makamo naye akiwa ametengewa chakula kama
baba yake Sindi. Alikuwa Sega kaka yake Sindi.
Chakula kililika kimya kimya huku redio iliyokuwa
imenyanyunyiwa mkonga wake katika kutafuta stesheni ikisoma taarifa ya habari.
‘Peter baba mate hayo jamani….unakula samaki mbona hugusi
ugali’ Mama Sindi alimsema mwanawe wa kiume na kufanya waliokaa mkekani kucheka
kichinichini kana kwamba hawakutaka kuonekana wakicheka wakati kula.
88888888888888888888888
Kulipambazuka, anga likitakata kwa mawingu machache na ugavu
wa bluu wenye kupendeza. Ndani ya jiji la Dar es Salaam katika moja ya
maghorofa Masaki kulikuwa na hali ya kukosa utulivu. Mwanamke aliyekuwa ameketi
sofani alionekana kutoka kulia muda si mrefu na bado alikuwa akipangusa machozi
na kujaribu kutulia kama vile mumewe alivyokuwa akimuasa
akishirikiana na binti yao
aliyekuwa kando yake.
Mlango wa sebuleni ukafunguliwa na polisi watatu wakaingia
mmoja akiwa amevalia kiraia na wengine wakiwa na sare. Yule aliyevaa kiraia
alikuwa na radio call mkononi pamoja na faili dogo. Mzee Kritus Agapela
akasimama haraka na kusabahiana na yule polisi aliyevaa kiraia, akiwapuuza wale
wengine.
Mke wa Kritus na binti yake nao wakisimama na kumsogelea yule
polisi
‘aah..mmm…bado hatujapata fununu zozote za aliko kijana wako
ila…tumepata kiellezo ambacho nadhani kinaweza kutupa mwanga wa kujua anaweza
kuwa sehemu gani…’ Polisi yule aliongea taratibu na wasikilizaje wake
wakimtolea macho kwa hamu kubwa ya kusikia alichotaka kusema
‘….tumefuatilia kule alikoanzia safari na inaonekana itakuwa
amjeruhiwa kidogo….mpaka sasa tuna kiatu ambacho kinakuja na kikifika
tutawataka mkitambue kama ni chake…naaa…’ wakati akivuta
sentensi yake ili kupata neno la kumalizia sentensi yake Mzee Kristus
alionyesha hali ya kukereka zaidi
‘Stupid!....nimeshindwa kufanya shughuli zangu…..kila kitu
kimesimama kwangu….. familia hailali usingizi sababu ya suala hili na wewe
unaniletea habari ya kutambua kiatu?....kiatu?...Inspekta?’ Mzee Kristus
alifoka kwa ukali
‘Mzee tuna…’ alikatishwa tena
‘Sijali mnaleta kiatu ama bukta….i need my Son! ….my
son!...sio habari za viatu….sikuja kufungua jalada la kupotelewa na kiatu
polisi…. it is Jerry!...aliyepotea ni Jerry Kristus Agapela sio ndala wala
raba…’ akaondoka kwa mwendo wa jazba akiishia ndani na kuiacha familia yake
ikimtazama Inspekta kwa huzuni.
Yule polisi akaaga kwa unyonge kidogo, akiwa amefadhaishwa na
majibu ya Mzee Kristus. Alikuwa akifanya
kazi usiku na mchana akimtafuta kijana huyu aliyepotea katika mazingira ya
kutatanisha. Mzee Kristus alihitaji taarifa za kila hatua na kila alipopewa
taarifa hizo hakuonyesha kuridhishwa na nguvu iliyotumika kumsaka kijana wake.
Akaondoka na kumuacha yule mama na binti wake wakifarijiana
kwa huzuni…..
…..SAFARI IMEANZA UNGANA NAMI KATIKA SIMULIZI HII…..
Siwezi kusema lolote kwa sababu ndiokwanza mwanzo ila inaonesha mwanzo mzuri nategemea itakua nzuri kuliko karata tatu nitafurahi sana ikiwa hivo
ReplyDelete