Thursday, January 10, 2013

BARAZANI: ......MAMBO HAYAENDI??



Habari zenu wadau…..nafarijiiika sana ninapoona mnazidi kuongezeka taratibu! na ni matumaini yangu Mungu anawajaalia kwa kadiri ya kila mja na  gawio lake.

Nisizunguke tu kama tiara….niseme lililonileta hapa!....kweli kuishi ni kujifunza na unajifunza uyaongoze maisha yaliyo bora. Ukiwa unaishi tu bila kujifunza mwenzangu kaa chini kwanza urudie alphabet za maisha yako pengine kuna mahali umeruka alphabet muhimu!



katika safari ya maisha sidhani kama unategemea kila kitu kikuendee sawa….kila kitu kinyooke tu, yaani uuone mteremko mwanzo mpaka mwisho…..jamani si utaishi shimoni sasa….

maisha sharti  kupanda kidogo….upate hata cha kusimulia wajukuu zako…..ila sasa kuna wakati unaweza kuhangaika na mpando mwaka mzima. Yarabi salama kipindi kama hiki unaweza kukamatana uchawi hata na mama yako mzazi….shida juu ya shida, ukigusa hiki chali….ukibeba kile chini…ukigeukia huku ngumi….ukisema utazame kule konzi……mradi tafrani tupu!

Ni wakati kama huu wengi stress/ depression huwa zinatukamata kisawasawa. Roho za uchungu zinatujaa, kwanini mimi….kwanini mimi…sasa ulitaka yamkute nani? haya basi unasali mpaka unahisi magoti yanakufa ganzi, Mungu naye ndio kama vile unatumia lugha asiyoielewa. Unakata tamaa!

Ukisikia mtu kajiua au kajidhuru…..unamuona mjinga kwelikweli….taratibu hayajakugomea mwenzangu…..maisha hayajakununia ukajua kuna kukosa tu bila kupata. hayajakufika ndugu yangu…..maana kuna mhenga wa zamani mmoja yalimkong’ota  yapi sijui akili ikamnyooka barabara….akaona atuachie urithi wa msemo….MZIGO WA MWENZIO KWAKO KANDA LA SUFI….

Sasa wale wenzangu na mimi….inafikia mahali tunaitwa fungu la kukosa! yawe kwa mkono wa mtu, samahani wenye imani zenu msoamini uchawi upo na watu wanautumia kutesa wenzao nyamaza tu…..au yawe ndio majaaliwa kuwa unasumbuka na kusumbuka hola…mpaka Mungu aseme yatosha….USIKATE TAMAA!

Hayaendi ndio ila ndio yasikufanye utake kukatisha maisha, wala usichoke kukosa Kumuomba Mungu mwenye rehema maana anatoa kwa awamu na tulivyo wegi tumtumainiao, anapochelewa usichoke kumshtua, usichoke kumlilia, usichoke kumkumbusha na atakusikia tu!

Maisha ni kama vita, tunapigana kufa na kupona, hapo ulipo acha kulia, acha kufikiria mikosi inayokuandama, acha kusononeka na kukoda, acha kabisa kujiita fungu la kukosa, acha acha acha kusema Mungu amekuacha, acha kukisubiria kifo kama mkombozi, acha kuangalia waliofanikiwa wakikuringishia, acha kujiona hufai duniani…..

Mungu ana makusudi yake…..zidisha juhudi hata uanguke mara mia…simama futa vumbi….mwambie Mungu asante kisha songa mbele….yawezekana pale ulipoamua kuishia ilikuwa imebaki hatua moja ufikie utakako, uombako ama atamanipo.

MAMBO HAYAENDI…..ONDOA BREKI, BADILI GIA IKISHINDIKANA SHUKA USUKUME MRADI MAISHA YANASONGA MBELE

MUNGU AKUBARIKI WEWE UNAYEPITIA NYAKATI NGUMU….HAUKO PEKE YANGU RAFIKI…UKO PAMOJA NAMI, UKO PAMOJA NA MUNGU ANAKUJAALIA  JAPO UHAI….

Laura!!

1 comment:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger