Friday, November 28, 2014

UREMBO NA LAURA:.... DETOX WATER NA FAIDA ZAKE MWILINI....


Kwa rehema za Mwenyezi Mungu. Natumaini wasomaji wangu mu  wazima… kuwa tu na ule uzima ni jambo la kushukuru Mungu.

Leo nawaletea hiki kitu kinaitwa kuondoa sumu mwilini… ninaposema sumu simaanishi sumu kama ile ya panya… La hasha! Nazungumzia sumu, hizi takataka za mwilini.

Unajua na hii milo yetu tunayokula si ajabu tu kujisikia ovyo ovyo kila siku na ukapanga foleni kumuona dokta na ukaambiwa huna hata malaria. Lakini ndio mwili haueshi uchovu na maradhi yasoeleweka! 

Na hospitali hizi za siku hizi hawawezi kukuacha ukatoka bila kupewa dawa!...
Sasa hii kudetox mwili kwa maji , ndio kama kuupunguzia mwili kadhia na kuuimarisha. Nyumba inakarabatiwa seuze mwili, tena mwili wa binadamu! Hii si yakukosa ndugu yangu!

Zipo aina nyingi za detoxification…. Zipo dawa za vidonge, zipo dawa za hali ya kimiminika hasa kwenye bidhaa za Forever living na GNLD… zipo detox diet, na detox  ya maji ambayo mimi ndio nitaizungumzia maana ni nafuu mnooooo na rahisi sana kutengeneza!

Kwanza tujue DETOX WATER NI NINI?


Huu ni mchanganyiko wa maji na virutubisho kadhaa (matunda etc) vyenye nia ya kuusafisha mwili na mifumo yake. Ni kinywaji murua kabisa, chenye ladha  fulani tulivu na chenye manufaa makubwa mwilini mwako kuliko unavyofikiria.

FAIDA ZA DETOX WATER

1. Hukupa nguvu (energy)… ile hali ya kuhisi kuchoka choka bila sababu  hupotea kabisaaaa

2. Huondoa ‘sumu’ mwilini. Tunajua mwili hujisafisha kwa kutoa taka kupitia jasho n.k lakini unapodetox mwili unaondoa hata zile taka ambazo kwa namna moja ama nyingine hazikutoka ipasavyo. Yaani kama ni usafi basi ndio umeamua kuchukua brashi sabuni na maji… full kutakata!!



3. Inapunguza uzito… wale wenzangu na mie wanaofuata masuala ya diet… Detox water inakusaidia kupunguza kilo pia na mbali na hayo inaondoa ile hali ya ngozi kusinyaa unapoanza kupungua. Hapa nina ushuhuda binafsi

4. Inaongeza kinga ya mwili… kuna watu huwa hawamalizi wiki bila kuugua ugua, utasikia mara tumbo, mara mafua, mara kichwa, macho kizunguzungu. Hii inamaanisha mwili wako hauhimili magonjwa madogo madogo. Hujawahi kuona mtu anapita kwenye vumbi dakika tu mafua yanamuanza na mwingine atatotaka hapo kawaida tu… ina maana kinga ya mtu wa pili iko juu.

5. Inakupa ngozi murua!.... Detox water ni nzui kwa afya ya ngozi. Sikudanganyi! Ni nzuri mnoooo maana pamoja na kukusaidia kunywa maji kwa wingi pia kile kilichomo kwenye maji kinasaidia sana kung’arisha ngozi yako.

6. Inakuwezesha kunywa maji kwa wingi…. Kuna watu kumaliza lita moja ya maji ni shughuli nzito kwa madai kuwa maji hayana ladha… Sasa Detox water inakusaidia sana kukuwezesha kunywa maji mengi itakiwavyo maana yana ladha fulani utataka kunywa kila muda… na mbali na hayo maji ni dawa nzuri sana ingawa watu wengi wanaidharau….

Hata kama utapaka vipodozi vya mamilioni kama huna utaratibu wa kunywa maji bado ngozi yako itakosa mvuto tu na ndio utakimbilia kujing'arisha kwa vitu vya kuchubua! Maji ni kila kitu katika urembo na afya! 
Sijui kwanini watu wanangoja waandikiwe hospitali kuwa wanywe maji mengi!

7. Inaleta mabadiliko chanya mwilini…. Trust me kadiri unavyotumia haya maji kuna mabadiliko utayaona mwenyewe mwilini mwako.  Hii ni Lazima!

8. Inaleta pumziko la akili…. Detox water inakupa relaxation…. Unapotoka katika mihangaiko yako na kuamua kupumzika huku ukipata kinywaji hiki nyumbani…. Akili hupata pumziko zuri sana. Zipo njia nyingi za kupambana na stress za maisha na hii ni moja wapo. Unapoweza kuishinda stress hakika maisha lazima utayatazama katika matazamo chanya!

9. Utajisikia mwepesi!.... kadiri  unavyotumia utausikia mwili una wepesi fulani…. Yaweza kuwa ni kupungua kwa kilo, ama kupungua kwa stress ama kwa kuona kuwa unachotumia kinaleta mabadiliko chanya!

10. Mwisho Detox water inakupa pumzi safi…. Watu wenye vinywa vinavyotoa harufu na jasho kali la kwapa. Detox water ni tiba nzuri sana na kinga pia!... unakwenda haja ndogo mkojo msafi kweli... unaanzaje kupata UTI jamani!

MATOKEO 
wakati wa kutumia Detox water

Yes! Unapoanza kutumia haya maji kuna hali fulani utaipata… unapaswa kujua hizi hali ili kuondoa mshtuko au hisia mbaya kuwa maji yanakudhuru. Hapana ndio hasa yanavyofanya kazi mwilini. Maana yanaenda kushtua sehemu mbalimbali ndani ya mwili na kuongeza utendaji kazi. Hivyo si ajabu utakapo anza kutumia ukapata dalili ziafuatazo

-          Kuhara… Hii ndio dalili kubwa kua mwili unajisafisha. Sio ile kuhara kama kipindu pindu. Hapana! Ni ile safari za chooni zitazidi sio kwa kukojoa tu bali kwenda haja kubwa laini pia
-          Unaweza hisi kichwa kinauma… ni kawaida na hali hii itapotea mara moja
-          Koo linaweza kupata hali ya kukaza kidogo au kupatwa na kikohozi kidogo
-          Unaweza hizi kuchoka!... 
yes kuchoka zaidi! 
Lakini baada ya muda mfupi tu haya yote yatatoweka na utajisikia vizuri mnoooooo! 
yaani sana...mnashangaa watu wengine hawazeeki...siri ndio kama hizi
safisha mwili jama!

Kumbuka tu kuwa, Hali hizi sio lazima zije kwa pamoja. Inategemea mtu na mtu. Na pengine unaweza usipate hata hali moja kulingana na namna mwili wako ulivyo. Japo mara nyingi asilimia kubwa  hupata tu hali ya kwenda haja kila mara kwa siku za mwanzo

UTENGENEZAJI WA DETOX WATER.
Hii ninayokupa hapa ni moja tu ya aina za detox water ziko nyingi sana

UNAHITAJI
-          Maji ya kunywa lita 1-2

-          Tango kubwa moja au Tikiti maji ½  au 1


-          Majani  ya Mint –
Haya majani kama wewe ni mpishi mzuri huwezi kukosa kuyajua bwana!
Walio Dar haya majani yako teeele kariakoo na nadhani
katika masoko mengi tu huwa yapo

bahati mbaya sijui kwa Kiswahili yanaitwaje,  (ANAYEYAJUA ANISAIDIE) ila ni majani fulani madogoma dogo yanatumiaka sana kwenye upishi… ukienda sokoni yapo katika mafungu mafungu madogo madogo na ukipika chakula ukayaweka yana harufu nzuri sana na ladha ya aina yake. Tumia kupikia nyama weweeee...utajilamba hahahahaaaa!

-          Tangawizi..imenye ndio ukate


-          Limao 1 au zaidi ukikosa limao basi hata ndimu. 
kulingana na wingi wa maji yako na ladha uitakayo


Ila Limao ni bora zaidi.

-          Chupa moja la kutosha kiwango cha maji yako. Chupa au jagi liwe na mfuniko, ni vema ikiwa chupa au jagi  la kioo ila ukikosa hata ya plastiki ni poa tu.



JINSI YA KUTENGENEZA

-          Osha na maji safi, kisha Katakata tango lako bila kumenya kama ni tikiti maji basi ondoa zile mbegu zake na ulimenye
-          Menya tangawizi na uioshe pia, kisha kata kata vipande

-          Osha limao au ndimu yako na kata vipande

-          Osha mint yako na uchukue vijani 10-15…umewahi kuchambua mchicha?... basi vile unavyobakisha kule mwisho na vijani vyako vibaki hivyo

-          Vyote hivi tia ndani ya chupa kisha mimina maji yako

-          Funga vizuri na utikise kidogo kisha weka kwenye friji, wengine huweka barafu pia

-          Laza maji yako humo mpaka asubuhi siku inayofuata

-          Anza kunywa glasi kwa glasi au mrija Lol!

-          Unaweza kuyanywa kwa siku mbili kama ni mvivu wa kunywa maji

-          Ila nakushauri uyamalize ndani ya saa 24

-          Kunywa haya maji kwa siku 14 mfululizo na ukishindwa basi fanya kila wikendi unaposhinda nyumbani

-          Watakaofuata siku 14 mfululizo baadaye  unaweza kuanza kuyanywa mara mbili/ tatu kwa wiki kulingana na nafasi yako ila nakuhakikishia utajijengea mazoea mazuri ya kunywa maji kwa afya ya mwili wako.

-          Mabaki yale ya tango au tikiti na hata limao unaweza kuvitafuna taratibu kila unapokunywa maji.

Kwanini utumie gharama kubwa sana kusafisha mwili, kutibu magonjwa  madogo madogo wakati vipo vitu vya gharama nafuu kabisa tena homemade tu vya kukuepushia hiyo kadhia!!.... ukijua faida ya tikiti mwilini, tango, mint, tangawizi, limao na maji huwezi acha jaribu hii kitu!

Hii ndio detox water niliyokuletea leo. Natumaini kuna kitu umejifunza toka kwangu

Nikutakie siku njema!
Na karibu tena katika safu hii ya urembo na Laura!!


4 comments:

  1. ubarikiwe Dada Laura. napenda sana makara zako za urembo na natamni nikuone. maana mara nyingi nikisoma makara zako napata kitu cha maana sana.

    ReplyDelete
  2. Asante Dada Mimi pia natumia iyo na nakaribia wiki sasa, nikimaliza iyo chupa moja huwa naongeza majj na kunywa tena na tena sinywi maji mengine yoyote. Ila Mimi hua nailaza kwenye sakafu maana sina frij

    ReplyDelete
  3. Je yanafaa kwa mama anayenyonyesha?

    ReplyDelete
  4. Ahsnt san kwansim zur mung akubariki

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger