Sunday, March 16, 2014

SINDI...NA LAURA PETTIE (60)

60

Walitembea hatua kwa hatua wakielekea kwenye meza moja iliyokuwa kwenye kona. Meddy akamvutia kiti Nadina na kumuonyesha ishara ya kuketi. Robo tatu ya watu ilikuwa imewatumbulia macho wao kiasi cha kumfanya Pamella atazame pembeni katika namna ya kuonyesha kutofurahishwa na ile hali ya watu kumshangaa Nadina pasipo sababu maalumu.
‘Huyo binti ni nani?’ Santina alimuuliza tena Pamella ambaye hakujibu kitu zaidi ya kushusha pumzi na kumtazama Nadina kwa macho ya uadui. Msema chochote akakamata kipaza sauti na kuomba waalikwa washiriki kitu kilichokuwa mbele yao.


Aliwaomba waalikwa watazame kwenye ua dogo walilovishwa wakati wakiingia ndani ya ukumbi. Nyuma ya hilo ua kulikuwa na namba, na kama namba yako itatajwa itakupasa kutimiza kile utakachoambiwa.

Watu wakapiga makofi safari wote wakiwa wameketi kwenye viti, huku Bi. harusi na mumewe wakiwa sehemu yao wakifuatilia hiyo burudani. Meddy alikuwa ameketi kando ya Jerry na Pamella alikuwa na mpambe wake mwingine.

Zikatajwa namba mbili tatu, mwingine akiambiwa aimbe kiitikio cha wimbo fulani, mwingine akiambiwa amuinue mtu yoyote aliye ambatana naye na kumtambulisha kwa watu mradi ilikuwa burudani ya kutosha. wakati wakikaribia kuumaliza huo mchezo MC akasema sasa alikuwa anaichagua namba ya mwisho.

Akachagua moja ya karatasi za namba zilizokuwa juu ya meza kwa wingi, akaifungua na akaitaja hiyo namba akiongeza na mbwembwe kuwa namba hiyo inaenda sambamba na zawadi ya jumla kwa waalikwa ambayo itachukuliwa na mtu mmoja. Hili tangazo lilileta ukimya kwanza kutokana na wengi kuchungulia maua yao na kuangaza huku na kule kumjua mwenye hiyo namba.

MC akarudia tena na tena  kuitaja kabla ya Meddy kunyanyuka polepole na kuibua vicheko na makofi ukumbini. Akatembea kwa madaha kumfuata MC, alipomfikia MC akaokota kikaratasi toka kapuni na kumsomea
‘kuna boksi la apple juu ya meza, chukua boksi hilo na umpe mtu unayempenda sana aliye hapa ukumbini…na mtu atakayepokea hilo apple alifungue na kutusomea kilichomo’ MC akazungumza akitabasamu na akimuonyesha Meddy mahali lilipo hilo boksi. Meddy akalifuata na kusimama nalo kama mtu aliyekuwa anawaza wapi pa kulipeleka.

Pamella na Santina wakatazamana. Santina akitabasamu pengine akidhani Meddy angelimfanyia surprise ya kumpelekea lile apple na kufuta mitafaruko yao.

DJ akaachia wimbo wa taratibu wakati watu wakimtazama Meddy alivyokuwa anaangaza macho huku na kule kisha taratibu akanyanyua mguu na kuanza kupiga hatua. Camera zikimmulika, screen kubwa zilizokuwa ukumbini umo zikimuonyesha yeye na boksi lake. Mwanga wa taa za wachukua camera ukielekea kule alikokuwa anaelekea. Shabash!

Camera ikammulika Nadina, Mwanga wa taa ukammulika Nadina, Screen zote ukumbini zikammulika Nadina. Kwa dakika moja nzima kitu kama msisimko kiliwapitia watu.
Namna alivyokuwa anamtazama Meddy kwa mshangao, na vile alivyokuwa amepambwa na kuvutia kilichokuwa kinaoonekana  kwenye screen kilitosha kuwafanya wanaume wamuonee wivu Meddy na wanawake watamani kuwa katika ile nafasi ya Nadina.

Akamfikia na Nadina akawa bado ameduwaa kitini mpaka pale Meddy alipomfuata kando yake na kupiga goti moja chii mithili ya mtu anayechumbia. Makofi yakalipuka ukumbini.
Nadina akajikaza lakini alikuwa natetemeka vibaya mno muda ule. Akalipokea boksi huku bado akimtazama Meddy anavyonyanyuka na kusimama kando yake. Akayarudisha macho kwenye boksi na sijue la kufanya.
Hakuwa hata amempa mawazo MC wakati akiongelea lile boksi. Akalitumbulia macho tu na Meddy akagundua Nadina alikuwa hajui cha kufanya. Akamuinamia na kumnong’oneza alifungue na kusoma karatasi iliyomo.

Kwa mikono inayotetemeka akalifungua boksi na kukumbana na maapple kadhaa ndani yake kabla ya kuliona karatasi hilo.
Akalichukua na kulifungua. MC akiwa ameshakaribia na kumuwekea kipaza sauti karibu na mdomo.
‘Huduma yoyote utakayochagua, utaipata bure kwa miezi sita toka MARINO Collection & Hair Salon’ Nadina  akasoma kwa sauti ya kutetemeka kidogo lakini pasipo kukosea. Akatabasamu na kuruhusu makofi huku watu wakicheka maneno ya utani aliyoyatamka MC kwa Nadina.

Kwake yeye Nadina, zawadi ile haikuwa na maana sana. Hakuijua hiyo Marino wala ughali wa huduma zao au ubora wao, wala hakujua huduma hizo ni zipi. Alitabasamu tu kukamilisha ile kazi.

Sherehe zikarudi kwenye mstari, akina Santina wakiwa wamekosa hata raha ya kwenda kujipakulia chakula, akina Fiona wakijificha migongoni mwa watu kama nyumba ya kobe na Dennis Mazimbwe akinyanyuka taratibu na kuondoka ukumbini pasipo kula, mwenye harusi akikosa amani mara kadhaa alipomtazama Nadina ambaye naye alimtazama tu huku mara kadhaa akitabasamu.

Baada ya chakula, kutoa zawadi, na mengineyo ya muhimu muziki ulishika kasi, watu walijimwaga ukumbini kucheza na kusalimiana na watu waliofahamiana nao.
Nadina alishaomba kuondoka, kwake yeye pale hapakuwa mahala pake, alihisi utofauti mkubwa kwa kuwaangalia watu na mavazi yao, vyeo vyao na hata rangi zao. Japo alifanana nao kwa nje kutokana na mavazi ya gharama aliyokuwa amevaa lakini moyoni alihisi hakustahili kuwa pale.

Meddy akaagana na Jerry na kuamua kuondoka pamoja na Nadina badala ya kumuitia taksi. Akamuweka Nadina ubavuni na kumleta mbele ya Pamella. Akamtambulisha kama rafiki yake. Pamella akajitutumua kutabasamu wakati akiupokea mkono wa Nadina ambaye tabasamu lake tulivu liliashiria ushindi Fulani. Santina hakuupokea mkono wa Nadina lakini bado Nadina alitabasamu tu kuonyesha hakukwazwa na ile hali.

Baada ya maongezi mawili matatu, Meddy aliguswa begani na kugeuka
‘Mr. Salmon!’ akashangaa huku akimuachia Nadina na kuushika vema mkono wa huyo mzee aliyemgusa na kumgeuza.
Mzee Salmon, akamtazama Nadina mabaye alimsalimia kwa salamu ya ‘Shikamoo’ iliyokwenda sambamba na goti la heshima. Mzee akacheka na kuiitikia kifahari kana kwamba alikuwa hajapata kuisikia salamu ile muda mrefu.

Wakataniana kama ilivyoada na hapo hapo akisalimiana na akina Jerry, Pamella na Santina kabla ya kujirejesha kwa Meddy kama mtu mwenye kitu cha kusema
‘Binti anaitwa nani?’ akauliza Mzee Salmon
‘Nadina’ Meddy akajibu haraka akijua wazi Nadina asingejibu haraka
‘… Amewahi kufikiria kuwa mtangazaji wa redio au Tv?... sababu mpaka dakika hii nimeshmuweka kwenye listi ya waajiriwa wangu’ Mzee Salmon akatania na kuzusha vicheko. Alikuwa Mkurugenzi na mmiliki wa kampuni inayoendesha kituo maarufu cha luninga na redio. Moja kati ya vituo vilivyokuwa vikitajwa kama vituo vya kisasa vyenye malipo mazuri. Ilikuwa kazi mno kupata ajira katika kituo chake.

 ‘…wakati anaisoma ile karatasi…I was like… this is it!..perfect…unique.. amazing voice of the moment!’ Mr. Salmon akazungumza kwa bashasha akiwaacha midomo wazi Pamella na Santina. Nadina mwenyewe akimtazama tu na kulivuta tabasamu la kuona yote yale kama ndoto.

Akatoa business card na kumpatia Meddy.
‘Wiki moja ya kufikiria ofa hii…’ akaonyesha userious mwingi kwenye kauli yake kiasi cha kumshangaza Meddy mwenyewe. akaitikia kwa kichwa na kumtazama anavyompa mkono Nadina na kuagana nao. Meddy na Nadina wakatazama  na kucheka.

Wakaondoka taratibu na kulifuata eneo la kutokea. Pale getini wakakutana na watu kadhaa waliokuwa wanasalimiana. Wengi walichana na mazungumzo yao na kusalimiana na Meddy.
‘… kuna matangazo ya nguo kwenye magazine yetu ya mwezi ujao, kama hutajali njoo tufanye kazi pamoja…kwa kila nguo utakayovaa tunakulipa pesa nzuri sana’ mmoja wa wamiliki wa magazine kubwa nchini alizungumza na Nadina, akivutiwa na mvuto alionao binti huyu.
Business card ikatua mikononi mwa Meddy ambaye hakukataa kuipokea ila aliomba muda tu wa kufikiria hilo. Wakaondoka na kurudi nyumbani, wakiacha shamra shamra za sherehe ya harusi ya Jerry Agapella na Pamella Okello zikielekea ukingoni.
8888888888888888888888888888

Anga la bluu, Jua limshachomoza, ni asubuhi iliyobarikiwa hewa safi ya kuvutia na uangavu wa kupendeza. Pamella Okello Agapella anaamka asubuhi hii akiwa mtu mpa. Mke halali wa Jerry. Akiwa hapo kitandani anazitazama pete zake zilizopangana vyema kidoleni pake na kuzifurahia. Anatabasamu zaidi anapoligusa tumbo lake. Mimba yake inakua, anangoja tu wakati muafaka amueleze mumewe kuwa alikuwa na mtoto wake tumboni mwake.

Anaamka taratibu akinyoosha na kuangalia vizuri mazingira ya kile chumba cha hoteli walicholala na mumewe. Anatabasamu anapoziangalia nguo za Jerry zilizokuwa zimetundikwa kwenye sofa dogo mbele ya kitanda. Anawaza ndivyo atakavyokuwa anaziona kila siku kuanzia siku ile. Anatabasamu zaidi na kujisikia hali Fulani ya fahari.

Wakati akiwaza haya, Jerry anatokea bafuni akiwa amejifunga taulo. Anamatazama Pamella na kutabasamu
‘Mume wangu…’ Pamella anamuita katika namna ya kujipa mamlaka kuwa sasa kweli Jerry alikuwa mumewe. Jerry anamfuata kitandani na kumbusu, wanabusiana kwa sekunde kadhaa kabla ya Jerry kujiinusha na kulifuata sanduku lililokuwa kabatini.
‘Kabla hatujaenda honeymoon nahitaji kuweka sawa kitu mahali… natoka kidogo nitarudi baada ya masaa mawili hivi’ Jerry anaongea akitoa Tshirt na kuanza kuivaa

‘…babe make sure unarudi kwa wakati, sitaki kukaa mwenyewe kabisa…and… hivi… yule binti aliyekuja na Meddy unamjua?’ Pamella akamuuliza Jerry huku akimtazama anavyozunguka huku na kule akijiandaa
‘ yeah namjua…’ Jerry akajibu akivaa suruali yake
‘who is she to Meddy?’ Pamella akauliza akikunja uso na Jerry akatabasamu
‘Usiniambie unatarajia Meddy atakuwa msela msela maisha yake yote’ Jerry akamjibu
‘..No!...i mean amemtoa wapi… ametokea wapi?’ Pamella akakazia maswali yake ya kutaka kujua Nadina alikotokea
‘Hayo maswali ayaulize mama yake Meddy sio wewe babe… otherwise huwa ni vema umuulize Meddy mwenyewe’ Jerry akakwepa kumuelezea Nadina kwa vile tu hakutaka kusema Nadina alikuwa msichana toka danguroni. hakutaka kulizungumzia hilo kama Meddy mwenyewe hakuwa amelisema kwa Pamella ambaye pia ni rafiki yake wa karibu tu.

‘Haelekeo kumfaa Meddy…’ Pamella akatoa dukuduku lake na Jerry akageuka kumtazama tu bila kuongeza neno. Wakaagana na Pamella akabaki mwenyewe. Lile tabasamu likipotea, akajirudisha nyuma na kujibwaga kitandani kama mzigo, akaitumbulia macho dari, akili ikikimbilia mbali zaidi. Akakumbuka!

‘… toka nimesema toka… toka… toka… una pa kwenda au huna mimi sijui…’ Pamella alikuwa anamwambia Nadina aliyekuwa amempigia magoti na kumsihi kwa machozi asimfukuze pale nyumbani kwa Patrick alikokuwa naafanya kazi za ndani.

Pamella akakusanya vifurushi vya Nadina na kuvirusha nje ya geti, mfuko wa plastiki ukichanika na nguo kutawanyika hapo nje. Akarudi pale alipokuwa amepiga magoti Nadina akilia kwa uchungu.
‘…dada mimi sijalala na shemeji… najiapiza na Mungu ananiona mimi… dada mimi nitaenda wapi?...’ Nadina alikuwa anaongea huku analia wakati akiishika miguu ya Pamella ambaye alimpa teke akimtaka asimguse.

‘Na nisingemkuta anakushika je?... ungeniambia?... Malaya kubwa wewe hebu fuata takataka zako nje…mbwa we…’ Pamella akamvurumushia matusi mengine ya nguoni wakati Nadina akijieleza. Alipoona haeleweki akamshika na kuanza kumburuza, akamburuza akiwa amemkwida kama mwizi na kumsukumia nje.

Nadina akaangukia nje kama mzigo. Akaomba apewe hata nauli kwani mshahara wake wa miezi miwili alikuwa nao bosi wake Patrick Mazimbwe aliyemuomba amtunzie na siku atakapouhitaji basi angeuomba. Pamella akamsonya na kumwambia anampa dakika tano na kutoweka na akimkuta hapo nje atampigia kelele za mwizi. Kwa kuogopa kuchomwa moto bila hatia Nadina akanyanyuka na kukusanya vitu vyake na kuondoka.

Kumbukumbu hii ilikuja vizuri kichwani mwa Pamella. Akikumbuka siku aliyomkuta Patrick anambembeleza Nadina awe mpenzi wake. Aliyasikiliza maongezi yote na kuona yote na alijua wazi Nadina hakuwa na kosa kwani hakuelekea kukubaliana na Patrick.

Aliona njia pekee ni kumtimua Nadina wakati Patrick akiwa hayupo na ndivyo alivyofanya. Kumuona Nadina kwenye harusi yake, akiwa amependeza na mbaya zaidi akiwa na Meddy rafiki yake kuliivuruga akili yake mno. Mpaka dakika ile alikuwa bado na hali ya kutoamini kama ni Nadina ndiye aliyekuwa amemuona.

Akavuta pumzi, akihisi kuumwa kichwa ghafla, Nadina angemueleza ukweli Meddy na Meddy angelimchukulije na Meddy angemueleza Jerry kilichotokea uko nyuma Jerry angemuona yu mwanamke wa aina gani. Hakutaka kuanza kutia ndoa yake doa la kuonekana si mwanamke mwema!

Akawaza na kuwazua, akaamua ilimpasa kumuona Nadina na kuongea naye iwe kwa heri au shari!

Mwenye mawazo asubuhi hakuwa Pamella peke yake, Fiona Agapella alikuwa mezani, chai ya asubuhi ikiwa kama shubiri. Haikupita kooni kabisa. Siku ya jana haikuwa njema kwake. Kristus alikuwa amemtamkia maneno makali sana na kule kumuona mtoto wa Adella, dada yake, ndio kulimvurugia siku zaidi.

‘Kuhusu Agapella…pengine ni hasira tu… tumuongelee Nadina’ Iloma alijaribu kumpa moyo na Fiona akamtazama kana kwamba Iloma hakujali hisia zake
‘Sikuwahi kufikiria Nadina yu hai bado… sijalala… nimeweweseka usiku mzima… amefikaje kwa Meddy?... anafanya nini?... ana maisha gani?.... nimemkumbuka na Adella, sijui yuko wapi dada yangu… sijui kma nina cha kumjibu kuhusu mtoto wake aliyeniachia bila kumpa hata jina’ Fiona akakisukumia mbele kikombe cha chai na kunyanyuka. Akitoka mezani na kwenda kuketi kwenye sofa. Iloma akamfuata na kuketi kando yake.

‘…Mtafute uzungumze naye…yaliyopita si ndwele’ Iloma akatoa tena wazo jepesi jepesi wakati Fiona akijiinamia na kukumbuka kitu

‘Lala hapo ukichoka kufa tu… mi’ hela za mchezo sina kabisa’ Fiona alikuwa anamjibu Nadina aliyekuwa amelala kitandani akionekana mgonjwa
‘Mama naumwa..’ akalalamika na Fiona akamtazama akimsonya
‘….wewe mwanamke mwenzangu sasa, ingia mtaani usake pesa za kukuweka mjini..huu ujinga unaoniletea hapa na ushakuwa mtu mzima mi siuwezi… kuna mabwana kibao hapo baa jirani… akili kichwani mwako…vinginevyo lala hapo ukichoka kufaaa’ Fiona alimjibu bila tone la huruma.

‘ Au nikusaidie!... subiri’ Fiona akatoka zake akimuacha Nadina anaugulia pale kwenye godoro chini. Aliporejea akarudi na mwanaume, akamuonyesha Nadina alipo huku akimwambia Nadina pesa hiyo utajua chaa kufanya upate hela ya hospitali na inayobaki aikabidhi kwake.

Nadina akatokwa tu na machozi na hata mwanaume mwenyewe alimuonea huruma. hakumfanya chochote zaidi ya kumpatia pesa tu na kutoka. Nadina akenda hospitali. Aliporejea Fiona akaomba kujua pesa iliyobaki ilipo. Nadina akampa elfu moja ambayo kwa Fiona aliona kama dharau. akamvuta na kumkung’uta kwanza.

usiku wa siku ile Nadina akaona pale palikuwa jehanamu. Akakusanya vitu vyake na kuishia zake mitaani. Ikawa ndio siku ya mwisho Fiona Agapella kumuona na kumsikia Nadina. Miaka 12 ilikuwa aimepita!

Jana akamuona, akamuona Nadina tena katika muonekano uliomduwaza. Wakati akimsimulia Iloma alichokuwa anakikumbuka. Simu ya Fiona ikaita. Akaichukua toka mezani ilikokuwa na kuipokea.

‘Niniiiii…weee…ngoja kwanza…niniii?’ akaiteremesha simu huku akiwa na hali ya kuchanganyikiwa. iloma akamtolea macho
‘kuna nini?’ kwa wasiwasi akamuuliza
‘Eti Agapella amekusanya vitu vyangu vyote na kuvipakia garini… niseme niko wapi waniletee… hivi hii ndio talaka?... Kristus ananidhalilisha hivi  mimi?... Leo Agapella ananifanyia hivi mimi?’ Fiona alikuwa naalengwa na machozi. mishipa ya kichwa ikimtutumka. Akanyanyuka na kuelekea  chumbani. Wakati huo simu ya Iloma ikiita kule juu ya meza ya kulia chakula.

Akaifuata na kuitazama. Mpigaji alikuwa Agapella aliyem ‘save’ jina lake kama Boss. Akaipokea na kusikiliza huku akitazama nyuma yake mara kadhaa
‘…nimeondoka kila kitu kinachomhusu mke wangu wa zamani…now the house is all yours Iloma…na process za talaka zitaanza soon kama hutaniamini baada ya hili sijui nifanye nini uniamini sasa’ Agapella alikuwa anaongea taratibu, sauti ikionyesha furaha Fulani kama mtu aliyeutua mzigo.

 Iloma hakujibu kitu alitulia na simu mkononi wakati akigeuka na kumtazama Fiona aliyekuwa amerejea kwenye kochi akihangaika kumpigia simu Agapella huku akilia. Iloma akauma midomo yake, moyo ukimuuma zaidi na akijihisi msaliti kwa rafiki yake Fiona. Alimhurumia!
8888888888888888888888

Vurugu za kichwa hazikuwa kwa Fiona peke yake, Dhoruba la Nadina lilikuwa limempitia pia Mwanasheria Dennis Mazimbwe. Akiwa mbele ya meza yake ya kazi. Dennis alikuwa kama mtu aliyepigwa na butwaa ghafla. Aliikodolea macho meza yake ya kazi pasipo kupepesa macho kwa sekunde za kuunda dakika.

Akili ilikuwa inapambana na kumbukumbu za kutosha kichwani mwake. miaka kadhaa iliyopita alikuwa na vurugu nyingi kichwani mwake baada ya mkewe kumkimbia na watoto na image ya kampuni yake kuyumba pia. Alikuwa katikati ya msongo ulimfanya aitandike pombe nguvu zote kukwepa kuwaza na kuumia.

Usiku mmoja alikunywa pombe kiasi cha kushindwa kuendesha gari na mmiliki wa sehemu aliyokuwa anakunywa alimpigia simu Patrick aje kumchukua kaka yake akihofia kama angeendesha basi angesababisha maafa.

Patrick akampitia na kumpeleka kwake kwa nia ya kumfanya alale pale kisha asubuhi azungumze naye. Akamuacha kwenye sofa kwanza kwani alikuwa na Pamella garini na ilimpasa amrejeshe kwake haraka kisha aje kushughulika na kaka yake. Alimbwaga kwenye kochi na kumtaka msichana wake wa kazi Nadina afunge milango.

Patrick akaondoka, pamoja na ulevi aliokuwa nao, Dennis alimtazama Nadina alivyokuwa akifunga mlango na kumuandalia chakuka mezani, akamfuata, akamshika, akataka kumkumbatia, akamtaka kumbusu lakini pingamizi lilikuwa kubwa toka kwa Nadina. Pombe zake zikamtuma atumie nguvu na nguvu ile ikamfanya wabiringishane. kwa kujua Nadina alielekea kumzidi nguvu akachomoa bastola yake na kuiweka pembeni ya Nadina ambaye machozi yalimtoka kimya kimya wakati akibana koo kujizuia kupiga kelele

Akavumilia, akavumilia yote yaliyotendwa na Dennis juu ya mwili wake mpaka pale Dennis alipomaliza haja zake na kutulia juu ya mwili wake. Alikuwa akitetemeka na aliogopa hata kumsukumia kando akihofia kufa. akaitazama ile bastola kwa woga, maskini akitiririsha machozi mengi kimya kimya. Dennis alikuwa amembaka!

Pamoja na pombe ile Dennis alijua alichofanya, na alikumbuka vyema asubuhi ya siku iliyofuata mara tu alipoamka. Roho ilimuuma mno, roho ilimsuta, aliilaumu pombe, akamlaumu shetani lakini mwisho wa siku alijilaumu mwenyewe. Alikuwa amemfanyia ukatili wa ajabu binti wa watu na tabia ya kunywa pombe kupitiliza ikaishia hapo!
Akaondoka pasipo kumuona, wiki mbili baadaye Dennis alipita kwa Patrick kumuona Nadina, alitaka kuzungumza naye lakini hakumkuta. Patrick alimwambia Nadina alitoroka kwani alienda kazini na aliporejea hakumkuta.

Dennis Mazimbwe akajua kutoroka kwa Nadina lazima kulihusiana na tukio lile alilomfanyia usiku wiki mbili zilizopita. Akaumia sana! Mwanamke huyo aliyetoweka ghafla baada ya unyama wake alikuwa amemuona usiku uliopita. Kiwewe kilichompata usiku ule bado kilikuwa kinamuandama. Mwili ulimsisimka alipokiwaza kitendo alichokifanya.

Taratibu akainyanyua picha iliyokuwa juu ya meza na kuileta uswa wa uso wake. Akaitazama! ilikuwa picha ya Nadina pale kwenye ile sherehe ya harusi. Akaitazama kwa sekunde kadhaa kabla ya kuivuta droo na kuiweka ile picha.
Akashusha pumzi ndefu, akiwaza na kuwazua
88888888888888888888888888

Sindi Nalela alikuwa na mzigo wa kuni kichwani wakati akikatiza pori kufuata kijumba alichokuwa anaishi. Kwanza alipunguza mwendo na kusimama kabla ya kugeuka taratibu na tumbo lake lililokwisha jitokeza vema na kutazama nyuma.

Kulikuwa na gari tofauti na gari alilolizoea la Francois, hili lilikuwa gari la kisasa kabisa na la kuvutia. Akasimama kama mlingoti akilitazama namna linavyojongea na kumfikia. Kioo cheusi kikateremka na dereva wa hilo gari akatazama uso kwa uso na Sindi.
Alikuwa Daniella Mazimbwe!
‘Francois yupo?’ Daniella akamuuliza Sindi kwa Kiswahili. Mzigo uliokuwa kichwani mwa Sindi ukaanguka, akaduwaa kwa kule kugundua dereva alikuwa mzungu na kule kusikia mzungu akiongea Kiswahili.

Aliona kama nyota ya jah imemuwakia, kwa sekunde kadhaa Sindi alimtolea macho Daniella na asimjibu, wala asimuonyeshe dalili za kutaka kujibu.


ITAENDELEA…..

2 comments:

  1. simply ur the best laura..the connection of stories is so fine

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger