Sunday, March 2, 2014

SINDI....NA LAURA PETTIE (58)

58
()
Alitembea taratibu akilivuka geti la kutoka casino ya Madame ya Adella, alitembea akiyumba yumba, sio tu kwa ulevi aliokuwa ameutwika kwa muda ule bali kwa uchovu na mvurugiko wa akili aliokuwa nao. Meddy aliingia garini kwake na kuketi kwa takribani dakika kadhaa akiwaza, na alichokuwa akiwaza hakukielewa sawasawa pia. matukio yalikuja akilini mwake na kutoweka kama mwanga wa radi.




Kwa dakika nzima aliyoketi pale garini akiutumbulia macho usukani pasipo kuutambua akilini, Meddy alisali kimoyomoyo kwa imani yake, aligundua juhudi zake, nguvu zake na pengine hata ujanja wake wa kibinaadamu usingefua dafu ya kupambana na mwanamke fedhuli kama Adella.

Alitaka kumshirikisha Jerry Agapella, alitaka sana kuupata msaada wake sio tu wa kifedha bali pia hata njia ya kumkomesha mwanamke huyu. Aliamini vichwa viwili visingeshindwa kupata njia ya kuugawanya moyo wa Adella hata kama si kwa kumpata Nadina basi kumuachia kumbukumbu ya maumivu. Alikitaka kisasi!!

Akakumbuka kitu! Jerry hakuwa katika hali ya kuvurugwa, alikuwa akitarajia ndoa, harusi, furaha ya maisha mapya na sio kuambiwa Sindi alikuwa ameuawa na kwamba alikuwa pale danguroni kwa kipindi ambacho hata yeye hakukijua. Alimjua Jerry vizuri, na alijua mapenzi yake kwa Sindi yalivyo. Taarifa yoyote mbaya kuhusu Sindi ingemtandika Jerry na kumgaragaza.

Akaubeba msalaba wa maumivu na hatia kwa moyo uliopondeka kupitiliza, akipanga kuyaweka wazi yote baada tu ya fungate la Jerry kwani asingeweza kuishi na siri ile akiwa na amani na furaha.

Mkono wake wa kulia ukashika ufunguo na ktaka kuutekenya lakini kivuli cha mtu kando yake kikamfanya ageuke na kutazama nje kupitia dirisha la gati lake lililokuwa wazi. Mtu yule aliyesimama kando akainama na kukutanisha uso wake na wa Meddy.

Akashusha pumzi na kuonyesha hali ya kutafuta cha kuongea
‘tunaweza kusogea mbali na hapa kwa maongezi?’ yule mtu akauliza huku akishusha pumzi tena kama mtu aliyetua mzigo mzito baada ya kutamka maneno yale. Meddy akamtazama kwanza, akamtazama tu asitie neno la kukataa wala kukubali. Halmashauri ya kichwa chake iliitisha kikao cha dharura.

‘wapi?’ akajikuta akijibu kwa swali na mtu yule akamsogelea zaidi
‘kuna camera eneo hili.. ondoa gari hapa na uelekee upende huu…’ akamuonesha kwa kidole huko alikotaka aelekee kisha akamalizia maelezo yake
‘… kuna nguzo ya umeme hapo mbele simama hapo na uningoje’ akatamka neno la mwisho na kutoweka pasipo kumpa Meddy nafasi ya kuongea lolote. Meddy akaduwaa kidogo akijiuliza maswali ya tahadhari ambayo majibu yake yalibaki kitendawili.

Akafungua sehemu mbele ya kiti cha abiria na kuitazama bastola yake. Alihakikisha uwepo wake kabla ya kuichomoa na kuipachika ndani ya koti lake alilokuwa amevaa wakati huo. Akaliondoa gari na kuelekea kule alikoambiwa. Aliiona hiyo nguzo ya umeme hata kabla ya kuchanganya mwendo, hapakuwa mbali na pale alipotoka katika maegesho, ila hapa palikuwa na giza la kusisimua.

Akaegesha gari mahali alipoona pana uficho wa kutosha na kutulia, kwa mara ya kwanza aliitazama saa iliyokuwa garini humo karibu na redio ya gari na kugundua ilikuwa inaelekea saa tano kasoro. kama binadamu alisisimka mwili lkini moyo wa kiume ulimpa ujasiri wa kuendelea kusubiri. Alizitazama sekunde kwenye ila saa zikikatika na kubadili dakika toka 10: 48 mpaka 10: 53. Dakika tano nzima zilikwisha pita na kuanza kuondoa hali ya subira. Alikutumia kioo cha pembeni kutazama kila lililokuwa linajiri nyuma yake. mpaka muda ule alishaona magari matatu yakiondoka eneo la maegesho.

ghafla tu akashtukia kioo cha upande wa abiria kikigongwa na haraka Meddy akafyatua kitasa na kuruhusu yule mtu aingie garini. Akaingia kwa haraka na kumtaka Meddy aondoe gari pale na kuelekea gizani zaidi.

‘kwa misingi ipi sasa… sijajua nia na madhumuni ya kuniweka hapa ujue’ meddy akasita kuondoa gari kwanza kwa kuweka wazi wasiwasi wake.
‘kwasasa naomba uniamini kwanza… na sidhani kama unataka dakika ulizopoteza hapa zipotee bure… tafadhali’ kijana yule akaongea kwa kusihi na msisitizo wake ulimfanya Meddy awashe gari kwa shingo upande na kufuata maelezo ya ule kijana.

Wakatokomea gizani kidogo na kusimama…
‘nadhani unamjua marehemu Tuma’ kijana akaanza maelezo yake na Meddy akatanua ukubwa wa macho yake kiasi cha kuonekana kushangaa badala ya kujibu swali
‘…alikuwa mpenzi wangu!’ kijana hakuujali sana ule mshangao
‘Tuma?’ Meddy akauliza na yule kijana akishindwa kuelewa swali lile limaanisha kutoamini Tuma alikuwa mpenzi wake au hakuwa anamfahamu Tuma.

Ukimya wa yule kijana ukamfanya Meddy ajishtukie ghafla
‘Namfahamu ndio… unaishi mule ndani?’ Meddy akakurupuka kuuliza sasa kiherehere kikimtambalia maungoni kama siafu waliotibulia katika msafara wao

akaitikia kwa kichwa, akimpa nafasi Meddy atulie na kumsikiliza. Alijua kwa kiherehere kile asingelimuelewa ni nini anataka.
‘Enhe!..’ akaitikia Meddy na kumfanya yule kijana ajue Meddy alikuwa tayari kusikiliza
‘pamoja na yote aliyopitia pale ndani… Tuma nilimpenda kwa moyo wote kwani alichonisaidia maishani mwangu anabaki kuwa mwanamke mwenye thamani kubwa kuliko hata hao watakatifu nje ya hili jumba…’ akajieleza kwa uchungu sana

‘Pole sana…’ akamudu kutamka hayo tu huku akijizuia kutouliza chochote akichelea kuharibu mtiririko wa maelezo.

‘Tuma amemtumikia Adella kwa miaka mingi sana… yote machafu ameyajulia humu kuanzia kujiuza mpaka kubeba dawa za kulevya… sikutarajia Adella akubali tuma azikwe na jiji na sio kujitolea kumzika japo kwa heshima ya kudanganyia… kamtumia, kamletea msongo wa mawazo, kamfanya ajiue na kamzika kama takataka…huu kwangu ni zaidi ya unyama…maumivu ninayosikia hapa… nataka Adella ayasikie hata theluthi yake’ yule kijana akaongea haraka haraka na kujiinamia. Meddy akahisi ahueni ghafla. Msaada wa ulikuwa umemjia katika namna ya ajabu kabisa na zaidi maumivu yake hayakulingna na huyu kijana.

‘…Unadhani mimi nitakusaidia nini?’ meddy akauliza kama mtego tu
‘najua Nadina alipo..’ akajibu yule kijana na kumfanya Meddy akaribie kuingiwa na wehu wa ghafla
Akataka kumuuliza zaidi lakini hata maneno yalikwamia kooni. Akayatumbua macho ka bidii zote huku akimwemwesa midomo yake katika namna ya kubabaika.
‘…Nimekuona mara kadhaa ukipishana kauli na Adella…na ninajua unamtafuta Nadina… sijui mnachokwaruzania lakini nimeotea unataka sana kumkwangua Adella… niko upande wako’ Kijana yule akaongea kwa hasira za chinichini

‘Nadina yuko wapi?’ Meddy akauliza yale maelezo mengine ya yule kijana yakipita masikioni mwake kama upepo na asiyaelewe.
‘nataka uniahidi kwanza kuwa Ukimpata utamuondoa hapa na utamuweka mbali na Adella… nataka auhisi uchungu wa kushindwa…angalau ajisikie na yeye ni binadamu ana moyo wa maumivu’ kijana wa watu akaongea akionekana kujikaza kiume.

‘Hilo sio la kuwa na mashaka nalo… ni jambo la kufa na kupona… yuko wapi?’ Meddy akauliza kwa shauku zaidi na kijana yule akamuliza kama anataka kumchukua muda ule. Meddy hakuitikia bali alifungua mlango wa gari na kutaka kutoka ikiwa ni ishara ya kuwa tayari kwenda uko aliko.

Yule kijana akamzuia na kumtaka avute subira. Yeye akaishia na kumuacha Meddy garini. Zile dakika alizokuwa anasubiria zilikuwa kama karne moja na nusu. Alikaribia kutoka garini na kumfuata yule kijana lkini subira ilimtembelea tena na tena.

Nusu saa baadaye, alimuona mtu akitokea gizani na mtu begani. Moyo wa Meddy ulikaribia kusimama ghafla. Akajitoa mule ndani ya gari na kumfuata yule kijana ambaye alimuonyesha ishara ya kufungua mlango wa gari ili amuweke Nadina.

Huku akitetemeka Aliufungua mlango kwa haraka na yule kijana akamuingiza nadina kwenye siti ya nyuma ya gari akiwa hajitambui.
meddy alikuwa analengwa na machozi wakati akimtazama yule kijana
‘kwanini usiondoke?’ akamuuliza
‘Ndio nitaleta mashaka na atanisaka… nitakuwa mlengwa namba moja… nitatoka ile sio leo wala kesho… kwa sasa angalau nataka kuona Adella atakavyoweweseka’ akasigina taya zake kuonyesha alijikaza tu kuongea vile.

Meddy akachomoa wallet yake na kumpatia yule kijana idadi ya noti ambazo hata hakuzihesabu. Akampiga piga begani kama kumshukuru na kumpa moyo kwa yaliyomkuta. Akaingia garini lakini kabla ya kuliondoa yule kijana akalifuata dirisha la kiti cha abiria na kumchungulia Meddy
‘Mfiche mbali zaidi… asirudi mikononi mwa mtu huyu… atamuua mara moja’ akaonya na Meddy akakubaliana naye. Akaliondoa gari.

Aliendesha kwa kasi, aliendesha huku mara kadhaa akigeuka nyuma kumtazama Nadina aliyekuwa amepoteza fahamu, kwa sekunde kadhaa aliona ni kama ndoto. mpaka alipoingiza gari nyumbani kwake na kumuomba mlinzi amsaidie kumuingiza ndani yule binti.

Akazungumza na mlinzi na kumpa tahadhari kisha akaingia ndani mpaka chumba alichomuweka Nadina. Bado alikuwa hana fahamu zake.
Akampigia simu daktari aliyekuwa akimtibu Agapella Hospitali na mara moja akaja usiku huo na kuanza kumhudumia Nadina.

‘…anahitaji kupumzika zaidi na uchunguzi zaidi… lakini kwanini usimpeleke hospitali?’ Dokta akamuuliza mara baada ya kumhudumia
‘Nina sababu za msingi dokta… nashukuru kwa msaada wako… lakini..si akimaka anaweza kula chochote?’ Meddy akauliza kwa mashaka
‘Siwezi kuwa na hakika kwa sasa mpaka hapo atakapozinduka na kuweza kuongea…ila chakula chepesi kitamfaa zaidi…anaonekana dhaifu sana’ Dokta akaongea akivua gloves zake na kuagana na Meddy.

Baada ya kuhakikisha dokta alikuwa ameondoka Meddy akarudi chumbani mule na kusimama katika chumba kile kando ya kitanda akimtazama Nadina aliyekuwa usingizini pamoja na drip ya dawa mkononi iliyokuwa imeshikiziwa kwenye mlango wa kabati.

Alitembelewa na amani, alitembelewa na furaha, alitembelewa na hali ya utulivu ndani ya moyo. Akaitazama saa yake ya mkononi. Ilikuwa saa nane na vichapo kadhaa. usiku wa manane!

Akavuta kiti na kuketi kando ya kitanda cha Nadina, akatulia hapo akimtazama na kuvigusa viganja vya mikono ya Nadina iliyokuwa imetulia ikipokea maji ya drip. Alikuwa amemshinda Adella katika namna ambayo hakuitarajia. Mungu alikuwa amemuonyesha muujiza aliouomba!
888888888888888888888888

Asubuhi ya saa nne kukiwa ndio kwanza kumekucha. Adella alikuwa ofisini kwake pamoja na vijana wake wa kazi. taarifa kuwa mzigo wake wa madawa ulikuwa umefika salama china zilimfurahisha sana. Kijana mwingine akamuwekea bfriefcase ndogo yenye hela mbele yake.

Akazitazama na kutabasamu
‘Good job!...sasa niwape wiki nzima ya mapumziko na kila mmoja atapokea bonus yake… lets toast!’ akazungumza kwa furaha akinyanyua glasi yake ya mvinyo tayari kwa kupokea mvinyo uliokuwa umefuatwa kabatini na kufunguliwa. Aliyekuwa anaufungua mvinyo huo alikuwa yule kijana aliyekuwa anaongea na Meddy jana usiku. Aliufungua akitabasamu zaidi.
Akammiminia bozi wake na wengine kisha yeye mwenyewe. Wakainua glasi juu tayari kwa kugongesha glasi lakini kabla ya kufanya hivyo mlango ukafunguliwa na binti akaingia mbio mbio huku akihema.

‘Nadina ametoroka…’ akatamka akitetemeka kana kwamba angeambiwa yeye ndiye aliyemtorosha
Adella akaponyokwa na ile glasi, uso ukiwa na bumbuwazi la ghafla, pasipo kujali ilipoangukia ile glasi Adella akatoka mule ofisini huku akifuatwa na wale vijana kwa kasi.
Yule aliyemtorosha akawa wa mwisho baada ya kuunywa mvinyo wake kwa mkupuo.

Adella alisimama mlangoni akikitazama kile chumba alichokuwa akitunzwa Nadina. kilimtia kinyaa kiasi cha kukunja uso lakini bado lile bumbuwazi lilionekana usoni pake.
Akababaika, akaweweseka, akahamanika almanusura ale mweleka kwenda chini lakini vijana wakamuwahi na kumshikilia.

Jasho likamvamia, jasho likamtoka
‘Manafanya nini hapa…tawanyika… msakeni alipo na hatokuwa mbali…msiache pori lolote hapa karibu…mumlete akiwa hai…mataka kummaliza mimi mwenyewe sasa…now…nimesema now!’ Adella alitetemeka mpaka sauti. Macho yake yaliwiva na kujaa machozi. uso ulikakamaa na kujaa mishipa ya hasira wakati midomo ikimtetemeka.

Hakuwa mtu wa kushindwa, kutoroka kwa Nadina kulimaanisha muda wowote angekuwa mikononi mwa Meddy mshindani wake. hilo hakutaka litokee. Alihisi mwili ukimfa ganzi kwa hasira alizokuwa nzo muda huo.

Akajikwatua toka mikononi mwa wale waliokuwa wamemshika akifoka na kuamrisha Nadina aletwe pale ndani ya saa 24. kijana aliyemtorosha alimtazama kwa huruma na kutikisa kichwa. Alijua Adella alikuwa na hali gani muda ule na ndivyo alivyokuwa anataka!
8888888888888888888888

Sindi Nalela alikuwa akiwasha jiko la kuni nje ya kibanda alichokuwa anaishi. Francois alikuwa akinyoa ndevu zake wakati akiwa ameketi kwenye kiti na kioo kukining’iniza kwa uzi  kwenye kingo ya paa la kibanda.

Sindi alimtazama kila mara wakati akipuliza moto na kuchochea kuni ziwake na kuchemsha chai. Alipohakikisha kila kitu kilikuwa kama alivyotaka. Alinyanyuka na kuingia ndani. Akajitupa kwenye kitanda chake na kutulia hapo. Alikuwa akitafuta namna ya kumweleza yule mzee kuwa alikuwa anataka kuondoka sasa.

Francois akaingia na kupitiliza mpaka kwenye kile chumba kilicho na nyara za serikali. Akachukua muda kidogo kutoka na alipotoka akavuta stuli ndogo na kuketi kando ya kitanda cha Sindi, akampatia mfuko.

Sindi akaupokea na kuchungulia kilichokuwa ndani ya mfuko. Uso ukachanua kwa furaha. Kulikuwa na gauni, viatu aina ya raba, nguo ndogo ya mtoto,  khanga, makte na juisi ya pakti.

Sindi akafurahia na kushukuru kwa ishara ambayo Francois aliielewa na alifurahia pia kuona Sindi akiwa na furaha. hata lile wazo la kuanza kujieleza likampotea ghafla wakati akivitazama vile vitu. Francois akamuaga kuwa anatoka na angerejea muda mfupi baadaye. Sindi akatulia na kujilaumu kwa kutojieleza lakini ile nguo ya mtoto iliyokuwa kando yake ilimrejeshea tabasamu. Akalipapasa tumbo lake kwa furaha kubwa.
8888888888888888888

Nadina alizinduka asubuhi hiyo akiwa peke yake kwenye chumba kizuri mno. kwa macho malegevu alitembeza macho yake mpaka mlangoni na asione mtu. Alitaka kunyanyuka lakini mwili ulimuuma mno. akajirudisha kitandani taratibu na kujaribu kuiweka sawa akili yake na kujiaminisha hakuwa katika kile chumba chenye harufu mbaya ya kuumiza mapafu.

Alikusanya nguvu tena na kujiinua kwa taabu, na sasa akiiona pia drip iliyokwisha na kuchomolewa ikiwa kando. hakuelewa alikuwa wapi, akakishika kichwa chake kwa maumivu yaliyompitia na kujitazama. alikuwa amevaa shati la kiume mwilini mwake, akalisogeza shuka lililokuwa limemfunika mpaka kiunoni na kutazama vidonda vyake vya kuunguzwa na chuma.

Vilikuwa vimefungwa bandeji safi na mwili wake ulikuwa msafi kiasi cha kumshangaza yeye mwenyewe. Akaupeleka mkono wake w kushoto nyuma ya bega la mkono wa kulia na kujipapasa. kulikuwa na bandeji ngumu sehemu hiyo.

Mazingira hayakumweleza kuwa alikuwa hospitali. Swali la pale palikuwa wapi lilimsumbua na kumfanya ajikusanye na kujiondoa kitandani. huku akipepesuka na kushikilia ukuta alitembea taratibu na kuufikia mlango uliokuwa umeegeshwa tu.

Akaufungua na kutoka kutoka, akiwa ameushikilia ukuta akatembea taratibu kukatiza kordo iliyokuwa inaelekea sebuleni.
kadiri alivyokuwa akisogea ndivyo alivyosikia sauti za watu zikiongea. Akasita kidogo kabla ya kufika mwisho wa kordo na kusimama mbele ya wanaume wawili waliokuwa wakiongea pale sebuleni.

‘Nadina!’ Meddy akamuita kwa mshangao wakati Jerry Agapella akimtazama kwa mshangao
Meddy akainuka haraka na kumfuata, akamshikilia na kumleta kwenye kochi. Akamketisha. akimpima joto la mwili, akimuuliza anavyojisikia wakati Nadina alikuwa bado katika ile hali ya kulegea.

‘…huyu ni rafiki yangu Jerry Agapella!’ Meddy akamtamka akiwa na nia ya kumtoa Nadina katika hali ya wasiwasi.

ile hali ya kulegea ikapotea ghafla, akamtazama Meddy kwa kukunja ndita na kumtazama Jerry akimkodolea macho kama mtu asiyeamini. Mdomo wake ukiachama kila sekunde. Alitaka kusema neno ambalo lilikwamia kooni. Alimtazama Jerry Agapella katika namna ya kutoamini ni yeye. Akakumbuka simulizi ya Sindi ambaye kwake alikuwa marehemu. Akakumbuka vizuri wakati Sindi akilitaja jina la Jerry Agapella. Nadina akasimama na kuanza kurudi kinyumenyume kama mtu anayeogopa kitu. Alionekana kuwa na kiwewe ambacho hata Jerry alikiona na kilimfanya asimuelewe Nadina.

‘Si…si..sindi…’ akatamka kwa sauti ya kutetemeka, sauti ya chini, huku machozi yakianza kujaa machoni kabla ya kutiririka

ITAENDELEA…..

1 comment:

  1. Jmn laura mbna ujaipost fb? Jery cjui atajua ukwel kuhusu sindi I can't wait ya 59

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger