Tuesday, June 18, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (22)

22
Pamella Okello alijikuta akiiachia simu idondokee mapajani mwake pasipo kujitambua. Mikono ikalala juu ya usukani kiuchovu huku macho yake yakitembea taratibu mule ndani ya gari na asielewe kila alichokitazama. Mdomo wake uliokuwa wazi ulidhihirisha bumbuwazi lililomtembelea ghafla kwa wakati ule.

 Taratibu akashusha pumzi na kufumba macho katika namna ya kuumeza ule ujumbe aliousoma kama mtu anayemeza kaa la moto. Akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa pengine akitaka kuiweka sawa akili yake ama tu alitaka kupingana na kile kilichosomwa na macho yake.




Alitaka sana kuishika tena simu na kurudia kuusoma ule ujumbe, ajiridhishe kuwa haukutoka kwa Jerry lakini moyo ulisita alihisi kuurudia mara mbili kungeuchana moyo wake vipande viwili. Akashuka garini kama mtu aliyemriwa na kurudi ofisini kwake.

Dakika mbili mule ndani ya ofisi ilikuwa kama kukalia moto kwa sekunde mbili tu. Alisimama akakaa, akawasha kiyoyozi na kukizima hapo hapo akiinyanyua simu yake na kuirudisha mezani pasipo kuitumia. Kiwewe!
888888888888888888

Jerry Agapela alikuwa sofani akisoma gazeti moja la michezo huku akitazama Luninga nyumbani kwa Meddy Hakim ambaye alikuwa pembeni akiandika andika mambo kadhaa kwenye laptop yake, kisha akaitua pembeni na kumtazama Jerry ambaye naye alitupa gazeti pembeni na kushusha pumzi ndefu akionekana wazi lile gazeti lilikuwa geresha mikononi mwake.

‘Atakutafuta tu’ Meddy akamsemesha akimtazama kwa huruma
‘Sijali….’ Jerry akajibu uso wake ukilisaliti jibu lake waziwazi
‘unajali Jerry….nimekushauri umjibu hivyo kupima kama kweli hajali wewe kuwa na mtu mwingine…. uhitaji kuhamanika kama hivi’ Meddy kwa msisitizo. Aliona dhahiri ushauri aliompa Jerry ulikuwa unamtesa sasa baada ya kumjibu uongo Pamela ambaye hakumjibu kitu chochote. Hali ile ilimletea Jerry wasiwasi.

‘Angalau angenipigia kuthibitisha….it shows hanipendi kweli….nimemjibu vile na bado yuko kimya…hata meseji ya kutaka ukweli hajatuma let alone kunipigia kabisa…’ Jerry akababaika na kuobnyesha hofu yake waziwazi.

‘She is a smart woman Jerry!.... usitarajie atajiburuza mbele yako after the whole drama…. leo ni birthday yake…hebu mchunie sasa na usimtamkie lolote kama nilivyokushauri…jibu ulilompa liwe zawadi kwake….i swear hatamaliza saa 24 toka sasa hajakutafuta…. na kama atavuka hizo saa 24 move on Jerry she is not into you for real!’ Meddy akamjibu kwa kirefu, akinyanyuka na kwenda zake jikoni. Jerry akakipakata kichwa chake kilichoanza kuwa kizito mithili ya jiwe  la mwamba.

Meddy akarejea pale sebuleni akiwa na vinywaji kwenye glasi mbili. Akamuwekea Jerry mbele yake kwenye kistuli kidogo nay eye kurudi kukeri pale pale kimtazama Jerry namna alivyokuwa amekipakata kichwa chake. Akamsikitikia!

Kama mtu aliyekurupushwa Jerry akainua kichwa na kumtazama Meddy.
‘It is over…I’m done Meddy… nitaumia hivi mpaka lini…lini?’ Jerry akauliza kwa sauti iliyojaa maumivu
‘Now you are talking like a man!....’ Meddy akakolezea akinyanyua glasi yake hewani kama ishara ya kuunga mkono kauli ya Jerry

‘Baadaye..’ akaaga kwa kunyanyuka ghafla na kutoka mule ndani pasipo kumuaga Meddy vizuri. Meddy akakunja uso na kumshangaa lakini hakutaka kumzuia. Akamwacha atoke na kwenda zake. Dakika moja baadaye simu yake iliiita na mpigaji alikuwa Pamella.

‘Yes mama sema…’ Meddy akaitikia akinyanyuka kwenda kufunga mlango ulioachwa wazi na Jerry
‘Serena Hotel kuanzia saa moja jioni….my birthday party…don’t miss it dear’ Pamella akatoa maelezo yake
‘Nakuja mwenyewe au nije na kampani’ Meddy akauliza akitabasamu na akilisubiria jibu la Pamela kwa hamu kubwa

‘Whatever dear!...ila usikose tu’ Pamela akajibu baada ya kusita kwa sekunde kadhaa. Wakaagana na Simu zikakatwa. Meddy akacheka peke yake, akitikisa kichwa pia huku taratibu akiifuata rimoti na kuongeza sauti ya luninga iliyokuwa inaonyesha wimbo mmoja wa mahadhi ya dancehall. Akaucheza akwa furaha asijue alichokuwa anakifurahia.
88888888888888888888

Jerry Agapella alielekea hotelini akapumzika na kufanya mambo yake kwanza kisha akatoka na kurudi garini ambako alielekea anakobadilishia nguo na kuvaa anavyojua kisha akaliacha gari hapo na kurudi kwa Sindi Nalela.

Jioni hiyo akamkuta Sindi akimalizia kupika chakula cha usiku kwenye kordo. hawakusalimiana. Baada ya kuingia ndani na kuketi dakika mbili ndani, Sindi akaingia na kumpita tu bila kumsemesha chochote. alikuwa na sufuria mkononi alilolishika kwa vitambaa na kwenda kulitua chini karibu na stuli iliyokuwa na beseni la vyombo kwa juu.

Alipogeuka ili atoke Jerry akamuita, akasimama bila kugeuka
‘Ni jeuri au nini?’ Jerry akamuuliza
‘kwani vipi?’ Sindi naye akamuuliza akiwa kasimama vile vile pasipo kugeuka
‘nenda kamalize shughuli zako nataka kuongea na wewe’ Jerry akamhimiza
‘Nimeshamaliza’ akajibu Sindi kimkato na  Jerry akajikuta akimshangaa

‘Una ugomvi na mimi?’ akamuuliza na hapo ndipo Sindi alipogeuka kwa hasira
‘Nyanza anakuja lini?.... uliniahidi nini?.... sioni chochote ulichotimiza tangu unilete hapa…hii ina maana gani?’ Sindi akauliza kwa hasira na Jerry akaduwaa kwanza kwani hakutegemea maswali kama yake wakati kama ule.

‘Okay!....ndio maana nimekwambia umalize shughuli zako ili tuongee’ akajitetea akijua  alichomuitia mwanzo hakikuwa kile alichotaka kuongea sasa. Sindi ahakumjibu alitoka na kuishia zake nje akimuacha Jerry ametabua uso kwa mshangao.

Wiki ilikuwa imekatika tangu usiku ule aliomgusa Sindi. Asubuhi yake hawakusemeshana na Sindi alionekana kuwa na hasira za hapa na pale. Jerry akaondoka na kwenda kwa Meddy ambako alikaa siku sita huku akiwa amemuaga Sindi kuwa anafuatilia mambo yake mkoani.

Siku sita alizobaki mwenyewe Sindi alipata nafasi ya kutafakari mengi mno, alikumbuka nyumbani, alimkumbuka Nyanza, aliwakumbuka rafiki zake na wazazi wake lakini kikubwa alikumbuka ahadi za Jerry tangu alipokuwa kijijini mpaka alipomleta mjini. Akazihesabu ahadi zilizotimizwa, hakupata hata moja ya kumtuliza, akawaka hasira, akimsubiri Jerry kwa ghadhabu na ndio hivyo kajikuta akimnunia tangu alipoingia.

Baada ya pilika pilika zote za jioni hadi giza lilipoingia, Jerry na Sindi wakakaa mezani kula, huku ukimya ukiwa mheni wako katika kipindi chote cha mlo. Hakuna aliyemsemsha mwenzake wala aliyedai chumvi imezidi ama hata kuomba kioande cha limao akolezee kwenye samaki. Walikula kimya kimya.

Wakapisha kuingia maliwatoni na ndio sasa wakaketi mmoja kitandani mwingine kwenye sofa. Wakitazamana.
‘Nipe muda kidogo Sindi mambo ya hela hayajakaa sawa’ Jerry akajitetea
‘Sijakataa kuhusu hela ila lini sasa atakuja?’ Sindi akasisitizia ahadi iwe wazi
‘mwezi ujao nadhani nitakuwa nimepata nauli’ Jerry akajibu tu kumfurahisha Sindi akijua wazi hakuwa hata na mpango wa kwenda kijijini kule sababu ya Nyanza.

Nuru ikachomoza usoni pa Sindi baada ya jibu lile, mwenyewe uzuri wake ukichomoza upya na kule kuoga na kutakata, kula na kutulia ndani. Sindi alikuwa amenawiri mno. Rangi yake nyeupe ikawiva vizuri, ngozi yake ikalainika na kung’aa kama ya mtoto mchanga achilia mbali nywele zake za asili zilizokuwa laini kujaa kichwani na kuuongezea uzuri wa Sindi. Jerry akameza mate!

Sasa wakaongea mengine mengi na Jerry akamkabidhi Sindi pesa ya mtaji aliyokuwa anaitaka.
‘Mbona mtaji nimeshapata kwa kusuka….  nimenunua vifaa vya kazi  vile pale’ Sindi akamuonyesha Jerry mfuko wa plastiki uliokuwa na hivyo vitu
‘Basi hiyo ongezea tu’ hakutaka airudishe

‘Hapana, hii tuweke kwenye kibubu, kujazia jazia kodi ya chumba nami nikipata katika biashara yangu nitakuwa najazia tu…mwisho wa mwezi tuna kitu cha kulipa kodi, umeme na maji kwa pamoja’ Sindi akatoa mawazo yake na Jerry akajikuta akiitikia na kukubaliana naye, moyoni akikiri Sindi alikuwa na akili za maisha.

Wakachangamka kwelikweli na mazungumzoa yakapamba moto. Saa nne usiku wakatengana kwenye pazia na kuutafuta usingizi. Lakini ni kama usiku ilikuwa unajirudia. Hawakulala walikodoleana macho kwenye pazia na wasionane.

Jerry akavumilia kidogo na usiku ulipotengamaa akashindwa, akanyanyuka na kumfuata Sindi kitandani. Kimya kimya Sindi naye akageuka pasipo kubisha wala kusukumana akampokea Jerry maungni mwake na kumruhusu amguse alipotaka. Hali ile ikazidi, hakuna aliyetaka kumtoa mwenzake maungoni mwake

Jerry ambaye akili yake ilishahamia sayari nyingine akajiinua kidogo na kumuuliza Sindi kama kama alikuwa tayari kwa lile tukio alilotaka kulifanya na Sindi akaitikia kwa kichwa nap engine hakuushirikisha ubongo. kwa wakati ule hata ungemwambia tukamchinje Nyanza nadhani angeitikia ndio na asijielewe.

Zikazuka purukushani za hapana na pale na alajiri ya asubuhi hiyo Jerry  Agapela akambikiri Sindi Nalela. Akili ilipomrejea Sindi alilia mno asubuhi ile kwa majuto na misuto! ila ndio chenza lilishamenywa!
888888888888888888888

Taa za rangi hafifu ziliongeza nakshi katika sebule hili kubwa ya kisasa. Muziki wa taratibu wa ala uliokuwa ukisikika toka kwenye spika kubwa zilizokuwa hapo sebuleni, zilijenga mahadhi ya mahaba yenye kuvutia zaidi.

Pamela Okello alikuwa amesimama dirishani akitazama nje, mkono akiwa na glasi yenye mvinyo ambayo aliipeleka mdomoni mara kadhaa mpaka pale alipoona asingeweza kuipeleka mdomoni tena. Alishusha pumzi na kugeuka, akapiga hatua chache na kuifikia meza iliyokuwa na vinywaji mbalimbali. Akaitua ile glasi na kulifuata kochi kubwa lililokuwa mbele yake.

Pamela akaketi hapo, uso wake mzuri ukionyesha kujawa na mahangaiko yaliyokisumbua kichwa chake. Akajikunyata kwenye lile kochi akiitazama sakafu pasipo kuitambua akilini mwake.
‘Jerry..’ akaliita hili jina kwa sauti
‘Nooo…Noooo’ akapaza sauti akiyukla mwenyewe huku akihema kwa ghadhabu. Akasimama haraka na kuifuata ile glasi yenye mvinyo, akaibugia kwa mkupuo hali mikono ikimtetemeka

‘Bastard!...’ akapayuka tena na kuibamiza ile glasi sakafuni, machozi yakimvamia na kumtetemesha. Akalia peke yake kwanza na akionekana wazi kutaka kupambana ile hali.
‘Ooh Mungu wangu….’ akalalamika akitembea kivivu na kuketi kwenye sofa dogo. Akaibebesha miguu yake katika sofa na kuikumbatia akizidi kuhamanika.

‘Simu yake iliyokuwa kwenye mkono wa kochi hilo alilokalia ikaingia ujumbe na Pamela akaichukua na kuufungua
‘sikufichi kitu Pamela..ni kweli Jerry anatoka na Sindi kama alikujibu hivyo nadhani alimaanisha….vipi Patrick alikurudisha salama after party?’ aliusoma ule ujumbe akimalzia kwa kufumba macho kuashiria ujumbe ule ulimuumiza sana.

Meddy alikuwa anaushindilia mkuki moyoni mwake. Alishavumilia kutokusikia lolote toka kwa Jerry lakini alipoutaka ukweli wa ile meseji kupitia Meddy Hakim, rafiki mkubwa wa Jerry, jibu alilolipata lilimkata maini, likamuwewesesha na zaidi likamfanya aukumbuke uwepo wa Sindi na kujaribu kujilinganisha naye mbele ya Jerry. Isingewezekana aachwe kupapatikiwa kirahisi rshisi sababu ya Sindi!

Akiwa katika hamaniko lile, kengele ya mlango ikalia, akasonya akiitazama saa ukutani na siweze hata kukisia ugeni ule ulikuwa wa nani asubuhi ile. Akatoka chumbani kwake na kuelekea sebuleni ambako, aliukorokochoa mlango na kuufungua.

akanyoosha shingo yake na kuchungulia nje kupitia mlango wa chuma uliokuwa umetangulia kabla ya ule wa mbao. Moyo ukapiga mkambi! Alikuwa Fiona Agapela mama wa kambo wa Jerry. Maswali mia moja yakakimbizana kichwani mwake kwa kasi ya ajabu kidogo yaubomoe ubongo wake. Hakuwahi kumzoea mwanamke huyu wala kumkaribisha kwake sembuse kusalimiana naye kwa bashasha sasa ni kipi kilichokuwa kimemleta asubuhi ile?

Alimtazama Fiona Agapela kwa Mshangao kupitia lile Lango la chuma hali Fiona akimtazama kwa uso uliojaa mashaka na wasiwasi uliochanganyikana na hali ya kutia huruma. Pamella akahisi ule haukuwa ujio wa heri na ndivyo ilivyokuwa!

……. HAYA SASA….. FIONA KAFUATA NINI KWA PAMELA?

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger