Sunday, June 2, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (19)

19
Patrick Mazimbwe alisimama akiwatazama binadamu hawa wawili kama viumbe vilivyotokea sayari nyingine. Alijikuta akitaka kuzungumza na kunyamaza kwa wakati mmoja na pengine alitamani hata kuimba ila ndio kwa wakati ule mifumo ya fahamu ilishatawanyika kila mfumo na njia yake, akabaki mwenyewe tu na akili za kukodoa macho. Kufumania kipaji si kila mtu anahimilia vishindo!


Pamela alikuwa wa kwanza kumsukumia mbali Jerry, akiwa anameza mate kwa juhudi mithili ya mtu aliyelazimishwa kumeza vipande vya mawe. Alitaka kujiteteta kwa sauti ya kupaa lakini sauti yake ilimsaliti na ikamfanya aachame midomo yake na kuimwemwesa pasipo kumudu hata kumuita Patrick kwa jina lake.

Kwa kujua ameingilia shughuli ya watu, Patrick akageuka na kuutanua mlango kisha akajitoma nje asizungumze hata neno moja kuikaripia ile hali aliyoikuta. Pamela sasa nguvu ya kunyanyuka toka pale sofani ikamvaa kimiujiza, akajikuta anatoka mbio almanusura ajigonge kwenye meza iliyokuwa mbele yake. Akatoka nje akiliita jina la Patrick kwa sauti kubwa na kusihi.

Huku ndani Jerry bado alikuwa pale sofani akiwa kama mtu aliyepigwa na bumbuwazi.  Alitikisa kichwa kulia na kushoto katika namna ya kutoamini na kushindwa kujua baada ya lile tukio ni nini kingefuata.

Alikuwa anamjua Patrick kama mpenzi wa Pamela nay eye mwenyewe alishatambulishwa kwa Pat kama rafiki wa karibu mwenyewe Pamela akienda mbali na kuhitimisha utambulisho kwa cheo cha ukaka wa hiari. Kukutwa katika hali ile kulimfanya ajione zoba kwelikweli mbele ya Patrick ambaye kwa kuondoka bila kutia neno ndio kabisa aliwafanya wagoni wake watahayari!

Aliwasikia Pamela na Patrick wakijibizana uko nje lakini hakuthubutu kutoka, alibaki pale sofani kama mtu aliyekalia gundi ya maji. Wakati akiwaza na kuwazua, mlango ukatanuliwa tena na Pamela akaingia akionekana kuchanganyikiwa zaidi ya alivyotoka. Uso wake ulikuwa umelowa machozi na mwili ulionekana kunyong’onyea kupitiliza. Akasimama katikati ya sebule yake akimtazama Jerry na siongee neno lolote.

‘Get out!’ akamuamrisha kwa sauti ya kinyonge, sauti iliyoashiria kwa wakati ule alitaka kubaki mwenyewe nap engine iliashiria hakutaka kuulizwa lolote wala kujadili lolote. Jerry aliliona hili lakini hakutaka kulitii. Alisimama na kumsogelea Pamela
‘Nitazungumza na Partick’ akajibebesha mzigo
‘Toka nje…’ Pamela akaamrisha tena safari hii sauti akipaa kwa ukali na mwili wake ukitetemeka
‘Pamela mimi ndio chanzo cha yote haya…’ Jerry alizidi kutaka kuubeba ule mzigo lakini Pamela alionyesha dhahiri kutotaka kumsikiliza, akampita na kuelekea chumbani kwake akiubamiza mlango wa chumbani kwa nguvu zote kiasi cha Jerry kushtuka.

Mwanaume akasimama pale asijue atoke na kwenda zake ama amfuate Pamela na kumtuliza. Kwa Sekunde kadhaa halmashauri ya kichwa chake ikamtaka aondoke kuepusha shari zaidi lakini katibu mwenezi wa moyo wake akamshupalia na wazo la kumfuata Pamela chumbani. Akapiga hatua mpaka mlangoni na kusimama pale kwa sekunde kadhaa kabla ya kuamua kugeuza njia na kumfuata Pamela chumbani.

Alipoufungua mlango kwa kukinyonga kitasa na kuusukumia mbele, alitanguliza kichwa kwanza na kumchungulia. Pamela alikuwa ameketi kitandani akilia huku simu ikiwa sikioni, Alikuwa akimbembeleza Patrick kwa kuzungumza huku akilia. Alikatiwa simu na akahangaikia tena kuipiga ile simu.

Jerry akamfuata kwa kasi na kumnyang’anya ile simu. Kitendo kile kilifanya Pamela amrushie vibao Jerry ambaye alividhibiti kwa kumkumbatia Pamela kwa nguvu zote mpaka alipotulia na kulia kifuani pa Jerry kwa kwikwi na hasira nyingi.

‘Pam I know how you feel…I know…. but trust me…Pat hawezi kukusikiliza now…. pull yourself together…. Pamela!’ Jerry aliongea akiwa ameshikilia mashavu ya Pamela na kuuinua uso wake ili amtazame. Alijisikia vibaya mno kuona mwanmke anayempenda akilia vile kwa kuhamanika na zaidi yeye akiwa chanzo. Alitaka kwanza kumuweka sawa Pamela ambaye aliitikia kwa kichwa lakini machozi yakizidi kumtoka.

‘I love Pat…I love him…cant stand losing him jamani’ Pamela alilalamika kwa uchungu bila kujua ni kiasi gani kauli ile ilimuumiza Jerry.
‘Okay…lakini ana hasira sasa…unapozidi kumtafuta ndio unazidi kumfanya akasirike…I’m a man na najua atakavyokuwa anajisikia…. huwezi pata suluhisho muda huu…. unanielewa’ Jerry alijaribu tena kumtoa Pamela katika ile hali ya kuchanganyikiwa.

‘amesema nisimtafute tena…amesema hataki kuniona’ Pamela sasa alianza kueleza alichoelezwa na Patrick, rafiki yake wa kiume wa mwaka mmoja sasa ambaye ndiye haswa aliyekuwa ameshapanga naye kufunga ndoa. Mwanaume ambaye moyo wake na akili zake  zilishafikia uamuzi wa kutulia naye sit u kwa mapenzi aliyokuwa anampa bali pia kwa uwezo wake kifedha na kule kumhudumia kwa kila alichotaka. Pamela aliona bahati yake ilikuwa imetumbukia nyongo.

Jerry alifanya kazi ya ziada kumtruliza Pamela ambaye hatimaye alitulia na kuweka kufikiri kwa umakini bila taharuki ya kuachwa. Wakaagana na Jerry akaondoka zake. Usiku ule Pamela alihangaika kujizuia kutoigusa simu yake na kumtafuta Patrick, alijaribu kuufuata ushauri wa Jerry na akaweza!

Kuna kitu walikisahau, kitu kikubwa mno!...Patrick alikuwa amemuona Jerry Agapela ambaye alisharipotiwa kutafutwa kila kona…kwa wakati ule hamaniko lao halikuwafanya wagundue hili haraka, wala halikuwapitia akilini haraka!
888888888888888888888888

Sindi Nalela alishapanda kitandani kulala, wakati aliposikia Jamila akimuita mlangoni. Akaamka na kuwasha taa kisha kafungua mlango ili kumsikiliza Jamila.
‘Umeshalala?’ Jamila akamuuliza uso ukiwa na dalili zote za kutaka kuingia ndani ya chumba chake
‘Ndio nilikuwa najiweka kitandani…vipi kwani?’ Sindi akauliza akiutanua mlango zaidi ili Jamila aingie ndani, naye kama mtu aliyekuwa anangoja kuruhusiwa kuingia, akajitoma ndani na kujikaribisha kwenye sofa, akimtazama Sindi aliyekuwa anafunga mlango wake kwa ufunguo na komeo. Akatoka mlangoni na kuja kujiweka kwenye kitandani akipiga muhayo mrefu na kumtumbulia macho Jamila.

‘Ndio unarudi?’ Sindi akamuuliza baada ya kugundua Jamila alikuwa bado katika yale mavazi ya kutokea. Jamila akajibu kwa kutikisa kichwa na hapo hapo akimkodolea macho Sindi, Umbeya ulikuwa umemkaba kupitiliza. Njia nzima alitembea akijikwaa sababu ya kile alichokiona na alitaka sana kufika aendako ili amuweke Sindi chini kama hivi alivyomuweka.

‘Jerry yuko wapi?’ akamuuliza Sindi kwa pupa
‘Mmm, ameenda kazini…’ Sindi akajibu akionyesha wasiwasi
‘Kazini kwake ni wapi?’ Jamila akauliza kama mtu aliyetaka uhakika wa habari Fulani aliyokuwa nayo na ndio akazidi kumfanya Sindi achahatike bila mpango

‘Sijui….naa vibarua vyake uko…sijui wapi kwa kweli ila ndio ana shifti zake mara usiku mara asubuhi’ akajibu Sindi akimkazia macho Jamiala na akitamani kumuwashia na tochi ili amuone vizuri na ile hamaki aliyoingia nayo.

‘Kwani vipi?’ Sindi akauliza mwenyewe  akihema kwanza na akimtazama Jamila aliyekuwa amejiinamia ghafla na kuguna.
‘Mwenzangu…. mjini hapa dada kunamambo ukiyaona unaweza kuzimia mbele ya umati wa watu wallah’ akamfumba fumba maneno akimuacha Sindi njia panda.
‘Kwani imekuwaje?’ Sindi sasa alitoka kitandani na kuja kuketi kwenye lile sofa alilokalia Jamila

‘Nimemuona mtu kama Jerry akishuka kwenye gari hizi zimeingia sana siku hizi…’ Jamila akajieleza na Sindi akashindwa kumuelewa haraka
‘Gari gani?’ akauliza Sindi utadhani alijuanaiana za magari mjini
‘Eeh jamaini gari gani hizi sijui….zinaitwaje sijui…gari f’lani za gharama kwelikweli…. ziko juu juu hivi’ maelezo yake wala hayakumpa picha Sindi ya nini alitaka kuzunngumzia

‘Labda gari la bozi wake’ Sindi akajaribu kurahisisha maongezi
‘Alikuwa nayendesha mwenyewe…na alivyokuwa amevaa….hapana dada yaani kwanza nilitaka kusema niemmfananisha ila ni Jerry huyu huyu jamani…alikuwa anaingia New Afrika hoteli pale…. shost huyu bwana unamjua vizuri maana mi leo kidogo nigongwe na gari nikiyashangaa haya mambo’ Jamiala akajieleza na Sindi akajikuta akicheka kwa sauti kwanza kama mtu aliyekuwa akisimuliwa maajabu ya dunia.

‘Hapaba sio Jerry…kwanza hana gari, pili uko mahotelini mmmh….’ Sindi akakanusha
‘Sindi nimemuona kwa macho yangu…. amevaa shati la mikoo mifupi…kachomekea mkanda nje…kiatu chini na saa zile za bei… hpana ni yeye nimemuona jamani’ Jamila akatetea alichoona lakini Sindi akampinga zaiid na zaidi akidai duniani wawili wawili.

Mwisho wa yote Jamila akakubali kwa shingo upande kuwa pengine alifananisha. akaga akaondoka. Sindi alipobaki mwenyewe akatulia na kutafakari maneno ya Jamila, hakuona ukweli wowote wa kuulinganisha na Jerry anayemjua. akapanda kitandani na kulala.

Jamila hakukosea, aliyemuona alikuwa Jerry mwenyewe, Jerry Agapela! Muda huo aliomuona ndio muda aliokuwa akielekea New Afrika hotel kupata chakula cha jioni na kubadilia nguo kisha kuelekea kwa Pamela, baada ya kutoka kwa Pamela ambako aliacha sekeseke la kutosha Jerry alichoma mafuta kurejea New Afrika hotel kulala.

Mbali na Jamila, kuna mtu mwingine alikuwa amemuona, mtu mwingine ambaye hakutarajia kumuona Jerry eneo kama lile katika hali kama ile. Jenifa agapela mdogo wake alikuwa amemuona kaka yake wakati akiwa nje ya hoteli ile ndani ya gari la mwanaume aliyefika naye hapo. alimuona kaka yake akitoka nje ya hotel na kuingia garini. Kwanza alipiga yowe kibwa mule ndani ya gari akijaribu kumuonyesha yule boyfriend wake alichokiona lakini ikawa amechelewa na Jerry alishaingia ndani ya gari.

Jenifa usiku huu alikuwa chumbani kwake akiwa mwenye hofu, mwenye mtihani na mwenye kuchanganyikiwa. Alikuwa amemuona Jerry kabisa, alishindwa kuamua amueleze baba yake kuhusu alichokiona ama amueleze mama yake wa kambo kwanza. Alitulia akiwa amekumbatia mto wake na kukodoa macho yake ukutani kama mtu aliyekuwa akitafuta majibu ya mtiririko wa mswali yake ukutani hapo.

Akakata shauri kumweleza Fiona kwanza!


....TWENDE KAZI....

1 comment:

  1. Dada we noma.... wapi naweza kukuona sister

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger