Tuesday, February 11, 2014

SINDI....na LAURA PETTIE (56)

56

Nadina aliwatazama wale walinzi akiwa amekata tamaa, akakiachia kifurushi chake cha pesa kidondoke chini na kusimama kama sanamu. Wakamkamata, wakamfunga mikono nyuma na kumkokota wakikiacha kile kifurushi kilichokuwa na pesa pale chini. Nadina akageuka na kukitazama wakati wakimkokota na kumsukuma, wakimburuza, wakimdhalilisha na kumdhihaki.


Madame Adella alikuwa amesimama katikati ya majengo yake akivuta sigara yake na walinzi wawili wakiwa nyuma yake. Usoni alionyesha dalili zote za kujaa hasira. Zikasikika kelele na purukushani nyuma ya jengo mojawapo. Mabinti wakikimbizana kuchungulia nje kupitia madirishani au vibarazani uko maghorofani. Wachache wakitoka nje na kusimama mbali kushuhudia Nadina akikokotwa na walinzi na kuletwa mbele ya Adella.

Nadina akasukumwa kwa nguvu na kupepesuka, maskini akaangukia mita chache toka alipo Adella. Mlinzi mmoja akamfuata na kumnyanyua kwa kuvuta nywele zake huku akimuamrisha kupiga magoti. Kwa taabu Nadina akapiga magoti kwa mtindo wa kukalia visigino vyake. Alikuwa akihema si tu kwa hofu bali pia kwa hasira aliyokuwa nayo. Dhamira yake ya kukimbia haikutimia!

Alikuwa ameinamisha kichwa chini macozi yakimbubujika huku mikono yake ikiwa imefungwa nyuma. Adella akapiga pafu moja refu na kuachia moshi wa mafungu matatu aliyoupulizia hewani kisha taratibu akapiga hatua kadhaa na kumfikia Nadina.

‘Nilishakuonya binti… na mara zote huwa naonya mara moja tu ya pili unakuwa mfano kwa wenzako’ Adella akaongea akitabasamu kwa mbali na Nadina akajitutumua na kuinua uso wake juu kumtazama Adella
‘Niue…niue tu…’ akasema kwa ujasiri  akiwa amelegea kwa uchovu wa kuburuzwa mpaka pale, hakubahatika kuurudisha uso chini kwani Adella alimuwahi na makofi matatu makali ya kupokezana mashavu. Kofi la kwanza lilitua shavu la kulia likafuata kofi la pili lililopigwa kwa sehemu ya nyuma ya kiganja cha Adella kwenye shavu la kushoto kisha akamalizia la tatu kwenye shavu la kulia. Yalikuwa makofi ya haraka na ya nguvu. Nadina aliyumba akaenda chini kwa mara nyingine wakati Adella akihema na kumtazama kwa ghadhabu. Hakutarajia Nadina amjibu wakati ule.

‘Tukutane Pepo ya Mateso’ akatamka akirusha kile sigara iliyokuwa mkono wa kushoto juu ya mwili wa Nadina, ikatua kwenye paja na kwa uchungu Nadina akatamani kutumia mikono yake kuiondoa lakini ndio vile ilikuwa imefungwa nyuma. Akajitutumua kujigaragaza lakini Adella aliukanyaga ule mguu kwa nguvu na kuifanya ile sigara itulie juu ya mwili wa Nadina na kumuunguza.

Nadina akalia, akalia kwa yowe na uchungu, akifurukuta kwa maumivu ya kuchomwa na ile sigara na kule kukanyagwa. Wale Mabinti waliokuwa wanalishuhudia lile tukio wakashika mioyo yao kwa hofu, wengine wakitazama pembeni na wengine wakirudi vyumbani kuepuka kuona Nadina navyolia. Wachache walitirirkwa na machozi.

Aliporidhika akaondoa mguu na kupiga hatua akiondoka eneo lile. Nadina akalia kichinichini akijitahidi kuusogeza mguu ili sigara ile idondokee pembeni. Akaweza lakini ndio alishaungua kiasi cha kutisha. Walinzi wakamuinua na kuanza kumburuza wakiwa wamemshikilia makwapani na yeye akishindwa kutembea sawasawa kiasi cha kufanya mara kadhaa alegee kufanya magoti yaburuzike chini.

Akapelekwa chumba kile kile alicholala na Sindi siku ile alipotaka kumuokoa Sindi. Akasukumiziwa humo na kufungiwa. Pale chini kulikuwa na mikojo, kulikuwa na uchafu wa kutosha. Alikuwa amechoka, alikuwa na njaa, alikuwa na maumivu, alikuwa na hasira, alikuwa na majonzi. Dunia ilikuwa imemuelemea mabegani. Kwa mara ya kwanza maishani mwake Nadina alitamani malaika wa kifo amtembelee.
88888888888888888888

Usiku wa ulipita na kukapambazuka. Meddy alikuwa macho akiwa amelala chali kwenye sofa akionekana kutopea mbali kimawazo. haikuwa kawaida yake kuwa pale muda ule, siku zote aliamkia mazoezini lakini kwa siku ile hata hamu ya kujinyoosha viungo hakuwa nayo. Mawazo yalienda kasi sana kichwani pake, akikumbuka siku ile aliyompokea Sindi kituoni Ubungo kwa maelezo ya Jerry. Alimkumbuka vyema. Alikuwa binti mrembo mno, mzuri sana pamoja na kukosa matunzo stahiki lalkini bado Sindi Nalela alikuwa na mvuto wa kipekee. akazikumbuka dimpose na mwanya mdogo ulijitokeza wakati akitabasamu wakati anamuonyesha chumba atakachokuwa akiishi.

Akatikisa kichwa na kujitoa katika yale mawazo, akaketi kitako na kukibeba kichwa chake kwa mikono yake miwili ni kama vile alitaka kumbukumbu ile ipotee. Akili yake ilikuwa inagoma kukubali kuwa Sindi alikuwa mfu kwa wakati ule, hakutahili kufa vile wala  hakustahili kuwa danguroni mule… akahisi kama hatia ikimnyemelea kua hakufanya juhudi kumshawishi Jerry amtafute Sindi kwa hali na mali.

Meddy akarudia kulala chali, mikono yake ikilala nyuma ya kisogo, akatulia na kuitazama dari, macho yakifumba na kufumbuka taratibu mithili ya mtu anayenyemelewa na usingizi. Akashusha pumzi ndefu akili yake ikihamia kwa Nadina. Ghafla mlango wake ukagongwa na akajikuta akikatiza mawazo yake na kuinuka kwenda kuufungua mlango.

Jerry Agapella akaingia akiwa na mfuko mkubwa wa kutunzia suti.
‘Aisee, leo vipi?’ Jerry akauliza akikivuka kizingiti cha mlango na kuingia ndani
Meddy akaufunga mlango na kumgeukia Jerry. Hakumjibu kitu alirejea kuketi pale sofani na kuinua kicha kumtazama Jerry.

‘Unaumwa?’ Jerry akadadisi wakati akiweka suti kwenye moja ya masofa na kuketi soga lingine
‘Vipi wamemaliza kuziandaa suti?’ Meddy akauliza kwa sauti ya unyonge akijaribu kujiweka sawa na pengine kubadili mazungumzo lakini taswira yake usoni iligoma kutoa ushirikiano kabisa. Jerry akatulia tu pasipo kujibu kisha ghafla akasimama na kuja kuketi kweye lile sofa kubwa alilokuwa ameketi Meddy.

‘Kuna tatizo gani Meddy?’ Jerry akauliza uso ukionyesha hofu
‘Aaah…mambo ya bishara hizi kaka’ akajitetea akijua wazi anadanganya
‘…mashati ya sendoff tayari?’ akajitahidi tena kubadili mada na Jerry akaitikia kwa kichwa akiwa bado hajaielewa hali ya Meddy. Alikuwa rafiki yake sana ambaye hawakufichana kitu kuanzia mambo ya kipato, kazi, biashara mpaka mapenzi na kwa hakika alijua wazi mpaka Meddy kuwa katika hali ile ya kukosa furaha lililokuwa linamkabili lilikuwa kubwa sana.

‘Wamemuondoa Nadina?’ akauliza kwa kukisia tu na asijue alielekea kupatia
‘Tuachane na hayo Jerry…. tufocus kwenye inshu za maana zilizo mbele yetu’ Meddy akakwepa kuongelea tatizo na  hapo hapo akiumia zaidi

‘Come on Meddy… huwezi kupretend kila kitu kiko sawa wakati si kweli… kuna tatizo gani?... hatufichani kitu… kwanini usiwe wazi?’ Jerry akambana zaidi na Meddy akajikuta anasimama na kufumba macho kwanza. Akiomba akili yake ikae sawa na siropoke lolote kuhusu Sindi

Jerry naye akasimama
‘Ni juu ya mapenzi?.... kazi? nini?’ Jerry alitaka kuelewa na Meddy akamgeukia ghafla machozi yakimlenga, akaweweseka, akababaika kiume kipigana na hali ya uchungu. Akazidi kumuweka Jerry kwenye wakati mgumu

‘Hanitaki tena…’ akajitutumua kuongea na Jerry akaguna na kurudisha kichwa nyuma
‘Nani?’ akauliza
‘Nadina’ Meddy akajibu akimeza mate kwa nguvu  kiasi cha kufanya koo lake  lfanye shimo la sekunde

Jerry akacheka, akacheka tena, akacheka mfululizo na kuketi sofanikwa kujitupa
‘You can’t be serious Meddy… yaani nilijua ni kitu kikubwa sana kuwa labda kuna mtu amekufa… yaani uko hivi sababu ya msichana kusema hapana kwako… Be serious Meddy acha ubwege!’ akamnanga rafiki yake

Meddy hakujibu alijitahidi kutabasamu na akitamani pia kulipua bomu ili aone kile kicheko cha Jerry na dhihaka zake zingekatika vipi na kuleta hali gani mule ndani. akajikaza na kuzikubali lawama.

‘Malaya unayemuokota danguroni Meddy unaanzaje kumuingiza moyoni kiasi cha kukuumiza?...Nasty!... mtu analalwa ovyo kwa tamaa ya pesa… kajileta kwenye danguro kujiuza ili ajikimu kimaisha unaanza vipi kumpa heshima yote hiyo… tupa kule’ Jerry akaongea kwa dharau zaidi ya mwanzo

‘Tuongee mambo mengine please!’ Meddy akaona akinyamaza Jerry atamfanya aongee asichotaka kuongea
‘… tuongee ukweli bwana, unaheshimika Meddy…. wanawake wangapi wanajigonga kwako… leo hii unashindwa hata kwenda mazoezini kama kawaida yako kisa demu wa danguroni?...’ Jerry akacheka

‘Tuachane na hayo Jerry’ Meddy akasisitiza kwa sauti ya kukemea lakini Jerry hakuiona hiyo hali
‘Bora hata nisikie unatoka na Clarita sio takataka hizo..’ Jerry akamlizia sentensi yake na kushuhudia Meddy akisimama na kumtazama kama mtu aliyepatwa na kiwewe kwa yale maneno yake
‘…una maisha yako na mimi nina yangu, unajua Sindi alipo?... mwanamke uliyemjuaza mimba ukamtelekeza unajua alipo?... au nay eye ukimkuta danguroni utamuita takataka?...’ Meddy aliongea kwa jazba
‘Hey hey hey Meddy…. calm down…’ Jerry akamuwahi na kutaka aketi chini na hapo hapo akili yake ikishindwa kuelewa Sindi anaingiaje katika yale mazungumzo. Kwa kutambua alikokuwa anaelekea kimaongezi si kuzuri Meddy akamtazama Jerry na kujaribu kutulia

‘Niko ndani napumzika’ akamuaga Jerry na kuanza kuchapua hatua za kuondoka oale. Jerry akabaki anamtazama na asimuelewe katu. Wahenga walisema mzigo wa mwenzio kwako kanda la sufi!!
88888888888888888888

mlango wa kile chumba alicholala Nadina ulifunguliwa. Mwanga ulioingia kupitia mlangoni ulimuumiza macho Nadina kiasi kwamba hakuweza kumuona vyema mtu aliyekuwa amesimaama kwenye kizingiti cha mlango ule. Akafinya macho na kujitahidi kufumbua lakini hakuweza mwanga ulimzidi nguvu.

Wakaingia watu wawili na kumnyanyua, hakuwa na nguvu ya kusimama hivyo walimkokota tena kwa mtindo ule ule wa kushika makwapa naye magoti ya kiburuzika chini. akauma meno kwa uchungu akivumilia kule kuchubuka. Alikuwa na njaa hakuwa na nguvu hata ya kusimama wima sembuse kutembea.

Akaingiza sehemu ambayo hakuwahi kuingia kabla  ambako kulikuwa na vyuma kama bembea lakini virefu kwenda juu. Wakamfunga hapo mikono yote miwili ikiwa juu kwenye fundo moja. kwa zile dakika mbili tatu alihisi mabega yalitaka kuchomoka sababu alikuwa ananing’inia. akauma meno na kufumbua macho. Wenzake ambao hakujua idadi yao walikuwa wamesimama kama kundi la wanakwaya wakimtazama kwa huruma.

Ni kama vile waliitwa pale kuona ni nini kilitaka kutendeka, hakika alianza kuona ni namna gani Adella alimaanisha angekuwa mfano kwa wenzake. Adella akaingia akiwa amevalia gauni lake pana na kilemba cha kuvutia. akatembea kwa madaha huku wale mabinti wakisogea mbali naye kwa hofu.

akasimama mbele ya Nadina na kumtazama kwanza kwa sekunde kadhaa
‘Kwanini umemuua Tima?’ swali la maneno matatu tu lilipita kwenye ubongo wa Nadina kwa uzito wakutosha kabisa. akajikuta akiinua uso kwa kasi na kumtazama Adella kwa mshangao uliombatana na kuta macho kwa juhudi zote. alichachatika!

Midomo iliyopaswa kumtetea kwa juhudi zote iliwayawaya na kutetemeka, Hakuikumbuka hata ile barua ya Tima aliyoitunza kwenye matiti yake. Machozi yakambubujika.

Wakati akiwayawaya na kutokwa na machozi akamtazama Adella anavyogeuka na kuwatazama wale mabinti waliokuwa mle ndani
‘Nilishasema na narudia kusema… ukishaingia hapa wewe ni mali yangu… huna haki.. huna ruhusa… huna uwezo wowote wa kuwa juu yangu!... utanitumikia mpaka  nitakaposema sasa u mavumbi na mavumbini urudi… na kama una bahati ya mtende utaishi kama uko peponi… lakini kwa vinyamkera vinavyojaribu kupambana na nguvu ya Adella… tunaonyana mara moja kisha mara pili unakuwa mfano kwa wengine kama hivi…’ akageuka na kumfuata Nadina aishika sehemu ya shingo ya gauni la Nadina na kulitatua katikati.

Gauni likatii na kuserereka, likachanika vipande viwili mpaka mwisho na kumuacha Nadina mtupu mbele ya wenzake huku ile barua aliyokuwa ameipachika kwenye brezia ikidondoka miguuni pake pasipo yeye wala Adella kuiona.

Nadina akajiinamia na kulia, akalia kwa kugugumia wakati Adella akitabasamu. taratibu akamtazmaa mlinzi mmoja aliyekuwa mbali kidogo na kumpa ishara ya kumsogezea kitu ambacho mlinzi alikijua. Karai lililokuwa na mkaa likaletwa likiwa na chumba ndani. Nadina alipoliona akataharuki, akajifurukutisha pale aliponing’inizwa akipiga yowe kubwa la hofu, akihangaika pengine kwa kudhani angejiondoa lakini alikuwa amedhibitiwa ipasavyo na ile kamba kule juu

‘Sikumuua Nadina…sikumuua mama..sikumuua…naapa mama naapa mama sikumuua’ Nadina akapayuka akitoa macho, akimsihi Adella amsikilize amuelewe na akili yake ikaikumbuka ile barua akajitazama kwenye kifua lakini haukuwepo akatazama kwa kuweweseka kule chini kuangalia kama ilikuwa imedondokea popote akaiona lakini wakati akijiandaa kusema mlinzi aliyekuwa nyuma yake akamuwekea plasta mdomoni.

akashindwa kuongea, Adella kwa maringo akakishika kile chuma kwa kitambaa, akakitazama kile chuma kilishabadilika na kuwa chekundu kwa mbali. Kisha huku akitabasamu akamsogelea Nadina ambaye mishipa ya shingo ilikaribikia kumkatika kwa kusimama.

‘hii itakufanya uongee bila kusitasita… kwanini umemuua Tima wangu na kutoroka… ingawa najua pengine uligundua alishirikia mauaji ya yule Malaya mwenzio Sindi… lakini nataka uongee vizuri… vizuri kabisaaa na uwe mfano kwa hawa wengine’ Adella akawageukia wale mabinti.

Sura zao zilijaa hofu, walikumbatiana na wengine wkitazama nyuma
Adela akamgeukia Nadina ambaye alifurukuta akitaka aondolewe ile plasta mdomoni ili amwambie ushahidi alionao. akatazama chini akijaribu kumuonyesha Adella ile karatasi chini lakini Adela akaikanyaga kwanza pasipo kujua kisha akatazama uko chini. hakuna kitu cha ajabu.

‘Camera zinaonyesha wewe ndio uliingia mara ya mwisho na ukatoka na kuutupia ufunguo chini ya mlango… kama hukukusudia kumuua kwanini hukupiga kelele kuita watu?... kwanini ulifunga mlango na kutoroka kabisa nje ya nyumba… kwanini Nadina…kwanini?’ Adella akauliza lakini tayari akiwa ameshamuhukumu na zaidi kule kumfunga plasta mdomoni hakukumpa nafasi Nadina ajitetee.

Ule mkono wenye chuma cha moto ukarudi kwenye karai lenye mkaa wa moto, ukalivirigisha lile chuma na kulitoa kwenye mkaa, akatembea na kile chuma mpaka nyuma ya Nadina. akakipachika pembeni kidogo yap le unapoanzia uti wa mgongo.

Nadina akatoa macho kwa nguvu zote, mishipa ya uso na shingo ikamtutumka kiasi cha kuonekana imevimba, macho yakajaa wekundu  wakati mishipa ya mikono ikimjaa na kusimama. Machozi yakamchuruzika kwa kasi wakati alipoyafumba macho kwa juhudi zote huku akihangaika kujisogeza mbele kuepa kile chuma pale mgongoni na asiweze.

alihisi maumivu mpaka kwenye chemba ya moyo lakini sauti haikutoka, ilizuiliwa kwa makusudi. jasho likamtoka mwili ukamzizima akihisi ganzi ikimtembelea mwilini kwa maumivu aliyoyasikia.

wenzake wkafumba macho na kukumbatiana huku wengine wakilia kwa uchungu. Adella akarudi mbele ya Nadina akitabasamu.
‘Mwanamke aliyekuzaa wewe alaaniwe duaniani, ahera na peponi’ akamtukana Nadina akirudisha kile chuma kwenye moto na kukichochea tena na safari hii Nadina akakiona kile chuma kikija mbele yake. Akafurukuta masikini, akafurukuta mno na uchungu mkali ukapita mishipani mwake wakati chuma kile kikigonga katikati ya mapaja yake vile alitataka ayatanue mapaja yake. Uchungu wa chuma kile ulimfanya ayatanue mapaja yake lakini Adela aliendelea kuchezesha kile chuma kile kulia na kushoto pale pale katikati ya mapaja yake.

Nadina akakaza mishipa akivumilia ile hali mpaka akalegea na kupoteza fahamu. Adela akarudisha kile chuma kwenye mkaa na kumuamrisha mlinzi aliyekuwa yuma amfungue mdomo na yule aliyeleta karai alete maji na kumwagia. Sekunde mbili tatu Nadina karudiwa na fahamu akiwa amelegea kupitiliza.

hakuweza tena kuongea kitu, hakuweza hata kunyanyua uso, alijilazimisha kutanua mapaja yake ili vile vidonda vya chuma pale katikati ya mapaja visigusane lakini kwa ule mtindo aliwekwa wa kuning’inizwa kutanua mapaja ilikuwa ni adhabu nyingine tosha.

Adella akamrisha aweke pale saa nzima kisha aondolewe na kurudishwa kwenye kile chumba
‘Maji tu na kipande cha mkate… bado tutarudi hapa kuzungumza’ Akatamka kwa amri na kuwatazama wale mabinti
‘Welcome to my  Empire ladies’  akainua mikono juu kama mtu anayewalaki wapendwa wake. Wale mabinti walikuwa mabinti wapya katika kazi ile na ndio kwanza walikuwa wameingizwa, kwa tukio lile kila mtu alishika roho yake mkononi, kila mtu aliapa utiifu bila kupenda. Adella akatembea taratibu na kutoka lile eneo akiwaacha hoi wale mabinti.
Nadina alikuwa alikuwa ananing’inia pale kama mzoga huku mapaja yake yakivuja damu na kule mgongoni kukivuja damu. Alikuwa amekumbatia mwamba wa maumivu!!
888888888888888888888888888

Adella aliingia ofisini kwake na kumkuta Meddy akiwa ameketi anamsuburi, Akamsabahi akitabasamu na kukifuata kiti chake wakati Meddy akishindwa kujibu ile salamu na kubaki kumtazama tu.

‘Nikusaidie nini Mr. Mohamed?’ akauliza Adella baada ya kujiweka sawa kwenye kiti chake
‘Nadina… ‘ akaanza na Adella akampa ishara ya kuishia hapo hapo
‘Nadhani unazijua sheria za humu ndani…. kwangu mimi huyu nadina ni kama chombo tu ambacho mtu anakikodisha anakitumia na kukirudisha… wewe mkodishaji ukifika hapa kukodisha bidhaa na ukaambiwa haipo unapaswa kuheshimu jibu ulilopewa lakini unapoanza kuulizia bidhaa kana kwamba ni yako na una haki ya kuipata unapoitaka… unavuka mipaka kijana…. sijui tunaelewana?’ Adella aliongea haraka na kwa jazba ya mbali akiona wazi Meddy alitaka kulivalia njuga suala la Nadina.

Meddy akamtazama Adella na asimmalize
‘Vipi kuhusu Sindi?’ akaona aweke wazi mashaka yake
‘how many times do I need to answer this question Meddy?... you are smart enough to know unaniboa sana… unanikera… Sindi is dead… DEAD!!... so?’ Adella akauliza kijeuri, hasira zikianza kumpanda taratibu

Meddy akababaika, akatingisha kichwa kama mtu asiyeamini kile kile alichoambiwa
‘Na Nadina umemuua pia?’ akauliza sauti ikimtetemeka
‘No!... sijamapata bado ile nikimpata nitakutaarifu uhudhurie japo mazishi’ Adella akatabasamu akijilaza kwenye kiti chake na kujizungusha. Meddy kasigina magego yake na kubamiza ngumi mezani akiwa amesimama, akihema kwa hasira

‘dare not to touch Nadina…’ akaongea akibananisha meno na Adella akacheka kwa kejeli naye akisimama na kutazama na Meddy

‘…Let us bet… you get her first  you take her I get her first I kill her’ Adella akaweka karata mezani na Meddy akamtazama kwa hasira kupitiliza. Ilikuwa kama kumuweka rehani Nadina. kwamba akimpata yeye kwanza atamchukua na akimpata Adella basi atamuua.

‘Fine!...’ meddy akaitikia akitikisa kichwa juu chini kwa haraka, hasira zikiwa pomoni.
‘Now get out…’ Adella akamfukuza

Meddy akamtazama tu Adella na asijue amfanye nini sasa. Akageuka na kuondokoka kwa haraka wakati Adell akicheka kwa sauti zaidi kwani alijua wazi Nadina alikuwa mikononi mwake tayari. akajizungusha kwenye kiti chake kwa maringo. Akifungua droo moja na kutoa kijiubao kidogo cha kuzawazishia kucha. Akaendelea kujizungusha huku akisawazisha kucha zake.
88888888888888888888

Jioni ya saa moja usiku ya siku hii…. kwenye eneo la wazi la nyumba ya Okello kulikuwa na shughuli ya wanawake, Singo iliyoenda sambamba na kibao kata. Taa zilimulika eneo hilo lililopambwa kwa mikeka ya kisasa ya kila rangi, vijimito hapa na pale huku vikuba vya waridi vikiwa huku na kule na chetezo za udi zikifuka moshi mzuri wa kuvutia kwenye kila pembe ya mwisho wa mkeka.

Hewa ilitawaliwa na harufu nzuri mno ya kuvutia, sare ya shughuli ikiwa gauni pana la hudhurungi, refu mpaka chini na mkanda wa chuma cha rangi ya dhahabu kiunoni. Shughuli ilijaa watuwaliotakata haswa wakinogesha ile sare kwa madini ya ratili kadhaa…mwenye dhahabu, mwenye almasi, mwenye  madini ya fedha mwenye tanzanite kila mtu alikuwa cha kupambia shoo.

kwenye kona moja kulikuwa na wapiga ngoma wanawake waliokuwa na sare yao… kulikuwa na chakacha linarindima hapo na wanawake wachache wakikata nyonga kuringishia wenzao. Mara vikasikia vigelegele na wale waliokuwa makundi makundi wakayaacha kundi na kujumuika. Pamella alikuwa anaingia akiwaka waka kwa lesi aliyokuwa amefunikwa nayo… ile chakacha ikachanganyia sasa, wanawake wakanesa nesa naye mpaka alipoketi …ngoma ikanyamaza pah!... kukawa na ukimya ghafla… kisha mirindimo ikaanza tena safari hii ukasikia wimbo maarufu wa zamani

‘Bembea ee ooh bembea ee… bembea ee ooh bembea ee… bembea ee oo bembea mtoooto…nyamaza mwana kulia bembea mtoooto ukilia waniliza bembea mtooooto’ mirindimo wa huu wimbo iliamsha hoi hoi na nderemo… Yule mfundaji yule LP alikuwa anaingia na kundi lake, wakiwa na vikapu, godoro, na sanduku… wakikata nyonga na mizigo yao kichwani na wasiangushe kitu

Pamella akasogeza lesi pembeni ili afaidi vile viuno ila msimamizi wake akamzuia, Wanawake waliojiweza kwenye uchezaji wakaingia kati kupokea vile vitu huku nao wakikata viuno mpaka chini pasi kuviangusha.

Santina alikuwa mmoja wa wanawake waliopokea kikapu kimoja wapo na kukatika nacho mpaka chini kiasi cha watu kumpigia vigelegele na kumtuza. hakujua tu kule ghorofani kwa juu Mzee Okello alikuwa akimtazama na mvinyo wake mkononi na asimmalize. alipokabidhi kikapu mwanamke mmoja akamnong’oneza kitu na Santina akajiondoa taratibu huku akiangaza huku na kule kama vile hakutaka watu waone anavyotoka. Okello alimuona!

Akatoka lile eneo na kutoka hadi mbele ya nyumba yam zee Okello, akasimama hapo akiangaza tena na tena bila kujua kule juu Mzee Okello naye alihamia upande ule aliokuwa na kumtazama kutokea kule juu. Akatoka mpaka nje na kumkuta Meddy amesimama upande wa pili wa barabara akiwa ameegemea gari lake.

Santina na Meddy wakatazamana tu pasipo kuongea kitu. kisha Santina akavuka barabara na kumfuata Meddy akafikia kumkumbatia kwa nguvu wakati Meddy akiwa wima vile vile bila kumgusa Santina. Ikamchukua sekunde kadhaa Meddy kuinua mikono na kumkumbatia Santina.

Walipoachiana Santina alikuwa analengwa na machozi wakati Meddy akiwa anamtazama tu pasipo kusema neno
‘Asante kwa kuja Meddy’ akatamka Santina na Meddy akaitikia tu kwa kichwa
‘Nafurahi mlinzi wako amekuwa mwaminifu kiasi cha kukufikishia ujumbe.. sikujua kama angekwambia nilichomwambia’ Santina akajiongelesha wakati Meddy akimtazama tu pasipo kusema chochote.
‘ I miss you’ Santina akatamka akimtazmaa Meddy machozi na Meddy akashusha pumzi na kutazama chini mikono yake ikiwa ndani ya suruali yake sasa.

Wakati wakitazama bila neno, Mzee Okello akawa ameshashusha mpaka pale getini akisalimiana na baadhi ya wanawake waliokuwa wanaingia muda ule kwenda kwenye sherehe

Kule kusalimiana kuwa kuna mapotezea muda wa kumfuatilia Santina vizuri.
‘Twende mahali hata dakika tano tu tuongee’ Santina akamuomba Meddy ambaye wala hakusema kitu, aligeuka na kumfungulia mlango wa gari akauacha wazi nay eye kuzunguka upande wake na kuingia garini. Santina akajitosa garini na kufunga mlango. Meddy akaondoa gari na Okello akalitazama lile gari kwa hasira akikunja ngumi  kwa nguvu na kufumba macho.

Akagutuka na kuchukua simu yake, namba kadhaa akaipapasa papasa na punde akaiweka sikioni
‘… Nimekupa kazi ya kufuatilia nyendo za Santina unajua alipo?’ akaongea kwenye simu akifumb amacho kama mtu anayesikilizia maumivu ya ndani
‘…vizuri…sasa hakikisha najua alipoelekea muda huu’ akaongea tena na kukata simu.

Akatembea kurudi ndani, akimpita mkewe Rebecca ambaye alikuwa anatokea ndani pasipo kumsemesha si kwa makusudi bali hakumuona na wala akili yake haikuwa pale

ITAENDELEA…..

3 comments:

  1. hivi siku adella akijua nadina ni mtoto wake itakuaje? maana hya mateso anayompa mh!!!!

    ReplyDelete
  2. peti harakisha basi adela amjue nadina jamani,post fasta 57 basi na ww?

    ReplyDelete
  3. Ujamzungumzia sindi telemundo ndefu kama isidingo iwaishe bs Jerry akutane na sindi

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger