57
Robo tatu ya mgahawa
ilikuwa tupu usiku huo wa saa mbili na vichapo kadhaa. Watu wawili watatu
waliokuwa mgahawani hapo hawakuzidi watano ukijumuisha na uwepo wa Meddy na
Santina katika meza moja iliyokuwa kwenye kona. wachache walionekana kuingia na
kuchukua huduma ya ‘Take away’.
Meddy alikuwa ameketi upande uliomfanya aupe mgongo mlango wa
kuingilia mgahawani hapo huku Santina akiwa ameketi kwa kuupa mgongo ukuta.
Walikuwa wakitazamana na maongezi yao yakiwa na msomaji na msikilizaji.
Hakukuwa na majibizano!
Santina aliongea na Meddy alibaki kuwa msikilizaji tu,
asimbishie wala asikubaliane naye sembuse hata kujibu maswali aliyokuwa
anaporomoshewa.
‘To me it was not a one night stand Meddy..’ Santina akatetea
kule kukutana kwao kimwili kwa mara moja na kisha kuachana.
Meddy akatazama pembeni kana kwamba ile kauli ya Santina
ilikuwa dhihaka Fulani, alipoyarudisha macho yake usoni pa Santina akafungua
mdomo.
‘umemaliza?’ kwa mara ya kwanza Meddy akaongea kwa kumtandika
Santina swali lililomnyong’onyeza.
‘Meddy!... ina maana mimi kukuita hapa umeona kama
nakupotezea muda?’ Santina akaonyesha huzuni yake usoni, uso wake mzuri ukijaa
simanzi ghafla
‘ni zaidi ya kunipotezea muda Santina!... nilichokwambia mwaka
mmoja uliopita hakijabadilika… ni sawasawa na hiki ninachokwambia sasa hivi…
sikuhitaji!’ Meddy akaongea haraka, kwa jazba za chini chini na kinyongo ambacho
Santina hakuona sababu yake.
‘Lakini kwanini?.... nilikufanyia nini?.... tulikuwa na
uhusiano mzuri tu kama marafiki… iweje baada ya kulala na mimi uniache kinyama
vile?’ Santina akahoji kwa uchungu akipambana kike kujiweka katika hali ya
kawaida pamoja akiizuia ile jitimai iliyoanza kumuelemea. Laiti tu asingelikuwa
mahali pa wazi pengine angeliangua kilio cha mfiwa!
Meddy akamkata Santina jicho kali la ‘acha unafiki’
‘ulikuwa mwanamke wa kipekee kwangu Santina lakini kwa sasa
hata urafiki wako siuhitaji tena… na wakati mwingine utakapotaka kuonana na
mimi ni vema ukiwa na kitu cha maana cha kuongea…’ akaongea tena kwa jazba za
kukamia chinichini huku akiusogeza uso wake mbele zaidi kule aliko Santina.
‘….usijaribu tena kunipotezea muda wangu kijinga hivi’
akasimama na kutoa wallet mfuko wa nyuma wa suruali, akaifungua na kuchomoa
noti kadhaa za elfu kumi na kuziweka juu ya meza.
‘kwa ajili ya vinywaji na taksi ya kukurudisha nilikokutoa’
akatamka taratibu, akigeuka na kupiga hatua zake ndefundefu pasipo kugeuka
nyuma wala kuaga. Santina akauma midomo
yake na kuizamisha kwa ndani. Mishipa ya shingo ilimkakamaa wakati akipigana na
nguvu ya machozi. Hakutaka kulia hadharani.
Pigo alilopewa na Meddy lilikuwa la shoka hasa! Akajikaza na
kutaka kunyanyuka lakini miguu ilikosa nguvu ya kumtoa pale. vinywaji
vilivyokuwa mbele yake havikuguswa hata theluthi na wala hakuwa na hamu hata ya
kupiga funda kudhaa kufidia ile pesa.
Akabaki ameketi pale akizitazama zile glasi huku akili yake
ikijikusanya upya na moyo wake uliokatika vipande vipande ukizidi kutawanyika.
Hakyatarajia mapokezi kama yale toka kwa Meddy!
8888888888888888888888888
Kule kwenye sherehe mambo yalikuwa motomoto, Palikuwa pamechangamka mno, kwa walio mita chache toka kwa nyumbani kwa Okello
walijua kulikuwa na sherehe ingawa kistaarabu sauti ya muziki ilisikika kw
mbali kidogo. taksi iliyomrudisha Santina ilifunga breki mbele ya geti na akateremka
kwa kasi kidogo na kuubamiza mlango wa taksi. Akaingia getini na kwa hatua za
haraka akalifuata lango la kuingilia ndani badala ya kuelekea upande uliokuwa
na sherehe.
akaufikia mlango mkubwa wa kuingilia ndani na kuufungua.
Akajitosa ndani na kuufunga kisha kuuegemea kwanza akiwa amefumba macho na
kuelekeza uso juu. mikono yake ikiwa
imeshikilia pochi yake ndogo mapajani. Akatulia vile kwa sekunde mbili kabla ya
kushusha pumzi na kuzitazama ngazi zilizokuwa zinaelekea juu ghorofani. Alitaka
kuingia chumbani kwake na kupumzika tu.
Hakuwa na hamu ya kujisherehesha tena. Akili ilishavurugika,
baba halisi wa mtoto wake hakuwa na muda naye na mbaya zaidi hakutaka hata
kumsikia lakini zaidi ya yote ndiye mwanaume aliyekuwa anampenda kwa dhati.
Akavua viatu vyake virefu kwa awamu na kuvishika mkono mmoja
na pochi, ule mwingine ukivuta gauni lake refu kwa juu na kupiga hatua za
kichovu kuzielekea ngazi. Mzee Okello naye alikuwa akitokea juu na kufika
katikati ya zile ngazi wakati Santina akiwa ndio kwanza anapandisha ngazi ya
kwanza.
Santina akainua uso juu na kumtazama Mzee Okello, pasipo
kusema neno akapandisha ngazi mpaka pale alipokuwa amesimama
okello na kumpita taratibu ngazi ya pili toka ampite Okello.
Akasimama baada ya kuitwa na Okello. hakugeuka!
‘Ulienda wapi?’ Okello akamtupia swali, yeye akiwa
ameshageuka kumtazama Santina
‘Kama mpaka umejua nimetoka sidhani kama hujui nilikwenda’
Santina akajibu na kutaka kupandisha ngazi zaidi lakini Okello akamuwahi
‘itakupasa uchague moja kuwa na Meddy ila umrudishe mtoto wangu au kukaa na mtoto na
uachane na Meddy’ Okello akaongea kwa sauti ya chini lakini yenye msisitizo.
Santina akashusha pumzi. Alikuwa amechoka, alikuwa na hasira, alikuwa na huzuni
na haya maneno ya Okello yalimfikia kama matusi ya nguoni. Akageuka mzima mzima
na kumtazama Okello kwa jicho kali sana, ukimya ukapita kati yao
‘…sawa!... ila itakupasa kuchagua uwe na mimi na familia ako
ijue au uwe na familia yako na unikose mimi… huwezi kuwa na vyote wakati mimi
nikikosa kimoja… it is not fair’ Santina akageuka na kuanza kupiga hatua za
haraka zaidi akapotelea juu.
Mzee Okello akabaki njia panda pale kwenye ngazi lakini
asijue kuwa kuna mtu alikuwa amesimama kule chini kwenye ngazi akimtazama.
Alipogeuka ili aendelee kuchuka ngazi akakutana uso kwa uso na Annie, shemeji
yake, dada wa mke wake.
Wakatazamana katika namna ya kushangaana, Annie akionekana
kuzubaa ghafla na Okello akiwa na mshtuko. Wakapishana tu kimya kimya kila
mmoja akiwaza lake.
88888888888888888888888
Kumekucha!
Asubuhi hiyo ikawadia, Nadina alikuwa sakfuni hoi, taabani,
akifumbua macho kwa taabu sana na kuyafumba tena. vurumai za kufunguliwa ka
kufuli la mlangoni na mlango wenyewe zikamfanya afungue tena macho kwa taabu
zaidi. Njaa ilikuwa inamkong’ota kisawasawa, hakuwa na nguvu hata ya kujisogeza
pembeni achilia mbali kufukuza nzi waliokuwa wakimzunguka na kumng’ong’a.
Waliongia wakanyanyua na kuanza upya kumburuza, akakunja uso
kwa nguvu alizobaki nazo kuhimilia maumivu ya kuburuzwa mpaka kwenye kile
chumba alichotesewa usiku uliopita. Akafungwa kwa mtindo ule ule lakini safari
hii akijihisi nusu mfu. Dakika tatu baadaye Adella akaingia na kusimama mbele
yake.
Kwa macho malegevu yliyochoka kwa mateso na maumivu, njaa na
simanzi akamtazama Adella kama mtu anayeomba asimkaribie.
‘Uko tayari kuongea?’ Adella akamuuliza na Nadina ambaye
alimtazama tu Adell pasipo kujibu, pasipo kuongea chochote kile, pasipo
kujitetea. taratibu aliyashusha macho yake na kutazama chini tu.
‘Naona kiburi chake bado hakijalainika… Mnaweza kujisevia
mnavyotaka asubuhi hii mpaka nitakapojisikia kumuona tena baadaye’ Adell
aliongea kwa sauti kubwa, alitaka amri ile isikike kwa walinzi wale wawili
waliokuwa pale pamoja na Nadina mwenyewe. Akageuka akitabasamu na kuanza kupiga
hatua. Nadina aliyeisikia kauli ile alijua haraka Adella alikuwa ametoa ruhusa
ya wale walinzi kumbaka.
Akatoa mlio wa sauti ya kuita ila hakuweza kutamka alilotaka kutamka, Machozi yalimjia
kwa kasi na kumporomoka wakati akijaribu kumtazama Adella ambaye alisimama
pasipo kugeuka kingoja kusikia lolote toka kwa Nadina.
Mdomo wa Nadina ulimwemweseka, wakati machozi yakimbubujika,
hakuwa na nguvu maskini, hakuwa na kauli ya kuongea, mpaka dakika ile alikuwa
anakaribia kukamilisha siku mbili bila maji wala chakula. Angeongea vipi? na
mateso aliyopata nguvu ya kujitetea angetoa wapi? Adella akachoka kungoja na
kumgeukia Nadina.
Vile vidonda kwenye mapaja vilikuwa vinasisimua kwa
kuvitazama tu, mwili wake ulikuwa umechakaa mno, kupitiliza kwa vipigo na
mateso. Nadina akakusanya nguvu na
kutamka
‘Nisa..me..he…’ akaishia hapo na kutetemka mdomo.
Adella akamtazama zaidi na kubwea kwa dharau. kisha akageuka
‘mnaweza kukata kiu mnavyotaka!’ akatamka tena na kuondoka
eneo lile, akafungua mlango na kutoka wakati sauti ya Nadina ikipaa kwa uchungu
na maombolezo ya kusihi. Adella hakugeuka wala hakurudi kutengua amri yake.
Alilifikia gari lake na kuingia siti ya nyuma baada ya kufunguliwa mlango na
dereva wake. gari likaondoka
Nusu saa baadaye wakati Adella akiwa kwenye gari lake akiendelea
na safari yake, Nadina alikuwa amelala chini kwenye kile chumba akiwa kama nusu
mfu. Alikuwa pale kama mzoga Fulani ulioandamwa na nzi. sura ya Tima ikimjia
akilini na kutoweka, sura ya Sindi ikimjia akilini na kutoweka. katikati ya
maumivu yale Nadina akatabasamu…
8888888888888888888888
Sindi Nalela alikuwa
ameketi juu ya ukingo wa mawe akiitazama bahari, mdomoni alikuwa anaimba
wimbo wa Nadina. Alikuwa akiokota vijimawe vidogo na kuvirusha kwenye maji
wakati akiimba. Asubuhi ile alikuwa amemkumbuka Nadina mno, alikuwa amemkumbuka
Tima na akatamani kumuona japo amshukuru tu kwa kumtoa katika jehanamu ile
ingawa hata pale alipokuwa hapakuwa peponi lakini angalau aliishi kama binadamu
huku akiwaza ni nini kingefuata.
Alikuwa amekumbuka nyumbani kwao sana sana sana, Hakuna siku
iliyopita bila kumkumbuka mama yake na mdogo wake Peter. Alitamani afumbe macho
na kujikuta nyumbani kwao akizozana na Peter, akikwaruzana na mama yake,
akiruka dirishani na kuonana na Nyanzambe wake.
Akawakumbuka wote kisha akili yake ikmkumbuka Jerry Agapella.
Safari hii akamjia kama kipande cha
sinema, akikumbuka mizozo yao. Ule imbo aliokuwa anaimba ukapotea mdomoni
akajikuta akijikaza kupambana na machozi. katika kipindi kifupi cha maisha yake
alikuw amepitia mambo ya ajabu mno kiasi kwamba alitamani kujifinya ili kujitoa
katika ndoto.
‘Jerry!’ akaita kwa sauti akitabasamu, akifuta machozi haraka
sana na kuligusa tumbo lake lililoanza kuchomoza barabara.
Akapepepa macho kule baharini kisha kuyapeleka pembeni ambako
alimuona yule mzungu akimpa ishara ya kumfuata kule chini. Akanyanyuka na
kuteremsha hadi kule alikokuwa yule mzungu.
Akampa ishara ya kuchukua kuni zilizokuwa kando yake na
kuzipeleka nyumbani. kisha akamuonyesha gari na yeye na mbwa kuwa anaondoka na
angerejea usiku sana.
Sindi akatulia kama mtu ambaye hakuelewa. Mzungu akacheka.
Akarudia tena!
Akajinyooshea yeye, akamnyooshea mbwa wake, akamuonyesha gari kisha akafanya vitendo kama
mtu anayeendesha, halafu akanyoosha mkono wake wa kulia toka kushoto kwenda kulia
akimuonyesha njia anayoitumia kuondokea.
Sindi akaitikia kwa furaha kuwa alikuwa ameelewa hapo.
Mzungu akajinyooshea yeye kisha anyooshea ile njia na kisha
kunyooshea nyumbani, akamnyooshea sindi kidole na kufanya ishara ya kulala.
Sindi akatulia kidogo kabla ya kuelewa na kuitikia kwa kichwa haraka sana.
Yule mzungu akampa ishara mbwa aende garini, wkti akimsaidia
kumpatia Sindi kuni ili asipate shida kuinama. Akambusu pajini na kumuaga.
Mzungi akatokomea. Sindi kajitwika kuni na kuanza kupandisha kimpando kidogo
kurejea nyumbani.
Akakatiza kijipori alichoanza kukizoea na kufika kwenye
kijichumba chao. Baada ya kuingia ndani na kujifungia akakuta mkate na chai
vimefunikwa karibu na kitanda chake. akajua Mzee alikuwa amemuandalia. Wakati
akitaka kujiweka kitandani kwake akaona mlango wa kile chumba cha pili ukiwa
wazi. Shauku ya kujua kilichomo ikamvaa.
taratibu kwa mwendo wa kunyata akaufuata mlango na kusimama
kizingitini. Pumzi ndefu zikamshuka na kwa kusitasita akatanguliza kichwa na
kuchungulia. Mwanga uliokuwa ukitkea kwenye vijiupenyo vilivyobaki kweye mbao
zilizotumika kujengea kila kibanda zilimuwezesha kuona vitu vilivyomfanya abaki
mdomo wazi.
Kulikuwa na pembe za faru, pembe za ndovu, ngozi za wanyama,
madumu ya njano ya lita hamsini yakiwa mengi sana, na magunia ambayo hakujua
ndani yake kuna nini. kulikuwa na sindano za ukubwa tofauti tofauti kubwa na
madawa ya kila aina. Kulikuwa na masanduku ya chuma ambayo matatu aliyaona
kwenye gari muda mfupi tu wakati mzungu akiondoa gari na kuondoka. Sindi
akahisi uoga Fulani ukimtembelea. Huyu Mzungu alikuwa nani?
Akatoka mule chumbani na kuja kuketi kitandani pake akiw na
hali ya kushangaa na kuogopa kwa wakati mmoja. Akawaza aondoke pale na
kukimbilia popote kule atakokutana na
msaada mwingine. Wazo hilo lilimkaa mno Sindi kiasi cha kumfanya atazame
viatu vyake. Akisita sita kuchukua uamuzi uliomjia ghafla!
8888888888888888
Jerry Agapella alikuwa akikaanga mayai jikoni wakati
alipohisi mlango ukifunguliwa na mtu kuingia. Akatega sikio na kuisikia sauti
ya Pamella ikimuita. Akatabasamu!
Pamella akaingia na kumlaki mumewe mtarajiwa kwa busu la
mdomoni wakati Jerry akiwa na kikaangio mkononi
‘my wife!’ akamtania Pamella aliyekwenda kujiegemeza kwenye
kabati ililokuwa limeungana na meza yenye jiko la kupikia. Akalipa mgongo
kabati na akawa anamtazama Jerry usoni.
‘Sijakuona siku ngapi sijui…jana nimelala saa nane usiku leo
nimeamkia hapa’ Pamella akajieleza na Jerry akatabasamu na kumtazama Pamella
‘unazidi kuvunja mila na desturi tu…’ akazungumza akigeukia
kikaango na kugeuza yai lake
‘… hakuna anayejua niko hapa, halafu sikumuona Jenifa jana
wala Clarita’ Pamella akaonyesha kushangaa
‘Come on babe!... wewe
na Clarita ni wa kualikana sherehe?’ Jerry akamshushua akizima jiko na kufuata sahani kwenye kabati
‘Okay! tuache ya Clarita… Jenifa je?’ Pamella hakutaka
kushindwa
‘hamjawahi hata kusalimiana kwa tabasamu… na huwa sielewi
kwanini nyiwe wanawake wawili muhimu maishani mwangu hamuelewani’ Jerry akawa
amesharudi na sahani na kupakua yai lake. Sasa akasimama na sahani yenye yai
akimtazama Pamella
‘…Jenifa hanipendi na siku zote amekuwa akitaka Clarita ndio
awe na wewe… unadhani sijui?’ Pemlla akaongea kama mtu anayesuta
‘hujafanya juhudi zozote za kuuteka moyo wake… badala ya
kumfunza upendo ndio unazidi kumpanda juu… she is my sister… the one and only
sister…do the needful… awe upande wako’ Jerry akaongea taratibu akigeuka na
kuelekea chumba cha kulia chakula
Pamella akang’aka huku akimfuata Jerry nyuma
‘Khaaa!... nimlambe miguu?.... hell no!’ Pamella akakataa
kushuka
‘Hell yeah!... huwezi kusema unampenda Jerry wakati
unamchukia Jenifa’ Jerry akampinga akiweka sahani mezani na kumgeukia Pamella
‘Huh!... nani kasema namchukia?’ Pamella akamuuliza yeye
akionekana kuyachukulia yale mazungumzo kwa umakini zaidi huku Jerry
akitabasamu hpa na pale kuonyesha alikazia yale mazungumzo kumchemsha tu
Pamella Okello.
‘humsalimii…hujawahi kumletea zawadi yoyote ile… hujawahi
kumpa pole kwa kufiwa na mama… hujawahi kumsaidia kumuuguza mama…hujawahi
kumwambia unampenda… hujawahi kumuuliza kwanini anakuchukia... so now tell me
umeshafanya juhudi gani kuonyesha upendo kwa Jenifa…mind you ni mdogo sana
kwako… unashindana naye?’ Jerry akaongea akihesabu aliyoyatamka kwa kupangua
vidole.
Pamella akatoa macho tu, mdomo ukibabaika, akijiona mjinga
kupita maelezo. Jerry akatabasamu na kumpita akirudi jikoni
‘Kama huwezani na Jenifa utawezana na Fiona?’ akamuuliza
wakati akimpita na kumfanya Pamella ajisikie vibaya zaidi. Akahisi alikuwa na
mshindano na jenifa kwa mambo yasiyoa na msingi. Akageuka na kumfuata Jerry
jikoni, akamkuta akitoa glasi kwenye kabati.
‘Jenifa yuko wapi?.... labda nimtafute nizungumze naye’
akajieleza
Jerry akageuka na glasi zake na kumtazama Pamella usoni
‘…huna habari naye kabisa kiasi cha kutojua kuwa Yeye na
Clarita hawapo mji huu kwa takribani mwezi sasa… wapo mapumzikoni… kabla ya
harusi watakuwa hapa!... usimvurugie mapumziko yake…’ Jerry akazidi kumfanya
Pamella ajisikie vibaya zaidi
‘hiki ni nini?... ulikuwa unangoja nije ndio uniambie haya
maneno?’ Pamella akawaka sasa na Jerry akamgeukia
‘…kuna chochote cha uongo au kibaya nimekitamka?’ Jerry
akauliza na hakujibiwa, akageuka akitabasamu na kuondoka jikoni. Pamell
akasikitika, ukweli ulimuuma na upende mwingine akaona ‘attention ya upendo’
ilikuwa kwa Jenifa zaidi kwa vile Jerry hakusema kwanini Jenifa asimtafute yeye
Pamella kumvuta kwake
Haraka akamfuata Jerry kule sehemu ya kulia chakula na
kumkuta akiwa anamimina juisi kwenye glasi
‘Hivi Jerry maishani mwako umeshawahi kumpenda mwanamke wka
dhati?’
‘Yeah…’ Jerry akajibu akiwa anaitazama juisi yake
anayoimimina kwenye glasi
‘ni mwanamke gani?’ Pamella akauliza akilini mwake akihisi
angelitajiwa Jenifa kutokana na majibizano yao muda mfupi
‘Sindi’ Jerry akajibu akimaliza kumimina na kumtazama
Pamella.
Namna alivyotoa macho, namna alivyoachama mdomo, namna
alivyotunduwaa ndiko kulikomfanya Jerry Agapella acheke kidogo na kumfuata
Pamella pale alipokuwa amepigwa bumbuwazi
‘…Mwanamke mwenyewe ni wewe Pam!’ akatamka akiipitisha mikono
yake kiunoni pa pamella na kuikutanisha mgongoni pake. Akamvutia kwake zaidi na
kumkumbatia lile tabasamu likitoweka usoni baada ya kumlaza Pamella kifuani
pake na Pamella lile bumbuwazi likipotea na tabasamu kuja taratibu lakini pia
akijiwa na hali ya kutoamini alichojibiwa. Kwa kiasi Fulani alijuta kuuliza
swali lile Siku tano tu kabla ya ndoa!
888888888888888888
Casino ya Madame imechangamka jioni hii kabla ya kuzama
vizuri. Meddy amesimama kwenye maegesho akiwa na simu mkononi.
‘…. Nipo mbali sana aisee… hapana… kesho basi… sio nakukwepa
kaka…kuna mambo mengi yananizonga kwa sasa… poa basi…poa… haya bwana’ akakata
simu. Jerry Agapella aliyekuwa chumbani kwake naye akabaki na simu yake
mkononi.
Mishemishe za Meddy alizijua vema lakini siku mbili tatu hizi
Meddy amekuwa mnyonge sana, amekuwa ovyo sana na amekuwa akikwepa kuonana naye.
Alihisi kulikuwa na kitu kikubwa kilikuwa kinaendelea maishani mwa Meddy na
hakutaka kumshirikisha.
Mwanzoni alihisi ni kitu kidogo lakini kwa kumtazama Meddy na
mambo yake sasa alianza kuingiwa na hofu kubwa juu rafiki yake. Akaiona hiyo
kesho waliyokubaliana kuonana kama nusu karne. Alitaka sana kujua nini kilikuwa
kimemsibu rafiki yake!
meddy baada ya kukata simu aliingia kwenye Casino akifuata
taratibu zote na kwenda kule kwenye eneo la vinywaji. Dakika tano tu zilitosha
kujua kulikuwa na mabinti wapya kwenye viunga vya wacheza uchi. Mabinti wazuri
sana waliojinyonga na kucheza kiumaridadi kwenye vyuma vilivyojengwa katika
viunga hivyo. Wakiwa na nguo za ndani tu zenye kuvutia na kutamanisha.
Hakutamani hata mmoja!
Wanaume waliojazana sehemu hizo wengine wakiwa wenyewe kama
yeye na wengine wakiwa na wanawake walionekana kuendelea na burudani za mule
ndani kwa raha zao wakati yeye akiwa na hekaheka zake kwa mara nyingine ten
andani ya Casino ile.
Kinywaji kilichokuwa mbele yake hakikusogea, Alimtazama yule
mcheza uchi kwenye chuma na wala asimtambue akilini. kwa mbali dj wa siku hiyo
akaachia mirindimo ya wimbo maarufu wa Nadina wa Nenda na wala usiangalie
nyuma.
mirindimo ya kuanza kwa wimbo ule ukamfanya Meddy ajisikie
vibaya sana, akamuita mhudumu aliyepita kando yake na sahani ya vinywaji
‘Nadina yuko wapi?’ akamuuliza moja kwa moja na binti yule
akamtolea macho kana kwamba alikuwa amemuuliza kama mahali wanapouza nyama za
watu.
‘naweza kukupa pesa…eeh… kama utaniambia…kama uta…’
akababaika Meddy akijilaza upande ili achomoe wallet yake lakini macho ya yule
binti hayakuwa kwake tena yalikuwa juu kuelekea dirisha la ofisi ya Adella na
Adella mwenyewe alikuwa amesimama dirishani hapo. Binti akarudisha macho yake
kwa kasi ya ajabu mbele ya Meddy. Akimeza mate kwa juhudi na hofu ikijitandaza
usoni pake kuliko kawaida
‘Sijui…’ akajibu akijiondoa mbele ya Meddy haraka sana wakati
Meddy alikuwa bado kimtazama Adella kule juu kwenye dirisha. Taratibu Adella
akatoweka dirishani na Meddy akashusha macho yake chini kwa taabu akiweweseka.
Ule mkono ulioenda nyuma kushika wallet ulitoka taratibu na kurudi mezani.
Dakika nzima ikamkatikia, wenge likimtawala kwa muda. Ghafla
tua akagutuka kuona kiti cha mbele yake kikivutwa na Adella akaketi mbele yake.
Wakati huo wimbo wa Nadina ukiendelea hewani na watu wakimuuliza msichana huyo.
‘hatuna sheria wala muamuzi lakini bado tuna mipaka ya
shindano letu… Please! don’t mess with my waitress’ Adella akaongea akitabasamu
Meddy akamtazama tu, hakuweza hata kumjibu chochote. Adella
akasogeza kichwa chake mbele zaidi
‘When I’m done nikuite kwenye mazishi?’ akauliza na kungoja
jibu lakini hakupata zaidi ya kushuhudia koromeo la Meddy likipanda na kushuka
kwa nguvu na kisha taya zake kucheza kutokana na kuuma magego yake kwa hasira.
‘Oh!... nitakuletea kadi ya mwaliko basi!...keep on fighting
back… but make sure you don’t fight your own back’ akaongea taratibu na
kuinuka. Kwa madaha ya kike akaiacha ile meza na kutokomea akimuacha Meddy bado
anamtazama kwa ghadhabu. Ile njia alioelekea akakutana na yule binti aliyekuwa
anaongea na Meddy.
Kikasikika kibao kikali kilichomuwewesesha binti wa watu na
kufanya watu kadhaa akiwemo Meddy watoe macho na kushangaa tu. Adella
akaendelea na safari yake. Binti wa watu akijisugulia shavu lake kwa juhudi
zote. Meddy akahisi kutetemeka kwa ghadhabu, alijua Adella alifanya vile
makusudi kufikisha ujumbe kwa wahudumu wengine kuwa hakukutakiwa maongezi ya
nje ya kazi kwa Meddy!
Kazi ya kumsaka Nadina ilianza kuwa ngumu zaidi kwake, wakati
akihamanika pale mezani. Nadina alikuwa amelala kule kwenye kile chumba, vile
vile, pale pale na aliusikia vema ule wimbo na kukumbuka wakati anauimba na
kumtazama Meddy. Akakumbuka ahadi aliyompa kabla ya kukishuhudia kifo cha Tima.
kuwa angeongea naye kuhusu Sindi. Akaikia mlango ukifunguliwa taratibu na mtu
akuingia kwa tahadhari. Ni dhahiri mtu aliyeingia hakutaka watu wajue alikuwa
ameingia pale.
Nadina akajilazimisha zaidi kufungua macho, ila hakuweza
lakini akaiona vema sahani ya chakula ikitua mbele yake na maji ya kunywa. na
mtu huyo aliyeingia akamfungua kamba alizofungwa mikononi kule mgongoni na
kumnyanyua. Nadina akauma meno alikuwa na amaumivu kila kona.
Akasaidiwa kuketi na sasa akatazamana na mtu huyu aliyejitosa
kumfanyia haya. hakumuona vema, alionekana kama kiwingu Fulani wakati
akimsogezewa maji mdomoni na kumnyweshwa haraka kiasi cha mengi kumwagikia
chini
88888888888888888888
Saa tatu usiku katika mitaa ya jiji hili mbele ya mgahawa wa
kisasa kabisa. Gari la mzungu linaonekana likiwa limeegeshwa hapo na watoto
wawili watatun wa mitaani wakilizunguka na kulishangaa sit u kwa uchakaavu wake
bali pia kwa ule muundo wake wa kizamani.
watu anapita nje ya mgahawa huo hawaachi kugeuka na
kulishangaa. Mwenye gari yuko ndani ya mgahawa akizungumza na mtu. Mwanamke
mzungu mwenzake, ni Daniella mke wa Dennis Mazimbwe, mwanasheria mashuhuri.
Wanazungumza kifaransa ingawa Daniella si mfaransa…
‘….usiniambie umerudi porini kuendelea na mambo yako
Francois!’ Daniella anashangaa
‘niko makini zaidi ya mwanzo…’ akajitetea akigida kinywaji
chake
‘hata kama! huwezi kujua nani anakufuatilia….Dennis hawezi
kuhatarisha tena taaluma yake kukuondoa hatiani kama utashikwa tena’ Daniella
akamuonya
‘una hofu mno!... najua ninachofanya… hii ni mara ya mwisho
na nitarejea nyumbani’ akatabasamu wakati Daniella akiteremsha pumzi taratibu
‘na iwe mara ya mwisho kweli…. Dennis hajui kma uko
hapa…Dennis hajui kama umerudi kujiingiza kwenye biashara haramu… mbaya zaidi
passport yako imeisha muda wake tayari…Francois usiwe mbinfsi kiasi hiki…
unadhani nitalala kwa raha huku nikijua umeishia jela?’ Daniella alieleza
wasiwasi wake na ile hofu ikizidi kuonekana
Mzungu akavishika viganja vya mikono ya Daniella
‘…sitakuangusha! nitarejea nyumbani nikimaliza ninachofanya’
akajitahidi kumtuliza Daniella
‘Sijui sababu yaw ewe kufanya biashara haramu….lakini
ninachojua bado una nafasi ya kutumia taaluma yako ya udakatari wa wanyama vizuri na kihalali… achana na hivi
vitu Dk. Francois…. nakuomba… mtoto wako pekee atakuwa amekukumbuka sana… na
sidhani hata marehemu mkeo anafutahia haya unayoyafanya’ Daniella akaongea kwa
uchungu zaidi.
‘…sawa…sawa… ngoja nirejee porini… nimekuja kununua vyakula
pamoja na nguo… kuna binti ninaishi naye’ Francois akaongea akitabasamu na
akiubeba mfuko uliokuwa pembeni ya miguu yake na kuuweka mezani
Daniella akakaza macho ghafla na kuyatumbua
‘binti?...’ akauliza
Na Francois hakujibu kitu zaidi ya kutabasamu, akanyanyuka na
kusimama mbele ya Daniella akijiandaa kuondoka. Akatoa wallet yake na Daniella
akamzuia na Francois akarudisha wallet yake kwenye mfuko wa nyuma wa suruali.
‘nitalipia… lakini huyo binti ni nani?’ akauliza Daniella
‘Nitamleta uzungumze naye au haya nanny najua ataelewana
naye…ni mzuri mzuri sana…mdogo tu…na mjamzito’ Francois akatabasamu tena wakati
akimuelezea Sindi
‘Mungu wangu!.... Anko usiniambie umempa mimba binti wa watu
wakati ukijua huwezi kuishi hapa..’ Daniella anaye akasimama
‘hapana…hapana… sio hivyo… hazungumzia kifaransa na wote na
mimi sijui kuongea kiingereza fasaha na sidhani kama anakijua… nimlete umuone?’
Francois akauliza akimtazama Daniella mtoto wa mdogo wake
‘Ndio..mlete ndio… huwezi kukaa na binti mjamzito porini uko…
mlete haraka sana…’ Daniella akajibu akiwa makini
‘na usimwambie chochote Dennis kuhusu uwepo wangu hapa…’
Francois akaonya
‘Kama hivyo ndivyo unavyotaka…ni sawa… safari njema na uwe
mwangalifu’ Daniella akamuaga akitoka pale mbele ya kiti na kumkumbatia mjomba
wake.
Wakatoka kwa pamoja na asimuone Fiona na Iloma waliokuwa
wanapata chakula kwenye mgahawa huo.
‘Sikujua hata wazungu ni mapepe…’ Fiona akaongea akiwatazama
Francois na Daniella wakitoka nje
‘Kwanini?’ Iloma akauliza akirudisha macho mlangoni kule
kuwatazama wanavyoishia
‘Huyo mwanamke ni mke wa Dennis Mazimbwe’ Fiona akatabasamu
kama mtu aliyepata wazo
‘lakini wote wazungu ukute ni ndugu yake…’ Iloma akampinga
‘watajijua wenyewe… ngpja kesho nikamuone Dennis na mikwara
kibao… ataniambia tu kinachoendelea kwenye maisha ya Kristus… I don’t give up
that easily’ Fiona akaongea kwa kujiamini sana na Iloma akimtolea macho tu..
ITAENDELEA….
sasa story imeanza kunoga.
ReplyDelete