Friday, December 20, 2013

SINDI...NA LAURA PETTIE (49)

49

Gari aina ya Acadia iliserereka barabarani ikiwa katika mwendo wa kasi kiasi, dereva aliyekuwa ameukamata usukani kwa mikono yote miwili alikuwa akibubujikwa na machozi kiasi cha kushindwa kuona mbele vizuri. Akauondoa mkono wa kushoto toka kwenye usukani na kuutumia kupangusa machozi yaliyoonekana kuuelemea uso wake.


Akaurudisha mkono kwenye usukani na kukata kona, akiiacha barabara ya lami na kukamata njia yenye changarawe, akaongeza mwendo kidogo, sasa akiuma midomo yake na kuimeza kwa ndani katika namna ya kujaribu kujiweka sawa, alibana pumzi kidogo na kufanya mishipa ya shingo imsimame kabla ya kuiachia pumzi sambamba na ile midomo yake. Taratibu ule mwendo kasi ukapungua kadiri alivyokuwa akiikaribia nyumba ya ghorofa moja iliyokuwa  mita kadhaa mbele yake.

Akapunguza mwendo na kusimama upande wa pili wa nyumba ile, akzima gari na kushusha kioo cha dirisha lake taratibu, akaitazama, akaingalia na  kuikodolea macho ile nyumba iliyokuwa inavutia machoni si tu kwa ujenzi wake bali pia mng’ao wa taa nyingi zilizokuwa zimewashwa usiku huu wa saa tano kasoro.

Daniella mke wa Dennis Mazimbwe akakilaza kichwa chake kwenye kiti wakati akiyahamisha macho yake toka kule kwenye ile nyumba na kutazama mbele. Akili yake ilikuwa katika ushindani na dhamira yake moyoni. Alitaka kuteremka toka mule garini na kuingia ndani ya nyumba ile ya Mzee Okello. Alitaka kuonana na Rebecca pamoja na mumewe, alitaka kuyasema yote ya moyoni mwake mbele ya Okello. Alitaka Rebecca aonje hata theluthi ya uchungu anaousikia kuona ndoa yake ikiparaganyika sababu yake.

Dhamira yake ilibeba kisasi cha ajabu, kilichovaa joho la hasira na kofia ya chuki lakini akili yake haikubweteka na kukubaliana na dhamira yake. Aliona kama alikuwa anaelekea kuleta athari zaidi kubwa kuliko zilizopata kujitokeza. Akatulia vile akitazama mbele kama mtu aliyepotewa na akili.

‘…huwezi kulia tu maisha yako yote sababu ya Dennis…anapaswa kuamua kuwa na wewe au huyo mwanamke… Daniella you deserve the best… kwanini umpiganie mwanaume?...why?... yeye ndiye anapaswa kukupigania usiondoke kama kweli anakupenda… niahidi hutalia tena sababu ya Dennis na kama itatokea fungasha vifurushi vyako na uanze maisha yako… mtaliki!’ maneno ya mama yake wakati akizungumza naye yalipita kichwani mwake kama kipande cha sinema. uso wake ulitulia na hata machozi yalishakoma kutoka.

Daniella akashusha pumzi ndefu, akipunguza ukubwa wa macho yake na ndita mbili zikikunjika usoni pake. Pumzi ile ikamrejesha pale alipokuwa. Akazikusanya nywele zake za rangi la samawati na kuzirudisha nyuma, akizifunga kwa chupio yaliyokuwa amebandika kichwani pake.

Kama mtu aliyepata wazo jipya, akawasha gari lake na kuliondoa eneo lile taratibu. Akili yake ilifanya uamuzi pale pale na alipotoka pale alielekea lodge moja ya kisasa na kuamua kuutumia uisku ule peke yake, akiutafakari uamuzi wake nap engine akijipa mikakati ya kuutekeleza. Wakati akifanya uamuzi wa kulala nje, mumewe alikuwa katika hekaheka ya kumtafuta mpaka pale alipopata uhakika kuwa Daniella alikuwa salama ndipo naye alipouweka ubavu kitandani, ikiwa ni usiku wa saa nane na vichapo kadhaa.
888888888888888888888

Wakati watu wengine wakiusaka usingizi kwa bidii zote, Patrick Mazimbwe alikuwa chumbani kwake akipiga funda kadhaa za pombe. Uso wake ulikuwa mtulivu mno na wala hakuonekana kuwa na maumivu yoyote wakati ule. Alikuwa ameketi kwenye sofa lililokuwa chumbani kwake na kunyoosha miguu juu ya stuli aliyoiweka mbele yake. Pembeni kwa mbele aliweka laptop iliyokuwa ikionyesha picha zake na Pamella, zikipishana sekunde hata sekunde. Alizitazama taratibu huku chupa ya pombe kali ikipanda kuelekea mdomoni na kushuka taratibu kisha kutua juu ya paja lake la kushoto bila kuachiwa.

Alitabasamu, tabasamu lililokosa tafsiri rasmi, akaikodolea macho picha ya Pamella Okello iliyojitokeza kwa mara nyingine, akaitazama ilivyotulia pale na kisha kupotea kabla ya kujitokeza nyingine iliyowaonyesha yeye na Pamella wakiwa ufukweni. Picha ile ilidumu kwa sekunde moja tu na Patrick akajikuta akiifunga laptop yake pasipo hata kuizima.

Akatulia tu, akatulia sasa akiwaza mawazo yaliyokuja katika mpangilio mbovu. kichwa kikamzunguka, kwa wakati ule hakuona thamani hata ya pumzi aliyokuwa anaivuta. Kwa wakati ule ndio aligundua ni kiasi gani alikuwa namapenda Pamella Okello kuliko Clarita Gabson. kwa wakati ule ndio aligundua ni kiasi gani furaha yake ilikuwa imajengwa juu ya msingi wa uwepo wa Pamella. Kama kuna mtu angelimweleza kuwa mapenzi yanaua wiki chache zilizopita si ajabu angelimcheka kupitiliza, lakini sasa hali aliyokuwa akiisikia na kuihisi ilitosha kumhakikishia kuwa mapenzi yanaua!

Akabugia pombe yake kwa fujo mno, nyingine ikishindwa kuingia mdomoni na kuchuruzika pembeni, Alipoitua ile chupa alikuwa akihema mithili ya mwanariadha aliyemaliza mzunguko wa mbio za kuruka viunzi. Akaangaza angaza mule chumbani kana kwamba alitarajia kuona taswira yoyote ya kumpa ahueni, hakuona chochote, hakuona lolote, hakuona yoyote! Akafumba macho na kusikilizia maumivu ya moyo! kuachwa ukusikie tu na kukusoma karatasini!
88888888888888888888

Wingu lililokuwa limetanda usiku uliopita, lilileta mvua ya asubuhi na mapema. Mvua ya rasharasha iliyonyesha bila kukatika tangu alfajiri. Baridi ndogo iliyohitaji japo koti la kuzugia iliongeza utamu wa mvua ile ya asubuhi. Dennis aliingia ofisini kwake, koti yake likionekana kuwa na matone machache ya mvua iliyomnyeshea wakati akitoka kwenye maegesho na kulifuata jengo la ofisi.

Alivua koti lake na kulitundika sehemu yake, akaifuata meza yake ya kazi na kuitua briefcase yake juu ya meza. Macho yake akatua kwenye  karatasi chache zilizokuwa zimeunganishwa pamoja. Akakunja uso wakati akiziokota na kuzisogeza usoni, zile ndita zikawa tatu sasa.

Mkono wa huohuo uliokuwa na zile karatasi, ukaziminyia kidogo na kuifuata simu ya mezani. Akabonyeza namba mbili tatu na kusikilizia
‘Huu ni upuuzi gani hapa mezani?’ akahoji akiwa ametoa macho, jazba zilikuwa zinapanda kwa kasi ya ajabu. Hakungoja hata yule aliyempigia amjibu. Akakata simu na kuurejesha mkonga sehemu yake, kisha akachanua tena zile karatasi na kuzisoma kwa mara ya pili kana kwamba akili yake ilikuwa imesahau yote aliyoyasoma mara ya kwanza
Sekretari wake akafungua mlango na ukingia kwa kasi kidogo, uso ukiwa na wasiwasi
‘hizi barua za wiki iliyopita zinaletwa kusainiwa leo kwa misingi ipi?’ Dennis akauliza kwa sauti kali kidogo
‘Zilisahaulika kwenye faili la barua zinazoingia…samahani kwa hilo’ Skretari akajitetea na asijue moto aliouwasha
‘Ulisahau?... unalipwa mshahara hapa kusahau vitu?... hujui majukumu yako?... ujinga gani huu sasa?... hebu nenda kaandike barua zenye tarehe ya leo na uwatumie fax ya kuwaomba radhi kwa kuchelewesha majibu.. uzembe wa aina hii siutaki ofisini hapa na kama unadhani akili yako haina uwezo wa kutunza kumbukumbu kaa pembeni…kuna watu wanahitaji kufanya kazi ufanisi sio kuleta excuse za kijinga jinga kama hizi’ Dennis akagomba kwa ghadhabu na kumtupia sekretari wake zile karatasi.

Binti wa watu akaziokota kiunyonge na kutoka mule ofisini akiwa na maswali mengi kichwani. Ni mwaka wa tano sasa tangu aanze kufanya kazi na Dennis Mazimbwe. haikuwahi kutokea kugombezwa namna hii, kwa staili hii kwa kosa kama hili kwani ni mara nyingi walikuwa wakisahau vitu na kuvirekebisha kirafiki tu bila kukaripiana kama watoto.

Dennis akajihisi ahueni baada ya kutolea hasira zake kwa sekretari wake. Akaketi kitini na kuanza kushika hiki na kile lakini dakika moja tu ilipokatika kijana mmoja akaingia ofisini kwake akiwa na faili mkononi.
‘Mr. Mazimbwe… kuna appointment mbili leo jioni sasa tunata…’ kijana wa watu hakumalizia hata kauli yake kwani Dennis alimkata jicho kali na kumjibu katikati ya maelezo yake
‘hivi ni kwanini hamuwezi kufinalize kitu bila kuleta miguu yenu humu ndani… sidhani kama mtindo huo ndio nitakuona mchapakazi Edgar!... please show yourself out!’ Dennis akamalizia kwa kuinamia laptop yake na kuendelea na alichokuwa anafanya. Yule kijana akawayawaya kidogo akionekana kupigwa na butwaa kwa lile jibu. Taratibu akaondoka zake.

Nafuu nyingine  ikamtembelea Dennis, asijue ni kiasi gani nafuu aliyokuwa anaitafuta ilikuwa imewaumiza wengine wasiohusika na vurugu zake kichwani. robo saa tu zikapita, Simu yake ikaita, akaipokea na sekunde kumi na tano tu baadaye Rebecca Okello akaingia mule ofisini.

Alikuwa amevalia gauni lake jeusi ilililonakshiwa kwa kitambaa cha kitende kiunoni kilichochanuka kama mwamvuli. Lilikuwa gauni lililombana kiasi na kuonyesha umbile lake tulivu la kiutu uzima. Lilikuwa limeishia chini kidogo tu ya magoti. kiatu chake kirefu kiasi kililandana rangi na kile kitambaa cha kitange kiunoni na sehemu ya kola.

kichwani alikuwa na afro dogo, tulivu, lililozungushiwa utepe mwembamba wa kitenge. Alionekana kama mwanamke wa kisasa aiwakilishaye afrika. Weupe wake wa asili uliokoza na kurutubishwa na vipodozi, uliirudisha nyuma miaka ya Rebecca. Alikuwa mrembo! mrembo hasa!... Pochi yake aliibana kwapani mkono wa kushoto wakati akiingia kwa kuusukuma mlango kwa mkono wa kulia uliokuwa pia na funguo za gari.

Akaingia mwanamke, akiichafua pia ile ofisi kwa manukato yaliyosisimua pua yoyote ya mwanaume rijali aliyejua thamani ya manukato. Dennis akainua uso na kumtazama Rebecca alivyoufunga mlango na kuchapua hatua kadhaa kumfuata. Akatembea mpaka pembeni ya kiti cha Dennis na kujiegemeza kwenye ukingo wa meza mbele ya Dennis.

Wakatazama tu! Dennis akiwa ameketi kwa mtindo wa kulaza kichwa kwenye kiti chake huku akijizungusha taratibu kulia na kushoto
‘Why are you doing this to me Dennis?’ Pamella akauliza kwa sauti ya kubembeleza. midomo yake minene iliyonakshiwa kwa rangi yam domo ikimwemweseka na kuzidi kuvutia pale meno yake meupe yaliyopoonekana

Dennis akajiinua kidogo na kushusha pumzi kwa nguvu. Ilihitajika nguvu ya ziada kumshinda shetani!
‘Becca!..’ Dennis akaita kwa sauti ya chini kisha akasita kwanza
‘… Daniella is back’ akajieleza na kujieleza uko kukamkera kweli Rebecca aliyejikuta akitazama kando
‘nisikilize mama… nisikilize basi’ akabembeleza Dennis akiugusa mkono wa Rebecca ambaye taratibu aligeuza kichwa na kumtazama Dennis ambaye alijiinua na kusimama wima, Akamzidi Rebecca urefu na aikawa zamu yake kumtazama Rebecca toka juu

‘…kuna wakati nahisi tunakoelekea kila kitu kitakuwa wazi… I won’t be safe’ akatoa hofu yake uso wake pia ukionyesha ile hofu waziwazi
‘Kwanini?... kwanini usiwe safe?’ Rebecca alijaaliwa uzuri wa kubabaisha ila si ubongo wa kufikiri kwa kina. Mungu hakupi vyote!
‘wewe ni mke wa mtu Becca… Okello mumeo ni mtu tunayefahamiana… what if akijua kinachoendelea?... what if akijua Pamella si binti yake…ni binti yangu… hawezi kuniacha salama’ akajaribu kumuelewesha lakini Rebecca ahakuonyesha kushrushwa na hilo

‘La Pamella haliwezi kujulikana labda mimi na wewe mmoja wetu atoe siri… kitu ambacho hakiwezekani… kuhusu mimi na wewe… mi sioni cha kumfanya akudhuru… mapenzi yakiisha  yameisha na nina uhuru wa kuwa na mwingine’ Rebecca akajieleza na kumfanya Dennis azidi kuuona umbumbu wa mwanamke huyu aliyeiteka nafsi yake kwa miaka mingi. Utu uzima ulikuwa umemfika Rebecca, lakini tabia na uwezo wake wa kufikiri ulikuwa wa Rebecca yule yule aliyemuona kwa mara ya kwanza katika harusi ya Okello na Rebecca.

‘… hata tukimuweka pamella kando… mimi ni mwanaume…I know how it feels mke wako, mwanamke unayempenda unapohisi tu kuwa anaguswa na mwanaume mwingine achilia mbali kuachwa na kwenda kwa mwingine… naweza kuua Rebecca.. naweza kufanya jambo la kijinga sana… kwa vile najua inavyouma’ Dennis akaongea kwa upole akimtazama Rebecca usoni.

‘Kwa hiyo ina maana Daniella akiamua kuwa na mtu mwingine utaumia pia?’ Rebeca akamtega
‘Sana!... sana tu… sitaki kukuficha Rebecca… sisis ni watu wazima sasa… mapenzi ya kitoto hakuna tena… nakupenda Becca but that doesn’t mean simpendi Daniella… I love her, she is my wife… amepita mengi sana sababu yangu…’ Dennis akaongea akiutazama uso wa Rebecca uliokuwa umesinyaa na kujaa hali ya kutotaka kusikia yale aliyokuwa akiyasema Dennis

‘So unamoenda zaidi yangu si ndio?’ Rebecca akauliza akiukwatua mkono wake toka mkononi mwa Dennis
‘Siwezi sema juu ya hili Rebecca…it wont be fair na sitaki kudanganya’ Dennis sasa akamsogelea zaidi Rebecca na kutaka kumtomasa lakini akazuiwa

‘I swear Dennis… nimeolewa na Okello nikakuta watoto wengine kwake… nikamzalia okello mtoto mmoja tu wa kike na akwa wa kike pekee kwa Okello na bahati mbaya si wake ni wa kwako… hivyo nina mtoto mmoja tu maishani mwangu niliyezaa na wewe.. Dennis ukiniacha nakuhakikishia utakuja kunizika… sitanii…ukiniacha ni umeniua… sijali kitu…’ Rebecca akatoa onyo

‘Usiseme hivyo Babe… no! sina hata wazo la kukuacha Rebecca.. sina kabisaaa… it is me and you mpaka mwisho…ondoa hayo mawazo ya kujiua sijui kufa…please!’ akamsogelea zaidi na kumkumbatia Rebecca kuongezea nguvu yale maneno yake lakini uso wake ulionekana kuelemewa na maneno yake mwenyewe. Kauli za Rebecca kujiua kwa ajili yake zilishajirudia sana kiasi alihofu zingetimia endapo angejaribu kufanya alichotaka kufanya. Kumuacha Rebecca moja kwa moja!

Wakaachiana na Rebecca Okello akatabasamu, nuru na amani ya moyo vikionekana moyoni mwake.
‘You are my life Dennis… I wish tuwataliki wenzi wetu na tuoane sisi… nimechoka kuibia ibia mapenzi Dennis… ila kama huwezi kumtaliki Daniella angalau na mimi nijali kama unavyomjali yeye… usiniache Dennis… nitakufa!’ akarudia tena ile kauli na kumkera Dennis sasa

‘Rebecca!’ akamuita kwa msisitizo, akimshika mabega yote mawili
‘…naomba usirudie hii kauli ya kufa kwa ajili yangu… sikuachi sawa?... sikuachi Rebecca…’ Akajikuta akiahidi tena na tena pasipo kuwa na uhakika na kile anachoahidi.

Wakatazamana na kukumbatiana tena kwa mahaba mazito.
‘Baba Pamella!’ Rebecca akamuita Dennis, akamtania kwa kumuita vile wakiwa vile vile walivyokumbatiana na Dennis akacheka akimuachia Rebecca na kumbusu pajini kwa upendo.
8888888888888888888888

Jerry na Pamella walikuwa mbele ya mtaalamu wa kuandaa harusi. Ofisi ya mtaalamu huyo ilikuwa kubwa iliyosheheni mambo mengi ya fani yake. Mwanadada huyu alikuwa ameketi kwenye kiti cha peke yake akiwatazama Jerry na Pamella waliokuwa wamebanana katikati kwenye sofa moja la kutosha watu wawili.

Kwa haraka tu, Pamella Okello alionekana kuwa na furaha zaidi ya Jerry Agapella.
‘nataka rangi wa pinki iliyopauka na nyeupe na kahawia hivi…yaani kitu mchanganyiko  Fulani mzuriii… eti honey we unaonaje?’ Pamella akamuuliza Jerry ambaye alionekana kutokuwepo katika yale mazungumzo

‘Jerry!’ Pamell akamsukuma kidogo na kumshtua Jerry
‘Oh.. what…nini?’ akauliza akijitutumua kutabasamu. Pamella akaeleza tena mawazo yake na Jerry akaitikia tu bila kupinga
‘Babe… kila kitu unasema sawa sawa… huna chochote cha kuongeza jamani?’ Pamella akalalamika
‘nakuamini babe…’ Jerry akajibu na kumbusu midomoni Pamella. Yule mtaalamu wa kupanga harusi akatabasamu tu na kuwatazama wapendanao hao ila hata yeye alihisi bwana harusi hakuwa na ile hali ya kufurahia mipango ya harusi yake. Akamezea!

‘sasa mimi nitakupa sample ya namna tunavyopamba… mfano kuna viti na meza aina tofauti tofauti na kuna mpangilio wa matukio katika harusi… it is just we make your event very unique in a way hata wewe unabaki na kumbukumbu safi kabisa’ Mtaalamu akasafishia njia kazi yake na Pamella akaitikia ilhali Jerry alipepesa macho tu.

Wakajadiliana hapo na kufikia muafaka wa kurudi tena siku mbili mbele. Wakatoka hapo kwa mtaalamu na kutoka nje ambako mvua sasa ilishaacha kunyesha ila manyunyu yalibaki yakidondoka taratibu. Pamella akasimama kado ya gari lake na kumtazama Jerry aliyekuwa naongea na simu. yale manyunyu yalimfanya akunje uso na kuukinga kwa kiganja cha mkono.
‘Hey…bye babe!’ Pamella akamuita Jerry aliyekuwa bado akiongea na simu na kumpungia mkono. Alihisi angezidi kulowana kwa kumngoja Jerry ambaye wala hakuysjali sana yale manyunyu. Jerry naye akampungia mara tatu na kuendelea na simu yake

Pamella akaondoa gari na kuishia zake, Jerry akmaalizia mazungumzo na kulifuata gari lake. Akawasha na kuliondoa akielekea nyumbani kwao.
Alimkuta baba yake jikoni akikaanga mayai.
‘Wasaidizi wako wapi?’ Jerry akashangaa
‘sio kila wakati unahistaji kuzungukwa na watu… wakati mwingine kuwa mwenyewe kunakupa nguvu ya kuufurahia uhai ulio nao’ baba yake akamjibu akigeuza yai lake lililokuwa limeungua vibaya mno.
Akazima jiko na kulipakua yai lake kwenye sahani.
‘leta uma na kisu tushambulie hiki kitu’ akamuagiza mwanae yeye akitangulia kuelekea sehemu ya kulia chakula

Jerry akacheka kwanza wakati akilifuata kabati, pale mezani Jerry alimpa baba yake uma na kisu, yeye akijimiminia maji tu na kuketi kiti kilicho mbele ya baba yake
‘Huli?’ baba yake akamuuliza akianza kukata lile yai
‘Nope!... lilivyoungua hivyo?... no! enjoy tu’ Jerry akacheka kwa sauti akimtazama baba yake aliyekuwa amekunja uso baada ya kutupia kipande cha yai mdomoni.

alipoanza kutema vitu alivyohisi visingemezeka, Jerry akazidisha kucheka zaidi. Mzee Agapella akaisogeza sahani pembeni na kuvuta karatasi ya kufutia mdomo. Akajifuta na kuiweka ndani ya ule msosi.

Sasa akamgeukia kijana wake huku naye akijimiminia maji.
‘You don’t look excited wakati ni harusi yako Jerry’ baba yake naye akatoa wasiwasi wake
‘niko sawa baba… ni vile mambo mengi sana… kuna harusi, kuna kazi ofisini na mambo mengine binafsi… ila niko sawa’ Jerry akajitetea
‘Umepewa likizo ya mwezi mzima…na nimekaimu nafasi yako ofisini mpaka urejee… nini kinakupa hofu Jerry?... unaoa binti mzuri, rafiki yako wa siku nyingi, mwanamke anayetoka katika familia kubwa inayofahamika na zaidi una support toka kila mahali…. nini kinafanya uwe mnyonge mnyonge hivi?’

‘Niko sawa kabisa… labda ni hofu tu ya kuwaza ndoa itakuwaje… nimeona mengi baba toka ndoa yako na mama hadi nah ii ya Fiona ambayo sijui ndio imeshavunjika au lah… naona kama ndio mwanzo wa maisha mengine kabisa’ Jerry akajitetea akitafuta sababu ilhali akijua wazi kilichokuwa kinamnyong’onyesha si kile alichokiongea.

Mzee Kristus Agapella akamtazama kijana wake kwa umakini mkubwa. Aliiona hofu ya mwanawe na akahisi hali ya kujilaumu pia kwa kumletea ile hofu aliyotaja. Akajitutumua kutabasamu

‘Jerry!’ akamuita kwa upole akimsogezea uso mbele kuleta umakini
‘ndoa haina kanuni kama hesabu!... kitakachoijenga ndoa hii ukute ndio kinachoivuruga ndoa ile… ndoa ni wewe na mwenza wako!... ni maisha ya kila siku kati yako na mwenza wako… Kilichonitokea mimi si lazima kikutokee wewe labda tu ufuate nyayo nilizofuata mimi… I made a mistake Jerry… na majuto ya kosa nililofanya kwa Sophia nitaingia nayo kaburini!... najua siwezi kubadili kitu lakini nimechagua kuishi maisha ya kujisamehe nikiamini mimi ni binadamu nakosea na kupotoka’ Mzee akaongea kwa hisia zaidi

‘I married Sophia for love… nikamuona Fiona kwa tamaa… sijui hata akili ilikuwa wapi.. sijui hata ilikuwaje lakini maisha niliyoishi na Sophia ndio maisha ninayoyaita ya furaha… muoe mwanamke unayempenda kwa dhati…ambaye unadhani hutaona udhaifu wake kwa mapana kuliko ubora wake… you will be happy son!... ndoa sio harusi siku zote zipo nyakati za msiba pia… zipo nyakati za kushikamana na kutengana… zipo nyakati za kulia pamoja na kulia peke yako lakini mwisho wa siku ni upendo wa dhati ndio uwaleta tena pamoja na kudumisha ndoa… anayekuvumilia ndiye anayekupenda!’ Mzee akatulia kidogo kupisha mate yapite kooni

‘… tunatoka nje…sawa! tunacheza rough nje…hiki sio kitu cha kufichana Jerry lakini mwanaume anayemuheshimu mke wake hatokaa afanye rough hizi kwa uwazi wa kumfanya mkewe ajue! Never! ever!’ akatikisa kichwa kwa msisitizo
‘and you let mom know uko na Fiona!’ Jerry akaongea kwa sauti ya kumsuta

‘Yes!... na ndipo majuto yalipo na ndipo maswali yalipo… sijui ilikuwaje… sijui Jerry…’ Agapella akawa mkweli kwa kijana wake
‘and I hope Pamella ndiye mwanamke uliyetayari kumvumilia na kuona mapungufu yake kwa mbali sana… niko sahihi?’ baba yake akamuuliza na Jerry akatabasamu tu. Swali hili hakulijibu mdomoni bali alilijibu moyoni kwa kutamka kimoyomoyo ‘hapana!’
8888888888888888888888888888

Nadina alitembea kwa madaha kwenye kordo ya kuelekea kwenye vyumba vyao vya kulala. alipoukaribia mlango wa chumba chake alivua kiatu kimoja na kuchechemea kidogo kabla ya kuvua cha pili na kuvishika mkononi. Akaufikia mlango na kuufungua, akiusukumia mbele na kutanguliza kichwa akitabasamu.

Akaguna na kurudisha nyuma kichwa chake, akautanua mlango kwa mapana ya kutosha na kuingia shingo ikimnyoosha na kukitanguliza tena kichwa kuchungulia huku na kule. Akamuona Sindi Nalela ameketi kitandani kwa mtindo wa kujikunyata kama mtu asikiaye baridi.
‘Sindi..Sindi…’ Nadina akaita kwa hofu akivitupa vile viatu mkononi na kumharakia Sindi pale kitandani. Akaketi na kumtikisa Sindi aliyekuwa anatetemeka na kupepesa macho kama mtu alijawa na hofu kupitiliza, ama aliyeona kitu cha kushtukiza.

‘Sindi… nini kimetokea?’ akamuuliza akizidi kujisogeza karibu yake na kumtikisa. kule kumkaribia kukamfanya Nadina aone damu puani mwa Sindi na damu ile ikamsisimua na kumfanya atanue macho yake zaidi kana kwamba alitaka kuihakiki ile damu kwa kutumia macho.

Moyo ulipiga kwa kasi ya ajabu mno, mikono ikamtetemeka wakati ile damu ilipokuwa inazidi kutokeza puani na kuchuruzika kuelekea kwenye midomo ya Sindi. Nadina akachanganyikiwa zaidi Sindi alipoanza kulegea na akionekana wazi kuishiwa nguvu
‘Jerry…’ Sindi akatamka kwa sauti hafifu macho yakimlegea zaidi na ile damu kuongeza kuongezeka taratibu. Nadina akanyanyuka na kutafuta kanga, akaitumia kufuta ile damu na hapo hapo akipata akili ya kumlaza chali kitandani kabla ya kutoka kuomba msaada.

hakujua wala kukisia Sindi alikuwa amekutwa na masaibu gani.
‘jerry…’ akaita tena na umakini wa Nadina ukaongezeka baada ya kulisikia jina hili kwa mara ya pili
‘Jerry ni nani?...Sindi…Sindi…Jerry amekufanyaje?’ Nadina alihaha kutaka kujua zaidi wakati Sindi akielekea kupoteza nguvu zaidi
‘namtaka Jerry..’ akasema tena kwa shida safari hii machozi yakitiririka pembezoni mwa macho yake na ile damu ikiongezeka

‘Mungu wangu…Jerry ni nani?... Sindi jamani… Sindi…Sindi’ Nadina sasa alikaribia kuwehuka, akauliza kwa kupayuka, akauliza kwa hamaki, akauliza akitetemeka. Sindi akamtazama tu akimwemwesa midomo yake. Ni kama vile alitaka kusema neno kamili lakini sauti yake ilikwamia kooni. Alikuwa amelegea kupitiliza na damu haikuacha kumtoka puani. Sindi akatabasamu, tabasamu lililoashiria maumivu yaliyogusika kwa mikono ya binadamu.

Nadina akasimama ghafla na kumtazama Sindi kwa macho ya mshtuko. alitetemeka mpaka utumbo. alimtazama Sindi vile alivyokuwa amelegea na zile damu na lile tabasamu. Kwa mikono iliyotetemeka akamuinamia tena huku akilengwa na machozi na kuitazama blauzi ile aliyoivaa Sindi. akaitazama kwa umakini na kukitumia kidole chake cha shahada kusugua unga mweupe ulionekana kwa mbali juu ya ile blauzi.

Akalisugua lile eneo na kukipeleka kile kidole puani. Akahisi kuishiwa nguvu, akahisi kuhamanika, kutetereka machozi yakamtiririka. Alihisi kumpoteza Sindi, alihisi kulikuwa na zaidi ya maumivu katika maisha ya Sindi.

Sindi amekuwaje?... nini kimempata?... Siri ya Dennis na Rebecca ipo salama?... Daniella ameamua nini?... Jerry ana lipi linalomsibu asifurahie harusi yake ijayo… Majibu yote yapo hapa hapa!!


ITAENDELEA…..

3 comments:

  1. I appreciate your project!

    ReplyDelete
  2. namba 50 naisubiria kwa hamu sana

    ReplyDelete
  3. iam speechless laura nasubiria sehemu ya 50 tuu

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger