Thursday, December 5, 2013

SINDI....na LAURA PETTIE (48)

48

Casino la Madam Adella lilikuwa na utulivu ulioambatana na muziki wa taratibu uliokuwa ukiporomoshwa na Dj aliyekuwa zamu, taa za rangi ya bluu na nyekundu zilimulika ndani ya Casino hilo na kuleta mchanganyiko wa rangi uliohamasisha mahaba. Watu wengi walionekana kutulia sehemu zao huku wahudumu waliovalia nguo fupi za kuacha sehemu kubwa ya miili yao wakihudumia kwa kupita pita huku na kule kwa madaha.


Katikati ya casino hiyo kulikuwa na meza ya duara  iliyojengewa juu kidogo,  Katikati ya meza kulikuwa na mlingoti ambao binti aliyevalia nguo maridadi za ndani alikuwa akijinyonga nyonga na kuchezea mlingoti ule huku akifuatiza ule muziki wa taratibu, alionekana kuchota akili za wengi mule ndani walioonekana kufurahia uchezake wake.

Pamoja na burudani ile, bado Jerry Agapella alikosa utulivu wa nafsi. Akili yake iligoma kuona hali chanya mule ndani, akajikuta tu akitikisa kichwa katika namna ya kusikitika na kumgeukia Meddy aliyekuwa amezamisha akili yake kwa yule binti kule mlingotini.
‘Aisee, I’ve to go…’ akanena akimtazama Meddy ambaye hakumsikiliza wala kumsikia.

‘Meddy!’ akaita tena kwa msisitizo wa kubweka na Meddy akamgeukia akitabasamu, pengine kwa kudhani mwenzake alikuwa pamoja naye katika kuburudika. Akakumbana na uso uliojaa ndita kadhaa usoni, akashangaa!

‘Vipi?!’ akauliza akishangaa na hapo hapo akitupa jicho kule mlingotini na kisha kurudisha macho kwa Jerry. Ni kama vile hakutaka kupitwa na miondoko ya yule binti.
‘Come on Meddy… hebu nisikilize kwanza’ Jerry aliiona ile hali ya kupaparika kwa Meddy. Akahisi asingeeleweka bila kuulazimisha umakini wa Meddy uhamie kwake na akafanikiwa. Meddy akajigeuza mzima mzima na kumtazama Jerry.

‘Sioni cha kuniweka hapa… mi si shabiki wa kuangalia tupu za wanawake maeneo kama haya Meddy…’ Jerry akaongea kwa msisitizo
‘Just a minute na binti atakuwa hapa… unakimbilia wapi?’ Meddy akamtuliza
‘Sio kukimbia, sifurahii haya mazingira… mimi sio mtu wa makasino Meddy’ Jerry sasa aliongea kwa ghadhabu kidogo
‘Okay!... nipe dakika 15 na binti atakuwa hapa… ukishamuona tu nitakupa funguo uondoke na gari’ akamatuliza kwa unyonge uliochanganyikana na hali ya kutokukubaliana na Meddy akalazimika kutazama pembeni tu akikwepa kuizamisha akili yake katika mazingira yale.

Sekunde chache tu tangu marafiki hawa wabishane, Nadina akatokezea kwenye lango la kuingilia na kutembea kwa madaha kuifuata meza ya akina Meddy. Robo tatu ya wanaume waliokuwa mule ndani waligeuza shingo zao kumtazama Nadina aliyetembea taratibu, akimwagika kama mpunga unapopembuliwa, akikwatua hatua kwa hesabu za kukokotoa, akijumlisha hatua zake kwa tabasamu mantashau.

Akakatiza meza kadhaa, akikwatua mikono ya wanaume wakware waliokimbiza mikono yako japo kukigusa hata kiganja chake. Akawafikia akina Meddy na kuwasabahi. Jerry akajilazimisha kutabasamu na waakti huo huo macho yake yakionekana kumezwa na urembo wa Nadina. Alikuwa na mwanya! mwanya mdogo uliotenganisha safu ya meno yake kiustadi kiasi cha kutamanisha aendelee kuuweka wazi kila sekunde iendayo kwa Maulana.

‘Umelipia?’ akauliza kwa sauti laini iliyomtekenya Meddy mpaka kwenye nyongo.
‘Yeah!... usiwe na hofu’ Meddy akajibu akitoa risiti yake na kumpatia Nadina ambaye aliipokea a kuitazama kisha kumrudishia Meddy huku akitabasamu tena na kuzidi kumuua mwanaume wa watu.

‘Jerry!... kutana na Nadina hapa’ Meddy akatoa utambulisho na Jerry akatabasamu tu huku Nadina akiinamisha kichwa chake chini na kukinyanyua kama ishara ya heshima na kuukuali utambulisho ule.
‘Mmmh!... Huyu ni rafiki yangu kipenzi anaitwa Jerry’ Meddy akamtambulisha Jerry na Nadina akatabasamu zaidi
‘Nashukuru kukufahamu’ akatamka kwa bashasha akitanguliza mkono wake wa kulia mbele ya Jerry ambaye naye akajikuta akiutoa mkono wake na wakasabahiana kwa kutikisa ile mikono yao.

Maongezi ya hapa na pale yakapamba moto. Nadina alikuwa mcheshi, mchangamfu mwenye stori za kufurahisha. Wakati wakiendelea na mazungumzo yaliyoonekana hata kumchota Jerry. Nadina akafuatwa na mmoja wa wahudumu na kunong’onezwa kitu sikioni. Nadina akageuka ghafla na kutazama kule alikokuwa Dj na wakati huo mhudumu akiondoka zake. Akatabasamu na kumgeukia Meddy

‘Nataka kuimba!’ akazungumza akiwa anajiandaa kutoka kitini. Meddy na Jerry wakatazamana na kisha kugeuka kumtazama Nadina aliyekuwa ameshaa nza kulifuata jukwaa tulivu lililokuwa na pazia lililomulikwa na taa kali ya blue. Akasimama katikati ya lile jukwaa dogo akiwa na kipaza sauti kilichokuwa kimesimamishwa katika kifaa chake. Mwanga ule ulimpendezesha zaidi.

Mara moja tu akamtupia Meddy jicho kisha akamtazama Dj aliyekuwa kwa juu kidogo na kuitikia, ikiwa ni ishara ya kumruhusu aachie ala za wimbo aliotaka kuuimba. Ikasikia Ala tulivu lakini iliyorindima katika mahadhi ya muziki wa zouk. ala ile ilipaa hewani na kuvuta hisia za wengi walioacha kila kilichokuwa mbele yao na kumtazama Nadina.

Hata Sindi Nalela aliyekuwa chumbani, aliisikia ala ile na kufunga jarida lake kwanza, akatega sikio
‘Nadina’ akaita kwa upole akijua ni Nadina ndiye aliyetaka kuimba. Kwa wiki nzima alikuwa akiufanyia mazoezi wimbo huo akishirikiana na yule Dj wa casino na tayari alishauimba mara mbili kwenye casino hilo. Akashusha pumzi na kusikilizia zaidi

Kule Jukwaani Nadina alipasua anga ghafla kwa kuanza kuimba
‘Moyo wangu… roho yangu…nafsi yangu vina maumivuuu… najaribu najaribu kukusahau lakini maumivu yamegoma kunitoka… Eeh mungu wangu Mungu wangu naumia japo nacheka usoni na tabasamu mdomoni…’ akaimba akivuta sauti, akiipandisha na kuishusha kisha taratibu akasikilizia muziki ukichanganya na kukifikia kiitikio kilichoonekana kuanza kukaririwa na baadhi ya watu waliopata kuusikia siku mbili tatu nyuma alipouimba hapo Casino.

‘….juu ya yote ….Nenda nenda nenda na wala usiangalie nyuma…na wala usinitafute tena na wala usinikumbuke… nimekubali kwa moyo mmoja tuuu… kuwa sitokuwa nawe …mileleee… nenda nenda nenda na wala usiangalie nyuma…’ akakirudia kiitikio kile kwa madaha, akiimba kwa hisia

Jerry aliyekuwa anamtazama na kumsikiliza kwa makini alihisi kulengwa na machozi. Ilikuwa ni kama wimbo ule ulikuwa mahsusi kwake. Alimkumbuka Sindi. Akashusha pumzi na kunyanyuka, akimgusa Meddy begani na Meddy akageuka na kumtazama
‘usiku mwema!’ akajibu akichukua ufunguo wa gari uliokuwa mezani na kuondoka taratibu, akimuacha Meddy anamatazama tu. Jerry akatoka mpaka kwenye maegesho na kusimama hapo, akafumba macho na kusikitika.
‘Sindi uko wapi mama?’ akaongea mwenyewe akionekana wazi kuumia moyoni.

Kule ndani ya Casino, Madam Adella aliyekuwa ofisini kwake pia, alitanua pazia na kutazama kule kwenye Casino, akiona moja kwa moja pale jukwaani. Wimbo ule ulimgusa sana, alionekana kuumia pia.
‘Binti yangu… kweli nimeenda na sikuangalia nyuma…’ akaongea mwenyewe akifunika pazia na kurudi kitini. uso wake ukiwa na simanzi nzito. Ni dhahiri pamoja na kumkimbia binti yake miaka mingi iliyopita lakini kama mwanamke na mzazi, moyo wake ulikuwa na kovu la majuto na hasira dhidi ya nafsi yake.

Kule chumbani kwa Sindi, Sindi alikuwa katika dimbwi la machozi, alifuta machozi na kuimba sambamba na Nadina kwenye kile kiitikio ambacho kilihitimisha wimbo na ala tu kubaki hewani.
‘Ooh Jerry…Jerry jamani…’ akaomboleza kimya kimya masikini, maneno yale yalikuwa kama alikuwa akitamkia Jerry. Alilia akilishika tumbo lake, akikisha kiumbe chake toka kwa Jerry Agapella. Tumaini la kumuona tena likiwa limezimika na kupotea kabisa.

Nadina akashuka jukwaani, akipigiwa makofi na kupongezwa. Akamfikia Meddy aliyenyanyuka na kumlaki kwa kumkumbatia. Akijisikia fahari zaidi kuwa binti aliyepasua anga muda mfupi uliopita alikuwa wake, katika meza yake na hilo aliliona wazi kwa namna watu walivyomkodolea macho Nadina.

‘Sipati maneno ya kutosha kuelezea ulivyo na kipaji’ Meddy akaongea akiwa ameishika mikono yote miwili ya Nadina ambaye alibaki akicheka kwa furaha.
Wakaongea kimahaba, wakifurahia kuwa pamoja. Wakati wakiendelea na furaha yao, Adella akawafikia kwenye meza ile na kusimama pembeni yao.
‘Long time no see Meddy’ akamsemesha Meddy
‘Ooh No! mbona nipo almost kila wiki…’ Meddy akajitetea
‘Umemlipia mrembo wangu?’ akauliza uso ukikosa hata tabasamu la uongo
‘najua kila kitu kilicho hapa kinapatikana kwa cash… usijali she is mine usiku mzima na get a bonus too…’ Meddy akajibu akilala ubavu na kuchomoa wallet. Akatoa noti kadhaa na kuziweka mezani, akazisukuma mpaka ule upande wa Adella na kuziacha hapo.

Adella akabinua nyusi zake juu, akionekana kushangazwa na ule ukarimu wa Meddy. Akamung’unya midomo yake wakati akizichukua zile pesa. Wakati akiziesabu, simu ya Meddy ikaita na akawataka radhi akinyanyuka na kwenda kuongelea pembeni.

Adella akamtazama Nadina kwa jicho kali kidogo, kisha akamsogelea na kumuinamia, akiweka mdomo wake usawa wa sikio, akaachia maneno yake
‘Usije ukachanganya kazi na hisia zako binafsi… ni marufuku na zaidi ya yote Meddy is mine...’ Akajiinua akimuacha Nadina akipoteza nuru usoni mwake huku yeye Adella akitabasamu sasa na kumtazama Meddy aliyekuwa anarejea pale. Akamuinamia Meddy na kumbusu shavuni, na pasipo kujua dhamira ya Adella kufanya vile Meddy akachekelea busu lile na asijue ni kiasi gani alikua anamsaidia Adella kudhihirisha maneno yake.
88888888888888888888888888

Usiku ule chumbani kwa Rebecca Okello, mama yake Pamella. kulikuwa na hali ya kutokuelewana kati ya Okello na mkewe Rebecca. Walishalala na kuzima taa lakini ugomvi wao ulifanya Mzee Okello  awashe taa na kuketi kitandani akimtazama mkewe aliyekuwa amelala kwa kumpa mgongo.
Nimekukuta unalia… nakuuliza tatizo husemi… nakugusa hutaki… nikueleweje sasa?’ Okello alimuuliza mkewe ambaye wala hakujitikisa sembuse kujisumbua hata kumtazama mumewe

‘Becca!’ mumewe akamuita kwa kubembeleza lakini pia hakuitikiwa.
‘kama inshu ya Pamella na Jerry…. mtoto amekuja leo akasema amekubali kuolewa na Jerry na ndio kitu kilichokuwa kinakuumiza… now what Becca!.. una nini?’ Okello alikomaliza kujua tatizo la mkewe na akamfanya atupe shuka na kujiinusha akimgeukia mumewe

‘Niache…sawa?... nina matatizo yangu’ akajitetea, macho yakionekana kuvimba na kuvilia wekundu wa kulia
‘matatizo yapi ambayo huwezi kunishirikisha mimi mumeo?... kama ni mamabo yenu ya upatu mmedhulumiana uko si useme upewe pesa’ Mume akajaribu kuotea hata shida ya mkewe ili tu amuweke sawa kipenzi chake lakini ikawa kazi bure tu

‘Zima taa tutale… Nimechoka!’ akajibu kwa ufupi akirejea kulala alivyokuwa amelala. Okello akazima taa na kujiweka kitandani. Wakigeuziana migongo na kuacha nafasi ya kutosha kuweka gunia kubwa la mkaa kati ya mgongo na mgongo.
kule alikogeukia Pamella hakulala, alikuwa ameutumbulia ukuta macho akiwaza yake.
That handsome man… caring… devoted husband of your age is my husband…my husband…husband not a boyfriend!... with due respect now take care your old man please because I’m back…. see you around!’ maneno ya Daniella kule supermarket yalipita kichwani pake vema akiikumbuka waziwazi dhihaka ya Daniella kwake. Akafumba macho na machozi ya hasira yakamtiririka
‘She is my wife Becca… na nahitaji kuwaona watoto wangu’ akayakumbuka maneno ya Dennis kwake mara tu alipolalamika kuhusu Daniella. Sasa akalia kwa kwikwi zilizoshindwa kujificha na Okello akajikuta akijiinusha na kuwasha taa tena. Akaketi kitako

‘Becca… talk to me honey!’ akaongea akijitahidi kumgeuza mkewe ambaye aligeuka akili na kukubali kuweka ubavuni pa mumewe aliyejitahidi kumtuliza. Masikini bila kujua mkewe alikuwa akimlilia mwanaume mwingine kabisa.

Rebbeca aliumia kuona wakati akijitahidi kutatua tatizo la Pamella na Patrick ili abaki na Dennis kwa amani, tatizo lingine kubwa limeibuka na lile la kwanza kujizima. Akaumia zaidi kuona Dennis alikuwa anagemea upande wa Daniella sasa huku akisahau nay eye ni mke wa mtu.
888888888888888888888888

Hekaheka za usiku hii zinaishia nyumbani kwa Dennis anayeingia kwake akiwa amelewa kiasi cha kuyumba kidogo. Anapoingia chumbani anakuta chumba chake kitupu. Anaduwaa na kuangaza mpaka maliwatoni ambako haoni hata kivuli cha mtu aliyetarajia kumuona. Anatoka na kukifuata chumba cha wageni, pasipo kugonga anajaribu kufungua na kukuta mlango umefungwa kwa ndani.

Anaugonga kwa jazba, akimsihi huyu aliyendani aufungue haraka. anapotumia nguvu zaidi kugonga na kunyonga kitasa. Daniella anafungua na Dennis akaingia chumbani humo kwa kasi
‘what are you trying to do Ella?’ akamuuliza  mkewe aliyekuwa ndani ya gauni la kulalia
‘we are no longer husband and wife… nikafanye nini chu…’ akajitetea na Dennis akamuwahi
‘Sijakutaliki Daniella… hiyo excuse yako siielewi’ Dennis akampandishia
‘Niko hapa kwa ajili ya watoto tu… usinilazimishe mengine nisiyotaka’ Daniella naye akaja juu
‘Watoto?... na unawajengea picha gani unapolala nje ya chumba chako cha kulala… unawapa ujumbe gani sasa… kama upo hapa kwa ajili yao huu ni ujumbe gani unawapa?’ Dennis hakujali tena kwamba ule ulikuwa ni usiku usiohitaji kelele zile

‘Nimeingia humu baada ya wao kulala Dennis…ni wewe ndio unayeleta picha isiyoeleweka… tabia zako zimenishinda…nimekuchoka Dennis… imagine unaingia hapa ndani muda kama huu… wewe ni baba wa aina gani sasa?’ Daniella akajitetea tena na akigomba kwa sauti na ugomvi wao ukawaamsha watoto wao waliotoka chumbani na kuja kusimama mlangoni wakati wazazi wao wakijibishana

‘Are you guys fighting?’ mtoto mmoja akauliza na kufanya wanandoa hawa wakatize majibizano na kuduwaa wakati wakiwatazama watoto wao
‘No!..No honey… twende mkalale…’ Daniella akajitahidi kutabasamu akiwafuata watotot wake na kuwaongoza kurudi chumbani. Akatumia dakika kadhaa kisha akatoka na kufunga mlango polepole.

Dennis alikuwa amesimama kwenye kizingiti cha ule mlango wa chumba alichokuwemo Daniella. Alikuwa amejiegesha hapo akimsubiri mkewe. Daniella naye akasimama kwenye kizingiti cha mlango aliofunga na kumtazama Denis usoni.
‘Please Ella…’ Dennis akabembeleza na Daniella akamtazama tu bila kujibu kitu, ni kama vile alikuwa na hasira naye ila alijikaza kutoilipua tena muda ule. Akaingia chumbani mule alikokuwa na kutoa mto wa kulalia, akatoka na kuelekea chumba chao cha kulala huku Dennis akimfuata nyuma.

Chumbani mule Daniella alilifuata kochi kubwa na kuweka mto pale, kisha taratibu akalifuata shuka kitandani.
‘hapana Ella… lala tu kitandani mimi nitalala kwenye kochi’ akamsemesha mkewe aliyekubaliana na ombi lake akarejesha mto kitandani na kupanda kitandani. Dennis akashusha pumzi za kusikitika kisha taratibu akaaanza kutatua vifungo vya shati lake na kulivua. Mwili wake uliojengeka kiume ukawa wazi na Daniella akamchungulia kwa kuibia, akamtazama mumewe huyu kwa upendo na matamanio wakati akielekea bafuni. Akatabasamu hata yeye hakujua kwanini alitabasamu!
8888888888888888888888888

Siku chache baadaye, Pamella Okello alifikia tamati y mahusiano yake na Patrick kwa kumwambia ukweli kuwa uhusiano wao ulikuwa umefikia mwisho. Patrick hakukubali, alitaka sababu na Pamella hakuwa tayari kusema alikuwa mbion kuolewa na Jerry. Akamlazimisha tu kukubali kuwa uhusiano wao umefikia kikomo.
‘Sikuelewi Pam… ghafla hivi… why?... nimekufanyia nini mpaka unafikia uamuzi kama huu?... why?’ Patrick alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa wakati akiongea na Pamella kwenye simu siku moja tu baada ya Pamella kumueleza ukweli wenye kuumiza.

Pamella aliyekuwa nashuka kwenye gari nyumbani kwao, alifunga mlango wa gari kwa mguu baada ya kuelemewa na simu sikioni, mkono mmoja ukiwa na mifuko ya shopping. Akatembea hatua mbili tatu na kusimama kwanza

‘Patrick… nimejitahidi kuwa mkweli na muwazi… it is over… najua inauma but nimeona ni bora kuwa mkweli kuliko kukufanyia visa bure’ akajitetea na asijue mwenzake alikuwa amechanganyikiwa kiasi gani. Patrick akaongea mfululizo akijitetea kwa kosa ambalo hata hakulijua, Pamella akamkatia simu na kuizima. Patrick alipoijaribu tena na kukuta imezimwa akainama kwa uchungu, akisigina magego yake na kupambana na maumivu ya moyo kiume. Aliumia kupita neno lenyewe maumivu!

Wakati Pamella akizozana na Patrick uku nje, kule ndani mama yake alikuwa akigombana na Dennis kwenye simu.
‘huwezi kuniamrisha nisikupigie simu au nisikutumie meseji Dennis… Daniella ni nani akupangie wakati wa kuwasiliana… sikuelewi… nitatuliaje wakati naona wazi unavyoegemea kwa Daniella… sikuelewi Dennis… jana hukupokea simu yangu… missed call 4 na ushindwe kutuma hata meseji…. usinitajie jina la Daniella sitaki kulisikia…. so what?.... hata mimi nina mume Dennis…  Dennis!...Dennis!...Dennis!’ akaita mara kadhaa kabla ya kugundua simu ilikatwa kitambo.

Akahisi msumari wa moyo ukititia moyoni. Akaketi kwenye kochi akiwa ameushikilia moyo wake kana kwamba ulikuwa mbioni kuchomoka na kutimua mbio. Dennis alikuwa amemuumiza mno. akajikaza mtoto wa kike asilie, asipige mayowe, akajikaza hasa mpaka mishipa ya shingo ikamsimama dede. Wakati huo huo binti yake akafungua mlango na kuingia kwa furaha.

Akamfuata mama yake kwa mbwembwe pale kwenye sofa na kuketi kando yake akitua ile mifuko kwenye meza ndogo mbele yao
‘Pale saluni kwa Marino wamefungua massage centre… mama it is amaziiiing’ Pamella alimsemesha mama yake akitanua mfuko mmoja na kutoa kujipeperushi kilichokuwa na maelezo kuhusu hiyo huduma, alipogeuka kumpatia mama yake akagundua akili y mama yake haikuwa pale

‘Mama!... kuna tatizo?’ akamuuliza mama yake akimgusa pajani kumshtua na mama yake akamgeukia taratibu na kumtazama binti yake usoni. Alionekana wazi kuwa na maumivu ya moyo, mawazo na huzuni.
‘Mama… huzuni ya nini na nimekubali kuolewa na Jerry uliyekuwa unamtaka!... nini tena sasa?’ akamuuliza mama yake ambaye hakumjibu kitu. Alinyanyuka taratibu na kuanza kuchapua hatua kuelekea ndani.

Pamella akasimama wima na kumtazama mama yake kwa huruma ya kumsikitikia
‘Ni kuhusu Dennis?’ akaotea na kupatia.
mama yake akasimama pasipo kugeuka, akafumba macho na kusikilizia ukweli ule ukimchoma vizuri. kameza mate na kufumbua macho kilegevu, alishaanza kulengwa na machozi sasa. akageuza kichwa tu na kumtazama binti yake. akautanua mdomo wake apate la kunena na akakosa,  akajikuta tu akikirudisha kichwa chake mbele na kuchapua hatua za kivivu kuelekea mbele

‘Mom, this is not fair… not fair at all… baba akijua sidhani kama…’ Pamella akaongea kwa sauti akimfuata mama yake nyuma na mama yake akamgeukia haraka sana kabla ya kumalizia sentensi yake
‘Pamella Please…stay out of this… please’ machozi yakashuka wakati kope zake zikimwemweseka na kuruhusu machozi, akageuka haraka na kukaza mwendo akimuacha pamella amemtolea macho ndi!. Aliumia kwa kushindwa kujiongoza. Nafsi ilimsuta, alikuwa mama wa aina gani wa Pamella lakini hisia zake kwa Dennis hazikuangalia alikuwa nani kwa nani. Akahitimisha ya wahenga mapenzi hayana umri!
8888888888888888888888

‘Baba bwana… mimi sijapanga harusi kubwa hivyo… iwe ndogo ya kisasa inatosha’ Jerry Agapella aliongea na baba yake wakati akijiandaa kuondoka hapo kwao alikofika kumsabahi baba yake

baba yake akacheka kwanza akitikisa kichwa
‘Aah wapi… balozi mstaafu hawezi kuruhusu harusi ya kijana wake pekee iwe kama sherehe ya ubatizo… come on Jerry!’ akampiga piga kijana wake begani na wote wakatembea hatua moja kuufuata mlango.

Wakati wakiukaribia, mlango ukafunguliwa na mlinzi akaingia na kuutanua zaidi mlango akiashiria alitaka mtu aliyekuwa nyuma yake aingie. Mzee Agapella akatabasamu zaidi akionekana kumjua aliyetarajia kuingia.
Iloma akaingia mule ndani na kusimama mbele ya mtu na baba yake, huku mlinzi akirudi kazini kwake na kufunga mlango.

‘You look beautifu Iloma’ akamsifia na Iloma akatabasamu kwa aibu na kuinamisha kichwa chini, ile asante yake ikimezwa na lile tabasamu.
‘Oh.. Jerry kutana na iloma… my friend’ Mzee agapella akatambulisha ile ‘my friend’ ikisindikizwa na tabasamu kali na Jerry akiitafsiri alivyojua na kuitikia kwa kichwa

wakapeana mikono, na Mzee agapella akamtambulisha Jerry kama kijana wake mkubwa. Wakamtaka radhi Iloma na kutoka nje wakimuacha anashangaa ukubwa wa lile hekalu, mapambo na vitu vya thamani vyenye kuvutia pale sebuleni.
‘Fiona ndio alikuwa naishi hapa…duh!’ akashangaa zaidi akiumiza shingo kwa kubinua uso juu kushangaa kila lililopita machoni pake.

Pale mlangoni, Jerry alimtazama baba yake kwa jicho la msuto
‘Hujamtaliki Fiona bado…’ akamkumbusha
‘Mara moja katika maisha Jerry… jaribu kufurahia maisha bila kuingiza lakini this lakini that… unamuonaje?’ Mzee agapella akaweka uzee kando kwanza
‘She is the booomb dad… just make sure she doesn’t explode in there’ akamtania baba yake na kumfanya acheke sana wakati yeye akiteremsha ngazi chache mbele ya lango lao na kulifuata gari lake. Wakapungiana mikono na Agapella akarudi ndani.

Alipoingia tu, akatumbukiza mkono kwenye mfuko wa suruali yake na kutoa kidani cha almasi. Akamfuata Iloma aliyekuwa amesimama mbele ya kabati la kioo lililokuwa na samaki wadogo wadogo  waliokuwa wakifungwa hapo.
‘mnawalisha nini?’ Iloma akauliza akishangaa zaidi
‘Vipo vyakula maalumu…’ Agapella akajibu akizungusha mikono yake shingoni mwa Iloma na kukilaza kile kidani.

‘aaawww… asanteee’ Iloma akajibu akikipapasa kile kidani kwa mkono mmoja na ule mwingine ukinyanyua nywele zake kwa nyuma ili Agapella akifunge kile kidani. Alipomaliza Iloma akamgeukia na kumtazama Agapella usoni kisha akajiinamia kukitazama kile kidani.. Kiliwaka na kuvutia mno.
‘It is Diamond!’ Agapella akamtajia aina ya madini ya kidani na kile na Iloma akamtazama kwanza kabla ya shukrani kummiminika.

Akamuongoza nje kwenye bustani kulikokuwa na meza pamoja na viti. Wakaketi hapo wakiongea hili na lile na Iloma akishindwa kabisa kuibua inshu ya Fiona kama walivyokubaliana na Fiona. Alimpigia simu Agapella na kudai alikuwa amekubali mwaliko wake na hapo hapo akimdanganya Fiona kuwa alikuwa amempigia Agapella na kujitambulisha kama rafiki wa Fiona. Fiona akamsaidia kumuelekeza na kumpa maneno ya kuongea ili kumtetea lakini nafasi ya kuanzisha mada ya Fiona au tu kujitambulisha kama rafiki wa Fiona, ilikosekana, ilishindikana na mkutano wao ukaisha bila Fiona kuzungumziwa!
88888888888888888888888888888

Jioni hii baada ya pilika pilika za kazi na mambo chungu nzima. Dennis Mazimbwe akaingia kwake akiwa na uchovu wa kutosha. Watoto wake wakamlaki na kuongea naye hili na lile naye akiwaahidi wikendi atawapeleka dar es salaam zoo.

akaingia chumbani kwake na kumkuta Daniella akishona kifungo cha shati kwa sindano ya mkono. Wakasabahiana na Dennis aipomfuata mkewe ili ambusu shavuni, Daniella akakwepa. Dennis akaachana naye na kwenda kuweka vitu vyake kwenye meza anayoweka vitabu vyake na kisha kuingia bafuni.

Simu ya Dennis ikatoa mlio wa kuita, Daniella akaitazama tu, ikatoa mlio wa kuingia meseji na Daniella akanyanyuka na kuifuata ile simu. Akaifungua
‘Dennis babe plz call me’ akausoma ule ujumbe ulitoka kwa Rebecca aliyeseviwa kwa jina lake. Daniella katikisa kichwa kulia na kushoto. Mwanamke aliyempa onyo siku chache zilizopita alikuwa hajaonyeka!

Dennis akatoka bafuni akifuta kichwa kwa taulo, akashangaa kuona mkewe ameketi kitandani na simu yake mkononi.
‘Rebecca again!... she wont leave me alone… why are you guys doing this to me?... why Dennis… nimeacha vyote kwetu… kila kitu nikaambata nawe ukiwa huna kitu… nimekupa watoto dennis… nimevumilia tabu zote mpaka hapa… Kwanini unanifanyia hivi?’ Daniella akaongea kwa hasira akilia kwa kwikwi, akiomboleza kwa hasira

Dennis akajaribu kuingilia kati na kumbembeleza lakini ikawa kazi bure kabisa. Alikataa kuguswa na mumewe, alikataa kumsikiliza.
‘It is time Mr. Okello ajue mkewe ananivunjia ndoa yangu…’ akaongea kwa hasira akitoka mule chumbani na Dennis akiharakia kuvaa ili amuwahi mkewe. Daniella alitoka mbio mpaka sebuleni na kukumbana na Nanny aliyempokea na kumuweka kifuani, akimbembeleza na kujaribu kumtuliza Daniella. Dennis akatokea pale sebuleni wakati Nanny akiwaondoa watoto na kuwataka waende nje kwanza.

Wanawake hawa wawili wakamtazama Dennis kwa ghadhabu. Daniella alikuwa akijaribu kuzuia machozi huku akigombana na mumewe aliyemtaka wazungumzie lile sula kwanza kabla ya kumfuata Okello. Mlango ukafunguliwa na Patrick akaingia kwa jazba.

Aliingia moja kwa moja na kumfuata Dennis kaka yake, akamtandika ngumi moja kali iliyompepesusha na kukaribia kumbwaga kochini. Akiwa bado na ile hali ya kushangaa Patrick akamvaa ili amkung’ute kisawasawa lakini Nanny akamuachia Daniella na kukimbilia kuamulia ugomvi wa mtu na ndugu yake.

‘Heeeeey!’ Nany akapiga ukelele wa nguvu na kuwaachanisha hawa ndugu kwanza. Wote wakihema kwa hasira
‘hongera!... hatimaye Pamella ameniacha… it was you… you bastard!’ Patrick amatusi kaka yake na kutaka kumvaa tena lakini Nanny akawazuia na Daniella sasa alikuwa amemshikilia Patrick.
‘Nimefanya nini?.... nimeongea na Pamella lini?....’ Dennis alihoji kwa mshangao na hasira juu

‘Sio wewe uliyenitishia niachane na Pamella… hukuwa wewe?... na Nanny ni shahidi yangu hapa… haukuwa wewe?.... nijibu… she is no longer mine… happy  now?...’ Patrick aliongea kwa hasira akiweweseka na machozi kumtoka kwa hasira. Mwanaume uvumilivu ulifika kikomo

‘so… mama na binti yake wanatoka na mtu na kaka yake… wow!... unamtishia Patrick aachane na Pamella Okello wakati wewe umeshindwa kuachana na Rebecca Okello?... Oh Mungu wangu’ Daniella akajiinamia na taratibu akalifuata kochi na kuketi huku akilia.
Patrick sasa akabaki mdomo wazi, akiwa haamini alichosikia. Akarudi kinyume nyume na kuufikia mlango, akaufungua na kutoka. wakati Daniella akisimama na kuufuata mlango pia, akatoka na kuubamiza. Dennis aliyebaki kama mlevi akasimama na kumtazama Nanny kichovu, jasho likimtoka.

‘umefanya nini hiki sasa?’ Nanny akamuuliza kwa huruma
‘… angalau ungejitoa kafara kwa kumuacha Rebecca ili Patrick awe na mwanamke anayempenda… hukuifikiria hata furaha ya mdogo wako?’ Nannya akamuuliza kwa sauti ya upole ila yenye kusuta
‘Sio hivyo!’ Dennis akajibu akiweweseka
‘Ni nini sasa?’ Nanny akamuuliza akimsogelea Dennis na kumketisha chini kwenye sofa. akakaa kando yake na kumtazama Dennis aliyekuwa amejiinamia.

‘Dennis!’ Nanny alisisitizia kujibiwa
‘Pamella ni binti yangu wa damu… my real daughter’ akapasua ukweli kwa sauti kuvuta, sauti ya kujuta, sauti ya kutetemeka. Nannya akakuza macho yake saizi ya ndimu changa. Aliyakodoa hasa almanusura yamchomoke!

Daniella ameenda wapi?....Patrick atachukuliaje?... nini kitafuata?... jiunge nami hapahapa USIKOSE!


ITAENDELEA…. NIPE MAONI YAKO KUHUSIANA NA SIMULIZIA HII  NDUGU MSOMAJI

3 comments:

  1. sasa utamu ndio umeanza jamani iloma naye kwa mzee Agapella je Fiona akijua itakuwa nini

    ReplyDelete
  2. rebecca ndoa itamshinda cku c nyingi

    ReplyDelete
  3. Sawa, Fiona akijua sijui patatosha? Yani utamu hadi masikioni lahaulah

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger