Wednesday, December 25, 2013

SINDI... NA LAURA PETTIE (50)

50

Alisimama mbele ya Sindi Nalela kama binadamu aliyevukwa na fahamu, aliyekosa utashi na kupigwa bumbuwazi. Nadina akarudi kinyume nyume kwa hatua hafifu zilizokosa uelekeo wa maana. Macho yako yalimwemweseka katika namna ya kuzidiwa na ile hali ya bumbuwazi, midomo yake iliyokuwa wazi ilitulia vile vile mithili ya mtoto asubiriaye tonge la ugali. Akarudi nyuma mpaka alipogota ukutani, mikono ikiwa kifuani pake.


Akamtumbulia macho Sindi na asijue afanye nini. Akili iliyokwenda matembezi ghafla ikamrejea, akajikuta tu akiutafuta mlango na kutoka mbio pasi hata kuufunga itakiwavyo. Akakimbia kwa pupa na wahaka akiangaza huku na kule kana kwamba msaada alioutaka ungetokea popote hewani.

Mbio zake zikamfikisha mapokezi ambako, wateja wachache walikuwa katika utulivu mkubwa wakipitia albamu na wengine wakiongea kwa simu na wawili watatu wakiwa meza ya mapokezi. Hakujishughulisha nao kwani kwa haraka tu alijua wateja wale walikuwa wageni eneo lile. wazoefu hakupita mapokezi!

Akamfuata msichana mwenzake aliyekuwa hapo mapokezi na kumsogezea uso
‘Umemuona Da’ Tima?’ akamuulizia mwanadada aliyepata kuongea nao siku za nyuma na kuwaasa kutulia. Akili yake ilimkumbuka na ndiye hasa aliyeona angemsaidia kwa wakati ule.

Yule msichana akatikisa kichwa kulia na kushoto, naye uso ukionekana kutaka kujua kulikoni kutokana na  taharuki iliyokuwa ikijionyesha usoni pa Nadina. Wanaume waliokuwa mapokezi wakamtupia jicho Nadina kwa matamanio! Hakuwajali!
Akatoka mbio kuelekea nje ya jengo la mapokezi huku nyuma wanaume watatu wakikimbizana mapokezi kuulizia oda ya yule binti, wakakatwa maini na jibu la kuwatosha
‘Ameshalipiwa!’

Nadina katoka nje na kusimama kwa muda akili yake ikishindwa kwenda sambamba na nguvu ya mwili wake. alitaka kukimbia huku na kule akimsaka Tima lakini akili yake ilimfanya asimame kwanza kwani kukimbia tu bila kujua pa kuanzia kukimbilia kungemchosha zaidi na kumpotezea muda.

Kama mtu aliyegutushwa na kitu kilichomjia ghafla kichwani pake, akanyanyua miguu na kutoka tena mbio kulifuata jengo la Casino. Akaingia kwenye Casino lile na kupishana na watu waliojazana humo. Akafanya kazi ya ziada kupangua mikono ya wanaume waliomvutia huku na kule na kufanikiwa kupanidsha ngazi zilizokuwa zikielekea vyumba vilivyo juu. Akalifikia lango zito la kusukuma na kulipita. Kelele za Casino zikabaki nje na utulivu wa hali ya juu ukatawala kwenye kordo ndefu iliyopita katikati ya vyumba vilivyotazamana.

Akatembea kwa tahadhari akiangalia namba za vyumba zilizokuwa zimebandikwa katika kila mlango. Hakukumbuka sawia namba aliyopewa na Tima mwenyewe siku ile. Akapiga ishara ya msalaba, sasa akiukumbuka uwepo wa Mungu katika hali kama hii. Sala ikamtoka na asijue alisalia kitu gani. Mawazo yalikwenda kasi mno na kumuacha mtupu kichwani. Wakati akiukaribia mlango wa mwisho kabisa, ghafla akasikia mlango ukifunguliwa na Tima akatoka ndani ya chumba kimoja wapo. Akiwa bado anahangaika na funguo kwenye kitasa cha mlango. Nadina alishageuka na kutabasamu, angalau katika maisha yake aliushuhudia muujiza wa kujibiwa sala hapo kwa papo.

Akamfuata Tima kwa kasi ya ajabu na tima akajikuta akigeuka kumtazama Nadina vile alivyokuwa akimjia kasi
‘Unafanya nini huku?’ Tima akauliza, mashaka yake yakishindwa kujificha na akajikuta akiangaza kordoni kama kuna mtu alikuwa anawaona
‘Nahitaji msaada wako da’ Tima’ Nadina akasema kwa unyonge
‘Nani sijui… hebu sikiliza kwanza…’ Tima akamshika Nadina mkono na wakati huo mkono wenye funguo ukirudi kwenye tundu la mlango na kuufungua mlango kwa kasi. Akamuingiza Nadina ndani nay eye kuingia pia. Akaufunga mlango na kumkodolea macho Nadina.

‘kuna nini?’ akauliza Tima
‘Sindi anaumwa sana…’ Nadina akajibu kwa wasiwasi
‘Nini?... umemwambia kiongozi wenu?’ Tima akauliza naye wasiwasi ukimzidi, alimkumbuka Sindi na alikumbuka hali yake ya ujauzito.
Nadina akakataa kwa kutikisa kichwa tu

‘Ni kuhusu mimba?’ akauliza tena
‘Mmh mmh’ Nadina akakataa kwa kuguna na kutikisa kichwa huku akihema kwa nguvu kiasi cha kufanya mabega yake yafanye kazi ya kupanda na kushuka.

‘sasa kuna nini?’ sauti ya Tima alipaa kidogo na akajishtukia ghafla na kujikuta akigeuka nyuma kana kwamba alihisi kuna alimsikia
‘Sijui lakini nahisi ni zaidi ya kuumwa kawaida… sijui… anatoka damu puani na…na .. sijui amekuwaje… ni kama ametumia kitu… sielewi’ Nadina aaliongea akirusha rusha mikono na senyensi zake zikikosa mpangilio unaoeleweka. Aliwayawaya!

Tima akatoa macho sasa, na taratibu akashusha pumzi kwa nguvu. Akili yake ikifanya kazi mara mbili ya kawaida.
‘Okay…twende tukamuone tujue cha kufanya but… next time usijaribu kuingia huku bila ruhusa binti!.... umenielewa?’ akamuuliza Nadina wakati akiufuata mlango na Nadina akaitikia tu asijali sana lile onyo kwani kama si kumtafuta Tima wala asingewaza kuingia eneo lile. Wakatoka kwa tahadhari na kulifuata lile lango zito. Wakatokezea kwenye Casino na kuwapita watu wakielekea nje.

Wakakimbizana huku na kutokea kule mpaka chumbani kwa Sindi na kumkuta akiwa amelala vile vile, damu iliyokuwa imemtoka puani alishaacha hata hivyo ilikuwa imechuruzika vya kutosha mpaka shingoni.

Tima alisisimkwa na ile hali, almanusura apige yowe la hofu. Akameza mate kwa juhudi kubwa kabla ya kujikaza na kumsogelea Sindi, huku akitetemeka akaushika mkono wa Sindi uliokuwa umelala hewani ukining’inia na kupima mapigi ya moyo. Aliyahisi kwa mbali.
‘naomba simu yako mara moja’ akamuomba Nadina simu
‘Haturuhusiwi kuwa na simu’ Nadina akajibu na akajikuta akikumbuka alikosea mno kumuomba Nadina simu. Akajipekua kwenye suruali yake ya jeans na kutoa simu yake, haraka akazitafuta namba za mtu aliyehitaji msaada wake na kuongea naye.

Dakika 15 baadaye, Mwanaume mmoja mtu mzima alikuwa akimhudumia Sindi kwenye chumba kingine. Yule Mwanaume mtu mzima alimaliza kazi yake na kumfunika vizuri Sindi kisha akasimama na kuwageukia Tima na Nadina.
Akashusha pumzi kidogo na kuvua miwani yake ya macho.
‘amejioverdose dawa za kulevya…’ akatoa jibu la awali
‘Dawa za kulevya!!?’ Tima na Nadina wakauliza kwa mshangao, kwa pamoja kana kwamba waliambizana waulize kwa pamoja.

‘Yes!... sijajua ni dawa gani mpaka niithibitishe maabara… ila kwa hii huduma ya kwanza she will be okay… apate tu muda wa kupumzika zaidi na kutuliza akili… she will be fine na atahitaji kuwa chini ya uangalizi vinginevyo kuna hatari kubwa sana ya kumpoteza yeye na kiumbe aliyenaye tumboni…’ Dokta akaongea kwa msisitizo akiwaacha tima na Nadina katika mshangao mzito.

Vichwa vyao viwaza kwa pamoja…  Sindi alikuwa ametoa wapi madawa?... alianza lini?...hii ni mara yake ya kwanza?... kwanini akatumia dawa hizi ilhali alionekana kuwa msichana mwerevu mno. mawazo yale yaliyojaa maswali vichwani mwao yaliwafanya wamtumbulie dokta macho kana kwamba majibu ya maswali yalisomeka usoni pa tabibu yule. Nje ya mlango wa chumba kile msichana mmoja aliyekuwa akiwasikiliza kwa kuibia!
888888888888888888

Watoto wa Daniella na Dennis walikuwa sebuleni wakitazama luninga, ghafla tu wakaanza kunyang’anyana  rimoti kila mmoja akitaka kutazama sehemu aliyotaka yeye na si mwenzake. Purukushani zile zikawafanya wakimbizane kiasi cha kumkera mama yake aliyekuwa akiandaa chakula cha baba yao mezani.
‘Hey!... imetosha sasa! weka hiyo rimoti chini na muende vyumbani mwenu sasa hivi’
‘Mama..’ pacha mkubwa aliyeshika rimoti akataka kulalamika na mama yake akamkata jicho kali lililomfanya ateremshe rimoti mezani na kuanza kujongea taratibu kutoka eneo lile la sebule.

Watoto walipotokomea vyumbani, Daniella akasikia mlango ukifunguliwa na Dennis akaingia akitokea kazini. Daniella akatabasamu na kumfuata mumewe, akamsabahi, akampokea akimbusu mumewe shavuni. Dennis akahisi anaota wakati akiiachia briefcase yake ichukuliwe na Daniella. Akamtazama mkewe kwa mshangao wa waziwazi wakati akielekea chumbani na yeye kumfuata nyuma.

Kule chumbani, Daniella aliitua briefcase ya Dennis na kumgeukia mumewe
‘ukishaoga… chakula kiko tayari mezani… niko jikoni’ akatabasamu na kutoka mule chumbani akimuacha mumewe na ile hali ya kushangaa zaidi.

Dennis akaoga na kurudi sebuleni kwenye meza ya chakula. Akamkuta mkewe hapo akimsubiri. Uchangamfu aliokuwa nao Daniella ulimfanya Dennis naye achangamke kidogo ingawa alionekana kutatizika mno. Daniella akampakulia chakula na kumpatia
‘You look beautiful Ella’ Dennis akamsifia mkewe, kwa mara ya kwanza tangu waanza migogoro Daniella alikuwa amejipamba, alikuwa amevaa mavazi ya kuvutia na si nguo pana pana zilizomfanya aonekane mtu mzima kuliko umri wake.

Alikuwa amejipura usoni na kutengeneza nyusi zake, uso wake ulitulia vizuri na nywele zake zilikuw zimetengenezwa na kuvutia mno. Alikuwa Daniella halisi aliyemuona miaka mingi iliyopita na kuvutiw anaye! Dennis alimtazma mkewe kama mtu asiye amini huyu aliyekuwa mbele yake alikuwa Daniella.

‘’Thanks’ Daniella alijibu akitabasamu na aibu ya kike ikimpitia na kuzidi kumfanya Dennis ahisi anaota. Hakukumbuka mara ya mwisho kuiona hali ile ilikuwa lini hasa. Daniella akampatia sahani mumewe nay eye kujipakulia. Wakala kwa furaha, wakicheka na kuongea mambo mengi ya kufurahisha.

Wakati Daniella akinyanyuka kwa ajili ya kuondoa vyombo, Dennis akasimama na kumzuia mkewe. Wakatazamana machoni kwa sekunde za kutosha, mboni za macho yao zikicheza kulia na kushoto… mkono wake wa kushoto uliushika mkono wa kulia wa Daniella wakati mkono wa kulia ukiinuka na kuteleza taratibu usoni pa mkewe akianzia mwanzo wa nywele, akaserereka na kuligusa shavu kabla ya kukishika kidevu na kukisogeza usawa na midomo yake. Wakaumana, macho yakikosa nguvu na kufumba, wakabusiana kimahaba na kila mmoja sasa akimshika mwenzake na kumpapasa kwa nguvu zote. mahaba mahabani!

Daniella akajitoa maungoni mwa mumewe ghafla wakati Dennis akionekana kuzidi kumuhitaji kupitiliza. akatembea taratibu kuondoka eneo la kulia chakula na kuyafuata makochi. Akaketi na kumngoja Dennis amfikie na kuketi kando yake.

Dennis akataka kumvamia tena mkewe lakini safari hii Daniella akamzuia
‘Nahitaji kukwambia kitu Dennis’ Daniella akasema kwa sauti ya upole tu na Dennis akatulia na kumsikiliza mkewe, alitamani Daniella aendelee kubaki katika hali ile ile ya utulivu, abaki na lile tabasamu, abaki na ule uzuri aliokuwa nao muda ule.

‘…tumepita misukosuko mingi sana Dennis… mimi na wewe tumelala njaa pamoja… tumetafuta watoto kwa bidii zote pamoja… hata ulipotaka kunirudisha kwetu kwa vile tu uliona maisha ninayoishi siyastahili… sikukubali… nilitaka kupita na wewe hatua zote kwa vile nilikupenda na ninakupenda Dennis’ Daniella akaongea taratibu, akimtazama Dennis machoni na kukishikilia kiganja cha mkono wa Dennis kwa upendo..

Dennis akakosa la kusema, akatabasamu akijua wazi aliyoyaongea Daniella yalikuwa zaidi ya ukweli.
‘… nakupenda pia Daniella’ akajitutumua kujibu.
‘…but Dennis… I think it is time to let you go!’ Daniella akapoteza lile tabasamu sasa
‘Ella…why?... how?’ mshtuko mwanzo wa taharuki, Dennis alimtolea macho mkewe kana kwamba alitaka ukubwa wa macho yake uwakilishe mshtuko wake

‘Dennis!’ Daniella akamuita kumtuliza
‘…nilipogundua una uhusiano na Rebecca… nilitaka uwe uongo…uwe uvumi tu… na ulipokataa katakata nikafarijika… lakini nilipokushika na Rebecca ukakiri kuwa mna uhusiano… niliumia sana… sana…sana Den’ Daniella akatulia na Dennis akajiinamia
‘…ukaomba msamaha na ukaahidi usingerudia… it took me six months to forgive you na kurudi katika maisha ya ndoa… it was not that easy… lakini bado Dennis… kumbe  haukuachana na Rebecca mpaka nilipokushika tena…’ Daniella sasa kawa analengwa na machozi na Dennis alikuwa amejiinamia vile vile akisigina magego yake. Ukweli ulimuuma!

‘….nikaamua kupambana na Rebecca… unajua yoooote yaliyotokea baada ya vita yangu na Rebecca… nilikubali kushindwa…nikaondoka na watoto… kwa ajili ya kuwa nao karibu na kwa ajili ya kukuumiza!’ Daniella akatabasamu kwa uchungu wakati Dennis akiinua uso na kumtazama mkewe. Alitamani kumnyamazisha!

‘… nikaendelea kukutishia kuwa ningekutaliki na usingewaona watoto tena… I’m sorry I used our own kids kukutisha, kuendelea kukuweka karibu nami…it was so selfish’
‘Daniella Please!’ akalalama Dennis
‘…nimesali sana Mungu anirejeshee mume wangu… airejeshe familia yangu… sikutaka kusikiliza ushauri wa mtu kuhusu wewe… nilitaka urudi, ukiri makosa na tuanze moja… ila naona hilo halitotokea kamwe… Rebecca anapendwa zaidi yangu na siwezi kupambana naye tena sababu yako!... this time ameshinda pia…I surrender!’ Daniella akauma midomo na kukusanya nguvu kisha akahitimisha

‘… now… leo hii… hapa mbele yako!... nakupa uhuru wa kunitaliki au mimi nianze kukutaliki na ubaki na watoto endapo watataka kubaki na wewe… sitaki kupelekana mahakamani wala kuwa na migogoro isiyoisha… nakubali kupoteza haki zangu zote na kukuachia amani… niko tayari kuanza upya maisha bila kujali nguvu niliyowekeza nyuma…’ Daniella akatulia akipepesa macho kuzuia machozi yasimdondoke

‘Sitaki kukutaliki Ella’ Dennis akamudu kutamka sentensi hii
‘Una chaguzi mbili tu!... umuache Rebecca Okello kimoja na urudi kwangu au uniache niondoke kwa amani na ubaki na Rebecca… na endapo utachagua kubaki na mimi na ukaendelea kucheat na Rebecca na nikaujua ukweli baadaye… adhabu pekee kwako itakuwa ni kuondoka na watoto wote wawili and never come back again wala kutuona tena!’

Dennis akakodoa macho, masharti yale yalipita kama shoti ya umeme mwilini. Daniella akasimama na kumbusu mumewe mdomoni.
‘You have two days to think about this honey!...’ Daniella akagongea msumari kuhusua uamuzi wake,kisha akajiondoa taratibu na kuishia zake akimuacha Dennis kwenye hali ya kutokujielewa. Akakumbuka barabara kauli ya Rebecca asubuhi ya siku hiyo juu ya kujiua kama ataachwa. Akaifikiria kauli ya mkewe ambaye ameshamuumiza mno, akawaza kutowaona watoto wake tena. Kwa sekunde mbili tatu alizowaza haya yote alihisi mwili na roho vikiachana na kurudiana ndani ya sekunde! Alichachatika!
8888888888888888888

Mchana wa siku iliyofuata, Ndani ya duka kubwa la mavazi ya harusi la Marino, huyu Marino ndio yule aliyempokea Sindi na kumremba alipoletwa na Adella kule saluni, Pamella alikuwa chumba cha kujaribishia nguo, huku mama yake akiwa na Marino mwenyewe wakiongea na kumsubiri Pamella ajitokeze.

Alipotokezea Marino na Rebecca wakaguna kuonyesha kutopendezwa na lile gauni
‘No darling… this doesn’t suit you… you can do better… here we go…’ Marino akaongea akinyanyua gauni lingine na kumpatia Pamella

‘... mama hili gauni la sita sasa unalikataa… hivi hatuwezi kuchagua kitu simple tu jamani’ Pamella akalalamika akilikusanya lile gauni alilovaa na kujiburuza nalo kurudi kule ndani
‘it is your specila day Pam… you have to look special dear…’ Marino akamjibia Pamella aliyebaki kucheka cheka mwenyewe.  Marino aliyempelekea gauni Pamella akarudi kwa Rebecca na kumsogelea kimbeya
‘Nasikia it is Jerry Agapella’ Marino akauliza kishambenga, muonekano wake wa ki’gay’ ukinogesha pozi zake
Rebecca akaitikia kwa kichwa, akaitikia kifahari zaidi, jina la Agapella halikuwa jina dogo mjini.
‘aaaaw!... Bingo!... I don’t have to miss darling…’ akashadadia Marino akitupa tupa mikono yake kike
‘No way out Marino… huwezi kukosekana the super stylist in town’ Rebecca akampamba na wakajikuta wakigongesha mikono na vicheko juu

‘Mama… hili linabana sana tumbo.. zipu haifungi’ Pamella akalalamika kule ndani na Marino akageuka haraka kumuwahi mteja ‘ sweet nakuja’ Marino akampoza.

Rebecca akabaki mwenyewe akiangaza angaza mpaka Marino na Pamella walipotoka mule kwenye chumba cha kujaribia. Kwa sekunde tatu Rebecca alimtazama mtoto wake kwa mshangao. Gauni lilikuwa limemkaa vizuri mno! akatikisa kichwa kuitikia kuwa lile ndilo gauni lililokuwa chaguo lake.

‘this is it Pam!... ndio gauni la kuvunjia siku na kuacha historia baby… you look amazing’ akamsifia binti yake akimfuata pale alipokuwa amesimama akijitazama kwenye kioo cha pembeni. Wakati anamfikia mlango wa duka ukafunguliwa na Annie, dada yake Rebecca akaingia!

‘Wow! Ma’ mkubwa Annie’ Pamella akapiga ukelele akiweweseka kwa furaha na kumkimbilia mama yake mkubwa. Wakakumbatiana kisha Annie akauchukua mkono wa Pamella wenye pete na kukitazama kito
‘Don’t tell me ni Tanzanite’ Annie akauliza kiushabiki akiitazama pete ya uchumba ya Pamella
‘Yeaaah!...’ akaitikia kifahari na kukumbatiana tena kwa furaha kisha akawafuata Marino na Rebecca na kuwasalimia kwa kuwakumbatia
‘Nimemuona mumeo kwenye picha… mzuriii..mzuri mnooo…utamuweza? maana mjini hapa atawindwa mpaka basi au ndio mwanzo wa ugonjwa wa moyo mwanangu’ Annie akaweka mkono wake kwenye moyo wa Pamella, akifanya watu wacheke sasa

‘Umeingia na ndege ya saa ngapi?’ Rebecca akamuuliza
‘Niko town tangu jana mbona…. I wanted to surprise you guys… naona sughuli imeanza’ annie akazungumza akilitazama duka juu juu
‘Na ndio tulikuwa tunakungoja wewe tujue what is next…’ Rebecca akajibu kwa shauku

‘Ni binti pekee wa Okello… hii inabidi iende kiitifaki haswaaa… lazima tuache historia kidogo midomoni mwa watu… au sio honey?’ akamuuliza Pamella naye akaitikia kishabiki kwa furaha
‘Kabisaaaa!’
‘haya umeandaa nini?’ Rebecca akuliza naye kwa shauku
‘…tunaanza na singo party… bi harusi wetu atachuliwa na vikorombwezo toka mombasaaaa… kisha inakuja kibao kata kuna msondo huo unatoka lamu…’ Annie akaelezea akitamba na wenzake wakacheka
‘….enheeee!’ wakaitikia wasikilizaji
‘Then tuna kitchen party… hapa kuna mfundaji sijui mshamsikia anaitwa Laura Pettie wenyewe tunamuita LP a.k.a msema lolote popote…’ akauliza kwanza
‘hahahahahaa LP?... mamaaaa aunt jamani kweli?… nishamsikia huyu dada… mambo yake super hasaaa’ Pamella akashadadia
‘LP nilimuona kwenye kitchen party ya yule mtoto wa mbunge… nilimpenda bure kwa kweli ila nikasikia kumpata sasa shughuli…’ Rebecca akaingilia

‘basi ndio umempata sasa… yaani niliposikia harusi tu pah! nikasema huyu dada asikose hii shughuli kabisaaa… tutamalizia na sendoff yetu kama kawa… usiwe na hofu mwanangu… mama zako asili yetu mombasa na shughuli zetu unazijua… kitu classic…  unakwenda kwa mume kwa heshima zote…unaagwa kwa shughuli zote mjini… uko kwa mume wajue hawajakuokota mtini… wala hawajakutoa ndani kama kontena bandarini… na tuwahakikishie kwenu hujafukuzwa wala hujachokwa…ila umeagwaaa’ Annie huyu akatamba mwenyewe. Lile dera lake la kisasa, na ule mkoba wa gharama changanya na viatu mchuchumio wa haja… uongeze na manukato ya bei mbaya na lemba la kinaija. Picha ya nje tu ilitosha kukwambia Annie alikuwa mama shughuli!

Vicheko vikatawala kwanza
‘Mashangazi zake wanakuja lini?’ Annie akauliza akivunja vicheko
‘Siku moja kabla ya sendoff… watakuja na ndege kwa pamoja, wanasubiriana Nairobi kwa baba yake mkubw Pamella’ Rebecca akajibu
‘Watakuta tushafanya yetu!’ Annie akajibu akimgeuza Pamella kwenye kioo ili walione gauni vizuri lile gauni alilokuwa amevaa

Shughuli ya harusi ilikuwa imepamba moto mno. Na washughulikaji ndio hawa walikuwa shughulini kuandaa shughuli.

Wakati Pamella akihangaikia gauni lake, kule kwa Jerry. Fundi alikuwa na kazi yake.
‘… koti lifike hapa?’ fundi aliyekuja kumpima suti Jerry aliuliza akiwa na tepu ya kupimia.
‘ shuka chini kidogo’  Jerry akajibu akiangalia vema hapo alipotaka koti la suti yake liishie. Meddy aliyekuwa na kinywaji mkononi, akiwa amekunja nne kwenye sofa mbele ya Jerry na fundi aliguna kuonyesha kutoridhishwa na urefu wa koti

‘hili litakuwa koti au kanzu sasa… liweke juu kidogo bwana’ akashauri na Fundi akapandisha kidogo na kuuliza ‘hapa?’
‘Eeh hapo hapo…’ Meddy akajibu na Jerry akatazama hapo aliposhauri Meddy.
‘Okay! fanya hapo basi’ akakubali
‘… hivi mkeo ameshafanya shopping ya nguo yake?’ Meddy akauliza
‘Sijui kwa kweli’ Jerry akajibu akigeuka kufuatiza maelekezo ya fundi na kazi yake ya kumpima na kuandika daftarini.
‘Hapo ndipo ninapokushangaa aisee..’ Meddy akanogesha soga

‘Kwanini?’ Jerry akabweua wakati akiuliza
‘Ni harusi yako lakini wala hauna ile hali ya mshawasha kuwa unaoa…’ Meddy akadadisi kijanja
‘Sasa ulitaka nivae bango usoni au niweke tangazo hapo getini kuwa sasa naoa and i’m so excited?’ Jerry akauliza na kufanya fundi acheke kichinichini na Meddy acheke kwa sauti, yeye akiweka akiba kicheko chake.

‘ ile hali inakuja automatically bwana… kwako siioni hata kidogo’ Meddy akapingana naye
‘Kwani mtu aliye excited anakuwaje?’ Jerry akauliza akitanua mikono hewanikupima urefu wa mikono ya suti
‘tumuulize fundi… yeye ameshapima watu wanaotarajia kuoa… hivi kusema kweli unavyomuona huyu jamaa ni mtu anayengoja harusi yake kwa hamu?’ Meddy akamchonoa fundi mtu mzima aliyebaki kucheka tu

‘Fundi mwenyewe amecheka tu… vile ameona huna ile furaha inayojulikana’ Meddy akachochea mawazo yake na kumfanya Jerry atikise kichwa tu.
Fundi akamaliza kazi yake na kuongea na mteja wake hili na lile kisha wakaagana. Jerry akajitupa kwenye sofa na kutikisa kichwa
‘Nimechoka aisee!... yaani hapa robo tatu ya shughuli zote zinafuatiliwa na watu lakini bado hii robo iliyobaki imenichosha mno’ akalalamika

‘… bado wiki mbili sijui… utapumzika na mamaa Pamella… sometime siamini you guys are getting married…’ Meddy akatabasamu alipoyasema haya akimtazama Jerry
‘Me too…’ Jerry naye akaitikia bila tabasamu bali hali ya kuchoka zaidi
‘but be honest Jerry… hujamuwaza Sindi kabisa tangu umchumbie Pamella?’ Meddy akajikuta akishindwa kuvumilia na kuhoji

Meddy akageuka kichovu na kumtazama rafiki yake.
‘Sio kumuwaza… I dream about her almost every single night’ akajibu akitikisa kichwa juu chini
‘Nini??!...  come on Jerry… what?!’ Meddy akaiona ile glasi ina uzani wa kilo kumi, akaitua kwenye meza ndogo pale sebuleni na kumtazama Jerry kwa mshangao wa kutoamini alichosikia na Jerry wala hakujishughulisha naye, ndio kwanza alishusha pumzi, na uso wake ulioonyesha kukosa furaha ukielekea mbele ya luninga.

Meddy alikuwa akihisi alichokuwa akikiwaza kichwani mwake kilikuwa sahihi ila kwa kukisikia toka kwa Jerry mwenyewe alipata zaidi ya uhakika na akaona wazi uamuzi wa Jerry kumuoa Pamella ulikuwa sawa na kulifunika bomu linalohesabu dakika kwa mikono yake mwenyewe.
88888888888888888888888
Sindi Nalela alizinduka toka kwenye usingizi mzito na kufumbua macho yake kwa taabu. Kwa macho malegevu yalijaribu kuangalia usawa ule alioamkia na kumuona Nadina akiwa amelala kwenye kiti kilichokuw akando yake.

Akatabasamu kivivu na taratibu lile tabasamu likatoweka, na wakati huo akili yake ikianza kufanya kazi na kuyatambua mazingira aliyokuwemo hayakuwa mazingira aliyoyazoea. akajilazimisha kuangalia huku na kule lakini bado hakupatambua kwa namna yoyote.

Akataka kumuita Nadina, lakini sauti yake ikakwamia kooni na akajikuta akimwemwesa midomo yake pasi kutoa neno. akainua mikono yake kwa taabu na kugundua kulikuwa na drip iliyokuwa ikiingiza maji mwilini mwake. Akashtuka zaidi na kutaka kujiinua lakini maumivu ya kichwa yakamrejesha chini haraka sana, akitumia ule mkono mwingine kukishikwa kichwa chake. ukelele mdogo wa kuvumilia maumivu ya kichwa ulimshtua Nadina toka usingizini.

‘Oh.. Sindi umeamka/… unajisikiaje?... sindi… Sindi’ Nadina akamhoji Sindi akiwa ameshamfikia Sindi pale kitandani. Akataka kumporomoshea maswali mengi kwa wakati mmoja lakini akakumbuka ushauri wa daktari kuwa alipaswa kumuacha apumzike kwanza.
‘Kiu…maji…maji’ kwa sauti ya kukwaruza Sindi akaomba maji na Nadina akaifuata chupa ya maji iliyokuwa kwenye mfuko kando ya kitanda na kuitoa. Akamrudia Sindi na kujaribu kumuinusha ili aketi wima angalau, alipomuweka sawa kidogo hukua akiwa bado amemshikilia akafungua chupa ya maji na kuanza kumnywesha

mlango ukafunguliwa kwa nguvu na Adella akaingia mule chumbani, moja kwa moja mpaka alipo sindi, akampokonya Nadina ile chupa ya maji na kuirushia mbali, akaushika mkono wa sindi uliokuwa na drip na kuichomoa drip bila kujali maumivu wala utalaamu uliohitajika kuchomoa ile drip akausukumia mbali ule mlingoti uliotengenezwa kushikilia drip. Sindi akapiga yowe la maumivu. Wakati Adella akimsukuma Nadina kando na kummuangushia chini Sindi. midomo ya Adella iliachia kila aina ya tusi lililomjia akilinia

Ni wakati huo ndio Tima naye aliingia kwa kasi pale na kukuta uharibifu wa Adella huku Sindi akiwa sakafuni kama mzigo
‘Angalau mara moja katka maisha yako Adella…fanya ubinadamu!’ Tima akasema kwa uchungu wakati Adella akimtazama Sindi pale chini

‘…ubinadamu?... nimewahi kuonyeshwa ubinadamu hadi nijue kuwaonyesha wengine?... huyu Malaya asitake kucheza na mimi kabisa…. nitakuua we’ binti… usiniletee umajinuni kwenye biashara zangu… pesa nilizotoa kukuleta hapa sikuzitoa uje kujiuguza sijui kudeka deka kusiko na kichwa wala miguu… you do drugs it your problem… your damn problem!...not mine… not my business… amka toka toka hapo chini na urejee kazini sasa hivi’ Adella akaamrisha akihema kwa hasira

‘Anaumwa’ Nadina akamtetea na Adella akageuka na kumtazama Nadina
‘mara moja katika maisha yako…jifunze kutokuingilia mambo yasiyokuhusu… na alaaniwe mwanamke aliyekuzaa wewe.. kafie mbele uko’ akamuonyesha mlango na nadina kwa woga akajitoa na kutoka nje.

Adella akamtazama Sindi pale chini
‘Simama’ akamuamrisha
Sindi akajitahidi kusimama lakini mwili haukuwa na nguvu
‘Unaleta kiburi sio?’ akamuuliza akimuamrisha tena kusimama. Sindi akajitutumua kwa nguvu zote lakini nguvu ile aikuweza hata kumpigisha magoti sembuse kumuinua na kumsimamamisha

Adella akamvaa Sindi na kuanza kumtandika ngumi na mateke. Tima akampigia kelele za kumuomba amuachie lakini hakuthubutu kumgusa Adella. Alipoona Sindi anaelemewa na kipigo cha Adella akaropoka!
‘ni mjamzito!... she is pergnant’ Tima akasema akitetemeka, akilengwa na machozi na wakati huo huo akigeuka kumtazama Nadina aliyekuwa nalia mlangoni.

Adella akasimama ghafla na kumtazama Tima kwa mshangao,  akamkodolea macho Tima na kwa mara ya kwanza naye akakosa la kusema kwa sekunde kadhaa. Alimtazama Tima na kukimbiza macho kumtazama Sindi pale chini alipokuwa anatweta
‘Ana nini?’ akauliza kwa sauti kali mno, macho yakizidi kumtoka
‘Ana mimba’ Tima akajibu kwa sauti ya chini, sauti ya kusihi huruma, sauti ya kurai huruma, sauti ya kukata tamaa.

‘Mimba??... mimba ya nani?’ Adella bado alikuwa hajaelewa hata moja!
‘Sijui… lakini ameingia hapa akiwa na mimba tayari’ Tima akazidi kuweka wazi, moyo ukimuuma mno, hakutarajia angekuwa wa kwanza kuifichua siri ile hata kidogo lakini hakuwa na jinsi.
‘Siwaelewi… it seems kuna mambo yanaendelea humu ndani wakati bosi nikiwa sina habari… Tima… Timaa… Timaaa’ Adella akaita kwa hasira akipasa sauti zaidi kwa kila neno alilotamka

‘Please!... angalau huyu kuwa na huruma naye… nilipoteza mimba yangu nikiwa na miaka 16 tu… please!... muache azae… muache amshike mtoto wake mikononi mwake… angalau tulichokosa mimi na wewe yeye akipate… najua unajua ni kiasi gani inauma kupoteza mtoto’ Tima akaanguka chini na kupiga magoti mbele ya Adella. Akimuombea Sindi nafasi ya kuilea mimba yake…

Adella akacheka, akacheka kicheko cha hasira, kicheko kilichoanza kwa sauti na kuishia chini taratibu
‘…kama sikupata moyo wa kumtazama mtoto wangu usoni baada ya kumzaa mwenyewe kwa mikono yangu… sidhani kama nina moyo wa kumuachia mwingine apate kile nilichokosa mimi… call the doctor nowr… ana wiki moja ya kuuguza majeraha ya abortion na atarejea kazini akiwa na nidhamu zaidi ya hii uliyonayo wewe!’ Adella akampita Tima na kutoka nje. Akimuacha Tima akifumba macho na kububujikwa na machozi. Nadina akimfuata Sindi kwa kasi na kulia pamoja naye. yule yule msichana aliyekuwa akiwachungulia wakati walipokuwa wakiongea na dokta na huyu huyu aliyekuwa akiwachungulia sasa wakiwa wanalia, umbeya wake ulishafanya kazi!
888888888888888888888

Saa nne na vichapo kadhaa usiku, Jerry aliendesha gari taratibu na kulisimamisha mbele ya nyumba ya Pamella. Pamella mwenyewe akiwa garini.
‘Unatakiwa kukaa nyumbani kwa wazazi wako Pam… not all alone like this mpaka ukichukuliwa rasmi’ Jerry aliongea akimtazama mchumba wake Pamella ambaye  alitabasamu tu na kumbusu Jerry pajini

‘Leo nimejisikia kuwa mwenyewe… nitalala hapa kwa mara ya mwisho then kesho nitahamia home kabisa… you are just like my dad… always overprotective!.. I’ll be fine’ Pamella akajitetea
‘Sihofii usalama wako Pam… you have been living all alone kwa muda mrefu… nazungumzia mila na desturi et al’ Jerry akampinga kimzaha akimfanya Pamella acheke
‘… okay hubby to be!... nitafuata mila… kesho asubuhi nitarudi nyumbani nitulie ndani’
Pamella akasema kimadeko akimtazmaa mchumba wake

‘,,,naaaa’ Pamella akalivuta hilo na kwa mbwembwe kisha kuimung’unya midomo yake
‘Na nini?’ Jerry akauliza uso ukiwa na umakini
‘Na mila zinasema hutakiwi kuniona tena mpaka siku ya sendoff’ Pamella akasema lake
‘aaah wapi.. come here’ Jerry akakataa akimvutia Pamella kwake na kuanza kumbusu wakati huo huo Pamella akiringa na kukataa kupigwa busu. Wakatekenyana kama watoto kisha wakatulia wenyewe.

‘…  usiku mwema babe!’ Jerry akaaga na Pamella akajileta mwenyewe mbele ya Jerry na kuruhusu busu la mdomo. Wakakumbatiana na Pamella akashuka garini
‘Thank you kwa dinner Jerry; akamshukuru akiwa anamchungulia kwenye dirisha la mlango wa gari baada ya kushuka na kufunga mlango wa gari.

‘Mila na desturi zinasema… hupaswi kuniita Jerry tena… naitwa mume mtarajiwa’ Jerry akamkosoa tena na Pamella akacheka kwa sauti huku mwenzake akikosa hata tabasamu
‘Okay okay okay… asante kwa dinner mume wangu mtarajiwa…’ Pamella akashukuru tena
‘Asante kushukuru… hivi umepata gauni?’ akamuuliza akikumbuka hiyo inshu kwani ni yeye ndiye mwenye jukumu la kulilipia
‘Yeah!... nitakupitisha dukani kwa Marino au nitakuja na picha za gauni ulione’ Pamell akajieleza
‘Okay .. fine!... take care’ Jerry akamrushia Pamella busu la mbali na kuwasha gari. lile tabasamu alilokuwa nalo likitoweka wakati akipangua gia na kuingiza gari barabarani. akazama mawazoni!

Pamella akalifuata geti lake na kuingia ndani.
‘dada…’ mlinzia akamuita mara baada ya kumfungulia
‘Pumzika tu… tutaongea kesho’ akamjibu mlinzi, akilini akijua mlinzi alitaka kuanza kumueleza shida zake ili aombepesa. alishamzoea kwa tabia yake hii. Kwa usiku huu alihisi kuchoka mno, hakutaka kabisa kuketi pale nje kusikiliza stori za mlinzi, akamjibu mkato akijua angempa pes hizo asubuhi bila kuhitaji kusikia.

akatembea akitabasamu na kucheka mwenyewe baada ya kukumbuka utani wa  Jerry kuhusu mila. Akakorokochoa mlango na kuingia ndani. akaufunga mlango na kuuondoa ufunguo mlangoni. Kulikuwa na giza mno, mwanga wa mbalamwezi uliopita dirishani kulikokuwa hakujazibwa na mapazia yaliyokuwa yameachwa wazi ulileta mwanga kidogo wa kuweza kuona anakopita.

Akageuka na moyo wake ukapiga mkambi, ghafla tu alihisi baridi mpaka kwenye mifupa, ule ufunguo aliokuwa nao mkononi ukidondoka sambamba na pochi. aliona kiwiliwili cha mtu kwenye sofa. Moyo ulipiga mara mbili ya kawaida na msisiko uliompitia mwilini ulimsisimua mpaka vinyweleo kumsimama.
‘Oh Mungu wangu..’ akasema kwa hofu mkono wa kulia ukiwa kifuani, na ule wa kushoto ukitetemeka mno na kupapasa ukutani  upande huo wa kushoto ili kuifikia swichi. Akawasha taa!

uso kwa uso na Patrick Mazimbwe!... msisimko mwingine ukapita mwilini mwake kama shoti ya umeme.
likuwa ameketi kwenye sifa lililokuwa mbele ya Pamella, mezani kukiwa na chupa ya pombe kali na mikononi akiwa na bastola ndogo aliyokuwa anaitazama na kuigeuza geuza kama mtoto mdogo anayelichunguza toi lake.

Pamella alitetemeka, lakini akatetemeka zaidi wakati Patrick alipoinua uso wake na kumtazama usoni kwa macho makali mno huku machozi yakimtoka. hata nguvu za kupiga yowe zilimuishia!

ITAENDELEA….

1 comment:

  1. Jmn laura nakupenda bure ila plz ifanye jery na sind waonane kapitia mengi mno

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger