Mpenzi msomaji!
Tunauanza mwezi mpya… mwezi wa
mwisho wa mwaka…mwezi wa likizo kwa
wengi na mwezi unaojulikana kama mwezi wa sikukuu. Christmas na Mwaka mpya ni wiki chache zijazo. Ni jambo la kumshukuru
Mungu sana kuwa mimi na wewe mpaka dakika hii tupo hai na kwamba pamoja na
changamoto zote za kidunia na kiimani bado tungali hai tukipewa nafasi nyingine
ya kunyoosha njia zetu na kurekebisha hapa na pale. Tunasema Asante Mungu!
Kama ilivyo ada tunapouanza
mwaka, wengi wetu huwa tuna zile New Year’s Resolutions!.... mipango ya mwaka mpya kwa mwaka mzima. Na sasa tunapoelekea
kuumaliza mwaka tunapaswa kukaa chini na kutazama ni yapi tumeweza kuyatimiza
na yapi yamekwama na kwa sababu zipi. Kwa ujumla ni wakati wa kujitathmini kwa
kina na kujiandaa kumalizia yaliyokwama na pengine kupanga mengine mapya.
Yawezekana yapo tuliyoyapanga lakini kutokana na sababu za maana na zisizo
za maana kama uzembe na kukata tamaa basi tumeshindwa kuyatimiza. Si busara
kuyatupa mbali na kutafuta mapya, ni vema tujitathmini ni kwa vipi mambo haya
hayakutimia ili kuyajua kwa undani madhaifu yetu na kuyafanyia kazi.
Kwa kuuanza mwezi nina neno kwako msomaji! Mambo haya SITA nimeona ni mazuri tukiyafanyia kazi wakati tunapoelekea kuumaliza mwaka.
1. ONDOA VINYONGO, MINUNO,
HASIRA NA VISASI:
….. katika safari yetu ya maisha hapa duniani yapo
mambo na wapo watu ambao hutukwaza kwa kiasi cha kuacha makovu mioyoni mwetu…
tunaapa kutowasamehe…. Tunaapa kuwachukia kila tunapowaona….
Mpendwa msomaji!
Kwa imani yangu ya kikristo tumeagizwa kusamehe duniani ili
Baba Mungu apate kutusamehe pia dhambi zetu…. Wakati tunapoelekea kuumaliza
mwaka ni vema tuitue mizigo hasi chini na kujaza mioyo yetu amani na utulivu
wa nafsi….
Samehe hata kama hujaombwa msamaha! Msamehe na jisamehe! Na uanze
mwezi mpya wa mwisho wa mwaka ukiwa na roho safi isiyo na chochote hasi dhidi
ya mtu mwingine! Kukaa na vinyongo, hasira na visasi moyoni dhidi ya mtu
hakukusaidii kitu zaidi ya kukufungia mibaraka kwako na kizazi chako!
2. OMBA MSAMAHA WA DHATI:
…. Waombe radhi uliowakosea. Wahenga walisema
Kiburi si maungwana. Inakufaidia nini kujaa kiburi kiasi cha kushindwa kuomba
radhi kwa mtu uliyemuumiza na unajua fika kuwa umemuumiza? Jishushe na umpe
mwenzio amani ya moyo! Hakika hata wewe utajisikia amani kupatana na mtu
uliyemkosea hata kama hatokusamehe hapo hapo lakini utakuwa umejitoa lawamani.
3. ANZA KUANDAA MIPANGO YAKO
…. Binadamu huwa tunapanga ila Mungu huwa
ana mipango yake inayompendeza yeye. Pamoja na hili, haituzii kuanza kujipanga.
Usisubiri kesho, usisubiri mwakani. Nafasi ya kurekebisha uliyokosa kuyafanya
kwa wakati uliopita anza leo kurekebisha japo hata kwa kukaa chini na kupanga
ni namna gani utarekebisha…. Usiogope kujikosoa na kuyaona madhaifu yako kwa
uwazi. Itakusaidia kupambana na changamoto zijazo…. Yawezekana ulipanga kuwa na
biashara yako…. Usingoje krismasi ipite anza leo hii tar 1 kuweka mawazo yako
ya wapi uanzie!
4. SAIDIA WENGINE WAFANYE WATABASAMU
…. Wasaidie watu wengine kufikia malengo
yao hata kwa kuwapa moyo na mawazo chanya. Usishiriki katika kumdidimiza
mwenzio… kuna mema mengi Mungu
amekufanyia kwa mwaka huu. Hata kama unayapima mema hayo kwa kulinganisha na ya
mtu mwingine… bado kuwa na afya njema, kuwa na kama ulivyo, kuwa na watu wako, kuwa hai ni kati ya mema
unayopaswa kuyashukuru kwa Mungu na kuyarejesha kwa njia ya kufariji wengine….
Mnunulize mtu zawadi na umpatie pasipo sababu yoyote…. Mpe chakula
masikini ili uone tabasamu lake usoni… zungumza na mtu aliyekwama mpe matumaini
ya maisha… msaidie mzee kwa furaha uone shukrani yake usoni…. Mpishe njia mwenzio kwa nidhamu…
mfungulie mlango mwenzio kistaarabu… msalimie mtu ambaye siku zote huwa humsalimii…mpe bonus
mtumishi wako wa ndani…. Mpigie simu ndugu yako aliye mbali ambaye ni ndugu yako wa karibu lakini huwa huna mawasiliano naye...mtu kama bibi, shangazi, babu , baba mkubwa...baba mdogo au ndugu yako wako wa damu nk...
unaweza hata ukamwambia rafiki yako.... mpenzi wako...mwenzi wako namna anavyogusa maisha yako...ukamshukuru akiwa hai kuliko kungoja siku yake ikifika ndio maneno yakutoke akiwa ameshatangulia!
Na mengine mengi! Yote kwa yote fanya jambo lolote lililo ndani ya uwezo wako
kumfanya mtu mwingine atabasamu!
5. JIPONGEZE
Wengi tunaishi tukiyatafuta maisha na kusahau kuyaishi maisha yenyewe
Jipongeze hata kwa kitu kidogo ulichofanikiwa kukifanya.... Jipe muda ukafanye massage.... toka nenda mahali mbali ukapumzike wewe na wmenza wako au peke yako.
Jinunulie kitu cha kukufurahisha.... jiambie maneno mazuri ya kujenga nafsi .... usikae ukajiambia maskini mimi... kwanini mimi.... sina bahati hiyo na kadhalika. maneno mabaya huumba haraka!
5. KIKUBWA TATHMINI UHUSIANO WAKO NA MUNGU!
.... wengi tunajisahau
sana katika hili. Tunadhani siku pekee ya kuongea na Mungu ni siku ya kumuabudu…
ni wakati unapokwamba tu ndio umkumbuke Mungu…. Jiulize ni Mara ngapi pasipo
sababu yoyote umetabasamu ukamshukuru Mungu wako…. Pengine baada ya chakula cha
mchana… pengine baada ya kuitazama meza ya ofisi yako…pengine baada ya kutazama
watoto wako…pengine baada ya kulitazama gari lako ama tu kwa kujihisi mwenye
bahati kuwa hivyo ulivyo, hapo ulipo!.... jiulize ni mara ngapi katika maisha
yako umeongea na watu kuhusu Mungu katika namna ya kuwakumbusha uwepo wake?
Kuna watu wanadhani mambo ya Mungu hayawahusu…. Au ni ujanja
f’lani kutokuzungumzia kuhusu imani na Mungu hadharani lakini Shetani
anapokutandika na majanga haraka sana watu husema Mungu nisaidie…maombi yenu
wapendwa nk!
Tunapoelekea mwishoni mwa Mwaka tunapaswa kujipongeza na
kujirekebisha pia!
Kwa siku ya leo naishia hapa!
Niwatakie mwezi mpya mwema! Panapo majaaliwa basi tukutane tena wakati mwingine
Laura Pettie
Laura jaman imebidi nije kwa blog yako huku maana naona kama kule sikufaidi kabisa
ReplyDeleteManeno mazuri
ReplyDelete