Thursday, April 28, 2011

SIRI YANGU......na Laura Pettie

....Hadithi hii niiandika muda kidogo lakini nimeona si mbaya kama nitaiweka humu kama mwanzo tu wa yale niliyoyaahidi...Ni hadithi inayohusu maisha ya msichana Karen...ilikuwaje mpaka yaliyomo yakabaki kuwa siri yake...lets share!

Karen


Upepo mwanana ulivuma toka pande mmoja kuelekea upande mwingine, upepo huo uliyayumbisha makuti makavu yaliyokuwa yakining’inia minazini na kuleta raha isiyo kifani. Minazi ile nayo iliinamia upande na kuzidi kuleta mandhari ya kuvutia hapa ufukweni mwa bahari. Nilikuwa nimetulizana pembezoni kidogo mwa mgahawa uliopo hapa coco beach. Kopo la soda aina ya cocacola lilikuwa mkononi hali mawazo yangu yakiwa kule baharini ambako watu walionekana kuyafurahia maji bahari.


Ilikuwa kawaida yangu kupumzika mahali kama hapa kila mwisho wa wiki. Yote hii ilikuwa ni kutafuta namna ya kujisahaulisha machungu niliyokumbana nayo miezi miwili iliyopita. Machungu ambayo kwa namna moja ama nyingine yameyabadili maisha yangu na kunifanya niyaone katika yalivyo ndani ya upande mwingine wa shilingi. Katikati ya wiki nilifanya kazi mpaka saa tatu za usiku na niliporejea nyumbani niliishia kulala kwa uchovu mpaka alfajiri ya siku iliyofuata. Nilikuwa mtoto wa tatu na wa mwisho katika familia yetu. Kaka yangu Brian alikuwa daktari katika hospitali moja binafsi. Dada yangu Debby alikuwa anamiliki saluni yake binafsi na mimi kitinda mimba nilikuwa muhasibu. Baba yetu alikuwa mwenye kumiliki biashara mbalimbali hali mama alikuwa msaidizi wa baba katika biashara zake na mara nyingi alikuwa akikaa kwenye duka lililokuwa karibu kabisa na nyumbani. Katika kukua kwangu nilikuja kugundua kuwa baba na mama walikuwa katika mgogoro mzito ambao hawakutaka kuuweka wazi kwetu! Mgogoro huo uliokuwa ukifukuta chini kwa chini uliniacha ndani ya maswali mazito!

Mara nyingi niliposhtuka usingizi usiku niliwasikia wazazi wangu hawa wakizozana kwa sauti za kunong’ona na nilishindwa kuelewa kilichokuwa kinapelekea hali hiyo kati yao. Mara kadhaa baba aliondoka nyumbani na kukaa wiki mbili hadi tatu bila kurejea nyumbani na tulipomuhoji mama alibakia kulia na kutuambia kuwa hakukuwa na kitu kibaya kati yao. Mpaka namaliza chuo na kuajiriwa bado sikuwa naelewa kilichokuwa kinawakosanisha wazazi wangu.

Ukweli ni kuwa sikuipa akili yangu nafasi ya kujua kuwa katika kitu mapenzi zipo raha na karaha na kwa hakika ilikuwa zamu yangu kupambana na kitu karaha ya kuachwa mpweke ndani ya dunia hii ya mapenzi. Sikuwahi kuwaza kuwa mapenzi yanaumiza hivi hususani linapokuja suala la kuachwa bila huruma, bila hatia wala kupewa njia ya kukabiliana na huu mtihani….Inshallah! machozi ya mnyonge Mungu huyalipa na kuyalipia.

Mwaka mmoja uliopita nilivikwa pete ya uchumba na aliyekuwa mchumba wangu wa siku nyingi Dokta Kelvin Nashon. Sherehe hiyo ya kuvishana pete ilifanyikia katika hoteli ya kitalii ya Paradise huko Bagamoyo. Huku tukishuhudiwa na ndugu, jamaa na marafiki mimi na Kelvin tulifikia uamuzi huo mara baada ya uchumba wetu kutimiza mwaka mmoja, mwaka mmoja wa misukosko ya hapa na pale, mwaka mmoja ulioweka hatihati ya kuachana na ndio huo Mwaka mmoja uliojaa kila aina ya mbwembwe za penzi shatashata, kweli kivumacho hakidumu na kikidumu jua kweli kigumu. Nilimpenda Kelvin mno na ndiyo maana licha ya kutokea hayo yaliyouumiza moyo wangu nahisi bado nampenda Kelvin. Niliamini tungefunga ndoa na Kelvin miezi michache tu baada ya kuvikwa pete ile lakini hilo halikutimia. Kelvin amefunga ndoa miezi miwili iliyopita na msichana aliyekuwa kipenzi cha wazazi wake.

Ingawa alishanieleza toka awali kuwa wazazi wake wamemtafutia mchumba toka kwao Bukoba lakini sikufikiria kuwa ingefikia hatua hii yakuachwa solemba na pete yangu kidoleni. Nililia sana lakini pia nilikuja tambua kuwa sitaweza kuibadili historia na kilichobaki ni kuukubali ukweli kuwa mimi Karen nimeachwa na Kelvin mwanaume niliyempenda kuliko kitu chochote hapa duniani. Sijui ni nilidanganywa, sijui nilizuzuka lakini yote kwa yote, alichonitendea Kelvin kilikuwa zaidi ya maumivu na zaidi ya aibu. Waliokuwa wakichukia kupendana kwetu walipata cha kusema, walipata cha kucheka…Kelvin kwanini ulinitendea hivi bila huruma?

Uchungu wa kuachwa na Kelvin ulinirudia mara kwa mara kunifanya niwe mnyonge mno, nilizikumbuka mara kadhaa nyakati tamu na za kusisimua tulizokuwa pamoja, ilikuwa ni kama msomaji anavyofungua ukurasa mmoja baada ya mwingine, yote yamebakia kama kumbukumbu tu. Kelvin si wangu tena!. Licha ya familia yangu kuwa nami kwa kila hali lakini bado jereha la moyo aliloniletea Kelvin lilikuwa bichi kabisa. Ni bora basi asingenivisha pete hii ambayo kila ninapoitazama natokwa na machozi, ni bora basi angeniacha awali kabla sijamuingiza moyoni mwangu!

Kelvin amenitupa, Kelvin amenisaliti na ameniacha kama kipofu katika msitu wenye kiza kinene. Uchangamfu niliokuwa nao ulitoweka kabisa na ilifikia hatua mimi Karen nikakoroga sumu na kujaribu kujiuua ili tu kuiepuka aibu na jitimai iliyonikumba kutokana na mkasa huo! Baba yangu aliyekuwa nchini Kenya kikazi alirejea haraka Tanzania mara tu alipopewa taarifa kuwa nilikuwa hospitali mahututi sijitambui. Kuponea kwangu chupu chupu kuliwafanya wazazi wangu wawe karibu zaidi na mimi ili kunifanya nisijisikie mpweke,

wakasahau kuwa raha kamili ya dunia ni mambo matatu ni yale alowahi kuyataja hayati Shaaban Robert. Kwanza afya ujaliwe kuwa nayo mtu, pili akili upewe umiliki vitu lakini zaidi ya haya upendwe na mtu!.....

ITAENDELEA....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger