Friday, April 29, 2011

SIRI YANGU 2.... na Laura Pettie


Ijapokuwa sasa naanza kuikubali hali hii lakini bado Kelvin anazunguka kichwani pangu na nahisi moyo wangu ukiumia zaidi ninapozitazama picha zake, ninapokumbuka nyakati za furaha tulizokuwa pamoja, nyakati tamu ambazo kwa hakika najua hazitajirudia tena katika anga hili la karima. Muda huo wa jioni ya jumapili hiyo tulivu Nilikuwa ufukweni hapo pamoja na rafiki yangu Iloma aliyekuwa ameambatana na mumewe Jonas. Iloma alikuwa mfanyakazi mwenzangu na rafiki yangu mkubwa wa tangu utotoni. Yeye alikuwa tayari ameshaolewa na kubahatika kupata mtoto wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja. Wakati Iloma na mumewe Jonas wakiogelea pamoja na mtoto wao mimi nilibakia pale ufukweni nikiwatazama namna walivyokuwa wanafurahia maisha yao ya ndoa. Nilihisi nikiwaonea wivu kwa amani na upendo uliokuwepo kati yao. Nilihisi uchungu ambao naweza sema hausemeki mdomoni wala hauandikiki karatasini. Ilikuwa ni mithili ya mvuke wa maji ya moto penye kidonda kibichi.
Nilijiinua taratibu na kuanza kutembea kuelekea upande uliokuwa hauna watu zaidi. Nilizidi kupiga hatua na kutafuta mahali palipokuwa pamefichana na kuketi hapo. Nilihisi upweke, nilihisi uchungu na simanzi zikinikaba na kunifanya nijiinamie na kulia kwa kwikwi.
“ Kelvin…Kelvin why!... Why Kelvin…”
nilipayuka mwenyewe bila kujali kama kuna mtu anayeniona ama kunisikiliza. Niliyainua macho yangu juu na kuzitazama mbingu huku machozi yakizidi kunitiririka kwa fujo. Mikono yangu niliifumbata kifuani na sasa nilishindwa kuhimili uzito wa majonzi niliyokuwa nayo na nikaangua kilio cha nguvu.

Nililia sana nisijue hata cha kufanya pale nilipokuwa nimeketi. Mara zote nilitamani kukurupuka usingizini ili yale yote yageuke kama ndoto, lakini wapi hali iliendelea kuwa halisi na isiyo na hata chembe ya kiini macho!


“ sikustahili hukumu hii Kelvin, sikustahili maumivu haya mimi sasa kwanini umenifanyia hiv?” nilijiuliza pasipo kuwa na uhakika wa kupata jibu toka kwa huyo niliyemkusudia. Nililia kwa dakika kadhaa kisha taratibu nilijaribu kujizuia kulia. Ingawa hisia zilinitawala lakini pia nilijua kuwa kulia vile kusingebadili chochote katika historia chungu aliyoniachia Kelvin.

Nilivuta pumzi mara kadhaa na kuziteremsha kwa nguvu nikijaribu kuacha kulia hata hivyo nilishindwa kabisa kujitawala. Kilio cha chini kwa chini hakikukoma na machozi nayo yalizidi kuteremka kwa mithili ya kijito cha maji kitokacho bondeni..


Nikiwa nimeketi chini, niliikunja miguu yangu na kuyafanya magoti yawe egemeo la kidevu changu na mikono iliikumbatia miguu yangu hali macho yangu yaliyoviringwa na machozi yakiitazama bahari pasipo kuitambua akilini. Nilishtuliwa na mkono uliotua katika bega langu la kushoto. Nilihisi mshtuko usio wa kawaida mara baada ya mguso huo. Niliugeuza uso wangu kwa haraka na kumtazama mgusaji huyo aliyenifanya nihisi hisia Fulani za faraja moyoni mwangu. Alikuwa Jonas mume wa rafiki yangu mpenzi Iloma.



“ mbona umejificha huku Karen….na hupaswi kuwa katika hali hii kila mara” alinisemesha kwa upole hali akichuchumaa na kuzifanya nyuso zetu ziwe mkabala. Alikuwa mwanaume wa kuvutia mpole na mwenye sura nzuri ya kusisimua na mara nyingi watu walipenda kumfananisha na mwanamuziki Robert Kelly, urefu wake wa kadri, weusi wake wenye mvuto na sauti yake ya kiume iliyo nzito na tulivu, kwa hakika viliwafanya watu wa kila rika wazidi kumpenda Jonas.

Mbali na uzuri wa sura yake Jonas alikuwa na haiba ya upole na ucheshi na mara nyingi uso wake ulipambwa na tabasamu pana la kuhangaisha!
“ jonas haya ni maisha yangu ninayoyastahili”

“ hapana Karen, you still have a chance to be happy!” alinijibu akijiweka sawa kwa kuketi pale mchangani kando yangu. Macho yake maangavu yalimetameta na kutoa nuru ya faraja.

“ kwa vipi Jonas na Kelvin ameondoka na furaha yangu…huwezi kukisia hata robo tu ya maumivu niliyonao ndani ya moyo wangu,

kwanini amenifanyia hivi mimi mbona nilijitahidi kuwa mpenzi bora kwake sasa kwanini ameniacha katika hali hii jonas?” niliongea kwa ghadhabu na taratibu nikajiinamia tena kuanza kulia upya. Najua nilimpa Jonas wakati mgumu mno, alijisogeza karibu yangu na kuketi ubavuni pangu kisha taratibu aliupitisha mkono wake wa kuume mgongoni pangu na kunivutia ubavuni pake. Nilijikuta nikiuficha uso wangu kifuani pa Jonas. Nilihisi faraja na kupata ahueni kuwa mikononi mwa mtu kama huyu.

Pasipo kutarajia nikaizungusha mikono yangu kiunoni pa jonas na sasa kila mmoja aliyasikilizia mapigo ya moyo ya mwenzake. Tulitulia hivyo kwa sekunde kadhaa nami nikijitahidi kuzizuia kwikwi za kilio. “huyu ni mume wa rafiki yako Karen!” mawazo hayo yalipita kwa kasi akilini mwangu na nikajikuta najiondosha mikononi mwake ghafla na kusimama mbele yake hali macho yetu yakitazamana sawia. Niligundua sikupaswa kuwa nae pale.

“ u mrembo sana Karen!” alinitamkia kwa sauti ile ile ya kubembeleza. Sikumjibu kitu zaidi ya kuanza kupiga hatua na kumuacha pale alipokuwa ameketi. Nilirudi hadi pale nilipokuwa nimeketi mwanzoni na kumkuta Iloma akimvalisha mtoto wake sweta. Alionekana kukasirishwa na jambo.
“ Karen umemuona wapi Jonas?” Iloma aliniuliza mara tu aliponiona
“ aah!... kwani alikuaga anakwenda wapi?” nilimuuliza nikianza kuhisi kuwa Jonas hakuwa amemuaga mkewe wakati ananifuata kule nilikokuwa nimeketi.
“ hujamuona?” alinitupia tena swali badala ya kujibu swali nililomuuliza. Nilishidwa kumpa jibu la kumridhisha lakini hata hivyo nilizuga kwa kumkaribia na kumchukua mtoto.
“ ni bora tukiondoka sasa naona mtoto anakufa na baridi ya hapa beach” nilijisemeza kukwepa maswali zaidi ya Iloma aliyekuwa anaonekana kuwa na wasiwasi na mahali aliko mumewe.
“ Karen nimeanza kuchoshwa na tabia za Jonas…ni bora kama tutaongea kesho ofisini” iloma aliniambia kwa msisitizo kidogo, macho yake yalionyesha umakini katika kile alichokuwa anataka kunieleza. Nilimtumbulia macho tu pasi kuongea lolote. Niliteremsha pumzi za haraka na kumuuliza
“ Jonas amekufanyia nini Iloma?” nilimuuliza kwa mshangao kidogo
“ nadhani ni tatizo linalokua taratibu na kama sitalitafutia suluhisho mapema jungu bovu litageuka magae Karen” aliongea kwa huzuni.Aliniacha njia panda!
“ Kwani Jonas ame…” sikuweza kuimalizia sentesi yangu kwa vile Jonas alitokea upande wa pili mahali tulipokuwa tumeegesha gari. Iloma alimtazama mumewe kwa hasira kidogo na kuelekea kule alikokuwa amesimama.
“ hata hapa Jonas kwanini unataka kunitia aibu hivi mbele ya rafiki yangu!” nilimsikia Iloma akimfokea Jonas kwa hasira pengine bila kujua kuwa nilikuwa nae huko alikokuwa. Jonas hakumjibu kitu zaidi ya kuzunguka upande wa dereva na kuingia garini. Niliwafuata nikiwa nimempakata mtoto na kuingia garini. Safari nzima ya kuelekea nyumbani ilitawaliwa na ukimya wa ajabu licha ya Jonas kujaribu kumsemesha mkewe lakini Iloma alionekana wazi kuwa na kisirani fulani. Kwa hakika sikuwaelewa wanandoa hawa. Waliniteremsha nyumbani kwetu na wao wakaendelea na safari yao.

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger