HEBU TUNZA YA LEO YAKUSITIRI KESHO EBO!!
Ni kitambo kweli
hatujakutana barazani hapa… kuzungumza hiki na kile lakini leo kwa kudra za Mwenyezi
Mungu tuko pamoja tena. Alhamdullilah!
Basi hivi juzi
kati hapo katika mishughuliko ya hapa na pale nikakutana na kijana mmoja ambaye
nilipata tu kufahamiana naye kipindi cha nyuma. Kwanza nilisikitika si tu kwa
ile hali aliyokuwa nayo bali pia ulinganisho niliofanya kipindi cha nyuma
nilichomuona na sasa hivi alivyo. Tunasema maisha yanapanda na kushuka ni
kweli! ile sasa kuna wanaopandishiwa kisha wanayashusha wenyewe...!
Miaka miwili
iliyopita huyu kaka alikuwa mmoja wa wale vijana waliokuwa na maisha ambayo
kijana yoyote wa rika lake angetamani kuwa nayo. Sehemu ya kuishi, gari la
kutembelea na pesa ya kubadili mboga.
Ingawa ndio
kwanza alikuwa ameyaanza maisha lakini kwa kipindi kifupi hicho alikuwa
ameyapatia. Sasa juzi kati nilipokutana naye ndio mdomo ulinishuka kama kidevu
cha punda! Kama ilivyo hulka ya binadamu kuuliza kulinikamata nikianzia
kujiuliza mwenyewe mpaka kuuliza wengine! Kulikoni?
Ndio sasa
nikaambiwa jamaa aliyapatia maisha lakini ndio vile akili zingine aliwaachia
marafiki wamshikie na wakamshikia kwelikweli wakamuachia ya kuvukia barabara. Hakuna
baa ambayo hakutoa ofa, hakuna binti ambaye alimvutia na akampita tu… hakuna
starehe iliyokuja na ikampita… akawa mwema kwa kila mtu aliyetaka kukopa laki
na asilipe sawaa.. aliyetaka elfu hamsini akahonge hayaaa…aliyataka yote kwa
pupa!
Si akiba,… wala
vitega uchumi… alijua kesho ipo ingemletea ya kula kesho kutwa akisahau kutunza
ya leo imsitiri kesho na keshokutwa. Jambwe! Kwisha habari yake! Sasa jiulize
wale aliokuwa akitanga njia nao wako wapi?... unaambiwa hakuna hata nusuru ya
kusema huyu alimlia vyake leo kamsitiri. Hakuna!
Ndugu yangu,
kijana mwenzangu!.... hawa watu tunaowaita marafiki tunapokuwa kileleni ndio
hawa hawa wanageuka wageni tunaposhuka sakafuni. Hawa hawa wanakusifia
kwelikweli ndio hawa hawa watakusimanga utakaposhuka… maisha ni wewe, wema
tuufanye kwa kadiri tukikumbuka kuna kesho sio kwa kutegemea wema unaoufanya
leo basi utakuletea malipo utakapoanguka. Sahau!
Tenda wema kwa
kiasi ndugu marafiki wanafirisi…huamini?... ishi kwa malengo jua kuna
kuporomoka kesho!... kijana starehe haziiishi duniani kila uchao kuna mapya kama
matoleo ya simu!... utayaweza? Utayamaliza?...
Sijasema usisaidie
ndugu na marafiki!...angalia uwezo wako kwanza ndugu yangu…usitake kumfurahisha
kila mtu mbele yako… wakati hali yako mwenyewe ukunga ukijikuna watoka unga….utalia kilio cha
mbwa mdomo juu.
Nimemaliza!
Wasalaam
LAURA
maneno kuntuuu
ReplyDelete