…..sasa tusikie zaidi toka mtandaoni….
Ilikuwa ni Julai
30 1999, mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina la Brenda Dement nchini Marekani
aliyekuwa akiishi kwenye mji wa Barabo Wisconsin Kaskazini mwa Marekani,
alikuwa Picnic na wanae pamoja na marafiki zake wawili kandokando ya mto
Wisconsin, ambapo ndio aligundua mabaki ya mwili wa binadamu yaliyokuwa
yamefungwa kwenye mifuko ya nailoni ya kuhifadhia uchafu, maarufu kama mifuko
ya Rambo hapa nchini.
Baada ya uchunguzi zaidi
mwanamke huyo alikuja kugundua kuwa katika eneo lile ilikuwepo mifuko mingi
iliyokuwa na mabaki ya mwili wa binadamu ambao ulikuwa umekatwakatwa kinyama
utadhani nyama ya ng’ombe buchani. Polisi walifahamishwa kuhusu kupatikana kwa mabaki yale ya
mwili wa binadamu na walipofika kwenye eneo la tukio walichukuwa mabaki yote lakini
miguu haikupatikana, ili kwenda kuifanyia uchunguzi zaidi. Uchunguzi wa awali ulithibitisha kwamba yale mabaki yalikuwa
ni ya mwanamke mwenye asili ya Afrika ingawa hawakuweza kutambua sura yake
kutokana na kichwa chake kuchunwa ngozi yote kiasi cha kutotambulika.
Pamoja na wataalam wa maiti kuyachunguza kwa makini mabaki ya mwili ule, lakini
walishindwa kabisa kugundua sababu ya kifo cha mtu yule. Ili
kutambua kwamba mwili ule ni wa nani, ilibidi polisi waanze kuchunguza kesi
zaidi ya 2,000 za wanawake walioripotiwa kupotea katika jimbo la Wisconsin lakini hakuna mtu yeyote
aliyefananishwa na mabaki ya mwili ule.
Wakati mabaki yale yanapatikana
yalikuwa na siku tatu tangu kutupwa mtoni lakini iliwachukuwa polisi miezi sita
kutambua kwamba mwili ule ulikuwa ni wa nani. Na ili kuutambua mwili huo
ilibidi polisi waombe msaada kutoka kwenye kitengo maalum cha uchunguzi wa
kutumia teknolojia ya kisasa katika kutengeneza taswira kilichopo katika mji wa
Milwaukee.
MICHORO ILIYOTUMIKA KUMTAFUTA MWIVANO |
Polisi walituma picha za kichwa cha mwili ule
kwenye kitengo hicho, walizoiga kwa kutumia mashine maalum inayotumia compyuta
iitwayo Computer Tomography
Scan, maarufu kama TC Scan. Jopo la wataalam hao wakiongozwa na mtaalam wa
mafuvu ya bianadamu Profesa Robert Crockett walitenegeneza sura nne za mtu
mmoja zinazofanana.Muonekano wa sura hizo nne
ulipelekwa kwa wataalam wengine walioko katika jimbo la Kentucky ambapo waliiboresha na kuifanya ionekane ni ya
msichana aliyekuwa mionekano tofauti tofauti.
Muonekano wa kwanza ulikuwa wa
msichana aliyekuwa na nywele ndefu, wa pili ulikuwa ni wa msichana aliye na
nywele fupi, wa tatu aliyekuwa amefunga kitambaa kichwani na muonekano wa nne
ulikuwa ni wa msichana aliyevaa miwani, Mionekano yote minne ilikuwa imebeba
sura ya mtu mmoja.
Picha zile
zilisambazwa katika majimbo yote ya Marekani ili kuomba msaada kwa mtu yeyote
atakayeweza kumtambua mtu mwenye sura ile. Hazikupita siku nyingi mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina
la Shari Goss alikwenda kituo cha polisi na kuwajulisha kwamba zile picha
zilizosambazwa zinafanana kabisa na za msichana aitwae Mwivano Mwambashi
Kupaza, ambaye alikuwa ni binamu wa mume waliyetalikiana aitwae Peter Kupaza
mhamiaji kutoka Afrika Mashariki nchini Tanzania.
Alipoonyeshwa mabaki ya mwili
ule, mwanamke yule alizidi kuthibitisha kwamba hata ile mifuko iliyohifadhia
yale mabaki ya ule mwili ambayo ni ya duka moja maarufu liitwalo Woodman’s
Grocery. Ni duka ambalo Peter Kupaza alikuwa anafanyia manunuzi yake ya kila
siku na alikuwa na kawaida ya kuhifadhi ile mifuko.
Mnamo January
31, 2000,
polisi walikwenda katika eneo la Middleton kwenye majengo yaliyoko katika
barabara ya Pleasant View mahali alipopanga Peter Kupaza ili kumhoji. Kupaza
aliwaeleza Polisi kwamba Mwivano alirejea nyumbani nchini Tanzania tangu April 25, 1999.
Alisema ana
uhakika kwamba Mwivano alishafika nchini Tanzania baada ya kupiga simu nchini Tanzania na kuzungumza na baba yake Mwivano. Kupaza alizidi kuwaeleza Polisi kwamba
Mwivano alipanda basi kuelekea katika Jimbo la Iowa ambapo huko angekutana na mtu
aliyemtaja kwa jina la Shadrack ambaye wangesafiri pamoja kurejea nchini Tanzania. Kupaza alikiri kutofahamu ubini wa Shadrack na namna ya
kuwasiliana naye, kwani hakuwa na anuani yake na wala namba yake ya simu.
Aliendelea kuwaeleza
wapelelezi wa polisi kwamba kabla Mwivano hajaondoka nchini Marekani alikuwa
akiishi pale pale katika jiji la Madison, lakini katika eneo jingine akiishi
pamoja na rafiki zake wa Kikorea ambao alikuwa akisoma nao, na siku
alipoondoka, waliondoka pamoja kupitia katika jimbo la Iowa. Alieleza kwamba, siku Mwivano anaondoka alimpa kiasi cha dola
1,500 kama gharama za usafiri. Awali Kupaza
aliwaeleza polisi kwamba Mwivano hakuwahi kufika wala kuishi pale alipokuwa
akiishi, lakini baadaye katika mahojiano hayo Kupaza alikiri kwamba Mwivano
aliwahi kufika pale nyumbani kwake mara kwa mara.
Alipoonyeshwa zile picha
zilizotengenezwa, zenye taswira ya Mwivano ambazo ndizo zilizotambuliwa na
mwanamke waliyetalikiana naye, Kupaza alisema hamtambui mtu mwenye sura ile na
kwamba sura ile haifanani na ya Mwivano.Historia inaonyesha kwamba Peter Kupaza na Mwivano Mwambashi
Kupaza ni mtu na dada yake, kwa maana ya mtoto wa baba mkubwa na mdogo ambao
waliishi jirani huko kijijini kwao Usambaani, kabla ya Kupaza hajakutana na
aliyekuwa mkewe Shari Goss.
Shari Goss alikuwa ni mwanamke wa kizungu kutoka nchini Marekani
aliyekuwa akifanya kazi za Kimishenari kwenye miaka ya 1990, nchini Tanzania kabla ya kukutana na Peter Kupaza na
kuanza uhusiano. Baadae Peter
Kupaza na Shari Goss waliondoka nchini na kwenda kuishi nchini Marekani mwaka
1993, ambapo walifunga ndoa na kuishi pamoja kama mume na mke katika jimbo la Wisconsin kwenye mji wa Madison. Mnamo January 1997, Mwivano Mwambashi Kupaza alikwenda nchini Marekani na
kuungana na kaka yake Peter Kupaza pamoja na mkewe Shari Goss ambap waliishi pamoja.
Baadae Mwivano
alianza kusoma Kiingereza kwenye chuo kiitwacho Wisconsin English Collage, kilichopo katika mji wa Madison. Peter Kupaza na Shari Goss
walitalikiana katikati ya mwaka 1997 baada ya Kupaza kumbaka dada yake Mwivano
na kumpa ujauzito. Baada ya
kutengana Kupaza na Mwivano waliondoka kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi na Shari na kuhamia kwenye eneo lingine. Inasemekana Kupaza alimlazimisha Mwivano kutoa ule ujauzito kwenye kliniki
ya Madison ambapo kwa mujibu wa ushahidi
uliopatikana kutoka kwenye kliniki hiyo, Mwivano alifanikiwa kuutoa ujauzito
huo aliopewa na kaka yake.
Kwa mujibu wa ushahidi
uliokusanywa kutoka kwenye kliniki hiyo, ulionesha kwamba Mwivano alijaza fomu
maalum ya kutoa mimba sambamba na nakala kivuli (Photocopy) ya viza yake ya
kuingia nchini Marekani pamoja na nakala Kivuli nyingine ya leseni ya udereva
iliyotolewa katika Jimbo la Wisconsin. Taarifa
za kiuchunguzi kutoka kwenye maabara ya kuchunguza alama za vidole ilikuja
kuthibitisha kwamba alama za vidole zilizopatikana kwenye fomu za kliniki
ambayo Mwivano alitolea mimba zinafanana kabisa na alama za vidole zilizokutwa
kwenye mabaki ya mwili uliookotwa ambao ulikuja kuthibitishwa kwamba ni wa
Mwivano.
Baada ya Polisi kukusanya
ushahidi wote uliopatikana ikiwa ni pamoja na kumhoji Peter Kupaza, Polisi hao
walianza kupekua nyumba aliyokuwa akiishi Kupaza kwa kutumia mbwa maalum
waliokuwa wakimilikiwa na kampuni iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Canine Solutions International. Mbwa hao wakiwa wanaongozwa na mwanamama aitwae Sandra
Anderson waliweza kugundua mabaki ya damu iliyoganda kwenye ukuta wa choo
ambapo vipimo vya DNA vilikuja kuthibitisha kwamba damu ile ilikuwa ni ya
Mwivano.
Polisi pia
walikuta vitu ambavyo vilikuja kuthitishwa na Shari kuwa vilikuwa vikimilikiwa na Mwivano.
Vitu hivyo vilikuwa ni Biblia, saa ya mkononi, vito vya dhahabu na nguo, ikiwa
ni pamoja na mifuko ya plastiki inayofanana na ile iliyohifadhia mabaki ya
mwili wa Mwivano. Kutokana na ushahidi uliopatikana Peter Kupaza alitiwa
nguvuni kwa kutuhumiwa kumuuwa dada yake binamu Mwivano Mwambashi Kupaza. Mnamo
Juni 18, 2000, Peter Kupaza ambaye alikuwa akitetewa na Wakili aliyetajwa kwa
jina la Catherine alifikishwa katika mahakama ya Sauk County na kusomewa mashitaka ya kumuuwa dada yake
Mwivano Mwambashi Kupaza na kuukatakata mwili wake na kisha kuutupa katika mto
wa Wisconsin.
Mahakamani hapo walikuwepo pia wazazi wa Mwivano, ambao walisafiri
wakitokea nchini Tanzania ili kusikiliza shauri hilo. Baada ya kusomewa mashitaka hayo ya mauaji ya dada yake,
Kupaza alikanusha katakata kumuuwa dada yake, huku machozi yakimtoka alisema “Mwivano
ni dada yangu, Mwivano ni dada yangu wa damu, ni sehemu ya familia yangu, kamwe
sikumuuwa, ninakanusha kabisa kutenda kosa hilo”
Ukweli ni kwamba kesi hiyo
ilivuta hisia za watu wengi waishio katika mji wa Madisoni ikiwemo jamii ya
Watanzania waishio katika mji huo, hivyo mahakama ilikuwa ikifurika sana kila
siku kesi hii ilipokuwa ikisikilizwa na wahudhuriaji wengi walikuwa wakitokwa
na machozi kwa kuhuzunishwa na unyama aliotendewa Mwivano Kupaza binti mbichi
wa miaka 25.
Kesi hiyo ambayo iliendeshwa kwa kutegemea zaidi ushahidi wa
kimazingira, iliendelea kusikilizwa kwa upande wa mashitaka kuleta mashahidi
wake. Akitoa ushahidi wake pale mahakamani, aliyekuwa mke wa Peter Kupaza Bi
Shari Goss aliiambia mahakama hiyo kwamba Kupaza alipokwenda nchini Marekani
hakuwa na fedha za kujikimu na katika kipindi chote alichoishi naye hakuwahi
kuwa na kazi hadi mwaka 1997, Mwivano alipowasili nchini Marekani na kuishi nao.Shari aliendelea kusema kwamba kuanzia mwaka 1997 ndipo
kupaza alianza kufanya kazi.
Lakini
wafanyakazi wenzie walipohojiwa walisema kwamba Kupaza hakuwahi kuajiriwa bali
alikuwa kibarua wa kufanya kazi maalum( Part-time job) Hiyo ilikuwa ni katika
kukanusha madai ya Kupaza kwamba alimpa Mwivano kiasi cha dola zipatazo 1,500 kama nauli ya kurejea nchini Tanzania.
Alipoulizwa kwamba aliwezaje
kuweka akiba ya kiasi hicho cha fedha, wakati hakuwa na historia ya kuwa na
kipato kinachofikia kiasi hicho, Kupaza alisema kuwa fedha hizo alikuwa
akijiwekea kidogo kidogo nyumbani na sio benki.Hata hivyo kulikuwa na
wasi wasi mwingine, kwani mwaka 1998 baada ya kutalikiana na Shari Goss Kupaza
alishindwa kulipia gharama za gari alilokuwa amelikodisha kwa matumizi yake
binafsi. Inasemekana Kupaza alishindwa kulipia gharama za kukodi gari
kutokana na ukosefu wa fedha uliotokana na yeye kutokuwa na ajira ya kudumu.
Kutokana na sababu hiyo ya ukosefu wa ajira ya kudumu, Kupaza pia
alikosa hata fedha za kulipia gharama za talaka mahakamani. Katika fomu ya mahakama Kupaza aliandikisha Thamani zake zote , lakini
hakuandikisha kiasi chochote cha fedha alichoweka akiba nyumbani, ingawa
alimuandikisha Mwivano kama
mtegemezi wake katika fomu hiyo.
Akiendelea kutoa ushahidi wake
Shari aliielezea mahakama kuhusu tabia ya
unyanyasaji aliyokuwa nayo mumewe huyo mpaka wakatalikiana. Pia alielezea
historia ya Kupaza aliyokuwa nayo kijijini kwao huko Sambaani nchini Tanzania ya kupenda kuchinja mifugo waliyokuwa
nayo pale nyumbani kwao. Shari
aliongeza kusema, “Kupaza alikuwa na utaalam wa kutumia kisu kwa uhodari wa
hali ya juu wakati wa kuchinja mifugo.”
Pia alibainisha kuwa Kupaza alikuwa ni katili sana kwa wanyama. Naye baba wa marehemu
Mwivano, mzee Mwambashi Kupaza akitoa ushahidi wake, alisema kwamba hakuwahi
kuwasiliana na mwanae Mwivano tangu Juni 1998, na pia hakuwahi kuwasiliana na
Peter Kupaza kwa zaidi ya miaka miwili nyuma. Hata hivyo na yeye pia aliungana
na Shari Goss kuthibitisha kwamba Peter Kupaza
alikuwa anajua vizuri sana kutumia kisu wakati wa kuchinja mifugo kule kijijini
kwao ambapo mzee Mwambashi alikiri kwamba kuchinja mifugo wanayofuga pale
kijijini kwao ni sehemu ya mila na desturi zao.
Shahidi mwingine
aliyeitwa alikuwa ni Shadrack Msengi, ambaye alikuwa ni Mtanzania anaeishi
katika Jimbo la Iowa. Huyu ndiye aliyetajwa na Kupaza
kwamba, Mwivano alikwenda Iowa ili kuungana naye ili wasafiri pamoja
kurejea nchini Tanzania. Katika ushahidi wake, Shadrack Msengi
alikiri kuwafahamu Peter Kupaza na Mwivano ambao alisoma nao shule moja nchini Tanzania, lakini alikanusha kuwasiliana na
Mwivano tangu alipowasili nchini Marekani.
Pia Shadrack alisema kwamba
hakuona kama kulikuwa na sababu ya Mwivano kusafiri
kwenda Iowa kabla ya kusafiri kwenda nchini Tanzania. Shahidi mwingine binti wa Kitanzania aishiye nchini Marekani
aitwae Faith Mmanywa, rafiki wa karibu wa Kupaza ambaye nae kama Kupaza
alihamia nchini Marekani akitokea nchini Tanzania mwaka 1998, akitoa ushahhidi
wake alisema, mnamo Septemba 1999 (Baada ya mwili wa Mwivano kuwa
umeshapatikana lakini ukiwa bado haujatambuliwa) Kupaza alimpigia simu na
kumweleza kwamba Mwivano amesharudi nchini Tanzania na asingeweza kurejea
nchini Marekani tena.
Kupaza aliendelea kumweleza Bi
Mmanywa kwamba sababu ya yeye kumpigia simu ni kutaka kumjulisha kuwa Mwivano
amerejea nchini Tanzania na kwamba amemuachia jukumu zito la
kujiandaa kuoa siku yoyote. Jukumu lingine alilolieleza Kupaza ni lile la kumshawishi Bi
Mmanywa ahamie katika Jimbo la Wisconsin. Pia Kupaza alimjulisha Bi Mmanywa
kwamba, kwa mujibu wa taarifa alizopata kutoka nyumbani nchini Tanzania ni kwamba Mwivano alikuwa amejiunga na
shule ya uuguzi nchini Tanzania. Awali katika mahojiano na polisi,
Kupaza alisema kwamba ana uhakika mwivano yupo nchini Tanzania kwa sababu alipiga simu na kuongea na
baba yake Mwivano, kitu ambacho baba yake mwivano alikanusha pale mahakamani.
Alipoulizwa ni kwa nini
aliwadanganya polisi kuhusu kuthibitisha kwamba aliongea na baba yake mwivano
kwa simu na kujulishwa kuwa Mwivano yuko nchini Tanzania wakati haikuwa kweli? Akijibu swali hilo Kupaza alidai kwamba alilazimika
kuwadanganya polisi kwa sababu alihofia kuwa Mwivano angeshtakiwa kwa kuwepo
nchini Marekani kinyume cha sheria kwa sababu Viza yake ilikwisha muda wake.
Lakini hata
hivyo Kupaza alishindwa kutoa sababu ya kumdanganya Mmanywa kuhusu Mwivano
kurejea nchini Tanzania. Katika utetezi wake Kupaza alisema kuwa alimweleza Bi Mmanywa
kwamba Mwivano alikuwa ameomba na kukubaliwa kujiunga na chuo cha uuguzi nchini
Tanzania kabla hajaenda nchini Marekani na kwamba huenda angerejea nchini
Tanzania kujiunga na masomo ya uuguzi.
Lakini hata hivyo hakukanusha
madai ya Mmanywa kwamba yeye Kupaza alipata taarifa za Mwivano kuwa
ameshajiunga na Chuo cha uuguzi nchini Tanzania kutoka kwa baba yake Mwivano mzee
Mwambashi Kupaza. Shahidi mwingine aliyetoa ushahidi wake katika kesi hiyo ni
Brenda Dement, mama aliyeona mabaki ya mwili wa marehemu Mwivano kule mtoni.
Akiongozwa na mwendesha mashitaka Bi Rhoda Ricciard, Brenda alisema kwamba,
siku ya tukio alikwenda Picnic yeye na watoto wake watatu, pamoja na rafiki
zake wawili, ndipo walipogundua mabaki ya mwili wa binadamu yakiwa kwenye
mifuko ya takataka.
Hata hivyo Brenda alibainisha
kwamba katika eneo hilo alikuwepo mtu mmoja mweupe (Mzungu) aliyekadiriwa kuwa
na umri wa miaka 40 au anayekaribia miaka 50 ambaye alikuwa akirandaranda
katika eneo hilo, lakini akionekana kama mtu mwenye wasiwasi hivi. Baada ya wao kugundua kuwepo
kwa mabaki ya mwili wa binadamu katika eneo lile, mtu yule aliwafuata na
kuwashauri wawajulishe polisi.
Baadae mtu yule alitoweka
mahali pale akiwa ndani ya gari dogo jeupe aina ya Van, kabla ya polisi kufika
kwenye eneo la tukio. Huo ukawa ni utata mwingine, kwani Kupaza alikuwa ni
mwafrika mweusi. Hata hivyo mwanasheria wa Mahakama ya Sauk Patricia Barett,
aliukataa ushahidi ule unaohusu mtu mweupe (Mzungu) kuonekana katika eneo la tukio.
Lakini mwendesha
mashitaka Rhoda Ricciard alisema kwamba upande wa utetezi unaruhusiwa kuibua
ushahidi ambao huenda ukabainisha kwamba watu wengine walihusika na mauaji
yale. Katika utetezi wake mwingine Kupaza aliiambia mahakama kuwa haoni sababu
ya yeye kushitakiwa kwa kosa la kumuuwa dada yake Mwivano, kwa sababu wataalam
waliochunguza mwili wa marehemu wameshindwa kuthibitisha sababu za kifo cha
Mwivano.
Mnamo Juni 21, 2000 Jopo la
washauri wa mahakama ya Sauk walitumia takribani saa 9 kufanya majumuisho ya
ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashitaka vikiwemo vielelezo vya
mifuko iliyohifadhia mabaki ya mwili wa Mwivano na ule wa alama za vidole,
ambapo walikubaliana na upande wa mashitaka kwamba peter Kupaza alimuuwa dada
yake Mwivano Mwambashi Kupaza mnamo Julai 1999.
Katika majumuisho hayo jopo la washauri wa mahakama hiyo walizingatia
ushahidi ufuatao;Kielelezo cha kwanza
kinaonesha kwamba Kupaza alidanganya kwenye fomu yake ya kuomba kazi katika
kampuni nyingine mnamo Juni 1999, miezi miwili baada ya Mwivano kusemekana
ameondoka mjini Madison kuelekea Iowa, ambapo Kupaza alijaza jina la Mwivano
katika fomu hiyo akimtaja kama ni mtu ambaye kampuni inaweza kuwasiliana naye
iwapo itatokea dharura inayomhusu yeye Kupaza. Hata hivyo anuani ya mwivano
iliyojazwa kwenye fomu hizo ilikuwa siyo sahihi.
Taarifa hizo za kupaza, kwenye
fomu ya kuomba ajira zilichukuliwa na mahakama kama ni za uongo. Pili mabaki ya mwili wa
Mwivano yalikutwa kandoni mwa mto Wisconsin, ambapo inasemekana Kupaza anaufahamu
vizuri sana mto huo, kwani mfanyakazi mmoja
aliyekuwa akifanya kazi na Kupaza, aliieleza mahakama katika ushahidi wake
kwamba wakati fulani aliwahi kuzungumzia mto huo na Kupaza. Katika maelezo yake
mfanyakazi huyo alimnukuu Kupaza akiulezea mto huo kuwa ni mzuri sana lakini ni hatari pia.
Tatu mabaki ya mwili wa
Mwivano yalikuwa yamekatwakatwa kwa umahiri mkubwa na kulikuwa na muonekano
uliionesha kwamba aliyeukatakata mwili ule alikuwa na utaalam wa kufanya kazi
buchani, utaalam ambao inasemekana Kupaza anao kutokana na ushahidi uliotolewa
na Shari Goss pamoja na baba yake Mwivano mzee Mwambashi Kupaza kuwa Peter
kupaza alikuwa na uzoefu ya kuchinja wanyama kutokana na mazingira aliyokulia
kule kijijini kwao Sambaani nchini Tanzania ambapo tabia ya kujichinjia mifugo
majumbani ni jambo la kawaida.
Nne Kupaza alikuwa amejitengenezea kalenda yake mwenyewe ambapo alikuwa
amejipangia majukumu ambayo alikuwa ameyagawa kwa wiki. Katika kalenda hiyo kulikuwa na maneno matatu ambayo yaliandikwa kwa lugha
inayotumika nchini Tanzania, lakini hata hivyo Lugha hiyo
haikutajwa pale mahakamani.
Kalenda hiyo ilikuwa na neno “Bodo” neno ambalo lilitafsiriwa na baba yake
Mwivano, Mzee Mwambashi Kupaza baada ya kuombwa kufanya hivyo na mahakama, kuwa
lina maana ya kuangukia kitu au kuwa juu ya kitu ambacho kinaanguka.
Neno la pili lilikuwa ni “Mushingwa”Hili nalo lilitafsiriwa kama siku iliyotengwa (Chosen day) au siku maalum iliyotengwa
(Special chosen day)
Neno la mwisho lilikuwa ni “Fanya kazi”, neno hili liliandikwa kwa lugha ya
Kiswahili kama lilivyosomwa pale mahakamani. Maneno
yote hayo yaliandikwa katika kalenda hiyo yalidhihirisha kwamba Kupaza
alikuwana jambo la siri alilokuwa amelifanya na hakutaka mtu mwingine afahamu.
Kwa kujumuisha ushahidi wote
uliotolewa mahakamani hapo, mnamo Juni 23, 2000 , Peter Kupaza aliyekuwa na
umri wa miaka 40 wakati huo, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani na alipewa
uwezekano wa Parole akishatumikia kifungo cha miaka 31 gerezani na kuonesha
nidhamu katika kipindi chote atakachokuwa gerezani.
Baada ya hukumu ile kutolewa wazazi wa marehemu Mwivano waliridhia mtoto
wao mpendwa kuzikwa nchini marekani, ambapo mazishi yake yalifanyika Juni 21,
2000, siku ya Jumapili saa 8 mchana katika makaburi ya Westby ikiwa ni siku
moja baada ya Peter Kupaza kuhukumiwa na takribani mwaka mmoja tangu mwivano
alipouawa.
Katika mazishi hayo, kitengo
cha ulinzi wa amani (Sheriff Department) cha Sauk County kilipeleka kikosi cha askari wa heshima
ili mkuongoza mazishi hayo. Mara baada ya mazishi, Shari Goss ambaye ndiye aliyekuwa
mwenyeji wa wazazi wa marehemu Mwivano katika kipindi chote cha kesi ya Kupaza,
aliungana na waumini wa kanisa lake pamoja na wafanyakazi wa mahakama ya Sauk
County, kuwapa pole wazazi wa Mwivano ikiwa ni pamoja na kutoa fedha
walizochanga ili kuwapa wazazi hao kama rambi rambi zao.
Wazazi wa Mwivano walitoa
shukrani zao kwa watu wote waliowasaidia, tangu walipofika nchini Marekani
mpaka shauri la mtoto wao lilipokwisha, kisha wakarejea nchini Tanzania. Naye
Peter Kupaza kwa upande wake alikata rufaa ambayo ilitupwa mwaka 2003, na
kuamriwa aendelee kutumikia kifungo chake. Hata
hivyo mwaka mmoja baadae, yaani mwaka 2004, Peter Kupaza alikata rufaa nyingine
akituhumu ushahidi wa mbwa wa kunusa walioongozwa na mwanamama Sandra Anderson,
kuwa haukuwa ni wa kuaminika. Kwani
Sandra alikiri katika mahakama ya Michigan kwamba alipandikiza vielelezo vya
ushahidi katika kesi nyingine. Hivyo Kupaza alituhumu kwamba huenda na kwenye kesi yake
Sandra alipandikiza Vielelezo vya ushahidi pia.
Rufaa yake hiyo nayo ilitupwa
mnamo Mei 25, 2006.
MIMI HII KESI IMENIACHA HOI KWA KWELI..... i had to search and search seeeeearch huh!
CREDIT: MTAMBUZI,
JAMII FORUM
No comments:
Post a Comment