15
Wakati jua la alfajiri likichomoza Sindi Nalela alikuwa
shambani pamoja na mama yake. Kazi za kutifua ardhi ilikuwa ikiendelea kwa kasi
huku kila mmoja akiwa kimya na Sindi akionekana mwenye uso mzito uliojaa
mawazo.
Mama Sindi akasimama wima na kulisimamisha jembe mbele yake. Akamatazama Sindi alivyokuwa
akikazana kulima pasipo hata kupumzika.
‘Hivi lini mwanangu utaukubali kweli?’ akamsemesha Sindi
ambaye hakugeuka wala hakuonyesha ishara yoyote kuwa alikuwa amemsikia mama
yake
‘Sindi!’ Mama yake akamuita kwa sauti ya juu kidogo na Sindi
akapunguza taratibu kasi ya kulima na hatimaye akaacha kabisa na kusimama wima
naye akiegesha jembe mbele yake. hakumtazama mama yake usoni.
‘unajiumiza bure Sindi….umenuna tangu juzi huongei na mtu
ndani…. utadhani sisi ndio tuliopokea mahari…’ mama yake akamlalamikia
Sindi akashusha pumzi kwa nguvu kidogo kiasi cha mabega yake
kuonekanayakinyanyuka na kushuka, kisha akamgeukia mama yake
‘sijisikii kuzungumzia haya mambo..’ akajibu kwa mkato
akitupa jembe pembeni na kuchapua hatua ndefu ndefu kuufuata mti uliokuwa
umbali mfupi toka eneo la shamba. Akatandua khanga aliyokuwa ameitundika hapo
mtini kabla ya kuanza kulima na kujifunga kiunoni kisha akaokota ndala zake alizozivulia hapo na kuzibana kwapa la kushoto. Akashika njia na
kuondoka akimuacha mama yake anamsemesha kilugha kwa sauti ya kulaumu.
hakugeuka!
Alitembea taratibu akikwanyua vitawi kwa mkono wake wa kulia
na kuvirusha hewani. Alipolimaliza pori ,
akaona watu wakikimbia kuelekea uelekeo mmoja. Zile mbio ziliashiria tafrani
mahali.
Akasimama kwanza na kukodoa macho ya mshangao, naye akitamani
kukimbia pamoja nao na asijue kilichokuwa kinawakimbiza. Akatafuta wa kumuuliza
na asimuone kila mmoja alikuwa na haraka ya kufika uko walikokuwa wanakimbilia.
Sindi akanyoosha shingo na kutazama kule walikokuwa
wanaelekea watu. Hakuna cha kumstua pia. Akaaamua kuchanganya miguu kuufuata
ule uelekeo. Hata mbili tatu akamuona Alma
akitokea kule waliokuwepo watu na kuja huku walikotokea. Akafarijika!
‘kuna nini uko?’ akamuuliza Alma
alyeonekana kuwa na haraka kupitiliza
‘Twende kwanza..’ Alma
akamshika mkono na kumpigisha kona kali, sindi akaunga mchakamchaka usio rasmi
akiwa na Alma. Wakakimbia mpaka njia iliyokuwa inaelekea zahanati na Sindi
akasimama akihema na kuinama kushika magoti
‘Kuna nini kwanza?’ akauliza kwa ukali huku pumzi zilizotoka zikikosa
usawa na zile zilizoingia
‘Namfuata mama’ Alma
akajibu akijiandaa kuanza kukimbia tena pasipo kujali kama
Sindi angemfuata nyuma au lah.
‘ngoja kwanza…’ Sindi akamzuia ‘ kuna nini?’ akauliza akimeza mate kwa
juhudi kubwa kutokana na kule kuhema kulikombana.
‘Mama Nyanza ameanguka na kuzimia…’
‘Nini?’ Sindi akajikuta anasimama wima ghafla na kule kuhema
kukikata bila kutarajia
‘Mama nani…imekuwaje kwanza?’ Sindi sasa akamfuata Alma
kwa kasi pengine akitamani ambebe juu juu na kukimbia naye kuelekea uko
zahanati. Alma akampa ishara ya
kutulia kwanza na wakianza tena kukimbia kuifuata zahanati ambayo kwa pale
walipokuwa ilikuwa imebaki mara tatu ya
mwendo waliokwisha kimbia.
Mama Nyanza alikuwa katikati ya watu wakimpepea na wengine
wakisema awahishwe zahanati huku wengine wakitaka mama Alma
angojwe palepale kuepusha gharama kubwa ambazo hakuna hata mmoja aliyetaka
kuzibeba kwa wakati ule.
Uamuzi wa kumngoja mama Alma
ukapita na kukawa na hekaheka sasa ya kumpa huduma ya kwanza na watu wakiongea
hili na lile kuhusiana na kilichotokea. Wakati mama Nyanza akiwa chini ya
uangalizi wa majirani zake. Nyanza Mugilagila alikuwa mjini.
Ndani ya siku mbili alishapata mnunuzi wa kile kibanda cha
mama yake na kwa roho moja, alichukua hati ya kiwanja na kuondoka nayo
akimuachia mama yakenujumbe kuwa ameiuza nyumba na kiwanja kwa laki tisa na
kwamba laki tano angelipa mahari na zinazobaki angefanyia harusi na kwamba
angemjengea nyumba nyingine nzuri zaidi.
Mama Nyanza hakuamini alichokisoma asubuhi hii, alihisi
mchomo wa moyo, hamaki na hasira ndani yake. Alikuwa ameihangaikia hiyo nyumba
ya vyumba viwili kwa takribani miaka karibu sita. Akijinyima apate sehemu
ambayo angepaita kwake mara baada ya ndugu wa marehemu mumewe kumkatili kwa
kuzoa mali zote
alizotafuta na mumewe,
Leo hii Nyanza alikuwa ameitoa rehani sababu ya
mwanamke.Alikuwa ameipoteza nguvu yake kwa jambo ambalo kwake halikuwa na maana
yoyote. Pale alipokuwa amesimama aliona pakizunguka, ardhi ikinyanyuka na
kushuka. Akatoka nje akiyumba an akupaza sauti kumuita Nyanza japo alijua
hakuwepo pale wala karibu na pale.
Mama wa watu akaanguka nje ya fensi ya nyumba aliyokuwa
anaishi na kupoteza fahamu. Watu waliokuwa wakitoka shambani ndio waliomuona na
kumuondoa, wakimkimbiza kwa mwenyekiti kuomba msaada.
Mpaka mama Alma, nesi maarufu pale kijijini, alipofika na
kumkagua mama Nyanza, Sindi bado alikuwa hajajua kilichotokea. na kule mjini
Nyanza aliamua kulala na kuanza safri ya kurudi kijijini kesho yake.
Usiku wa siku ile, Nyanza alitulia nyumba ya kulala wageni,
akizitazama zile pesa kwa tabasamu. Laki tisa! kwake zilikuwa kama
milioni tisa taslimu. Alizifunga vizuri na kuziweka chini ya mto wa kulalia.
Akajikunyata kitandani, ndani ya shuka. Uso ukiwa na nuru ya matumaini pasipo
kujua balaa alilomletea mama yake.
888888888888888888888888
Wakati Nyanza akihisi ahueni moyoni usiku ule, Sindi alikuwa
na Maria pamoja na Alma chumbani wa
Sindi. Alma alikuwa amejilaza
kitandani kitandani miguu yake kuanzia magotini ikijikunja na kuchezeshwa
hewani, akiwa amelalia tumbo na kutumia viwiko vya mikono yake kujiinusha
kidogo juu akiwatazama Maria na Sindi waliokuwa wanasukana. Sindi alikuwa
kitandani na Maria alikuwa ameketi sakafuni, mabega yake yakipita katikati ya
miguu ya Sindi akisukwa.
‘Milioni mbili?’ Alma
aliuliza, Maria akageuza kichwa na
kumtazama sindi ambaye alijikuta akicheka kwanza.
‘Hamjasikia au hamjanielewa?’ Sindi akawauliza
‘kha! hebu kwanza…’ Maria akajigeuza mzima mzima na sasa
akawa anawatazama rafikize hawa wawili kwa awamu kisha akamgandishia Sindi
macho.
‘kwa hiyo mahari ya Mzee Dunia inarudishwa halafu?’ Alama akauliza kwa shauku
‘nataka nikakae mjini kwa muda mpaka hali itulie ndio
nitarudi’ Sindi akajieleza alakini ikawa kama vile
ametumia lugha isiyoeleweka
‘nini?’ Alma na
Maria wakauliza kwa pamoja kama watu walioambizana na Alma
akijiinusha na kuketi vizuri.
‘Jamani kipi msichoelewa?’ Sindi akawashangaa
‘Hapo pa kwenda mjini…hebu rudisha sinema nyuma kidogo tuone
vizuri….steringi anavyoenda mjini’ Maria akatania na kufanya wote watatu
wacheke na kugongesha viganja vyao.
Sindi akafanya utani wa kuchezesha vidole kama
mtu alieshika remote control ya tv na kufanya kicheko kizuke upya
‘Kwamba tukisharudisha mahari….hapa ndani hapatakalika si
ndio… kuna kubanwa hela umetoa wapi na nini na nini…. sasa mimi nitatrokea
mjini kwanza…’ Sindi akawa anajieleza huku wenzake wakimskiliza kwa makini mno.
Alma akadakia
‘Kuna mahali pa kufikia…sio mjini ukang’ae macho ste…’
hakumalizia
‘tulia nimalizie basi…’ Sindi naye akamdaka akamziba Alma
mdomo
‘….kuna mtu atanipokea na atanipa mahali pa kuishi mpaka hapo
Jerry atakapo kuja mjini’ akamalizia ana kuwatazama wenzake kwa awamu. Maria
akajikohoza kwa muda na kufanya wenzake waanze kucheka tena
‘Mmmh Nyanza anajua haya?’ Maria akauliza
‘ Ningemweleza saa ngapi na mtu ameondoka sijui hata yuko
wapi?’ Sindi akajitetea
‘…zaidi ya kujua atakubali tuuende mjini na Jerry wakati
walishachapana ngumi…we toroka zako kimya kimya shosti…ukisema umshirikishe
Nyanza balaa lake unalijua ’
Alma akatoa ushauri ambao hata
kabla hajaumalizia Maria alikuwa meshaukubali kiasi ya kunyoosha kiganja chake
hewani kuomba kugongewa tano na Alma.
‘Sadaktaaa….namuunga mikono na miguu’ Maria alinyanyua miguu
hewani na kuichanua. Sindi na Alma
wakacheka na Sindi akamchapa kibao miguu ili airudishe chini miguu yake.
‘Sasa akija akanikuta nimeishia atanielewaje?’ Sindi akaleta
wasiwasi wake
‘unajua anarudi lini…mtu hakukuaga…mtu hana hata senti ya
kumrudishia Mzee Dunia bado tu unamfikiria….mi mapenzi yenu haya ya moyo kwa
moyo siyawezi…dunia moyo mwenzake pesa’ Maria akamnanga Sindi
‘Utamwachia hata kiujumbe mradi tu usimtaje Jerry wa watu
tu…..vinginevyo utamuokota tena pori
lingine’ Alma akaonya akipiga piga
piga miguu yake kufukuza mbu.
‘ mmmh jamani…’ Sindi aliusitia ule ushauri
‘mmh nini sasa?.... halafu sasa huyu Jerry ndio inakuwaje
mkishasaidiana kuikimbia ndoa ya hii…. maana cha bure duniani pumzi tu….’ Maria
akata uhakika
‘nimeshakwambia tumepishana kuwa marafiki tu…ana wake na mimi
nina wangu jamani’ Sindi akatetea
‘Na ndio atoe milioni mbili za kukopa wapi sijui uko ili
amuokoe msichana na msichana huyo ni rafiki tu….hadithi za mitume bado zipo
duniani wallah….’
‘yetu macho….ila tu muombe sana
Mungu huyu kaka asikuuze madanguroni uko maana mwenzangu upeo wa macho yako
umeishi shinyanga mjini duka la pembejeo…huko Dar kuna maduka haswaa’ Alma
akamkoga shoga yake
‘We nawe ulifika lini dar ukayaona hayo maduka….’ maria
akamshushua
‘Umesahau nilienda kwenye harusi ya mama mdogo?’ akatamba Alma
‘Yaani kuingia mjini na Coaster la shinyanga basi ndio
mkazunguka mjini kote kuona maduka….’ Maria akamponda
‘Wivu tu….bora wenzio tumeosha hata macho duka la pembejeo….
we ukitoka mbali sana pale
zahanati’ Alma akarudisha dongo na
maria akasimama na kumvamia Alma
akimfinya na Alma akimvutia Sindi
kwake kujikinga na dhoruba za maria. Ukatawala utani wa kufinyana na kukingana,
wakasahau mjadala wao na mwisho wa siku wakalala pamoja pale chumbani kwa
Sindi.
88888888888888888888888
Sindi Nalela alishafanya uamuzi wa kuikimbia ndoa yake na
Mzee Dunia. asubuhi hii aliamkia kwa mama Nyanza, wakati huo Nyanza alikuwa
bado hajarejea
Hali ya mama Nyanza haikuwa njema hata kidogo. hakuwa na
nguvu za kunyanyuka, alionekana kama mtu aliyetaka
kupooza kuanzia kiunoni huku mwili ukimtetemeka. Sindi alipoingia kumtazama na
kumuachia barua ambayo alitaka imfikie Nyanza. Alishapata uhakika toka kwa
rafiki wa Nyanza kuwa angerejea siku hiyo na muda ambao angerejea, Mama Nyanza
alimtazama kwa jicho kali sana
‘Shikamoo mama’ akasalimia akipiga goti la heshima
‘Mchawi mkubwa wewe! …toka nyumbani kwangu…toka nje mchawi
wewe’ Mama Nyanza alimkaripia na Sindi akamtazama kwa huruma akitafuta maneno
ya kumwambia na kukosa.
‘ nina ujumbe wa Nyanza’ Sindi akamudu kusema shida yake
‘Binti!...naomba utoke’ Mama Nyanza alisema akitetemeka na
machozi yakimjaa macboni
‘Lakini mama….’
‘toka nje…’ Mama Nyanza alifoka tena akichukua kikombe cha
bai kilichokuwa karibu yake kumrushia Sindi, kwa hasira akahaha kutafuta
kingine cha kumrushia na kule kuhaha kukamfanya aanguke kama
mzigo toka pale kitandani alipokuwa amelala. Hakuwa na uwezo wa kunyanyuka na Sindi aliachama kwa mshangao baada ya
kugundua hali ya mama Nyanza.
Akamkimbilia ili amanyanyue lakini mama nyanza alimnasa vibao
na kumtaka asimguse na ishie zake. Akamrushia maneno ya ghadhabu na kumtukana
kwa hasira kiasi cha Sindi kuona asingeeleweka hata kidogo. Akaiweka bahasha
ile juu ya meza huku machozi yakimtoka.
‘Mama angalau nifikishie huu ujumbe kwa Nyanza…nakuomba mama’
aliongea huku akipokea matusi toka kwa Mama Nyanza ambaye bado alikuwa pale
chini akiongea huku machozi yakimtoka.
Sindi akaondoka pale ndani akilia, akaenda kuonana na Jerry
kule anakofundishia ambako ndiko alikopewa pesa za safari pamoja na za mahari.
Sindi akarudi kwao na kuziweka zile fedha kwenye mfuko pamoja na barua ndani.
akaviweka mahali ambapo lazimababa yake angepagusa. Kwenye kabati lenye redio.
Huku nyuma Nyanza alirejea nyumbani lakini hali aliyomkuta
nayo mama yake ilimuacha hoi, ilimharibia furaha yake. Akalia sana
akimtaka mama yake anyanyuke na kutembea. Mama yake alikuwa kimya pasipo
kumsemesha, alikuwa akimtazama tu pasipo hata kumkaripia. Machozi yake
yaliongea kuhusu hasira zake na hali yake wakati ule. ile Barua aliyoiacha
Sindi ilikuwa chini yam to wa kulalia aliokuwa ameuegemea mama Nyanza. hakuwa
ameifungua ila barua, aliamua tu kutompatia Nyanza kwa hasira alizokuwa nayo
ndani ya ile barua kulikuwa na ujumbe…
Mpenzi wangu Nyanza,
naomba upatapo ujumbe huu uje haraka kilimamoto kule
porini, nina mengi ya kukwambia na kukueleza. Kwa wazazi wangu nimetoroka ila
kwako siwezi, nataka kukuaga, nataka kukwambia nitakuwa wapi na unifuate vipi,
nataka kukuachia hata pesa kidogo za chakula na kumsaidia mama. Imebidi
niondoke kuikwepa ndoa ambayo ingetutenganisha milele. Nakupenda sana
sana sana
sana na nimefanya
hivi kwa ajili yako kwani najua huna uwezo wa kumrudishia Mzee Dunia mahari
yake.
Nitakusubiri!
Wako
Sindi
Nalela
Sindi na wenzake walimsubiri Nyanza mno. Mpaka giza
lilikaribia kuingia. nyanza hakutokea. Sindi aliketi chini akilia, alilia sana
na kuwapa marafiki zake kazi ya kumbembeleza. Akaagana nao huku nao wakilia.
Akatembea akielekea pori dogo
ambalo angelivuka na kungoja usafiri. aligeuka mara kadhaa kuwatazama rafiki
zake ambao walikuwa wamesimama wakilia na kumtazama anavyoshia.
Walipogeuka na kuanza kuondoka Sindi naye aligeuka na
kujitahidi kuondoka bila kuangalia nyuma.
Sindi akatoroka kijijini kwao! Nyanza akiwa hana taarifa
zozote. Akawa anajipanga kuamkia kwa Mzee Nalela kupinga ndoa ya Sindi na
kurudisha mahari ya Sindi iliyotolewa na Mzee Dunia. Asijue kilichokuwa
kinatokea uko kwa Mzee Nalela kwa wakati huo
…… ITAKUWAJE?.....ENDELEA KUFUATILIA!! NIPE MAONI YAKO
No comments:
Post a Comment