16
Taarifa za kutoweka kwa Sindi zilisambaa kama
upepo wa kimbunga. Nyumbani kwa Mzee Nalela kulikuwa na hekaheka kubwa. Watu
walikuwa wakijazana kila dakika iliyokatika. Kulikuwa na hekaheka ya kutosha
muda huo wa saa nne usiku.
Wakati haya yote yakitokea Nyanza alikuwa chumbani kwake
akiwa amepitiwa na usingizi baada ya kikao kirefu na mama yake na wakishindwa
kufikia muafaka na kuelewana.
Saa sita na vichapo
kadhaa, Nyanza alikurupushwa usingizini na kishindo cha hali ya juu. Aliinuka
na kuketi kitandani akitega masikio kwa bidii na kujaribu kuiweka akili yake
sawa.
Maruweruwe ya usingizi bado yalikuwa yamemganda kichwani
wakati alipoona mwanga mkali wa tochi mbili au zaidi vikipishana katika namna
ya kusaka kumulika kitu wakati huo huo sauti ya mama yake ikisikika.
Akachanganyikiwa!
‘Yuko wapi?...’ kikasikika kibao Pah! ‘...sema upesi’ sauti
ya kuamrisha iliyoenda sambamba na mlio wa kibao kingine ukasikika tena. Nyanza
akajiinusha haraka na kukwanyua T shirt iliyokuwa imetundikwa kwenye msumari
ukutani. Akatoka huku akiwa anaivaa na wakati huo huo akigongana na watu wawili
walioonekana kutoka chumba kilichotumika kama ghala yao
na kuja kule alikokuwa.
Akataka kuwauliza walichokuwa wanakifanya mule ndani lakini
hakuipata nafasi hiyo. Wale watu wawili ambao baadaye alikuja kuwatambua kama
polisi walimvamia na kumtandika virungu mwilini wakimkwida kama
mwizi na kumtoa nje.
Kwa namna alivyokuwa akishambuliwa kwa kipigo Nyanza hakupata
hata nafasi ya kuinua uso kumtazama mama yake aliyekuwa analia na kuomba
mwanawe aachiwe kwa kuwa hana hatia. Pale nje walimtandika vya kutosha kisha
wakampigisha magoti, mikono yake ikikutana nyuma ya shingo kama
mateka. alikuwa hoi, akivuja damu kama mhalifu.
Kulikuwa na giza
lakini mwanga wa mbalamwezi ulikuwa mkubwa wakutosha kumuona Mzee Dunia
akipishwa na polisi wakati akimkaribia pale alipokuwa amepiga magoti. Mzee
Dunia akamuinua uso kwa kukinyanyua kidevu chake kwa fimbo ya kutembelea
aliyopenda kutembea nayo mkononi.
‘kijana…. sidhani kama nahitaji
kutumia nguvu zaidi ya hii niliyotumia….ukinipa ushirikiano sekunde moja tangu
sasa utakuwa huru…’ Mzee Dunia aliongea kwa kituo, kwa hatua akimpa nafasi
Nyanza amuelewe kama alivyotaka kueleweka lakini Nyanza
ahakumuelewa!
‘Nimekosa nini?’ Nyanza akauliza akihema, meno yake yakiwa na
rangi nyekundu kutokana na damu iliyokuwa inamtoka mdomoni sababu ya kipigo.
‘Sindi yuko wapi?’ Mzee Dunia akauliza kwa upole kama
mzazi anayemuuliza mwanawe ni wapi alipoiweka kalamu yake.
‘Sindi?..yuko wapi?....unamaanisha nini?’ Nyanza alitoa amcho
kwa taharuki ya ghafla akiwa hajamuelewa Mzee Dunia ambaye alifumba macho na
kutabasamu kwa sekunde kadhaa na alipofumbua, alimtandika Nyanza kofi kali la
shavuni lililompepesusha Nyanza na kumdondosha chini, yowe kubwa likimtoka na
kumfanya mama yake alie kule ndani na kuwasihi wampige yeye sio kijana wake.
Wale askari wakamnyanyua Nyanza na kumpigisha tena magoti kama
mwanzo.
‘Narudia tena Sindi yuko wapi?.....usidhani nimeacha shughuli
zangu kuja kukubembeleza kijana…..wala sikuharibu mafuta yangu mpaka mjini
kuchukua polisi kuja kukubembeleza mtoto….najua alikuwa msichana wako na
nilishakuona naye…. usinichezee akili…Sindi yuko wapi?’ Mzee Dunia akalirudia
lile swali ambalo sit u lilimchanganya Nyanza bali pia lilimuongezea maswali
ambayo kwa wakati ule yalikosa majibu kabisa sembuse jiu la kumpa Mzee Dunia.
Kushindwa kule kujibu na kubaki kimya akiwa amehamanika
vibaya mno, kulimfanya Mzee Dunia awape ishara wale polisi ya kumpakiza Nyanza
kwenye gari walilokuja nalo. Wakati wakimnyanyua mama Nyanza alishasota kwa
magoti mpaka mlangoni akijaribu kuvuka kizingiti cha mlango huku akilia na
kupiga mayowe kijana wake aachiwe.
Nyanza alilia kama mtoto sio kwa
maumivu ya kipigo aliyokuwa nayo bali kwa ile hali ya mama yake aliyoisababisha
na kabla hajarekebisha alikuwa katika sakata ambalo hakujua hata lilipoanzia.
Nyanza akachoropoka mikononi mwa polisi na kumkimbilia mama
yake. Watu waliokuwa wamesimama mbali na eneo lile walisikitika, wanawake
walilia na wengine walitazama pembeni kwa huzuni wakichelea kuona namna Nyanza
alivyokuwa akipigwa kama Nyoka wakati askari wale
walipokuwa wakimtenganisha na mama yake.
Mama na mwanawe walikumbatiana kwa nguvu zaidi wakati polisi
wakiwaachanisha kwa kipigo.
‘Wataniua mama…wataniua’ Nyanza alilia kama
mtoto mdogo aliyehitaji ulinzi wa mama yake, alilia kwa hofu. Wakati wakizidi
kukumbatiana kwa nguvu askari mmoja alimpiga mama Nyanza kichwani kwa kirungu
chake.
Kipigo kile kilimteteresha mama Nyanza na taratibu akaachiana
na mwanawe a kulegea kurudi ardhini. Nyanza akaburuzwa kama gunia huku akilia na kumuita mama yake ambaye
aliangua chini na kutulia pasipo kutikisika.
Akapandishwa kwenye gari la polisi huku akiendelea kupigwa
naye akipiga makelele kumuita mama yake. Gari la polisi likaondoka likifuatiwa
na gari la Mzee Dunia. Watu waliokuwa
wamesimama mbali wakakimbizana kumuwahi mama Nyanza pale chini.
Watu walikuwa wamesimama makundi makundi kila mmoja akiongea
lake. Wapo waliojifanya kuujua ukweli na wapo ambao walihangaika kuujua ukweli
ila walioujua ukweli halisi walikuwa wamesimama pamoja. Jitimai ikiwa imewatembelea!
Mchezo walioucheza ulikuwa umeleta matokeo tofauti na waliyotegemea. Mpunga
waliolima ulichipusha mchicha!
Jerry Agapela, Alma
na Maria walikuwa wamesimama kama wafu, wakilitazama
gari la polisi lilivyokuwa likiishia huku polisi wakiwa wamekanyaga Nyanza pale
kwenye gari alipokuwa amelala kwa kujikunyata.
Jerry aliumia sana ,
alikuwa anajua kila kitu, alikuwa anajua alipo Sindi Nalela, ilikuwa kama
vile yeye ndiye aliyeleta sakata lote lile.
888888888888888888888
Asubuhi ya saa mbili na nusu, Sindi alikuwa stendi ya mabasi
akingoja basi la Allys katika eneo la kukatia tiketi za basi hilo .
Mkatisha tiketi alishafahamishwa kuhusu Sindi na alishamfahamisha atakaye
mpokea uko Dar kuwa Sindi angekuja na basi lipi la Allys.
Masaa machache baadaye Basi la Allys lilikuwa likiiacha
Shinyanga na kuanza kuitafuta Tabora. Sindi alikuwa ameketi dirishani, akiwa
amekilaza kichwa chake kwenye kioo cha dirisha. Mikononi mwake akiwa
amekumbatia mfuko uliokuwa na nguo zake. Alionekana kuzama mbali sana
kimawazo. Roho ilimuuma sana kwa
Nyanza kutoukubali wito wake.
Alikuwa akiweweseka kimoyomoyo na kushindwa kuelewa ni kipi
hakikueleweka kwa Nyanza hadi asifike kugana naye. Kuna wakati alihisi
kumasirikia na kumlaani kwa ujeuri wake. Hakujua tu, dhoruba iliyokuwa imemkumba
Nyanza sababu yake!
Sindi alisafiri salama na kuingia Dar saa mbili usiku. Pamoja
na giza lile Sindi alishangaa wingi
wa magari na watu mara tu walipoikaribia ubungo. Alikuwa akiangaza angaza huku
na kule akionekana kuifurahia mandhari ya Dar aliyokuwa akiisikia miaka mingi
tu.
Basi lilipoingia kituoni na kusimama, abiaria walianza
kushuka, madereva taksi nao wakijazana mlangoni mwa basi kuwahi wateja huku
ndugu na jamaa nao wakitaka kuwalaki ndugu zao. Sindi aliteremka kwenye basi
kwa tahadhari, akafanya kazi ya ziada kubenjua bega lake la kulia kukataa kule
kuguswa guswa na madereva taksi ambao wengine walimpa nafasi na wengine
walizidi kumuandama sasa.
‘Sitaki!’ Sindi alijibu kwa ukali, mtu mmoja alipotaka
kumpokea kile kifurushi cha nguo zake. Akajitoa mbali na basi lile na kusimama
akiangaza angaza lakini ghafla akamuona mtu akimjia pale alipokuwa amesimama
huku akitabasamu na kuchezesha funguo mkononi. Sindi hakutabasamu, alimkazia
macho yule mtu mpaka alipomkaribia.
‘Hujambo Sindi?’ Meddy Hakim, rafiki wa Jerry alimsabahi
Sindi ambaye aliposikia jina lake likitajwa
akajua huyu ndiye aliyekuwa mwenyeji wake
‘Shikamoo’ akasalimia na kupiga goti la kugusa sakafu.
Madereva taksi na makuli kadhaa waliokuwa eneo lile waliwatupia macho huku
wengine wakimtania Meddy
‘Kaka mali
ya wapi hiyo?...kaka umeona ulete toka kijijini kabisaa…. wacha weee’ makelele
yalisikika na Meddy alijikuta akicheka na kutikisa kichwa. Akataka kumpokea
kile kimfuko chake cha nguo
‘hapana asante ’
akajibu akipiga tena goti
Meddy akamuonyesha mahali alipokuwa amepaki gari ambalo
lilikuwa taksi iliyoandika Ilala ubavuni. Wakati wakitembea Sindi akashangaa
kumuona mwanamke mnene aliyekuwa akipita kando yake na kikaptura kifupi
kilichoacha sehemu kubwa ya mapaja yake nje. Sindi akaachama mdomo na kushangaa
waziwazi. kule kushangaa kulimfanya asione mwisho tofali lililokuwa mbele yake.
Akajikwaa almanusura aanguke.
Meddy alitaka kucheka lakini akajizuia na kumpa pole Sindi
ambaye aliona aibu hata kuipokea. Wakaondoka pale na kuelekea Sinza kwa Remmy.
Akakaribishwa kwenye chumba kilichokuwa kama
sebule na hapo hapo kukiwa na kitanda. Meddy Hakim akampa ufunguo wa chumba na
pesa kadhaa. akmataka amngoje kidogo. Meddy akatoka.
Sindi aliangaza angaza huku na kule na akishangaa vitu vya
mule ndani ikiwemo zulia zuri la kuvutia. Akajiweka sawa aliposikia mlango
ukifunguliwa na Meddy akitangulia akiwa amefuatana na msichana mwingine wa rika
lake.
‘mgeni mwenyewe huyu hapa anaiwa Sindi Nalela’ Meddy
akamtambulisha
‘Anhaa…karibu anti’ yule dada akaitikia akimpa mkono Sindi
ambaye aliupokea na kubonyea chini kwa adabu kiasi cha kumfanya yule dada
atabasamu zaidi
‘Sindi…huyu ndio atakuwa mwenyeji wako kwa kipindi
hiki…anaitwa Jamila’ MEddy akamtambulisha Jamila kwa Sindi
‘Asante …nashukuru
kukufahamu’ Sindi akajibu kwa aibu kidogo
yakafuatia maongezi madogo madogo kati ya Jamila na Meddy
kisha MEddy akaaga na kuondoka zake akimuacha Jamila pale ndani.
‘Ngoja nikuletee chakula…kama unataka
kuoga kuna bafu nje….maji tunachota kwenye kisima nyuma nitakuonyesha kesho….ila jiandae ukaoge ngoja
nikuwekee maji’ jamila akamsemesha kisha akatoka na Sindi akabaki mwenyewe
akikitazama hiki chumba mara mbilimbili. Kwake kilikuwa chumba kizuri mno
kulinganisha na alikotoka.
Akaoga, akala, akalala, siku yake ikawa imeshia hapo huku
kule kijijini hali ikiwa tete siku nzima. Alma
na Maria wakiogopa hata kujadiliana kuhusu Sindi. Waliogopa mno kuunganishwa na
Nyanza katika kesi ile. Mzee Dunia alikuwa amegoma kuupokea pesa zake za
mahari, yeye alimtaka Sindi tu!
Mzee Nalela aliziona pesa alizoachiwa na Sindi na maelezo
kuwa zilikuwa fidia ya mahari. Hakujua alikozitoa mwanaye lakini alipozitoa kwa
Mzee Dunia zilikataliwa. Mzee Dunia akidai pesa ile isingefidia aibu
aliyompatia mpaka dakika ile.
Mama Sindi na wanawe walishafukuzwa pale kwao na walikuwa
wanajisitiri kwa rafiki wa Mzee Nalela. Waliambiwa wasikanyage pale mpaka Sindi
apatikane. Sindi alikuwa ameacha zahma
ya kutosha kwa kila mtu!
8888888888888888888
Kuna kitu kilikuwa kimetokea pale kijijini, kitu kikubwa sana
ambacho kilikuwa kinamsubiri Nyanza aachiwe hata kwa dhamana. Wiki mbili baada
ya kukamatwa, Nyanza aliachiwa kwa masharti. Huku akichechemea alirudishwa
kijijini na kuachwa mbele ya nyumba yao .
Nyanza aliuhisi ukimya uliokuwa umeitembelea nyumba yao .
Alitembea kwa taabu na kuingia uani huku akiangaza huku na kule. Muda huo wa
saa mbili asubuhi wanakijiji wengi walikuwa mashambani wakilima. Wakati
akiukaribia mlango wa kuingilia ndani mdogo wake Nyanza alitoka na kukimbilia
kaka yake, akamkumbatia na kulia kwanza.
‘Mama yuko wapi?’ Nyanza akauliza lakini mdogo wake hakujibu
kitu. Alilia kwa kwikwi pasipo kusema chochote. Nyanza akaachana na mdogo wake
na kuingia ndani haraka. Alimsaka mama yake huku na kule na asimuone. Akarudi
nje pale alipomuacha mdogo wake.
‘Mama yuko wapi?’ akarudia swali lake, mwili ukimtetemeka.
Mdogo wake alimtazama tu akitiririkwa na machozi huku akianza kutembea kuondoka
pale uani na kutoka nje. Nyanza akawa anamfuata kama
kivuli, wakaiacha nyumba yao na
kushika njia iliyokuwa inaelekea makaburini. Nyanza akahisi kichwa kikiwa na
uzito wa dunia.
‘Pale…’ akamuonyesha tuta kubwa lililokuwa na msalaba wa mti.
Nyanza akatulia tu akilitazama lile tuta. Hakulia wala kuongea alisimama pale
pale akilitazama lile tuta ambalo ndilo lilikuwa kaburi la mama yake.
Akatembea taratibu mpaka kwenye lile kaburi, akapga magoti
mbele yake na kutulia akilitazama kama mtu asiyeamini
kile alichokuwa anakitazama. Mikono ilikuwa inamtetemeka kadiri alivyokuwa
analitazama lile kaburi huku mboni za macho yake zikielekea katika maji.
Akafumba macho na kuruhusu mtiririko wa machozi.
Sindi alikuwa ameondoka maishani mwake na asijue alipo,
alikuwa amepigwa vya kutosha na kuzuiwa kumuona mtu yoyote ndani ya wiki mbili,
anaporudi nyumbani anakuta mama yake amelala usingizi wa mauti, pasipo
kumtimizia ahadi ya nyumba mpya, pasipo hata kumzika. Nyanza alilia, alilia,
alilia mno lakini machozi yale hayaubadili ukweli uliokuwa mbele yake…..
Wakati akilia na kuomboleza, mdogo wake alimpatia ile bahasha
aliyoikuta kwenye mtonwa kulalia wa mama yake. Nyanza akaifungua na kuisoma
huku akiilowanisha na machozi. Uchungu ulimshika maradufu. akanyanyuka na
kushika njia kuelekea kule kilima moto ambako alipaswa kuonana na Sindi. Kama
mwehu akazunguka eneo lile akiliita jina Sindi kwa kupayuka. Nyanza alikuwa
amechanganyikiwa!
JE NINI KITAFUATA?....JERRY YUPO AU NAYE AMETIMKIA MJINI?....
No comments:
Post a Comment