Mpo wasomaji wangu?
Haya tunaendelea na mapya ya mwaka
mpya… kila jumatano tutakuwa na kipengele cha MEKONI… meko kwa Kiswahili ni
jikoni na kama nilivyoahidi kulete burudani mbalimbali basi kila jumatano
tukutane kwenye safu hii ya Mekoni.
Ukaangaji nyama unasumbua watu wengi tu. Wapo wasiojua kabisaaaa na wapo wanaojitahidi
hapa na pale lakini ndio nyama inatoka ngumuuu kama kipande cha jiwe Lol… wapo
pia mafundi wa kukaanga na akikukaangia lazima ulambe sahani… twende kazi sasa!
Mwaka huu usipijua kupika vizuri baaasi tena!
Ukaangaji nyama hauna kanuni moja. Zipo kanuni nyingi tu za
kukaanga nyama na ikatoka poa kabisa, laini na tamu. Mi nakuletea njia mojawapo.
MAHITAJI... itategemea na kiasi unachotaka kupika
- Nyama
- Kitunguu swaumu
- Kitunguu maji
- Tangawizi... menya na uitwange, au isugue iwe laini
- Limao/ ndimu/ vinegar
- Chumvi
- Binzari ya pilau/ binzari masala/ curry powder/ meat masala na vingine unavyopenda
- Pilipili manga
- Mafuta kiasi cha kutosha
JINSI YA KUKAANGA
1. Osha na katakata nyama yako katika vipande vyenye ukubwa unaotaka
2. Weka nyama yako kwenye chombo safi kisha tia Limao/ ndimu au vinegar. Chagua kimojawapo. Weka vitunguu swaumu ulivyotwanga na uchanganye na nyama vizuri.
Weka viungo vyako unavyotumia, iwe binzari ya pilau, binzari masala, chichen masala, royco au kiungo chochote unacoaka kutumia kuleta ladha murua...mimi hutumia Binzari masala. nyunyuzi pilipili manga kidogo sana kama hupendi ladha ya pilipili kisha tia chumvi!
Changanya vizuri kuhakikisha nyama imechanganyikana na viungo vyako barabara
3. Hatua hii inayofuata si muhimu sana ila wapo wanaoipitia....watu huweka tomato sauce, au nyanya za kopo kwenye mchanganyiko. Kisha weka kwenye friji kwa dakika 40... kuweka nyama kwenye friji kwanza husaidia viungo vyako kuingia vyema kwenye nyama na pia hulainisha nyama. hii ni moja ya njia za kufanya nyama itoke lainiiii.... unaweza kuitumia hata katika ukaangaji kuku.
4. Baada ya dakika 40 kupita toa nyama yako kwenye friji na ubandike sufuria lenye mafuta kiasi kukaangia nyama yako. usiweke mengi sana!
5. Mafuta yakishapata moto.... kuwa makini kidogo mafuta yasipate moto saaaana kiasi kwamba ukiweka nyama zinacharuka, dakika mbili zinaungua huku hazijaiva
6. Mafuta yakipata moto tia vitunguu vyako, vikaange kidogo kisha tia nyama yako geuza geuza kwa muda kisha funika. mvuke unaotokana na kufunika unaivisha nyama vizuri sana. igeuze geuze mara kwa mara ili kuepusha kushika chini. na kama inashika sana unaweka maji kidoooogo kisha unafunika.
unaweza ongeza mafuta kwa kadiri ya wingi wa nyama yako
7. Kama utapenda wakati inakaribia kuiva katia karoti na pilipili hoho hoho kubwa kubwa ukichanganya hoho nyekundu na kijani inapendeza sana na ugeuze geuze mara kwa mara.
utaona kama mafuta yanaishia hivi na nyama inaanza kushika kwenye sifuria. cheki nyama yako kama imeiva kama bado ongeza tena maji kidogo sana. usimimine puuuuuu anhaaa! utaharibu pishi lote halafu uje unisingizie sikukuelekeza vizuri hahahahaaa
nyama itajikaanga mpaka ubaki wewe na sufuria na mwiko...bila maji na mafuta kidogo
Ipua nyama yako uichuje kwenye chujio mafuta yadondoke.
Baada ya yote hayo mlo wako unakuwa tayari.... ulie kwa chipsi...ulie kwa pilau...ulie kwa ugali yote heri!
Nimeelewekaaaa?!
asante kwasomo zur miss😚
ReplyDeletemapishi ya nguruwe lini dada
ReplyDeleteOkay
ReplyDelete