Thursday, May 23, 2013

SINDI.....NA LAURA PETTIE (17)

17

‘Look at my new baby out there …. surely can’t get it enough’ Pamela aliongea kwa mbwembwe, akizungusha macho yake kwa madaha  na kutembea kwa mikogo akifuatisha midundo ya muziki iliyokuwa ikisikika wakati akiingia ndani ya nyumba ya Meddy Hakim, Kunduchi. Meddy alitabasamu na kuchungulia nje kulitazama vizuri hilo gari jipya la Pamela aina ya Verossa. Akafunga mlango na kumgeukia Pamela ambaye alishutupia mkoba kwenye kochi na kuifuata meza ya vinywaji. Akajimiminia whisky kidogo na kurudi kuketi kwenye kochi lile lile alilotupia mkoba wake, akibebebsha mguu juu ya mguu.



‘Another gift?...’ Meddy akauliza akisonta dole gumba nyuma kuashiria kuzungumzia gari la Pamela.
‘You wish!…. zimenitoka milioni hizi…’ akachanua vidole vyake vyote kumi na kuviweka hewani. akamalizia ‘ Cash!’
‘wow!...and that is my girl’Meddy akaongea akitabasamu na kumsonta Pamela kwa kidole cha shahada pekee. Pamela akacheka na Meddy akatembea taratibu kwenda kupunguza sauti ya muziki uliokuwa unasikika toka kwenye luninga.

Akaipunguza sauti ya muziki kiasi cha kukaribia kutosikika, kisha akaketi kochi lingine mbele ya Pamela
‘na msichana ameshaletwa?’ Pamela akauliza kwanza kabla ya kuipeleka glasi ya whisky yake kinywani
‘na sehemu ya kuishi amepewa’  Meddy alijibu akijirudisha nyuma na kuulaza mgongo wake sofani, mikono ikinyanyuka juu na kulala kwenye ukingo wa juu wa sofa, miguu ikikunja nne.

Pamela akabweua kwanza, uso ukionekana kujaa mshangao
‘Unajua sijamuelewa Jerry… wakati bado hata hajasolve inshu yake na familia yake…anajiongezea majukumu mengine ya ajabu ajabu’ Pamela aliongea kwa mtindo wa kulalamika
‘Labda amempenda yule msichana…’ Meddy akatoa wazo na Pamela kidogo apaliwe na ile whisky aliyoikimbizia mdomoni

‘Whaat!....Jerry Agapela?...huyu huyu Jerry?’ Pamela akafanya kudhihaki kidogo
‘Yeah… huyu huyu… kwanini  ashindwe kumpenda?.... yule binti mzuri sana….ni kukosa matunzo tu ndio kumemfubaisha’ Meddy akatetea hoja yake

‘Not the Jerry Agapela I know….kama ni uzuri angeshamchukua Clarita yule rafiki wa mdogo wake…. yule dada ni mwisho….namzidi kila kitu kuanzia elimu mpaka pesa lakini kuongozana naye tu lazima ujisikie insecure….’
‘Clarita mzuri ndio lakini Sindi ni ana mvuto wa kipekee akiwa amechakaa tu yuko hivi…je akioga akatakata?’ Meddy aliuliza akicheka

‘Nakuhakikishia hakuna kitu mapenzi pale…..kutakuwa na kitu kingine sio mapenzi kabisa’ kwa kujiamini Pamela akambishia Meddy
‘au…au kwa vile he is into you?’ Meddy akamtega Pamela
‘Come on! ni zaidi ya hilo…..namjua Jerry vizuri mno and I’m sure mpaka nikiolewa mimi ndio Jerry ataoa…. yaani kaniachia mwili na roho wengine wote anawaona takataka tu… labda nikishaolewa ndio moyo wake utaamua kupenda tena’ Pamela akaongea kwa tambo za kike.

Meddy akacheka na kutazama stuli ndogo iliyokuwa kando yake, ambayo ilikuwa na simu yake. Akakaza macho na kuitumbulia macho ile simu iliyotoa mwanga kuashiria kuita kwa simu.
Akaisogelea stuli na kuikwanyua ile simu. Akaipokea na kuzungumza kidogo kisha akakata simu na kumtazama Pamela.

‘ Jerry ataingia Dar usiku wa leo’ akampa taarifa Pamela ambaye alitabasamu tu
8888888888888888888888

Nyanza Mugilagila, aliomboleza kwa siku kadhaa na siku mbili nzima akishinda kaburini kwa mama yake akilia mpaka kupoteza fahamu. Watu wazima pale kijijini walimuweka chini na kuzungumza naye. Maisha yalipasa kusonga mbele. Ilimpasa kuubeba mzigo wa kumsomesha mdogo wake sasa. Kulia vile kusingebadili kitu zaidi ya kumuongezea unyonge utakaomshinda kufanya kazi.

Kifo cha mama yake kilimuumiza sana, alikufa akiwa bado hajapatana naye kuhusu yeye kuuza nyumba, uonevu aliofanyiwa na Mzee Dunia ndani ya wiki hizo mbili, ulimfanya ashindwe hata kumzika mama yake, lakini yote kwa yote kitendo cha Sindi kuondoka na sijue atampata wapi tena ndio kilimvunja nguvu zaidi.

Moyo wake ulikuwa na majeraha mno, faraja pekee aliipata kanisani alikoshinda mara baada ya kazi. Alikuwa akimlilia Mungu ampe utulivu wa moyo, amrudishe Sindi mikononi mwake. Biblia haikutoka mfukoni mwake hata alipoenda shamba kufanya vibarua Nyanza alitembea na biblia yake ndogo.

Wiki hiyo ndio wiki ambayo Jerry Agapela pia aliondoka. Hakumuaga Nyanza si kwa kupenda wala kumkwepa bali Nyanza mwenyewe hakupatikana kirahisi, hiyo akaondoka pasipo kugana naye, pasipo hata kumwambia msichana aliyekuwa anamlilia kila siku, alikuwa anajua alipo!

Kwa kiasi Fulani maisha yaliosnga mbele, Wazazi wa Sindi wakihangaika kumsaka binti yao bila mafanikio. Mzee Dunia akiikataa mahari na kudai angelimngoja Sindi hata karne nzima.  Sega akapata pesa za chuo huku familia yake ikipata nyongeza ya kuboresha maisha yao hapa na pale na Nyanza akishuhudia maisha yake yakibadilika na kuwa ya upweke na sononi nyingi.
88888888888888888888888

Sindi Nalela alishaanza kuyazoea mazingira ya pale alipokuwa anaishi. Ilishatimia wiki ya tatu tangu afike pale. Alishapajua dukani kwa mangi, kwa mama muuza mkaa, gengeni kwa Myao na hata kuifahamu ilipo Machimachi guest house iliyokuwa njiani ukitokea kituoni.

Jioni hii baada ya kuchota maji na kujaza ndoo zake ndani Sindi aliitoa jiko lake kwenye kordo na kuanza kupika. Alipomaliza kuunga dagaa zake jikoni akalifunika sufuria na kutoka nje uani ambako wanawake kadhaa walikuwa wakisukana huku mmoja akifua.

‘We Sindi…’ yule mwanamke msusi akamuita Sindi aliyekuwa anamwaga maji machafu kwenye karo. Sindi akageuka na kumtazama kama kawaida yake uso wake ukiwa na tabasamu pana, alitarajia kusikia utani juu yake na akapatia.
‘huku nyuma jamani….hebu tugawane hizo nyama’ Yule msusi akamtania Sindi akiyanyoonyea makalio ya Sindi.

Wanawake waliokuwa pale uani wakacheka kwanza, kila mmoja akianza kumtania
‘Mwenyewe akiinama kupika kordoni….. hupiti maana anaenea kordo nzima’ huyu alikuwa anasukwa
‘hebu uko! msimsakame mtoto wa watu…. na shepu zenu za kabati la nguo’ aliyekuwa anafua akadakia, akifua huku amesimama wima  na kufanya wenzake wote wacheke
‘Una utani na mama mkorosho…. na hashuo lake la bata kunyonyolewa kimyakimya…juzi akavaa suruali na shati la kitenge’. mwanamke aliyekuwa anafumua nywele akingojea kusukwa alisimulia, akimsema mama mwenye nyumba na wenzake wakaitikia ‘Enhee…’

‘yaani angevikwa kisadolini kichwani…usingejua mbele wapi pembeni wapi…anakwenda ama anarudi….nilicheka ndani humu hadi nikajiombea poh!’ yule mama alisema akicheka na kuionyeshea namna huyo aliyekuwa akimsema alivyokuwa anafanana. Mazungumzo yakanoga, Sindi akiwa anacheka tu na kufuatilia yale maongezi kabla ya kimya kupita ghafla.

Akina mama wale wakatazama kwa pamoja mlango wa chuma wa kuingilia pale uani. Sindi naye akageuka na kutazama ule mlango uliokuwa nyuma yake. Akamuona Jerry!
Akageuka haraka na kumfuata kwa mwendo wa hatua za kukimbia. Akamsabahi huku akipiga goti mpaka chini na kumpokea mfuko wa Rambo aliokuwa ameubeba.

Jerry aliwasalimia wale akina mama na kuongoza na Sindi kueleka ndani
‘umeme upo?’ Jerry akauliza wakati akiingia ndani
‘haujarudi tangu ulipokatika mchana’ Sindi akajibu akifunga mlango na kuutua ule mfuko juu ya stuli ya mbao iliyokuwa kando yake

‘dah! na joto hili…’ Jerry alilalamika akifungua vifungo vya shati na kuketi kitandani
‘za kazini?’ Sindi alimuuliza akimpatia maji ya kunywa Jerry, akayapokea na kupiga mafunda kadhaa, akabweua na kunyoosha mkono uliokuwa na glasi kuirudisha kwa Sindi.

‘Nikusongee ugali au nikupikie wali…kuna dagaa kigoma nimepewa na jamila nikawapika’ Sindi akauliza kwa adabu
‘hapana….nimeshiba’ Jerry akajitetea akijilaza kwa kulalia mgongo na kutanua zaidi lile shati hivyo kuacha kifua chake wazi. Sindi akababaika kidogo, hakujisikia vema kumtazama Jerry katika hali ile.

Tangu aliporejea toka kijijini, Jerry amekuwa akiishi na Sindi chumba kimoja lakini wakilala sehemu tofauti. Jerry alilala kwenye sofa moja lililotenganishwa na pazia upande uliokuwa na kitanda alicholala Sindi. Walishakaa pamoja na kuzungumzia hatma ya Sindi na Jerry akamuomba amvumilie kidogo ili atafute pesa za kumsomesha hata ufundi cherehani. Sindi akakubali!

Ukimya ulipita kati yao, Sindi akiibia ibia kumtazama Jerry ambaye kwa kujilaza kule alionekana kutembelewa na usingizi. Dakika mbili baadaye Jerry akagutuka na kuamka.
‘Nimechoka sana’ alilalamika Jerry
‘nikuwekee maji uoge?’ Sindi akamuuliza
‘hapana nina shifti ya usiku kazini….sasa hivi rafiki yangu atanipitia’ jerry akainuka kuanza kufunga vishikizo

‘…halafu’ Sindi akasita kwanza akimpisha Jerry aliyekuwa analifuata sanduku dogo la nguo. Kule kusita kumalizia kukamfanya Jerry amgeukie Sindi
‘Halafu nini?’ akamuuliza
‘Nataka kuanza biashara ya vitumbua….hili eneo kuna wapika chapatti na maandazi zaidi hakuna vitumbua’ Sindi akatoa mawazo yake
‘kupika vitumbua!’ Jerry akamshangaa lakini ghafla akagundua mshangao wake haukustahili kutokea pale

‘Sasa utanitunza mpaka lini….maisha ni kusaidiana’ Sindi akaongea kiunyenyekevu
‘mtaji wake ukoje?’ Jerry akauliza akifungua sanduku na kutoa bahasha ndogo iliyokuwemo humo ndani
‘Jamila kasema kama elfu 50 zinatosha kuanzia’
‘Mmmh…’ Jerry akaguna
‘Nitafutie hata elfu 20….zilizobaki nitazipata tu’ Sindi akamtoa wasiwasi
‘Wapi?’ akauliza kimashaka
‘kusuka yeboyebo hapa elfu 10…nikipata wateja watatu…ndani ya wiki hii nitakuwa nimetimiza hizo pesa’ Sindi akamalizia na kumtazama Jerry usoni kama mtu aliyengoja ruhusa ya kile alichoongea kutimizwa.

‘Kesho nikirudi unikumbishe tuongelee hili jambo….’ akatoa ahadi na Sindi akamtandika swali gumu ambalo si tu hakulitarajia bali pia hakutaka hata kulisikia

‘Ulisema Nyanza atakuja ili nikae naye huku….vipi umewasiliana naye?’ Sindi akauliza na Jerry akajikuta akimtazama Sindi kwa namna isiyoeleweka
‘una haraka naye sana?’ Jerry akauliza kwa sauti yenye msokoto wa wivu
‘hapana… nilitaka tu kujua mmefikia wapi katika suala hilo’ akajitetea akiinamisha kichwa chini.

Jerry akafanya yake na kutoka, akimuaga Sindi kuwa alikuwa anaelekea kazini shiti ya usiku
888888888888888888

OFISINI KWA MZEE KRISTUS AGAPELA
Kwanza  alimtazama huyu mtu aliyekuwa mbele yake kana kwamba aliongea kitu ambacho kiliishia nje ya sikio lake.
‘Umesema?’ akauliza kwa sauti ya juu akimkaribia yule mtoa taarifa
‘Nimemuona Jerry..’ akarudia kauli yake lakini kabla ya kuimalizia yote Mzee Agapela akamuwahi
‘Jerry?....My son?’ Agapela akauliza kama mtu aliyetaka uhakika zaidi na yule mtoa taarifa akatingisha kichwa juu chini mara mbili.

Mzee Kristus akatunduwaa, kama zoba akatembea akiweweseka mpaka kwenye sofa lililokuwa ifisini hapo na kuketi taratibu mithili ya mtu aliyekuwa analiogopa lile kochi. Macho yake yakarejea usoni pa yule mpelelezi aliyemkodisha mwenyewe.
‘How is him?’ akauliza sauti ikitetemeka
‘Anaonekana mzima wa afya na…na…’ yule mpelelezi akasita na kumuongezea wasiwasi Mzee Agapela aliyekuwa anahema kwa nguvu kila sekunde iliyokatika
‘Na nini….what?’ akauliza Agapela macho yakimtoka pima

‘Alikuwa amevaa mavazi machakavu…. kama vile mtu mwenye maisha ya chini sana’ Mpelelezi akamalizia dukuduku lake na kuzidi kumpa kitendawili Mzee wa watu
‘una uhakika uliyemuona ni Jerry Agapela?’ Mzee akaona kama anadanganywa waziwazi. Ni kweli alikuwa anamtafuta mtoto wake lakini hakutarajia kusikia habari zake kwa mtindo huu.

‘Mzee nina uhakika alikuwa Jerry ingawa amekuwa na nywele nyingi kichwani lakini nina uhakika ni Jerry…’ Mpelelezi akalifuata begi lake dogo na kutoa bahasha ya khaki kama zile za kutumia barua na kumpatia mzee Agapela.

Picha mbili za Jerry akiwa na mfuko wake wa rambo begani akivuka barabara eneo la mchikichini, zililala mikononi mwake. Akaachama mdomo huku mikono ikimtetemeka. alikuwa Jerry!
‘Ni nini hiki?...’ akauliza akizitazama zile picha huku akihemea mdomo sasa.
‘aliekea wapi… ulishindwa nini kujua aliko?’ Mzee agapela alikaripia kwa jazba kule kuhema kukizidi na akajikuta akaushikilia moyo wake kwa miko yake na picha zile kudondoka chini.

‘Mzee….Mzee vipi?’yule mpelelezi alimuwahi Mzee agapela pale chini na kuzikota zile picha haraka na hapo hapo akijaribu kumhoji Mzee yule.

Ghafla Fiona akafungua mlango wa ofisi na kuingia ndani
‘Beibiii leo twe…. heeey kuna nini?’ alikatiza alichotaka kusema na kukimbilia pale sofani alikokuwa mumewe akigugumia maumivu ambayo yalionekana kutokea kifuani upande wa moyo.
‘Waambie mapokezi tunahitaji huduma ya kwanza haraka…..’ yule mpelelezi akamuagiza Fiona ambaye alitoka haraka kurudi mapokezi.

Mzee Agapela huku akihema kwa taabu akammvuta yule mpelelezi karibu yake
‘Asijue chochote’ akasema kwa kubana meno na yule mpelelezi aliielewa ile kauli lakini wakati Mzee Agapela akimuachia yule mpelelezi Fiona alikuwa anaingia na aliliona lile tukio dogo na kumfanya akunje uso kwa kutokuelewa nini kilikuwa kimezungumzwa pale.

Mzee Agapela akaondolewa na kuwahishwa hospitali huku akipatiwa huduma ya kwanza. Fiona alibaki nyuma wakati Mzee Agapela akiteremshwa toka ofisini kuelekea lilipo gari. Alitulia na kuwatazama yule mpelelezi na mumewe kwa awamu. Alihisi kulikuwa na kitu alichopaswa kukijua. Swali lilikuwa ni kitu gani?
88888888888888888888888888888888


Jua lilishazama na usiku kuingia na kulitawala anga. Ndani ya nyumba ya kubwa ya Meddy Hakim, Jerry na Meddy walionekana wakitembea kuufuata mlango wa kutokea nje.
‘ and for how long Jerry?....utamchezea akili mpaka lini?....’ Meddy aliongea na Jerry wakati wakitoka nje ya nyumba ya Meddy na kwenda kuketi sehemu iliyokuwa na meza pamoja na viti vya plastiki katikati ya bustani.

Jerry alikuwa nadhifu ,no usiku huu, ndani ya mavazi yake ya gharama, akiwa na glasi ya juisi pamoja na simu zake mbili mkononi, huyu ndiye aliyekuwa Jerry Agapela halisi.
‘…na siwezi kumwambia ukweli sasa kuwa siko kama anavyonifikiria…. nimeshampa image ya mtu duni anayehustle kusaka maisha…. ghafla tu nimwambie ni hivi na hivi kamwe hatonielewa’ akajitetea akivuta kiti n akuketi

‘na unadhani utaficha mpaka lini?....worse enough ulimuahidi kumleta boyfriend wake pia…. you know what Jerry?..... unatengeneza hatari kubwa sana mbele yako, kuahidi kitu usichoweza kutimiza....Jerry!!…. pengine kabla ya yote naomba uwe mkweli kwangu’ Meddy akaongea kwa jazba kidogo

‘kuhusu?’ Jerry akauliza
‘je unamtaka Sindi?’ akampasulia ukweli na hali ya kubabaika ikajitokeza usoni mwa Jerry ingawa alijaribu kuificha hali ile kwa tabasamu.
‘come on…this is man to man talk… nataka kusikia toka kwako kabla sijakwambia kitu’ Meddy alisisitiza
‘Meddy!.... Sindi sio mpenzi wangu bwana…’ akajitetea kizembe
‘Sijasema ni mpenzi wako….nazungumzia suala la kumtaka au whatever utakavyotafsiri….’ Meddy akakaza uzi

‘No!’ Jerry akadanganya akiumia moyo
‘Una uhakika?’ Meddy akauliza tena na kufanya Jerry amtazame kwa mashaka
‘na wewe usiniambie unamtaka Sindi just kwa vile nimekwambia sio mpenzi wangu’ Jerry akaonya na Meddy akaliona jibu la kweli la swali lake.
‘kwanini?.... yule si mchumba wa mtu’ Meddy akaipa nguvu hoja yake
‘I’m serious Meddy….leave the girl alone’ akanyanyuka na kuondoka pale mezani akirudi ndani. Meddy akacheka taratibu na kutikisa kichwa chake.

Wakati Jerry akiishia ndani, geti likafunguliwa na Pamela akaingia kwa mwendo wa haraka akiwa andani ya mchuchumio wake, alipiga hatua ndefu ndefu za kupimia shamba. Akamfuata Meddy, uso ukionekana kujaa shari tupu

‘Jerry yuko wapi?’ akauliza kwa sauti ya ukali
‘kwani nini kimetokea?’ naye akamhoji Pamela
‘where is him?’ akasisitiza hasira na jazba zikizomeka usoni mwake
‘ndani’ Meddy akajibu akitumia kichwa kuonyesha uko ndani na mshangao wa waziwazi ukiwa umemjaa.

Pamela akageuka  na kuanza kuelekea uko ndani lakini kabla hajafika, Jerry naye alitoka ndani na kuja uelekeo ule ule aliokuwa akijia Pamela. Walipokaribiana Pamela akainua mkono wa kulia na kuachia kofi kali sana shavuni pa Jerry.

Lilikuwa kofi kubwa sana , lililomuacha Pamela  mwenyewe aliyelirusha kofi lile akitetemeka…

…NI NINI KIMETOKEA?.... 

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger