12
SEHEMU YA 12
Jerry Agapela alimtazama mdogo wake kwa huzuni, katika umri kama
ule alipaswa kuwa mwenye furaha na ari ya kutimiza ndoto zake, lakini haikuwa
hivyo Jenifa alikuwa na jukumu kubwa la kumuangalia mama yake kwa takribani saa
24 za siku yake.
Alilala kwa taabu akiingoja kesho bila matumaini yoyote.
Kutoka maisha ya hali ya juu mpaka maisha duni ya kutojua kama
angepata hata mlo wa siku moja au la ulikuwa ni mtihani mkubwa mno kwa Jenifa
Agapela.
Jerry alijitahidi kutulia, akiacha kulia kwa kugundua alizidi
kumchanganya Jenifa ambaye alikuwa akimtazama kama
mhimili wake kwa wakati ule. Akashusha pumzi na kutazamana na Jenifa ambaye
sasa alicha kulia kwa kwikwi na kuendelea kufuta machozi yaliyomjaa machoni
mwake kila sekunde.
‘Umepata kodi?’ Jenifa akauliza akivuta kamamsi nyepesi
ziloiozletwa na kule kulia. Kerry akaitikia kwa kichwa, maskini alijaribu
kutabasamu katikati ya ile huzuni.
‘Umepata wapi?’ Jenifa akauliza kwa sauti ya upole lakini
macho yake yakimtazama Jerry moja kwa moja kwenye mboni ya macho yake, ni kama
vile hakutaka kudanganywa. Jerry
hakujibu swali lile, alishusha kichwa chini nah ii ikampatia jibu Jenifa.
‘Pamela!’ akajijibu lakini pia alilitamka lile jina
kujiridhisha kuwa alichokuwa amejibu kilikuwa sahihi. Jerry akaitikia kwa
kichwa, moyo wake ukipata dhoruba kali kwa kuhisi kushuka kwa uanaume wake
mbele ya mdogo wake. Hakutaka kumdanganya!
‘Here we go again…’ Jenifa akatamka akiwayawaya
‘unadhani ningefanyaje Jeni….huoni karibia tutatupiwa vitu
nje’ Jerry akajitetea kwa bidii akiwa ameshusha sauti isiisikiwe na baadhi ya
wtau waliokuwa butanini pale. Jenifa akanyanyua mikono kama
mateka, uso wake ukiwa umetahayari na yale machozi yakikatika ghafla.
‘hata kama Jerry….tatizo sio msaada…’
akadakia Jenifa
‘kumbe?’ Jerry naye akamdaka haraka wote wakionekana kuanza
kutembelewa na jazba
‘tatizo mtoa msaada…. hukuweza kufanya kitu kingine tukapata
kodi zaidi ya kusbiri pesa za Pamela kila siku?’ Jenifa alihoji kwa hasira bila
kujua ni kiasi gani alikuwa anazidi kumuumiza Jerry
‘Jenifa!’ Jerry aliita kwa sauti iliyojaa ghadhabu, akiwa
amemtolea macho mdogo wake na ile sauti yake ikipaa na kuwageuza shingo watu
waliokuwa eneo lile. Kule kuangaliwa na watu kumfanya ajishushe na kupepesa
macho kuangalia ni wangapi walikuwa wameshtushwa na kelele zake. Akashusha
pumzi na kujaribu kuidhibiti hasira aliyokuwa nayo wakati Jenifa aliyekuwa
anamtazama kaka yake kwa hasira akigeuka na kutazama pembeni.
‘Najaribu kufanya kila ninachoweza Jeni…..I’m trying….mle,
mama apate chochote cha kutia tumboni…najaribu Jeni….angalau tusiadhirike
zaidi….it seems huoni jitihada zangu…’ Jerry aliongea akipepesa macho na
kutetemeka midomo
‘Sijasema sioni jitihada zako’ Jenifa alijibu pasipo
kumtazama kaka yake
‘then tatizo liko wapi?’ Jerry akauliza akimtazama mdogo wake
na asimuelewe
‘Pamela!’ akajibu Jenifa na kumfanya Jerry afinye uso wake
kidogo na kupunguza ukubwa wa macho yake, ilhali paji la uso wake likijenga
ndita kadhaa
‘Amefanya nini?’ Jerry akauliza akizidi kuukunja uso wake
Jenifa akajibu. Jibu jepesi tu, jibu lililomfanya Jerry
ajikute akitabasamu kwa huzuni na kutikisa kichwa kulia na kushoto mara kadhaa
huku akitazama chini.
‘unasemaje?’ akamtaka Jenifa alirudie jibu lake
‘Simpendi!’ Jenifa akalirudia kwa msisitizo
Jerry akashusha pumzi kwa mkupuo wa nguvu, alihisi hasira. Kama
si kuwa katika mazingira yale waliyokuwepo si ajabu angemtandika mdogo wake
kofi moja la kumrejeshea ufahamu katika neva zake. Jerry hakuwa na kazi ya
maana licha ya elimu aliokuwa nayo, aliishi kwa vibarua vya hapa na pale
ambavyo wakati mwingine alijisikia hata aibu kuvifanya, lakini ilimpasa
kugangamala ili maisha yaende.
Pamela Okello, msichana aliyekuwa rafiki yake na mtu wake wa
karibu ndiye hasa aliyekuwa akiokoa jahazi mara kwa mara kila alipikwama uko
kwenye vibarua vyake.
Hakupenda kumtegemea Pamela, wala hakuwa najisikia fahari
kupokea pesa za mwanamke kwa matatizo yake, lakini angefanyaje?....angelipaje
kodi hali pesa yote aliyopata ilitumika kuwatunza wao watatu.
Jerry alihisi mdogo wake alikuwa akiyatazama maisha kirahisi
zaidi kwa vile tu alikuwa akiletewa chochote kilichopatikana pasipo kujua
shuruba na madhila aliyokuwa akikutana nayo kaka yake katika hizo harakati za
kutafuta pesa na kisha kuambulia pesa ndogo sana
iliyotosha kuishia kwenye chakula na nauli.
‘Tutaonana baadaye’ akaamua kuaga ili kuepusha shari zaidi
‘Kama anakupenda sana
aje akusaidie kumuuguza mama hapa hospitali’ Jenifa akaipalilia shari wakati
Jerry akinyanyuka
‘Jeni Please!...’ Jerry akamjia juu mdogo wake akimsonta kwa
kidole cha shahada cha mkono wa kushoto, Jeni akageuza uso na kuunyanyua kidogo
kumtazama usoni kaka yake aliyekuwa amesimama kando yake.
‘na bado huoni dharau anayoifanya?....mtu anakuja kumuona
mama yako hata kumgusa mkono anaona kinyaa?.... halafu bado unamtetemkea kwa
vijipesa vyake…’ jenifa aliongea kwa hisia na hasira ndani yake. Jerry akazidi
kumkunjia uso!
Jenifa naye akasimama, na kuivutia juu suruali ya jeans
aliyokuwa amevaa, kisha akamtazama kaka yake aliyekuwa bado amemkunjia uso,
akimtazama katika namna ya kutomuelewa
‘na sijaona kinachokufanya umkatae Clarita sababu ya mwanamke
kama huyu… kwa
Pamela you are after money Jerry ..shame on you!’ Jenifa alitoa dukuduku lake.
Akimtaja Clarita rafiki yake kipenzi ambaye amekuwa akimlilia Jerry miaka kwa
miaka kiasi cha kuamua kuondoka nchini na kwenda nje kimasomo angalau kujiweka
mbali na mwanaume anayempenda.
Jenifa akaondoka na kuelekea wodini, akimuacha kaka yake
anamtazama mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yake. Jerry akarudi chini
taratibu na kuketi pale alipokuwa ameketi mwanzo. Kauli za Jenifa zilimuumiza sana ,
alimpenda Pamela toka moyoni ingawa ni kweli Pamela hakuwahi kumkaribia mama
yake kila alipofika hospitali kumsindikiza kumuona.
Ni kweli mara kadhaa Pamela alikuwa akibaki garini na
kutoenda wodini kumuona mama yake, akidai kelele za mama yake na vile
alivyokuwa amekonda kulimuogopesha. Yeye binafsi hakuona ubaya wowote lakini
matendo yale kwa Jenifa yale yalikuwa matusi ya nguoni!
88888888888888888888888
Hali ya Sophia Agapela ilizidi kuwa mbaya siku hadi siku na
mumewe hakukanyaga kumuona mkewe hata siku moja, wala hakujali watoto wake
walikuwa wapi, na wakifanya nini. Alisha
muhamishia Fiona ndani ya jumba lake uko
masaki na maisha kwake hayakusimama, yaliendelea!
Mchana wa siku hiyo ya jumamosi. Fiona alitoka kwa rafiki
yake Azda wakiwa wanasindikizana kuelekea getini, Fiona alicheka kicheko kirefu
cha ushindi, akiongea kwa tambo za kike. Yake mavazi ya gharama aliyokuwa
amevaa yalimfanya azda amkodolee macho mara mbilimbili.
‘hajaenda hata kutoa pole ya uongo na kweli?’ Azda akauliza
kwa mshangao, wakisimama kwanza na kuongea vizuri
‘Nini kumuona? hata simu ya kumjulia hali hakuna….unamjua
Fiona au unamsikia?....niliaga kwetu, nikaagwa nikaagika!’ Fiona alitamba.
Mkono wake wa kushoto ulijikunja na kuining’iniza pochi kubwa ya gharama,
kitenge cha wax toka Holland
kilimkaa vyema na fundi akautendea haki ule mshono wa ile nguo ya Fiona.
Kichwani alikuwa na nywele za bandia, zilizoshonewa
kiumaridadi, achilia mbali kabisa kiatu kirefu alichokuwa amevaa,
kilicholandana na rangi ya kitenge alichokuwa amevaa.mapambo ya dhahabu za
uzani wa kutosha yalihitimishwa na ufunguo wa gari aliokuwa ameushika mkono wa
kushoto sambamba na simu za bei mbaya mbili. Kwa jicho la kwanza tu ungekiri
mwanamke huyu alikuwa na maisha ya hali ya juu mno!
‘Heheheheeee haloo ya kihindi….’ Azda akashabikia akicheka
pia
‘Veeevee’ wakaitikia pamoja kishabiki na kucheka zaidi
‘Yule mganga kiboko ya reli wallah…. waganga na waganguzi uko
Saint Imakulata wanamshindilia midawa tu hahahahaaa….wangejuaaaa!...’ Fiona
alitamba
‘Yaani balaa…. ‘ Azda akaitikia wakianza tena kutembea kisha
wakasimama tena
‘Wiki hii ..’ Fiona akasema akifanya ishara ya kufunika kitu
‘Eeeh! usinambie!’ Azda akakodoa macho yake kwa bidii
‘Ndi hivyo…nataka hizi karaha za simu kila siku sijui
anakulilia sijui kazidiwa sijui bili ziniondoke kabisaaa’ Fiona akaongea kwa
kujiamini na sasa wakianza tena kuelekea getini.
‘Mmh! una roho mwaya…’ Azda alitembelewa na hofu kidogo
‘Ya chuma cha pua….shoga ngoja niwahi uko kwa babu ikamalizie
kazi, utasikia tu….’ Fiona akaaga, na azda akamsindikiza mpaka getini
alikomuacha atoke mwenyewe kisha yeye Azda akafunga geti na kusimama pale
getini akiwa na uso uliojaa hali ya kutoamini.
‘Vipi ameenda?’ mdogo wake Azda aliyekuwa anaanika nguo mbali
kidogo na lilipo lile geti akamshtua dada yake
‘Kaenda mwenzangu….yaani Fiona ana roho jamani…. Sophia huyu
huyu ndiye aliyemsitiri alipofukuzwa kazi….. Sophia huyuhuyu ndiye
aliyemtafutia hii kazi anayofanya na ndiye alimsaidia hata akaonekana mtu hapa
mjini…’ Azda akaongea kwa mshangao uliochanganyikana na huzuni, mkono wa
kushoto ukilala kifuani kama mtu anayesikia maumivu ya
moyo.
‘Hivyo!?’ mdogo wake Azda aliachana na nguo zile na kumsogelea
dada yake
‘Yaani alikuwa rafiki yake wa kupika na kupakua…. leo hii
kamfanyia mandingo dada wa watu jamani…maana aliona kumtoa kwa mumewe
haitoshi…kamlaza na kitandani….na hivi ndio anataka kumzika kabisa!’ Azda
akamfanya yule mdogo wake amtolee macho kana kwamba Azda alikuwa akigeuka kuwa
zimwi mbele ya macho yake.
Wakasikitika kwa pamoja, huku kila mmoja akiwaza lake
8888888888888888888
Sophia hakumaliza wiki tangu ile siku ambayo Fiona aliongea
na Azda. Sophia alikufa!
Saa chache kabla ya kufa Fiona alimtembelea hospitalini na
akamkuta akiwa na hali yake ya siku zote ya kulia na kuomba aitiwe mumewe.
Alipomuona Fiona alinyamza ghafla, alitulia tu akimtazama Fiona huku machozi
mengi yakimtoka. Alimeza mate kwa uchungu, yakipita kooni kwa taabu.
‘hata wewe?...hata wewe Fie?’ Sophia alimuuliza akilikatiza
jina la Fiona kama alivyopenda kumuita enzi za urafiki wao.
‘Mume wangu yuko wapi?’ Sophia akauliza akizidi kutiririkwa
na machozi
‘Mumeo?...Sophie!...bado unahesabia tu kuwa una mume?’ Fiona
akamuuliza kwa kejeli lakini uso wake ukionyesha huruma, kama
mtu angelikuwa mbali akiwatazama si ajabu angelihisi Fiona alikuwa akitoa
maneno mazuri ya faraja kwa mgonjwa.
Sophia hakujibu kitu, aliendelea kumtazama Fiona kwa huzuni
na pengine majuto ya kumkaribisha nyoka maishani mwake. Fiona akangaza angaza
huku na kule kabla ya kufunua mkoba wake na kutoa kitu kama
unyoya, akaupitisha haraka usoni pa Sophia na kuurudisha mkobani kwa kasi ya
ajabu. Sophia akapoteza uwezo wa kuongea hapo hapo!
Huku akitabasamu Fiona akamuinamia Sophia na kumtazama namna
alivyokuwa akihangaika kutoka kuongea pasipo kuweza. aliyaona mateso yote
aliyokuwa akiyapata Siphia pale kitandani wakati mishipa ya shingo ikimkakamaa
kwa nguvu alipotaka kuzungumza.
‘Tulia ufe taratibu dear…uhitaji kukurukakara zote hizi’
akamwambia kwa upole akitabasamu, taratibu akajiinua na kusimama wima, kwanza
akatoa gloves na kuzivaa, kisha akitoa kile alichokikusudia!
Fiona akaangaza tena kitahadhari na kisha kwa haraka
akaikamata chupa ya drip iliyokuwa pembeni yake ikining’inia na kuipachika ile
sindano aliyoitoa mkobani. Sophia akafurukuta, akitamani kupiga kelele,
akitamani kumzuia Fiona asimtendee unyama ule lakini hakuweza kusogeza hata
kidole.
Sumu iliyokuwa ndani ya Sindano iliishia kwenye drip na Fiona
akairudishia sindano mkobani.
‘Kalale pema peponi’ akasema akitabasamu, tabasamu la ushindi
kisha akatoka kwa madaha na kutokomea. Sophia alilia kwa uchungu, akionekana
kuumizwa na ila hali pasipo kuweza hata kusogea.
Jenifa aliyekuwa anasuuuza vyombo nje, alirejea wodini alikokuwa mama yake na akipishana na
Fiona pasipo kumtambua lakini aligeuka na kumtazama pengine akivutiwa na vile
alivyovalia.
Akaingia na kuweka vyombo juu ya kabati, kisha akaketi kwenye kiti kilichokuwa kando
akisoma gazeti lake. Hakumtazama mama yake, aliketi na kuendelea kusoma gazeti
la udaku alilolikuta juu ya kabati huku mama yake akimtazama katika namna ya
kutaka kumuomba msaada. Jenifa alizidi kutopea gazetini, akicheka ile
alichokuwa anakisoma pasipo kujua mama yake alikuwa katika maumivu makali mno!
……TUKUTANE HAPAHAPA….. UNA MAONI GANI MSOMAJI?
No comments:
Post a Comment