Friday, October 18, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (43)

43


Siku hii ilijaaliwa mawingu mazito yaliyofifisha ukali wa jua na kuleta  hali ya ubaridi iliyokuja na kutoweka. Ndani ya saluni kubwa ya kisasa ya wanawake iitwayo Marino kulikuwa na pilika pilika za hapa na pale. Huyu akioshwa nywele, yule akisuguliwa kucha hapa wakiwekana rolazi na kule wakitindana nyusi, mradi kulikuwa na hekaheka za hapa na pale.



Mmiliki wa hiyo Saluni aitwaye Marino Marino, mtanzania mwanaume mwenye asili ya Italy alikuwa amesimama mbele ya kioo akimchana mteja nywele huku akipiga soga na wateja wake pamoja na wafanyakazi. Kiswahili chake cha kuunga unga kiliwachekesha wengi mule ndani, changanya na aina ya soga ndio kabisa watu walionekana kuchangia soga na kucheka kila mara.

Marino akamtaka radhi mteja aliyekuwa anamchana nywele huku akikichomeka kitana alichokuwa anakitumia katika nywele za mteja na kumgeukia mteja aliyeingia na binti mmoja muda ule.
‘Shanshuuu!... ukipotea ukija lazima uje na mizinga ya nyuklia’ Marino akasema kwa madoido kidogo na kufanya watu mule ndani wacheke. Adella aliyekuwa ameongozana Pamoja na Sindi alicheka huku akigeuka  kusalimiana na baadhi ya watu aliokuwa akifahamiana nao.

Marino akamshika mkono Sindi na kumuelekeza kiti cha kukaa. Akaachana na Sindi na kurejea kwa Adella.
‘Enhe! ya wapi hii?’ akauliza Marino kiumbea  huku wachache waliokuwa karibu nao wakitega masikio

Adella akajichekesha akilikwepa lile swali na Marino akamuelewa na wakaishia kugongesha viganja vyao. Adella akitafuta pa kuketi na Marino akirejea kwa yule mteja.

Stori za hapa na pale zikapamba moto, Sindi Nalela akiwa ameduwazwa na yote yaliyokuwa yakiendelea mule ndani. kuna maswali yalikuwa yakipishana kichwani mwake tangu alipoambiwa alipaswa kwenda saluni kuwekwa sawa. Akili yake haikumpa majibu ya maswali yake lakini alijitahidi kuyachukulia chanya yote aliyoshindwa kuelewa.

Saa moja baadaye, Sindi akawekwa mbele ya kioo, Marino akiwa nyuma yake, akijaribu kutathmini cha kuzifanya nywele ndefu za asili za Sindi ili zikae katika mtindo utakaoboresha urembo wake.
‘Tuziweke dawa?’ Marino akamuuliza
‘Hapana… hapana… mmh mmh hapana’ Sindi akakataa akitikisa kichwa pia kuonyesha msisitizo. Marino akakuna kichwa. Hazikuwa nywele ngumu za kipilipili, alikuwa na nywele laini zilizojaa vizuri na kuvutia. Marino akakaza macho kwenye kioo akiitazama sura ya Sindi na kutafakari cha kufanya.

Wazo likamjia haraka, akatabasamu na kumuonyesha Sindi alama ya dole gumba akiashiria kupata ufumbuzi
Shughuli ikaanza mara moja. Marino akihangaika na nywele huku mhudumu mwingine akimsafisha kucha. Dakika 45 zilitosha kumtoa Sindi kwenye kiti na kusimama mbele ya Adella na wateja wengine kama msichana mrembo mno!

Nyusi zake zilikuwa zimetindwa kiustadi, huku midomo yake ya kuvutia ikinakshiwa na rangi ya mdomo iliyoshabihiana vyema na rangi ya ngozi yake. Alivutia kuliko neno lenyewe mvuto lilivyoweza kumaanisha.

Akahamishiwa upande uliokuwa na duka la nguo na kuanza kazi ya kuchaguliwa nguo. Alikataa suruali na kaptura akidai hakuzoea mavazi hayo, alikataa nguo zenye kuacha mgongo wazi ama nguo zenye kumbana na kuonyesha umbile lake la wastani lililogawanyika kike haswa. Wakaingiua katika upande wa viatu, Adella akacheka kupitiliza kila mara Sindi alipojaribu viatu virefu. Vilimshinda, vilimtoa ushamba!

Baada ya pilika pilika ya kurekebishana hapa na pale. Sindi akiwa na mifuko mingi ya vitu alivyonunuliwa, Safari ya kurudi kwa Adella ikaanza, Akiwa ameketi siti ya nyuma, Adella alimtazama kupitia kioo cha mbele na kukiri, msichana huyu alikuwa mzuri, ….mzuri mno! na kwa gharama alizomgharamikia leo alitarajia zingerudi mara mia zaidi kwa kutumia huo uzuri wake. Akatabasamu kifedhuli!
88888888888888888888888888888

Fiona Agapella alikuwa na mchecheto wa kutosha. aliiizunguza sebule yake mithili ya mkimbia riadha wa mbio fupi. Akashika hiki na kukiacha akahamisha kile na kukiweka pale, mradi akili yake haikuwa katika mpangilio wa kujielewa ni nini hasa alikuwa anafanya!

Mlio wa hodi iliyobishwa mara moja tu, ulimkimbiza mpaka mlangoni kwa kasi ya ajabu. Akaufungua mlango kwa pupa na kuuvutia upande wake. Iloma akajitoma ndani akiwa na uso uliojaa taharuki. Akamtazama Fiona aliyekuwa amemkodolea macho huku akionekana wazi kutetereka kupitiliza.

‘Hajafa?’ Iloma akauliza akitikisa kichwa kulia na kushoto, sauti yake ikitoka kwa sauti ya chini iliyojaa tahadhari. Fiona anaitikia kwa kichwa akisita sita kama mtu asiyekuwa na uhakika na jibu lake. Iloma akshusha pumzi kwa nguvu, akimeza mate kwa bidii kiasi cha kufinya kingo za midomo yake kama mtu aliyemeza kitu kichachu.

ukimya ukawatembelea na wakabaki kutazaman kila mmoja akiwaza lake kichwani. Fiona akahisi uzito way ale aliyokuwa akiwaza ukimuelemea mabegani. akatembea kinyonge na kujitupa sofani huku shoga yake akimfuatiza kwa macho na asijue ampongeze au amhurumie.

Iloma akaketi kando yake taratibu, akimtazmaa kitahadhari na pengine aliyoyapanga kuyasema yakikimbilia kusikojulikana na kumuachia kichwa kitupu mithili ya pakacha. Faraja aliyotaka kuitoa iliyeyuka, akabaki kama msukule uliopotea njia!

‘Why?...’ Fiona akakurupuka na kuhoji kwa ghadhabu kiasi cha kumshtua Iloma
‘This can’t be true iloma… tell me kuwa naota… it can’t be true’ Midomo ya Fiona ilitamka ikicheza cheza na machozi sasa yakimlenga. Alikuwa na hofu iliyochanganyikana na ghadhabu. Alitetemeka kiasi cha kufanya meno yake kinywani yagongane kama mtu anayesikia baridi kali. Kwa mara nyingine alihisi mpango wake ulikuwa umeshindikana!

‘No!...Nooo!’ akapiga yowe na kujiinamia akilia. Iloma akamsogelea na kumkumbatia akijaribu kumtuliza.
‘Fiona!...FiFi’ Iloma aliacha kumkumbatia na kumtazama usoni, akijaribu zaidi kumuondoa katika ile hali ya sononi na hasira.
‘Relax! …sawa… tulia kwanza…’ Iloma alijaribu tena kumuweka sawa rafiki yake huku akili yake pia ikishindwa kumpa maneno ya kumfariji. Alichoshindwa kukifanya kilikuwa ni jambo jema kabisa, hakupaswa kumtoa uhai mumewe na katika hali kama ile alikosa pia maneno ya kumweleza ukweli kuwa alichokuwa anakipigania kilikuwa dhambi kisheria achilia mbalia mbele za Mungu baba!

Fiona akamtazama Iloma kwa hasira kana kwamba yeye ndio aliyemtibulia mipango yake.
‘unajua kwanini nafanya hivi?... unajua kwanini nakuwa hivi?... unajua kwanini naua hivi sababu ya mali… do you know why?’ Fiona aliongea kwa sauti iliyopanda swali baada ya swali kiasi cha kufanya swali lake la mwisho litoke kwa sauti ya kumpayukia mtu aliye mita mbili mbele. Machozi yakamtiririka, huku koo lake likididimia ndani kuzuia kwikwi za kilio. Iloma naye akalengwa na machozi akitikisa kichwa kulia na kushoto kuyajibu yale maswali ya Fiona, aliyotoka mfululizo.

‘Sijawahi kupendwa kwa dhati… sijawahi kuonja mapenzi ya kweli… hata mtu aliyenileta duniani alinichukia kiasi cha kunitupa ili tu aolewe na mtu mwenye mali… ooh Mungu wangu… hata mwanaume wa kwanza maishani mwangu aliniacha sababu tu alipata msichana aliyetoka katika familia yenye mali... mjomba wangu aliyenilea alinibaka kwa mwaka mzima…mwaka mzima Iloma… mwaka mzima!!... nikiwa na miaka kumi tu ili apate mali, ili mizimu impe mali…’ Fiona akafumba macho na kuruhusu machozi yafanye njia zaidi mashavuni mwake. Iloma akaumizwa na yale maneno ya Fiona

‘unahitaji msaada Fifi’ iloma akamshauri huku akimtazama kwa huruma na kupangusa machozi yaliyokuwa yanamtoka bila kujijua.

‘Sidhani…’ akafumbua macho na kumjibu iloma, midomo ikimtetemeka
‘mpaka nafsi yangu itimize inachotaka’ akajibu na kuvuta pumzi, akiishusha kwa ujasiri na kujaribu kujiondoa katika ile sononi. Tabasamu la kulazimisha likimvaa na kushindwa kuipunguza hali ya simanzi usoni pake.
‘Fiona!... kubali kuwa una matatizo… na unahitaji msaa..’ hakumalizia akakatizwa na Fiona aliyenyanyuka na kusimama hatua moja mbele
‘I’m okay… I’m fine iloma… it’s okay… nitaimaliza hii inshu ninavyojua… Sijawahi kukubali kushindwa… na nitakapokubali itamaanisha sitakuwa hai’ akaongea kwa kujiamini. akishusha pumzi kwa sauti na kupangusa machozi.

Akalifuata kabati lililokuwa na chupa za pombe na kujimiminia kiasi kwenye glasi, akapiga funda moja la mkupuo na kulimeza kwa bidii zote huku rafiki yake akimtazama kwa masikitiko. Iloma alijua rafiki yake alikuwa na mambo mengi nyuma katika maisha, mambo aliyoyabebea kisasi, hasira na uchungu kiasi cha kumfanya awe hivyo alivyo na hakuwa tayari kuwa wazi zaidi na kupewa msaada.

Akili yake ilimsukuma kumwambia mumewe Kristus kuhusu maisha ya nyuma ya mkewe ili kumnusuru Kristus na familia yake achilia mbali Fiona mwenyewe lakini moyo wake ulisita, alimjua Fiona vizuri kama alivyokijua kiganja chake, ingemchukua dakika moja tu kumpoteza juu ya uso wa dunia. Alibaki njia panda!
8888888888888888888888

Wakati Fiona akihamanika nyumbani kwake. Pamella Okello alikuwa yu kitandani akiongea kwenye simu. Alikuwa ameketi, akiwa amenyoosha miguu na kujifunika shuka mpaka kiunoni. Mkono mmoja ulikuwa umeshikilia simu na mwingine ulikuwa na tissue iliyokuwa ikipangusa makamasi yaliyokuwa yakimsumbua kutokana na kule kulia.

Alipepesa macho yaliyokuwa bado na wekundu, huku akijaribu kutoyakaribisha machozi mengine. Akaongea kwa muda kisha akakata simu na kuirudhia kando. Mkono uliokuwa na simu ukabeba paji la uso wake na ule wenye tishu ukalala chini ya huu uliobeba paji kama egemeo. Akatulia hivyo kwa sekunde kadhaa kabla ya kusikia mtu akigonga mlango wa chumba chake.

‘Sihitaji chochote, endelea tu na kazi zingine’ akajibu akijua anazungumza na mhudumu
‘No! Pam ni mimi’ sauti ya mama yake ikasikika kule mlangoni na kumfanya Pamella atazame kando kama mtu aliyeona kichefuchefu

‘Pam please…fungua mlango… we need to talk darling’ mama yake alibembeleza na Pamella hakujibu kitu. Aliutazama mlango kwa huzuni na kutikisa kichwa.
‘Pam!’ mama yake aliita akigongagonga mlango
‘Please mama… naomba uondoke tu.. sijisikii kuongelea lolote muda huu’ Pamella akajibu akitega sikio kusikia jibu la mama yake

‘Najua una hasira… lakini yote kwa yote mimi bado ni mama yako… cant you give me a chance to explain kuhusu ulichoona’ mama yake aliongea kwa kubembeleza zaidi huku akipunguza sauti yake wakati akimalizia sentensi yake

‘Najua nilichoona mama please!... sidhani kama unahitaji kujieleza’ Pamella aligoma na mama yake akazidi kumsihi afungue mlango.
Kama mtu aliyechoshwa nay ale malumbano, Pamella alinyanyuka na kwenda kufungua mlango. Mama yake akaingia na kusimama katikati ya chumba cha bintiye huku akimtazama namna alivyourudishia mlango na kwenda kuketi kitandani. Akamfuata na kuketi kando yake.

‘Nisamehe kwanza!... but tunahitaji kuongea kama wanawake wawili watu wazima mbali na kuwa mama na binti yake’ akaanza kujieleza na Pamella akamkodolea macho tu
‘I didn’t mean to hurt you Pam…’ akaanza kujieleza
‘na ndio umeshaniumiza mama… nilikueleza toka mwanzo kuhusu mimi kuwa na Patrick Mazimbwe… nilikwambia wiki ile ya kwanza uliyofika mama… how come unaflirt na na another Mazimbwe wakati unajua binti yako anauhusiano na mmoja wao… Mama! heshima ya wapi hii?.... unanifundisha nini sasa?...’ Pamella alionge haraka na kwa uchungu.

‘Pamella si kwamba …I mean…najua umeumia… may be niseme.. I just don’t know nikueleweshe vipi?’ mama yake alibabaika kiasi cha kushindwa kupangilia sentensi zake katika mpangilio unaoeleweka
‘Kuhusu nini?... worse enough mama you are cheating on Daddy!!... tena na mtu wa karibu tu… No!.. sitaki kuongea lolote kuhusu hili jambo’ Pamella akanyanyuka na kwenda kuufungua mlango, akimuonyesha mama yake ishara ya kutoka nje

‘Pamella… I’m your mother! right!’ Rebecca alikuja juu sasa
‘I doubt it…’ Pamella akajibu kwa kujiamini na kumfanya Rebecca amtolee macho
‘Pam!... umesemaje?’ Rebecca bado alikuwa haamini kama binti yake alikuwa amemjibu vile
‘I doubt if you are my mother…. mothers cant hurt their daughter this way… they cant share men from the same family with their daughters…’ Pamella akampasulia ukweli
‘Pamella!’ bado hakuamini anachosikia, akamsogelea binti yake akiwa amemtolea macho
‘…. ndio maana ulikazana kuvunja mahusiano yangu na Patrick kwa sababu unajua unamtaka Dennis… see how selfish you are… at least ningekuwa mwanao ungejitolea kumkosa Dennis kwa ajili ta furaha yangu lakini ona ulichofanya na punguani kama Dennis’
paah! kibao cha shavu kikasikika barabara. Rebecca alikuwa ameachia kofi moja kali shavuni pa bintiye

‘hujui ulikotoka Pamella…kama ningetaka kuolewa na Dennis ningeolewa naye hata kabla ya wewe kuliona jua wala kumuona Patrick… siombi msamaha kwa ulichokiona kwasababu nina uhakika ndoa yako na Patrick ni batili hata kabla yaw ewe kuona ulichoona… you are not marrying him. Full stop!!’ akatamka kwa kuuma meno na kutoka mule chumbani akimuacha Pamella anasugua shavu lake na pengine asielewe lolote aliloongea mama yake kabla ya kutoka. Maswali mengi yalikimbizana kichwani mwake pasipo kupata majibu.
8888888888888888888888888888888

Sindi Nalela na Nadina wanaangalia vitu alivyorejea navyo Sindi. Wanavijaribisha kwa pamoja na wakati wakiongea na kucheka. Mlango wa chumba unafunguliwa na Adella anawapa taarifa kuwa waje sebuleni. Sindi anaotoa kahanga yake na kuivaa kiunoni juu ya gauni lake jipya aina ya max.

Wanapofika sebuleni wanakuta wasichana wenzao kama zaidi ya kumi wakiwa wameketi na wengine wamesimama wakimtazama Adella aliyekuwa ameketi kwenye sofa lililotazama na kule walikosimama wale mabinti.
‘Wewe umevaa nini hicho?’ akamkaripia Sindi mara tu alipoingia pale sebuleni na wenzake wote wakamgeukia huku wengine wakicheka kichinichini

Sindi akacheka pia akijua pengine adella alitaka kumtania, lakini haikuwa hivyo
‘Binti umeshaingia hapa tafadhali fuata sheria za hapa… hebu ondoa hiyo khanga na marufuku kuonekana umevaa khanga ndani ya nyumba hii… umenielewa?’ akamkaripia Sindi kwa sauti ya amri na kuipoteza nuru iliyokuwa usoni pa Sindi sekunde chache tu zilizopita. Sindi akaiondoa khanga yake na kuitundika begani.

‘Sasa tusikilizane…’ Akaanza Adella akitembeza macho kuhakikisha wote walikuwepo
‘Delila yuko wapi?’ akauliza, akimtaja mmoja wa mabinti anaowafuga humo ndani
‘amelala… anaumwa Madam’ binti mmoja akajibu na Adella akakunja uso kumtazama yule aliyejibu

‘Nilishasema… kama mtu anaumwa anatakiwa anifuate yeye mwenyewe aniambie anaumwa…huu upumbavu wa kusemeana f’lani hayupo anaumwa… nitakapogundua kuwa anayetajwa kuumwa hayupo na anasingizia kuumwa…wewe uliyemsemea na yeye aliyesingizia mtapokea adhabu sawa… sitarudia tena haya maneno…sawa?’

Wachache wakaitikia kwa kichwa, wengine wakamkodolea macho tu. wakionekana kuyazoea maonyo ya aina ile. Sindi na Nadina walionekana kutoelewa vema kilichokuwa kinaendelea. Kila mara walitazamana na kuguna kwa kukunja ndita usoni

‘… Nimepokea malalamiko kadhaa toka kwa wateja… mabinti… hapa kwangu mteja ni mfalme..anasikilizwa anatekelezewa anachotaka!... sasa tabia ya nyie kuanza kuomba pesa zaidi ili mteja atimiziwe hiki au kile…. next time likija lalamiko la aina hii… mnajua huwa nachukua hatua gani… utafanya kazi miezi mitatu bila mshahara!’ akatamka kwa msisitizo na kufanya mabinti wa watu wamtoklee macho zaidi na miguno ya chini chini ikiendelea

‘… Shari!’ akaita na binti mwenye hilo jina akajisogeza mbele akitokea nyuma alikokuwa amesimama
‘hili onyo la mwisho darling…. kwa vile nitakapokuita tena kukuonya nitahakikisha nimekukata na masikio pia maana naona hayana kazi tena kama tunafanya kuonyana kila siku bila utekelezaji… Baby!...’ akamuita kwa upole wa kinafiki na kumtazama usoni

‘…. Mwanaume akisema umchezee nachi hata kwa masaa matatu… you have to dance masaa hata matano zaidi… majibu ya sitaki, siwezi au nyodo za aina yoyote kwa mteja sitazivumilia zaidi… msiniharibie biashara kabisaaa… umenielewa?’ akamuuliza huyo Shari naye akaitikia tu kwa kichwa
‘Haya toka hapa…usinipe kizunguzungu…’ akamuondoa na kuanza kuzungumzia ratiba na mambo mengine yahusuyo biashara yao. alipowaomba watawanyike Sindi na Nadina walibaki wamesimama mbele yake.

‘Nyie vipi… hamkuelewa niliposema mtawanyike mkajiandae na kazi’ akawauliza akiichukua sigara yake iliyokuwa kwenye kishungi na kuvuta pafu moja.
‘Sisi si watu wajikoni na usafi?’ Sindi akauliza akiona yote waliyoambiwa wenzake hayakuwahusu wao kwa vile walikuja kwa ajili ya kazi za ndani.

Adella akaachia moshi wa sigara usambae hewani, akiupuliza kwa madoido na kisha kuachia kicheko kirefu cha sauti
‘Watu wa wapi?’ akauliza ule mkono ulioshoa sigara ukitumia kidole gumba kugusa nyuma ya sikio, kwa staili ya nipashe!

‘Jikoni’ Nadina akajibu
‘Acheni upumbavu… yaani msifanye nikanyanyuka hapa nikatembeza ngumi ghafla… nyie mna nini msifanye wanayofanya wenzenu?... haya basi ngoja niweke mambo kwenye mstari…. hakuna cha kazi za jikoni wala za barazani…. hapa tuna kazi za chumbani tu baaasi…’ akaongea akiwatazama mabinti hawa ambao hofu ilionekana wazi machoni mwao

‘Mi sitaweza kwakweli bora niwe wazi. sijawahi kuwa Malaya maishani mwangu’ Sindi akajitetea
‘Ningekukuta bikra ningekuelewa, Malaya ana alama usoni?... kila aliyekuja hapa alisema hataweza mwisho wa siku waliweza tu… nawe utaweza tu mwanangu…’
‘Lakini sivyo tulivyokubaliana mama’ Nadina anaye akatoa yake

adella akacheka tena, kwa kibehi kubwa hasa
‘hivi nyie na mimi tunamakubaliano gani?... mabinti msinipotezee muda wangu… naomba mtoke hapa upesi kabla sijaharibu sura ya mtu… nenda mkalie uko ndani.. sijui msali wee mwisho wa siku mtahudumia wateja wangu nipate dola zangu… kama mkenge ndio ummeshauvaa na kama mjini ndio mshaingizwa… hapa kujiuza tu maadili utaendeleza kwenu nikishakuchoka… haya potea!’ Amri ikatoka kwa ukali na akina Sindi wakajikuta wanaondoka kurudi vyumbani mwao

Sindi Nalela akapoteza matumaini yote, nusu saa tangu atoke mbele ya Adella alihisi dunia imemtandika fimbo ya utosi. Alilia na kuomboleza na akisali alivyojua. Nadina yeye alijifungia bafuni, akilia kivyake na akikumbuka alikotoka.

Jioni ya siku ile ndio siku ambayo Sindi Nalela aliiweka katika kumbukumbu ya kichwa chake. Wakati mteja alipoletwa chumbani kwake na Nadia kuombwa apishe. Sindi alisimama mbele ya mwanaume huyu mtu mzima kwa huzuni kubwa. Mengi yalipita katika kichwa chake kwa sekunde mbili tatu alizosimama mbele ya mwanaume huyu wa makamo, aliyeonekana kuwa bora tu kimaisha nap engine mwenye mke na watoto wa umri wake yeye Sindi.

Mteja huyu anamsogelea Sindi na kujaribu kumbusu mdomoni lakini Sindi anaikwepa midomo ya mteja na kuipangua mikono iliyotaka kutua mabegani mwake. Yule mteja anashangaa kidogo na kumtazama Sindi usoni. Anayaona wazi machozi ya Sindi yaliyokuwa yakiteremka kimya kimya.

‘anapojaribu kumgusa tena Sindi, anaambulia kusukumiwa mbali na Sindi anajisogeza mbali naye. Mteja yule mtu mzima, anamfuata Sindi na kumshika kwa nguvu akimlazimisha kumvutia kitandani lakini Sindi anapambana naye. Purukushani ndogo tu inazuka na Sindi anajinasua kwa kuamua kumng’ata mkono.

Mteja anamuachia na kupiga yowe dogo la maumivu huku Sindi akikimbilia bafuni na kujifungia. Kwa hasira, Mteja yule anavaa na kutoka mule chumbani akielekea mapokezi anakomuulizia Adella. anaonyeshwa chumba ambacho ni kama ofisi ya Adella mule ndani.
‘Mambo gani haya Ade?... kitu gani hiki?’ anamuonyesha alama ya kung’atwa na meno aliyoachiwa na Sindi
Khaaa! nani huyu?.... pole pole pole Mr. Zaki… pole sana.. wait a minute darling’ Adella akampooza mteja wake akifuata pamba na dawa na kumpagusa lile eneo alilong’atwa wakati mteja akifoka kwa kuhusu huduma mbovu na wasichana wasio na nidhamu. Adella anatumia lugha laini kiumpooza.

Wanatoka mpaka mapokezi
‘Hey, mpeleke kwa  Shari huyu mteja… na nani alipewa huyu baba chumba namba 10?’ anatoa maelezo yanayofuatiwa na swali huku uso ukiwa na ndita kadhaa
‘Sindi’ mtu wa mapokezi akajibu na yule mama akamgeukia yule mteja na kumtaka radhi tena na tena na akimuahidi anakopelekwa ni kwa mtu anayejua anachofanya.

‘hapana!... sidhani kama nina mood ya kuwa na mtu tena… na nilipoingia nilimchagua huyo huyo na ndiye ninayemtaka’ yule mteja aligomea kupelekwa kwa mwingine
‘… kwa leo nadhani itakuwa ngumu… bado yu mgeni kidogo na inahitajika nguvu ya ziada kumuweka sawa… unajua tena jamani’ kajitetea Adella
‘Basi mnirudishie dola mia zangu… mpaka hiyo next time ila kwa mtindo huu youu need to train them kwanza kabla ya kumkabidhi kwa mteja…. biashara hii ina ushindani… unapokuja sehemu kama hii unategemea utulivu wa mwili na akili na huduma bora sio purukushani kama hizi Ade…’ Mteja alimpa ushauri huku akipokea pesa zake na kuagana nao. akaondoka

‘Mpumbavu huyu…. nimetoka kuongea sasa hivi… mambo hayahaya…ngoja!’ Adella akakusanya nguo yake na kupandisha ngazi akivifuata vyumba vilivyoko juu. Akakisaka chumba namba kumi na kukiona. alipofungua mlango akamkuta Sindi anajikanda kwa maji mkono aliokuwa umeshikwa na yule baba wakati wa kuvutana.

Adella akamvamia kwa kasi na kumkusanya kama mzigo, akambwaga chini na kuanza kunshushia kipigo cha uhakika. ngumi, vibao, mateke, akaokota na ndala ya Sindi na kuanza kumpiga nayo kila mahali alipochoka alisimama na kumkanyaga kwa hasira kisha akaendelea kumshushia kipigo. Sindi akajikunyata pale chini akilia kwa mayowe. Wenzake walikuwa kwenye mlango ya vyumba vyao wakisikilizia sakata hilo.

Alipotosheka akasimama kando yake akihema kwanza
‘hakuna chakula cha usiku leo… angalau njaa itakukumbusha kuwa asiyefanya kazi na asile’akatoka na kumuacha Sindi amelala chini akiwa hoi kwa kipigo.

Sindi alijikunyata akilia, alilishikilia tumbo lake akilikwepesha na kipigo, alijua alikuwa anamlinda mtoto wake. Alilia pale chini akiwa kama nusu mfu mpaka Nadina  na binti mwingine walipoingia na kumnyanyua. Alikuwa hoi kwa kipigo pua yake ilikuwa inavuja damu, huku pembeni ya jicho kukionekana kuchubuka na sehemu kadhaa za mwili.

Maumivu aliyokuwa anayasikia muda ule, yalitosha kumkumbusha nyumbani kwao Shinyanga. laiti angejua, laiti tu angekuwa na uwezo wa kujua yajayo asingemsikiliza Jerry Agapella. Pengine sasa angekuwa na maisha bora kuliko yale yaliyokuwa mbele yake.

ITAENDELEA…..



1 comment:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger